MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU 0%

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU Mwandishi:
Kundi: Vitabu mbali mbali

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

Mwandishi: NDUGU ZETU WA KISUNNI
Kundi:

Matembeleo: 44535
Pakua: 3487

Maelezo zaidi:

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 22 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 44535 / Pakua: 3487
Kiwango Kiwango Kiwango
MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

Mwandishi:
Swahili

12

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

KUAMINI QADAR YA ALLA

Kwa mujibu wa Hadith iliyosimuliwa na Umar (r.a), kuamini Qadar ni nguzo ya sita ya Imani ya Kiislamu. Katika hadithi hii ndefu, Umar (r.a) anasimulia: Siku moja tulipokuwa tumeketi pamoja na Mtume(s.a.w.w) alitutokea mtu mmoja ambaye nguo zake zilikuwa nyeupe kama theluji na nywele zake nyeusi sana, hakuwa na dalili zozote za msafiri, ingawa alikuwa mgeni kwetu sote. Halafu alikaa mbele ya Mtume hali magoti yake yakikabiliana na yale ya Mtume na akaweka mikono yake katika mapaja ya Mtume halafu akasema:

"Ewe Muhammad nifahamishe juu ya Uislamu" na Mtume akasema: "Ni kushuhudia kuwa hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allah, kusimamisha Swala, Kutoa Zakat, Kufunga mwezi wa Ramadhani na Kuhiji Makkah kwa mwenye kuweza" Halafu yule mgeni akasema:

"Umesema kweli.Tulistajaabu kwa nini aliuliza halafu akasadikisha. Halafu akasema: "Nifahamishe juu ya Imani". Mtume akasema: "Ni Kumuamini Allah, Malaika Wake, Vitabu vyake, Mitume Wake, Siku ya Mwisho na Qadar, Kheri yake na Shari yake". Kisha akasema: "Nifahamishe juu ya Ihsan". Na Mtume akamjibu:"Ni kumuabudu Allah kama kwamba unamuona, kwani ingawa humuoni, Yeye anakuona". Halafu akasema: "Nifahamishe juu ya Siku ya Kiyama". Mtume akamjibu kwamba hajui mwenye kuulizwa zaidi ya mwenye kuuliza Akasema:

"Nifahamishe dalili zake" Mtume.Akasema: "Ni wakati ambao mjakazi atamzaa bibi yake, na utakapoona wachungaji maskini, wenye nguo zilizoraruka na wasio na viatu wanashindana kujenga maghorofa".Yule mgeni alipoondoka, Mtume alikaa kimya kwa muda halafu akasema: "Ee Umar, unamfahamu muulizaji?" Sote tukajibu kuwa Allah na Mtume wake ndio wajuao. Mtume akasema: "Huyo ni Jibril, amekuja kuwafundisheni dini yenu". (Muslim)

Maana ya Qadar Neno "Al-Qadar" limetumika katika Qur-an kwa maana ya "kiasi", kipimo", kukadiria kipimo maalumu". Hebu turejee aya zifuatazo ambamo neno Qadar limetumiwa:

﴿إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ ﴾

"Kwa hakika Sisi tumekiumba kila kitu kwa kiasi (chake makhsusi)" (54:49)"...

﴿وَخَلَقَ كُلَّ شَيْءٍ فَقَدَّرَهُ تَقْدِيرًا﴾

Na (Mwenyezi Mungu) Ameumba kila kitu na Akakikadiria kipimo (chake)" (25:2)

﴿وَالْقَمَرَ قَدَّرْنَاهُ مَنَازِلَ حَتَّىٰ عَادَ كَالْعُرْجُونِ الْقَدِيمِ﴾

"Na mwezi tumeupimia vituo, mpaka unakuwa (mwembamba) kama chaparare la mtende kuu kuu". (36:39).

Tukizingatia aya hizi, tunajifunza kuwa Allah(s.w) ameumba ulimwengu huu na vyote vilivyomo kwa mujibu wa kanuni zinazotawala mzunguko wa jua, mwezi, nyota, dunia na sayari nyingine. Kutokana na mizunguko ya jua, mwezi na dunia tunapata urefu wa mchana na usiku, hesabu ya miezi, majira, n.k. Kuna kanuni zinazotawala ukuaji wa mimea. Kutokana na kanuni hizo, mimea huzaa matunda yenye rangi na ladha mbali mbali.Kwa ujumla Allah (s.w) ameumba kila kitu kwa lengo, maalumu na ameweka kanuni madhubuti zinazokiwezesha kila kiumbe kifikie lengo lake kama anavyotukumbusha katika Qur-an:

﴿سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الْأَعْلَى ﴿١﴾ الَّذِي خَلَقَ فَسَوَّىٰ ﴿٢﴾ وَالَّذِي قَدَّرَ فَهَدَىٰ﴾

"Litukuze jina la Mola wako aliye Mtukufu.Aliyeumba (kila kitu) akakitengeneza.Na akakikadiria (kila kimoja jambo lake) na akakiongoza (kufanya jambo hilo). (87:1-3)

Pia matukio yote yako katika Qadar ya Allah (s.w).Hapana tukio lolote linalotokea liwe la kheri au la shari kwa mwanaadamu, ila limo katika Qadar ya Allah (s.w) kama tunavyojifunza katika Qur-an:

﴿ وَاللَّـهُ خَلَقَكُم مِّن تُرَابٍ ثُمَّ مِن نُّطْفَةٍ ثُمَّ جَعَلَكُمْ أَزْوَاجًا وَمَا تَحْمِلُ مِنْ أُنثَىٰ وَلَا تَضَعُ إِلَّا بِعِلْمِهِ وَمَا يُعَمَّرُ مِن مُّعَمَّرٍ وَلَا يُنقَصُ مِنْ عُمُرِهِ إِلَّا فِي كِتَابٍ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ﴾

Na Mwenyezi Mungu amekuumbeni kwa udongo, kisha kwa tone la manii, kisha akakufanyeni wanaume na wanawake. Na mwanamke yoyote hachukui mimba wala hazai ila kwa ilimu Yake (Mwenyezi Mungu). Na mwenye kupewa umri hapewi umri (zaidi) wala hapunguziwi umri wake ila yamo hayo katika Kitabu (cha Mwenyezi Mungu). Bila shaka (kuyapitisha) haya ni sahali kwa Mwenyezi Mungu. (35:11)

﴿مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ﴾

Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwishaandikwa katika Kitabu (cha Mwenyezi Mungu) kabla Hatujauumba. Kwa yakini hilo ni sahali kwa Mwenyezi Mungu. (57:22)

Mtazamo wa Uislamu juu ya Qadar Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, ni makosa makubwa kudhani kuwa mtu anaweza kufanya jambo lolote lile kinyume na Qadar ya Allah (s.w). Na ni makosa makubwa pia kudhani kuwa mtu anaweza kumlaumu Allah (s.w) kwa maovu anayotenda. Utatanishi wote wanaoupata watu juu ya suala hili unaondoka kwa sababu Uislamu umegawanya maisha ya binaadamu katika maeneo makuu mawili:

(a) Eneo ambalo binaadamu hana hiari, na

(b) Eneo ambalo binaadamu anao uchaguzi. Binaadamu hana hiari kabisa katika baadhi ya mambo katika maisha yake. Mambo hayo humtokea atake asitake. Hana uwezo wa kuyachagua wala kuyabadilisha.Kwa mfano mtu hana hiari ya kuwachagua wazazi wake.Hawezi kuchagua tarehe ya kuzaliwa wala nchi atakayozaliwa.Hawezi kuchagua rangi ya ngozi yake wala aina ya nywele, rangi ya macho, kimo au vipawa vingine.

Damu itazunguka mwilini bila kuipangia yeye safari hiyo, moyo wake utadunda bila yeye kuuamrisha.Mwili mzima wa binaadamu unafanya kazi bila yeye kuupigia kura. Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu binaadamu hataulizwa au kuhisabiwa juu ya jambo lolote ambalo yeye hakuwa na hiari nalo.Yaani hakuna mtu atakayeulizwa kwanini wewe ulizaliwa siku ya Jumanne badala ya Jumatano? Au kwa nini ulifariki mwezi wa Shaabani badala ya kusubiri hadi mwezi wa Ramadhani? Au kwanini ulikuwa mrefu namna hii badala ya kuwa na kimo cha wastani? Kwa hakika ni rehema kubwa ya Allah (s.w) kwamba mambo hayo hatuyadhibiti sisi wenyewe.

Hebu fikiria kama moyo ungelikuwa unapiga kwa amri yetu, tungeliwazaje kulihakikisha hilo tunapolala usingizini au tunaposahau? Matatizo yangekuwa hayo hayo lau myeyusho wa chakula (digestion) ungelikuwa uko chini ya udhibiti wetu, n.k.

Kuna eneo ambalo binaadamu anao uhuru wa kuchagua hili au lile. Mtu anaweza kwa mfano kuchukua bastola na kumuulia mtu mwingine na kupora mali yake au anaweza kuchukua chakula na kumpa mwenye njaa. Mtu anaweza kutumia pesa zake kwa kuwanunulia nguo wazazi wake, au anaweza kwenda nazo kilabuni kunywea pombe. Mtu anaweza kumuamini Allah (s.w) na kumtii na anaweza kukataa kumuamini na akaamua kumuasi. Mtu anaweza kusema kweli au akiamua anaweza kusema uwongo.Anaweza kumtendea mwenziwe haki au anaweza kumdhulumu.Katika eneo hili binaadamu ni Mas-uli, yaani atahisabiwa na Allah (s.w) kwa yote aliyoyafanya kwani ni mambo ambayo binaadamu amepewa uhuru wa kuchagua kutenda hili au lile.

﴿إِنَّا هَدَيْنَاهُ السَّبِيلَ إِمَّا شَاكِرًا وَإِمَّا كَفُورًا﴾

"Hakika Sisi Tumemuongoa, (tumembainishia) njia. Basi atakuwa mwenye shukurani au mwenye kukufuru" (76:3)

﴿وَقُلِ الْحَقُّ مِن رَّبِّكُمْ فَمَن شَاءَ فَلْيُؤْمِن وَمَن شَاءَ فَلْيَكْفُرْ﴾

"Na sema: Huu ni ukweli uliotoka kwa Mola wenu, basi anayetaka naamini na anayetaka na akufuru." (18:29)

﴿ أَلَمْ نَجْعَل لَّهُ عَيْنَيْنِ ﴿٨﴾ وَلِسَانًا وَشَفَتَيْنِ ﴿٩﴾ وَهَدَيْنَاهُ النَّجْدَيْنِ﴾

"Je, hatukumpa(binaadamu) macho mawili? Na ulimi na midomo miwili?Na tukambainishia zote njia mbili?" (90:8-10)

Hivyo ni dhahiri kuwa katika eneo hili binaadamu hajapangiwa na Allah (s.w) lipi aje kulifanya atake asitake. Allah (s.w) amempa mwongozo wa kuufuata lakini kampa na hiari ya kuufuata au kuuacha. Na ndio maana ataulizwa.Ukweli kuwa watu wanaweza kumuasi Allah (s.w) ni ushahidi tosha kuwa watu wanao uhuru wa kuchagua kutenda mema au maovu, kwani lau si hivyo watu wote wangekuwa kama Malaika.

Hata hivyo, kwanza, isidhaniwe kuwa maadamu watu wanao uhuru wa kuchagua kutenda lolote basi Allah (s.w) hajui mpaka jambo hilo litokee.Yeye anayajua yote atakayofanya mja hadi hatima yake ya mwisho siku ya kiyama hata kabla mtu huyo hajazaliwa.

﴿وَمَا مِن دَابَّةٍ فِي الْأَرْضِ إِلَّا عَلَى اللَّـهِ رِزْقُهَا وَيَعْلَمُ مُسْتَقَرَّهَا وَمُسْتَوْدَعَهَا كُلٌّ فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ﴾

"Na hakuna mnyama yeyote (kiumbe chochote) katika ardhi ila riziki yake iko juu ya Mwenyezi Mungu. Na anajua makao yake ya milele na mahali pake pa kupita tu (hapa duniani). Yote yamo katika kitabu kinachodhihirisha (kila kitu)" (11:6)

Allah (s.w) anayajua atakayoyachagua mtu kuyafanya lakini hakumshurutisha kuyafanya

Pili, isidhaniwe pia kuwa maadamu mtu amechagua kumuasi Allah (s.w), basi mtu huyo anapotenda uovu huo Allah (s.w) huchukia lakini hana uwezo wa kumzuia. Mtu hawezi kufanya lolote ila kwa idhini ya Allah (s.w). Yaani mtu anaweza tu kutenda jema au ovu kwa sababu ya kutumia vizuri au vibaya neema alizopewa na Allah (s.w).

Kwa mfano tusema mtu amekusudia kwenda kuswali Ijumaa lakini kabla hajaondoka Allah (s.w) akamnyang'anya mtu huyo neema ya akili au fahamu, au akakosa nguvu hata za kukaa, ni dhahiri kuwa hataweza kuswali Ijumaa. Na hivyo hivyo kwa mtu aliyekusudia kwenda kuvunja duka na kupora mali kabla ya kufanya hivyo akavunjika mgongo au akatiwa upofu machoni, ni dhahiri kuwa hawezi kutenda lile alilolikusudia. Hivyo mema au maovu hayatendeki kinyume na uwezo wa Allah (s.w).

13

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

SUALA LA UONGOFU

Badhi ya watu hujiuliza: Kama sote tuna fursa sawa sawa ya kuchagua kutenda mema au maovu mbona Qur-an yasema Mwenyezi Mungu humuongoza amtakaye na humuacha kupotea amtakaye? Uongofu utokao kwa Mwenyezi Mungu uko wa namna mbili: Kwanza uongofu kwa maana ya kumfahamisha mtu njia sahihi ya kufuata. Na pili uongofu kwa maana ya msaada utokao kwa Mwenyezi Mungu.

Uongofu kwa maana ya kwanza, yaani kujulishwa njia ya heri na ya shari, na kujulishwa jambo lipi mtu atende na lipi aliwache, ni uongofu ambao kila mtu anaupata. Na uongofu huo ni wa namna tatu kwanza ni: fitra, yaani kupandikizwa uongofu katika nafsi yake mtu:

﴿وَنَفْسٍ وَمَا سَوَّاهَا ﴿٧﴾ فَأَلْهَمَهَا فُجُورَهَا وَتَقْوَاهَا﴾

Na kwa nafsi na aliyeitengeneza.Kisha akaifahamisha uovu wake na wema. (91:7-8)

Na uongofu wa namna ya pili ni kipawa cha akili, ambacho kinaweza kutumika kuisadikisha imani. Na namna ya tatu ni uongofu aliopewa binaadamu kwa kupitia Mitume na Vitabu vya Mwenyezi Mungu. Hivyo kila mtu amepata uongofu kutoka kwa Mwenyezi Mungu angalau kwa njia mbili za mwanzo.

Uongofu kwa maana ya msaada wanaupata wale tu wanaoamua kuufuata kikweli kweli ule uongofu waliopewa. Tuseme mathalan mtu fulani amepotea mjini au hajui njia ya kwenda mahali fulani akaamua kumuuliza askari: Baada ya kumuelekeza mtu yule aliyepotea aseme: Sikuamini, mwongo mkubwa wee!! Askari atamwambia: Sawa fuata njia unayoijua. Lakini iwapo mtu aliyepotea baada ya kuelekezwa atasema: Ahsante sana kwa kunielekeza nafikiri nitafika ninakokusudia, askari anaweza kumwambia: Subiri kidogo mimi nakwenda huko huko nitakupeleka hadi unapokwenda. Huu ni mfano tu, na Mwenyezi Mungu hawezi kufananishwa na askari au kiumbe yeyote.Kusudio hapa ni kuonesha kuwa watu wanaofuata muongozo wa Mwenyezi Mungu huzidishiwa uongofu:

﴿وَالَّذِينَ اهْتَدَوْا زَادَهُمْ هُدًى وَآتَاهُمْ تَقْوَاهُمْ﴾

Na wale wanaokubali kuongoka anawazidishia uongofu na anawapa (jaza) ya ucha Mungu wao. (47:17)

﴿نَّحْنُ نَقُصُّ عَلَيْكَ نَبَأَهُم بِالْحَقِّ إِنَّهُمْ فِتْيَةٌ آمَنُوا بِرَبِّهِمْ وَزِدْنَاهُمْ هُدًى﴾

Sisi tunakusimulia habari zao kwa kweli. Hakika wao walikuwa ni vijana waliomuamini Mola wao Nasi tukawazidisha uongofu.(18:13)

Ili kuweka wazi zaidi uongofu wa aina hii ya pili hebu tuizingatie kwa makini aya aifuatayo:

﴿إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ يَهْدِيهِمْ رَبُّهُم بِإِيمَانِهِمْ تَجْرِي مِن تَحْتِهِمُ الْأَنْهَارُ فِي جَنَّاتِ النَّعِيمِ﴾

Hakika wale walioamini na kufanya vitendo vizuri, Mola wao atawaongoza kwa sababu ya imani yao (wende katika Pepo) Itakuwa inapita mito mbele yao katika mabustani yenye neema. (10:9).

"Allah (s.w) humwingiza katika rahma zake amtakaye na kumwacha kupotea amtakaye" Muradi wa aya zenye melekeo huu ni kuwa Allah(s.w) ametoa sifa za waumini kama zilivyoaminishwa katika Qur'an mf.( 23: 1-11), (25: 63-77), (8:2-4), (49: 1-13,15), (70:19-35), n.k.

Hawa ndiyo "anaowataka" basi anayetaka awepo katika kundi hilo hana budi ajipambe kwazo. lakini pia ametoa sifa za wafiki, washirikina, makafiri, .n.k kama zilivyoanishwa katika qur'an (33:12-20), (2:8-20), (3:166-171), (4:135-152), n.k. Watu watakojipamba na sifa hizi basi Allah huwaacha ( akawaelekezea huko) kupotea, Allah (s.w) ni mwadilifu, humrahisishia mja kila akitakacho cha kheri au cha shari, ndiyo maana pia anasema, "Haakhirishi ya watu mpaka watu wabadilishe yayokuwa katika nafsi zao....." Mbona kuna Uovu na Mateso Duniani? Kuna baadhi ya watu ambao huuliza hivi: Iwapo Mwenyezi Mungu anawapenda waja wake mbona anaacha maovu na mateso yaendelee duniani?Kwa nini asiyazuie?

Kwanza : ni makosa kumhukumu Mwenyezi Mungu ambaye ni Mjuzi wa kila kitu kwa vipimo vya kibinaadamu. Hii ni kwa sababu binaadamu mara nyingi anaathiriwa na hisia zake binafsi na maslahi yake katika kufanya maamuzi yake. Kwa mfano tunaamuaje kuwa kitu fulani ni chema au kibaya? Tuchukue mifano rahisi.Mvua ikinyesha mkulima aliyepanda mazao anamshukuru Mwenyezi Mungu lakini mtu anayekwenda pikiniki au anayefanya sherehe ya harusi, mvua hasa ikinyesha kutwa nzima ni nuksi kubwa kwake!Au tuseme mtu amekodi teksi anawahi ndege uwanjani kwenda kumzika mama yake.

Kwa sababu ya msongamano wa magari barabarani amechelewa kufika uwanjani na hivyo ndege imemwacha na safari kaikosa. Atalaani mtu huyo na kudai kuwa huo ni mkosi mkubwa. Baada ya nusu saa akisikia kuwa ndege ile imeanguka na watu wote wamekufa utamsikia anamshukuru Mungu kwa bahati njema aliyoipata! Binaadamu hawana haki ya kumuuliza Mwenyezi Mungu kama tunavyofahamishwa katika Qur-an:

﴿لَا يُسْأَلُ عَمَّا يَفْعَلُ وَهُمْ يُسْأَلُونَ﴾

Haulizwi (Mwenyezi Mungu) anayoyafanya lakini wao (viumbe wataulizwa).(21:23)

Hii haina maana kuwa binaadamu wanakatazwa kujaribu kutafuta hikima ya Mwenyezi Mungu katika kuamrisha au kukataza kwake mambo, La!Kinyume chake wanahimizwa kufanya hivyo. Wanachokatazwa ni kujaribu kumhukumu Mwenyezi Mungu au kuyakataa na kuyapinga yale ambayo hikima yake hawaijui. Hivyo katika hizo jitihada za kujaribu kubahatisha kuona hikima ya kuyaacha maovu na mateso yawepo baadhi ya watu wanasema kuwa lau si kuwepo kwa uovu watu wasingejua nini wema, bila kuwepo maradhi watu wasingejua thamani ya afya na bila ya mauti watu wasingeyathamini maisha. Wengine wanasema hata wadudu wabaya tunaodhani wanawabughudhi binaadamu, tunadhani hivyo kwa sababu tu hatujajua thamani yao kwetu.

Jambo la kukumbuka ni kuwa kwa mujibu wa Qur-an binaadamu katika kipindi chote cha maisha yake hapa duniani yupo katika majaribio. Na majaribio hayo yatachukua sura mbali mbali za heri na shari. Na jingine ni kwamba ili mtihani huo uwe na maana yoyote watu lazima wawe na hiari ya uchaguzi. Hii ina maana kuwa watu wanaweza kuchagua uovu pia. Hivyo iwapo Mwenyezi Mungu atawapa watu hiari ya uchaguzi lakini atahakikisha hawachagui kufanya ufisadi na uovu nini maana ya kutoa mtihani? Hii haina maana kuwa baada ya kuumbwa ulimwengu Mwenyezi Mungu ameususa na kuuacha uende vyovyote utakavyokwenda, La!Bali kila kitu kipo katika Qadar yake.

Maana ya Kuamini Qadar katika Maisha ya Kila Siku Kwanza, Kwa kujua kuwa fursa, bahati, vipaji na neema zote alizonazo hakuzipata kwa uwezo wake, hanabudi kuvitumia vitu hivi kama amana aliyokabidhiwa na Mola wake. Hanabudi kuitumia amana hii vizuri ili kumuwezesha kufikia lengo la kuumbwa kwake. Muumini wa kweli ana yakini kabisa kuwa atakapo khini amana aliyokabidhiwa na Mola wake, atakuwa ni mwenye kukosa shukrani na atastahiki kuadhibiwa.

﴿ثُمَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ﴾

Kisha kwa hakika mtaulizwa siku hiyo juu ya neema (mlizopewa mlizitumiaje)" (102:8)

Pili : Kwa kujua pia kuwa fursa, bahati, vipaji na neema zote zinatoka kwa Allah (s.w), halalami pale atakapokuwa amekadiriwa vitu hivi kwa uchache. Yaani hatalalama na kukata tamaa pale atakapokosa fursa mbali mbali, atakapofikiwa na bahati mbaya, atakapodhikishwa vipaji na neema mbali mbali. Bali ataridhika na alichokadiriwa na Mola wake na pia atamshukuru Mola wake kwa kumpangia amana ndogo anayoiweza kuitunza, kwani huenda kama angelikabidhiwa amana kubwa zaidi ya hiyo aliyonayo, angelishindwa kuitunza na kuwa miongoni mwa waliofeli mtihani.

Tatu : atajitahidi kutumia fursa, bahati, vipaji na neema zote alizotunukiwa na Mola wake kwa kadiri ya uwezo wake, kisha matunda ya jitihada hizo huyategemeza kwa Mola wake. Akipata matunda mazuri yaliyotarajiwa hafurahi kupita kiasi, bali atakuwa na furaha ya kawaida ikiambatana na kumshukuru Mola wake kwa kuzidisha kutenda wema kwa kuswali Sunnat-shukra, kutoa sadaqa, kufunga sunnah, n.k. Akipata matunda dhaifu asiyoyategemea, hatakata tamaa na kusononeka, bali ataridhika na matokeo hayo, na ataona ndio makadirio ya Allah (s.w) na ndiyo yenye manufaa naye. Atashukuru na kusema "Al-hamdulillah 'Alaa kullihaali"

Nne : anapotokewa na misuko suko mbali mbali iliyo nje ya uwezo na jitihada za binaadamu, huwa ni mwenye kutulizana na kusubiri akijua kuwa:

﴿مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ ﴿٢٢﴾ لِّكَيْلَا تَأْسَوْا عَلَىٰ مَا فَاتَكُمْ وَلَا تَفْرَحُوا بِمَا آتَاكُمْ وَاللَّـهُ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ﴾

"Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwisha andikwa katika kitabu kabla hatujaumba.Kwa yakini hilo ni sahali kwa Allah, Ili msihuzunike sana juu ya kitu kilichokupateni. Na Allah hampendi kila ajivunaye, ajifaharishaye" (57:22-23)

Muumini wa kweli anajua kuwa misiba na misuko suko mbali mbali ni katika qadar ya Allah (s.w) kama tunavyojifunza katika aya ifuatayo:

﴿وَلَنَبْلُوَنَّكُم بِشَيْءٍ مِّنَ الْخَوْفِ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ الْأَمْوَالِ وَالْأَنفُسِ وَالثَّمَرَاتِ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ﴾

"Na tutakutieni katika misuko suko na hofu, njaa, upungufu wa mali na watu na matunda.Na wapashe habari njema wale wanaosubiri. (2:155)

Tano : Mtu anayeamini Qadar ya Allah (s.w), siku zote huyaweka mategemeo yake yote kwa Allah (s.w) ambaye ndiye mdhibiti wa kila jambo. Huendelea kutimiza wajibu wake kwa ujasiri na subira hata anapokuwa katika mazingira magumu kwa kuwa anayakini kuwa:

﴿قُل لَّن يُصِيبَنَا إِلَّا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَنَا هُوَ مَوْلَانَا وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ﴾

"... Halitatusibu ila alilotuandikia Mwenyezi Mungu, Yeye ni Mola wetu. Basi waislamu na wamtegemee Mwenyezi Mungu tu" (9:51)

SURA YA NNE

LENGO LA MAISHA YA MWANADAMU

Lengo la maisha Ili mwanaadamu aweze kuishi maisha yenye maana hapa ulimwenguni hanabudi kuwa na ujuzi wa yakini juu ya Lengo, Hadhi na Dhima aliyonayo hapa ulimwenguni.Lengo la kuumbwa watu limebainishwa katika Qur-an kama ifuatavyo:

﴿وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ ﴾

Sikuwaumba majini na watu ila wapate kuniabudu. (51:56)

Aya hii inabainisha wazi kuwa watu hawakuletwa hapa ulimwenguni kwa lengo lingine ila kumuabudu Allah (s.w) tu. Kumuabudu Allah (s.w) ni kufanya Ibada kwa ajili ya Allah (s.w). Maana ya Ibada kwa Mnasaba wa Lengo la Kuumbwa Ibada ni neno la Kiarabu linalotokana na neno "Abd" lenye maana ya Mtumwa au mtumishi. Hivyo kumuabudu Allah (s.w) ni kumtumikia Allah (s.w) kitumwa au kumtumikia Allah (s.w) kikweli kweli bila ya kuwa na hiari katika utumishi huo. Kwa maana hii, lengo la kuumbwa mwanaadamu ni kumtumikia Allah (s.w) kwa unyenyekevu bila ya kumtumikia mwingine yeyote kinyume na mwongozo wake.

Kwa hiyo, ili mwanaadamu aishi kulingana na lengo la kuumbwa kwake, hanabudi kumuabudu Allah (s.w) katika kila hatua na kila pumzi ya maisha yake kwa kuzingatia na kufuata maamrisho yake yote na kuacha makatazo yake yote na kuchunga bara bara mipaka yake kwa kila atakalolifanya. Kwa maana nyingine kila kitendo atakachokifanya mtu kwa lengo la kupata radhi ya Allah (s.w) kitakuwa ni Ibada. Kwa mfano kuchuma mali kwa kuzingatia mipaka ya Allah (s.w) ili kupata riziki ya halali na mahitajio muhimu ya maisha ni Ibada. Kula chakula kizuri na halali ili upate afya nzuri itakayokuwezesha kutekeleza majukumu yako ya kifamilia na ya kijamii kwa ujumla ni Ibada Kulala au kujipumzisha ili uweze kupata nguvu mpya ya kiakili na kimwili itakayokuwezesha kutekeleza majukumu yako kwa jamii ni Ibada. Kwa ujumla kila kitendo kizuri cha halali kilichotendwa kwa kuchunga mipaka ya Allah (s.w) kwa nia ya kumuwezesha mtu kuwa katika hali nzuri ya kutekeleza wajibu wake kwa Allah (s.w) na kwa jamii kwa ujumla ni Ibada.

Mtazamo Potofu Juu ya Maana ya Ibada Baadhi ya watu wameifinya ibada ya Allah (s.w) kwa kuinasibisha na matendo maalumu tu kama vile kuswali, kutoa zakat na sadaqa, kufunga, kuhiji, na ibada nyingine za sunnah zilizoambatana na hizi. Kwa mtazamo huu, matendo yaliyo nje ya Swala, Zakat, Swaum,na kadhalika. si ibada. Je, tutakuwa tumefikia lengo la kuumbwa kwetu kwa kutekeleza tu hizi ibada maalumu? Ukichunguza utaona kuwa muda wanaotumia Waislamu katika kutekeleza ibada hizi maalum ni mdogo sana. Kwa mfano muda tunaotumia kuswali swala tano za siku, ibada ambayo Waislamu wanaitekeleza kwa wingi kuliko ibada nyingine yoyote katika nguzo za Uislamu, ni mdogo sana. Jaalia tunachukua dakika 20 kwa kila swala; hivyo tutahitaji dakika 100 tu katika sa 24 za siku. Hii ni na asilimia 7 (7%) tu ya muda wa siku.

Kuhusu Zakat, kiasi kinachotakiwa kutolewa na tajiri aliye na mali iliyofikia nisaabu ni asilimia 2.5 (2.5%) tu. Vile vile tukichukua mfano wa funga ya Ramadhani, tutaona ni muda mfupi tu tunaotumia katika funga. Jalia tunafunga mwezi mzima wenye siku 30 na kila siku tunafunga kwa saa 14 katika nyakati za kiangazi, ambapo mchana ni mrefu kuliko usiku. Kwa mfano huu kiasi tunachofunga ni sawa na asilimia 5 (5%) ya muda wa mwaka.

Kwa mifano hii michache utaona kuwa lengo la kuumbwa kwetu halitatimia kwa kutekeleza tu hizi ibada za Swala, Zakat, Funga, Hija, n.k. bali tunatakiwa tumuabudu Allah (s.w) muda wote wa saa 24 kwa maisha yetu yote. Hivi ndivyo Allah (s.w) anatuamrisha katika aya zifuatazo:

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ادْخُلُوا فِي السِّلْمِ كَافَّةً وَلَا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ﴾

"Enyi mlioamini! Ingieni katika Uislamu wote, wala msifuate nyayo za shetani, kwa hakika yeye kwenu ni adui dhahiri" (2:208)

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ﴾

"Enyi mlioamini! Mcheni-Mwenyezi Mungu kama ipasavyo kumcha,wala msife isipokuwa mmekwisha kuwa Waislamu kamili." (3:102)

Aidha, Allah (s.w) anatufahamisha kuwa wale wenye akili miongoni mwa wanaadamu ni wale wanaomuamini Allah (s.w) na kumuabudu katika kila kipengele cha maisha yao kama tunavyojifunza katika aya ifuatayo:

﴿إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ ﴿١٩٠﴾ الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَـٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ﴾

Katika kuumbwa mbingu na ardhi na mfuatano wa usiku na mchana ziko hoja (za kuonyesha kuwepo kwa Allah (s.w) kwa wenye akili.Ambao humkumbuka Allah wakiwa wima, wakiwa wamekaa na wakiwa wamelala. Na hufikiri umbile la mbingu na ardhi (tena na tena kisha wanasema), Mola wetu! Hukuviumba hivi bure (pasina lengo).Utukufu ni wako. Basi tuepushe na adhabu ya Moto (3:190-191).

Aya hizi zinatuusia kuwa tumuabudu Allah (s.w) katika shughuli zetu zote tunazozifanya tukiwa tumesimama, tukiwa tumekaa na tukiwa tumelala. Tutahesabika kuwa katika ibada katika kila sekunde ya maisha yetu pale tutakapofanya kila jambo au kila shughuli ya kibinafsi au kijamii kwa kuzingatia mwongozo wa Allah (s.w) na kuchunga bara bara mipaka aliyotuwekea.

Vinginevyo kumuabudu Allah (s.w) kwa baadhi ya wakati, haikubaliki kabisa kama tunavyojifunza katika aya ifuatayo:

﴿أَفَتُؤْمِنُونَ بِبَعْضِ الْكِتَابِ وَتَكْفُرُونَ بِبَعْضٍ فَمَا جَزَاءُ مَن يَفْعَلُ ذَٰلِكَ مِنكُمْ إِلَّا خِزْيٌ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يُرَدُّونَ إِلَىٰ أَشَدِّ الْعَذَابِ وَمَا اللَّـهُ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ﴾

"...Je! Mnaamini baadhi ya kitabu na kukataa baadhi (yake)? Basi hakuna malipo kwa mwenye kufanya haya katika nyinyi ila fedheha katika maisha ya dunia; na siku ya kiyama watapelekwa katika adhabu kali. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na yale mnayoyatenda" (2:85).