TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA Juzuu 7

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA 33%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
  • Anza
  • Iliyopita
  • 16 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 14672 / Pakua: 3584
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA Juzuu 7

Mwandishi:
Swahili

1

2

3

4

13

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA SABA

﴿وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا أَوْ قَالَ أُوحِيَ إِلَيَّ وَلَمْ يُوحَ إِلَيْهِ شَيْءٌ وَمَن قَالَ سَأُنزِلُ مِثْلَ مَا أَنزَلَ اللَّـهُ وَلَوْ تَرَىٰ إِذِ الظَّالِمُونَ فِي غَمَرَاتِ الْمَوْتِ وَالْمَلَائِكَةُ بَاسِطُو أَيْدِيهِمْ أَخْرِجُوا أَنفُسَكُمُ الْيَوْمَ تُجْزَوْنَ عَذَابَ الْهُونِ بِمَا كُنتُمْ تَقُولُونَ عَلَى اللَّـهِ غَيْرَ الْحَقِّ وَكُنتُمْ عَنْ آيَاتِهِ تَسْتَكْبِرُونَ﴾

93.Na ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule amzuliaye uwongo Mwenyezi Mungu. Au mwenye kusema: Nimeletewa Wahyi; na hali hakuletewa wahyi wowote Na yule asemaye: Nitateremsha kama alivyoteremsha Mwenyezi Mungu. Na lau ungewaona madhalimu watakapokuwa katika mahangaiko ya mauti na Malaika wamewanyooshea mikono. Zitoeni roho zenu; leo mtalipwa adhabu ifedheheshayo kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyasema juu ya Mwenyezi Mungu yasiyokuwa haki, na mlikuwa mkizifanyia kiburi ishara Zake.

﴿وَلَقَدْ جِئْتُمُونَا فُرَادَىٰ كَمَا خَلَقْنَاكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ وَتَرَكْتُم مَّا خَوَّلْنَاكُمْ وَرَاءَ ظُهُورِكُمْ وَمَا نَرَىٰ مَعَكُمْ شُفَعَاءَكُمُ الَّذِينَ زَعَمْتُمْ أَنَّهُمْ فِيكُمْ شُرَكَاءُ لَقَد تَّقَطَّعَ بَيْنَكُمْ وَضَلَّ عَنكُم مَّا كُنتُمْ تَزْعُمُونَ﴾

94.Na hakika mtatujia wapweke kama tulivyowaumba kwanza. Na mmeacha nyuma yenu yale tuliyowapa. Na hatuwaoni waombezi wenu pamoja nanyi ambao mlidai ni washirika.

KUMZULIA UWONGO MWENYEZI MUNGU

Aya 93-94

MAANA

Na ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule amzuliaye uwongo Mwenyezi Mungu.

Kumzulia Mwenyezi Mungu uwongo ni kumtengenezea mambo ambayo hayana chimbuko katika Qur’an wala Hadith au katika misingi ya akili. Na hayo yanakuwa kwa mambo yafuatayo:

• Kuhalalisha aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu au kuharamisha aliyoyahalalisha.

• Kumsingizia Mwenyezi Mungu, kwa makusudi, yale asiyokuwa nayo au kumfanyia washirika au kuwa ana watoto na mabinti.

• Kudai Utume kwa asiyekuwa Mtume. Hilo ameliashiria Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa kauli yake: Au mwenye kusema: Nimeletewa Wahyi; na hali hakuletewa Wahyi wowote. Jumla hii inaungana na ile ya ‘Amzuliaye Mwenyezi Mungu uwongo.’ Ni katika mlango wa kuunganisha mahsusi kwenye ujumla.

• Na yule asemaye: Nitateremsha kama alivyoteremsha Mwenyezi Mungu.Yaani mlaanifu huyu anadai kuwa ana uwezo wa kutunga Kitab kitakachofanana na Qur’an katika utukufu wake. Imesekana kuwa mtu huyo ni Abdullah bin Sa’d bin Abu Sarh. Wengine wamesema ni Nadhr bin Harith.

Kwa ufupi ni kwamba kila mwenye kumnasibishia Mwenyezi Mungu kitu chochote bila ya kutegemea kauli ya Mwenyezi Mungu na ya Mtume au misingi ya akili basi huyo ni mzushi, mwongo mkubwa na anayestahiki shutuma na adhabu.

Na lau ungewaona madhalimu wanavyokuwa katika mahangaiko ya mauti na Malaika wamewanyooshea mikono.

Mahangaiko ya mauti ni maumivu ya kukata roho, Wafasiri wametofautiana katika makusudio ya kunyoosha mikono ya Malaika. Je, makusudio ni kunyoosha kiuhakika wakati mtu anapokata roho, au ni fumbo tu la kufananisha vituko vya mauti?

Sisi hatuoni haja yoyote ya mzozo huu, Kwa sababu akili haikatai kuweko Malaika wala kuwa na mikono wanaoinyoosha au ndimi za kuzungumzia. Kwani Wahyi umelieleza hilo, kwa hiyo ni wajibu kuamini. Msingi huu wanautegemea Maulama wote Waislamu katika kuthibitisha itikadi na sharia.

Zitoeni roho zenu; leo mtalipwa adhabu ifedheheshayo kwa sababu ya yale mliyokuwa mkisema juu ya Mwenyezi Mungu yasiyokuwa ya haki, na mlikuwa mkizifanyia kiburi ishara zake.

Haya yote ni maneno ya Malaika wakiwaambia wazushi wakati wa kufa. Nayo ni lawama na shutuma kwa uzushi wao na kukana kwao haki. Kuna Hadith isemayo: "Anayekufa kiyama chake kimesimama." Kwa sababu hii wamesema baadhi ya wajuzi kwamba mtu ana viyama viwili, kidogo ambacho ni mauti na kikubwa, ufufuo.

Shutuma za Malaika kwa anayemzulia Mwenyezi Mungu uwongo, katika Kiyama kidogo, ni onyo la vituko vya Kiyama kikubwa atakavyokumbana navyo. Imam Ali anasema: "Kifo kwa Mumin ni kama kuvua nguo chafu na kufungua minyororo na kuvaa kanzu ya kifahari na kushukia kwenye maliwazo. Ama kwa kafiri, ni kama kuvua kanzu ya kifahari na kuvaa gwanda chafu, na kutoka kwenye maliwazo kwenda kwenye vitisho na adhabu kubwa."

Na hakika mtatujia wapweke kama tulivyowaumba kwanza.

Yaani mwanadamu atakutana na Mola wake kesho, kama alivyotoka tumboni mwa mamake hana chochote.

Afadhali angeliingia ardhini kama alivyotoka - haulizi wala haulizwi, lakini atarudi akiwa ni mwenye kuulizwa. Alhamdulilah, mwenye kuuliza ni mwadilifu hamdhulumu yeyote na atamfanyia mtu vile alivyowafanyia watu alipokuwa katika uhai wake wa kwanza. Ikiwa ni kheri basi itakuwa kheri na ikiwa ni shari basi ni shari.

Wametofautiana wanavyuoni kuhusu kufufuliwa kuwa je, ni kwa roho tu, au ni kwa roho na kiwiliwili pamoja. Dhahiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu: kama tulivyowaumba kwanza, inafahamisha kufufuliwa kwa roho na kiwiliwili kwa sababu vyote viwili vimeumbwa pamoja.

﴿كَمَا بَدَأْنَا أَوَّلَ خَلْقٍ نُّعِيدُهُ وَعْدًا عَلَيْنَا إِنَّا كُنَّا فَاعِلِينَ﴾

"Kama tulivyoanza umbo la awali tutalirudisha tena, Ni ahadi iliyo juu yetu, hakika sisi ni watendaji" (21:104)

Na mmeacha nyuma yenu yale tuliyowapa.

Mtu atarudi ardhini akiwa ameacha watu wake, marafiki mali na ufalme.

Na hatuwaoni waombezi wenu pamoja nanyi ambao mlidai ni washirika (wa Mwenyezi Mungu) kwenu.

Kama vile masanamu, nyota na mengineyo mliyokuwa mkiyaabudu na kuwatawalisha wafisadi na wapotevu.

Kwa hakika yamekatika (mahusiano) baina yenu.

Yaani hamna mawasiliano yoyote ya duniani.

Na yamewapotea mliyokuwa mkidai katika madai ya uwongo kwa wale mliowafikiria kuwa ni washirika au waombezi mbele yake, na yamepotea matumaini yenu baada ya kufichuka uhakika; na mwema ni yule atakayefuzu kupata radhi za Mwenyezi Mungu na maghufira yake.

﴿إِنَّ اللَّـهَ فَالِقُ الْحَبِّ وَالنَّوَىٰ يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَمُخْرِجُ الْمَيِّتِ مِنَ الْحَيِّ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ فَأَنَّىٰ تُؤْفَكُونَ﴾

95.Hakika Mwenyezi Mungu ndiye mpasuaji mbegu na kokwa. Humtoa aliye hai katika maiti na ni mtoaji wa maiti katika aliye hai. huyo ndiye Mwenyezi Mungu basi mnageuzwa wapi?

﴿فَالِقُ الْإِصْبَاحِ وَجَعَلَ اللَّيْلَ سَكَنًا وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ حُسْبَانًا ذَٰلِكَ تَقْدِيرُ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ﴾

96.Ndiye mpambazuaji wa asubuhi; ameufanya usiku kuwa mapumziko na utulivu, na jua na mwezi (kwenda) kwa hesabu, Hayo ndiyo makadirio ya Mweye nguvu, Mjuzi.

﴿وَهُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ النُّجُومَ لِتَهْتَدُوا بِهَا فِي ظُلُمَاتِ الْبَرِّ وَالْبَحْرِ قَدْ فَصَّلْنَا الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ﴾

97.Na yeye ndiye aliyewafanyia nyota ili muongoke kwazo katika viza vya bara na baharini. Hakika tumezifafanua ishara kwa watu wanaojua.

﴿وَهُوَ الَّذِي أَنشَأَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ فَمُسْتَقَرٌّ وَمُسْتَوْدَعٌ قَدْ فَصَّلْنَا الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَفْقَهُونَ﴾

98.Na Yeye ndiye aliyewaanzisha nyinyi kutokana na nafsi moja. Pako mahali pa kutulia na pa kupita njia. Hakika tumezifafanua ishara kwa watu wanaofahamu.

﴿وَهُوَ الَّذِي أَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجْنَا بِهِ نَبَاتَ كُلِّ شَيْءٍ فَأَخْرَجْنَا مِنْهُ خَضِرًا نُّخْرِجُ مِنْهُ حَبًّا مُّتَرَاكِبًا وَمِنَ النَّخْلِ مِن طَلْعِهَا قِنْوَانٌ دَانِيَةٌ وَجَنَّاتٍ مِّنْ أَعْنَابٍ وَالزَّيْتُونَ وَالرُّمَّانَ مُشْتَبِهًا وَغَيْرَ مُتَشَابِهٍ انظُرُوا إِلَىٰ ثَمَرِهِ إِذَا أَثْمَرَ وَيَنْعِهِ إِنَّ فِي ذَٰلِكُمْ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ﴾

99.Naye ndiye aliyeteremsha maji kutoka mbinguni na kwayo tunatoa mimimea ya kila kitu, Kisha tukatoa kutokana nayo kijani, Tukatoa ndani yake punje zilizopandana, Na katika mitende yakatoka kwenye makole yake mashada yaliyo karibu. Na bustani za miza bibu na mizaituni na mikomamanga. Yanayofanana na yasiyofanana. Angalieni matunda yake yanapozaa na kuiva kwake. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaoamini.

HUTOA ALIYE HAI KATIKA MAITI

Aya 95-99

MAANA

Katika Aya hizi kuna mifano ya ajabu katika viumbe ambavyo anayemiliki utengenezaji wake ni Mwenyezi Mungu peke yake. Vilevile kufahamisha kuwepo Mwenyezi Mungu na utukufu wake. Mifano imetajwa kwa mpango ufuatao:

Hakika Mwenyezi Mungu ndiye mpasuaji mbegu na kokwa.

Ukiweka mbegu ya ngano au kokwa ya tende katika ardhi itapasuka chini na juu. Upande wa chini itatoka mizizi na kushuka ardhini, na upande wa juu utatoka mti utakaorefuka hewani. Kisha ile mbegu au kokwa itapotea na mchanganyiko wote kuwa kitu kimoja, sehemu moja itakuwa ardhini na nyingine itakuwa kwenye hewa.

Hakuna mwenye shaka kwamba kazi yote hii inategemea sababu zake za kimaumbile; kama vile mchanga, maji, jua na hewa, lakini vyote hivyo vinaishia kwa Mwenyezi Mungu peke yake, kwa sababu yeye ndiye aliyeumba maumbile, msababishaji wa sababu na mpatishaji wa mada ya kwanza kwa neno 'Kuwa' na ikawa.

UHAI UMETOKA WAPI?

Humtoa aliye hai katika maiti na ni mtoaji wa maiti katika aliye hai.

Si ajabu kuzalika kitu hai kutoka kwa kilicho hai mfano wake; na kisicho na uhai kutoa kisicho na uhai. Vilevile chenye uhai kuzaa kisicho na uhai, au kinyume chake. Msemaji mmoja alisema: "Uhai unazalikana kutokana na nguvu ya asili ya maumbile." Tumwulize msemaji huyu:

Ni nani aliyeifanya ipatikane asili hiyo, nguvu zake na utendaji kazi wake? Ikiwa msukumano tu unatosha kuleta uhai bila ya kuweko msaada wa Mwenyezi Mungu, basi kwa nini wanasayansi wameshindwa kutengeneza uhai kama vile watengenezavyo vyombo vya jikoni na mengineyo; pamoja na kuwa wamejaribu wakaleta msukumano; lakni baada ya kukata tamaa walisema kwamba kutengeneza uhai ni kuzito kuliko kumrudisha mzee utotoni.

Hebu tuchukulie kuwa wao wanajiona watafaulu katika kutengeza chembehai, je, wamefaulu kutengeza mdudu mdogo tu?.

Tuache binadamu na ubongo wake na wanyama na maumbile yao ya ajabu na tupige mfano wa hawa wadudu tunaowaogopa na kupiga madawa kuwauwa. Baadhi ya wataalamu wa wadudu wanasema hivi: "Baadhi ya wadudu wanaishi katika nyuzi joto 50 chini ya sifuri; wengine wanaishi nyuzi joto hizi hizi juu ya sifuri, wengine katika hewa ya sumu na wengine katika visima vya mafuta, na wana utaratibu mzuri sana katika maisha yao na kazi zao."

Ikiwa mwanaadamu anaweza kugundua satalaiti, maroketi na akili za Elktroni, lakini hawezi kabisa kutengeza bawa la mbu au chembe moja ya mbawa zake. Akili ya binadamu ni kubwa lakini ukubwa wake ni wenye kuhemewa mbele ya uweza wa ajabu ulioumba mbu na chungu na nyuki!

Yote hayo yako wazi, Lakini msiba mkubwa ni kuwa tumejisahau, hatujiangalii sisi wenyewe na uwazi wa uweza wa Mwenyezi Mungu mwenye hekima. Kama tukiangalia tutazidi imani kwa kiwango kikubwa kwa muumba aliye mkubwa. Tunachohitajia ni imani na imani yetu inahitajia akili kwa sababu imani bila ya akili ni kama uso bila macho.

Ndiyo, tunahitaji kuamini uweza wa Mwenyezi Mungu ili tufasiri yale yaliyoshinda akili za mabingwa, ambazo zimeshindwa kufasiri maumbile ya uhai. Na wengi wenye akili hizo wanakimbilia kwenye kitu kilicho nyuma ya maumbile, Uwezo wenye hekima na ujuzi, wanaufasiri kwa kusema kuwa ni asili ya uhai,huyo ndiye Mwenyezi Mungu basi mmegeuzwa wapi?

Anaema Enstein: "Hakika uoni wetu wa kidini ndio unaloelekeza uoni wetu wa kielimu". Ustadh Tawfiq Al-Ahkim aliongeza katika kitabu chake Fannul-adab: 'Huku bila shaka ni kukiri dini. Hakuna mtaalamu yeyote katika waliopiata aliyesema kuhusu dini kama alivyosema huyu."

Nasi twaongeza juu ya kauli ya Al-Hakim, kwamba siri pekee ya kukubali wataalamu wa karne ya ishirini ni kuwa uoni wa dini ndio chimbuko la uoni wa kielimu, ni kuendelea kwa elimu katika karne hii na kuwa ilikuwa nyuma katika zama zilizopita. Kila inapopiga hatua elimu ndipo dini inapozidi kupata watetezi; kama Einstein anayekubali ukuu wa dini na kuamini kuwa ni haki ambayo haiingiliwi na batili mbele yake wala nyuma yake.

Ndiye mpambazuaji wa asubuhi; ameufanya usiku kuwa mapumziko na utulivu, na jua na mwezi (kwenda) kwa hesabu.

Mwenyezi Mngu (s.w.t) ametaja katika Aya zlizotangulia mifano ya utukufu wake kwa kupatikana uhai kwenye ardhi; na katika Aya hii ametaja mifano mitatu ya mbinguni:

Kwanza : kuwa ameitoa asubuhi kwenye usiku, hilo ni fumbo la kupatikana mchana ambao watu wanahangaikia riziki na kupanga mambo yao.

Pili : kwamba yeye Mwenyezi Mungu ameuleta usiku kwa ajli ya kutulia na kupumzika kutokana na machovu za kazi ya mchana kutwa.

Tatu : kwamba ameweka Jua na Mwezi kwa kiasi mahsusi cha haraka na polepole kwa namna ambayo ardhi inakuwa na harakati mbili: Harakati za masaa 24, hisabu ya siku moja, na harakati za mwaka, ambazo ndani yake mna misimu mine ambayo ni hisabu ya mwaka mmoja. Mwenyezi Mngu (s.w.t) amesema:

﴿هُوَ الَّذِي جَعَلَ الشَّمْسَ ضِيَاءً وَالْقَمَرَ نُورًا وَقَدَّرَهُ مَنَازِلَ لِتَعْلَمُوا عَدَدَ السِّنِينَ وَالْحِسَابَ﴾

"Yeye ndiye aliyelijaalia Jua kuwa mwanga na mwezi kuwa nuru na akaupimia vituo ili mjue idadi ya miaka na hisabu' (10:5)

Utauliza : kwa hiyo basi kupatikana usiku na mchana ni natija ya mzunguko wa ardhi , basi kuna wajihi gani wa kutegemeza kwa Mwenyezi Mungu?

Jibu : kwa sababu yeye ndiye Muumba mbingu na ardhi na kwake yeye ndio mwisho wa sababu zote , kwa hali yoyote ni kuwa makusudio ya kwanza ya kila yaliyokuja katika Aya hizi ni kuwa hakuna kitu katika vitu vya ulimwengu vilivyopatikana kwa sadfa na kibahati, isipokuwa kumetokana na aliye Mjuzi, Mwenye hekima aliyekipa kila kitu umbile lake na kukikadiria.

Hayo ndiyo makadirio ya weye nguvu, Mjuzi, Na Yeye ndiye aliyewafanyia nyota ili muongoke kwazo katika viza vya bara na baharini. Hakika tumezifafanua ishara kwa watu wanaojua.

Nyota hapa ni kutoa Jua na Mwezi kama inavyofahamika kutokana na mpangilio wa maneno. Katika kitabu Qur-an walilmul-hadith anasema bingwa wa falaki James Jentis: "Tunapotaka kujua nyumba fulani katika mji iko wapi tunauliza jina la mtaa kisha namba yake, basi ni hivyohivyo katika nyota, kwani katika hizo kuna zilizo maarufu kwa majina yake mahsusi nazo ni alama muhimu wanazozifuata mabaharia katika majahazi yao na waendeshao vyombo na wapanda wanyama. Ni misafara mingapi inyokwenda kwa ramani ya mbinguni na nyota wakati dira inapoacha kufanya kazi?"

Na Yeye ndiye aliyewaanzisha nyinyi kutokana na nafsi moja. Pako mahali pa kutulia na pa kupita njia. Hakika tumezifafanua ishara kwa watu wanaofahamu.

Nafsi iliyoumbwa kila moja kutokana nayo ni mtu wa kwanza ambaye watu wote wametokana naye ambaye ni Adam.

Tumezungumzia kwa ufafanuzi tulipofasiri Juz.4 (4:1) Razi ametaja kauli sita katika kufasirimahali pa kutulia na pa kupita njia .

Wafasiri wengi wamesema 'kutulia' ni kutulia manii katika migongo ya wanaume na 'pa kupita njia' kuwa katika matumbo ya uzazi ya wanawake. Katika Aya hakuna linalofahamisha hilo, wala lolote katika maana sita alizozinukuu Razi.

Imepokewa kutoka kwa Imam Sadiq(a.s) kwamba: yeye amegawanya waumini katika mafungu mawili; mwenye kuamini imani ya kweli inayotulia mpaka kufa, ambaye maneno yake yanaafikiana na vitendo vyake, na mumini ambaye imani yake inalegalega iko kwa muda tu, inamwondoka kabla ya kufa; maneno yake yanatofautiana na vitendo vyake.

Hakika tumezifafanua ishara kwa watu wanaofahamu.

Na asiyefahamu dalili hizi za ulimwengu juu ya ukuu wa muumbaji, mwanzilishi, basi huyo ni katika wale waliokusudiwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿صُمٌّ بُكْمٌ عُمْيٌ فَهُمْ لَا يَعْقِلُونَ﴾

"Ni viziwi ni mabubu ni vipofu kwa hivyo hawafahamu" (2:171)

Naye ndiye aliyeteremsha maji kutoka mbinguni na kwayo tunatoa mimea ya kila kitu.

Mvua ndio chimbuko la maji tamu, lau si hiyo ardhi ingelikuwa kame isiyo na uhai. Mwenyezi Mungu ametegemeza kushuka maji kwake yeye, kwa sababu yeye ndiye msababishaji wa sababu, kwake huanza kila kitu hata kama mzunguko utakuwa mrefu kiasi gani.

Kisha tukatoa kutokana nayo kijani.

Dhamiri ya 'nayo' inarudia kwenye mimea. Makusudio ya kijani ni ubichi, yaani kutokana na mmea huchipua matawi mabichi. Inasemekana kuwa maana ya kijani hapa ni ubichi zaidi.

Tukatoa ndani yake punje zilizopandana.

Dhamiri ya 'ndani yake' ni ndani ya hiyo kijani, yaani tunatoa mashuke katika matawi kama vile ya ngano nk, na kama mfano wa, tunda la komamanga ambalo tembe zake zinapandana.

Na katika mitende yakatoka kwenye makole yake mashada yaliyo karibu.

Yaani ni rahisi kuyachuma au kuwa kukurubiana kwa wingi wake.

Na bustani za miabibu na mizaituni na mikomamanga.

Yaani tunatoa katika mimea aina hizi tatu. Mwenyezi Mungu amezitaja kwa njia ya kupigia mfano ambayo kutokana nazo itajulikana mingine.

Yanayofanana na yasiyofanana.

Katika mimea kuna inayofanana katika umbile na ladha na mingine haifananai.

Angalieni matunda yake yanapozaa na kuiva kwake.

Yaani zingatieni vipi linatoka tunda mwanzo, linakuwa dogo lisilo na manufaa kisha linabadilika badilika mpaka kuiva na kuwa na ladha tamu.

Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaoamini.

Makusudio ya wanaoamini siyo wale wanaoamini tu, bali ni wale wanaotikia mwito wa imani na kunufaika na dalili na hoja. Ama wenye nyoyo zilizofungwa wanazipita kama wanyama.

Kwa ufupi makusudio ya kwanza ya mifano hii ya ardhini na mbinguni ni kuleta uzindushi kuwa vitu vya ulimwengu huu na vilivyomo ndani yake vinatokana na uanzilishi na upangiliaji.

Ni muhali kuwa vimekuja kisadfa katika mtazamo wa kiakili na kimaumbile.

Hizo mbili zinahukumu kwa mkato kwamba kila liliopo limepatikana kwa matakwa na makusudio na kwa hekima ya hali ya juu anayoijua mjuzi na mjinga, wala hakuna kitu kinachobatilisha sadfa kama vile kukaririka tukio moja kila zinapokaririka sababu zake.

14

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA SABA

﴿وَجَعَلُوا لِلَّـهِ شُرَكَاءَ الْجِنَّ وَخَلَقَهُمْ وَخَرَقُوا لَهُ بَنِينَ وَبَنَاتٍ بِغَيْرِ عِلْمٍ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يَصِفُونَ﴾

100.Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu washirika majini, Hali yeye amewaumba. Na wamemsingizia kuwa na wana wa kike na wa kiume bila ujuzi. Ametakasika na ametukuka juu ya hayo wanayombandikiza nayo.

﴿بَدِيعُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَنَّىٰ يَكُونُ لَهُ وَلَدٌ وَلَمْ تَكُن لَّهُ صَاحِبَةٌ وَخَلَقَ كُلَّ شَيْءٍ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ﴾

101.Mbunifu wa mbingu na ardhi. Inawezekanaje awe na mwana hali hana mke, Na ameumba kila kitu. Naye ni Mjuzi wa kila kitu.

﴿ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ فَاعْبُدُوهُ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ﴾

102.Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu hakuna Mola (mwingine) isipokuwa Yeye; Muumba wa kila kitu, Kwa hivyo mwabuduni yeye. Na yeye ni mtegemewa wa kila kitu.

﴿لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ﴾

103.Hayamfikii macho, Bali yeye huyafikia macho. Naye ni Mpole Mwenye habari.

﴿قَدْ جَاءَكُم بَصَائِرُ مِن رَّبِّكُمْ فَمَنْ أَبْصَرَ فَلِنَفْسِهِ وَمَنْ عَمِيَ فَعَلَيْهَا وَمَا أَنَا عَلَيْكُم بِحَفِيظٍ﴾

104.Hakika zimewajia busara kutoka kwa Mola wenu. Basi atakayefungua macho ni faida yake mwenyewe; na atakayeyapofua ni hasara yake mwenyewe, Nami si mtunzaji wenu.

﴿وَكَذَٰلِكَ نُصَرِّفُ الْآيَاتِ وَلِيَقُولُوا دَرَسْتَ وَلِنُبَيِّنَهُ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ﴾

105.Na namna hii tunazifafanua ishara na waseme umesoma. Na ili tuyabainishe kwa watu wanaojua.

﴿اتَّبِعْ مَا أُوحِيَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ وَأَعْرِضْ عَنِ الْمُشْرِكِينَ﴾

106.Fuata uliyopewa wahyi kutoka kwa Mola wako. Hakuna Mola (mwingine) isipokuwa Yeye; na jitenge na washirikina.

﴿وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا أَشْرَكُوا وَمَا جَعَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ حَفِيظًا وَمَا أَنتَ عَلَيْهِم بِوَكِيلٍ﴾

107.Na kama Mwenyezi Mungu angetaka wasingeshirikisha. Na hatukukufanya uwe mtunzaji wao wala wewe si mlinzi juu yao.

WAMEMFANYIA MWENYEZI MUNGU WASHIRIKA

Aya 100-107

MAANA

Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu washirika majini.

Washirikina wako aina nyingi, kuna waliofanya masanamu ni miungu, kuna walioabudu nyota, walioabudu Iblisi na waliofanya giza kuwa ni Mungu. Kundi jingine wamefanya majini kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu ameeleza kuwapo Malaika na kwamba amewaumba kutokana na moto.

Katika Aya tuliyo nayo Mwenyezi mungu ameeleza tu kikundi ambacho kimewafanya majini ni washirika wa Mwenyezi Mungu, lakini hakubainisha aina ya majini hawa walioabudiwa na washirikina, je ni majini wa kuwazia tu au ni wengineo?

Kwa ajili hii ndipo wafasiri wakatofautiana, Kuna waliosema ni Ibilisi wengine wakasema ni giza na mengineyo ambayo hayana msingi wowote wa kielimu kabisa.

Kwa maana yoyote itakavyokuwa ni kwamba Mwenyezi Mungu amewajibu washirikina hawa kwa kifupituHali yeye amewaumba , na dhamir ya Amewaumba inawarudia majini. kwani wao ndio walio karibu na hiyo dhamir.

Inawezekana kuwa inawarudia wshirikina au wote, kwa sababu Mwenyezi Mungu ameumba majini na watu; kwa maana yakuwa ni vipi Mwenyezi Mungu awe na washirika naye ni Muumba wa kila kitu?

Na wamemsingizia kuwa na wana wa kike na wa kiume bila ujuzi.

Washirikina wa kiarabu walisema kuwa malaika ni mabinti wa Mungu, Mayahudi wakasema Uzair ni mwana wa Mungu na wakristo wakasema Masih ni mwana wa Mungu Maneno yote hayo ni dhana na madai bila ya ujuzi.

Ametakasika na ametukuka juu ya wanayombandikiza nayo.

Ametakata Mwenyezi Mungu na upungufu na yuko juu kuliko wanavyomsifu nayo, Mbunifu wa mbingu na ardhi. Yaani ameziumba bila ya mfano uliotangulia.

Inawezekanaje awe na mwana hali hana mke wa jinsia yake wala wa jinsia nyingine, kwa sababu hana mfano na kitu kingine naye ni mwenye kujitosha na kila kitu. Umetangulia ufafanuzi katika kufasiri Juz.5 (4:50)

Na ameumba kila kitu.

Na muumbwa hawezi kuwa mshirika na Muumba.

Naye ni Mjuzi wa kila kitu.

Pamoja na hayo ati hajui kama ana mtoto; lau angekuwa naye angelimjua. Kwa hivyo kuacha kujua jambo hakumaanishi kutokuwepo kulingana na asiyekiuwa Mwenyezi Mungu. Ama kulingana na Mwenyezi Mungu ni kuwa ujuzi wake hauepukani na kupatikana yanayojulikana.

Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu hakuna Mola (mwingine) isipokuwa Yeye; Muumba wa kila kitu, Kwa hivyo mwabuduni yeye.

Msemo unaelekezwa kwa washirikina maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amekusanya sifa zote za upweke, akaumba ulimwengu na vilivyomo na kupanga mambo yote basi yeye ndiye mwenye haki ya kumpwekesha kwa ibada wala msimshirikishe na yeyote pia msimnasibishie mke na mwana.

Hayamfikii macho.

Tumezungumzia kwa ufafanuzi kuhusu kumwona Mungu katika kufasiri Juz.1 (2:55)

Bali yeye huyafikia macho na mengineyo kwa sababu Yeye amekizunguka kila kitu.

Naye ni Mpole, Mwenye habari.

Mpole kwa waja wake, mwenye habari ya matendo yao na makusudio yao.

Hakika zimewajia busara kutoka kwa Mola wenu.

Makusudio ya busara hapa ni dalili na hoja za kuwepo Mwenyezi Mungu na kuwa Yeye ni mmoja, zikiwamo zile zilizotangulia kupasua mbegu na kokwa (konde), kuumba usiku na mchana, kuumba watu kutokana na nafsi moja na kuteremsha maji ambayo ni uhai wa kila kitu. Kutumia busara kuwa ni dalili ni katika hali ya kutumia kisababishi kuwa ni sababu. Kwani busara ni kujua kunakotokana na na moyo; na kujua huku kunatokana na dalili na hoja.

Basi atakayefungua macho ni faida yake mwenyewe; na atakayeyapofua ni hasara yake mwenyewe.

Baada ya kutoa dalili za mkato juu ya haki, hapa Mwenyezi Mungu anasema kuwa atakayefuata basi ameifanyia nafsi yake na atakayehalifu basi ameifanyia ubaya nafsi yake mwenyewe.

﴿إِنْ أَحْسَنتُمْ أَحْسَنتُمْ لِأَنفُسِكُمْ وَإِنْ أَسَأْتُمْ فَلَهَا﴾

"Mkifanya wema mnajifanyia wema nafsi zenu, mkifanya ubaya mnajifanyia nafsi zenu" (17:7)

Na namna hii tunazifafanua ishara na waseme umesoma. Na ili tuyabainishe kwa watu wanaojua.

Wakati wa Ujahiliyya Waarabu walikuwa hawajui kusoma, hawana elimu yoyote. Waliposikia Qur'an na wakaona fani za fasihi, aina kwa aina za hoja zinazowazima wao na yale wanayoyatukuza, Lakini bado waliendelea kukataa. Hali yao ilipokuwa hivyo walitafuta vijisababu wakasema: "Ewe Muhammad, Qur'an hii uliyokuja nayo umejifundisha tu wala sio Wahyi kutoka kwa Mungu".

Kwa maelekezo haya inatubainikia kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu: 'Na namna hii tunazifafanua ishara,' maana yake ni, tumetermsha katika Qur'an aina na dalili na ubainifu kwa makusudio ya kuongoka kwazo washirikina na waache kumwambia Mtume kuwa wewe umesoma.

Ama kauli yake: 'Ili tuyabainishe kwa watu wanaojua' maana yake ni tunazifanua Aya za Qur'an ili wanufaike nazo wale wanaojua maana yake uwaongoze kwenye imani na haki. Ama wajinga na wapotevu hakuna matarajio ya kuongoka kwao. mwisho wa mambo ni kuwa Aya hizi zinakata nyudhuru zao na kuwa ni hoja juu yao.

Fuata uliyopewa wahyi kutoka kwa Mola wako. Hakuna Mola (mwingine) isipokuwa Yeye; na jitenge na washirikina.

Hii ni amri ya Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake ya kuonya na kutoa bishara kwa Qur'an na kudumu juu ya hilo wala asijali ukanushaji wa washirikina na kukadhibisha na istihzai zao.

La kushangaza ni kauli ya asemaye kuwa Aya hii ni mansukh (imefutwa hukumu yake) na Aya ya kupigana. Mwenyezi Mungu hakumwamrisha Mtume kuacha kupigana na washirikina katika Aya hii mpaka isemwe kuwa ni mansukh ila amemwamrisha kufuatilila kuilingania haki na kutojali ukadhibishaji wa washirikina.

Kimsingi ni kuwa kulingania haki bila ya kujali ni jambo jingine na kupigana ni jambo jingine. Sharti ya kwanza ya naskh na mansukh (yenye kufuta na yenye kufutwa hukmu) ni kuwa maudhui yawe mamoja.

Na kama Mwenyezi Mungu angetaka wasingeshirikisha.

Yaani Yeye Mwenyezi Mungu mtukufu hakutaka kuwasukuma kwenye imani au kuwalazimisha kuacha ushirikina kwa neno 'kuwa ikawa' ambalo ameliumbia ulimwengu. Lau angelitaka waamini kwa matakwa haya basi wasingeshirikisha. Angalia tafsiri ya Juz.1 (2:26).

Na hatukukufanya uwe mtunzaji wao wala wewe si mlinzi juu yao.

Jumla ya kwanza na ya pili zina maana moja au maana yanayokurubiana wala hatufahamu lengo lolote la hilo isipokuwa kutilia mkazo; bali mkazo huu vilevile ni mkazo wa kauli yake: 'Na jitenge na washirikina.' Kwa sababu lau angelikuwa ni mtunzaji na mlinzi wao, basi isingelijuza kujitenga nao.

﴿إِنَّ إِلَيْنَا إِيَابَهُمْ ﴿٢٥﴾ ثُمَّ إِنَّ عَلَيْنَا حِسَابَهُم﴾

"Hakika ni kwetu sisi marejeo yao, kisha ni juu yetu sisi hesabu yao" (88:25-26)

﴿وَلَا تَسُبُّوا الَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ فَيَسُبُّوا اللَّـهَ عَدْوًا بِغَيْرِ عِلْمٍ كَذَٰلِكَ زَيَّنَّا لِكُلِّ أُمَّةٍ عَمَلَهُمْ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّهِم مَّرْجِعُهُمْ فَيُنَبِّئُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴾

108.Wala msiwatukane wale wanaoomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu wasije wakamtukana Mwenyezi Mungu kwa jeuri bila ya kujua, Kama hivyo tumewapambia kila umma vitendo vyao. Kisha marejeo yao yatakuwa kwa Mola wao, naye atawaambia yale waliyokuwa wakiyatenda.

﴿وَأَقْسَمُوا بِاللَّـهِ جَهْدَ أَيْمَانِهِمْ لَئِن جَاءَتْهُمْ آيَةٌ لَّيُؤْمِنُنَّ بِهَا قُلْ إِنَّمَا الْآيَاتُ عِندَ اللَّـهِ وَمَا يُشْعِرُكُمْ أَنَّهَا إِذَا جَاءَتْ لَا يُؤْمِنُونَ﴾

109.Na waliapa kwa Mwenyezi Mungu kwa ukomo wa viapo vyao, kuwa ikiwafikia ishara bila shaka wataiamini. Hakika ishara ziko kwa Mwenyezi Mungu tu. Na ni kitu gani kitakachowatambulisha ya kuwa zitakapowafikia hawataamini?

﴿وَنُقَلِّبُ أَفْئِدَتَهُمْ وَأَبْصَارَهُمْ كَمَا لَمْ يُؤْمِنُوا بِهِ أَوَّلَ مَرَّةٍ وَنَذَرُهُمْ فِي طُغْيَانِهِمْ يَعْمَهُونَ﴾

110.Na tutazigeuza nyoyo zao na macho yao kama walivyokuwa hawakuamini mara ya kwanza, Na tutawaacha katika upotevu wao wakimangamanga.

MSIWATUKANE

Aya 108-109

MAANA

Wala msiwatukane wale wanaoomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu wasije wakamtukana Mwenyezi Mungu kwa jeuri bila ya kujua.

Wamesema kuwa Waislamu walikuwa wakiwatusi makafiri na wao huwajibu kwa kumtukana Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kauli hii haiko mbali sana na maana. Mara nyingi hutokea hivyo kwa wanaotofautiana kidini.

Tamko la Aya pia halilikatai hilo, bali imepokewa kutoka kwa Imam Jafar Aswadiq(a.s) kwamba aliulizwa kuhusu kauli ya Mtume:"Hakika shirki inajificha zaidi kuliko mtambao wa chungu kwenye jiwe jeusi katika usiku wa giza"

Akajibu:"Waumini walikuwa wakiwatukana wanaoabudiwa na washirikina na wakawa wanamtukana anayebudiwa na waumini. Waumini wakakatazwa kuwatukana waungu wao ili makafiri wasimtukane Mungu wa waumini.

Kama kwamba waumni wamemshirikisha Mwenyezi Mungu bila ya kujua, Kauli yake Mwenyezi Mungu 'bila ya kujua', Ni ishara ya ujinga wa washirikina. Katika Aya kuna ufahamisho wazi kuwa; ambalo lina madhara zaidi ya manufaa ni haramu na kwamba Mwenyezi Mungu hatiiwi anapoasiwa.

Kama hivyo tumewapambia kila umma vitendo vyao.

Maana ya dhahiri ya jumla hii ni kuwa Mwenyezi Mungu kama alivyowapambia vitendo vyao, vilevile amewapambia wengine vitendo vyao hata washirikina. Lakini hakuna mwenye shaka kwamba maana haya sio makusudio, kwa sababu Shetani ndiye anayewapambia washirikina uasi kwa nukuu ya Aya 43 ya Sura hii.

Zaidi ya hayo ni kuwa Mwenyezi Mungu hamwamrishi mja wake ukafiri na ampambie kisha amwadhibu, bali ni kinyume na hayo. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ حَبَّبَ إِلَيْكُمُ الْإِيمَانَ وَزَيَّنَهُ فِي قُلُوبِكُمْ وَكَرَّهَ إِلَيْكُمُ الْكُفْرَ وَالْفُسُوقَ وَالْعِصْيَانَ﴾

"Lakini Mwenyezi Mungu ameipendezesha kwenu imani na akaipamba nyoyoni mwenu na amewaafanya muuchukie ukafiri na ufasiki na uasi" (49:7)

Kwa ajili hii tunatilia nguvu kuichukulia Aya kuwa Mwenyezi Mungu amewaumba watu katika hali inayoona vizuri vitendo anavyovifanya mtu na inayokwenda na desturi na akampa akili ya kupambanua baya na zuri. Lau angeliwaumba katika hali ambayo inaona ubaya wa vitendo vyake vyote, asingelifanya chochote. Haya ndiyo maana ya kauli yake hiyo Mwenyezi Mungu: 'Tumewapambia kila umma vitendo vyao' sawa na kauli yake:

﴿كُلُّ حِزْبٍ بِمَا لَدَيْهِمْ فَرِحُونَ﴾

"Kila kundi linafurahia kwa waliyo nayo" (23:53)

Nasi tunasema: "Kila mtu huridhia amali yake".

Kisha marejeo yao yatakuwa kwa Mola wao, naye atawaambia yale waliyokuwa wakiyatenda.

Kwa hiyo waumini waache kutukana waungu wa washirikina, maadamu Mwenyezi Mungu atawaadhibu.

Unaweza kuuliza : kuwa anayemtukana Mwenyezi Mungu au Mtume wake ni wajibu kumuua, lakini mbona Aya hii inafahamisha kuwa ataachiwa hisabu yake na adhabu yake siku ya Kiyama?

Jibu : Aya hii ilishuka Makka, siku waislamu walipokuwa dhaifu, wakiwa bado hawajapewa ruhusa ya kupigana. Kwa sababu kupigana wakati huo kulikuwa ni kama kujiua. Ama ulipokuwa na nguvu Uislamu, ikawa ni wajibu kutekeleza hukumu ya kuuawa kwa mwenye kutukana; wala haijuzu kuchelewesha.

Na waliapa kwa Mwenyezi Mungu kwa ukomo wa viapo vyao, kuwa ikiwafikia ishara bila shaka wataiamini.

Mwenyezi Mungu (swt) alimpa nguvu Mtume wake Muhammad(s.a.w.w) kwa dalili za kutosha juu ya Utume wake, lakini washirikina wa Kikuraishi wakamtaka Muhammad(s.a.w.w) muujiza maalum na kufanya ndio sharti la kuamini kwao. Wakaapa kwa kiapo cha nguvu kuwa kama Muhammad atawakubalia maoni yao watamwamini. Ndipo Mwenyezi Mungu akamwamrisha Mtume wake kuwaambia:

Hakika ishara ziko kwa Mwenyezi Mungu huziteremsha kwa hoja inayowasimamia wote. Zaidi ya hapo huteremsha au huacha kuteremsha kwa hekima yake na kupitisha kwake.

Waumini wakatamani Mwenyezi Mungu aitikie maombi ya makafiri kwa kuwataka wasilimu na waamini. Mwenyezi Mungu akawaambia kwa kauli yake:

Na ni kitu gani kitakachowatambulisha ya kuwa zitakapowafikia hawataamini?

Yaani kutoka wapi mmejua kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) akiteremsha muujiza waliotaka makafiri wataacha kufuru yao na inadi yao? Yametangulia maelezo kwa ufafanuzi katika kufasiri Sura hii, Aya 34 - 37 na katika kufasiri Juz.1 (2:118)

Na tutazigeuza nyoyo zao na macho yao kama kama walivyokuwa hawakuamini mara ya kwanza.

Tutazigeuza nyoyo zao na macho yao ni fumbo la kujua Mwenyezi Mungu hakika yao, Dhamir ya kumwamini inamrudia Muhammad au Qur'an. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu anajua kuwa washirikina hawataamini baada ya kushuka muujiza waliotaka, bali wao wataendelea kung'ang'ania upotevu wao wa kwanza waliokuwa nao kabla ya kushuka muujiza wanaoutaka. Wao ni watafutaji wa batili na upotevu, na wala sio watafutaji wa haki na uongofu.

Na tutawaacha katika upotevu wao wakimangamanga.

Yaani baada ya kung'anga'ania upotevu, pamoja na kusimamishiwa hoja, tutawaacha na upotevu wao mpaka ifike siku watakayopata malipo ya amali yao, Yamekaririka maana haya katika Aya kadhaa.

MWISHO WA JUZUU YA SABA

15

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

6

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TATU

SAURATU AL -IMRAN

Aya 1-6

﴿الم ﴾

1.Alif laam miim

﴿اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ ﴾

2.Mwenyezi Mungu hakuna mola isipokuwa yeye aliyehai msimamizi wa kila jambo.

﴿نَزَّلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ مُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ وَأَنزَلَ التَّوْرَاةَ وَالْإِنجِيلَ﴾

3.Amekuteremshia kitabu kwa haki kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake. Na aliteremsha Tawrat na Injil.

﴿مِن قَبْلُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَأَنزَلَ الْفُرْقَانَ إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِ اللَّـهِ لَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ ذُو انتِقَامٍ﴾

4.Kabla yake ziwe ni uwongozi kwa watu na ameteremsha upambanuzi. Hakika wale waliokufuru Aya za Mwenyezi Mungu wana adhabu kali, na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu Mwenye kutia adabu

﴿إِنَّ اللَّـهَ لَا يَخْفَىٰ عَلَيْهِ شَيْءٌ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي السَّمَاءِ ﴾

5.Hakika MwenyeziMungu hakifichiki Kwake chochote kilichomo ardhini wala kilichomo mbingu.

﴿هُوَ الَّذِي يُصَوِّرُكُمْ فِي الْأَرْحَامِ كَيْفَ يَشَاءُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴾

6. Yeye ndiye anaye kuundeni ndani ya matumbo ya wazazi kwa namna apendayo. Hapana mungu ila Yeye, Mwenye nguvu na Mwenye hikima.

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye kurehemu

MAANA

Yamekwishapita maelezo kuhusu (Alif Laam Miim) katika mwanzo wa Sura Baqara. Vile vile maelezo ya hakuna Mola, yameelezwa mwanzo wa Aya Kursiy (2: 255).

Amekuteremshia Kitabu kwa haki, kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake.

Makusudio ya Kitabu ni Qur'an; ambayo inasadikisha vitabu vilivyoteremshiwa Mitume waliotangulia. Kimsingi ni kwamba kusadikishwa yaliyoteremshiwa Mitume waliotangulia, hakulazimishi kusadikisha vitabu vinavyonasibishwa kwao na baadhi ya makundi. Na sisi waislamu tumeamini kauli ya Mtume(s.a.w.w) , lakini pamoja na hivyo hatuamini kila kilicho katika vitabu vya Hadith zilizoelezwa kutokana naye. Ama yule anayeamini vitabu vilivyotangulia, basi ni juu yake kuamini Qur'an, vinginevyo atakuwa anajipinga yeye mwenyewe, Kwa sababu Qur'an inasadikisha vitabu hivyo, Kwa hiyo kuikadhibisha Qur'an ndio kuvikadhibisha vitabu vingine.

Na aliteremsha Tawrat na Injil kabla yake, ziwe ni uwongozi kwa watu.

Kuisifu Tawrat na Injil kuwa ni uongozi, kunalazimisha kuwa vimeteremshwa kwa haki; kama ambavyo kuisifu Qur'an kuwa ni uwongozi kunalazimisha kuwa imeteremshwa kwa haki. Kwa hivyo basi, kila kimoja katika vitabu vitatu hivyo ni cha haki na ni uwongozi. Makusudio ya uwongozi hapa, ni ubainisho wa Mwenyezi Mungu (s.w.t) wa halali na haramu kupitia katika ulimi wa Mitume Yake.Na ubainifu huu unamaanisha kujua hukumu za Mwenyezi Mungu.

Ama kuzitumia hizo hukumu, kunahitaji aina nyingine ya uwongozi zaidi ya ubainifu.Mimi sikupata tamko jengine la kuelezea aina hiyo isipokuwa neno Tawfiq.Nayo inaashiriwa na neno lake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿ إِنَّكَ لَا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَهْدِي مَن يَشَاءُ﴾

"Kwa hakika wewe huwezi kumwongoza umpendaye, lakini Mwenyezi Mungu humwongoza amtakaye" (28: 56)

Qur'an inalitumia Neno Tawrat kwa maana ya wahyi ulioteremshiwa nabii Musa(a.s) ; na neno Injil kwa Wahyi ulioteremshiwa nabii Isa(a.s) . Lakini Qur'an imebainisha kuwa Tawrat na Injil inayozikubali sio zile zilizoko kwa mayahudi na wakristo hivi sasa. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

﴿مِّنَ الَّذِينَ هَادُوا يُحَرِّفُونَ الْكَلِمَ عَن مَّوَاضِعِهِ ﴾

"Miongoni mwa mayahudi wamo ambao huyabadilisha maneno kuyatoa mahali pake" (4:46)

﴿وَمِنَ الَّذِينَ قَالُوا إِنَّا نَصَارَىٰ أَخَذْنَا مِيثَاقَهُمْ فَنَسُوا حَظًّا مِّمَّا ذُكِّرُوا بِهِ ﴿١٤﴾ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ قَدْ جَاءَكُمْ رَسُولُنَا يُبَيِّنُ لَكُمْ كَثِيرًا مِّمَّا كُنتُمْ تُخْفُونَ مِنَ الْكِتَابِ ﴾

"Na kwa wale waliosema: Sisi ni wanasara (Wakristo) tulichukua ahadi kwao, lakini wakaacha sehemu ya yale waliyokumbushwa… Enyi watu wa Kitabu! Amekwisha wafikia mtume wetu, anayewabainisha mengi mliyokuwa mkiyaficha katika kitabu…" (5:14-15)

Wahubiri wa kimasihi wanayajua sana haya, lakini pamoja na hayo wanajisifu na kuwavunga watu kuwa Qur'an inakiri Tawrat na Injil iliyochezewa na mikono ya kugeuza.

Ilivyo, ni kuwa Qur'an yote ni moja na jumla moja; kwa hiyo haifai kuamini sehemu fulani na kukanusha sehemu nyingine.

Tawrat ni neno la Kiebrania lenye maana ya sharia; nayo imegawanywa kwenye vitabu vitano:

1. Mwanzo, chenye maelezo ya kuanza kuumbwa ulimwengu na habari za Mitume.

2. Kutoka, ndani yake mna historia ya wana wa Israil na kisa cha Musa.

3. Kumbukumbu la Tawrat, humo mna hukumu za sharia ya Kiyahudi.

4. Walawi, humo mna mambo ya ibada na ndege na wanyama walioharamishwa.

Walawi ni kizazi cha mmojawapo wa watoto wa Yakub anayeitwa Lawi.

5. Hesabu, ndani yake mna mkusanyiko wa koo za Wana wa Israil na majeshi yao. Vitabu hivi vitano ni mkusanyiko wa vitabu vidogo vidogo vipatavyo thelathini na tisa, na wakristo wanaviita Agano la kale. Ama Injil, asili yake ni neno la kiyunani; maana yake ni bishara (khabari njema). Na Injili kwa wakristo ni nne:

1. Mathayo: Historia ya kutungwa kwake ina kiasi cha miaka 60 (A.D) Na iliandikwa katika lugha ya kiarmenia.

2. Marko: iliyotungwa kwenye mwaka wa 63 au 65 (A.D) kwa lugha ya kiyunani.

3. Luka: iliyotungwa pia kwa lugha ya kiyunani kwa tarehe ile ya Marko.

4. Yohana: vile vile kwa lugha ya kiyunani kwenye mwaka 90 (A.D.) Rai ya wakristo ilithibiti mwanzoni wa karne ya 5 A.D kwa kutegemea vitabu ishirini na saba katika vitabu vyao. Wakasema kwamba ni ufunuo (wahyi) kutoka kwa Mungu kwa kimaana sio kitamko. Na wakavipa jina la Agano jipya, likiwa ni mkabala wa lile la zamani wanalolitegemea mayahudi. Kwa hiyo Agano la zamani, ni agano la Musa; na lile jipya ni la Isa, umepita ufafanuzi unaombatana na hayo katika Sura ya pili, Aya ya tatu.

Na ameteremsha upambanuzi

Yaani upambanuzi baina ya haki na batili. Wametofautiana sana kuhusu makusudio ya upambanuzi; je, ni akili, Zaburi, Qur'an au ni dalili inayopambanua baina ya haki na batili? Sheikh Muhammad Abduh amechagua akili

Mwenye Majmaul Bayan amechagua Qur'an, Tamko la Aya linachukua maana zote mbili

Hakika wale waliozikufuru Aya za Mwenyezi Mungu wana adhabu kali, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mwenye kutia adabu.

Wafasiri wanasema kwamba watu wapatao sitini katika wakristo wa Najran, Yemen, walimfikia Mtume mnamo mwaka wa tisa Hijria; mwaka uliojulikana kama mwaka wa ugeni. Kwani wageni wengi walimfikia Mtume kutoka sehemu mbali mbali za Bara Arabu, wakielezea utii na mapenzi yao kwake, baada ya Mwenyezi Mungu kumpa ushindi kwa maadui. Ugeni wa kinajran ulitoa hoja ya itikadi ya kikiristo ya utatu na uungu wa Isa. Kwa hoja ya kuwa Isa ni mtoto asiyekuwa na baba pamoja na miujiza aliyoifanya ambayo Qur'an imeielezea. Vilevile wafasiri wanasema Sura ya Al-Imran kuanzia mwanzo wake hadi Aya thamanini ilishuka juu ya wakristo wa Najran na majibu yao: Mwenyezi Mungu akaanza kwa kutaja Tawhid (umoja) ili kukanusha utatu; kisha akataja Qur'an, Tawrat na Injil kwamba vitabu vitatu hivi vinamwepusha Mwenyezi Mungu na mtoto na kugawanyika. Vilevile vinakanusha uungu wa Isa. Kisha Mwenyezi Mungu akataja:

Hakika Mwenyezi Mungu hakifichiki kwake chochote kilichomo ardhini wala kilichomo mbinguni

Ikiwa ni majibu ya kauli ya wakristo kwamba Isa alikuwa akijua ghaibu. Tena akaendelea Mwenyezi Mungu (s.w.t) kusema:

Yeye ndiye ambaye huwatia sura matumboni jinsi anavyotaka, hakuna Mola isipokuwa Yeye Mwenye nguvu na Mwenye hekima.

Mwenyezi Mungu anayataja haya ili abatilishe kauli ya Wakristo kwamba Isa ni Mungu kwa sababu ya kutokuwa na baba; kwa maana ya kuwa Mungu haumbwi na kuwa tumboni mwa mama. Akipenda anaweza kumuumba kupitia baba na kama akipenda anaweza kumuumba bila ya baba, kwa kiasi kile hekima yake takatifu inavyotaka. Kwa ufupi ni kuwa kutolea habari baadhi ya mambo ya ghaibu, kufufua baadhi ya wafu na kuzaliwa bila ya baba, hakumaanishi kuwa Isa (Yesu) ni Mungu. Kwa sababu Mungu ni yule anayejua mambo ya ghaibu, hakifichiki kwake chochote katika ardhi au mbinguni, Mwenye kufufua wafu wote sio baadhi, anayeweza kila kitu hata kuumba bila ya kitu kingine. Kwa dhahiri ni kwamba Isa hakuwa akijua ghaibu zote, wala hakuweza kufufua maiti wote na hakuumba yeyote tumboni mwa mama yake bila ya baba au na baba; bali kinyume chake ndio sahihi, kwani yeye ndiye aliyeumbwa ndani ya tumbo la uzazi

﴿هُوَ الَّذِي أَنزَلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ مِنْهُ آيَاتٌ مُّحْكَمَاتٌ هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ وَأُخَرُ مُتَشَابِهَاتٌ فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلَّا اللَّـهُ وَالرَّاسِخُونَ فِي الْعِلْمِ يَقُولُونَ آمَنَّا بِهِ كُلٌّ مِّنْ عِندِ رَبِّنَا وَمَا يَذَّكَّرُ إِلَّا أُولُو الْأَلْبَابِ ﴾

7.Yeye ndiye aliyekuteremshia Kitabu ndani yake zimo Aya zilizo waziwazi ambazo ndizo msingi wa Kitabu na nyingine zenye kufichikana. Wale ambao nyoyoni mwao mna upotofu wanafuata zile zinazotatiza kwa kutaka kuharibu na kutaka tafsiri yake. Na hajui tafsir yake isipokuwa Mwenyezi Mungu na waliozama katika elimu. Husema tumeziamini zote zimetoka kwa Mola wetu, Na hawakumbuki isipokuwa wenye akili.

﴿رَبَّنَا لَا تُزِغْ قُلُوبَنَا بَعْدَ إِذْ هَدَيْتَنَا وَهَبْ لَنَا مِن لَّدُنكَ رَحْمَةً إِنَّكَ أَنتَ الْوَهَّابُ﴾

8.Mola wetu! Usizipotoshe nyoyo zetu baada ya kutuongoza na utupe rehema kutoka kwako, Wewe ndiwe mpaji mkuu.

﴿رَبَّنَا إِنَّكَ جَامِعُ النَّاسِ لِيَوْمٍ لَّا رَيْبَ فِيهِ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُخْلِفُ الْمِيعَادَ ﴾

9.Mola wetu! Wewe ndiwe mwenye kuwakusanya watu katika siku isiyo na shaka ndani yake, Hakika Mwenyezi Mungu havunji miadi.

Aya 7 - 9

Yeye ndiye aliyekuteremshia Kitabu ndani yake zimo Aya zilizo waziwazi nazo ndizo msingi wa kitabu, Na nyingine zenye kufichikana.

Zilizo waziwazi ni Aya ambazo hazihitaji ufafanuzi na makusudio yake yanafahamika kwa njia ya mkato bila ya kuhitaji tafsiri, kuhusisha au kufutwa hukumu (Naskh). Wala haziwapi nafasi wale wenye maradhi ya kupoteza na kufikiri kwa taawili na kugeuza. Mfano: sema Yeye Mwenyezi Mungu ni mmoja Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila jambo Wala hadhulumu (hata amali) sawa na chembe Hakika Mwenyezi Mungu haamrishi uovu...Na kwamba Kiyama kitakuja hakuna shaka.

Na Aya nyenginezo ambazo anaweza kuzifahamu mwenye elimu na asiyekuwa na elimu. Ama Aya zenye kufichikana ziko aina nyingi: Kuna zinazofahamika kiujumla bila ya upambanuzi, mfano kauli yake Mwenyezi Mungu:

Na tukampulizia katika roho yetu (21:91) Kwa hakika kujua roho yenyewe hasa ni nini, hiyo ni siri ya Mungu haijui yeyote hata wataalamu pia. Na wala sio sharti anayeambiwa kitu kuwa lazima ajue anayoambiwa kwa upambanuzi, bali inatosha tu kufahamu kiujumla.

Nyengine ni zile zinazofahamisha jambo linalokataliwa na akili mfano, kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ ﴾

"Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema amestawi juu ya kiti cha enzi." (20:5)

Hapa akili inakataa kwamba Mwenyezi Mungu akae juu ya kiti, kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni zaidi ya wakati na mahali. Kwa hiyo hapo inabidi kuleta tafsiri kwa maana ya kutawala. Na hapana budi kuwa tafsiri (taawil) iwe ni dalili sahihi itakayotoa maana sahihi ya tamko; na hayo hawayajui isipokuwa watu maalum. Aya nyingine iliyofichikana, ni kukubali tamko baina ya maana mbili na zaidi, mfano:

﴿وَالْمُطَلَّقَاتُ يَتَرَبَّصْنَ بِأَنفُسِهِنَّ ثَلَاثَةَ قُرُوءٍ ﴾

Na wanawake walioachwa wangoje mpaka tohara tatu (2: 228)

Hapo kuna 'Quruw' ambalo linakubali maana ya tohara na hedhi. Nyengine ni kuwa tamko ni la kiujumla maana yake ya dhahiri yawaingiza wote ingawaje makusudio ni baadhi tu; mfano:

﴿وَالسَّارِقُ وَالسَّارِقَةُ فَاقْطَعُوا أَيْدِيَهُمَا ﴾

"Na mwizi mwanamume na mwizi mwanamke, ikatwe mikono yao" (5:38)

Hapo wametajwa wezi wote pamoja na kujulikana kuwa kuna wezi wengine hawakatwi; kama ikiwa mwizi ni baba wa aliyeibiwa, au mwaka wa njaa, au kilichoibwa kikiwa hakikuhifadhiwa, au thamani ya kilichoibiwa ikiwa chini ya robo dinari. Nyengine ni kufutwa hukumu na kuwekwa nyengine; kama vile kuswali kuelekea Baitul Maqdis, ambapo ilifahamika kuthibiti Kibla hiki na ikaendelea hukumu mwanzoni mwa uislam, kisha ikaja hukumu ya kufuta hilo na Kibla kikawa Al-kaaba.Sio sharti kutotarajiwa kujulikana Aya za kufichikana kabisa. Kwani aina zote ukiondoa ile ya kwanza, inawezekana kwa wanavyuoni wa Usul - wanaojua njia za taawili, hukmu za kuhusisha na za kiujumla, kufuta na kufutwa na kutilia nguvu baina hukumu mbili zinazopingana - kutoa hukmu za kuhusisha na za kiujumla, kupambanua baina ya kufuta na kufutwa, chenye nguvu na kisicho na nguvu na maana yanayoingilika akilini ambayo yamefanyiwa taawili baada ya kutoingilika akilini.

Ndio! Kwa asiyekuwa na elimu, hizo Aya za kufichikana zinabaki kuwa hivyo hivyo, kwa kuwa haijuzu kufanya taawili au kuchukua dhahiri inayokubali kuhusisha au kufutwa. Kwa ufupi ni kuwa wanavyuoni wanajua maana ya Qur'an ambayo kwao ni fasihi iliyo wazi. Kwa sababu haiwezekani kuwa Mwenyezi Mungu ateremshe maneno yasiyokuwa na maana au yasiyofahamiwa na yeyote. Itakuwaje hivyo ikiwa yeye mwenyewe Mwenyezi Mungu anaamrisha kuizingatia vizuri Qur'an; na mazingatio hayaji ila kwa kinachoingilika akilini; na kisichofahamika hakiwezi kuzingatiwa.

Unaweza kuuliza kuwa Mwenyezi Mungu amekisifu Kitabu Chake kitukufu kwamba Aya zake zote ni Muhkam (zenye maana wazi) pale alipotumia neno Uhkimat (11:1) Tena akasifu kuwa Aya zake zote ni Mutashabihat (zenye kufichikana) kwa kutumia neno Mutashabihat (39: 29). Na katika Aya hii tunayofasiri amekisifu kuwa baadhi yake ni zenye kufichikana na nyengine ziko wazi wazi. Je, Kuna njia gani ya mkusanyiko wa Aya hizi? Jibu: Makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu katika neno Uhkimat ni kuwekwa kwa mpango na kwamba yote ni fasaha iliyo na maana sahihi. Kwa hiyo tafsiri ni:

"(Hiki) ni Kitabu ambacho Aya zake zimepangwa vizuri" Makusudio ya Mutashabihat (kufichikana) ni kibalagha na kimwongozo. Kwa hiyo tafsiri ni: "Kitabu chenye kushabihiana"

Na kuwa nyengine ni Muhkamat na nyengine ni Mutashabihat, ni kama tuliyvotangulia kuelezea kuwa ni baadhi ziko wazi na baadhi zinatatiza zinazohitaji tafsir na tafsir inahitaji maarifa na elimu. Kwa hiyo hakuna mgongano baina ya Aya hizo tatu; ni kama mfano wa mwenye kusema: "Napenda safari, wala sipendi safari" lakini anakusudia kuwa anapenda safari katika nchi kavu lakini hapendi safari ya baharini. Sufi mmoja aliisema kumwambia Mola wake: Ee Mungu nimuonaye, hali yeye hanioni. Ee Mungu anionaye,wala mimi simuoni. Anakusudia kwamba anamuona Mwenyezi Mungu akimfadhilisha lakini Mwenyezi Mungu hamuoni yeye akimtii,na Mwenyezi Mungu anamuona akimuasi wala yeye hamwoni akimwadhibu.

Swali la pili, nini makusudio ya msingi wa Kitabu?

Jibu : Baada ya Mwenyezi Mungu kuelezea kwamba katika kitabu chake kuna Aya zenye kutatiza, ndipo akasema; lakini Aya za misingi ya itikadi - kama vile kumwamini Mwenyezi Mungu na kumwepusha na mshirika vilevile kuuamini utume wa Muhammad(s.a.w.w) na siku ya mwisho - ziko wazi zenye kubainisha makusudio bila ya mikanganyo yoyote; wala hazina nafasi ya kufanyiwa taawili, kuhusishwa au kuwa imefutwa hukumu yake; anaweza kuzifahamu mjuzi na asiyekuwa mjuzi; wakati huo zikiwa ni msingi katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa sababu zinaeleza itikadi, na nyenginezo ni matawi.

Kwa hiyo hakuna udhuru wowote kwa ugeni wa Yemen na wengineo kutaka Aya za kutatiza; kama vile Aya inayomsifu Isa kuwa roho wa Mwenyezi Mungu na kuacha Aya zilizo waziwazi zinazokanusha uungu wa Isa. Hakuna lolote kwa mwenye kujitia kutojua Aya waziwazi na kutaka Aya zinazotatiza isipokuwa ni maradhi ya moyo na kukusudia ufisadi tu. Swali la tatu: Kwa nini amesema: Msingi wa kitabu na asiseme Misingi ya kitabu.

Jibu : Amefanya umoja kwa kubainisha kwamba mkusanyiko wa Aya zote nyepesi kufahamika ni msingi wa Kitabu na wala sio Aya moja pekee kuwa ni msingi; mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu.

﴿وَجَعَلْنَا ابْنَ مَرْيَمَ وَأُمَّهُ آيَةً﴾

"Na tulimfanya mwana wa Maryam na mama yake ishara" (23:50).

Ishara moja, wala hakusema ni ishara mbili, kwa sababu kila mmoja ni fungu la kutimiza ishara kwa hiyo mama hawezi kuwa ishara bila ya mwana, na mwana hawezi kuwa ishara bila ya mama.

Wale ambao nyoyoni mwao mna upotofu wanafuata zile zinazotatiza kwa kutaka kuharibu na kutaka tafsiri yake.

Makusudio ya upotofu hapa ni kuiacha haki, na kutaka kuharibu ni ishara ya kwamba wenye makusudio mabaya wanatafuta yale yenye kutatiza na kuyafasiri kwa tafsiri ya kuharibu nyoyo na kuharibu watu na dini ya haki, kwa mfano wanatoa ushahidi kwa kauli yake Mwenyezi Mungu: "Na tukampulizia roho yetu" kwamba Masih ni jinsi ya Mwenyezi Mungu kwa sababu kila mmoja ni roho, na wanajitia kutojua Aya zilizo waziwazi mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿لَّقَدْ كَفَرَ الَّذِينَ قَالُوا إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الْمَسِيحُ ابْنُ مَرْيَمَ﴾

"Hakika wamekufuru wale waliosema: Mwenyezi Mungu ni Masih mwana wa Maryam." (5:17)

﴿مَّا الْمَسِيحُ ابْنُ مَرْيَمَ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِ الرُّسُلُ وَأُمُّهُ صِدِّيقَةٌ﴾

"Hakuwa Masih ila ni Mtume, na wamepita Mitume kabla yake, na mama yake ni mkweli." (5:75)

﴿ إِنَّ مَثَلَ عِيسَىٰ عِندَ اللَّـهِ كَمَثَلِ آدَمَ خَلَقَهُ مِن تُرَابٍ ثُمَّ قَالَ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴾

"Hakika mfano wa Isa mbele za Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam; alimwumba kwa udongo kisha akamwambia kuwa akawa." (3:59)

Zaidi ya hayo kuna Aya inayomuhusu Adam, isemayo:

﴿فَإِذَا سَوَّيْتُهُ وَنَفَخْتُ فِيهِ مِن رُّوحِي ﴾

"Nikishamkamilisha na kumpuliza roho yangu" (15:29)

Kwa hiyo basi kutokana na madai yao, Adam pia atakuwa ni Mungu. Katika Majmaul-bayan imeelezwa kuwa mwanzo wa Sura Al-imran mpaka zaidi ya Aya themanini, zimeshuka kwa ugeni wa Najran. Walikuwa watu sitini, wakafika Madina kwa Mtume. Ulipofika wakati wao wa kuswali walipiga kengele na wakaenda kuswali katika msikiti wa Mtume. Masahaba wakasema: "Mbona wanaswali msikitini kwako?" Mtume akasema: "Waacheni" Basi wakaswali wakielekea Mashariki. Walipomaliza kuswali, Mtume alimwambia Seyyid na Aqib ambao walikuwa viongozi wa msafara na majibizano yakawa kama hivi ifuatavyo: Mtume: Silimuni wakristo:

Wakristo: Tumekwisha silimu.

Mtume: Mmesema uongo, si waislamu kwa kudai kwenu kuwa Mwenyezi Mungu ana mtoto, kuabudu msalaba na kwa kula nyama ya nguruwe.

Wakristo: Ikiwa Isa si mtoto wa Mwenyezi Mungu, basi baba yake ni nani?

Mtume: Hamjui kwamba mtoto hufanana na baba yake?: "Hamjui kwamba Mwenyezi Mungu yuko hai, hafi? Na Isa alitoweka?

Wakristo: "Ndio."

Mtume: Hamjui kwamba Mwenyezi Mungu ni msimamizi wa kila kitu?

Wakristo: Ndio

Mtume: Je, Isa anaweza hivyo?

Wakristo: La!

Mtume: Hivi hamjui kuwa Mwenyezi Mungu hali, hanywi wala haendi chooni?

Wakristo: Ndio

Mtume: Hamjui kuwa Isa alichukuliwa mimba na mama yake, kama wanawake wengine, akanyonyeshwa na akalishwa chakula na kwamba Isa anakula ana kunywa na kwenda haja?

Wakristo: Ndio

Mtume: Basi atakuwaje Mungu?

Wakristo: Wakanyamaza wasiwe na la kusema, Ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha kuwahusu, mwanzoni mwa Sura Al-imran kiasi cha Aya thamanini.

Na hajui tafsiri yake isipokuwa Mwenyezi Mungu na waliozama katika elimu.

Baadhi ya watu wanasema ni wajibu kuweka kituo kati ya neno Mwenyezi Mungu na waliozama; na kwamba waliozama ni maneno yanayoanza upya; kwa maana ya kuwa Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anayejua Aya zenye kutatiza, na sio waliozama katika elimu. Kitu cha kuangalia katika kauli hii ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni Mwenye hekima, hawezi kuwaambia watu wasivyovijua na asivyotaka wajue; kama tulivyobainisha. Kwa hiyo sahihi ni kuwa neno 'waliozama katika elimu, linaugana na Mwenyezi Mungu; na kwamba maana yake ni anajua tafsiri yake Mwenyezi Mungu na waliozama katika elimu. Amirul-muminin Ali(a.s) anasema:"Hiyo ni Qur'an iliyonyamaza na mimi ni Qur'an inayosema"

Na Ibn Abbas alikuwa akisema: "Mimi ni miongoni mwa waliozama kaitka elimu; mimi ninajua tafsiri yake" Kwa ujumla ni kwamba mwenye elimu ya haki ni yule anayeepuka kusema bila ya ujuzi. Bali huko kuzama katika elimu ni kuepuka kusema bila ya ujuzi. Iko Hadith isemayo: "Kuepuka yenye kutatiza ni bora kuliko kujingiza katika maangamizi." Unaweza kuuliza kwa nini Mwenyezi Muangu (s.w.t) amefanya baadhi ya Aya za Qur'an ziwe wazi na nyengine zilizofichika? Kwa nini asizijalie kuwa waziwazi zote ? Ili aweze kufahamu mjuzi na asiyekuwa mjuzi?

Swali hilo limejibiwa kwa majibu mengi, lenye nguvu zaidi ni kwamba mwito wa Qur'an unamwelekea mjuzi na asiye na ujuzi, mwerevu na mjinga; na kwamba katika maana yako yaliyo maarufu na yenye kuzoeleka na wote hawahitajii elimu na kujifunza katika kuyajua; yanaweza kueleweka kwa ibara iliyo wazi anayoifahamu kila anayeambiwa. Maana nyengine yako ndani yasiyoweza kufahamiwa ila baada ya darasa na elimu.Wala haiwezekani kufahamika bila ya maandalizi hayo.

Hakika hii anaifahamu kila mtu, Basi hayo ndiyo yaliyofanya kuwa baadhi ya Aya ziwe dhahiri na nyengine za ndani; kuongezea kuwa mara nyengine hekima inataka kuweka maana ya ndani; kama kusema kwake Mwenyezi Mungu kupitia kwa Mtume wake:

﴿وَإِنَّا أَوْ إِيَّاكُمْ لَعَلَىٰ هُدًى أَوْ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴾

Hakika sisi au nyinyi tuko kwenye uongofu au upotevu ulio wazi (34:24)

Husema: "Tumeziamini, zote zimetoka kwa Mola wetu."

Hii ni jumla iliyoanza upya. Maana yake ni kuwa mjuzi wa haki husema kuwa Aya zilizofichikana na zile nyepesi zote ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na mwenye kuziacha nyepesi na kujishughulisha na za kutatiza tu, kwa kutaka kuharibu basi huyo ni mfisadi mwenye maradhi ya moyo.

Na hawakumbuki isipokuwa wenye akili

Wale ambao wanajua hekima katika kupatikana za waziwazi na zisizowazi katika Qur'an wala hawazifanyi zile zilizo wazi kuwa ni njia ya kupoteza

"Mola wetu! Usizipotoshe nyoyo zetu baada ya kutuongoza na utupe rehema kutoka kwako. Wewe ndiwe mpaji mkuu"

Hiyo ni dua anayoiomba kila mjuzi mwenye ikhlasi kwa kuhofia asiingie makosani na kufanya uzembe katika kutafuta yaliyo sawa.

﴿إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا لَن تُغْنِيَ عَنْهُمْ أَمْوَالُهُمْ وَلَا أَوْلَادُهُم مِّنَ اللَّـهِ شَيْئًا وَأُولَـٰئِكَ هُمْ وَقُودُ النَّارِ﴾

10.Hakika wale ambao wamekufuru hazitawafaa kitu mali zao na watoto wao kwa Mwenyezi Mungu; na hao ndio kuni za Moto.

﴿كَدَأْبِ آلِ فِرْعَوْنَ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا فَأَخَذَهُمُ اللَّـهُ بِذُنُوبِهِمْ وَاللَّـهُ شَدِيدُ الْعِقَابِ ﴾

11.Kama desturi ya watu wa firauni na wale waliokuwa kabla yao. Walikadhibisha Aya zetu, Mwenyezi Mungu akawatia adabu kwa sababu ya dhambi zao; na Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.

﴿قُل لِّلَّذِينَ كَفَرُوا سَتُغْلَبُونَ وَتُحْشَرُونَ إِلَىٰ جَهَنَّمَ وَبِئْسَ الْمِهَادُ ﴾

12.Waambie wale waliokufuru: Mtashindwa na mtakusanywa mtiwe kwenye Jahannam; nako ni makao mabaya.

﴿قَدْ كَانَ لَكُمْ آيَةٌ فِي فِئَتَيْنِ الْتَقَتَا فِئَةٌ تُقَاتِلُ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَأُخْرَىٰ كَافِرَةٌ يَرَوْنَهُم مِّثْلَيْهِمْ رَأْيَ الْعَيْنِ وَاللَّـهُ يُؤَيِّدُ بِنَصْرِهِ مَن يَشَاءُ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَعِبْرَةً لِّأُولِي الْأَبْصَارِ ﴾

13.Hakika ilikuwa ni ishara kwenu katika yale makundi mawili yalipokutana. Kundi moja likipigana katika njia ya Mwenyezi Mungu na jingine kafiri, likawaona mara mbili zaidi kuliko wao kwa kuona kwa macho hakika katika hayo kuna mazingatio kwa wenye busara.

Hazitawafaa kitu mali zao na watoto wao

HAZITAWAFAA KITU MALI ZAO NA WATOTO WAO

Aya 10 -13

MAANA

Hakika wale ambao wamekufuru hazitawafaa kitu mali zao na watoto wao kwa Mwenyezi Mungu; na hao ndio kuni za moto.

Mwenye kufuatilia Aya za Qur'an, yenye hekima, kuhusu kuwazungumzia matajiri, ataziona kuwa zinawataja kwa sifa mbalimbali mbaya kama ifuatavyo:

-Ujeuri, Mwenyezi Mungu anasema:

﴿ كَلَّا إِنَّ الْإِنسَانَ لَيَطْغَىٰ ﴿٦﴾ أَن رَّآهُ اسْتَغْنَىٰ ﴾

Hakika binadamu hupetuka mipaka kwa kujiona amejitosha (96: 6-7)

–Kuhadaika, Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَدَخَلَ جَنَّتَهُ وَهُوَ ظَالِمٌ لِّنَفْسِهِ قَالَ مَا أَظُنُّ أَن تَبِيدَ هَـٰذِهِ أَبَدًا ﴿٣٥﴾ وَمَا أَظُنُّ السَّاعَةَ قَائِمَةً﴾

"Na akaingia katika bustani yake na hali ya kuwa anajidhulumu nafsi yake akasema: "Sidhani kabisa kuwa itaharibika. Wala sidhani kuwa kiyama kitatokea…" (18: 35-36)

-Tamaa Mwenyezi Mungu anasema:

Na nikamjaalia awe na mali nyingi Kisha anatumai nimzidishie.(74:12-15)

-Kuwa na mawazo potofu kwamba mali itawakinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَقَالُوا نَحْنُ أَكْثَرُ أَمْوَالًا وَأَوْلَادًا وَمَا نَحْنُ بِمُعَذَّبِينَ ﴾

"Na wakasema: 'sisi tunazo mali nyingi na watoto wengi wala sisi hatutaadhibiwa." (34:35)

Mwenyezi Mungu ameziondoa dhana zote hizi kwa kusema kwamba mali na watoto hazitoshelezi kitu, bali mali zitamfanya aliye nazo kuwa kuni kesho; kama vile miti. Wapotofu wanadhani kwamba mali zao na watoto wao wataweza kuwahami hapa duniani, lakini wanapokabiliana na wenye haki ana kwa ana katika uwanja wa vita hubainika unyonge wao. Kwa sababu Mungu huwapa nguvu wakweli kwa nusura yake na humdhalilisha yule mfisadi aliye mwongo sana.

WENYE MALI

Historia haijajua watu waovu na wadhalimu wakubwa zaidi wakati huu kuliko wenye mali na utajiri waliolundika. Wao ndio wanaoleta fitina, uharibifu na vita; wanapanga kila mbinu kujaribu kuzuia harakati zozote za ukombozi popote pale ulimwenguni. Wanaanzisha vyama vya vibaraka wao, vikosi vya umoja, wapelelezi na majasusi katika pembe zote za dunia ili waugeuze ulimwengu uwe ni kinyang'anyiro cha shirika la mamilionea. Wao hawaamini Mungu wala utu au jambo lolote isipokuwa wanaamini hisa ambazo zitanyonya faida kutoka katika jasho la watu, damu yao na mustakbali wao. Dola zao zinajishughulisha kueneza hofu, wasiswasi na ukandamizaji wa kichumi na kisiasa kwa wanyonge. Wanatumia kila mbinu kuwagawaya watu wasiwe na umoja, ili watu wote wawatumikie wao.

Kwa ajili hiyo, ndipo uislamu ukaharamisha ulanguzi na utajiri usiofuata sharia na kuwakandamiza wanyonge. Na umewatisha wale wanaolimbikiza mali bila ya kuzitoa sabili na kuita wapetukaji mipaka.

Kama desturi ya watu wa firaun na wale waliokuwa kabla yao; walikadhibisha Aya zetu Mwenyezi Mungu akawatia adabu kwa sababu ya dhambi zao na Mwenyezi Mungu ni mkali wa adhabu.

Yaani wingi wa mali na watoto sio sababu ya kufuzu na kuokoka. Mara nyingi mafukara wameshinda matajiri na uchache ukashinda wingi. Historia imejaa ushahidi wa ukweli huu. Firaun na watu wake walikuwa wengi wenye jaha, usultani, mali na vifaa, lakini pamoja na hayo Mwenyezi Mungu aliwafedhehesha na kumpa ushindi Musa asiyekuwa na mali wala wingi wa watu; kama ambavyo alimpa ushindi Nuh kwa watu wa zama zake, Ibrahim kwa Namrud, Hud kwa Ad na Saleh kwa Thamud. Kwa hiyo wingi na utajiri sio hoja, Na wanaomkadhibisha Mtume Muhammad(s.a.w.w) nao mwisho wao utakuwa hivyo hivyo.

Waambie wale waliokufuru: Mtashindwa na mtakusanywa mtiwe katika Jahannam, nako ni makao mabaya.

Imeelezwa katika Majamaul-bayan kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) alipompa ushindi Mtume wake katika vita vya Badr,alipofika Madina Mtume aliwakusanya Mayahudi na kuwaambia: "Tahadharini yasije yakawapata yaliyowapata maquraish katika Badr." Wakamwambia: "Usihadaike, wewe umekutana na watu wasiojua vita; lau ungelikutana na sisi ungelijua kwamba sisi ni watu;" ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hii. Mwenyezi Mungu alitimiza miadi yake: Waislamu wakawaua Bani Quraydha wahaini na wakawafagia Bani Nadhir wanafiki, wakaichukua Khaybar na wakawatoza kodi wengine.

Hakika ilikuwa ni ishara kwenu katika yale makundi mawili yalipokutana na kundi moja lilipigana katika njia ya Mwenyezi Mungu na jingine kafiri, likiwaona mara mbili zaidi kuliko wao kwa kuona kwa macho.

Mwenyezi Mungu katika Aya hii anawaonyaMayahudi, manaswara, waislamu na wenye busara wote kwa ujumla kuhusu vita vya Badr wakati kilipokutana kikosi cha Mtume ambacho ni Muhammad na sahaba zake na kikosi cha shetani ambacho kilikuwa zaidi ya watu elfu, wakiwa wamejisheheneza silaha za kutosha. Na kikosi cha Mtume kilikuwa ni theluthi tu ya idadi yao, wakiwa hawana zana zozote zaidi ya farasi wawili, deraya saba na panga nane, lakini pamoja na hayo Mungu aliwaandikia ushindi hao wachache; Mwenyezi Mungu akawaonyesha washirikina kuwa waislamu ni zaidi yao ingawaje ni wachache.

Aya hii iko katika mwelekeo wa Aya inayosema:

﴿وَإِذْ يُرِيكُمُوهُمْ إِذِ الْتَقَيْتُمْ فِي أَعْيُنِكُمْ قَلِيلًا وَيُقَلِّلُكُمْ فِي أَعْيُنِهِمْ لِيَقْضِيَ اللَّـهُ أَمْرًا كَانَ مَفْعُولًا وَإِلَى اللَّـهِ تُرْجَعُ الْأُمُورُ ﴾

"Na mlipokutana, akawaonyesha machoni mwenu kuwa wao ni wachache na akawafanya nyinyi ni wachache machoni mwao, ili Mwenyezi Mungu atimieze jambo lililokuwa liwe, Na mambo yote hurejezwa kwa Mwenyezi Mungu" (8:44)

Kwa mnasaba huu ni vizuri tutaje nasaha ya Imam Ali(a.s) kwa khalifa wa pili alipomtaka ushauri katika vita vya Roma; Imam alisema:

"Yule aliyenusuru Waislamu wakiwa ni wachache bado yuko hai, hafi, wewe ukienda mwenyewe katika vita na ukakimbia basi waislamu hawatakuwa na ngome wala kimbilio. Wewe mpeleke mtu mwenye uzowefu na umwandalie watu wenye uzoefu na wenye ushauri. Ikiwa Mwenyezi Mungu atakudhihirisha ndivyo unavyotaka, vinginevyo utakuwa ni kimbilio la watu.

﴿زُيِّنَ لِلنَّاسِ حُبُّ الشَّهَوَاتِ مِنَ النِّسَاءِ وَالْبَنِينَ وَالْقَنَاطِيرِ الْمُقَنطَرَةِ مِنَ الذَّهَبِ وَالْفِضَّةِ وَالْخَيْلِ الْمُسَوَّمَةِ وَالْأَنْعَامِ وَالْحَرْثِ ذَٰلِكَ مَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَاللَّـهُ عِندَهُ حُسْنُ الْمَآبِ﴾

14.Watu wamepambiwa kupenda matamanio ya wanawake na watoto na mirundo ya dhahabu na fedha, na farasi wazuri, na mifugo na mashamba. Hivyo ni vitu vya anasa katika maisha ya dunia; na kwa Mwenyezi Mungu ndiko kwenye marejeo mazuri.

KUPENDA MATAMANIO

Aya 14

MAANA

Wametofautiana wafasiri kuwa ni nani anayewafanya watu kupenda matamanio. Baadhi wamesema ni Mwenyezi Mungu na wengine wakasema ni shetani. Lakini ukweli ulivyo, ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amempa mtu tabia ya kupendelea matamanio na shetani naye humtia wasiwasi mtu na kumfanyia nzuri amali mbaya; na ile mbaya anamfanyia aione nzuri. Hata hivyo kupenda wanawake, watoto na mali siko kubaya hasa; na wala Mwenyezi Mungu hakutuharamishia. Vipi isiwe hivyo na hali yeye Mwenyezi Mungu amesema: Waambie nimewahalalishia mema. Na Mtume(s.a.w.w) amesema: "Mimi ninapenda vitu vitatu katika dunia yenu: Manukato, wanawake, na kitulizo cha moyo wangu, Swala"

Makusudio ya matamanio hapa ni vitu anavyovipendelea mtu na kuhisi raha anapovipata. Unaweza kuuliza neno matamanio linakusanya maana ya mapenzi; kama ambavyo mapenzi yanakusanya maana ya matamanio. Kwa hivyo basi maana ya Aya yatakuwa kwamba watu wanapenda mapenzi na wanatamani matamanio, Na maneno ya Mwenyezi Mungu hayawezi kuwa katika hali hii ya kutonyooka.

Jibu : Kupenda kitu kuko namna mbili:

Kwanza : ni mtu kupenda kitu, lakini hapendi akipende, yaani nafsi yake inapenda kama ingewezekana asikipende kitu hicho, Kwa mfano mtu kupenda kuvuta sigara inayomdhuru, Mwenye pendo hili anataka limwondokee kila siku.

Pili : ni mtu kupenda kitu na yeye mwenyewe yuko radhi; kama mtu aliyezoweya kufanya amali za kheri. Mwenyezi Mungu anasema katika kumzungumzia Nabii Suleiman:

Hakika mimi ninapenda pendo la kheri (38:32)

Hili ni pendo la hali ya juu na mwenye pendo hilo hataki limwondokee.

Mrundo ni fumbo la wingi. Hadith inasema: "Lau mtu angekuwa na nyangwa mbili za dhahabu, basi angelitamani wa tatu; na wala hawezi kutosheka isipokuwa kwa mchanga." Kupenda wanawake, watoto na mali, kunapatikana wakati wote bali hayo ni matamanio ya kila nafsi. Ama kupenda farasi, wanyama na mashamba, Mwenyezi Mungu amekuhusisha kukutaja kwa wakati huo kwa sababu ndio vitu vilivyopendelewa zaidi. Wafasiri wengi kama vile Razi na mwenye Al-manar wamerefusha maneno katika kutaja kila moja katika aina hizi sita za ladha na starehe, lakini wametaja mambo ya dhahiri yanayojulikana na kuhisiwa na wote. Kwa hiyo hatukujishughulisha nayo na tunaonelea ni vizuri tutaje raha katika kifungu kinachofuatia.

RAHA

Baadhi ya watungaji wanaona kuwa raha inaweza kukamilika kwa binadamu kama akiwa na nguzo hizi nane: Afya, mke anayeafikiana naye, mali ya kutekeleza haja na jaha itakayohifadhi utukufu. Nafikiri mwenye rai hii ameangalia raha kwa upande wake na haja yake, sio kwa ilivyo hasa. Kama ni hivyo ataziweka wapi hisia za matatizo ya kilimwengu; kama vile hofu, mwisho mbaya na uongo, na matatizo mengineyo yanayousonga moyo. Kwa kweli kabisa raha kamili bado haijapatikana kwa binadamu; na ninafikiri haitapatikana katika maisha haya, ispokuwa maisha mengine. Ama raha ya upande fulani na wakati fulani imeweza kumpitia mtu, ijapokuwa utotoni. Ni vizuri kufafanua raha ya upande fulani kama ifutavyo: Kustarehe kuko kwa aina nyingi, kama kustarehe kwa kuangalia miti wakati wa maleleji na mito na maporomoko ya maji, au kusikiliza mashairi, au kustarehe kwa kusoma vitabu, na mengineyo katika mambo ya starehe za kiroho.

Katika starehe za kimaada ni wanawake, mali na watoto. Ama farasi wanyama na mashamba hiyo ni katika jumla ya mali. Lakini starehe hizi zote hazimpi binadamu raha kamili, kwa sababu dunia haimnyookei yeyote kwa kila upande. Akiwa ana uwezo wa kuyamudu maisha, basi atakuwa na matatizo ya nyumbani au katika uzao wake. Amirul Muumini Ali (a.s.) anasema: "Akipata raha mtu upande mmoja, atapata uchungu upande mwengine, Hawezi kupata mtu starehe ila atapata tabu" Ama raha ya upande fulani tu yaani katika hali fulani hiyo anaipata mtu. Mfano mzuri ni ule niliousoma katika baadhi ya vitabu. Mtungaji anasema: Familia moja ilitoka kwenda kwenye matembezi; akiwemo mama, watoto, ami, mjomba, baba na babu. Walipofika wanapokwenda, mtoto alielekea kwenye nyasi, mwengine akachuma maua, mama naye akatengeneza sandwichi, ami akatafuna tofaha, mjomba akazungusha gramafoni (kinanda), baba akajinyoosha mchangani akiwa anaangalia kondoo na babu naye akawa anajishughulisha na kuvuta buruma.

Basi ikawa kila mmoja anahisi raha kwa upande wake, lakini raha hiyo ni katika hali hiyo tu, sio katika hali zote, Hekima ya Mungu imepitisha kuwa raha kamili haiwezi kupatikana isipokuwa akhera. Kwa sababu hii ndipo akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu baada ya kutaja wanawake, watoto na mali kuwa kuna kilicho bora zaidi ya hivyo. Nimeona Riwaya kutoka kwa Imam Jaffar Sadiq(a.s) akizingatiya kuwa tawfiki ya Mungu ni nguzo miongoni mwa nguzo za msingi wa raha. Na, hakika hii nimeijua kwa hisia na majaribio.

﴿قُلْ أَؤُنَبِّئُكُم بِخَيْرٍ مِّن ذَٰلِكُمْ لِلَّذِينَ اتَّقَوْا عِندَ رَبِّهِمْ جَنَّاتٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا وَأَزْوَاجٌ مُّطَهَّرَةٌ وَرِضْوَانٌ مِّنَ اللَّـهِ وَاللَّـهُ بَصِيرٌ بِالْعِبَادِ ﴾

15.Sema: Je, niwambie yaliyo bora kuliko hayo kwa kwa wamchao Mungu? Kwa mola wao ziko bustani ambazo hupita chini yake mito; watakaa humo milele na wake waliotakaswa na wana radhi ya Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu anawaona waja.

﴿الَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا إِنَّنَا آمَنَّا فَاغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴾

16.Ambao wanasema: "Mola wetu! Hakika sisi tumeamini,basi tughufirie madhambi yetu. Na tuepushe na adhabu ya moto.

﴿الصَّابِرِينَ وَالصَّادِقِينَ وَالْقَانِتِينَ وَالْمُنفِقِينَ وَالْمُسْتَغْفِرِينَ بِالْأَسْحَارِ ﴾

17.Wanaofanya subira na wanaosema kweli na watiifu na wanaotoa na wanaoomba maghufira kabla ya Alfajiri.

YALIYOBORA

Aya 15-16

MAANA

Sema: Je, Niwaambie yaliyo bora kuliko haya kwa wamchao Mungu?

Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwanza ametaja kupenda wanawake, mali na watoto; kisha vitu vyote hivi akaviita anasa za dunia, na dunia inaondoka; na akabainisha kwamba kwake ndiko kwenye marejeo mazuri, yaani kwamba mtu baada ya kurejea kwa Mola wake atakuta mambo mazuri zaidi kuliko wanawake, mali na watoto na kuliko dunia yote. Baada ya hapo ndipo anafafanua kwa Aya hii.

Kwa Mola wao ziko bustani ambazo huipita chini yake mito; watakaa humo milele na wake waliotakaswa na wana radhi ya Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu anawaona waja.

Haya matatu ni bora kuliko wanawake, mali na watoto, nayo ni marejeo mazuri.

Kwanza : ni, pepo ambayo haitakwisha sio kama shamba, farasi na mifugo.

Pili : ni wanawake waliotakaswa na hedhi, hadathi na uchafu wote. Vilevile wametakaswa na kila kinyaa.

Tatu : ni radhi ya Mwenyezi Mungu ambayo ni kubwa zaidi kuliko dunia na akhera kwa pamoja. Yote hayo Mwenyezi Mungu ameyafanya ni malipo ya mwenye kuogopa kusimama mbele za Mola wake na akaikataza nafsi (yake) na matamanio.

Wanaofanya subira, na wanaosema kweli na watiifu na wanaotoa na wanaoomba maghufira kabla ya Alfajiri.

Mwenye kusubiri ni yule anayekabiliana na mambo kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu; na kuridhia natija ya makabiliano yake. Msema kweli ni yule anayesema ukweli hata kama unamdhuru. Mtiifu ni yule mwenye kufanya ibada akiwa mtiifu. Mtoaji ni yule anayejitolea mali na kuwatolea watu wake katika njia ya Mwenyezi Mungu. Na, wakati wa kabla ya alfajiri; ni wakati bora kuliko wowote kwa ibada na dua; kama ilivyoelezwa katika Hadith. Kwa sababu wakati huo uko mbali kabisa na shub'ha ya ria; Na, ni wakati ambao usingizi ni mtamu sana; kwa hivyo inakuwa tabu kuamka. Na amali bora zaidi ni ile yenye mashaka na tabu, ingawaje kuhudumia mtu ni bora zaidi kuliko Swala na Saumu.

MATUNDA YA IMANI

Sifa zote hizi tano (subira, ukweli, utiifu, kutoa na msamaha) ni matunda ya misingi mitatu ya dini; yaani kumwamini Mwenyezi Mungu mmoja aliye pekee, kuamini utume wa Muhammad(s.a.w.w) na kuamini siku ya mwisho. Misingi hii siyo kuwa ni mambo tu ya dini, bali inayo matunda na hakika zinazokusanywa na umbile tukufu, na amali yenye kunufaisha katika uhai. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّـهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ﴾

"Enyi mlioamini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume atakapowaita katika yale yatakayowapa maisha, (8:24)

Kila asili katika asili ya dini inasimama kwa misingi hii. Vilevile kila tawi katika matawi ya dini, ni misingi inayofungamanisha dini na matendo kwa ajili ya maisha. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿فَوَرَبِّكَ لَنَسْأَلَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٩٢﴾ عَمَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴾

Basi naapa kwa Mola wako tutawauliza wote. Juu ya yale waliyokuwa wakiyatenda. (15: 92 - 93)

﴿أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَعْلَمِ اللَّـهُ الَّذِينَ جَاهَدُوا مِنكُمْ وَيَعْلَمَ الصَّابِرِينَ ﴾

Je, mnadhani mtaingia peponi, bila ya Mwenyezi Mungu kuwapambanua wale waliopigana Jihadi miongoni mwenu na kuwapambanua waliofanya subira? (3:142)

Zimekuja Hadith kadhaa Mutawatir kwamba aina bora ya ibada na utiifu ni kufanya amali kwa ajili ya maisha mema na kwamba kubwa ya madhambi makubwa na maasi ni ufisadi na uadui kwa watu. Mtume anasema: "Karibu zaidi anapokuwa mja na Mola wake ni pale anapotia furaha katika moyo wa nduguye." Amirul-Muminiin anasema: "Masurufu mabaya siku ya marejeo ni uadui kwa waja" Mjukuu wake, Imam Baqir, naye anasema: "Mwenyezi Mungu ana watu waliobarikiwa, watu wengine wanaishi katika hifadhi zao; nao ni kama tone. Na kuna watu ni vikwazo, wala watu wengine hawaishi katika hifadhi zao; nao ni kama nzige kila kitu wanakitaka"

﴿شَهِدَ اللَّـهُ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ وَالْمَلَائِكَةُ وَأُولُو الْعِلْمِ قَائِمًا بِالْقِسْطِ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴾

18.Mwenyezi Mungu na Malaika na wenye elimu wameshuhudia ya kwamba hakuna Mola ila Yeye tu, Ndiye Mwenye kusimamia uadilifu. Hakuna mola isipokuwa Yeye,Mwenye nguvu Mwenye hekima.

﴿إِنَّ الدِّينَ عِندَ اللَّـهِ الْإِسْلَامُ وَمَا اخْتَلَفَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ إِلَّا مِن بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْعِلْمُ بَغْيًا بَيْنَهُمْ وَمَن يَكْفُرْ بِآيَاتِ اللَّـهِ فَإِنَّ اللَّـهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ ﴾

19.Hakika dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu. Na hawakukhitalifiana wale waliopewa Kitabu ila baada ya kuwajia ilimu. Kwa uhasidi uliokuwa baina yao. Na anayezikataa Aya za Mwenyezi Mungu basi Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.

﴿ فَإِنْ حَاجُّوكَ فَقُلْ أَسْلَمْتُ وَجْهِيَ لِلَّـهِ وَمَنِ اتَّبَعَنِ وَقُل لِّلَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ وَالْأُمِّيِّينَ أَأَسْلَمْتُمْ فَإِنْ أَسْلَمُوا فَقَدِ اهْتَدَوا وَّإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا عَلَيْكَ الْبَلَاغُ وَاللَّـهُ بَصِيرٌ بِالْعِبَادِ ﴾

20.Na kama wakikuhoji, basi sema: "Nimeusalimisha uso wangu kwa kumwelekea Mwenyezi Mungu, na walionifuata" Na waambie wale waliopewa Kitabu na wale wasiokuwa na kisomo na "Je,mmesilimu? Kama wakisilimu basi wameongoka; na kama wakikengeuka, basi juu yako ni kufikisha tu. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwaona waja

MWENYEZI MUNGU, MALAIKA NA WENYE ELIMU

Aya 18 - 20

MAANA

Mwenyezi Mungu na Malaika na wenye elimu wameshuhudia ya kwamba hakuna Mola isipokuwa yeye; Ndiye mwenye kusimamisha uadilifu, Hakuna Mola isipokuwa Yeye, Mwenye nguvu Mwenye hekima.

Kujishuhudia Mwenyezi Mungu yeye mwenyewe kuwa ni mmoja ni kutokana na vitendo Vyake ambavyo haviwezi yeyote isipokuwa Yeye; Mwenyezi Mungu anasema:

﴿سَنُرِيهِمْ آيَاتِنَا فِي الْآفَاقِ وَفِي أَنفُسِهِمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُ الْحَقُّ أَوَلَمْ يَكْفِ بِرَبِّكَ أَنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ﴾

"Tutawaonyesha ishara zetu katika upeo wa mbali na katika nafsi zao mpaka iwabainikie kuwa haya ni haki, Je haikutoshi kwamba Mola wako ni shahidi wa kila kitu" ? (41:53)

Ama ushuhuda wa Malaika kwa umoja wa Mungu ni kwamba wao wana maumbile ya imani. Makusudio ya wenye elimu hapa ni Mitume na wanavyuoni wote wanaomjua Mungu ambao wamekuwa makaimu wa Mitume katika kumlingania Mwenyezi Mungu. Na ushahidi wa mwanachuoni unaambatana na hoja ya kumkinaisha anayetafuta uhakika. Makusudio ya uadilifu hapa ni uadilifu katika dini na sharia na katika desturi ya maumbile na nidhamu yake, Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاءَ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا لَاعِبِينَ﴾

Na hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake kwa mchezo. (21:16)

Unaweza kuuliza nini makusudio ya kukaririka neno: 'Hakuna Mola isipokuwa yeye,' Katika Aya moja?

Jibu : Inajulikana kuwa katika njia ya Qur'an ni kukariri na kutilia mkazo misingi ya itikadi na misingi muhimu, hasa umoja. Hiyo ni kuondoa shaka. Tumefafanua kukaririka katika kifungu mbali, tulipofasiri Aya 48 Sura ya Baqara, Imesemekana kuwa makusudio ya kauli ya kwanza ni kujulisha kuwa yeye pekee ndiye anayestahiki kuabudiwa. Na, ya pili ni kujulisha kuwa hakuna yeyote mwenye kusimamia uadilifu isipokuwa yeye.

DINI YA MWENYEZI MUNGU NI UISLAMU

Unaweza kuuliza: Dhahiri ya Aya, Hakika dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni uislam, inafahamisha kuwa dini zote za mitume - hata dini ya Ibrahim - si chochote isipokuwa dini ya Muhammad (s.a.w.w.) na Qur'an tu? Jibu: Hapana, bali Aya hii inafahamisha kinyume kabisa na hivyo. Kwani dhahiri yake inatamka kwa lugha fasaha kwamba kila dini aliyokuja nayo Mtume miongoni mwa Mitume waliotangulia umbo lake linakuwa na mwito wa kiislamu ambao ameulingania Muhammad bin Abdullah (s.a.w.). Kwa ufafanuzi zaidi angalia hakika hizi zifuatazo:

1. Kabla ya jambo lolote kwanza, uislamu una mambo matatu; Kumwamini Mwenyezi Mungu na umoja wake, kuamini wahyi na Isma yake na kuamini ufufuo na malipo yake. Kila mmoja wetu anaamini kwa imani isiyokuwa na tashwish yoyote kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakupeleka Mtume yeyote isipokuwa kwa misingi mitatu hii. Kwa hali hiyo ndipo Mtume(s.a.w.w) akasema:"Sisi Mitume dini yetu ni moja"Akaendelea kusema: "Mitume ni ndugu katika shughuli (zao) baba yao ni mmoja na mama zao ni mbali mbali"

2. Neno: uislamu linatumiwa kwa maana nyingi; kama kunyeyekea, usafi na kusalimika na ila na uchafu. Hakuna mwenye shaka kwamba kila dini aliyokuja nayo Mtume katika Mitume wa Mwenyezi Mungu ni safi isiyokuwa na uchafu wowote. Kwa hiyo basi inafaa kulitumia neno uislam kwa dini zote za Mitume.

3. Rejea ya Qur'an ni moja, hakuna tofauti kati ya Aya zake, bali hiyo Qur'an inajifasiri yenyewe na kujitolea ushahidi hiyo yenyewe; kama alivyosema Imam Ali(a.s) :"Ikija Aya katika suala fulani au maudhui fulani, basi haifai kuiangalia peke yake, bali ni lazima kufuatilia kila Aya zilizo na uhusiano na suala hilo na maudhui hayo na kuzikusanya katika jumla moja kwa kuunganisha na nyengine, kisha tutoe maana moja katika Aya zinazooana" Tunapoangalia Aya zinazoelezea uislamu katika uhakika huu, tunakuta kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewasifu Mitume wote kwa Uislamu katika Aya nyingi. Kwa hivyo tunajua kuwa neno la Mwenyezi Mungu, Hakika dini mbele za Mwenyezi Mungu ni Uislamu linakusanya dini zote za haki. Siri ya hilo ni hayo tuliyoyaeleza kwamba dini zote za Mitume zinadhamini mwito wa kiislamu katika uhakika wake na dhati yake. Kwa kutilia mkazo imani ya Mwenyezi Mungu, wahyi na ufufuo. Ama tofauti inakuwa kaitka matawi na hukumu, sio katika misingi ya itikadi na imani.

Hebu tuangalie Aya ambazo Mwenyezi Mungu amewasifu Mitume kwa uislamu, tangu zama za Nuh(a.s) mpaka za Muhammad(s.a.w.w) , Amesema Mwenyezi Mungu kuhusu Nuh:

﴿وَاتْلُ عَلَيْهِمْ نَبَأَ نُوحٍ إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ يَا قَوْمِ﴿٧١﴾وَأُمِرْتُ أَنْ أَكُونَ مِنَ الْمُسْلِمِينَ ﴾

Na wasomee habari za Nuh alipowaambia watu wake Enyi watu wangu! ...Nimeamrishwa niwe miongoni mwa waislamu. (10: 71-72)

Kuhusu Ibrahim na Yakub anasema:

﴿وَوَصَّىٰ بِهَا إِبْرَاهِيمُ بَنِيهِ وَيَعْقُوبُ يَا بَنِيَّ إِنَّ اللَّـهَ اصْطَفَىٰ لَكُمُ الدِّينَ فَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ﴾

Na Ibrahim akawausia haya wanawe; na Yakub: "Enyi wanangu hakika Mwenyezi Mungu amewachagulia dini hii, basi msife ila mmekuwa waislamu" (2:132)

Kuhusu Yusuf anasema:

﴿أَنتَ وَلِيِّي فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ تَوَفَّنِي مُسْلِمًا وَأَلْحِقْنِي بِالصَّالِحِينَ﴾

"Wewe ndiwe mlinzi wangu katika dunia na akhera, nifishe hali ya kuwa ni Mwislamu" (12:101)

Kuhusu Musa anasema:

﴿وَقَالَ مُوسَىٰ يَا قَوْمِ إِن كُنتُمْ آمَنتُم بِاللَّـهِ فَعَلَيْهِ تَوَكَّلُوا إِن كُنتُم مُّسْلِمِينَ﴾

"Na Musa akasema: Enyi watu wangu! Ikiwa nyinyi mme mwamini Mwenyezi Mungu, basi mtegemeeni yeye kama nyinyi ni waislamu" (10:84)

Kwa Umma wa Isa anasema:

﴿وَإِذْ أَوْحَيْتُ إِلَى الْحَوَارِيِّينَ أَنْ آمِنُوا بِي وَبِرَسُولِي قَالُوا آمَنَّا وَاشْهَدْ بِأَنَّنَا مُسْلِمُونَ﴾

"Na nilipowafunulia wanafunzi (wako) kuwa niaminini mimi na Mtume wangu, wakasema: "Tumeamini na uwe shahidi kuwa sisi ni waislamu" (5:111)

Aya iliyo wazi kuliko zote na inayomuenea wa kwanza na wa mwisho katika Mitume, wafuasi wao na wafuasi wa wafuasi, ni ile isemayo:

﴿وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ﴾

"Na yeyote mwenye kutaka dini isiyokuwa ya Kiislamu, basi haitakubaliwa kwake, naye akhera atakuwa katika wenye khasara" (3:85)

Ikiwa Mwenyezi Mungu hatakubali isipokuwa Waislamu tu; na huku amekwisha wakubali Mitume kuanzia Adam, Nuh, Ibrahim, Musa, Isa na Mitume wote pamoja na wafuasi wao, basi natija itakuwa kwamba Mitume wote kuanzia Adam mpaka Muhammad(s.a.w.w) na wanaowafuata, ni waislamu. Imam Ali(a.s) anasema:"Uislamu ni kujisalimisha, kujislaimisha ni yakini, yakini ni kusadikisha, kusadikisha ni kukiri, kukiri ni kutekeleza na kutekeleza ni matendo."

Na hawakuhitalifiana wale waliopewa Kitabu ila baada ya kuwajia elimu kwa uhasidi uliokuwa baina yao.

Makusudio ya watu wa Kitabu hapa ni mayahudi. Inasemekana ni manasara. Na, inasemekana ni wote, na hiyo ndio sahihi kwa sababu tamko ni la kiujumla na hakuna dalili ya umahsusi. Linalotilia nguvu kuwa tamko ni la kiujumla, ni kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿وَمِنَ الَّذِينَ قَالُوا إِنَّا نَصَارَىٰ أَخَذْنَا مِيثَاقَهُمْ فَنَسُوا حَظًّا مِّمَّا ذُكِّرُوا بِهِ فَأَغْرَيْنَا بَيْنَهُمُ الْعَدَاوَةَ وَالْبَغْضَاءَ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ﴾

"Na kwa wale waliosema: Sisi ni Wanaswara tulichukua ahadi yao, lakini wakaacha sehemu ya yale waliyokumbushwa, kwa hivyo tukaweka baina yao uadui na bughudha mpaka Siku ya Kiyama." (5:14)

Kuhusu tofauti ya Mayahudi anasema: "Na Mayahudi walisema: 'Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba'

﴿وَأَلْقَيْنَا بَيْنَهُمُ الْعَدَاوَةَ وَالْبَغْضَاءَ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ﴾

"Na tumewatilia uadui na bughudha baina yao mpaka siku ya Kiyama." (5:64).

Katika mambo waliyohitalifiana Mayahudi ni uhai baada ya mauti. Baadhi yao wakasema, hakuna ufufuo kabisa, si katika maisha haya wala mengine na kwamba adhabu ya mwenye makosa na thawabu za mtu mwema zinapatikana katika maisha haya ya duniani. Kikundi kingine kinasema: "Watu wema watafufuliwa mara ya pili hapa duniani ili washiriki katika ufalme wa Masih ambaye atakuja zama za mwisho." Ama itikadi ya Kikristo iligeukageuka,kabla ya kudumu kwenye utatu. Mwanzo ilikuwa inalingania kwenye ibada ya Mungu mmoja, kisha wakagawanyika makundi mawili: Kundi moja lilikuwa katika shirk na jengine likabakia kwenye Tawhid lakini likatofautiana kuwa je, Isa ana tabia mbili ya kiungu na nyengine ya kibinadamu; au ana tabia ya kiungu tu? Na mengine mengi yaliyoandikwa katika vitabu vya historia za dini, Tofauti hizo za kikristo zimeleta umwagikaji damu wa kufehedhesha kusikokuwa na mfano katika historia ya binadamu.

Tofauti ya mayahudi na manaswara (wakristo) hazikutokana na kutojua uhakika. mayahudi walijua kuwa kuna ufufuo; kama ambavyo wakristo walijua kuwa Isa ni mja miongoni mwa waja wa Mungu, lakini walihitalifiana kwa kutaka ukubwa katika dunia kwa uhasidi na ufisadi.

VIKUNDI SABINI NA TATU

Imetangaa kwamba Mtume(s.a.w.w) amesema: "Mayahudi wamegawanyika vikundi sabini na moja, Wakristo vikundi sabini na mbili na umma wangu utagawanyika vikundi sabini na tatu." Maneno yamekua mengi sana kuhusu Hadith hiyo: Kuna mwenye kusema kuwa ni dhaifu, mwengine anasema hiyo ni Hadith iliyopokewa na mtu mmoja ambayo sio hoja katika maudhui. Watatu naye anasema kuwa neno "Vikundi vyote vitaingia motoni" ni katika vitimbi vya walahidi kwa kuwatia doa waislamu. Ama wanne amesema kwa tamko hili: "Vikundi vyote vitakuwa katika pepo isipokuwa wazandiki" Sisi tuna mashaka na Hadith hii, kwa sababu asili ni kuacha kuchukua lolote linalonasibishiwa Mtume(s.a.w.w) mpaka ithibiti kinyume (ukweli). Lakini kama tukihiyarishwa kati ya kukubali kwa "vyote vitakuwa motoni" na vyote vitakuwa peponi." Tutachagua peponi kutokana na sababu mbili:

Kwanza : Hiyo ndiyo iliyo karibu zaidi na rehema ya Mwenyezi Mungu.Pili : Kimsingi ni kwamba vikundi vya kiislamu vinavyotofautiana katika misingi (asili) havifiki sabini na tatu, kutofautiana katika matawi, hakupelekei kuingia motoni. Kwa sababu makosa kwenye matawi yanasamehewa yakiwa yametokea pamoja na kujichunga na baada ya kujitahidi.

Ni umbali ulioje kati ya Hadith hii inayonasibishwa kwa Mtume(s.a.w.w) na kauli ya Ibn Arabi katika kitabu Futuhat: "Haadhibiwi yeyote katika umma wa Muhammad(s.a.w.w) kwa baraka za Ahlu bait"

Na kama wakikuhoji, basi sema: Nimeusalimisha uso wangu kumwelekea Mwenyezi Mungu na walionifuata

Mara nyingi mwanachuoni wa haki hupambana na mbishi mwenye batili. Wala hakuna dawa ya huyu isipokuwa kuachana naye, Na yeyote mwenye kuhasimiana na mshari mwenye vurugu anakuwa mshirika wake katika dhambi.

Imam Ali(a.s) anasema:"Mwenye kubisha sana hupata dhambi. "Kwa ajili hii, Mwenyezi Mungu amemwamrisha Mtume wake Mitukufu kuachana na wabatilifu, walio wapinzani, kwani hakuna ziada ya ubainifu na hoja.

﴿فَإِنَّمَا عَلَيْكَ الْبَلَاغُ وَعَلَيْنَا الْحِسَابُ ﴾

"Hakika ni juu yako kufikisha tu, na ni juu yetu hisabu." (13:40)

Na waambie wale waliopewa kitabu, yaani mayahudi na manaswara,na wale wasio na kisomo, yaani washirikina katika waarabu.

Mwenyezi Mungu amewanasibisha na neno wasio na kisomo kwa sababu wengi wao hawakujua kusoma na kuandika, Je mmesilimu? Baada ya kuwajia hoja, Kama wakisilimu basi wameongoka kwani hakuna kitu chochote zaidi ya uislamu, isipokuwa kufuru tu na upotevu.

Na kama wakikengeuka basi juu yako ni kufikisha tu.

na kufikisha ndio mwisho wa kazi ya utume, kwani huko ndiko kunakotimiza hoja, Na Mwenyezi Mungu anawaona waja wote anawatendea wanayostahiki.

Faida tunazozipata kutokana na Aya hii ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemchagua Muhammad(s.a.w.w) kuwa Mjumbe Wake na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu amemwekea njia ya kuufikisha ujumbe huo ambao ni kutoa mwito kwa hoja na dalili; pamoja na kuidhibiti nafsi na kujiepusha na uhasama wa ubishani.

Kwa njia hii ya hekima hoja inatimia kwa mhalifu, mpinzani na asibakiwe na udhuru wowote au popote pa kukimbilia. Wafuasi bora zaidi wa Mtume kwenye njia yake, ni watu wa elimu wanaojua dini yake na sharia yake; wenye kulingania kushika mafunzo yake na mwenendo wake.

﴿إِنَّ الَّذِينَ يَكْفُرُونَ بِآيَاتِ اللَّـهِ وَيَقْتُلُونَ النَّبِيِّينَ بِغَيْرِ حَقٍّ وَيَقْتُلُونَ الَّذِينَ يَأْمُرُونَ بِالْقِسْطِ مِنَ النَّاسِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ﴾

21.Hakika wale ambao wanazikanusha Aya za Mwenyezi Mungu na wakawauwa manabii pasipo haki na wakawaua wanaoamrisha mambo ya haki, wabashirie adhabu iumizayo.

﴿أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَمَا لَهُم مِّن نَّاصِرِينَ﴾

22.Hao ndio ambao vitendo vyao vimeharibika katika dunia na akhera wala hawana wa kuwanusuru.

WANAOWAUA MITUME

Aya 21 – 22

MAANA

Hakika wale ambao wanazikanusha Aya za Mwenyezi Mungu na wakawauwa manabii pasipo haki na wakawauwa wanaoamrisha mambo ya haki, wabashirie adhabu iumizayo.

Unaweza kuuliza sharia zote za Mwenyezi Mungu na za watu zinaharamisha kuua, bali watu wote wanamuona muuaji ni mkosa, hasa ikiwa aliyeuwawa ni katika watu wema. Kwa hiyo basi kuelezea kuwa muuaji ni mwenye makosa anayestahili adhabu, ni kama kufafanua kilichofafanuka, na hali tunajua kuwa maneno ya Mwenyezi Mungu yako katika mpangilio mzuri?

Jibu : Makusudio hapa ni mayahudi na wakristo waliokuwako wakati wa Mtume(s.a.w.w) na wakakataa uislamu. Aya imeonyesha kuwa si jambo geni kwao kukataa na kuwa na inadi na uislamu. Kwa sababu mayahudi waliotangulia waliwaua manabii; kama vile Zakariya na manaswara waliotangulia waliwaua wale waliouonyesha wazi umoja wa Mungu na ubashiri wa Masih, kwa vile tu walikuwa wanaamrisha haki na uadilifu na kuutumia. Kwa hivyo Aya imo katika mfumo wa kukemea; kama ilivyo kuwa ni ya kuhofisha.

Swali la pili : Kuua hakukuwa kwa Ahlul-kitab waliokuwa wakati wa Muhammad(s.a.w.w) , sasa vipi wananasibishiwa wao pasipo haki?

Jibu : Tumekwishaeleza mara kadhaa kwamba waliokuja nyuma waliridhia yaliyofanywa na wa kale wao na mwenye kuridhia kitendo anakuwa mshirika, Mara nyingi anayoyafanya baba hutegemezewa mwana.Swali la tatu : Kuwaua manabii hakukuwa haki kwa hali yoyote, sasa kuna faida gani katika msemo huu?

Jibu : Ni kuonyesha kuwa fedheha ya kuwaua mitume si kwa sababu ya vyeo vyao na utukufu wao, bali ni fedheha isiyokuwa na udhuru wowote, na kwamba sio suala la watu au vikundi, bali ni suala zima la haki na ukosefu wa haki. Hao ndio ambao vitendo vyao vimeharibika katika dunia na akhera Kuharibika duniani ni kwamba wao wanalaaniwa na kila mtu, kutokana na athari zao mbaya walizoziacha. Ama huko akhera wanangojwa na adhabu.

KUAMRISHA MEMA NA KUKATAZA MABAYA

Mafakihi wametaja sharti za kuamrisha mema na kukataza mabaya, kama vile kutohofia mwamrishaji madhara ya nafsi yake, watu wake na mali yake. Lakini baadhi ya mafakihi wamelipinga sharti hili na kuwajibisha kuamrisha mema japo kutapelekea kifo; na wametoa dalili kwa Aya hii. Hoja yao ni kuwa mitume wameamrisha mema na kukataza mabaya, wakauliwa katika njia hii. Kwa ushahidi wa Qur'an tukufu. Tunavyoona sisi ni kwamba mitume katika tabligh walikuwa wana jambo ambalo wanavyuoni hawana. Wao walikuwa wakiongozwa na wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t); kama wakiuwawa katika njia ya tabligh, watakuwa wameuwawa wakiwa wanatekeleza amri ya Mwenyezi Mungu. Ama wanavyuoni, wanategemea yale waliyoyafahamu katika hukumu. Tunavyofahamu sisi kutokana na dalili hizi ni kwamba mtu yeyote inafaa kwake kunyamaza kwenye mambo mabaya ikiwa hakuna faida ya kidini na tena kuna madhara.

Ama ikiwa dhana yake imeelemea kuwa kutapatikana manufaa ya kidini kwa kuamrisha mema na kukataza mabaya, lakini kuna madhara, basi hapo itakuwa ni wajibu kuamrisha. Kwa hiyo lililopo ni kulinganisha kati ya kukinga nafsi na manufaa ya kuamrisha na kukataza. Ikiwa manufaa ya dini ndiyo muhimu; kama vile kuumaliza ukafiri, dhulma na ufisadi. Basi hapa itafaa kuyakubali madhara, na huenda ikawa wajibu. Na, ikiwa kujikinga na madhara ni muhimu zaidi kuliko kukataza mabaya; kama kukataza kula najisi, basi hapo itafaa kujikinga na huenda ikawa ni wajibu, kwa hivyo basi suala litakuwa linatofautiana kwa kutafautiana hali. Na, inatubainikia kwamba kuwalinganisha wasiokuwa Manabii katika suala hili la Manabii ni kuwalinganisha na kitu kilicho tofauti. Tutalirudia suala hili pale litakaponasibika.

﴿ أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ أُوتُوا نَصِيبًا مِّنَ الْكِتَابِ يُدْعَوْنَ إِلَىٰ كِتَابِ اللَّـهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ يَتَوَلَّىٰ فَرِيقٌ مِّنْهُمْ وَهُم مُّعْرِضُونَ ﴾

23.Je, huwaoni wale waliopewa sehemu ya Kitabu, wanaitwa kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu ili kiwahukumu baina yao, kisha baadhi yao wanageuka wanakikataa.

﴿ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوا لَن تَمَسَّنَا النَّارُ إِلَّا أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ وَغَرَّهُمْ فِي دِينِهِم مَّا كَانُوا يَفْتَرُونَ ﴾

24.Hayo ni kwa sababu walisema: Hautatugusa moto isipokuwa kwa siku chache tu, na yakawadanganya katika dini yao yale waliyokuwa wakiyazua.

﴿ فَكَيْفَ إِذَا جَمَعْنَاهُمْ لِيَوْمٍ لَّا رَيْبَ فِيهِ وَوُفِّيَتْ كُلُّ نَفْسٍ مَّا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ﴾

25.Basi itakuwaje tutakapowakusanya siku ambayo hapana shaka kuja kwake na itakapolipwa kila nafsi kwa ukamilifu kile ilichokichuma na wao hawataodhulumiwa.

MAYAHUDI TENA

Aya 23 - 25

MAANA

Je huwaoni wale waliopewa sehemu ya Kitabu wanaitwa kwenye kitabu cha Mwenyezi Mungu ili kiwahukumu baina yao, kisha baadhi yao wanageuka wanakikataa.

Wafasiri wanasema: Makusudio ya wale ambao wamepewa sehemu ya Kitabu ni mayahudi. Hapa Mwenyezi Mungu anasema waliopewa sehemu ya kitabu, na wala hakusema waliopewa Kitabu au watu wa Kitabu; kama ilivyo katika sehemu nyingine, kwa sababu mayahudi waliomhoji Mtume(s.a.w.w) na akawaita kwenye Tawrat iwahukumie, hawakuwa wamehifadhi Tawrat yote, isipokuwa walihifadhi baadhi tu, kama walivyosema wafasiri wengi. Au walihifadhi matamko tu, bila ya kuzingatia maana yake; kama alivyosema Sheikh Muhammad Abduh.

Wengi wao ni wale ambao wanalingania kwenye kuamini vitabu vya Mwenyezi Mungu na msimamo wa kibinadamu, lakini wanasema tu, bila ya kutekeleza kwa vitendo, Na, wakihojiwa, basi hubabaisha. Mifano ya hao ni mingi sana haina idadi. Kama vile watu walioanzisha vita na kuuwa mamilioni, wanadai kwamba wao ni watetezi wa amani. Miongoni mwazo ni zile dola ambazo zinawakandamiza watu huru na zinajigamba kuamini haki na uadilifu. Mfano mwengine ni mayahudi ambao Mtume(s.a.w.w) aliwaita kwenye Kitabu chao Tawrat na kuwaambia nendeni kwenye kitabu hicho, kwani ndani yake mna sifa zangu, lakini walikipa mgongo na kufanya inadi, ndipo ikashuka Aya hii. Kuna kundi la wafasiri waliosema kwamba Aya hii ilishuka kwa ajili ya yahudi mmoja aliyezini na yahudi mwenzake, na mayahudi wakatofautiana katika suala hilo katika makundi mawili. Kundi moja likataka apigwe mawe mpaka afe na kundi jingine likataka ipunguzwe adhabu hiyo. Mzozo ulipozidi wakenda kwa Mtume kuamuliwa; Mtume akahukumu kuwa apigwe mawe, lakini lile kundi la pili likakataa, ndipo Mtume akawakumbusha Tawrat ambayo imeelezea pia habari ya kupiga mawe mzinifu, lakiniwakakataa.

Kwa vyovyote itakavyokuwa sababu ya kushuka Aya hii, kwa hakika ina maana ya jumla na kumgusa yeyote mwenye kutangaza jambo, lakini yeye mwenyewe akajitia hamnazo na kulikataa. Kwa sababu linalozingatiwa ni matendo, sio alama na maneno matupu. Imam Ali(a.s) anasema:"Hatafuzu kwa kheri ila mwenye kuifanya, wala hatalipwa mtu malipo ya shari isipokuwa mwenye kuifanya"

Hayo ni kwa sababu walisema: Hautatugusa moto isipokuwa kwa siku chache tu, na yakawadanganya katika dini yao yale waliyokuwa wakiyazua.

Mwenyezi Mungu ameeleza aina nyingi za uovu wa mayahudi katika kitabu chake kitukufu; kama vile kuua kwao mitume, kuabudu ndama, kusema kwao kuwa watakaoingia peponi ni mayahudi tu, kusema kuwa wao ni wana wa Mungu na wapenzi Wake na kudai kuwa moto utawagusa siku chache tu. Mwenye Tafsir al-Manar amenakili kutoka kwa mwalimu wake Sheikh Muhammad Abduh kwamba yeye amesema: "Katika vitabu vya mayahudi walivyonavyo hamna kiaga chochote cha akhera."

Imenakiliwa kutoka kwa watu wanaochunguza na kufuatilia mambo kuwa Mayahudi hawaamini akhera, lakini kunukuu kunapingana na kauli ya Qur'an kwa mayahudi: "Hautatugusa moto isipokuwa kwa siku chache tu," na kule kusema kwao: "Hataingia peponi isipokuwa Yahud."Si jambo la kushangaza kusema kuwa wahenga wa Kiyahudi walikuwa wakiamini akhera; kisha waliofuatia wakageuza na wakaondoa katika vitabu vyao kila linalofungamana na akhera. Katika Tafsir Al-manar akinukuliwa Sheikh Abduh, anasema: "Watafiti wa kiulaya wamethibtisha kuwa Tawrat imeandikwa baada ya nabii Musa(a.s) kwa miaka nenda miaka rudi. La kushangaza zaidi kuliko yote hayo ni madai ya mayahudi, kwamba Mwenyezi Mungu anawapendelea wao na kwamba Mwenyezi Mungu amewaumba watu wengine kwa ajili ya kuwatumikia wao na kwa masilahi yao, sawa na wanyama. Kwa ajili ya fikra hii ndio wakajiita "Taifa la Mungu lilochaguliwa" Au "Taifa teule la Mungu" Tukiachilia mbali muhali wa madai haya na kutoingilika akilini, pia tunavyoona ni ndoto na ni kumhukumia Mwenyezi Mungu, kwani hakuna jambo lolote la ghaibu linaloweza kujulikana bila ya wahyi wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na, wahyi umekwisha walaani, kuwafedhehesha na kutaja adhabu yao.

Fedheha hiyo na adhabu itafichuka siku ambayo hawatakuwa na hila yoyote ya kuikinga, kwa hivyo ndipo Mwenyezi Mungu akasema:

Basi itakuwaje tutakapowakusanya siku ambayo hapana shaka kuja kwake na itakapolipwa kila nafsi kwa ukamilifu kile ilichokichuma na wao hawatadhulimiwa.

Thawabu za mtiifu hazitapunguzwa na huenda zikazidi, lakini adhabu haitazidishwa kabisa bali huenda ikapunguzwa na huenda Mwenyezi Mungu akasamehe kabisa. Mimi nina yakini kabisa kwamba mwenye kumtarajia Mwenyezi Mungu katika dunia yake hii, na wala asimtarajie mwengine amtegemee Yeye tu katika matatizo yote kwa hali yoyote itakayokuwa, akiwa na imani kwamba asiyekuwa Mwenyezi Mungu si chochote isipokuwa ni njia na chombo tu; mwenye kuwa hivi nina yakini kuwa bila shaka atakuta yanayomridhisha kwa Mungu hata kama atakuwa ana maovu.

﴿ قُلِ اللَّـهُمَّ مَالِكَ الْمُلْكِ تُؤْتِي الْمُلْكَ مَن تَشَاءُ وَتَنزِعُ الْمُلْكَ مِمَّن تَشَاءُ وَتُعِزُّ مَن تَشَاءُ وَتُذِلُّ مَن تَشَاءُ بِيَدِكَ الْخَيْرُ إِنَّكَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴾

26.Sema Ewe Mola uliyemiliki ufalme wote humpa ufalme umtakaye na humwondolea ufalme umtakaye. Na humtukuza umtakaye na humdhalilisha umtakaye. iko mikononi mwako kila kheri. Hakika wewe ni muweza wa kila kitu.

﴿ تُولِجُ اللَّيْلَ فِي النَّهَارِ وَتُولِجُ النَّهَارَ فِي اللَّيْلِ وَتُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَتُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَتَرْزُقُ مَن تَشَاءُ بِغَيْرِ حِسَابٍ﴾

27.Huingiza usiku katika mchana na huingiza mchana katika usiku na humtoa aliye hai kutoka aliye maiti na humtoa maiti kutoka aliye hai, Na humruzuku umtakaye bila ya ya hisabu.

HUMPA UFALME AMTAKAYE

Aya 26 - 27

MAANA

Dhahiri ya Aya kwa ukamilifu inalingana na hali ya waislamu katika siku za mwanzo wa Uislamu: ambapo wakati huo hawakuwa na ufalme, nguvu wala usultani. uislamu ulianza katika hali ya ugeni, kama alivyosema Mtume(s.a.w.w) . ufalme ulikuwa wa wafursi na warumi. Lakini baada ya kuja ushindi wa Mwenyezi Mungu, mambo yaligeuka; aliye duni akawa mtukufu na mtukufu akawa duni. wafursi na warumi wakawa wanatawaliwa na waislamu baada ya kuwa wao ndio watawala. Wasilamu wakawa watawala baada ya kuwa wanyonge wakiwaogopa watu, ndipo matakwa ya Mwenyezi Mungu yakathibiti aliyoyabainisha kwa kauli yake:

﴿ وَنُرِيدُ أَن نَّمُنَّ عَلَى الَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا فِي الْأَرْضِ وَنَجْعَلَهُمْ أَئِمَّةً وَنَجْعَلَهُمُ الْوَارِثِينَ ﴾

"Na tukataka kuwaneemesha wale waliofanywa wanyonge katika ardhi na kuwafanya wawe viongozi na kuwafanya warithi." (28:5).

Sema: "Ewe Mola uliyemiliki ufalme wote"

Makusudio ya kumiliki ufalme, ni uweza wake juu ya kila kitu; ni kama kusema Mwenyezi Mungu amemiliki uwezo. Ameleta neno ufalme kwa sababu athari ya kumiliki kitu chochote ni uwezo wa mwenye kumiliki kukitumia wala hapana yeyote anayeweza au kumiliki kitu; isipokuwa kwa kumilikishwa na Mwenyezi Mungu na kupewa uwezo juu yake.

Humpa ufalme umtakaye

Aliwapa waislamu mwanzo pale walipoitikia mwito wa uislamu na kuutumia kwa vitendo.

Na humuondolea ufalme umtakaye

Aliuvua kutoka kwa wafursi, na warumi na washirikina kwa sababu ya kuikufuru haki. Na humtukuza umtakaye, nao ni waislamu. Na humdhalilisha umtakaye nao ni wafursi, warumi na washirikina wa kiarabu.

Iko mikononi mwako kila heri

Makusudio ya kuwa mikononi ni kuwa na uwezo. Heri inakusanya kila lenye manufaa liwe la kimaana au kimaada, Na Mwenyezi Mungu amewapa heri nyingi waislamu kwa baraka za uislamu.

Hakika wewe ni muweza wa kila kitu.

Dalili ya uweza ni kuuvua ufalme kutoka kwa wenye nguvu na kuwapa wanyonge.

Huingiza usiku katika mchana na huuingiza mchana katika usiku.

Ambapo sayari zinakuwa na harakati kwa uweza na msaada Wake; nyingine huzizunguuka nyingine, hapo hupatikana misimu ya mwaka; mara nyingine huchukua usiku katika mchana katika msimu fulani mpaka ukawa na masaa15 na mchana ukawa masaa 9. na mara nyuingine huuchuwa mchana katika usiku katika msimu mwingine mpaka ukawa na masaa 15 na usiku ukawa masaa 9( [7] ).

Na humtoa aliye hai kutoka aliye maiti

Kama vile kumtoa mumin kutoka kwa kafiri na mtukufu kutoka kwa aliye dhalili. Na humtoa maiti kutoka aliye hai. Kama vile kumtoa kafiri kutoka kwa mumin na dhalili kutoka kwa mtukufu.

Na humruzuku amtakaye bila hisabu,

Kama alivyowaruzuku waislamu wa kwanza, ufalme na utukufu kwa baraka za uislamu. Na kama utauliza, kuwa je? ufalme wa mfalme dhalimu na usultani wake hutoka kwa Mungu na ni kwa utashi wake na matakwa yake? Utalikuta jibu la swali lako hili katika tafsiri ya aya 246 Surah Al-Baqrah, Zaidi ya hayo ni kwamba dhahiri ya Aya inatilia nguvu yale yaliyosemwa na kundi la wafasiri kuhusu sababu ya kushuka kwake. Kwa ufupi ni kwamba Mtume(s.a.w.w) alipochukua hatua ya kuchimba handaki kwa ushauri wa Salman Farisi aliwakatia dhiraa arubaini kila sahaba kumi, na Salman alikuwa na nguvu, hivyo Ansar wakamtaka awe nao wakasema: "Salman ni wetu" Mtume akasema kauli yake iliyo mashuhuuri: "Salman ni katika sisi Ahlul-Bait.

Wakati Salman alipokuwa akichimba akakabiliwa na jiwe lililomshinda. Mtume alipoambiwa, alichukua sururu kutoka mikononi mwa Salman na kulivunja jiwe kwa mapigo matatu. Katika mapigo hayo Mtume (s.a.w.w) aliona ikulu ya Fursi, Roma na Yemen; akawaambia sahaba zake: "Umati wangu utatawala ufalme wa Kisra na Kaizari". Basi wanafiki waliposikia waliyachezea shere maelezo haya, ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hii:

Sema: "Ewe Mola uliyemiliki ufalme wote! Humpa ufalme umtakaye na humwondolea ufalme umtakaye na humtukuza umtakaye na humdhalilisha umtakaye"

Ikiwa hii ndiyo sababu ya kushuka Aya hii au siyo, lakini dhahiri ya Aya haikatai, na matukio ya historia yanaunga mkono hilo.

﴿لَّا يَتَّخِذِ الْمُؤْمِنُونَ الْكَافِرِينَ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِ الْمُؤْمِنِينَ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ فَلَيْسَ مِنَ اللَّـهِ فِي شَيْءٍ إِلَّا أَن تَتَّقُوا مِنْهُمْ تُقَاةً وَيُحَذِّرُكُمُ اللَّـهُ نَفْسَهُ وَإِلَى اللَّـهِ الْمَصِيرُ﴾

28.Waumini wasiwafanye Makafiri kuwa ni marafiki badala ya waumini (wenzao). Na mwenye kuyafanya hayo, basi hana kitu kwa Mwenyezi Mungu ila mtakapojilinda nao kwa kujihifadhi na anawatahadharisha Mwenyezi Mungu na Yeye mwenyewe marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu.

﴿قُلْ إِن تُخْفُوا مَا فِي صُدُورِكُمْ أَوْ تُبْدُوهُ يَعْلَمْهُ اللَّـهُ وَيَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴾

29.Sema: Mkificha yaliyomo vifuani mwenu au mkiyadhihirisha Mwenyezi Mungu anayajua na anayajua yaliyomo mbinguni na yaliyomo ardhini. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.

﴿يَوْمَ تَجِدُ كُلُّ نَفْسٍ مَّا عَمِلَتْ مِنْ خَيْرٍ مُّحْضَرًا وَمَا عَمِلَتْ مِن سُوءٍ تَوَدُّ لَوْ أَنَّ بَيْنَهَا وَبَيْنَهُ أَمَدًا بَعِيدًا وَيُحَذِّرُكُمُ اللَّـهُ نَفْسَهُ وَاللَّـهُ رَءُوفٌ بِالْعِبَادِ ﴾

30.Siku ambayo kila nafsi itakuta kheri iliyoitenda imehudhurishwa Na iliyoyatenda katika uovu, itapenda lau kungekuwa na masafa marefu baina ya uovu huo na yeye. Na anatahadharisha Mwenyezi Mungu na Yeye Mwenyewe, na Mwenyezi Mungu ni mpole kwa waja.

URAFIKI NA KAFIRI

Aya 28-30

LUGHA

Neno: Awliya lina maana ya wasimamizi, Makusudio yake hapa ni marafiki kwa maana ya wasaidizi

MAANA

Waumini wasiwafanye makafiri kuwa ni marafiki badala ya waumini (wenzao).

Mwenyezi Mungu hakutosheka na kukataza tu urafiki na makafiri kwa kusema ni haramu; kama vile uongo na kusengenya, bali amekuzingatia kuwa ni kufuru, kwa dalili ya neno lake:

Na mwenye kuyafanya hayo, basi hana kitu kwa Mwenyezi Mungu.

Kwani dhahiri ya kauli hiyo ni kuwa Mwenyezi Mungu yuko mbali na aliye na urafiki na makafiri; na aliye mbali na Mwenyezi Mungu, basi yeye ni Kafiri. Hili linatiliwa nguvu na Aya hizi:

﴿ وَمَن يَتَوَلَّهُم مِّنكُمْ فَإِنَّهُ مِنْهُمْ﴾

"Na atakayefanya urafiki nao miongoni mwenu, basi huyo atakuwa pamoja nao" (5:51)

﴿ لَّا تَجِدُ قَوْمًا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ يُوَادُّونَ مَنْ حَادَّ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَوْ كَانُوا آبَاءَهُمْ أَوْ أَبْنَاءَهُمْ أَوْ إِخْوَانَهُمْ أَوْ عَشِيرَتَهُمْ﴾

Huwapati watu wanaoamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho kuwa wanawapenda wale wanaompinga Mwenyezi Mungu na Mtume Wake; hata wakiwa ni baba zao au watoto wao au ndugu zao au jamaa zao" (58:22)

Dhahiri ya Aya hizi inafahamisha kuwa mwenye kumfanya kafiri kuwa rafiki basi naye ni kafiri. Hata hivyo kuna aina mbali mbali za kumfanya rafiki, nyingine zinawajibisha ukafiri na nyingine haziwajibishi. Ufafanuzi ni kama ufatavyo:

AINA ZA URAFIKI NA KAFIRI

Kila aliyesema: Laillaha Illa Ilah Muhammadun rasulullah. Basi anakuwa na lile walilonalo waislamu wengine, na wao wako na lile alilo nalo, isipokuwa akiwafanya makafiri kuwa ni marafiki katika mojawapo ya hali zinazofuata:

1. Kuwa radhi na ukafiri wao, na hili ni muhali kwa mwislam kwa sababu kuridhia ukafiri ni ukafiri.

2. Kujikurubisha kwa makafari kwa upande wa dini kwa kujaribu kufasiri Aya za Mwenyezi Mungu Mtukufu, na Hadith za Mtume Wake kwa yale yanayoafikiana na mapenzi ya makafiri, maadui wa Mwenyezi Mungu na Mtume, kiasi ambacho tafsiri hiyo itapingana na misingi ya kiislamu na kiitikadi. Ikiwa kwa makusudi na kujua. Huu vile vile ni ukafiri. Unaweza kuuliza: Mtu anayefanya hayo kwa ukaidi ni kafiri bila ya wasiwasi wowote, lakini mwenye kuyafanya kwa kupuuza tu, inafaa awe fasiki tu, sio kafiri; sawa na mwenye kuacha Swala akiwa anaamini kuwa ni wajibu na akanywa pombe akiwa anaamini kabisa kuwa ni haramu? Jibu: Kutofautisha kati ya mkaidi na mpuuzaji kunakuja kwenye Fur'uu (matawi); kama vile Swala, kunywa pombe n.k. Ama kwenye mambo yanayorudia kwenye Usul (Misingi) ya dini na itikadi; kama vile umoja wa Mungu, utume wa Muhammad n.k. Basi kutamka tu kitu kinachokanusha kunawajibisha ukafiri. Ni sawa mtamkaji awe ametamka kwa ukaidi au kwa kupuuza.

3. Kuwa kachero au jasusi wa makafiri dhidi ya waislamu, Huyu ataangaliwa. Ikiwa amefanya hivyo kwa tamaa ya mali au jaha basi atakuwa mwenye makosa aliye fasiki, ama akifanya kwa sababu ya kuwapenda makafiri kwa kuwa wao ni makafiri na kwa kuwachukia waislamu kwa kuwa ni waislamu, basi huyo ni kafiri bila ya shaka yoyote.

4. Kuwapenda makafiri na huku akiwa anajua kabisa kwamba wao wanawapiga vita Waislamu wakiwa wanataka kuwadhalilisha na kuwatumia, basi huyu atakuwa ni mwenye dhambi na mshirika wa dhalimu katika udhalimu wake, hata kama huyo dhalimu ni mwislamu.

5. Kuwataka msaada makafiri wenye amani dhidi ya makafiri wasiokuwa na amani. Msaada huu unafaa kwa maafikiano ya Ijmai (kongamano). Watu wa historia na wafasiri wamenukuu kwamba Mtume(s.a.w.w) aliwekeana mkataba wa kusaidiana na Bani Khuzaa inagawaje walikuwa washirikina. Pia alimtaka msaada Safwan bin Umayya - kabla hajasilimu - kwenye vita ya Hawazan. Vilevile aliwataka msaada Mayahudi wa Bani Qaynuqa na akawagawanyia mali.

Bali yamekuja maelezo kutoka kwa Allama Hili kwamba kundi la mafakihi wamejuzisha kutaka msaada kutoka kwa makafiri katika kuwapiga vita waislamu walio madhalimu. Kwa sababu kuwataka msaada kunaambatana na haki, si kwa ajili ya kuibatilisha batili.

6. Kufanya urafiki kwa sababu za mambo ya kawaida yaliyozoeleka, kama kushirikiana katika kazi au biashara na mengineyo mengi ambao hayahusu dini. Urafiki huu pia unafaa kwa kongamano la maulamaa. Kwa sababu kumpenda kafiri kutakuwa haramu kama kutapelekea kufanyika jambo la haramu, ama kukiwa sio wasila wa kufanya maasi, basi si haramu; bali huenda kukawa kunapendekezwa kama kuna manufaa na heri kwa nchi au watu. Na, Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameamrisha upendano, kuzoweyana na kusaidiana kwa watu wote bila ya kuangalia dini au mila zao. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

﴿ لَّا يَنْهَاكُمُ اللَّـهُ عَنِ الَّذِينَ لَمْ يُقَاتِلُوكُمْ فِي الدِّينِ وَلَمْ يُخْرِجُوكُم مِّن دِيَارِكُمْ أَن تَبَرُّوهُمْ وَتُقْسِطُوا إِلَيْهِمْ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ﴾

"Mwenyezi Mungu hawakatazi kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakupigana nanyi kwa ajili ya dini wala hawakuwafukuza katika miji yenu. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao uadilifu" (60:8)

Sisi hatuna shaka kwamba katika makafiri kuna walio na hulka nzuri na tabia njema - ya ukweli, uaminifu na utekelezaji - kuliko wale tunaowaita na kujiita waislamu. Na kwamba kufanya urafiki nao ni bora zaidi - kibinadamu na kimaslahi ya umma - kuliko wale vibaraka wahaini wanaojionyesha kwa dini ya kiislamu. Maelefu ya rehema na amani yamwendee yule aliyesema: "Aliye karibu ni yule aliye karibu kwa tabia. Huenda aliye karibu akawa mbali zaidi ya aliye mbali na aliye mbali akawa karibu zaidi ya aliye karibu" Hakika hii huitambua mtu kimaumbile tu bila ya hisia zozote.

TAQIYA

Ila mtakapojilinda nao kwa kujihifadhi.

Historia ya Taqiya inaanzia na historia ya uislamu siku ulipokua dhaifu, na shujaa wa kwanza alikuwa Ammar bin Yasir, pale aliposilimu yeye, baba yake na mama yake; wakaadhibiwa na makafiri kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wakavumilia adhabu na adha bila ya kulalamika. Mtume akawapitia wakiwa wanaadhibiwa: Hakuzidisha chochote Yasir zaidi ya kusema: "Hali ndio hii ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu." Mtume naye akasema: "Vumilieni enyi familia ya Yasir hakika ahadi yenu ni pepo." Akawa Yasir na mkewe Sumaiya ndio mashahidi wa kwanza katika uislam. Washirikina wakamlazimisha Ammar kusema maneno kuhusu Mtume wa Mwenyezi Mungu, akasema kwa ajili ya kujikinga na madhara kwa ajili ya nafsi yake. Hapa baadhi ya Maswahaba wakasema kuwa Ammar amekufuru; Mtume akasema: "Hapana hakika Ammar imani imemtanda kuanzia utosini hadi nyayoni" Ammar akaja kwa Mtume akiwa analia na kujuta. Mtume akampangusa machozi na kuuwaambia: "Usilie, hata kama watarudia, basi wewe rudia uliyoyasema." Hapo ikashuka Aya kumhusu Ammar:

﴿ مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ ﴾

"Mwenye kumkufuru Mwenyezi Mungu baada ya kumwamini (ana adhabu kubwa) isipokuwa yule aliyelazimishwa hali ya kuwa moyo wake umetulia kwenye imani" (16:106)

Hakuna waliohitalifiana kuwa Aya hii, ilishuka kwa mnasaba huo wa Ammar. Kimsingi linalozingatiwa ni kuenea tamko, sio sababu za kushuka Aya, Na tamko hapa linamwenea kila mwenye kulazimishwa hali ya kuwa moyo wake umetulia kwenye imani. Kisha ndipo ikashuka Aya hii tunayoifasiri kutilia mkazo Aya hiyo ya kuhusu Ammar, kama zilivyo Aya nyingine zifuatazo:

﴿ وَقَالَ رَجُلٌ مُّؤْمِنٌ مِّنْ آلِ فِرْعَوْنَ يَكْتُمُ إِيمَانَهُ ﴾

Na akasema mtu mmoja Mumin katika watu wa firaun afichaye imani yake (40:28)

"Isipokuwa vile mnavyolazimishwa" (6:119)

Ruhusa ya Taqiya haikuja kwenye kitabu cha Mwenyezi Mungu tu, bali katika Hadith vilevile. Ar-Razi katika Tafsir Kabir, na Sayyid Rashid Ridha katika Tafsir Al-Manar, na wengine wanasema: "Musailama Al-Kadhab aliwashika watu wawili katika swahaba wa Mtume, mmoja akamwambia: "Je, washuhudia kuwa mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu?"

Yule mtu akasema: "Ndio," basi akamwacha. Yule wa pili alipomwambia hivyo hivyo, alikataa, basi akamuua. Mtume alipopata habari hizo alisema: "Yule aliyeuawa amekufa na yakini yake na ukweli wake pongezi ni zake. Ama yule mwengine ameruhusiwa, (kufanya hivyo) hana neno" Kuna Hadith katika Tafsir Al-Manar kwamba Bukhari katika Sahih yake akimnukuu Aisha anasema: "Mtu mmoja alibisha hodi kwa Mtume, Mtume akajisemea: "Mtu mbaya huyo", kisha akamruhusu kuingia na akazungumza naye vizuri."

Yule mtu alipoondoka Aisha akamwambia Mtume: "Si umesema uliyoyasema kuhusu mtu huyu, kisha umezungumza naye vizuri? Mtume akasema; "Hakika mwovu zaidi wa watu ni yule anayeachwa na watu kwa kujikinga na shari yake." Na katika Bukhari tena kuna Hadith ya Abu Dardai inayosema: "Sisi tunatabasamu kwenye nyuso za watu na nyoyo zetu zinawalaani" Zaidi ya hayo kuna Hadith nyingine zinafahamisha kujuzu Taqiya (kujikinga) kama vile Hadith: "Hapana dhara wala kudhuriana." Na "Umati wangu umesamehewa yale wanayolazimika nayo." Hadith zote hizi mbili ni Mutawatir kwa upande wa Sunni na Shia. Kwa kutegemea kitabu cha Mwenyezi Mungu na Hadith Mutawatiri za Mtume zilizo sahihi basi Sunni na Shia wamekongamana kwa kauli moja kuwa Taqiya inafaa. Anasema Al- Jasas mmoja wa Maimam wa Kihanafi katika juzuu ya pili ya kitabu Ahkamul Qur'an Uk. 10 chapa ya 1347 A.H. Ninamnukuu: "Ila kwa kujilinda nao" Yaani ni kuhofia kuangamia nafsi au baadhi ya viungo kwa hiyo kujilinda nao kwa kudhihirisha ukafiri bila ya kuutaikidi Na hilo limeafikiwa na watu wa elimu."

Ar-Razi katika tafsiri yake amemnukuu Hassan Al-Basri akisema: "Taqiya inajuzu mpaka siku ya Kiyama". Vilevile amemnukuu Shafi kwamba yeye amejuzisha Taqiya kwa waislamu wote, ikiwa anamhofia mwislam mwenziwe katika tofauti zinazorudia masuala ya dini. Mwenye Tafsir Al-Manar naye anasema kuhusu Aya hii: "Mwenye kutamka neno la kufru akiwa anajikinga na kuangamia kwa kulazimishwa sio kwa kuukubali ukafiri au kwa sababu ya kupenda dunia kuliko akhera, basi si kafiri na unakubaliwa udhuru wake kama alivyokubaliwa Ammar bin Yasir Na amesema Sheikh Mustafa Azurqaa katika Kitabu Fiq-hul-Islam Fi Thawbihil Jadidi mada ya 600, anasema: "Kutishwa mtu kuuliwa kwa kulazimishwa ukafiri, kunamhalalishia kudhihirisha ukafiri ikiwa moyo umetulizana na imani." Zaidi ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu, Hadith za Mtume na kongamano la Waislamu wa kisunni na kishia, pia akili inakubali Taqiya kwa sababu akili pia inaiona ni nzuri kutokana na desturi isemayo "Dharura inahalalisha yaliyokatazwa" Kwa hiyo basi inatubainikia kuwa Taqiya ni kanuni ya sharia wanayoitegemea Mujtahid wa Kisunni na kishia katika kutoa hukumu. Na kwamba dalili yake ni Qur'an, Hadith, kongamano na akili. Kwa ajili hiyo Taqiya inakuwa ni funzo la kiislamu kwa waislamu wote na kuaminiwa na madhehebu zote; na wala sio ya madhehebu maalum kama wanavyodhania Khawarij.

Hapa kuna swali linalojitokeza; nalo ni ikiwa Taqiya inafaa kwa Qur'an, Hadith, akili na kongamano kutoka kwa Shia na Sunni, kwa nini wanasibishiwe Shia tu, kiasi kwamba Masheikh wengi wa kisunni wameinasibisha kwa Shia na kuwakebehi nayo? Jibu: Kunasibishiwa au kuwa mashahuri zaidi kwa Shia, huenda ikawa ni kwa sababu ya kuwa wao walilazimika kuitumia zaidi ya watu wengine kwa kuangalia vikwazo vingi walivyovipata wakati wa utawala wa Bani Umayya, Bani Abbas na waliowafuatia( [8] ). Kwa sababu ya kulazimika Shia kuwa na Taqiya mara nyingi au zaidi kuliko wengine, ndio maana wakajishughulisha nayo na kuitaja katika vitabu vya fikh tena wakaifafanua kwa kubainisha mipaka yake na wakati wake wa kufaa kuifanya na kutofaa. Muhtasari wa waliyoyasema ni: Inafaa kwa ajili ya kuondoa madhara ya nafsi, na haifai kwa ajili ya kuleta manufaa au kuingiza madhara kwa mwengine. Ama yule anayeihusisha Taqiya na Mashia tu, ama atakuwa ni mjinga au atakuwa mwenye chuki. Hata hivyo hivi sasa Taqiya haitumiki (sana) baada ya kupita wakati wa hofu na vikwanzo.

Na anawatahadharisha Mwenyezi Mungu naye

Yaani na dhati Yake ambayo inajua kila kitu, yenye uweza juu ya kila kitu na kumlipa kila mtu kwa amali yake.

Na marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu.

Ambako italipwa kila nafsi ilichofanya.

Sema: mkificha yaliyomo vifuani mwenu au mkiyadhihirisha Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo mbinguni na yaliyomo ardhini.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kujuzisha Taqiya na kuiruhusu kwa mwenye kulazimika, anasema: linaloangaliwa mbele ya Mwenyezi Mungu ni lile lililo moyoni: na yeye anayajua ya moyoni mkifanya siri au kuyadhihirisha.

Siku ambayo kila nafsi itakuta kheri iliyoitenda imehudhurishwa

Lilivyokuwa Mwenyezi Mungu anajua kila kitu, muweza wa kila jambo; mkusanyaji wa watu siku isiyo na shaka. na mwadilifu asiyedhulumu, hayo yote yanamhakikishia mtu kukuta malipo ya amali yake. Baadhi wanasema, mtu atakuta amali yake kesho ikiwa kama umbo zuri la kupendeza kama ni ya kheri; au kama ni mbaya basi itakuwa na umbo la kutisha. Lakini inavyojulikana ni kwamba amali ni mambo ambayo hayabaki wala haiwezekani kuyarudisha na kuyaona. Kwa hiyo makusudio ni kuwa mtu siku ya kiyama ataona malipo ya amali yake sio hiyo amali yenyewe.

Na iliyoyatenda katika uovu, itapenda lau kama kungekuwa na masafa marefu baina ya uovu huo na yeye.

Herufi Wau hapa ni kuanza maneno; yaani mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu, hapo kesho atatamani kuweko na masafa kati yake na siku hiyo sawa na umbali wa Mashariki na Magharibi.

Na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja.

Hata waasi pia, kwa sababu amewalazimisha wanayoyaweza na amewahadharisha na mwisho mbaya wa maasi. Pia amefungua mlango wa toba kwa yule ambaye nafsi yake imefanya maovu. Kwa hiyo mwasi habaki na udhuru.

8

9