TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA Juzuu 7

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA 0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 6325
Pakua: 701


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 16 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 6325 / Pakua: 701
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA Juzuu 7

Mwandishi:
Swahili

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA SABA

KIMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA

KIMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA

KIMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED

KUPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU

UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI

Sura Ya Tano: Al - Maidah

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu

UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI

Kitabu hiki kilichoko mikononi mwako hivi sasa ni juhudi ya miaka mingi sana ya watu waliojitolea kuona kazi hii imefanikiwa bila ya kumsahau Marhum Abu Muhammad wa London.

Kama lilivyo jina la Tafsiri yenyewe ndivyo ilivyo Tafsiri yenyewe ambayo mwanachuoni huyu mahiri kabisa aliyeifafanua ni mtu aliyebobea katika fani zote ambazo mfasiri (Mfafanuzi) anatakiwa awe nazo.

Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya ameonesha cheche zake katika vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbali mbalimbali na hivyo kujipatia wasomaji wengi sana.

Msomi huyu, mwenye fikra huru na anayetetea kile anachokiamini, ni mtu mwenye mawazo mapana na kuyaangalia mambo kwa undani sana, kipaumbele chake ni katika maslahi ya umma huu na amejaribu sana kwenda na wakati.

Sifa kubwa pekee ya mwanachuoni huyu ni kuwa yeye hakujihusisha sana na kung'ang'ania madhehebu fulani tu, labda hii yatokana na wadhifa wake wa ukadhi aliokuwa nao katika nchi ya Lebanon ambayo ina madhehebu mengi, ambapo sula la madhehebu ni nyeti nchini humo, hata hivyo yeye aliweza kuamua matatizo ya watu kwenye ofisi yake kulingana na madhehebu yao pale walipomwendea, hiyo ilimsaidia sana hata kuweza kutoa kitabu kitwacho 'Al-Fiqh a'laa madhaahabil-khamsah' (Fikhi ya madhehebu matano) yaani ya Hanafi, Maaliki, Shafi, Hambali na Shia (ambacho twataraji kitatoka hivi karibuni Inshaallah).

Jambo lililotupa msukumo wa kukifasiri kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ni zile faida nyingi atakazozipata msomaji na kujua mambo mengi na ya ajabu yaliyo mapya kwake ambayo si rahisi kuyapata kwa wafasiri wengine.

Msomaji atapata faida katika fani za Sayansi, Siasa, Historia, Mashairi, visa vizuri, na Saikolojia miongoni mwa mengine; ndiyo maana msomaji atashangaa kidogo anapoisoma Tafsiri hii atakapoona mwandishi amewataja na kuwanukuu watu kama kina Mfalme Edward, wanasyansi kama kina Enstein, Charlie Champlin (Mchekeshaji maarufu), na wengineo,vile vile kutaja nchi mbalimbali zikiwemo za Afrika; kama vile Afrika ya kusini, Zimbabwe nk, hali inayoifanya tafsiri hii kuwa ni ya kipekee kabisa.

Mtindo alioutumia mwandishi ni sahali uliokusudiwa watu wa tabaka mbalimbali, wanavyuoni na watu wa kawaida.

Nia yetu ni kukigawanya kitabu hiki bure lakini tumelazimika kukiuza kwa bei nafuu ili kurudisha gharama za uchapishaji.

Mwisho : Shukrani kubwa iwaendee bila ya kuwataja watu waliojitolea usiku na mchana, jopo la wafasiri, wahariri, wachapaji, waliotupa moyo na kutoa maoni yao na walioisimamia ili kuhakikisha kwamba kitabu kimemfikia msomaji.

MAKOSA YA CHAPA

Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa, Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo. Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa.

Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswutu kwa swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146), Imeandikwa La Ya'alamuun, (hawajui) badala ya Ya'alamuun (wanajua). Mfano wa makosa haya hausameheki.

Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya Pili, sura (5:212), imeandikwa "Fawqahum ila yawmil qiyama" badala ya "Fawqahum yawamal qiyama" Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile.

Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu jabal amail 'Makosa ya chapa.'

Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: " Hatta idha balagha arbai' na sanah badala ya: Hattaidha balagha ashuddahu arbai ' na sanah"

Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko na kuufungia macho uzuri wa maana.

Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: "Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa, kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.

Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin(a.s) :"Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu."

Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mwenye jukumu la kunikubaliayale niliyoyapatia na kunisamehe niliyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani (Amin).

MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH

1

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA SABA

﴿لَتَجِدَنَّ أَشَدَّ النَّاسِ عَدَاوَةً لِّلَّذِينَ آمَنُوا الْيَهُودَ وَالَّذِينَ أَشْرَكُوا وَلَتَجِدَنَّ أَقْرَبَهُم مَّوَدَّةً لِّلَّذِينَ آمَنُوا الَّذِينَ قَالُوا إِنَّا نَصَارَىٰ ذَٰلِكَ بِأَنَّ مِنْهُمْ قِسِّيسِينَ وَرُهْبَانًا وَأَنَّهُمْ لَا يَسْتَكْبِرُونَ﴾

82.Hakika utawakuta walio shadidi kuliko watu wote katika uadui kwa walio amini ni Mayahudi na washirikina. Na utawakuta walio karibu mno kwa mapenzi ni wale wanao sema: Sisi ni Manasara. Hayo ni kwa sababu wapo miongoni mwao makasisi na wamonaki, na kwa sababu wao hawafanyi kiburi.

﴿وَإِذَا سَمِعُوا مَا أُنزِلَ إِلَى الرَّسُولِ تَرَىٰ أَعْيُنَهُمْ تَفِيضُ مِنَ الدَّمْعِ مِمَّا عَرَفُوا مِنَ الْحَقِّ يَقُولُونَ رَبَّنَا آمَنَّا فَاكْتُبْنَا مَعَ الشَّاهِدِينَ﴾

83.Na wanaposikia yaliyoteremshwa kwa Mtume, utaona macho yao yanamiminika machozi kwa sababu ya haki waliyoitambua, wanasema: Mola wetu tumeamini tuandike pamoja na wanaoshuhudia

﴿وَمَا لَنَا لَا نُؤْمِنُ بِاللَّـهِ وَمَا جَاءَنَا مِنَ الْحَقِّ وَنَطْمَعُ أَن يُدْخِلَنَا رَبُّنَا مَعَ الْقَوْمِ الصَّالِحِينَ﴾

84.Na kwa nini tusimwamini Mwenyezi Mungu na haki iliyotujia, na hali tunatumai Mola atuingize peponi pamoja na watu wema?

﴿فَأَثَابَهُمُ اللَّـهُ بِمَا قَالُوا جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا وَذَٰلِكَ جَزَاءُ الْمُحْسِنِينَ﴾

85.Basi Mwenyezi Mungu atawalipa, kwa yale waliyosema, Bustani zipitazo chini yake mito, Humo watakaa milele, Na hayo ndiyo malipo ya wafanyao mema.

﴿وَالَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَحِيمِ﴾

86.Na wale waliokufuru na kuzikanusha Aya zetu, hao ndio watu wa motoni

UADUI WA MAYAHUDI NA URAFIKI WAWAKRISTO

Aya 82 - 86

MAANA

Hakika utawakuta walio maadui zaidi kuliko watu wengine kwa walioamini ni mayahudi na washirikina.

Yaani mayahudi na washirikina ndio waliokuwa maadui zaidi kwa Waislamu. Mara nyingi watu wameitolea ushahidi Aya hii, kuwa dini ya kikristo iko karibu zaidi na Uislam kuliko dini ya kiyahudi. Hilo ni kosa ikiwa inakusudiwa dini ya kiyahudi na ya kikristo kabla ya kugeuzwa. Kwa sababu dini kwa Mwenyezi Mungu na Mitume wake ni moja tu kwa upande wa itikadi na msingi yake. Na kama ikikusudia baada ya kubadilishwa, basi zote mbili ni sawa (Ukristo na Uyahudi) hakuna yenye afadhali.

Usahihi ni kuwa uhasama wa mayahudi na washirikina katika Uislam unatokana na mgongano baina ya mwito wa kiislam na tabia iliyokuwa imeshika kasi katika Bara arabu mwanzo wa utume. Tabia hiyo ilikua ni mashindano ya kupora mali na watumwa. Vilevile riba, ghushi na mengineyo ya kutumia nguvu na utapeli. Tabia hii iliambukiza wafanyibiashara wa kigeni, kama walivyoambukizwa viongozi wa kiyahudi waliokuwa wakimiliki viwanda na biashara ya ndani.

Ukaja mwito wa Muhammad(s.a.w.w) unaohimiza uadilifu na kukataa dhuluma na unyonyaji wa aina zote, na kuzuia unyonyaji wa mayahudi na washirikina. Kutokana na hali hiyo ndipo pande zote mbili zikakutana na kukubaliana kwa pamoja kujiepusha na dini na itikadi na kuungana mkono kupigana na Muhammad(s.a.w.w) , adui wa wote wawili.

Kwa ufafanuzi zaidi ni kuwa uadui wa mayahudi na washirikina kwa waislam, ulikuwa ni kwa msukumo wa kidunia na wala sio wa kidini, lakini mayahudi walijificha nyuma ya pazia la dini kwa kujionyesha na unafiki; sawa na wafanyavyo leo watu wanaotafuta chumo la haramu. Zaidi ya hayo ni kuwa mayahudi na washirikina wanashirikiana katika ubaguzi. Lakini washirikina pamoja na ujahili wao walikuwa na moyo usiokuwa mgumu, wakarimu na wenye fikra huru zaidi ya mayahudi. Ndio maana wengi wao wakamwamini Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) na ni mayahudi wachache tu ndio waliomwamini Muhammad.

NI NANI WALIO KARIBU NAWAISLAMU KIMAPENZI

Na utawakuta walio karibu zaidi kwa mapenzi na waumini ni wale waliosema sisi ni wanaswara.

Baadhi wanaichukulia Aya hii na iliyo baada yake ni chombo cha kukoroga mambo, kwamba Uislamu unaelemea mojawapo ya majeshi mawili hivi sasa. Jambo hili ndilo lililotufanya tufafanue Aya hizi nne kwa namna ambayo haitaacha nafasi kwa wale wanaobadilisha mambo.

Hakika mwenye kuziangalia vizuri Aya hizi, hawezi kuwa na hata chembe ya shaka kuwa zinakamilishana na kwamba haifai kabisa kuifasiri moja pekee yake bila ya kuichanganya na wenzake.

Nazo ziko wazi kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakuwafanya bora manaswara, kwa ujumla, kuliko makundi mengine katika kuwa karibu kiurafiki, si kwa umbali wala karibu.

Isipokuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) alikusudia kikundi maalum kutoka manaswara (wakristo) kwa dalili ya kuwa yeye hakuishia hapo tu bali aliendelea kusema: "Hayo ni kwa sababu wako miongoni mwao makasisi na watawa, na kwamba wao hawafanyi kiburi." Tena akaendelea kusema: Na wanaposikia yaliyoteremshwa kwa mtume, utaona macho yao yanamiminika machozi kwa sababu ya haki waliyoitambua; wanasema: "Mola wetu! Tumeamini basi tuandikie pamoja na wanaoshuhudia"

Maana yake ni kuwa miongoni mwa manaswara (wakristo) wako walioujua Uislamu,wakaukubali kwa kutii, kukinai na kwa imani.

Historia inathibitisha hivyo; kama ambavyo inathibitisha chuki ya manaswara kwa Uislam na Waislam. Kwa mfano: Fedheha ya Wataliano huko Tripoli ya Magharibi, na Wafaransa katika Algeria, Tunisia, Morocco na Syria, Vile vile fedheha ya Waingereza katika Misr, Iraq, Sudan n.k.

Na leo hii[1] Marekani wanaaungana na mayahudi katika kulingamiza taifa la Palestina. Wanawapa silaha za kisasa maharamia hawa, kisha wanafanya uchokozi na kudai kuwa wao ndio waliochokozwa na kuungwa mkono na Marekani katika Baraza la Usalama na Umoja wa mataifa. Hapo Marekani husema: Huu ndio ukweli uadilifu na demokrasia.

Je, baada ya hayo na mengi yasiyokuwa haya, itasemwa kuwa wakristo wote wako karibu kwa urafiki na waislam? Haya hayasemwi ila na mjinga au mwenye kutaka kuwapoteza watu. Kisha mpotezaji huyu atasema nini kuhusu kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Na kwa nini tusimwamini Mwenyezi Mungu na haki iliyotujia, na hali tunatumai Mola atuingize pamoja na watu wema?."

Haki iliyowajia na kuiamini, ni ile waliyobashiriwa na Isa:

﴿وَمُبَشِّرًا بِرَسُولٍ يَأْتِي مِن بَعْدِي اسْمُهُ أَحْمَدُ﴾

"Na kutoa Bishara ya Mjumbe atakayekuja baada yangu aitwaye Ahmad" (61:6)

Hayo, bila shaka, yanatiliwa mkazo na kukanushwa na kauli yake Mwenyezi Mungu aliyoifuatilia bila ya upambanuzi wowote isemayo:

Basi Mwenyezi Mungu atawalipa, kwa yale waliyosema, Bustani zipitazo chini yake mito, humo watakaa milele na hayo ndiyo malipo ya wafanyao mema.

Ushahidi wa wema na kulipwa pepo kwa kundi hili la wakristo ni dalili ya mkato ya kusilimu, na kwamba ndilo pekee lililokusudiwa baada ya kusifiwa wema na thawabu.

Ama wakristo ambao wameikana haki baada ya kuijua au wakaipinga bila ya kuangalia dalili zake na ubadhirifu wake, hawa wamekemewa na Mwenyezi Mungu na kuwapa kiaga kwa kusema:

Na wale waliokufuru na kuzikadhibisha Aya zetu hao ndio watu wa Motoni.

Unaweza kuuliza : kuwa kauli ya waliokufuru na kuzikadhibisha Aya zetu, inamhusu kila mwenye kukufuru na kukadhibisha. Sasa je, kuna wajihi gani wa kuhusisha wakristo?

Jibu : Mfumo wa maneno unafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) baada ya kuahidi pepo wenye kuamini katika wakristo, amewaahidi moto wenye kung'ang'ania ukafiri miongoni mwao. Ameleta neno la jumla, ili kujumuisha kemeo kwa kila mwenye kuihalifu haki na kuipinga, jambo ambao halipingani na yale tuliyoyasema.

Kwa ufupi ni kuwa Aya hii iko wazi kuwa makusduio ni kundi mahsusi katika wakristo - wale waliojua haki na kuiamini. Na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawaingiza peponi kwa sababu ya imani yao na amali yao njema.

Tukikadiria kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu: "Na utawakuta walio karibu kwa mapenzi na waumin ni wale waliosema sisi ni manaswara," inawakusanya wakristo wote, basi itawajibika tuiache dhahiri ya Aya na tuihusishe na wale walioamini katika wao kwa sababu mbili:

Kwanza : kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja katika Aya kadhaa kuwa manswara wamemfanyia Mungu washirika, wakaficha jina la Muhammad(s.a.w.w) na wakawafanya wanavyuoni wao na watawa wao kuwa waungu badala ya Mwenyezi Mungu. Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) akakataza kuwafanya mayahudi na manswara kuwa marafiki. Na akasema:

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا الْيَهُودَ وَالنَّصَارَىٰ أَوْلِيَاءَ﴾

"Enyi Mlioamini msiwafanye marafiki mayahudi na manswara" (5:51)

Tukiunganisha Aya hii, na zilizo mfano wa Aya hii, juu ya kauli yake Mwenyezi Mungu na utawakuta walio karibu zaidi kwa mapenzi na waumin ni wale waliosema sisi ni manswara," maana yanakuwa:

﴿مِّنْهُمْ أُمَّةٌ مُّقْتَصِدَةٌ وَكَثِيرٌ مِّنْهُمْ سَاءَ مَا يَعْمَلُونَ﴾

"Miongoni mwao wako watu washikao njia ya wastani, na wengi wao wanayoyafanya ni mambo mbaya" (5: 66)

Pili : ni kuwa wafasiri wanasema, Aya hii tunayoizungumzia ilishuka kwa sababu ya Najashi, mfalme wa Uhabeshi[2] aliyekuwa mnaswara (Mkiristo). Kwani Mtume(s.a.w.w) alipoona adhabu inayowapata sahaba zake kutoka kwa washirikina, mwanzo mwanzo wa mwito wa Uislam, aliwaamuru kuhamia Uhabeshi na kuwaambia: "Huko kuna mfalme ambaye hadhulumiwi mbele yake yeyote." Wakaenda huko, miongoni mwao akiwemo Jafar bin Abu Talib. Wakapata amani kwa Najashi na ujirani mwema. Hilo lilikuwa mnamo mwaka wa tano wa kutangazwa Utume.

Zimekuja Hadith Mutawatir kuwa Najashi na Baraza lake, la Mambo ya dini na mambo ya kidunia, walisilimu mikononi mwa Jafar bin Abu Talib baada ya kuwasomea Aya za Qur'an Tukufu na kutaja mazuri ya Uislam. Na kwamba walibubujikwa na machozi waliposikia Aya za Mwenyezi Mungu.

Baada ya hayo tunasema kwamba yule anayetolea ushahidi kauli ya Mwenyezi Mungu (Na utawakuta walio karibu zaidi kwa mapenzi na waumin ni wale waliosema sisi ni manswara) kwamba ukristo na wakristo kwa ujumla wote wako karibu zaidi na Uislamu na waislamu kuliko wengine, na kunyamazia Aya zinazokamilisha Aya hii, anayefanya hivyo huyo hakijui Kitabu cha Mwenyezi Mungu au ni mwenye kujionyesha tu kwa kutaka kuongeza chumvi kwa kuutumia Uislamu na Qur'an au anaweza kuwa ni mhaini anayezitia sumu fikra dhaifu katika Uislamu ili zikubali madai ya maadui wa dini, wanaowasaidia Israil na kuwapongeza kwa uchokozi wao kwa Waarabu na Waislam.

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُحَرِّمُوا طَيِّبَاتِ مَا أَحَلَّ اللَّـهُ لَكُمْ وَلَا تَعْتَدُوا إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ﴾

87.Enyi mlioamini! Msiharamishe vizuri alivyowahalalishia Mwenyezi Mungu. Wala msipetuke mipaka. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wanaopetuka mipaka.

﴿وَكُلُوا مِمَّا رَزَقَكُمُ اللَّـهُ حَلَالًا طَيِّبًا وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي أَنتُم بِهِ مُؤْمِنُونَ﴾

88.Na kuleni katika vile alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu vilivyo halali na vizuri, na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye nyinyi mnamwamini.

MSIHARAMISHE VIZURI

Aya 87 - 88

MAANA

Enyi mlioamini! Msiharamishe vizuri alivyowahalalishia Mwenyezi Mungu.

Wamesema kuwa Aya hii imeshuka kwa Masahaba waliokuwa na hofu sana na Mwenyezi Mungu wakajiharamishia wanawake, vyakula vizuri na mavazi. Wakawa wanaswali usiku na kufunga mchana. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) akawaita na kuwasomea Aya hii, akasema: Ama mimi ninaswali usiku na ninalala, ninafunga na ninafungua na ninawaendea wanawake. Basi atakayejiepusha na mwenendo wangu si katika mimi."

Na kauli yake Mwenyezi Mungu;Wala msipetuke mipaka. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wapetukao mipaka, inafahamisha kuwa kuharamisha halali ni sawa na kuhalalisha haramu, yote mawili ni dhulma na ukiukaji mipaka.

Na kuleni katika vile alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu vilivyo halali na vizuri. Imetangulia tafsir yake katika Juz.2 (2:168)

﴿لَا يُؤَاخِذُكُمُ اللَّـهُ بِاللَّغْوِ فِي أَيْمَانِكُمْ وَلَـٰكِن يُؤَاخِذُكُم بِمَا عَقَّدتُّمُ الْأَيْمَانَ فَكَفَّارَتُهُ إِطْعَامُ عَشَرَةِ مَسَاكِينَ مِنْ أَوْسَطِ مَا تُطْعِمُونَ أَهْلِيكُمْ أَوْ كِسْوَتُهُمْ أَوْ تَحْرِيرُ رَقَبَةٍ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ ذَٰلِكَ كَفَّارَةُ أَيْمَانِكُمْ إِذَا حَلَفْتُمْ وَاحْفَظُوا أَيْمَانَكُمْ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ﴾

89.Mwenyezi Mungu hawachukuli kwa viapo vyenu vya upuuzi; lakini anawachukulia kwa mlivyoapa kwa nia. Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa wastani wa mnavyowalisha watu wenu, au kuwavisha au kumwacha huru mtumwa. Na asiyeweza kupata (hayo), basi afunge siku tatu. Hayo ndiyo kafara ya viapo vyenu. Na vichungeni viapo vyenu. Namna hii Mwenyezi Mungu anawabainisha Aya zake ili mpate kushukuru.

VIAPO VYA UPUUZI

Aya 89

MAANA

Mwenyezi Mungu Hawachukuli kwa viapo vyenu vya upuzi.

Viapo vya upuzi ni kuachia ulimi bila ya kukusudia; kama vile kusema: Hapana wallahi, kumjibu aliyeuliza Je umemwona fulani, au kusema: Sivyo wallah, kumjibu aliyesema: Hutaki hii na Viapo hivi havitiliwi manani wala havina kafara kama mtu akihalifu lile alilo liapia.

Na aliyesema hawezi kuhisabiwa kuwa mwongo, na mtu yeyote hawezi kumwambia umemwapia Mwenyezi Mungu uwongo.

Kwa maneno mengine ni kwamba viapo hivyo havina athari yoyote ya kiapo. Hata hivyo iliyo bora ni kuacha ikiwa mtu hajaghafilika.

Lakini anawachukulia kwa mlivyoapa kwa nia.

Yaani kiapo cha sharia ambacho ni wajibu kukitekeleza na kutiliwa manani, ni kile anachoapa mtu aliyebaleghe mwenye akili timamu, kwa kukusudia, kutaka na kuwa na hiyari.

Wameafikiana kuwa kiapo kinakamilika ikiwa ni kwa kuapa kwa jina la Allah au kwa mojawapo ya majina yake mema, kama vile Khaliq, Razak (Muumbaji na Mruzuku)

Shia na Hanafi wanasema: "Kiapo hakiwi kwa jina la Msahafu na Mtume au Al-Ka'aba, kutokana na Hadith isemayo:Ambaye ataapa, basi na ape kwa jina la Allah au aache."

Shafi, Malik au Hambal wanasema: "Kinakuwa kwa jina la Msahafu. Hambali amekua peke yake katika kusema kuwa kinakuwa kwa Mtume vilevile.

Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa wastani wa mnavyowalisha watu wenu, au kuwavisha au kumwacha huru mtumwa.

Akiapa na akavunja kiapo, yaani akifanya lile aliloliapia kuliacha au kuacha lile aliloapia kulifanya, ni wajibu kwake atoe kafara akihiyarishwa baina ya mambo matatu.

Kwanza : kuwalisha masikini kumi mlo moja kila mmoja, kwa pamoja au mbali mbali kwa sharti ya kuwa ni mlo wa chakula ambacho aghalabu yeye hula na famlia yake. Inajuzu kumpa masikini kibaba cha chakula badala ya mlo. Makusudio ya masikini, ni yule ambaye ni halali kumpa Zaka, Kibaba ni zaidi kidogo ya 800 gm.

Pili : ni kuwavisha masikini kumi. Inatosha ile inayoitwa nguo ya kawaida. Kwa sababu sharia haikuhusisha. Kwa hiyo yakachukulia maana yaliyozoeleka bila ya kutofautisha mpya na ya zamani; mradi tu isiwe imechakaa au iliyochanika.

Tatu : ni kumwacha huru mtumwa; wala hakuna utumwa leo.

Na asiyeweza kupata (hayo), basi afunge siku tatu.

Yaani akishindwa kuyapata hayo matatu yaliyotangulia, atafunga siku tatu. Na akishindwa kufunga, basi ataomba maghufira kwa Mwenyezi Mungu na kutaraji msamaha wake.

Hayo ndiyo kafara ya viapo vyenu.

Hayo ni ishara ya kulisha, kuvisha, kuacha huru mtumwa na kufunga baada ya kushindwa na mambo matatu.

Na vichungeni viapo vyenu. Kuvifanya ni vya kawaida. Kwani kiapo cha Mwenyezi Mungu kina heshima yake na utukufu wake. Mwenyezi Mungu anasema: "Wala msimfanye Mwenyezi Mungu ni pondokeo la viapo vyenu" Juz.2 (2:224)

Kuna Hadith isemayo:"Hakika Nabii wa Mwenyezi Mungu, Musa aliwaamuru waongo wasiape kwa Mwenyezi Mungu. Na mimi ninawaamuru waongo na wa kweli wasimwapie Mwenyezi Mungu."

Namna hii Mwenyezi Mungu anawabainishia Aya zake ili mpate kushukuru.

Amesema Razi: "Maana yako wazi." Hata hivyo Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaka kutukumbusha neema za kujua hukumu zake, ili tusizitoe mahali pengine.

2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA SABA

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالْأَنصَابُ وَالْأَزْلَامُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ﴾

90.Enyi mlioamini! Hakika pombe na kamari na mizimu na mburuga ni uchafu katika kazi ya Shetani. Basi jiepusheni nayo, ili mpate kufaulu.

﴿إِنَّمَا يُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَن يُوقِعَ بَيْنَكُمُ الْعَدَاوَةَ وَالْبَغْضَاءَ فِي الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ وَيَصُدَّكُمْ عَن ذِكْرِ اللَّـهِ وَعَنِ الصَّلَاةِ فَهَلْ أَنتُم مُّنتَهُونَ﴾

91.Hakika Shetani anataka kuwaingizia uadui na bughudha baina yenu kwa pombe na kamari na kuwazuia kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kuswali, basi je, mtakoma.

﴿وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَاحْذَرُوا فَإِن تَوَلَّيْتُمْ فَاعْلَمُوا أَنَّمَا عَلَىٰ رَسُولِنَا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ﴾

92.Na mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na tahadharini na mkikengeuka basi jueni kuwa ni juu ya mtume wetu kufikisha (ujumbe) tu waziwazi.

POMBE NA KAMARI

Aya 90 - 92

MAANA

Enyi mlioamini! Hakika pombe na kamari na mizimu na mburuga ni uchafu katika kazi ya shetani.

Tumezungumzia kwa ufafanuzi kuhusu pombe na kamari katika kufasiri Aya Juz.2 (2:219). Na kuhusu mizimu na Mburuga katika Aya ya 3 ya Sura hii tuliyonayo.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amenasibisha kwa shetani kunywa pombe, kucheza kamari, kuabudu masanamu na kuagulia kwa mburuga. Kwa sababu Shetani ndiye anayapendekeza na kuwaghuri watu kwayo.

Basi jiepusheni nayo ili mpate kufaulu.

Dhamiri ya jiepusheni nayo inarudia uchafu. Hiyo ni amri ya kujiepusha; na amri inafahamisha wajibu, hasa wakati wa kubainisha sababu. Na ameibainisha hapo kuwa sababu ya kujiepusha ni kufaulu. Hata kama kusingekuwa na dalili ya kuharamishwa pombe zaidi ya kuwekwa sawa na kuabudu sanamu, ingelitosha. Sikwambii tena kama tukiunganisha na (2:219, 7:32), Hadith Mutawatir na Ijmai ya Waislamu tangu wakati wa Mtume(s.a.w.w) mpaka siku ya mwisho.

Hakika Shetani anataka kuwaingizia uadui na bughudha baina yenu kwa pombe na kamari na kuwazuia kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kuswali.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutilia mkazo uharamu wa pombe na kamari, na akakulinganisha na kuabudu masanamu na akakujaalia ni uchaTafsir fu unaotokana na adui wa mtu, na tena akabainisha kuwa njia ya kujiepusha ni kufaulu, baada ya yote haya. Anaonyesha Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwamba kwenye mambo mawili hayo kuna uharibifu mara mbili:Kwanza : wa kijamii - kutoelewana pamoja na kuleta chuki na undani baina ya watu.

Pili : ni wa kidini - kuzuia kumkumbuka Mwenyezi Mungu na ibada zake. Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) akataka watu wakome kunywa pombe na kucheza kamari kwa ibara fasaha kabisaBasi je mtakoma ?

Uislamu unahimiza kwa mahimizo yote kuwa mtu aungane na Muumba wake na jamii yake, na kwamba mtu mbele ya Mungu na mbele ya watu, awe mwenye kuridhiwa na kuheshimiwa.

Na mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume kwa kuacha pombe na kamari na mengineyo yaliyoharamishwa.

Na tahadharini isije ikawapata adhabu ya Mwenyezi Mungu, kama mkihalifu amri yake na amri ya Mtume wake. Imam Aliy(a.s) anasema:

"Mwenye kuinasihi nafsi yake zaidi ya watu (wote) ni yule anayemtii Mola wake zaidi yao. Na mwenye kuihadaa nafsi yake zaidi ya watu (wote) ni yule mwenye kuasi zaidi yao."

Na mkikengeuka basi jueni kuwa ni juu ya Mtume wetu kufikisha tu (ujumbe) waziwazi.

Naye ametekeleza kikamilifu, akasimamisha hoja na kutoka katika jukumu la kufikisha. Atakayehalifu ni yeye peke yake na jukumu lake.

﴿لَيْسَ عَلَى الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ جُنَاحٌ فِيمَا طَعِمُوا إِذَا مَا اتَّقَوا وَّآمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ ثُمَّ اتَّقَوا وَّآمَنُوا ثُمَّ اتَّقَوا وَّأَحْسَنُوا وَاللَّـهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ﴾

93.Si dhambi juu ya wale walioamini na wakatenda mema wa vile walivyovila maadamu wakiwa na takua na wakiamini na wakitenda mema, tena wakawa na takua na wakaamini, tena wakawa na takua na wakafanya mazuri, Na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao mazuri.

WENYE TAKUA NA KUAMINI

Aya 93

MAANA

Wafasiri wameafikiana kwamba iliposhuka Aya ya kuharamisha pombe, baadhi ya Masahaba walimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) : Itakuwaje kwa ndugu zetu waliokufa wakiwa wanywaji?

Ndipo ikashuka Aya hii ambayo kwa ujumla inafahamisha kuwa mwenye kunywa pombe kabla ya kubainishwa hukumu yake, hapana vibaya juu yake ikiwa ni katika waumini wanaomcha Mungu. Kuanzia hapa ndipo mafakihi wakaafikiana kwamba kila kitu ni halali mpaka kikatazwe.

Baada ya kuafikiana wafasiri kuwa maana haya ndiyo makusudio katika Aya walihitalifiana katika sababu zinazowajibisha kukaririka takua mara tatu; ambapo mara ya kwanza kumetajwa, pamoja na Imani na amali njema, mara ya pili pamoja na Imani tu na mara ya tatu pamoja na uzuri.

Razi amenukuu, katika hilo, kauli tano. Mwenye Majmaul-bayan akasema: Makusudio ya takua ya kwanza ni kuacha kunywa pombe baada ya kuharamishwa; ya pili ni kudumu juu ya hilo na ya tatu ni kuacha maasi yote pamoja na kufanya mema.

Mmoja wa wafasiri wapya anasema: "Nafsi yangu bado haijatulia na chochote katika tafsir hii; wala Mwenyezi Mungu hajanifungulia chochote. Tunavyofikiria sisi - Mwenyezi Mungu ndiye mjuzi zaidi - ni kwamba lengo la kukaririka huku ni kubainisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwamba mwenye takua ya kweli ni yule anayemcha Mwenyezi Mungu katika hali zake zote, ujana, uzee na ukongwe, na katika dhiki na faraja. Na kwamba mwenye kufa juu ya hilo basi yuko katika amani na usalama.

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَيَبْلُوَنَّكُمُ اللَّـهُ بِشَيْءٍ مِّنَ الصَّيْدِ تَنَالُهُ أَيْدِيكُمْ وَرِمَاحُكُمْ لِيَعْلَمَ اللَّـهُ مَن يَخَافُهُ بِالْغَيْبِ فَمَنِ اعْتَدَىٰ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَلَهُ عَذَابٌ أَلِيمٌ﴾

94.Enyi mlioamini! Hakika Mwenyezi Mungu atawajaribu kwa baadhi ya mawindo yatakayofikiwa na mikono yenu na mikuki yenu, ili Mwenyezi Mungu amjue ni nani anayemwogopa kwa ghaibu, Basi atakayeruka mipaka baada ya hayo, atapata adhabu iumizayo.

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْتُلُوا الصَّيْدَ وَأَنتُمْ حُرُمٌ وَمَن قَتَلَهُ مِنكُم مُّتَعَمِّدًا فَجَزَاءٌ مِّثْلُ مَا قَتَلَ مِنَ النَّعَمِ يَحْكُمُ بِهِ ذَوَا عَدْلٍ مِّنكُمْ هَدْيًا بَالِغَ الْكَعْبَةِ أَوْ كَفَّارَةٌ طَعَامُ مَسَاكِينَ أَوْ عَدْلُ ذَٰلِكَ صِيَامًا لِّيَذُوقَ وَبَالَ أَمْرِهِ عَفَا اللَّـهُ عَمَّا سَلَفَ وَمَنْ عَادَ فَيَنتَقِمُ اللَّـهُ مِنْهُ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ ذُو انتِقَامٍ﴾

95.Enyi Mlioamini! Msiue windo na hali mko katika Ihram. Na miongoni mwenu atakayemuua kwa kusudi, basi malipo (yake) yatakuwa ni mfano wa aliyemuua katika wanyama wa kufugwa, kama watavyohukumu waadilifu wawili miongoni mwenu, mnyama apelekwe Al-kaaba (kama sadaka); au kutoa kafara kwa kuwalisha masikini; au badala ya hayo ni kufunga; ili aonje ubaya wa jambo lake. Mwenyezi Mungu amekwisha yasamehe yaliyopita; na atakayerudia, Mwenyezi Mungu atampa adhabu; na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye nguvu mwenye kuadhibu.

﴿أُحِلَّ لَكُمْ صَيْدُ الْبَحْرِ وَطَعَامُهُ مَتَاعًا لَّكُمْ وَلِلسَّيَّارَةِ وَحُرِّمَ عَلَيْكُمْ صَيْدُ الْبَرِّ مَا دُمْتُمْ حُرُمًا وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ﴾

96.Mmehalalishiwa kuvua baharini na chakula chake, kwa manufaa yenu na kwa wasafiri. Na mmeharamishiwa kuwinda bara maadamu mko katika Ihram, Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye kwake mtakusanywa.

HAKUNA KUWINDA KATIKA HARAM WALA PAMOJA NA IHRAM

Aya 94 - 96

MAANA

Enyi Mlioamini! Hakika Mwenyezi Mungu atawajaribu kwa baadhi ya mawindo yanayofikiwa na mikono yenu na mikuki yenu.

Makusudio ya baadhi ni mawindo ya bara tu. Kauli yake Mwenyezi Mungu yanayoafikiwa na mikono yenu na mikuki" ni fumbo la kuwinda, bila ya shaka. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameharamisha kuwinda bara katika Haram[3] na katika hali ya Ihram[4] jambo ambalo ni jepesi; sawa na alivyowaharimishia Wana wa Israil kuvua samaki siku ya Jumamosi (sabato).

Ili Mwenyezi Mungu amjue ni nani anayemwogopa kwa ghaibu.

Yaani Mwenyezi Mungu amewajaribu kwa kuharamisha kuwinda katika hali hii ili ampambanue yule anayemwogopa katika siri kama yule anayemtii katika dhahiri na yule anayejionyesha kwa kumtii na kumwogopa mbele ya watu na kumwasi katika uficho.

Basi atakayeruka mipaka baada ya hayo, atapata adhabu iumizayo.

Yaani mwenye kuhalifu amri ya Mwenyezi Mungu kwa kuwinda baada ya ubainifu huu na hoja, basi atastahiki adhabu ya Mwenyezi Mungu na mateso.

MAANA YA KUJARIBU KWA MWENYEZI MUNGU

Unaweza kuuliza : kuwa kwa Mwenyezi Mungu halifichiki lolote lilo katika ardhi wala katika mbingu; sasa kuna wajihi gani wa kauli yake Mwenyezi Mungu: "Hakika Mwenyezi Mungu atawajaribu, na kauli yake:"Ili Mwenyezi Mungu amjue anayemwogopa"

Jibu : Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) hamjaribu mja wake ili ajue ambayo hakuwa akijua, hapana! Kwani yeye anamjua zaidi kuliko yeye mwenyewe. Isipokuwa anamtia mtihani kwa mambo mengi; kama haya yafuatayo:-

Kuyafasiri yale yalioko katika nafsi ya mja yajitokeze. Ambapo hekima imepitishwa kutowahisabu watu kwa yale anayoyajua kwao wala yale yanayokuwa katika nafsi zao katika silika. Isipokuwa atawahisabu na matukio ya matendo. Silika ya kinafsi peke yake haina haja ya kuhisabiwa wala kupewa adhabu, maadam iko ndani tu ya binadamu na athari yake haionekani kwa macho au kusikiwa kwa masikio.

Imam Ali(a.s) anasema: "Mwenyezi Mungu anasema:Jueni kuwa mali zenu na watoto wenu ni fitna. Maana yake ni kuwa anawajaribu kwa mali na watoto ili abainike mwenye kuichukia riziki yake na mwenye kuridhia ugawanyo wake, ingawaje Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni mjuzi zaidi kuliko nafsi zao, lakini ni kudhihirisha vitendo ambavyo vinastahiki thawabu na adhabu.

Kumpambanua mwovu na mwema na kuidhihirisha hakika yake mbele ya watu na kumchukulia vile anavyostahiki. Na hayo, mara nyingi sana, hutokea katika maisha ya watu.

Kwa mfano wewe unajua Zedi ni katika watu wa elimu na maarifa. Ikawa yeye yuko baina ya watu wasiojua ujuzi wake, nawe ukataka wajue mwamko wake na elimu yake. Kwa hiyo ukamuuliza mbele ya watu, ili aseme na ajulikane.

Au pengine unajua kwamba yeye ni duni mjinga, na watu wanamdhania kuwa ni mjuzi mwenye hekima. Kwa hiyo ukafanya hivyo hivyo udhihirishe ujinga wake na uduni wake.

Watu wengi wao wenyewe hawajijui na wanasema : lau tungelikuwa na hali fulani, basi tungefanya kadha wa kadha. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu huwapa uwezo na fursa ili awe na hoja juu yao na ijulikane hakika yao na hali yao. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَمِنْهُم مَّنْ عَاهَدَ اللَّـهَ لَئِنْ آتَانَا مِن فَضْلِهِ لَنَصَّدَّقَنَّ وَلَنَكُونَنَّ مِنَ الصَّالِحِينَ ﴿٧٥﴾ فَلَمَّا آتَاهُم مِّن فَضْلِهِ بَخِلُوا بِهِ وَتَوَلَّوا وَّهُم مُّعْرِضُونَ﴾

"Na miongoni mwao wako waliomwahidi Mwenyezi Mungu kuwa: Akitupa katika fadhila zake, kwa hakika tutatoa sadaka na kwa hakika tutakuwa katika wanaotenda mema. Alipowapa katika fadhila yake wakaifanyia ubakhili na wakageuka na huku wao wanapuuza" (9:75-76)

Wana wa Israil walimtaka Musa awafanyie siku ya kupumzika na kufanya ibada, Mwenyezi Mungu akawajaalia siku ya Jumamosi (sabato).

Wakaahidi kutofanya chochote siku hiyo; kama walivyotaka, lakini ikawa samaki wanawajia sana siku hii na inapokwisha Jumamosi na samaki nao hupotea. Wana wa Israil wakafanya hila ya kuwavua na wakavunja ahadi.

Kwa hiyo kwenye wajihi wa kwanza tulioueleza - kudhihiri vitendo vinavyostahiki thawabu na adhabu, ndiyo yamechukuliwa maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu "Hakika atawajaribu Mwenyezi Mungu, ili amjue Mwenyezi Mungu anayemwogopa. Na ili awajue Mwenyezi Mungu wale walioamini" na mfano wa Aya hii.

Enyi mlioamini! Msiue windo na hali mko katika Ihram.

Wameafikiana Mafakihi kwamba kuwinda ndani ya Haram haijuzu kwa aliye katika Ihram na asiye katika Ihram. Ama nje ya Haram inajuzu kuwinda kwa asiyekuwa katika Ihram. Lau atachinja aliye katika Ihram windo basi litakuwa ni mfu ulio haramu kuliwa na watu wote.

Imeelezwa katika Kitab Fiqhu Sunna cha Sayyid Sabiq kwamba mpaka wa Haram ya Makka kwa upande wa Kaskazini ni sehemu inayaoitwa Tani'm, kilomita 6 kutoka Makka. Upande wa kusini ni mahali panapoitwa Ardhah, kilomita 12. Upande wa Mashariki ni Ja'rana kilomita 15.

Na miongoni mwenu atakayemua kwa kusudi, basi malipo (yake) yatakuwa ni mfano wa aliyemuua katika wanyama wa kufugwa, kama watakavyo hukumu waadilifu wawili miongoni mwenu. Mnyama apelekwe Al-K'aaba (kama sadaka); au kutoa kafara kwa kuwalisha masikini au badala ya hayo ni kufunga.

Mwenye kuwa katika Ihram akiuwa, au akiwa hayuko katika Ihram, lakini ameuwa ndani ya haramu, basi ikiwa mnyama aliyemuuwa ana mfano katika aina tatu za wanyama wa kufugwa - Ngamia, Ngombe, Kondo au Mbuzi, basi atakuwa na hiyari ya kuchinja mfano wa mnyama aliyeuliwa na mtoe sadaka; au kutoa thamani ya mnyama anyefanana na aliyemuua. Anunue chakula na kukitoa sadaka kwa masikini kila masikini vibaba viwili, kilogram 1.6 takriba. Wengine wamesema kuwa atatoa kibaba kimoja, au afunge kwa kila vibaba viwili siku moja, au kwa kila kibaba kimoja kulingana na kauli nyingine.

Maana ya "Kama watakavyohukumu waadiifu wawili" ni kushuhudia watu wawili waadilifu, kuwa mnyama huyu wa kufuga ni sawa na mnyama aliyeuawa.

Maana ya "Mnyama apelekwe Al-Kaaba" ni kuchinjwa huyo mnyama jirani ya Al-Kaaba na kutolewa nyama yake kwa masikini.

Ikiwa hakupata mfano katika aina zile tatu za wanyama wa kufugwa, basi atatoa kima cha mnyama mwingine wa kufugwa na anunue chakula na kukitoa sadaka; au kufunga, kwa ufafanuzi uliotangulia.

Ili aonaje ubaya wa jambo lake.

Kuwinda katika Haram au katika hali ya Ihram ni kuvunja mwiko wa Mwenyezi Mungu, kwa hiyo ndio akaadhibiwa mwindaji kwa kafara hiyo iliyotajwa. Maana ya ubaya wa jambo lake, ni mwisho wa kitendo chake kibaya.

Mwenyezi Mungu amekwishayasamehe yaliyopita ; ya kuwinda kabla ya kuharamishwa.Na atakayerudia kuwinda,Mwenyezi Mungu atampa adhabu kwa kung'ang'ania kwake dhambi.

Mmehalalishiwa kuvua baharini na chakula chake, kwa manufaa yenu na kwa wasafiri.

Dhamiri katika chakula chake inarudia bahari, kwa sababu mna vinavyoliwa visivyo vuliwa. Inawezekana kuwa dhamiri inarudia kinachovuliwa; na maana yawe Mwenyezi Mungu (s.w.t) amehalalisha kuvua na kula vilevile. Makusudio ya wasafiri ni wale wasiokuwa katika Ihram.

Na mmeharamishiwa kuwinda bara maadamu mko katika Ihram.

Yaani kuvua baharini ni halali kwa hali yoyote. Imam Jafar Assadiq(a.s) anasema:Usihalalishe chochote katika mawindo - ya bara - ukiwa katika Ihram. Wala usipokuwa katika Ihram pia usimfahamishe aliye katika Ihram au asiye katika Ihram, akawinda na wala usimwonyeshe kwani katika hayo kuna fidia kwa mwenye kufanya makusudi.

Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye kwake mtakusanywa.

Yaani jitahidi ni katika kumtii na kutafuta radhi zake, ili awalipe wema siku ya ufufuo.