MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU 0%

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU Mwandishi:
Kundi: Vitabu mbali mbali

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

Mwandishi: NDUGU ZETU WA KISUNNI
Kundi:

Matembeleo: 44455
Pakua: 3458

Maelezo zaidi:

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 22 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 44455 / Pakua: 3458
Kiwango Kiwango Kiwango
MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

Mwandishi:
Swahili

14

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

LENGO LA IBADA MAALUMU

Baadhi ya Waislamu, pamoja na kulifinyisha lengo la kuumbwa mwanaadamu kwa kulinasibisha tu na utakelezaji wa Ibada maalumu kama vile Swala, Zakat, Saumu, pia wamelifinyisha lengo la hizi ibada maalumu kuwa ziko pale ili:

(i) Kutupatia thawabu na kutuingiza Peponi tu na hazina mahusiano yoyote na maisha ya kila siku ya kibinafsi na kijamii.

(ii) Kuwa kifutio cha madhambi, hivyo mtu hufanya maovu kwa furaha, pasina hofu yoyote.

(iii) Kumfurahisha na kumfaidisha Mwenyezi Mungu. Huu nao ni mtazamo finyu wa hizi ibada maalumu kwa sababu.

Kwanza : Allah (s.w) mara tu baada ya kutufahamisha lengo la kuwaumba Majini na Watu, ametoa tahadhari kuwa wasije Majini na Watu wakadhania kuwa Allah (s.w) amewaumba kwa lengo hilo ili wamnufaishe, kwani yeye si muhitaji; bali viumbe ndio wanaomuhitajia kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:

﴿وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ ﴿٥٦﴾ مَا أُرِيدُ مِنْهُم مِّن رِّزْقٍ وَمَا أُرِيدُ أَن يُطْعِمُونِ ﴿٥٧﴾ إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الرَّزَّاقُ ذُو الْقُوَّةِ الْمَتِينُ﴾

"Sikuwaumba majini na watu ila wapate kuniabudu.Sitaki kwao riziki wala sitaki wanilishe.Kwa yakini Mwenyezi Mungu ndiye mtoaji wa riziki, Mwenye nguvu, madhubuti" (51:56-58)

Pili : Allah (s.w), pamoja na kutuamrisha kutekeleza hizi ibada maalumu, ametufahamisha vile vile lengo la kila ibada. Kwa mfano, kuhusu lengo la Swala tunafahamishwa:

﴿اتْلُ مَا أُوحِيَ إِلَيْكَ مِنَ الْكِتَابِ وَأَقِمِ الصَّلَاةَ إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ وَلَذِكْرُ اللَّـهِ أَكْبَرُ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مَا تَصْنَعُونَ﴾

"Bila shaka Swala (ikiswaliwa vilivyo) humzuilia (mwenye kuswali na) mambo machafu na maovu" (29:45).

Lengo la utoaji wa Zakat na Sadaqat linabainishwa kuwa ni kumtakasa mtoaji na makosa yanayosababishwa na umilikaji wa mali:

﴿خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا وَصَلِّ عَلَيْهِمْ إِنَّ صَلَاتَكَ سَكَنٌ لَّهُمْ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴾

"... Chukua Sadaqa katika mali zao uwatakase kwazo na kuwataja kwa uzuri (mbele yangu) na uwaombee dua..." (9:103).

Lengo la Swaumu nalo linabainishwa kuwa ni kumfanya mfungaji awe mcha-Mungu:

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ﴾

"Enyi Mlioamini! Mmeamrishwa kufunga kama walivyoamrishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha-Mwenyezi Mungu (2:183).

Mcha Mungu ni yule anayeishi kwa kufuata mwongozo wa Allah (s.w) na kuchunga mipaka yake katika kukiendea kila kipengele cha maisha yake.

Ibada ya Hija, pamoja na kumuandaa Al-Hajj kuwa Mcha- Mungu, inamtayarisha pia kuwa tayari kuipigania dini ya Allah (s.w) kwa mali yake na nafsi yake. Hadhi ya Waumini Hapa Ulimwenguni Hadhi tarajiwa ya mwanaadamu hapa ulimwenguni inabainika vizuri kwa kurejea kwa makini aya zifuatazo:

﴿وَإِذْ قَالَ رَبُّكَ لِلْمَلَائِكَةِ إِنِّي جَاعِلٌ فِي الْأَرْضِ خَلِيفَةً قَالُوا أَتَجْعَلُ فِيهَا مَن يُفْسِدُ فِيهَا وَيَسْفِكُ الدِّمَاءَ وَنَحْنُ نُسَبِّحُ بِحَمْدِكَ وَنُقَدِّسُ لَكَ قَالَ إِنِّي أَعْلَمُ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٣٠﴾ وَعَلَّمَ آدَمَ الْأَسْمَاءَ كُلَّهَا ثُمَّ عَرَضَهُمْ عَلَى الْمَلَائِكَةِ فَقَالَ أَنبِئُونِي بِأَسْمَاءِ هَـٰؤُلَاءِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٣١﴾ قَالُوا سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا إِنَّكَ أَنتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ ﴿٣٢﴾ قَالَ يَا آدَمُ أَنبِئْهُم بِأَسْمَائِهِمْ فَلَمَّا أَنبَأَهُم بِأَسْمَائِهِمْ قَالَ أَلَمْ أَقُل لَّكُمْ إِنِّي أَعْلَمُ غَيْبَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَأَعْلَمُ مَا تُبْدُونَ وَمَا كُنتُمْ تَكْتُمُونَ ﴿٣٣﴾ وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ أَبَىٰ وَاسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنَ الْكَافِرِينَ﴾

"(Wakumbushe) wakati Mola wako alipowaambia Malaika,Mimi nitajaalia khalifa katika ardhi.Wakasema (Malaika) utaweka humo watakaofanya uharibifu humo na kumwaga damu, hali sisi tunakutukuza kwa sifa zako na kukutaja kwa utakatifu wako? Akasema (Mwenyezi Mungu)"Hakika mimi najua msiyo yajua" "Na Mwenyezi Mungu akamfundisha Adam majina ya vitu vyote, kisha akaviweka mbele ya Malaika, na akasema, "Niambieni majina ya vitu hivi ikiwa mnasema kweli."Wakasema (Malaika): "Utakatifu ni wako! Hatuna ilimu isipokuwa ile uliyotufundisha; bila shaka wewe ndiye Mjuzi na ndiye Mwenye Hekima. Akasema (Mwenyezi Mungu),"Ewe Adam waambie majina yake" Alipowaambia majina yake alisema (Mwenyezi Mungu): "Sikukwambieni kwamba mimi ninajua siri za mbinguni na za ardhi; tena najua mnayoyadhihirisha na mliyokuwa mnayaficha?" Na (wakumbushe watu khabari hii): Tulipowaambia Malaika, "Msujudieni Adam" (yaani muadhimisheni kwa ile ilimu yake aliyopewa) Wakamsujudia wote isipokuwa Ibilis; akakataa na akajivuna; na (tokea hapo) alikuwa katika makafiri" (2:30-34).

Tunajifunza kutokana na aya hizi kuwa mwanaadamu amekusudiwa kuwa Khalifa wa Mwenyezi Mungu hapa ulimwenguni. Ukhalifa ni cheo chenye hadhi kubwa mbele ya Allah (s.w). Kuamrishwa kwa malaika kumsujudia Adam ni dalili tosha kuwa mwanaadamu anapochukua nafasi yake ya Ukhalifa anakuwa na hadhi kubwa mbele ya Allah (s.w) kuliko ile ya Malaika. Pamoja na Adamu kufundishwa majina ya vitu vyote aliahidiwa kuletewa mwongozo utakaomuelekeza kufuata njia sahihi ya maisha.

﴿قُلْنَا اهْبِطُوا مِنْهَا جَمِيعًا فَإِمَّا يَأْتِيَنَّكُم مِّنِّي هُدًى فَمَن تَبِعَ هُدَايَ فَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ ﴿٣٨﴾ وَالَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ﴾

Tukasema shukeni humo nyote, na kama ukikufikieni mwongozo utokao Kwangu basi watakaofuata mwongozo huo haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika. Lakini wenye kukufuru na kuyakadhibisha maneno yetu, hao ndio watokaokuwa watu wa Motoni humo watakaa milele." (2:38-39)

Nyenzo kuu inayomuwezesha mwanaadamu kuwa Khalifa ni elimu ya mazingira aliyotunukiwa na Mola wake na mwongozo alioshushiwa kutoka kwake. Majina ya vitu vyote inaashiria taaluma ya fani zote anazohitajia mwanaadamu katika kuendesha maisha yake yote ya kibinafsi na kijamii. Khalifa ni kiongozi kwa niaba ya Allah (s.w) hapa ulimwenguni.Yaani, yule anayesimamisha Ufalme wa Allah (s.w) au Dola ya Kiislamu katika jamii kwa kuhakikisha kuwa sharia za Allah (s.w) ndizo zinazotawala katika kuendesha kila kipengele cha maisha ya jamii ili kusimamisha uadilifu katika jamii hiyo. Jamii itaweza kuishi kwa furaha na amani ya kweli pale tu patakapokuwa na utawala unaosimamia haki na uadilifu.

Wanaostahiki Ukhalifa Pamoja na mwanaadamu kukusudiwa kuwa Khalifa katika ardhi, si kila mtu atakuwa Khalifa. Ahadi ya ukhalifa imetolewa kwa watu maalum kama tunavyojifunza katika aya ifuatayo:

﴿وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَىٰ لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّن بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئًا وَمَن كَفَرَ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ﴾

"Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na kufanya vitendo vizuri kuwa atawafanya Makhalifa katika ardhi kama alivyowafanya Makhalifa wale waliokuwako kabla yao, na kwa yakini, Atawasimamishia dini yao aliyowapendelea, na atawabadilishia amani baada ya hofu yao. Wawe wananiabudu, hawanishirikishi na chochote. Na watakao kufuru baada ya hayo, basi hao ndio wavunjao amri zetu (24:55)

Tunajifunza katika aya hii kuwa wanaostahiki kuwa Makhalifa wa Allah (s.w) ni waumini watendaji. Waumini watendaji ni wale waumini wa kweli kama wanavyobainishwa katika aya zifuatazo:

﴿إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ ﴿٢﴾ الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿٣﴾ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا لَّهُمْ دَرَجَاتٌ عِندَ رَبِّهِمْ وَمَغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ﴾

"Hakika wanaoamini kweli ni wale ambao anapotajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa khofu; na wanaposomewa Aya zake huwazidishia imani, na wakamtegemea Mola wao tu basi.Ambao wanasimamisha swala na wanatoa katika yale tuliyowapa.Hao ndio wanaoamini kweli kweli.Wao wana vyeo (vikubwa) kwa Mola wao, na msamaha na riziki bora (kabisa huko Akhera) (8:2-4)

﴿إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ ثُمَّ لَمْ يَرْتَابُوا وَجَاهَدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ﴾

Wenye kuamini kweli kweli ni wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake; kisha wakawa si wenye shaka, na wakaipigania dini ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao.Hao ndio wenye kuamini kweli. (49:15)

Pia kutokana na aya hii ya (24:55) tunajifunza kuwa ishara itakayotuonyesha kuwa Ukhalifa umesimama katika ardhi ni pale sharia za Kiislamu zitakapo tawala katika ardhi au pale dola ya Kiislam itakapokuwa imesimamishwa katika jamii kama ilivyosimamishwa wakati wa Mtume(s.a.w.w).

Dhima ya Waumini katika Jamii Dhima ya kwanza kwa waumini ni kujielimisha au kusoma kwa ajili ya Allah (s.w). Hii ndiyo amri ya kwanza ya Allah (s.w) juu ya waumini kama tulivyoona katika sura ya kwanza ya juzuu hii. Pia tumeona kuwa elimu imepewa nafasi ya kwanza katika Qur-an kwa sababu ndiyo nyezo kuu inayowawezesha waumini kumuabudu Mola wao ipasavyo na kusimamisha Uislamu katika jamii. Pia tumeona kuwa elimu tuliyoamrishwa kuitafuta ili tuwe makhalifa wa Allah (s.w) katika jamii ni fani zote za elimu zinazohitajika katika kuendesha maisha ya jamii (Qur-an, 2:30- 31) pamoja na elimu ya mwongozo (maarifa ya Uislamu) kutoka kwa Allah (s.w) kupitia kwa Mitume wake na vitabu vyake (Rejea Qur-an, 2:38-39).

Dhima ya pili kwa waumini ni kumcha Allah (s.w) ipasavyo kama anavyotuamrisha:

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ﴾

"Enyi Mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu kama ipasavyo kumcha, wala msife isipokuwa mmekwishakuwa Waislamu kamili" (3:102)

Kumcha Allah (s.w) ni kumtii Allah na kuchunga bara bara mipaka aliyotuwekea katika kuendea njia ya maisha yetu ya kila siku. Aya hii inawaamrisha waumini kufanya jitihada za makusudi za kumuabudu Allah (s.w) katika kila kipengele cha maisha na kudumu na ibada hiyo mpaka mwisho wa maisha yao ya hapa duniani.

Dhima ya tatu kwa waumini ni kulingania kheri au kuufikisha ujumbe wa Uislamu kwa watu ambao haujawafikia au kuwakumbusha wautekeleze wale ambao umeshawafikia.Hapana Mtume yoyote atakayeletwa baada ya mtume Muhammad(s.a.w.w). Hivyo dhima ya kulingania Uislamu iko juu ya waumini wote. Kufundisha na kulingania uislamu katika jamii ni jambo muhimu mno kwa waumini kama tunavyojifunza katika aya ifuatayo:

﴿وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلًا مِّمَّن دَعَا إِلَى اللَّـهِ وَعَمِلَ صَالِحًا وَقَالَ إِنَّنِي مِنَ الْمُسْلِمِينَ﴾

"Na ni nani asemaye kauli bora zaidi kuliko aitaye (watu) kwa (dini ya) Mwenye zi Mungu na mwenyewe akafanya vitendo vizuri (akawa Muislamu) na husema (kwa maneno yake na vitendo vyake); "Hakika mimi ni miongoni mwa waislamu." (41:33).

Tunajifunza kuwa baada ya Muumini kuufahamu Uislamu vilivyo na kujipamba nao katika maisha yake ya kila siku, hana budi kuulingania na kuufundisha katika jamii. Pia tunajifunza kutokana na aya hii kuwa kazi ya kulingania uislamu na kuufundisha ni bora kuliko kazi nyingine. Hii ndio kazi ya Mitume wa Allah (s.w). Dhima ya nne ya waumini ni kushikamana pamoja. Dhima hii imewekwa bayana katika Qur-an:

﴿ وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا﴾

"Na shikamaneni kwa kamba (dini) ya Mwenyezi Mungu nyote, wala msifarikiane" (3:103).

﴿وَاعْتَصِمُوا بِاللَّـهِ هُوَ مَوْلَاكُمْ فَنِعْمَ الْمَوْلَىٰ وَنِعْمَ النَّصِيرُ ﴾

Na shikamaneni na Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mlinzi wenu, Mlinzi bora kabisa, na Msaidizi bora kabisa.

﴿إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الَّذِينَ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِهِ صَفًّا كَأَنَّهُم بُنْيَانٌ مَّرْصُوصٌ﴾

"Kwa yakini Mwenyezi Mungu anawapenda w ale wanaopigana katika njia yake safu safu kama kwamba wao ni jengo lililokamatana barabara." (61:4)

Mshikamano wa Waumini umeamrishwa juu yetu na Allah (s.w) kwa sababu ndio msingi wa nguvu za waumini zitakazowawezesha kuwashinda maadui zao na kuuwezesha Uislamu kusimama katika jamii. Mshikamano wa waumini chini ya Uongozi wa Mtume(s.a.w.w) ni mfano wa kuigwa uliowazi:

﴿مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّـهِ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ تَرَاهُمْ رُكَّعًا سُجَّدًا يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانًا سِيمَاهُمْ فِي وُجُوهِهِم مِّنْ أَثَرِ السُّجُودِ ذَٰلِكَ مَثَلُهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَمَثَلُهُمْ فِي الْإِنجِيلِ كَزَرْعٍ أَخْرَجَ شَطْأَهُ فَآزَرَهُ فَاسْتَغْلَظَ فَاسْتَوَىٰ عَلَىٰ سُوقِهِ يُعْجِبُ الزُّرَّاعَ لِيَغِيظَ بِهِمُ الْكُفَّارَ وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ مِنْهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا﴾

"Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walio pamoja naye ni wenye nyoyo thabiti mbele ya makafiri na wenye kuhurumiana wao kwa wao. Utawaona wakiinama kwa kurukuu na kusujudu (pamoja), wakitafuta fadhila za Mwenyezi Mungu na radhi (yake). Alama zao zi katika nyuso zao,kwa taathira, (athari) ya kusujudu.Huu ndio mfano wao katika Taurati.Na mfano wao katika Injili (umetajwa hivi.Kuwa (wao) ni kama mmea uliotoa matawi yake; kisha (matawi hayo) yakautia nguvu, ukawa mnene ukasimama sawasawa juu ya kigogo chake, ukawafurahisha walioupanda; ili awakasirishe makafiri kwa ajili yao. Mwenyezi Mungu amewaahidi walioamini na kutenda mema katika wao msamaha na ujira mkubwa. (48:29).

Dhima ya tano ya waumini ni kuamrisha mema kama Allah (s.w) anavyotuamrisha:

﴿وَلْتَكُن مِّنكُمْ أُمَّةٌ يَدْعُونَ إِلَى الْخَيْرِ وَيَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ﴾

"Na wawepo katika nyinyi watu wanaolingania kheri (Uislamu) na wanaoamrisha mema na wanaokataza maovu.Na hao ndio watakaotengenekewa" (3:104)

Waumini hata kama hawajafikia hatua ya kusimamisha dola ya Kiislamu, hawana budi kufanya mambo mazuri na kutoa huduma mbali mbali kama vile elimu, afya, ujenzi wa barabara, utunzaji wa mazingira, n.k. zitakazopelekea kuboresha maisha ya jamii kwa ujumla. Pia waislamu wanawajibika kwa mshikamano wao kuweka mazingira ya kufanya mambo mazuri ya kuistawisha jamii kiasi cha kuwafanya watu wengine, kwa haja za kibinaadamu, waunge mkono. Vile vile waislamu kwa umoja wao, wanawajibika kujenga mazingira yatakayowalazimisha watu kufanya mema, hata kama dola ya Kiislamu haijasismama.

Dhima ya sita kwa waumini ni kutakataza maovu yasitendeke katika jamii (Qur-an 3:104).

Hata kama dola ya Kiislamu haijasimama katika jamii waumini hawana budi kujiepusha na maovu yote hata yale yaliyozoeleka katika jamii hiyo. Kisha kwa umoja wao waumini wanawajibika kuweka mazingira ambayo wafanya maovu wataona haya. Pia waumini wanawajibika kuweka mikakati ya makusudi ya kuzuia maovu yasifanyike katika jamii, hata kama dola ya Kiislamu haijasimama. Waislamu watakapofikia hatua ya kukaa kimya na kuacha maovu yakafanywa kwa wasaa katika jamii, wajue kuwa hata wao hawatasalimika na adhabu ya Allah (s.w) itokanayo na maovu hayo hata kama hawakushiriki kuyafanya.

﴿وَاتَّقُوا فِتْنَةً لَّا تُصِيبَنَّ الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنكُمْ خَاصَّةً وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴾

"Na iogopeni adhabu (ya Mwenyezi Mungu ya hapa duniani) ambayo haitawasibu peke yao wale waliodhulumu nafsi zao miongoni mwenu (bali itawasibu hata walionyamaza wasiwakataze, bali na wengineo pia); na jueni ya kuwa Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu".(8:25).

Katika kusisitiza umuhimu wa kuamrisha mema na na kukataza maovu Mtume Muhammad(s.a.w.w) anatuasa katika Hadithi zifuatazo:

Abu Said Al-Khudhri (r.a) ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema:

"Yeyote miongoni mwenu atakayeona jambo ovu na aliondoe kwa mkono wake, kama hawezi na aliondoe kwa ulimi; na kama hawezi kuliondoa kwa ulimi na achukie moyoni mwake; na huku kuchukia kwa moyo tu ni kiwango cha chini cha imani." (Muslim)

Hudhaifah (r.a) ameeleza: Nimemsikia Mtume wa Allah amesema: "Naapa kwa yule ambaye mkononi mwake yako maisha yangu, mtaamrisha mema na mtakataza maovu, vinginevyo, ni hivi karibuni tu adhabu ya Mwenyezi Mungu itakuwa juu yenu.Kisha mtamuomba Mwenyezi Mungu, lakini hamtajibiwa." Jabir bin Abdullah (r.a) ameeleza:

Nimemsikia Mtume wa Allah akisema: "Hapana mtu ambaye anafanya maovu mbele ya watu ambao wana uwezo wa kumzuia, lakini wasijali kufanya hivyo, ila Mwenyezi Mungu atawaadhibu wote hapa duniani kabla hawajafa." (Abu Daud, Ibn Majah).

Dhima ya saba ya waumini ni kufanya juhudi za makusudi au kuingia katika Jihadi kuhakikisha kuwa Dini ya Allah (s.w) inasimama katika jamii. Dini ya Allah (s.w) itasimama pale sheria za Allah zitakapokuwa ndizo zinazotawala kila kipengele cha maisha ya jamii. Kuusimamisha Uislamu katika jamii ni faradhi kwa Waislamu kama tunavyojifunza katika aya ifuatayo:

﴿وَجَاهِدُوا فِي اللَّـهِ حَقَّ جِهَادِهِ هُوَ اجْتَبَاكُمْ وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ مِّلَّةَ أَبِيكُمْ إِبْرَاهِيمَ هُوَ سَمَّاكُمُ الْمُسْلِمِينَ مِن قَبْلُ وَفِي هَـٰذَا لِيَكُونَ الرَّسُولُ شَهِيدًا عَلَيْكُمْ وَتَكُونُوا شُهَدَاءَ عَلَى النَّاسِ﴾

"Na ipiganieni dini ya Mwenyezi Mungu kama inavyostahiki (kupiganiwa).Yeye amekuchagueni (muwe uma ulio bora) wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika dini. (Nayo dini hii) ni mila ya baba yenu Ibrahimu; Yeye (Mwenyezi Mungu) alikuiteni Waislamu tangu (katika vitabu vya zamani) huko; na katika (Qur-an) hii pia mumeitwa jina hilo); ili awe Mtume shahidi juu yenu na nyinyi muwe mashahidi juu ya watu waliotangulia..." (22:78)

Aya hii inatuweka wazi kuwa dhima hii ya kusimamisha Uislamu, si kwa Waislamu wa Umma huu wa Mtume Muhammad(s.a.w.w) bali ni dhima kwa waislamu wa zama zote. Pia tunajifunza katika Qur-an kuwa Dhima aliyokuwa nayo Mtume(s.a.w) na kwa hiyo dhima ya wafuasi wa kweli wa Mtume(s.a.w.w) ni kuutawalisha Uislamu katika jamii kama inavyobainishwa katika aya zifuatazo:

﴿هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ﴾

Yeye ndiye aliyemleta Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki ili aijaalie kushinda) dini zote; ijapokuwa watachukia washirikina. (9:33, 61:9)

﴿هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ شَهِيدًا﴾

"Yeye (Allah) ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki,ili aijaalie kushinda dini zote. Na Mwenyezi Mungu atosha kuwa shahidi" (48:28)

Mwenyezi Mungu ni shahidi kuwa Mtume(s.a.w.w) pamoja na Waislamu waliokuwa pamoja naye, walisimamisha Dola ya Kiislamu yenye nguvu kuliko dola zote za Kitwaaghuti zilizokuwepo siku zile. Pia ni katika utaratibu wa Mwenyezi Mungu kuwa wakati wowote Waislamu watakapo simama kidete kutekeleze amri yake ya kusimamisha dini yake, atawanusuru na kuwapa ushindi.

Dhima ya nane ya waumini ni kuihami dini ya Allah (s.w) isihujumiwe baada ya kusimama katika jamii. Waislamu wanaamrishwa na Mola wao waingie vitani kuuhami Uislamu kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:

﴿ أَلَا تُقَاتِلُونَ قَوْمًا نَّكَثُوا أَيْمَانَهُمْ وَهَمُّوا بِإِخْرَاجِ الرَّسُولِ وَهُم بَدَءُوكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ أَتَخْشَوْنَهُمْ فَاللَّـهُ أَحَقُّ أَن تَخْشَوْهُ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٣﴾قَاتِلُوهُمْ يُعَذِّبْهُمُ اللَّـهُ بِأَيْدِيكُمْ وَيُخْزِهِمْ وَيَنصُرْكُمْ عَلَيْهِمْ وَيَشْفِ صُدُورَ قَوْمٍ مُّؤْمِنِينَ ﴾

"Je, hamtapigana na watu waliovunja ahadi zao na wakafunga nia ya kumfukuza Mtume, nao ndio (pia) waliokuanzeni mara ya kwanza? Je,mnawaogopa? Basi Mwenyezi Mungu anastahiki zaidi mumuogope, ikiwa nyinyi mumeamini." piganeni nao, Mwenyezi Mungu awaadhibu kwa mikono yenu, na awafedheheshe na akunusuruni juu yao na avipoze vifua vya Waumini (wafurahi). (9:13-14)

﴿أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تُتْرَكُوا وَلَمَّا يَعْلَمِ اللَّـهُ الَّذِينَ جَاهَدُوا مِنكُمْ وَلَمْ يَتَّخِذُوا مِن دُونِ اللَّـهِ وَلَا رَسُولِهِ وَلَا الْمُؤْمِنِينَ وَلِيجَةً وَاللَّـهُ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ﴾

Je, mnadhani kuwa mtaachwa, na hali Mwenyezi Mungu hakuwabainisha wale waliopigania dini miongoni mwenu na wasiwafanye rafiki wa ndani isipokuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Waumini. Na Mwenyezi Mungu anazo habari za yote mnayoyafanya" (9:16)

﴿ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا مَا لَكُمْ إِذَا قِيلَ لَكُمُ انفِرُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ اثَّاقَلْتُمْ إِلَى الْأَرْضِ أَرَضِيتُم بِالْحَيَاةِ الدُّنْيَا مِنَ الْآخِرَةِ فَمَا مَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا فِي الْآخِرَةِ إِلَّا قَلِيلٌ ﴿٣٨﴾ إِلَّا تَنفِرُوا يُعَذِّبْكُمْ عَذَابًا أَلِيمًا وَيَسْتَبْدِلْ قَوْمًا غَيْرَكُمْ وَلَا تَضُرُّوهُ شَيْئًا وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴾

"Enyi mlioamini! Mnanini mnapoambiwa 'Nendeni (kupigana) kwa ajili ya dini ya Mwenyezi Mungu' mnajitia uzito katika ardhi? Je, mumekuwa radhi na maisha ya dunia kuliko ya akhera? Lakini starehe za maisha ya dunia kwa (mkabala wa maisha ya) akhera ni kidogo tu.Kama hamtakwenda atakuadhibuni kwa adhabu iumizayo na atawaleta watu wengine badala yenu, wala hamtamdhuru (Mwenyezi Mungu) chochote (mkitopigania dini yake); na Mwenyezi Mungu ni muweza juu ya kila kitu." (9:38-39)

﴿انفِرُوا خِفَافًا وَثِقَالًا وَجَاهِدُوا بِأَمْوَالِكُمْ وَأَنفُسِكُمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ﴾

Nendeni (vitani) mkiwa wepesi na mkiwa wazito (wazima au wagonjwa); na piganieni dini ya Mwenyezi Mungu kwa mali zenu na nafsi zenu.Haya ni bora kwenu, ikiwa mnajua." (9:41)

Kupigania Dini ya Allah (s.w) ili isimame katika jamii na kuihami isiporomoshwe baada ya kusimama kwake ni Dhima kubwa kwa Waislamu na ni amali bora kuliko amali nyingine yoyote ile atakayoifanya Muumini.Katika kuonyesha ubora wa amali hii ya jihad, Allah (s.w) ameifananisha na biashara yenye kuleta faida kubwa isiyo na mfano wake kwa maisha ya hapa duniani na huko akhera kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا هَلْ أَدُلُّكُمْ عَلَىٰ تِجَارَةٍ تُنجِيكُم مِّنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿١٠﴾ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَتُجَاهِدُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ بِأَمْوَالِكُمْ وَأَنفُسِكُمْ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿١١﴾ يَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَيُدْخِلْكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ وَمَسَاكِنَ طَيِّبَةً فِي جَنَّاتِ عَدْنٍ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ ﴿١٢﴾ وَأُخْرَىٰ تُحِبُّونَهَا نَصْرٌ مِّنَ اللَّـهِ وَفَتْحٌ قَرِيبٌ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ﴾

"Enyi mlioamini! Je! Nikujulisheni biashara itakayokuokoeni na adhabu iumizayo? (Biashara yenyewe ni hii): Muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na piganieni dini ya Mwenyezi Mungu kwa mali zenu na nafsi zenu, haya ni bora kwenu; ikiwa mnajua.(Mkifanya haya) .atakusameheni dhambi zenu na atakuingizeni katika mabustani yapitayo mito mbele yake na (atakupeni) maskani mazuri mazuri katika Bustani za milele, huku ndiko kufuzu kukubwa. Na (atakupeni) kingine mnachokipenda: Nayo ni nusura itokayo kwa Mwenyezi Mungu na ushindi ulio karibu! Na wapashe habari njema waumini" (61:10-13)

﴿ إِنَّ اللَّـهَ اشْتَرَىٰ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ أَنفُسَهُمْ وَأَمْوَالَهُم بِأَنَّ لَهُمُ الْجَنَّةَ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَيَقْتُلُونَ وَيُقْتَلُونَ وَعْدًا عَلَيْهِ حَقًّا فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ وَالْقُرْآنِ وَمَنْ أَوْفَىٰ بِعَهْدِهِ مِنَ اللَّـهِ فَاسْتَبْشِرُوا بِبَيْعِكُمُ الَّذِي بَايَعْتُم بِهِ وَذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ﴾

Mwenyezi Mungu amenunua kwa waumini nafsi zao na mali zao, ili na yeye awalipe Pepo. Wanapigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, wanaua na wanauawa. Hii ndiyo ahadi aliyojilazimisha (Mwenyezi Mungu) katika Taurati na Injili na Qur-ani. Na ni nani atekelezaye zaidi ahadi yake kuliko Mwenyezi Mungu? Basi furahini kwa biashara yenu mliyofanya naye. Na huko ndiko kufuzu kukubwa.(9:111).

Kutokana na aya hizi tunajifunza kuwa kazi ya kupigania Dini ya Mwenyezi Mungu (Jihadi) imefanywa ni biashara mja anayofanya na Mola wake. Mtaji wa biashara hii ni kutoa mali na nafsi (nguvu kazi na ikibidi kuitoa roho muhanga). Faida ya biashara hii ni:

1. Kuokolewa na adhabu iumizayo hapa duniani chini ya Uongozi wa Twaaghut na huko akhera.

2. Kusamehewa dhambi.

3. Kuingizwa peponi na kufaidika na starehe zake.

4. Kupata nusra ya Allah (s.w) hapa ulimwenguni.

5. Kumshinda adui na kuweza kusimamisha dini ya Allah (s.w) katika jamii na kuleta amani ya kweli ya kudumu.

Umuhimu wa Kusimamisha Uislamu Katika Jamii

﴿إِنَّ الدِّينَ عِندَ اللَّـهِ الْإِسْلَامُ﴾

"Bila shaka dini (ya haki) mbele ya Allah ni Uislamu" (3:19)

﴿هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ﴾

"Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa Uongofu na dini ya haki ili aijaalie kushinda dini zote ijapokuwa washirikina watachukia." (61:9)

Imekuwa muhimu kuutawalisha Uislamu katika jamii kwa sababu kubwa mbili zifuatazo:

Kwanza : bila ya Uislamu kushika hatamu katika kuendesha shughuli zote za maisha ya jamii katika siasa, uchumi, utamaduni na katika kila kipengele kingine muhimu cha maisha ya jamii; Waislamu kamwe hawataweza kumuabudu Mola wao katika kila kipengele cha maisha. Waumini wa kweli ni wale wanaoufuata Uislamu wote katika kila jambo la kibinafsi au la kijamii wanalolifanya katika kuendesha maisha yao ya kila siku. Aidha waumini wa kweli huishi kwa kuzingatia wito wa Allah (s.w) ufuatao:

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ادْخُلُوا فِي السِّلْمِ كَافَّةً وَلَا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ﴾

"Enyi mlioamini! Ingieni katika hukumu zote za Uislamu, wala msifuate nyayo za shetani kwa hakika yeye kweni ni adui dhahiri" (2:208)

﴿وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا﴾

"Haiwi kwa mwanamume aliyeamini wala kwa mwanamke aliyeamini, Mwenyezi Mungu na mtume wake wanapokata shauri, wawe na hiari katika shauri lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hakika amepotea upotofu (upotevu) ulio wazi (kabisa)." (33:36)

Kwa mazingatio ya aya hizi, waislamu wanalazimika kufanya jitihada za makusudi, kwa kutumia mali na nafsi zao, kuhakikisha kuwa sheria za Kiislamu zinatumika katika kila kipengele cha maisha ya jamii ili kuweka mazingira ya kufuata hukumu zote za Uislamu katika siasa, uchumi, utamaduni; na kadhalika.

Tukumbuke kuwa, iwapo Waislamu tutabweteka na kuridhika kuishi maisha ya "mseto" ya kumuabudu Allah (s.w) kwa kuswali; kutoa Zaka, Kufunga, n.k. na kumuasi Allah (s.w) kwa kuridhia kufuata mfumo haramu wa siasa, uchumi; utamaduni,na kadhalika, tutastahiki adhabu kubwa ya kuwa dhalili katika jamii na kuwa na marejeo mabaya huko akhera kama tunavyokumbushwa:

﴿أَفَتُؤْمِنُونَ بِبَعْضِ الْكِتَابِ وَتَكْفُرُونَ بِبَعْضٍ فَمَا جَزَاءُ مَن يَفْعَلُ ذَٰلِكَ مِنكُمْ إِلَّا خِزْيٌ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يُرَدُّونَ إِلَىٰ أَشَدِّ الْعَذَابِ وَمَا اللَّـهُ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ﴾

"...Je! Mnaamini baadhi ya kitabu na kukataa baadhi (yake)? Basi hakuna malipo kwa mwenye kufanya haya katika nyinyi ila fedheha katika maisha ya dunia; na siku ya kiyama watapelekwa katika adhabu kali. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na yale mnayoyatenda." (2:85)

Pili : bila ya Uislam kushika hatamu katika jamii,ni muhali kupatikana furaha na amani ya kweli. Waislamu wanawajibu wa kuamrisha mema na kukataza maovu ili kuhakikisha kuwa panakuwa na maendeleo ya kweli katika jamii, kila mtu anapata haki zake na panakuwa na mazingira ya amani kwa ujumla. Allah (s.w) amewaleta Mitume na Vitabu ili kuwaongoza watu wasimamishe uadilifu katika jamii kama tunavyojifunza katika aya ifuatayo:

﴿لَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا بِالْبَيِّنَاتِ وَأَنزَلْنَا مَعَهُمُ الْكِتَابَ وَالْمِيزَانَ لِيَقُومَ النَّاسُ بِالْقِسْطِ﴾

"Kwa hakika tuliwapeleka Mitume wetu kwa dalili wazi wazi na Tukaviteremsha vitabu na hukumu pamoja nao, ili watu wasimamie uadilifu..." (57:25)

Kwa mujibu wa aya hii tunajifunza kuwa ni muhali kupatikana furaha na amani ya kweli katika jamii inayoongozwa kinyume na muongozo wa Mitume na Vitabu vya Mwenyezi Mungu, ambamo ndimo Uadilifu unamopatikana. Furaha na amani ya kweli katika jamii hupatikana tu pale maongozi ya jamii hiyo yatakapokwenda sambamba na maongozi ya Allah (s.w) kama tunavyojifunza katika aya ifuatayo:

﴿اللَّـهُ وَلِيُّ الَّذِينَ آمَنُوا يُخْرِجُهُم مِّنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ وَالَّذِينَ كَفَرُوا أَوْلِيَاؤُهُمُ الطَّاغُوتُ يُخْرِجُونَهُم مِّنَ النُّورِ إِلَى الظُّلُمَاتِ أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ﴾

"Mwenyezi Mungu ni mlinzi (kiongozi) wa wale walioamini.Huwatoa katika giza na kuwaingiza katika nuru.Lakini waliokufuru, walinzi (viongozi) wao ni matwaghut. Huwatoa katika nuru na kuwaingiza katika giza. Hao ndio watu wa motoni, humo watakaa milele" (2:257)

Katika aya hii Giza, huashiria maisha yaliyogubikwa na dhuluma za kila aina, maisha ya vita na mauaji, maisha ya ubabe, maisha ya uonevu, udhalilishaji na ukandamizaji wa kila namna, maisha ya samaki wakubwa kuwameza wadogo, maisha ya ujanja ujanja na utapeli, maisha ya maangamizi ya kila namna. Nuru katika aya hii inaashiria maisha ya uadilifu, upendo na kujaliana maisha ya kila mtu kupata haki yake inayomstahiki, maisha ya kuhurumiana na kusaidiana, maisha ya furaha na amani.

Matwaghut, katika Qur-an ni viongozi wa jamii wanaoongoza watu kinyume na mwongozo wa Mwenyezi Mungu kama ulivyobainishwa na Mitume wake na Vitabu vyake. Wanaoongoza kwa kuchupa mipaka na taratibu za Allah (s.w). Wanawaongoza watu kwa sheria walizotunga binaadamu zinazopingana na sheria za Allah (s.w).

Kutokana na aya hii tunajifunza kuwa; ambapo sera ya Allah (s.w) ni kuwatoa watu kwenye giza (maisha ya dhiki na mashaka) na kuwapeleka kwenye nuru (maisha ya furaha na amani) sera ya matwaghut ni kuwatoa kwenye nuru na kuwaingiza katika Giza. Hivyo Waislamu hawanabudi kushika hatamu ya maongozi ya jamii,ili kuinusuru jamii isiangamizwe na matwaghuti na kutumbukizwa kwenye giza.

ZOEZI - 4

1. Nukuu aya ya Qur-an au tafsiri yake inayotufahamisha lengo la kuletwa binaadamu hapa ulimwenguni.

2. "(Wakumbushe) wakati Mola wako alipowaambia Malaika, "Mimi nitaleta khalifa katika ardhi..." (2:30)

Kwa mnasaba wa aya hii khalifa ni...............................................

3. "Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na kufanya vitendo vizuri kuwa atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyowafanya makhalifa wale waliokuweko kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia dini yao aliyowapendelea na atawabadilishia amani baada ya hofu yao. Wawe wananiabudu, hawanishirikishi na chochote..." (24:55) Kutokana na aya hii tunajifunza yafuatayo:

(i).........................................................................................

(ii)........................................................................................

(iii)......................................................................................

(iv)......................................................................................

4. Waumini wa kweli katika jamii wanadhima ya kufanya yafuatayo:

(i)........................................................................................

(ii)......................................................................................

(iii).....................................................................................

5. Kwanini Waislamu wanalazimika kuusimamisha na kuuhami Uislamu katika jamii?

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini