TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA Juzuu 7

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA 0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 13164
Pakua: 2195


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 16 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 13164 / Pakua: 2195
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA Juzuu 7

Mwandishi:
Swahili

11

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA SABA

﴿قُلْ أَنَدْعُو مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُنَا وَلَا يَضُرُّنَا وَنُرَدُّ عَلَىٰ أَعْقَابِنَا بَعْدَ إِذْ هَدَانَا اللَّـهُ كَالَّذِي اسْتَهْوَتْهُ الشَّيَاطِينُ فِي الْأَرْضِ حَيْرَانَ لَهُ أَصْحَابٌ يَدْعُونَهُ إِلَى الْهُدَى ائْتِنَا قُلْ إِنَّ هُدَى اللَّـهِ هُوَ الْهُدَىٰ وَأُمِرْنَا لِنُسْلِمَ لِرَبِّ الْعَالَمِينَ﴾

71.Sema: Je, tuwaabudu wasiokuwa Mwenyezi Mungu ambao hawatunufaishi wala kutudhuru? Na turudishwe nyuma baada ya Mwenyezi Mungu kutuongoza? Kama yule ambaye mashetani wamempoteza; akiwayawaya katika ardhi, Anao marafiki wanaomwita kwenye uongofu: Njoo kwetu. Sema: Mwongozo hasa ni mwongozo wa Mwenyezi Mungu. Na tumeamrishwa tusilimu kwa Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe vyote.

﴿وَأَنْ أَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَاتَّقُوهُ وَهُوَ الَّذِي إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ﴾

72.Na simamisheni Swala na mcheni yeye; naye ndiye ambaye kwake mtakusanywa.

﴿وَهُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ وَيَوْمَ يَقُولُ كُن فَيَكُونُ قَوْلُهُ الْحَقُّ وَلَهُ الْمُلْكُ يَوْمَ يُنفَخُ فِي الصُّورِ عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْخَبِيرُ﴾

73.Naye ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi kwa haki, Na siku anayosema 'kuwa' basi huwa. Kauli yake ni haki. Na ufalme ni wake siku itakapopulizwa parapanda.

SEMA: JE: TUWAABUDU WASIOKUWA MWENYEZI MUNGU?

Aya 71-73

MAANA

Sema: Je, tuwaabudu wasiokuwa Mwenyezi Mungu ambao hawatunufaishi wala kutudhuru?

Mtume(s.a.w.w) aliwalingania washirikina katika kumwabudu Mwenyezi Mungu; nao wakamtaka aabudu masanamu yao. Inasemekana kwamba walitoa rai ya kuwa waabudu nao waungu wao na wao waabudu naye Mola wake.

Kwa vyovyote itakavyokuwa ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimwamrisha, katika Aya hii, kuwaambia kwa kukanusha, vipi tuache kumwabudu Mwenyezi Mungu anayenufaisha na kudhuru na tuabudu wale wasiojiweza wao wenyewe kujinufaisha au kujikinga na madhara?

Na turudishwe nyuma baada ya Mwenyezi Mungu kutuongoza.

Kurudi nyuma ni neno linalotumiwa kwa mtu aliyeiacha haki akafuata batili.

Kama yule ambaye mashetani wamempoteza; akiwayawaya katika ardhi. Anao marafiki wanaomwita kwenye uongofu: Njoo kwetu.

Huu ni mfano anaoutoa Mwenyezi Mungu kwa aliyekataa Tawhid na kwenda kwenye ushirikina au ulahidi. Kwa ufupi nikuwa mfano wa mtu huyu ni kama mfano wa mtu aliyekuwa katika msafara unakwenda kwa amani na salama.

Akauacha na akafuata njia yake jangwani bila ya mwelekeo wowote; kama ambaye amezungwa na mashetani. Basi wenzake wakamhurumia na kumwita: 'Njoo kwetu, hii ndiyo njia ya uongofu', lakini asiwajibu kwa kubabaika kwake. Ikawa mwisho wake ni balaa na maangamivu.

Mjuzi wa ghaibu na yanayoonekana, Naye ndiye mwenye hekima mwenye habari.

Sema: Mwongozo hasa ni mwongozo wa Mwenyezi Mungu.

Muundo huu wa kiubainifu unafahamisha kuwa mwongozo wa Mwenyezi Mungu haungiliwi na shaka yoyote; kama ambavyo unafahamisha kuwa mwongozo ni wa Mwenyezi Mungu peke yake katika kila kitu - katika itikadi sharia maadili na hali. Itikadi yoyote au fikra yoyote au kazi yoyote isiyokutana na mwongozo wa Mwenyezi Mungu basi ni ujinga na upotevu.

Na tumeamrishwa tusilimu kwa Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe vyote.

Hii ni katika kutaja mahsusi baada ya ujumla. Kwa sababu mwongozo wa Mwenyezi Mungu unaingia katika kila aliloamrisha Mwenyezi Mungu na kulikataza. Makusudio ya kuuhusisha Uislamu ni kukumbusha utukufu wake.

Na simamisheni swala.

Kwani hakuna mwongozo wala Uislam ila kwayo; ndiyo nguzo ya dini, ikikubaliwa hukubaliwa mengine na ikikataliwa hukataliwa mengine.

Na mcheni yeye Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu. Ameamrisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) takua baada ya kuamrisha swala, Kwa sababu hakuna swala wala imani sahihi bila ya takua, Kumwabudu Mwenyezi Mungu kweli ni kwenda kwenye njia yake na kumtii katika hukumu zote, sio baadhi tu.

Naye ndiye ambaye kwake mtakusanywa.

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:"Na itakuja kila nafsi pamoja na mwendeshaji na shahidi" (50:21).

Mwendeshaji atakayeiendesha hadi mahshar (watakapokusanya watu) na shahidi atakayeishuhudilia kwa yale yaliyoandaliwa kwa siku hii.

Naye ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi kwa haki.

Haki hapa ni ishara ya kuwa ulimwengu una kanuni zinazouhukumu na desturi inayokwenda nao kwa mpangilio bila ya mkorogano wowote. Hii ni dalili fasaha ya kuweko mpangaji wa mambo na atakayeilipa kila nafsi ililochuma.

Na siku anayosema 'kuwa' basi huwa, Kauli yake ni haki.

Katika maneno haya kuna kukadiriwa, kutangulizwa, na kuwekwa nyuma. Asili yake ni hivi: Kauli yake ni haki siku anapokiambia kitu kuwa, huwa. Maana yake ni kuwa kauli ya Mwenyezi Mungu inakuwa tu; na hudhihirika wazi hilo siku anapokiambia kitu kuwa, kikawa, Ni sawa aliyasema haya siku alipoanza kuumba viumbe au siku atakapowarudisha.

Kwa maneno mengine ni kuwa kauli ya Mwenyezi Mungu ndiyo kitendo chake katika kupatikana kitu bila ya kitu, na katika kukirudisha jinsi kilivyokuwa baada ya kuharibika na kuchangukana.

Na ufalme ni wake siku itakapopulizwa parapanda.

Kupulizwa parapanda ni fumbo la kufufuliwa walio makaburini. Na maana ya ufalme wa ufufuo huu ni kwamba yeye ndiye anayerudisha wafu kwenye uhai.

MASUFI

Mjuzi wa ghaibu na yanayoonekana.

Ghaibu ni mambo ya siri yaliyojificha, kama vile Malaika, ufufuo na mambo anayoyaficha mtu nafsini mwake. Na dhahiri ni yale yanayoonekana kidhahiri, kama vile ardhi, mbingu na anayoyafanya mtu wazi wazi.

Haya kwa binadamu ni sawa; ama kwa Mwenyezi Mungu hakuna ghaibu si katika mbingu wala ardhi, Hata hivyo masufi wanadai kuwa nafsi zao zinafichua ghaibu.

Ibn Al-Arabi, katika Futuhatil- makkiya mlango wa 302, anasema: "Hakika watu wa Mwenyezi Mungu wana macho wanayoonea na masikio wanayosikizia na nyoyo wanazofahamia na ndimi wanazosemea; si macho haya wala masikio au nyoyo na ndimi hizi. Kwa macho hayo wanaona na kwa masikio hayo wanasikia na kwa nyoyo hizo wanafahamu na kwa ndimi hizo wanasema na maneno yao yanapatia"

Naye ndiye mwenye hekima mwenye habari.

Yeye tu peke yake hana mshirika katika kupangilia mamabo ya viumbe vyake kulingana na heima yake na katika kujua siri zote. Basi hebu naamuogope Mwenyezi Mungu yule anayedai kuwa ana nyoyo mbili, ndimi mbili, macho mane na masikio mane.

﴿وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ لِأَبِيهِ آزَرَ أَتَتَّخِذُ أَصْنَامًا آلِهَةً إِنِّي أَرَاكَ وَقَوْمَكَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ﴾

74.Na Ibrahim alipomwambia baba yake Azar: Unawafanya masanamu kuwa waungu? Hakika ninakuona wewe na watu wako mko katika upotofu ulio wazi.

﴿وَكَذَٰلِكَ نُرِي إِبْرَاهِيمَ مَلَكُوتَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلِيَكُونَ مِنَ الْمُوقِنِينَ﴾

75.Na namna hii tukamwonyesha Ibrahim ufalme wa mbingu na ardhi ili awe katika wenye yakini.

﴿فَلَمَّا جَنَّ عَلَيْهِ اللَّيْلُ رَأَىٰ كَوْكَبًا قَالَ هَـٰذَا رَبِّي فَلَمَّا أَفَلَ قَالَ لَا أُحِبُّ الْآفِلِينَ﴾

76.Na usiku ulipomwingilia, akaona nyota, alinena: Hii ni Mola wangu. Ilipotua akasema: Sipendi wanaotua.

﴿فَلَمَّا رَأَى الْقَمَرَ بَازِغًا قَالَ هَـٰذَا رَبِّي فَلَمَّا أَفَلَ قَالَ لَئِن لَّمْ يَهْدِنِي رَبِّي لَأَكُونَنَّ مِنَ الْقَوْمِ الضَّالِّينَ﴾

77.Na alipouona mwezi unachomoza alisema: Huu ni Mola wangu. Ulipotua alisema: Asiponiongoza Mola wangu, hakika nitakuwa katika watu waliopotea.

﴿فَلَمَّا رَأَى الشَّمْسَ بَازِغَةً قَالَ هَـٰذَا رَبِّي هَـٰذَا أَكْبَرُ فَلَمَّا أَفَلَتْ قَالَ يَا قَوْمِ إِنِّي بَرِيءٌ مِّمَّا تُشْرِكُونَ﴾

78.Na alipoliona jua linachomoza alisema: Hili ndilo Mola wangu. Hili ni kubwa kabisa. Lilipotua alisema: Enyi watu! Mimi simo katika hayo mnayoyashirikisha.

﴿إِنِّي وَجَّهْتُ وَجْهِيَ لِلَّذِي فَطَرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ حَنِيفًا وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ﴾

79.Hakika mimi nimeuelekeza uso wangu kwa yule aliyeziumba mbingu na ardhi. Hali ya kuwa nimeacha dini za upotevu, tena mimi si katika washirikina.

IBRAHIM NA BABA YAKE NAWATU WAKE

Aya 74-79

MAANA

Na Ibrahim alipomwambia baba yake Azar: Unawafanya masanamu kuwa waungu? Hakika ninakuona wewe na watu wako mko katika upotofu ulio wazi.

Dhahiri ya Aya inafahamisha waziwazi kuwa Azar ni baba hasa wa Ibrahim Khalil(a.s) ; na kwamba alikuwa mshirikina muabudu masanamu; na kwamba Ibrahim alimkataza ushirikina na akamlingania kwenye Tawhid. Huu ndio ufahamisho wa Aya unaofahamika mara moja kwenye fahamu ya mjuzi na mjinga, bila ya kuweko ufafanuzi au tafsir.

Pamoja na hayo wafasiri wamerefusha maneno na wakatofautiana kuwa je, Azar ni baba hasa wa Ibrahim au ni baba yake kimajazi.

Tofauti hii inazalisha tofauti nyingine kuwa je mababa na mababu wote wa Muhammad(s.a.w.w) waliamini Mungu mmoja na wala haifai kuweko mshirikina hata mmoja, au inawezekana kuweko washirikina na wapwekeshaji? Baadhi ya maulama wametunga vitabu maalum vya hilo tu.

Shia wanasema baba na mababu zake wote Muhammad ni wapwekeshaji Mungu kutokana na Hadith isemayo:"Niliendelea kugura kutoka migongo ya watakatifu mpaka kwenye mifuko ya uzazi ya watakatifu hadi akanitoa Mwenyezi Mungu kwenye ulimwengu wenu huu."

Wakasema kuwa baba hasa wa Ibrahim anaitwa Tarik na kwamba Azar ni ndugu wa baba yake au babu yake wa upande wa mama yake, amepewa jina la baba kimajazi tu[8] .

Al-Alusi anasema, "Kundi kubwa la Sunni pia wanasema hivyo" Lakini mwenye Tafsir Al-manar na Razi wanasema: "Sunni hawaafikiani na Shia kwenye rai yao hii na wanasema inawezekana kuweko washirikina au walahidi katika mababu wa Mtume."

Dhahiri ya Qur'an iko pamoja nao, hasa kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿وَاذْكُرْ فِي الْكِتَابِ إِبْرَاهِيمَ إِنَّهُ كَانَ صِدِّيقًا نَّبِيًّا ﴿٤١﴾ إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ يَا أَبَتِ لِمَ تَعْبُدُ مَا لَا يَسْمَعُ وَلَا يُبْصِرُ وَلَا يُغْنِي عَنكَ شَيْئًا﴾

"Na mtaje Ibrahim katika Kitab, Hakika yeye alikuwa mkweli sana, Nabii, Alipomwambia baba yake: Ee baba yangu! Kwa nini unaabudu visivyosikia na visivyoona na visivyokufaa chochote" (19: 41-42)

Kwa vyovyote iwavyo hakuna faida ya mzozo huu, kwa sababu hauna uhusiano wowote na itikadi ya Kiislamu. Kwa sababu linalotakikana kwa Mwislamu ni kuamini Utume wa Muhammad(s.a.w.w) na Isma yake na kwamba yeye ni bwana wa Mitume na ni wa mwisho wao. Ama kuamini kuwa baba na mababu zake wote ni wapwekeshaji Mwenyezi Mungu, na kwamba Azar ni ami wa Ibrahim na sio baba yake, Yote haya si chochote katika itikadi ya Kiislamu.

Na namna hii tukamwonyesha Ibrahim ufalme wa mbingu na ardhi.

Makusudio ya 'namna hii' ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) kama ambavyo alimfichulia Ibarahim upotevu wa watu wake wa kuabudu kwao masanamu, pia alimfunulia maajabu ya mbingu na ardhi ili atoe dalili, kwa ustadi wa nidhamu yake na ufundi wa utengenezwaji wake, juu ya kuweko Mwenyezi Mungu, umoja wake na utukufu wake na awe miongoni mwa wenye yakini.

Aya hii inafahamisha mambo mawili:

Kwanza : itikadi ya Uislamu inaismamia uhuru wa rai na akili. Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakuwajibisha mtu kumwamini ila baada ya kumwekea hoja na akataka afanye uchunguzi.

Pili : kuwa dalili aliyoiweka juu ya kuweko kwake ni nyepesi na sahali kufahamiwa na watu wote bila ya kuhitaji juhudi wala sayansi au falsafa. Yatosha mtu kuangalia maajabu ya ulimwengu na utaratibu wake ili aweze kuongoka kwa Muumbaji wake na mtegenezaji wake.

Na usiku ulipomwingilia, akaona nyota, alinena: Hii ni Mola wangu.

Watu wa Ibrahim walikuwa wakiabudu nyota badala ya Mwenyezi Mungu. Akataka kuwavuta kidogo kidogo kwenye haki na kuwaelekeza kwenye mantiki ya kiakili na kimaumbile kwa upole na ulaini. Akangoja mpaka usiku ulipoingia na kufunga giza, akaona nyota wanazoziabudu. Akasema kwa kuigiza madai yao: 'Huyu ni Mola wangu'. Wakamwamini, lakini ilipotua na kupotea pambizoni, akili zao zilizinduka na mtazamo wao ukaona kuwa Mwenyezi Mungu habadiliki wala kugeuka na wala hifichwi na chochote.

Na alipouona mwezi unachomoza alisema kwa kutaka kuwavuta:Huu ni Mola wangu , kwa sababu ni mkubwa na una mwangaza zaidi kuliko ule wa kwanza.

Ulipotua alisema: Asiponiongoza Mola wangu, hakika nitakuwa katika watu waliopotea.

Anaashiria kuwa yeye bado hajatulizwa nafsi yake na nyota hizii; na kwamba yeye bado hajaongoka kwenye njia na akamtaka Mwenyezi Mungu amwokoe.

Na alipoliona jua linachomoza alisema: Hili ndilo Mola wangu. Hili ni kubwa kabisa. Lilipotua alisema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika hayo mnayoyashirikisha.

Jaribio la kwanza, la pili na la tatu yamepita na shaka ikabakia kama ilivyokuwa. Kwa hiyo hapana budi kujiepusha na kuabudu nyota, Kwani hazistahiki kuabuduiwa wala kutukuzwa. Baada ya kutangaza kujitoa katika waungu wao aliuelekeza moyo wake kwa Muumba wa ulimwengu na akasema:

Hakika mimi nimeuelekeza uso wangu kwa yule aliyeziumba mbingu na ardhi, hali ya kuwa nimeacha dini za upotevu, tena mimi si katika washirikina.

Hii ndiyo natija ya utafiti na kufikiria katika kitu chochote miongoni mwa vitu vya ulimwengu huu. Mtazamo mmoja tu, wa kuangalia sura yoyote katika sura za ulimwengu huu, lazima utapelekea kwenye yakini ya mkato kuwa Mwenyezi Mungu pekee yake ndiye Muumba wa mbingu na ardhi.

﴿وَحَاجَّهُ قَوْمُهُ قَالَ أَتُحَاجُّونِّي فِي اللَّـهِ وَقَدْ هَدَانِ وَلَا أَخَافُ مَا تُشْرِكُونَ بِهِ إِلَّا أَن يَشَاءَ رَبِّي شَيْئًا وَسِعَ رَبِّي كُلَّ شَيْءٍ عِلْمًا أَفَلَا تَتَذَكَّرُونَ﴾

80.Na watu wake wakamhoji. Akasema: Je, mnanihoji juu ya Mwenyezi Mungu na hali yeye ameniongoza? Wala siogopi wale mnaowashirikisha naye; isipokuwa Mola wangu akitaka kitu, Mola wangu ana wasaa wa kujua kila kitu. Je, hamkumbuki.

﴿وَكَيْفَ أَخَافُ مَا أَشْرَكْتُمْ وَلَا تَخَافُونَ أَنَّكُمْ أَشْرَكْتُم بِاللَّـهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ عَلَيْكُمْ سُلْطَانًا فَأَيُّ الْفَرِيقَيْنِ أَحَقُّ بِالْأَمْنِ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ﴾

81.Nitaogopaje hao mnaowashirikisha, na hali nyinyi hamwogopi kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kile ambacho hakukiteremshia dalili kwenu? Basi kundi gani katika mawili haya linastahiki kupata amani kama nyinyi mnajua?

﴿الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُم بِظُلْمٍ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ الْأَمْنُ وَهُم مُّهْتَدُونَ﴾

82.Wale walioamini na hawakuchanganya imani yao na upotevu, hao ndio watakaopata amani na ndio walioongoka. 83. Na hiyo ndiyo hoja yetu tuliyompa Ibrahim juu ya watu wake. Tunamuinua kwa vyeo yule tumtakaye, Hakika Mola wako ndiye mwenye hekima, Mjuzi.

JE, MNANIHOJI JUU YA MWENYEZI MUNGU

Aya 80 – 83

LUGHA

Neno 'hoja' linatumika kwa maana ya dalili zenye kuthibitisha haki; na hutumiwa kwa maana yale anayoyatolea hoja mdai kuthibitisha madai yake.

MAANA

Na watu wake wakamhoji.

Baada ya Ibrahim kuwapatia watu wake hoja inayoingia akilini kutokana na mantiki ya kiakili na kimaumbile, na kuthibitisha uharibifu na ibada yao ya mizimu na nyota, baada ya yote hayo nao walileta hoja zao dhaifu. Wakasema miongoni mwa waliyoyasema:

﴿قَالُوا وَجَدْنَا آبَاءَنَا لَهَا عَابِدِينَ﴾

"Tumewakuta baba zetu wakiyaabudu" (21:53)

Ndipo Ibrahim akawajibu kwa kusema:

Je, mnanihoji juu ya Mwenyezi Mungu na hali yeye ameniongoza?

Yaani ni hoja gani hizi kuhusu Mwenyezi Mungu na hali yeye ameniongoza kumjua kutokana na nafsi yangu na ulimwengu. Imetangulia katika sura hii Aya ya 71:

﴿قُلْ إِنَّ هُدَى اللَّـهِ هُوَ الْهُدَىٰ﴾

"Sema: Mwongozo hasa ni mwongozo wa Mwenyezi Mungu" (6:71) Ambao hauna shaka yoyote, vinginevyo ni ujinga na upotevu. Ama kuhofisha waungu wao alikujibu kwa kusema:Wala siogopi wale mnaowashirikisha naye wasiokuwa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu hawadhuru wala hawanufaishi, hawoni wala hawasikii,Isipokuwa Mola wangu akitaka chochote kwa kuniangushia sanamu kichwani kwangu linivunje fuvu, au kimondo cha nyota kitakachoniunguza.

Mola wangu ana wasaa wa kujua kila kitu.

Kwa hiyo siogopi kuwa nitapatwa na jambo lolote baya bila ya kujua yeye au kutaka.

Je, hamkumbuki kuwa miungu yenu si chochote na kwamba Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mwenye kudhuru na kunufaisha. Kwa sababu yeye ni Muumbaji wa kila kitu.

Nitaogopaje hao mnaowashirikisha, na hali nyinyi hamwogopi kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kile ambacho hakukiteremshia dalili kwenu?

Makusudio ya mliowashirikisha ni masanamu na nyota mnaoziabudu. Maana nikuwa mnataka niwaogope waungu wenu walioumbwa wanaoshindwa na nyinyi hamwogopi madai yenu ya kumfanyia Mungu washirika, madai ambayo ni uzushi usiokuwa na hoja wala dalili!

Kwa maneno mengine, Ibrahim aliwaambia je, mnanihofisha kwa wale wasiokuwa na uwezo, na nyinyi mmejiamini na kumfanyia uzushi yule mwenye nguvu na uwezo kwa wote?

Basi kundi gani katika mawili haya linastahiki kupata amani kama nyinyi mnajua?

Kundi linalomwamini Mwenyezi Mungu mwenye nguvu, mwenye kushinda, au linaloamini udhaifu ulio dhalili?

Wale walioamini na hawakuchanganya imani yao na upotevu, hao ndio watakaopata amani na ndio walioongoka.

Huu ni ubainifu wa kundi lililookoka katika makundi mawili na kwamba wao ndio waliomfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu katika imani yao na hawakuchanganya na imani hii kushirikisha katika itikadi wala katika kutii hawaa za kiumbe yeyote awaye. Hawa peke yao ndio waliosalimika, wenye kuongoka.

Na hiyo ndiyo hoja yetu tuliyompa Ibrahim juu ya watu wake.

Yaani hizo ndizo hoja ambazo tumemtia ilham Ibrahim , zinazoingia bongoni ambazo aliwahshinda nazo Ibrahim watu wake. Aya hii ni dalili wazi kwamba Mitume na wale wanaoongozwa na mwongozo wao katika maulama, ni maneno ya Mwenyezi Mungu na ubainifu wake; na kwamba kuwapinga ni kumpinga Mwenyezi Mungu hasa; kama ilivyoelezwa katika Hadith.

Tunamuinua kwa vyeo yule tumtakaye.

Utaipata Tafsir yake katika Juz 28 (58:11.) inshaallah Sababu ya kuinuliwa mtu kwa Mwenyezi Mungu ni imani na elimu, na kila moja katika hayo ina daraja ya juu na ya juu zaidi. Ibrahim alifikia ile ya juu zaidi mpaka akawa rafiki wa Mwenyezi Mungu (Khalilullah).

Hakika Mola wako ndiye mwenye hekima, Mjuzi.

Mwenye hekima aliyetakata na mchezo na matamanio, anajua anayostahiki kila mtu katika daraja na vyeo.

12

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA SABA

﴿وَوَهَبْنَا لَهُ إِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ كُلًّا هَدَيْنَا وَنُوحًا هَدَيْنَا مِن قَبْلُ وَمِن ذُرِّيَّتِهِ دَاوُودَ وَسُلَيْمَانَ وَأَيُّوبَ وَيُوسُفَ وَمُوسَىٰ وَهَارُونَ وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ﴾

84.Na tukampa Is-haq na Yaqub Kila mmoja tulimuongoza, Na Nuh tulimwongoza zamani. Na katika kizazi chake Daud na Suleiman na Ayyub na Yusuf na Musa na Harun. Na kama hivyo tunawalipa wafanyao mema.

﴿وَزَكَرِيَّا وَيَحْيَىٰ وَعِيسَىٰ وَإِلْيَاسَ كُلٌّ مِّنَ الصَّالِحِينَ﴾

85.Na Zakariya na Yahya na Isa na Ilyas; wote ni katika wema.

﴿وَإِسْمَاعِيلَ وَالْيَسَعَ وَيُونُسَ وَلُوطًا وَكُلًّا فَضَّلْنَا عَلَى الْعَالَمِينَ﴾

86.Na Ismail na Al-yasaa na Yunus na Lut; na kila mmoja tulimfadhilisha juu ya walimwengu wote.

﴿وَمِنْ آبَائِهِمْ وَذُرِّيَّاتِهِمْ وَإِخْوَانِهِمْ وَاجْتَبَيْنَاهُمْ وَهَدَيْنَاهُمْ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ﴾

87.Na katika baba zao na vizazi vyao na ndugu zao na tukawachagua na kuwaongoza katika njia iliyonyooka.

﴿ذَٰلِكَ هُدَى اللَّـهِ يَهْدِي بِهِ مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴾

88.Huo ni uongozi wa Mwenyezi Mungu, Kwa huo humwongoza amtakaye katika waja wake. Na kama wangelishirikisha bila shaka yangeliporomoka yale waliyokuwa wakiyatenda.

﴿أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ وَالْحُكْمَ وَالنُّبُوَّةَ فَإِن يَكْفُرْ بِهَا هَـٰؤُلَاءِ فَقَدْ وَكَّلْنَا بِهَا قَوْمًا لَّيْسُوا بِهَا بِكَافِرِينَ﴾

89.Hao ndio tuliowapa Kitab na hukumu na utume. Kama hawa wakiyakataa, basi tumekwisha yawakilisha kwa watu wasioyakataa.

﴿أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ هَدَى اللَّـهُ فَبِهُدَاهُمُ اقْتَدِهْ قُل لَّا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ أَجْرًا إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرَىٰ لِلْعَالَمِينَ﴾

90.Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewaongoza, basi fuata mwongozo wao. Sema: Siwaombi ujira juu ya haya. Haikuwa hiyo ila ni mawaidha kwa waimwengu wote.

NA TUKAMPA IS-HAQ NA YAQ'UB

Aya 84 - 90

MAANA

Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Aya hizi ametaja Mitume 18 akiwemo Ibrahim, Baadhi akawaashiria kwa baba zao, vizazi vyao na ndugu zao. Na amewasifu wote kwa hisani, wema na uongofu, na kwamba yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaneemesha Mitume waliotajwa kwa hekima na Unabii na baadhi yao akawaneemesha kwa kuteremshiwa Kitab.

Makusudio katika hayo ni kutoa hoja Muhammad(s.a.w.w) kwa Waarabu kwamba babu yao ni Ibrahim na wanawe wengi walikuwa wenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu.

Vilevile Mtume afuate nyayo za Mitume waliotangulia katika kulingania kwa Mwenyezi Mungu na kuvumilia adha. Huu ndio muhtasari wa madhumuni ya Aya hizi saba.

Uko wazi usiohitaji ubainifu wa kurefusha na ufafanuzi, lakini baadhi ya wafasiri wamekataa ila kurefusha, wakatoka nje ya maudhui ya Tafsir kufikia ambako hakuna uhusiano wowote na maisha.

Ni vizuri ifahamike kuwa majina ya Mitume yaliyotajwa katika Aya hayakuja kwa mpangilio wa wakati au ubora; kama ambavyo wametajwa kwa njia ya mifano tu.

Na tukampa Is-haq na Yaqub.

Dhamir ya 'tukampa' inamrudia Ibrahim. Is-haq ni mwanawe wa kumzaa na mama yake ni Sara. Yaqub ni mwana wa Is-haq, na mwana wa mwana ni mwana. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿فَبَشَّرْنَاهَا بِإِسْحَاقَ وَمِن وَرَاءِ إِسْحَاقَ يَعْقُوبَ﴾

"Basi tukambashiria Is-haq na baada ya Is-haq ni Yaqub." (11:71)

Kila mmoja Is-haq na Yaqubtulimuongoza .

Na Nuh tulimwongoza zamani kwani yeye ni wa zamani kuliko Ibrahim.

Na katika kizazi chake.

Dhamir inamrudia Nuh, yaani na kizazi cha Nuh, kwa sababu ndiye wa karibu kutajwa, Imesemekana kuwa inamrudia Ibrahim.

Daud na Suleiman na Ayyub na Yusuf na Musa na Harun.

Yaani wote hawa tumewaongoa kama tulivyomwongoza Nuh, Is-haq na Yaqub.

Na kama hivyo tunawalipa wafanyao mema.

Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamlipa mwema kwa wema, awe Mtume au sio Mtume; kama anavyomlipa mwovu kwa amali yake awe mweupe au mweusi. Na Zakariya na Yahya na Isa na Ilyas. Hawa vilevile ni katika aliowaongoza Mwenyezi Mungu.

Wote ni katika watu wema.

Na kila mwenye kutumia kipawa chake kwa kheri yake na kheri ya watu basi yeye ni mwema na mtengenevu.

HASAN NA HUSEIN NI WANAWA MTUME

Anasema Razi katika Tafsir yake kuhusu Aya hii: "Hakika Aya hii inafahamisha kuwa Hasan na Hussein ni katika kizazi cha Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) .

Kwa sababu Mwenyezi Mungu amemjaalia Isa ni katika kizazi cha Ibrahim, ingawaje yeye amenasibiana na Ibrahim kwa upande wa mama tu. Vilevile Hasan na Hussein ni katika kizazi cha Mtume wa Mwenyezi Mungu ingawaje wananasibika na Mtume kwa mama. Inasemekana kuwa Abu Jafar Al-Baqir, aliitolea dalili Aya hii mbele za Hajjaj bin Yusuf."

Mwenye Tafsir Al-Manar anasema: "Ninasema katika mlango wa Hadith Abu Bukra kwa Bukhari, iliyo Marfu'. (Hakika mwanangu, huyu ni Sayyid) yaani Hassan. Na neno mwanangu, kwa Waarabu, halitajwi kwa watoto wa binti. Na Hadith ya Umar katika Kitab Ma'rifatu Sahaba cha Abu Naim, iliyo marfu'; (kuwa kila mtoto wa Adam ukoo wao unatokana na baba yao, isipokuwa watoto wa Fatima, mimi ndiye baba yao na ni ukoo wao). Watu wakazoea haya, wakawa wanasema kuhusu watoto wa Fatima kuwa ni watoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) na ni kizazi chake na Ahlu bait (watu wa nyumbani) wake."

Maana ya maneno haya ni kuwa watoto wa Fatima(a.s) si watoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu kilugha, lakini ni watoto wake kisharia, kutokana na kauli ya Mtume 'mimi ni baba yao na ukoo wao.' Vilevile ni watoto wake kimazoweya, kwa sababu watu walizoweya kuwaita kuwa ni watoto wa mtume.

Wamekongamana kwa kauli moja maulama wa Sunni na Shia kwamba sharia inatangulia ufahamisho wa matamko kimazowea na kilugha; na kwamba mazoea yanaitangulia lugha. Kwa sababu, mwenye hekima huzungumza na watu kwa lile wanalolifahamu haraka sio kwa lile lililoandikwa katika kamusi za lugha.

Likija neno katika Aya au Hadith, na tukakuta Tafsir maalum ya maana yake katika Qur'an au Hadith, basi tamko hilo litachukuliwa katika maana haya maalum; na huitwa maana ya kisharia na kupuuzwa ile ya kilugha na kimazoea. Ikiwa hatukupata maana maalum, basi tutalichukulia kwa maana wanayoifahamu watu; na huitwa maana ya mazoea. Wakitolifahamu watu kwa maana hayo, basi itachukuliwa maana yake kutoka kwenye kamusi za lugha.

Kwa hiyo basi maana ya sharia yanakuwa katika ngazi ya kwanza, ya mazoea katika ngazi ya pili na ya kilugha katika ngazi ya tatu. Na imethibiti kisharia na kimazoea kuwa Hassan na Hussein ni watoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, Hivyo ikapuuzwa maana ya kilugha. Kwa sababu lugha inahukumiwa na sharia na mazoea.

Ama siri ya kuwa Hasan na Husein ni wana wa Mtume ingawaje si wanawe kilugha, ataipata mpekuzi katika sifa za hao wawili na hulka zao. Inamtosha mwenye kufanya utafiti wa sera ya Hasan kuwa Muawiya bin Abu Sufian hakupata wasaa wa Ufalme aliokuwa nao na huku Hassan bado yu hai. Na inamtosha mwenye kutafiti sera ya Hussein kwamba Yazid bin Muawiya dunia ilimzonga kwa kuweko Husein, kama ilivyomzonga baba yake, Muawiya kwa kuweko Hasan.

Na Ismail na Al-yasaa na Yunus na Lut , Vilevile tuliwaongoa.

Na kila mmoja tulimfadhilisha juu ya walimwengu wote katika zama zake.

Na katika baba zao na vizazi vyao na ndugu zao.

'Katika' hapa ni ya kubaadhisha; yaani baadhi yao Kwa sababu katika vizazi vyao na ndugu zao walikuwako makafiri; bali Isa na Yahya hawakuwa na kizazi.

Na tukawachagua na kuwaongoza katika njia iliyonyooka.

Sifa hizi ni utanguluzi wa kauli yake Mwenyezi Mungu:

Huo ni uongozi wa Mwenyezi Mungu, Kwa huo humwongoza amtakaye katika waja wake.

Yaani uongozi ambao ni wajibu kufuata ni ule waliokuja nao Mitume, wala hafuati mwongozo huu ila aliyepewa tawfiki na Mwenyezi Mungu.

Na kama wangeshirikisha, bila shaka yangeliporomoka yale waliyokuwa wakiyatenda.

Yaani hawa Mitume pamoja na ubora wao na utukufu wao wa vyeo, lau ingelitokea kufanya chembe ya kitu inayofahamisha shirk, basi bila shaka yangelibatilika yale waliyokuwa wakiyatenda na kuwa ni bure tu.

Lengo la ishara hii ni kuzindua kuwa Mwenyezi Mungu atawafanyia watu kulingana na amali zao si kulingana na vyeo vyao, na kwa watakavyoishilia wanapokufa, si kwa walivyoanzia uhai wao.

Hao ndio tuliowapa Kitab na hukumu na utume.

Hao, ni wale Mitume waliotangulia kutajwa. Na Kitab, ni jinsi ya Kitab inayochanganya vitabu vyote vya Mwenyezi Mungu vilivyoitangulia Qur'an, kama vile Mbao za Ibrahim, Tawrat, Zabur na Injil. Makusudio ya 'Hukumu' ni kujua kuhukumu na kila lile aliloliwekea sharia Mwenyezi Mungu katika halali na haramu.

Kama hawa wakiyakataa, basi tumekwisha yawakilisha kwa watu wasioyakataa.

Hawa, ni washirikina wa Kiquraish ambao wameukana Utume wa Muhammad(s.a.w.w) na kumfanyia uadui. Wanayoyakataa ni Utume. Makusudio ya watu ambao hawayakanushi ni Muhajirina na Ansari[9] ambao walimwamini Muhammad na wakamsaidia.

Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewaongoza, basi fuata mwongozo wao.

Hao wanaotajwa hapa ni Mitume waliotangulia kutajwa. Mwenyezi Mungu amemwamrisha Mtume wake mtukufu kufuata nyao zao katika kuilingania haki na kuvumilia adha katika njia yake.

Sema: Siwaombi ujira juu ya haya.

Kwa sababu dini haikuwekwa kuwa ni chumo na biashara.

Haikuwa hiyo ila ni mawaidha kwa walimwengu wote.

Dhamir ya hiyo ni Qur'an. Maneno haya ni dalili wazi kuwa Muhammad ametumwa kwa watu, wakati wote na mahali pote.

﴿وَمَا قَدَرُوا اللَّـهَ حَقَّ قَدْرِهِ إِذْ قَالُوا مَا أَنزَلَ اللَّـهُ عَلَىٰ بَشَرٍ مِّن شَيْءٍ قُلْ مَنْ أَنزَلَ الْكِتَابَ الَّذِي جَاءَ بِهِ مُوسَىٰ نُورًا وَهُدًى لِّلنَّاسِ تَجْعَلُونَهُ قَرَاطِيسَ تُبْدُونَهَا وَتُخْفُونَ كَثِيرًا وَعُلِّمْتُم مَّا لَمْ تَعْلَمُوا أَنتُمْ وَلَا آبَاؤُكُمْ قُلِ اللَّـهُ ثُمَّ ذَرْهُمْ فِي خَوْضِهِمْ يَلْعَبُونَ﴾

91.Na hawakumkadiria Mwenyezi Mungu kwa haki ya kadri yake, waliposema: Mwenyezi Mungu hakuteremshia chochote juu ya binadamu yoyote. Sema: nani aliyekileta Kitab alichokuja nacho Musa chenye nuru na mwongozo kwa watu? Mlichokifanya nyaraka- nyaraka, mkizidhihirisha na mkificha mengi, Na mkafundishwa msiyoyajua nyinyi wala baba zenu. Sema: Ni Mwenyezi Mungu, Kisha waache wacheze katika porojo zao.

﴿وَهَـٰذَا كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ مُبَارَكٌ مُّصَدِّقُ الَّذِي بَيْنَ يَدَيْهِ وَلِتُنذِرَ أُمَّ الْقُرَىٰ وَمَنْ حَوْلَهَا وَالَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ يُؤْمِنُونَ بِهِ وَهُمْ عَلَىٰ صَلَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ﴾

92.Na hiki ni kitab tulichokiteremsha, kilichobarikiwa, chenye kusadikisha yale yaliyokitangulia. Na ili uwaonye (watu wa) Ummul qura na walio pambizoni mwake. Na wale wanaoamini akhera, wanakiamini, Nao huzihifadhi Swala zao.

HAWAMHESHIMU MWENYEZI MUNGU KAMA INAVYOTAKIWA

Aya 91 - 92

MAANA

Na hawakumkadiria Mwenyezi Mungu kwa haki ya kadiri yake, waliposema: Mwenyezi Mungu hakuteremshia binadamu chochote.

Aya hii inafahamisha kuwa katika wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu kulikuwa na watu wanaokanusha wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa mtu yoyote, na wakisema kuwa Mwenyezi Mungu hakumtuma mtu yeyote kuwa mjumbe.

Lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakubainisha ni akina nani waliokanusha na kusema hivyo, Kwa ajili hii waliotofautiana wafasiri, kuhusu waliokusudiwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu. Je, ni washirikina wa Kiarabu au Mayahudi wa Hijaz?

Kuna kundi la wafasiri waliosema kuwa ni washirikina wa Kiarabu. Kauli hii inapingwa, kwanza kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimwamrisha Mtume wake kuwakabili na swali hili:

Sema: Ni nani aliyekileta Kitab alichokuja nacho Musa chenye nuru na mwongozo kwa watu?

Kimsingi ni kuwa swali hili linaelekezwa kwa yule anayekubali Utume wa Musa na Tawrat; na yajulikana kuwa washirikina wa Kiarabu hawakubali Utume wa Musa na Tawrat yake; vinginevyo wangelikuwa ni katika watu wa Kitab.

Pili, ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewatahayariza wakanushaji kwa kauli yake:

Mlichokifanya nyaraka-nyaraka, mkizidhihirisha na mkificha mengi.

Yaani kuwa nyinyi mmeibadilisha Tawrat, mkadhihirisha yale yanayoafikiana na hawaa zenu na mkaficha yale yasiyoafikiana nayo. Inajulikana kuwa walioibadilisha Tawrat ni Mayahudi, sio washirikina wa Kiarabu.

Kundi jingine la wafasiri limesema kwamba waliosema kuwa Mwenyezi Mungu hakuteremsha chochote kwa mtu, ni Mayahudi. Wakatoa dalili kwa mambo mawili: Kuwa Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake Muhammad amjibu anayesema hivi kwa Utume wa Musa na Tawrat, nalo ni jibu sahihi, kisha akatilia mkazo jibu hili kwa kuipotosha kwao Tawrat akasema: "Mlichokifanya nyaraka-nyaraka."

Kauli hii iko karibu na dhahiri ya Aya kuliko ile ya kwanza.

Na mkafundishwa msiyoyajua nyinyi wala baba zenu.

Msemo huu unaelekezwa kwa Mayahudi vilevile; na maana yake ni, vipi mnasema - Enyi Mayahudi - kuwa Mwenyezi Mungu hakuteremsha chochote kwa mtu yeyote na hali nyinyi mnaitakidi kwamba Musa ni mwanadamu na kwamba Tawrat imeteremshwa kwake? Na mmejua kutokana nayo yale mliyokuwa hamyajui nyinyi na baba zenu.

Miongoni mwayo ni kuwa nyinyi mlikuwa mkisoma katika Tawrat sifa za Muhammad kabla ya kutumwa kwake, wala hamkuwa mkimjua kwa ufafanuzi aliyekusudiwa. Mwenyezi Mungu alipomtuma na mkamjua aliyekusudiwa hasa, kwa kiburi na inadi yenu mkageuza na kuondosha yale yanayomwelezea.

Sema: Ni Mwenyezi Mungu.

Hili ni jawabu la swali lililotangulia (Sema: Ni nani aliyeteremsha Kitab alichokuja nacho Musa?

Jibu : hili ndilo lenyewe hasa na halikimbiliki. Kwa sababu Mayahudi wanakiri kuwa Tawrat inatoka kwa Mwenyezi Mungu. Na kwa ajili ya kukiri kwao huku ndio inawasimamia hoja na kuwajibu kauli yao ya kuwa Mwenyezi Mungu hakuteremsha chochote kwa mtu.

Kisha waache wacheze katika porojo zao.

Yaani sema haki Ewe Muhammad, na waache Mayahudi katika batili zao wala usijishughulishe na inadi zao na ria zao.

Huku ni kuwapa onyo na kuwapa kiaga, kama ambavyo pia ni kuwadharau na kuwapuuza.

Utauliza : Mayahudi wanaukubali Utume wa Musa(a.s) na kuteremshwa Tawrat, kama yalivyotangulia maelezo. Kwa hiyo imekuwaje Mwenyezi Mungu akawanasibishia kukanusha wahyi na Utume?

Jibu : Wao wanakanusha wahyi na Utume kwa dhahiri, kwa inadi na kiburi kwa Muhammad(s.a.w.w) na si kwa undani hasa.

﴿وَجَحَدُوا بِهَا وَاسْتَيْقَنَتْهَا أَنفُسُهُمْ ظُلْمًا وَعُلُوًّا﴾

"Na wakazikakataa kwa dhuluma na kujivuna, na hali ya kuwa nafsi zao zina yakini nazo" (27:14)

MITUME WA MWENYEZI MUNGU NA WANASAYANSI

Wanasayansi wengi wakati huu wanaamini kuweko Mwenyezi Mungu, Kwa sababu wameona kuwa ulimwengu huu unakwenda kulingana na kanuni thabiti, na iliyowazi inayohukumu, haiepukani nao kwa hali yoyote ile.

Kwa ajili hii imewezekana kuichunguza, kuikisia na kufaidika nayo. Huku ni kuthibitika kuweko nguvu ya hali ya juu nyuma ya ulimwengu inayofanya uhandisi na kujenga; na nguvu hiyo ndio Mwenyezi Mungu.

Kwa maneno mengine, si lazima mtu akitaka kujua kuweko kila kitu afanye majaribio katika vyombo na kukiona kwa macho, bali inatosha kwa kujua kwa elimu isiyo na shaka na dhana, ni sawa elimu hiyo iwe imetokana na majaribio na macho au imetokana na natija ya akili ya kiasili. Mwenye fikira na uchunguzi akitaamali ulimwnengu huu kwa taamuli ya kielimu isiyo na shaka shaka, lazima atakomea kwenye kumjua Mwenyezi Mungu.

Lakini Wanasayansi waliojua kuweko Mwenyezi Mungu kwa Kisayansi, wamekanusha kuwa ana wajumbe katika watu anaowapa wahyi na wakasema: Nguvu-asili (nature) peke yake ndio Kitab cha Mwenyezi Mungu na wala sio Tawrat, Injil na Qur'an.

Sina shaka kwamba wataalam hawa, lau wangelipa somo la Qur'an wakati mdogo tu katika muda ule ule walioutoa kwa kusoma sayansi wangelikinai kuwa Mwenyezi Mungu ana vitabu viwili: Ulimwengu na wahyi, Na kwamba mtu anavihitajia vyote viwili.

Kutokana na Kitab cha ulimwengu atajua Ufalme wa Mwenyezi Mungu na kumwamini. Na kutokana na Kitab cha wahyi atajua sharia ya Mwenyezi Mungu ambayo itamwangazia njia ya maisha, kusonga mbele na kujiepusha na maangamizo na matatizo ambayo yatachelewesha safari yake ya kwenda mbele.

Mtu ameumbwa ili afanye kazi katika maisha haya, kwa hivyo basi, hapana budi kwa kila anayefanya amali kuwa na njia anayoifuata katika kufanya kazi, Kwa sababu kujifanyia mambo ovyo ovyo hakupelekei kheri yoyote. Na Mwenyezi Mungu ndiye aliyememuumba mtu, anajua siri yake na dhahiri yake, nguvu yake na udhaifu wake na yale yanayomnufaisha na kumdhuru.

Kwa hiyo basi ni lazima kuwa yeye ndiye marejeo ya kwanza ya njia ambayo inapasa mtu kuifuata katika kazi yake; sawa na ilivyo kwa mgunduzi wa ndege na gari na mengineyo; ambapo inakuwa lazima kumrejea yeye katika kutaka kuitumia na kufaidika nayo. Kwa sababu yeye ndiye Ayajuae zaidi masilahi ya ndege na madhara yake.

Hakuna mwenye shaka kwamba kuifikisha njia ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake na kuwafahamisha kunafungika na Mitume na Manabii, kwa sababu wao ndio lugha ya Mwenyezi Mungu na ubainifu wake. Huu ndio wahyi hasa.

Anayetaka ufafanuzi na arejee kitab chetu Al-Islam wal-aql (Uislamu na akili) sehemu ya Utume na akili.

Na hiki ni kitab tulichokiteremsha, kilichobarikiwa, chenye kusadikisha yale yaliyokitangulia.

Hii, ni Qur'an Tukufu; na maana ni kuwa kama tulivyoteremsha Tawrat kwa Musa, Vilevile tumeiteremsha hii Qur'an Kwa Muhammad(s.a.w.w) nayo ina manufaa na faida nyingi kwa anayejua hukumu zake na siri zake na akazitumia.

Nayo Vilevile inasadikisha vitabu vya Mwenyezi Mungu ambavyo vimeteremshiwa Mitume wa Mwenyezi Mungu tangu zamani. Imam Ali anasema: "Jifundisheni Qur'an kwani hiyo ni mazungumuzo mazuri, na ifahamuni kwani hiyo ni utuvu wa nyoyo, na ifanyeni dawa kwa nuru yake kwani hiyo ni ponyo la nyoyo, na isomeni vizuri kwani hiyo ina visa vizuri."

Na ili uwaonye (watu wa) Ummul qura na walio pambizoni mwake.

Ummul-qura (Mama wa miji) ni Makka. Imeitwa hivyo kwa sababu mna nyumba ya kwanza iliyowekwa kwa ajili ya watu kumwabudu Mwenyezi Mungu.

Wastashriki (Wataalamu wa kimagharibi juu ya mambo ya uislamu) na kabla yao Mayahudi walidai kuwa Muhammad(s.a.w.w) ametumwa kwa Waarabu tu, kwa kutolea hoja Aya hii, na kusahau Aya nyingine; kama vile:

﴿وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِّلْعَالَمِينَ﴾

"Na hatukukutuma ila uwe ni rehema kwa walimwengu wote" (21:107)

﴿وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا كَافَّةً لِّلنَّاسِ بَشِيرًا وَنَذِيرًا وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ﴾

"Na hatukukutuma ila kwa watu wote, uwe mbashiri na muonyaji; lakini watu wengi hawajui" (34:28)

Wamejitia purukushani na Aya hizo na hali chimbuko la Qur'an ni moja. maneno yake yanajifasiri hayo yenyewe na Aya mbili hizi ni ubainifu wa kauli yake Mwenyezi Mungu: 'Na ili uwaonye (watu wa) Ummul qura na walio pembezoni mwake.'

Na Vilevile makusudio yake ni kuanza mwito wa Uislam, mwanzo kabisa, katika mji wa mwenye mwito huo; yaani Makka.

Mpaka utakapopata wafuasi ndipo uwape bishara walio kando kando yake; kama vile mwito wowote unavyoanza, ambapo unazaliwa kisha unatembea mabara yote.

Zaidi ya hayo imethibiti riwya kwa njia ya Mutawatir kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) aliwaandikia Wafalme na viongozi wote akiwalingania kwenye Uislamu, miongoni mwao ni Mfalme Kisra wa Fursi (Iran) na Kaizari wa Roma. Wastashriki wanajua hayo, lakini baadhi yao wanaficha wanayoyajua.

Na wale wanaoamini akhera, wanakiamini.

Dhamiri ya wanakiamini inarudia Kitabu ambacho ni Qur'an. Yeyote atakayeisoma Qur'an kwa uchunguzi na kuzingatia maana hutoka na kitu. Akiwa anamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, basi huzidi imani, na akiwa anamwamini Mwenyezi Mungu tu, basi ataamini wahyi na ufufuo; akiwa anamwamini Mwenyezi Mungu na ufufuo bila wahyi, basi ataamini Mitume na vitabu vya Mwenyezi Mungu, na hasa Utume wa Muhammad na Qur'an.

Akiwa anamkanusha Mwenyezi Mungu atamwamini; Kwa sababu Qur'an itamwonyesha dalili za hilo na kumhimiza kuichunguza. Nayo kwa asili yake humpeleka mtafiti, anayechunga haki, kwenye elimu.

Nao huzihifadhi Swala zao.

Ili daima wawe na mawasiliano ya kutegemewa na Mwenyezi Mungu. Ameihusisha kutaja Swala kinyume cha ibada nyinginezo kwa sababu ndiyo nguzo kubwa ya dini na inayodumisha imani. Miongoni mwa kazi za swala ni kumkataza mwenye kuswali uovu na mambo mabaya.