TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA Juzuu 7

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA 0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 13142
Pakua: 2179


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 16 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 13142 / Pakua: 2179
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA Juzuu 7

Mwandishi:
Swahili

9

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA SABA

﴿قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِنْ أَخَذَ اللَّـهُ سَمْعَكُمْ وَأَبْصَارَكُمْ وَخَتَمَ عَلَىٰ قُلُوبِكُم مَّنْ إِلَـٰهٌ غَيْرُ اللَّـهِ يَأْتِيكُم بِهِ انظُرْ كَيْفَ نُصَرِّفُ الْآيَاتِ ثُمَّ هُمْ يَصْدِفُونَ﴾

46.Sema: Mwaonaje kama Mwenyezi Mungu akichukua kusikia kwenu na kuona kwenu na akaziziba nyoyo zenu, ni nani Mungu mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu awezaye kuwaletea tena? Tazama jinsi tunavyozikariri ishara, kisha wao wanapuuza.

﴿قُلْ أَرَأَيْتَكُمْ إِنْ أَتَاكُمْ عَذَابُ اللَّـهِ بَغْتَةً أَوْ جَهْرَةً هَلْ يُهْلَكُ إِلَّا الْقَوْمُ الظَّالِمُونَ﴾

47.Sema: Mwaonaje ikiwafikia adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa ghafla au kwa dhahiri nani wataangamizwa isipokuwa watu waliodhulumu?

﴿ وَمَا نُرْسِلُ الْمُرْسَلِينَ إِلَّا مُبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ فَمَنْ آمَنَ وَأَصْلَحَ فَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ﴾

48. Na hatutumi Mitume ila niwabashiri na waonyaji. Na wenye kuamini na wakafanya wema, basi haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika. 49. Na wale waliokadhibisha ishara zetu itawagusa adhabu kwa sababu ya walivyokuwa mafasiki.

AKICHUKUA MWENYEZI MUNGU KUSIKIA NA KUONA

Aya 46-49

MAANA

Sema: Mwaonaje kama Mwenyezi Mungu akichukuwa kusikia kwenu na kuona kwenu na akaziziba nyoyo zenu, ni nani Mungu mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu awezaye kuwaletea tena?

Mtu ni usikizi, uoni na moyo. Lau haya yanamwondokea, basi hatakuwa ni chochote, mnyama atakuwa ni bora kuliko yeye. Hakuna mwenye shaka kwamba Mwenyezi Mungu anaweza kuvichukua hivyo, kwa sababu Yeye ndiye aliyeviumba.

Makusudio ya ishara hii ni kuwakumbusha Mwenyezi Mungu Makafiri kuwa wanaowafanya waungu asiyekuwa yeye hawatawakinga na madhara wala hawatawaletea manufaa:

﴿وَإِذَا أَرَادَ اللَّـهُ بِقَوْمٍ سُوءًا فَلَا مَرَدَّ لَهُ﴾

"Na Mwenyezi Mungu anapowatakia watu adhabu hakuna cha kuzuia" (13:11)

Tazama jinsi tunavyozikariri ishara, kisha wao wanapuuza.

Yaani tumesimamisha hoja juu yao zinazofuatiwa na hoja kwa mifumo mbali mbali, ili wawaidhike na wazingatie. Tukawaondolea nyudhuru zote ili waamini. Lakini dalili hizo mkato hazikuwadishia ila kuendelea na ukafiri, dhuluma na inadi.

Sema: Mwaonaje ikiwafikia adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa ghafla au kwa dhahiri nani wataangamizwa isipokuwa watu waliodhulumu?

Mara ya pili anawapa mawaidha na kuwatishia kuwaletea adhabu ambayo hawataweza kuikinga; ni sawa ingewajia ghafla kwa namna wasiyoijua au kwa wazi wazi kwa namna ya kuwa tayari nayo. Mara hii katika Aya hii anawaonya Mwenyezi Mungu na kuwapa onyo ili waiogope adhabu kabla ya kutukia kwake, na waelekee kwenye uongofu wao, lakini nyoyo zao zikasusuwaa na wala wasipondokee kwenye haki na uongofu.

Na hatutumi Mitume ila na waonyaji.

Hii ndiyo kazi ya Mtume, anawapa bishara watiifu na kuwaonya waasi. Kazi hii, pamoja na urahisi wa ufafanuzi wake na kueleweka kwake, lakini ndiyo kazi yenye mashaka makubwa na nzito. Kwa sababu inagusa maisha ya mataghuti moja kwa moja, na kuyaingilia masilahi yao na manufaa yao.

Mwishilio wa kazi ya Mtume ni kulipwa wema mwenye kuamini na kufanya matendo mema, na kuadhibiwa mwenye kukufuru na kuzikadhibisha ishara za Mwenyezi Mungu.

Na wenye kuamini na wakafanya wema, basi haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika.

Kwa sababu mwenye makosa ndiye anayehofia na kuhuzunika. Ama asiye na hatia huwa katika amani na utuvu.

Na wale waliokadhibisha ishara zetu itawagusa adhabu kwa sababu ya walivyokuwa mafasiki.

Ufasiki ni zaidi ya ukafiri. Kila kafiri ni fasiki, sio kila fasiki ni kafiri. Makusudio ya ufasiki hapa ni ukafiri, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: Waliokadhibisha ishara zetu.

﴿قُل لَّا أَقُولُ لَكُمْ عِندِي خَزَائِنُ اللَّـهِ وَلَا أَعْلَمُ الْغَيْبَ وَلَا أَقُولُ لَكُمْ إِنِّي مَلَكٌ إِنْ أَتَّبِعُ إِلَّا مَا يُوحَىٰ إِلَيَّ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الْأَعْمَىٰ وَالْبَصِيرُ أَفَلَا تَتَفَكَّرُونَ﴾

50.Sema: Siwaambii kuwa ninazo hazina za Mwenyezi Mungu, wala sijui ghaibu; wala siwambii mimi ni Malaika; sifuati ila ninayopewa Wahyi. Sema: Je, kipofu na mwenye kuona wako sawa? Je, hamfikiri?

﴿وَأَنذِرْ بِهِ الَّذِينَ يَخَافُونَ أَن يُحْشَرُوا إِلَىٰ رَبِّهِمْ لَيْسَ لَهُم مِّن دُونِهِ وَلِيٌّ وَلَا شَفِيعٌ لَّعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ﴾

51.Na waonye kwayo wale wanaoogopa kwamba watakusanywa kwa Mola wao. Hawana mlinzi wala mwombezi isipokuwa yeye ili wapate kuwa na takua.

﴿وَلَا تَطْرُدِ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُم بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ مَا عَلَيْكَ مِنْ حِسَابِهِم مِّن شَيْءٍ وَمَا مِنْ حِسَابِكَ عَلَيْهِم مِّن شَيْءٍ فَتَطْرُدَهُمْ فَتَكُونَ مِنَ الظَّالِمِينَ﴾

52.Wala usiwafukuze wale wanaomwomba Mola wao asubuhi na jioni kwa kutaka radhi yake; si juu yako hisabu yao hata kidogo, wala hisabu yako si juu yao hata kidogo, kwamba uwafukuze na uwe miongoni mwa madhalimu.

﴿وَكَذَٰلِكَ فَتَنَّا بَعْضَهُم بِبَعْضٍ لِّيَقُولُوا أَهَـٰؤُلَاءِ مَنَّ اللَّـهُ عَلَيْهِم مِّن بَيْنِنَا أَلَيْسَ اللَّـهُ بِأَعْلَمَ بِالشَّاكِرِينَ﴾

53.Na namna hii tumewajaribu wao kwa wao ili waseme: Je, hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewafadhili miongoni mwetu? Kwani Mwenyezi Mungu hawajui wanaoshukuru?

﴿وَإِذَا جَاءَكَ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِآيَاتِنَا فَقُلْ سَلَامٌ عَلَيْكُمْ كَتَبَ رَبُّكُمْ عَلَىٰ نَفْسِهِ الرَّحْمَةَ أَنَّهُ مَنْ عَمِلَ مِنكُمْ سُوءًا بِجَهَالَةٍ ثُمَّ تَابَ مِن بَعْدِهِ وَأَصْلَحَ فَأَنَّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴾

54.Na wanapokufikia wale wanaoamini ishara zetu waambie: Amani iwe juu yenu (Assalam alaykum), Mola wenu amejilazimisha rehema. Ya kwamba atakayefanya miongoni mwenu uovu kwa ujinga, kisha akatubu baada yake na akatengenea. Basi yeye ndiye mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

﴿وَكَذَٰلِكَ نُفَصِّلُ الْآيَاتِ وَلِتَسْتَبِينَ سَبِيلُ الْمُجْرِمِينَ﴾

55.Namna hii tunazieleza ishara na ili njia ya wakosefu ibainike.

SIFUATI ILA NINAYOPEWAWAHYI

Aya 50 -55

MAANA

Sema: Siwaambii kuwa ninazo hazina za Mwenyezi Mungu, wala sijui ghaibui, wala siwambii mimi ni Malaika; sifuati ila ninayopewa Wahyi.

Washirikina walimtaka Mtume(s.a.w.w) awaambie mambo ya siri, awatolee chemchem, awaletee Malaika, apande mbinguni na awaangushie hiyo mbingu na mengineyo ambayo hayana uhusiano wowote na Utume. Ndipo akateremsha Mwenyezi Mungu Aya hii na akamwamrisha Mtume kuwaambia, kuwa yeye si Mungu wala Malaika; isipokuwa yeye ni mtu anayepewa wahyi tu.

Kwa maneno mengine ni kuwa Mungu ana sifa zinazomhusu yeye tu; kama vile kuwa ni muweza wa kila kitu, mwenye kujua kila kitu. Vilevile Malaika ana sifa zinazomhusu; kama vile kupanda mbinguni na kuwa yeye hali wala hatembei sokoni. Ama Mtume ni mtu kama watu wengine; tofauti ni kuwa yeye analetewa wahyi tu kutoka kwa Mola wake, akimpa bishara ya malipo mazuri yule atakayemwitikia, na kumuonya kwa adhabu yule atakayempa kisogo.

Wala si mambo yanayohusu Utume, kutoa habari za siri na kuleta mambo yasiyokuwa ya kawaida. Kwa hiyo kuchanganya sifa za Malaika na Mitume yake ni ujinga na upofu.

Sema: Je, kipofu na mwenye kuona wako sawa?

Tofauti ilioje baina ya mjinga mpotevu ambaye hatofautishi baina ya sifa za Mwenyezi Mungu na sifa za Mtume, na yule anayefahamu kuwa Mtume ni mtu aliye na yale waliyo nayo watu wengine, isipokuwa yeye anapewa wahyi.

Je, hamfikiri? Kuwa Mtume siye Mungu wala Malaika na kwamba yeye ni mtoaji bishara na muonyaji, ili mzifanyie haki nafsi zenu na muamini Lailaha ila Ilah Muhammadur rasulullah? (Hakuna mola isipokuwa Mwenyezi Mungu, Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu)

Na waonye kwayo wale wanaoogopa kwamba watakusanywa kwa Mola wao.

Dhamir katika kwayo inarudia Qur'an, iliyotanguliwa kuashiriwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:"Sifuati ila ninayopewa Wahyi."

Wametofautiana wafasiri kuhusu wanaoogopa kukusanywa kwa Mola wao kuwa je ni waumini au makafiri, kwa kuangalia kuwa baadhi yao walikuwa wakiathirika kuhofishwa na Mtume na maonyo yake; kama ilivyoelezwa katika Tafsir ya Razi?

Tuonavyo ni kuwa baada ya Mtume(s.a.w.w) kuwaonya watu kwa hoja zinazowasimamia, Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimwamrisha, katika Aya hii, kuendelea na kufuatishia kuwaonya waumini kwa Qur'an ili wazidi imani, na waijue dini na hukumu zake.

Vilevile kuwaonya wasiokuwa waumini katika wale ambao kuna matarajio ya kuongoka kwao kwa kufuatisha kuonya na kukaririka.

Hawana mlinzi wala mwombezi isipokuwa yeye ili wapate kuwa na takua.

Yaani wakati unapowaonya wanakusikiliza na kunufaika na unavyowaonya na kujua kuwa hawana mlinzi wa kuwanusuru isipokuwa Mwenyezi Mungu, wala mwombezi yeyote atakayeombea mbele yake ila kwa idhini yake.

Wala usiwafukuze wale wanaomwomba Mola wao asubuhi na jioni kwa kutaka radhi yake; si juu yako hisabu yao hata kidogo, wala hisTafsir abu yako si juu yao hata kidogo, kwamba uwafukuze na uwe miongoni mwa madhalimu.

Asubuhi na jioni ni fumbo la kuendelea kumtaja kwao Mwenyezi Mungu na kumwabudu; kama kusema "Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu asubuhi na jioni."

Dhamiri ya Hisabu yao na juu yao inawarudia waumini wanaomwomba Mola wao. Maana ya si juu yako hisabu yao ni kuwa hisabu yao na hisabu ya wengineo, haihusiani na Utume wala si katika mambo yake. Hisabu yao iko kwa Mwenyezi Mungu tu peke Yake; sawa na ilivyo hisabu yako ewe Muhammad.

Mwislamu, kwa hakika, anaamini moja kwa moja kwamba Muhammad(s.a.w.w) ni Mtukufu wa viumbe vyote na wakati huo anaamini kuwa utukufu wa Muhammad haumwezeshi kumhisabu yeyote au kumwadhibu au kumpa thawabu. Hakika hisabu na malipo ni ya Mwenyezi Mungu na yanatokana na Mwenyezi Mungu pekee bila ya kuwa na mshirika.

Kwa fadhila hii ndipo Uislamu ukatofautiana na dini zote kwa kukanusha uwezo wa mtu kwa mtu mwingine vyovyote atakavyokuwa. Na kwa hali hiyo tunajifaharisha na kujitukuza kuliko Wajamaa, Wakomunisti, Mabepari, Wademokrasia na watu wa dini zote na madhehebu yote.

Wafasiri wametaja sababu za kushuka Aya hii, kuwa mamwinyi wa Kikuraish walimpitia Mtume(s.a.w.w) akiwa na Ammar bin Yasir, Khabbab, Bilal na wengine katika Waislamu wa hali ya chini, wakasema: "Ewe Muhammad umewaridhia hawa? Unataka tuwe pamoja na hawa? Hebu waondoe tuwe sisi tu peke yetu na wewe; kisha tukimaliza warudishe ukae nao ukitaka" Imesemekana kuwa Mtume(s.a.w.w) alitaka kuwakubalia, ndipo ikashuka Aya.

Dhahiri ya maneno hapa haiikatai hilo hasa kauli yake Mwenyezi Mungu: "Kwamba usiwafukuze na uwe miongoni mwa madhalimu." Kwa kuwadhulumu hao, ambao ni bora hasa kukaa nao na wapate faida kutoka kwako.

Kwa maneno mengine ni kwamba Mtume alitaka kuwakaribisha matajiri, ili afaidike nao, ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia mafukara ni bora kufaidika nao, Ukiacha ubora huu, basi umewadhulumu mafukara waumini katika kufaidika.

Utauliza : Je, kuacha lililo bora hakupingani na Isma?

Jibu : Kuacha lililo bora zaidi kunajuzu na wala si haramu, mpaka kupingane na Isma. Zaidi ya hayo ni kwamba Mtume hakujaribu kuwafukuza mafukara kwa kuwadharau kutokana na ufukara wao, bali ni kwa kupupia na kuwa na tamaa ya kusilimu viongozi. Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamfahamisha kuwa Uislamu hauna haja na hawa wenye kutakabari mataghuti; na kwamba iko siku watakuja silimu wakiwa madhalili walio chini; kama ilivyotokea baadaye.

Na namna hii tumewajaribu wao kwa wao ili waseme: Je, hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewafadhili miongoni mwetu?

Kujaribu Mwenyezi Mungu mja wake ni kumdhihirisha kwa watu hakika yake kwa njia ya vitendo vyake na kauli zake; kama tulivyofafanua katika kufasiri Juz hii (5:94)

Maana ni kuwa tumewajaribu matajiri kwa mafakiri, ili wamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwaneemesha, lakini hilo likawapeleka kuwa na kiburi na kujitukuza. Imam Ali(a.s) anasema:"Msizingatie mapenzi na chuki kwa mali na watoto tu, mkasahau fitina na mtihani katika utajiri" Amekwisha sema Mwenyezi Mungu (s.w.t):

﴿أَيَحْسَبُونَ أَنَّمَا نُمِدُّهُم بِهِ مِن مَّالٍ وَبَنِينَ ﴿٥٥﴾ نُسَارِعُ لَهُمْ فِي الْخَيْرَاتِ بَل لَّا يَشْعُرُونَ﴾

"Je, wanafikiri kuwa yale tunayowapa mali na watoto ndio tunawaharakishia katika heri? Bali hawatambui" (23: 55)

Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawajaribu waja wake wenye kutakabari katika nafsi zao kwa mawalii wake wanyonge machoni mwao. Musa bin Imran na nduguye Harun waliingia kwa Firaun wakiwa na majuba ya sufi na mikononi wameshikila fimbo.

Wakampa sharti la kusilimu ikiwa anataka ufalme wake na cheo chake kibakie. Akasema: Hamwoni ajabu eti hawa wananipa masharti yakubakia ufalme na cheo na wao wenyewe mnawaona walivyo na hali ya ufukara na udhalili?"

ASSALAMU ALAYKUM WA RAHMATULLAH

Na wanapokufikia wale wanaoamini ishara zetu waambie: Amani iwe juu yenu (Assalam alaykum), Mola wenu amejilazimisha rehema. Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) : "Mola wangu amenifundisha adabu, akaifanya nzuri adabu yangu." Ni adabu gani iliyo kama adabu ya Muumbaji wa mbingu na ardhi. Ni nafsi gani inayokuwa na kuleta matunda ya mafundisho ya Mwenyezi Mungu kuliko nafsi ya Muhammad?

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameifundisha nafsi hii njema na takatifu, ili kuiandaa na risala yake, risala ya rehema kwa viumbe ambayo kwayo na kwa mwenye nayo, zimetimia tabia njema.

Mwenyezi Mungu amemfundisha adabu Muhammad katika Aya kadhaa; ikiwemo Aya hii tuliyo nayo, ambayo inafundisha Mtume wa Mwenyezi Mungu na bora ya viumbe vya Mwenyezi Mungu, namna ya kufuatana na kuamiliana na wanyonge masikini.

Alikuwa akiwakabili kwa bashasha na makaribisho na kuwambia: Assalamu alykum (Amani iwe juu yenu), Mola wenu amejilazimisha rehema, Na alikuwa akiifunga nafsi yake kukaa nao maadamu wako mpaka waondoke wao.

Ikiwa Mtume ndiye aliyekusudiwa na Mwenyezi Mungu kwa mafunzo haya, basi sisi ndio tuliokusudiwa kufuata nyayo zake. Usimtukuze yeyote kwa mali au jaha au jinsi na rangi. Isipokuwa tumheshimu na kumtukuza kwa dini na tabia nzuri.

Baadhi ya wafasiri wapya wanasema: "Maisha ya watu kabla ya Muhammad(s.a.w.w) yalikuwa chini yenye kuwayawaya na Muhammad akayapandisha juu hadi kileleni; na hivi sasa yameondoka kwenye kilele kirefu na kuanguka huko New York, Washington na Chicago kwenye ubaguzi wa rangi."

Ndio! katika Usilam hakuna jinsia, rangi, jaha wala utajiri. Hakuna ubora katika Uislamu ila kwa takua. Kwa misingi hii ndipo inapopatikana siri ya kunyenyekea kwa wanavyuoni wa Kiislamu wanaofuatwa katika fatwa zao (marjaa). Mdogo na mkubwa anaweza kumfikia kwa njia ya usawa tu, bila ya kuweko bawabu au kizuizi na wanazungumza naye vile wanavyotaka na bila ya taklifu.

Ama baba mtakatifu (Papa) na wengineo katika viongozi wa dini, hakuna anayeota kukaa naye na kuzungumza naye ila waziri na wakubwa, tena amwekee wakati maalum na muda atakaozungumza naye.

Turudie kwenye kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: 'Na wanapokufikia wale wanaoamini ishara zetu waambie: Assalamu alaykum (Amani iwe juu yenu), Mola wenu amejilazimisha rehema.'

Assalamu alaykum warahmatullah, (Amani na rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yenu).

Haya ndiyo maamkuzi ya Kiislam, kumwombea unayemwamkua kuokoka na kila maovu na aishi kwa amani na utulivu na kwa rehema ya Mwenyezi Mungu na radhi zake, Kwani hakuna amani wala kuokoka ikiwa kuna ghadhabu yake Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ama ukiongozea Wa barakatuh (na baraka zake), utakuwa umemwombea mwenzako riziki pana.

Wapi na wapi maamkuzi ya marahaba, sabalkher na 'good night' na maamkuzi haya ya Mungu ya Kiislamu? Imetangulia kauli yake Mwenyezi Mungu; amejilazimisha rehema katika Aya 12 ya Sura hii. Na tukaeleza katika Tafsir yake kuwa rehema yake Mwenyezi Mungu Mtukufu haiepukani na dhati yake tukufu, sawa na uweza Wake na elimu Yake.

Ya kwamba atakayefanya miongoni mwenu uovu kwa ujinga, kisha akatubu baada yake na akatengenea.

Kuhusu toba, tumeweka mlango mahsusi kwa anuani ya toba na maumbile, katika kufasiri Juz.4 (4:18).

Basi yeye ndiye mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

Huyu ndiye Mola tunayemwabudu, husamehe mwenye kutubia na hurehemu waja. Kila mwenye kuwahurumia watu na akafanya kazi kwa ajili ya utengenevu wao, basi atakuwa amemwabudu Mwenyezi Mungu katika matendo yake; hata kama atapinga kwa ulimi wake. Na kila mwenye kuwaingilia watu katika haki zao, basi atakuwa amemkufuru Mwenyezi Mungu kivitendo, hata kama ataleta takbira na tahlili.

Namna hii tunazieleza ishara na ili njia ya wakosefu ibainike.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja katika Kitab chake sifa za watu wema, Vilevile ametaja sifa za wenye makosa ili lidhihirike kila kundi na alama yake. Zaidi ya hayo ni kwamba kujua moja ya vikundi viwili husababisha kujua kundi jingine; sawa na uongofu na upotevu.

﴿قُلْ إِنِّي نُهِيتُ أَنْ أَعْبُدَ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ قُل لَّا أَتَّبِعُ أَهْوَاءَكُمْ قَدْ ضَلَلْتُ إِذًا وَمَا أَنَا مِنَ الْمُهْتَدِينَ﴾

56.Sema: Nimekatazwa kuwaabudu wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu. Sema: Sifuati hawaa zenu, maana hapo nitapotea na sitakuwa miongoni mwa walioongoka. Sema: Nimekatazwa kuwaabudu wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu, Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameashiria njia ya wenye makosa, Katika Aya hii anaibainisha njia hiyo; kumwabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu.

﴿قُلْ إِنِّي عَلَىٰ بَيِّنَةٍ مِّن رَّبِّي وَكَذَّبْتُم بِهِ مَا عِندِي مَا تَسْتَعْجِلُونَ بِهِ إِنِ الْحُكْمُ إِلَّا لِلَّـهِ يَقُصُّ الْحَقَّ وَهُوَ خَيْرُ الْفَاصِلِينَ﴾

57.Sema: Hakika mimi ninayo dalili wazi itokayo kwa Mola wangu, nanyi mmeikadhibisha. Mimi sina haraka kwa mnayoyataka. Hapana hukmu ila ya Mwenyezi Mungu. Anasimulia yaliyo kweli; naye ni mbora wa wanaohukumu.

﴿قُل لَّوْ أَنَّ عِندِي مَا تَسْتَعْجِلُونَ بِهِ لَقُضِيَ الْأَمْرُ بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ وَاللَّـهُ أَعْلَمُ بِالظَّالِمِينَ﴾

58.Sema: Lau ningelikuwa nayo mnayotaka haraka, basi shauri lingekwisha baina yangu. na baina yenu Na Mwenyezi Mungu anawajua zaidi madhalimu.

SIFUATI HAWAA ZENU

Aya 56-58

MAANA

Sema: Nimekatazwa kuwaabudu wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu.

Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameashiria njia ya wenye makosa. Katika Aya hii anaibainisha njia hiyo; kumwabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu.

Sema: Sifuati hawaa zenu, maana hapo nitapotea na sitakuwa miongoni mwa walioongoka.

Kwa sababu kuomba kwao hakuna asili yoyote ila hawaa na upotevu, sasa vipi atafuata Mtume Mtukufu?

Sema:Hakika mimi ninayo dalili wazi itokayo kwa Mola wangu, nanyi mmeikadhibisha.

Yaani ninamwabudu Mwenyezi Mungu kwa ujuzi na nyinyi mnamkanusha; na mnaabudu masanamu kwa ujinga, Kwa mantiki gani mjuzi amfuate mjinga? Na mwenye batili amwongoze mwenye haki?

Sina haraka kwa mnayoyataka.

Mtume alipowatolea mwito wa kuamini walisema: "Tuletee mvua ya mawe kutoka mbinguni au tuletee adhabu kali."

Ndipo Mwenyezi Mungu akamwamrisha aseme: Sina haraka. Bali yako kwa Mwenyezi Mungu anaiteremsha wakati anaotaka wala mimi sina uwezo wa kuitanguliza au kuichelewesha.

Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu katika kuteremsha adhabu na kuitanguliza au kuiahirisha.

Anasimulia yaliyo kweli.

Yaani anasema kweli:Naye ni mbora wa wanaohukumu, hadhulumu yeyote katika hukumu yake.

Sema: Lau ningelikuwa nayo mnayotaka haraka katika adhabu, basi shauri lingekwisha baina yangu na baina yenu kwa kuangamizwa mwenye kudhulumu katika nyinyi

Na Mwenyezi Mungu anawajua zaidi madhalimu.

Huharakisha au kuchelewesha adhabu kulingana na vile inavyopitisha hekima yake.

10

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA SABA

﴿وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَمَا تَسْقُطُ مِن وَرَقَةٍ إِلَّا يَعْلَمُهَا وَلَا حَبَّةٍ فِي ظُلُمَاتِ الْأَرْضِ وَلَا رَطْبٍ وَلَا يَابِسٍ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ﴾

59.Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye; anajua kilichomo nchi kavu na kilichomo baharini; na halianguki jani ila analijua wala punje katika giza la ardhi; wala kibichi au kikavu, ila kimo katika Kitab kinachobainisha.

﴿وَهُوَ الَّذِي يَتَوَفَّاكُم بِاللَّيْلِ وَيَعْلَمُ مَا جَرَحْتُم بِالنَّهَارِ ثُمَّ يَبْعَثُكُمْ فِيهِ لِيُقْضَىٰ أَجَلٌ مُّسَمًّى ثُمَّ إِلَيْهِ مَرْجِعُكُمْ ثُمَّ يُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ﴾

60.Naye ndiye anayewafisha usiku. Na anakijua mlichokifanya mchana kisha huwafufua humo ili muda umalizike, Kisha kwake yeye ndiyo marejeo kwenu; kisha awaambiye mliyokuwa mkiyafanya.

﴿وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ وَيُرْسِلُ عَلَيْكُمْ حَفَظَةً حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ تَوَفَّتْهُ رُسُلُنَا وَهُمْ لَا يُفَرِّطُونَ﴾

61.Naye ndiye mwenye nguvu za kushinda juu ya waja wake, Na huwapelekea waangalizi, Hata mmoja wenu yakimjia mauti wajumbe wetu humfisha nao hawazembei.

﴿ثُمَّ رُدُّوا إِلَى اللَّـهِ مَوْلَاهُمُ الْحَقِّ أَلَا لَهُ الْحُكْمُ وَهُوَ أَسْرَعُ الْحَاسِبِينَ﴾

62.Kisha watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa haki. Hakika hukumu ni yake, naye ni mwepesi kuliko wote wanaohisabu.

HAZINA YA SIRI IKO KWAKE

Aya 59-62

MAANA

Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna aijuaye ila Yeye; anajua kilicho nchi kavu na kilicho baharini; na halianguki jani ila analijua wala punje katika giza la ardhi; wala kibichi au kikavu, ila kimo katika Kitab kidhihirishacho.

Yaani Mwenyezi Mungu anajua ulimwengu, yaliyotokea na yatakayotokea yote, ya kimada au ya kimaana. Ujuzi wake haufungiki na wakati, mahali au kuwa katika hali fulani kinyume na hali nyingine. Kwa sababu ujuzi wake ni wa kidhati si wa kuchuma; na dhati yake si ya wakati na mahali; wala haibadiliki kwa kubadilika matukio na hali.

Katika Hadith imeelezwa:"Hakika hazina za siri ni tano" Na Qura'n inasema:

﴿إِنَّ اللَّـهَ عِندَهُ عِلْمُ السَّاعَةِ وَيُنَزِّلُ الْغَيْثَ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْأَرْحَامِ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ﴾

"Hakika ujuzi wa Saa (Kiyama) uko kwa Mwenyezi Mungu. Naye huteremsha mvua, na anayajua yaliyo katika matumbo ya uzazi; na nafsi yoyote haijui itachuma nini kesho na nafsi yoyote haijui itafia nchi gani. (31:34)

Mwanafalsafa, Mulla Sadra anasema: "Vitu vyote vizima (kamili) au mafungu vinatiririka kutokana naye, naye ni msingi wa kila kilichopo, kiakili au kihisia na kwa kuwaza au kwa kuona. Na mtiririko wake kutokana naye hauepukani kuwa wazi mbele yake."

Allama Hilli anasema: "Kila kilichopo kisichokuwa Mwenyezi Mungu ni chenye kuwezekana, chenye kutegemezwa kwake. Atakuwa ni mwenye kukijua, ni sawa kiwe chote au baadhi; na ni sawa kiwe ni chenye kusimama hicho chenyewe au kwa kutegemea kingine, na ni sawa kiwe kiko machoni au mawazoni.

Kwa sababu kupatikana picha katika mawazo ni katika mambo yenye kuwa vilevile; kwa hiyo yanamtegemea Yeye. Na ni sawa picha hiyo ya mawazo iwe ni jambo lilioko au lisilokuwapo, linalowezekana au lisilowezekana. Ujuzi wake hauepukani na kitu chochote kiwezekanacho na kisichowezekana."

Naye ndiye anayewafisha usiku.

Kufa na mauti ni maneno mawili yenye maana moja katika kawaida ya ufahamu, nako ni kukosa uhai. Matamko yote mawili hutumiwa katika usingizi kimajazi. Kwa vile viungo hupumzika kufanya kazi kwa sababu ya usingizi. Na katika maana hayo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿اللَّـهُ يَتَوَفَّى الْأَنفُسَ حِينَ مَوْتِهَا وَالَّتِي لَمْ تَمُتْ فِي مَنَامِهَا فَيُمْسِكُ الَّتِي قَضَىٰ عَلَيْهَا الْمَوْتَ وَيُرْسِلُ الْأُخْرَىٰ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى﴾

"Mwenyezi Mungu huziua roho wakati wa mauti yake na zile ambazo hazijafikiwa na mauti katika usingizi. Basi huzizuia zile alizozipitishia mauti, na huzirudisha zile nyingine mpaka wakati uliowekwa" (39:42)

Y aani Mwenyezi Mungu anakata mawasiliano ya roho na mwili, kwa dhahiri na kwa hali halisi, wakati wa kufa na kuzizuia kwake. Uhusiano huu anaukata kwa dhahir, sio kwa hali halisi, wakati wa kulala; na wakati wa kuamka uhusiano huu unarudia kama ulivyokuwa na kubaki hadi wakati uliowekewa kufa kikweli. Kwa hiyo mwenye kulala ni maiti hai.

Makusudio ya kufa katika Aya hii ni mauti ya kimajazi. Imam Ali(a.s) anasema:"Roho ya mtu hutoka wakati wa kulala na kubaki miale yake mwilini, Kwa miale anaota ndoto. Akizinduka roho hurudi mara moja"

Na anayajua mlichokifanya mchana kisha huwafufua humo.

Humo ni mchana; na maana ya kuwafufua ni kuwaamsha usingizini. Wafasiri wamesema kuwa maneno haya ni dalili ya ufufuo na Kiyama. Kwa sababu usingizi unafanana na mauti, na kuamka kunafanana na kufufuka baada ya mauti.

Kisha kwake yeye ndiyo marejeo yenu; kisha awaambiye mliyokuwa mkiyafanya ya kheri na ya shari, katika usiku na mchana.

Kwa ufupi ni kwamba kila mtu anakufa kwa kwisha siku zake zilizoandikwa, kisha Mwenyezi Mungu atamfufua baada ya mauti, sawa na anavyomwamsha usingizini; kisha ailipe kila nafsi ilichokichuma na wao hawatadhulumiwa.

Ikiwa mtu atasema: Kwa nini Aya imehusisha kulala usiku na kufanya kazi mchana ambapo mtu mara nyingine hulala mchana na akafanya kazi usiku?

Tutamwambia Aya imekuja katika hali iliyo aghlab.

Naye ndiye mwenye nguvu za kushinda juu ya waja wake.

Inatosha kuwa amewazidi nguvu kwa vile wanadamu wanakuja katika maisha haya kwa nguvu na wanayaacha kwa nguvu. Imam Ali(a.s) anasema:"Hakuna chochote isipokuwa mmoja mwenye kushinda nguvu ambae kwake ni marejeo ya mambo yote yaliyoanza umbile lake bila ya kujiweza na yatakayokwisha bila ya kujizuia."

Na huwapelekea waangalizi.

Watunzaji hao ni Malaika. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

﴿وَإِنَّ عَلَيْكُمْ لَحَافِظِينَ ﴿١٠﴾ كِرَامًا كَاتِبِينَ ﴿١١﴾ يَعْلَمُونَ مَا تَفْعَلُونَ﴾

"Na hakika mna waangalizi, Watukufu wenye kuandika, Wanajua mnayoyatenda" (82:10-12)

Nasi tunaamini hayo, kwani Wahyi umeyaelezea na akili haiyakatai. Katika maneno ya Mwenyezi Mungu au ya Mtume haukuja ubainifu wa sifa za hao waandishi na maandishi; na akili hailazimishwi kufanya utafiti na kuuliza. Kwa hiyo tunayaacha katika ujuzi wake Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Ama kufananisha waandishi na polisi wa siri; kama ilivyo katika Tafsir Almanar na Maraghi, ni kama kufananisha ghaibu na yanayoonekana na kufananisha mbingu na ardhi ambazo zina tofauti kubwa.

Hata mmoja wenu yakimjia na mauti, wajumbe wetu humfisha nao hawazembei.

Utapata Tafsir yake katika Sura (32:11) Inshallah, Hayo vilevile ni katika mambo ya ghaibu yanayowezekana kiakili na yaliyothibiti Ki-Wahyi; sawa na watunzaji wanaoandika.

Kisha watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa haki ili wahukumiwe kwa hukumu Yake.

Hakika hukumu ni yake, naye ni mwepesi wa wanaohisabu.

Anahisabu, anahukumu na anatekeleza katika muda mchache sana. Kwa sababu haki iko wazi, hukumu itapitishwa na malipo yameandaliwa na kila kitu kitatimia kwa kutaka tu.

﴿قُلْ مَن يُنَجِّيكُم مِّن ظُلُمَاتِ الْبَرِّ وَالْبَحْرِ تَدْعُونَهُ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً لَّئِنْ أَنجَانَا مِنْ هَـٰذِهِ لَنَكُونَنَّ مِنَ الشَّاكِرِينَ﴾

63.Sema: Ni nani anyewaokoa katika viza vya nchi kavu na baharini? Mnamwomba kwa unyenyekevu na kwa sauti ndogo: Kama akituokoa na haya, hakika tutakuwa miongoni mwa wanaoshukuru.

﴿قُلِ اللَّـهُ يُنَجِّيكُم مِّنْهَا وَمِن كُلِّ كَرْبٍ ثُمَّ أَنتُمْ تُشْرِكُونَ﴾

64.Sema: Mwenyezi Mungu huwaokoa katika hayo na katika kila mashaka, Kisha nyinyi mnamshirikisha.

﴿قُلْ هُوَ الْقَادِرُ عَلَىٰ أَن يَبْعَثَ عَلَيْكُمْ عَذَابًا مِّن فَوْقِكُمْ أَوْ مِن تَحْتِ أَرْجُلِكُمْ أَوْ يَلْبِسَكُمْ شِيَعًا وَيُذِيقَ بَعْضَكُم بَأْسَ بَعْضٍ انظُرْ كَيْفَ نُصَرِّفُ الْآيَاتِ لَعَلَّهُمْ يَفْقَهُونَ﴾

65.Sema: Yeye ndiye awezaye kuwaletea adhabu kutoka juu yenu au kutoka chini ya miguu yenu; au awavuruge (muwe) makundi, na awaonjeshe baadhi yenu jeuri ya wenzao. Tazama jinsi tunavyozieleza ishara kwa njia mbali mbali ili wapate kufahamu.

﴿وَكَذَّبَ بِهِ قَوْمُكَ وَهُوَ الْحَقُّ قُل لَّسْتُ عَلَيْكُم بِوَكِيلٍ﴾

66.Na watu wako wameikadhibisha nayo ni haki. Sema: Mimi si kuwakilishwa juu yenu.

﴿لِّكُلِّ نَبَإٍ مُّسْتَقَرٌّ وَسَوْفَ تَعْلَمُونَ﴾

67.Kila habari ina wakati maalum, Na punde mtajua.

WAOKOA

Aya 63 - 67

MAANA

Sema: Ni nani anyewaokoa katika viza vya nchi kavu na baharini? Mnamwomba kwa unyenyekevu na kwa sauti ndogo.

Viza vya nchi kavu na baharini ni fumbo la shida na machungu anayoyapata mwanadamu katika mambo yote anayoyafanya bara na baharini; nasi tunaongezea (katika ufafanuzi wetu)'angani' baada ya kuwa katika zama za anga, ambako ni hatari zaidi kuliko nchi kavu na baharini.

Maana ni kuwa Ewe Mtume! Waulize Washirikina na Walahidi, ni nani wanayemkimbilia kumwomba katika saa ya dhiki na kumnyenyekea katika siri na dhahiri. Je,wanamkimbilia Mwenyezi Mungu au wanawakimbilia wanaowaabudu asiyekuwa Mungu?

Tumesema katika kufasiri Aya ya 41 katika Sura hii kwamba umbile la mtu linamtambua Muumbaji wake, lakini pazia ya kufuata na hawaa inauzuia mwanga wake machoni. Wakati wa shida inaondoka pazia hii na hutamka mtu kwa umbile lake safi. Hakuna yeyote anayeokoka na shida hii vyovyote alivyo, hata mwenye afya huogopa maafa na kuhofia mwisho mbaya, akiwa ana akili.

Imam Ali(a.s) anasema:"Mwenye shida sana hahitaji dua zaidi kuliko yule asiye na shida ambaye hasalimiki na balaa."

Kama akituokoa na haya, hakika tutakuwa miongoni mwa wanaoshukuru.

Yaani wanamfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu peke yake wakati wa shida na hofu na wanatoa ahadi wao wenyewe kuwa watampwekesha Mwenyezi Mungu na kumshukuru, kama akiwaokoa na viza vya nchi kavu na baharini. Mara tu wanaposalimika na kuwa katika starehe wanamshirikisha na kufanya ufisadi. Elimu imethibitisha kuwa udhaifu wa utu na matakwa yake unakwenda na hali; sawa na yalivyo maji hufuata rangi ya chombo yalimowekwa.

Sema: Mwenyezi Mungu huwaokoa katika hayo na katika kila mashaka.

Kwa hiyo ilikuwa ni juu yenu kuzitukuza neema za Mwenyezi Mungu na kuzishukuru.

Kisha nyinyi mnamshirikisha.

Lakini baada ya kuwaneemesha kwa kuokoka mmebadilisha neema ya Mwenyezi Mungu kwa ukafiri na shirki.

Sema: Yeye ndiye awezaye kuwaletea adhabu kutoka juu yenu. Au kutoka chini ya miguu yenu , kama mitetemeko na kudidimizwa ardhini,

Au awavuruge (muwe) makundi.

Yaani awachanganye-changanye na kuwafanya vikundi vinavyopondana visivyokuwa na msimamo; au amfanye mmoja wenu awe katika vita na ugomvi pamoja na nafsi yake, aridhie jioni yale yaliyomkasirisha asubuhi na kinyume, hali yake igongane wala asiwe na msimamo.

Na awaonjeshe baadhi yenu jeuri ya wenzao.

Yaani mpigane wenyewe kwa wenyewe.

Tazama jinsi tunavyozieleza ishara kwa njia mbali mbali ili wapate kufahamu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasimamisha hoja na dalili zilizo wazi juu ya haki, kwa hisia akili na maono, na anapiga mifano ya kila aina kwa mbinu mbali mbali ili waijue haki waifuate, na batili wajiepushe nayo; na atakayehalifu basi hoja imemsimamia na atastahiki adhabu.

Na watu wako wameikadhibisha nayo ni haki.

Msemo unaelekezwa kwa Mtume, dhamiri ya wameikadhibisha inarudia kwa Qur'an inayotamka dalili na hoja na adhabu ya mwenye kuikadhibisha.

Sema: Mimi si kuwakilishwa juu yenu.

Bali ni mtoa bishara na mwonyaji anayefikisha aliyotumwa na kumwachia Mwenyezi Mungu mambo ya hisabu na adhabu.

Kila habari ina wakati maalum.

Inawezekana Tafsir ya 'mahali maalum' Maana ni kuwa kila habari anayoitekeleza Mwenyezi Mungu ina wakati au mahali maalum bila ya kuhalifu.

Na punde mtajua wakati wa kutokea kwake. Hili ni kemeo na kiaga kwa kukadhibisha haki.

﴿وَإِذَا رَأَيْتَ الَّذِينَ يَخُوضُونَ فِي آيَاتِنَا فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ حَتَّىٰ يَخُوضُوا فِي حَدِيثٍ غَيْرِهِ وَإِمَّا يُنسِيَنَّكَ الشَّيْطَانُ فَلَا تَقْعُدْ بَعْدَ الذِّكْرَىٰ مَعَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ﴾

68.Na unapowaona wanaoziingilia Aya zetu basi jitenge nao mpaka waingie katika mazugumzo mengine. Na kama shetani akikusahaulisha, basi usikae baada ya kukumbuka pamoja na watu madhalimu.

﴿وَمَا عَلَى الَّذِينَ يَتَّقُونَ مِنْ حِسَابِهِم مِّن شَيْءٍ وَلَـٰكِن ذِكْرَىٰ لَعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ﴾

69.Wala si juu ya wale wenye takua hesabu yao hata kidogo, lakini ni mawaidha ili wapate kuwa na takua.

﴿وَذَرِ الَّذِينَ اتَّخَذُوا دِينَهُمْ لَعِبًا وَلَهْوًا وَغَرَّتْهُمُ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا وَذَكِّرْ بِهِ أَن تُبْسَلَ نَفْسٌ بِمَا كَسَبَتْ لَيْسَ لَهَا مِن دُونِ اللَّـهِ وَلِيٌّ وَلَا شَفِيعٌ وَإِن تَعْدِلْ كُلَّ عَدْلٍ لَّا يُؤْخَذْ مِنْهَا أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ أُبْسِلُوا بِمَا كَسَبُوا لَهُمْ شَرَابٌ مِّنْ حَمِيمٍ وَعَذَابٌ أَلِيمٌ بِمَا كَانُوا يَكْفُرُونَ﴾

70.Na waache wale walioifanya dini yao ni mchezo na upuuzi na yamewadanganya maisha ya dunia. Na wakumbushe kwayo, isije nafsi yoyote ikafungwa kwa sababu ya yale iliyoyachuma, Haina mlinzi wala mwombezi isipokuwa Mwenyezi Mungu, Na hata ikatoa kila fidia haitapokelewa. Hao ndio waliofungwa kwa sababu ya yale waliyoyachuma. Watapata kinywaji cha maji ya moto sana na adhabu chungu kwa sababu ya waliyokuwa wakiyakanusha .

MPAKAWAINGIE KATIKA MAZUNGUMZO MENGINE

Aya 68 - 70

MAANA

Na unapowaona wanaoziingilia Aya zetu basi jitenge nao mpaka waingie katika mazugumzo mengine.

Yamepita maelezo yake katika kufasiri Juz.5 (4:139)

Na kama shetani akikusahaulisha, basi usikae, baada ya kukumbuka, pamoja na watu madhalimu.

Msemo unaelekezwa kwa Mtume kwa dhahiri, lakini makusudio ni kwa mwingine kwa hali halisi. Kwa sababu Mtume ni mwenye kuhifadhiwa na madhambi na makosa na kusahau (maasum). Vinginevyo basi kauli yake na vitendo vyake na uthibitisho wake usingekuwa ni hoja na dalili mkato isiyokubali mjadala wala ubishi.

Wala si juu ya wale wenye takua hesabu yao hata kidogo, lakini ni mawaidha ili wapate kuwa na takua.

Yaani si juu ya waumini wanaomcha Mwenyezi Mungu chochote katika kufuatilia makafiri ambao wanaingilia Aya za Mwenyezi Mungu, lakini wawakumbushe na wawakataze ili wajiepushe kuingilia Aya za Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Ama Aya zifuatazo zina mambo yafuatayo:

Na waache wale walioifanya dini yao ni mchezo na upuuzi na yamewadanganya maisha ya dunia.

Kwa dhahiri amri inamwelekea Mtume na kwa hali ilivyo inamwelekea yeye na anayemfuata katika waumini. Anawaamrisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) waache kutangamana na wale ambao wameifanya dini yao ni mchezo na upuuzi na wala hakuwaamrisha kuwapuuza na kuacha kuwaonya. Kwa sababu kauli yake Mwenyezi Mungu:

Na wakumbushe kwayo ni amri ya kuwaonya.

Kila mwenye kuwa katika dini yoyote miongoni mwa dini na asiheshimu na kuitukuza misingi yake yote na hukumu zake zote, basi atakuwa ameifanya dini yake ni mchezo na upuzi. Mwenye kuifanyia dini chumo au akaita moja ya hukumu zake kwa namna ambayo inapelekea dharau, basi yeye atakuwa ndiye anayekusudiwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Walioifanya dini yao ni mchezo na upuzi.

Hakuna mwenye kutia shaka kuwa ambaye hana dini ni bora kuliko yule anayedharau misingi yake na hukumu zake. Kwa sababu huyu alivyo hasa ni kuwa ameifanyia dini mchezo na upuzi na hiyo ndiyo dini yake.

Na wakumbushe kwayo, isije nafsi yoyote ikafungwa kwa sababu ya yale iliyoyachuma. Haina mlinzi wala mwombezi isipokuwa Mwenyezi Mungu.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumwamrisha Mtume na waumini kutotangamana na wale walioifanyia mchezo dini yao, aliwaamrisha kuwakumbusha Qur'an wale ambao wanaingilia Aya za Mwenyezi Mungu na kucheza na dini ili wasiadhibiwe kwa yale makosa na madhambi yaliyo chumwa na mikono yao, katika siku ambayo hawatapata msaidizi wa kuwasaidia asiyekuwa Mwenyezi Mungu wala mwombezi atakayewaombea mbele ya Mwenyezi Mungu.

Na hata ikatoa kila fidia haitapokelewa.

Yaani kama ambavyo kafiri hatapata mlinzi wala mwombezi siku ya Kiyama, vilevile haitakubaliwa fidia yake kwa namna yoyote itakavyokuwa. Amesema Razi: "Mtu akifikiri namna ya adhabu kwa njia hii atakurubia kugwaya anapothubutu kumwasi Mwenyezi Mungu."

Hao ndio waliofungwa kwa sababu ya yale waliyoyachuma. Watapata kinywaji cha maji ya moto sana na adhabu chungu kwa sababu ya waliyokuwa wakiyakanusha.

Hao ni ishara ya wale walioifanyia mchezo dini. Na kufungika kwa waliyoyachuma; yaani wamewekwa rahani na matendo yao. Ama kupata kinywaji cha maji ya moto sana, ni kubainisha adhabu ya ukafiri wao na uasi wao.