MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU 0%

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU Mwandishi:
Kundi: Vitabu mbali mbali

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

Mwandishi: NDUGU ZETU WA KISUNNI
Kundi:

Matembeleo: 44541
Pakua: 3490

Maelezo zaidi:

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 22 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 44541 / Pakua: 3490
Kiwango Kiwango Kiwango
MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

Mwandishi:
Swahili

3

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

SURA YA TATU

IMANI YA KIISLAMU

MAANA YA IMANI IMANI

Imani ni neno la Kiarabu lenye maana ya kuwa na yakini au kuwa na uhakika moyoni juu ya kuwepo kitu au jambo fulani lisiloonekana machoni lakini kuna dalili za kuthibisha kuwepo kwake. Hivyo ili mtu awe na imani juu ya jambo lolote lile asiloweza kuliona, hanabudi kuwa na ujuzi wa kina utakaompa hoja au dalili za kutosha zitakazomkinaisha moyoni juu ya kuwepo jambo hilo.

NANI MUUMINI?

Imani ni kitu cha moyoni kisichoonekana lakini dalili za Muumini huonekana kwenye matendo. Katika Uislamu mtu hatakuwa Muumini kwa kudai tu bali uumini wake utaonekana katika matendo yake. Katika Qur-an tunafahamishwa kuwa:

﴿وَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ آمَنَّا بِاللَّـهِ وَبِالْيَوْمِ الْآخِرِ وَمَا هُم بِمُؤْمِنِينَ﴾

"Na katika watu wako wasemao, 'tumemuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na hali ya kuwa wao si wenye kuamini."( 2:8).

Si wenye kuamini kwa sababu hawajaingiza imani yao katika matendo, bali wamebakia kwenye kudai tu kuwa wao ni waumini pengine kwa kujiita majina au kuchagua kufanya vitendo fulani fulani tu.Muumini wa kweli ni yule atakayethibitisha imani yake katika mwenendo na matendo yake ya kila siku.

﴿إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ ﴿٢﴾ الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿٣﴾ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا لَّهُمْ دَرَجَاتٌ عِندَ رَبِّهِمْ وَمَغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ﴾

"Hakika wanaoamini kweli ni wale ambao anapotajwa Allah nyoyo zao hujaa hofu, na wanaposomewa aya zake huwazidishia imani na wanamtegemea Mola wao tu basi).Ambao husimamisha swala na wanatoa katika yale tuliyowapa.Hao ndio wanaoamini kweli kweli, wao wana vyeo (vikubwa) kwa Mola wao, na msamaha na riziki bora kabisa". (8:2-4).

﴿إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ ثُمَّ لَمْ يَرْتَابُوا وَجَاهَدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ﴾

"Wenye kuamini kweli kweli ni wale wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake kisha wakawa si wenye shaka na wanaopigania dini ya Allah kwa mali zao na nafsi zao.Hao ndio wenye kuamini kweli kweli" (49:15).

Kutokana na aya hizi tunajifunza kuwa waumini wa kweli ni wale wenye sifa zifuatazo:

(i) Wana yakini kuwa Allah (s.w) yupo Waumini wa kweli huwa na yakini nyoyoni mwao juu ya kuwepo Allah (s.w) na Mtume wake. Yaani wanashuhudia kwa dhati nyoyoni mwao kuwa Allah (s.w) ni Mola wao pekee na Muhammad(s.a.w.w) ni Mtume wake wa mwisho na katika matendo yao yote huishi kwa kufuata mwongozo wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na daima hukumbuka msisitizo wa aya ifuatazo:

﴿وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا﴾

"Haiwi kwa mwanamume aliyeamini wala kwa mwanamke aliyeamini,Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapokata shauri wawe na hiari katika shauri lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hakika amepotea upotofu ulio wazi (kabisa)." (33:36)

(ii) Humcha Allah (s.w) kwa kutekeleza amri zake Anapotajwa Mwenyezi Mungu au wanapokumbushwa juu ya maamrisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu, nyoyo zao hunyenyekea na kufuata kama walivyokumbushwa. Hufanya hivyo kwa kuhofu ghadhabu za Mwenyezi Mungu na kutarajia radhi zake.

(iii) Huongezeka imani yao kwa kusoma na kufuata Quran Wanaposoma aya za Mwenyezi Mungu huwazidishia imani. Kwa maana nyingine, waumini wa kweli hufuata mwongozo wa Allah (s.w) katika kuendesha maisha yao ya kila siku. Hawako tayari kufanya jambo lolote kinyume na mwongozo wa Allah (s.w).

(iv) Humtegemea Mwenyezi Mungu peke yake Hawamuogopi au kumtegemea yeyote kinyume na Mwenyezi Mungu. Wanamsimamo thabiti na hawayumbishwi na yeyote katika kutekeleza wajibu wao kwa Mola wao. Wana yakini kuwa aliyenusuriwa na Allah (s.w) hakuna wa kumdhuru na aliyeandikiwa kupata dhara na Allah (s.w) hakuna wa kumnusuru.

(v) Husimamisha swala Husimamisha swala katika maisha yao yote. Huswali swala tano kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa, na kwa hiyo hufikia lengo la swala kwa kutojihusisha kabisa na mambo machafu na maovu. Na zaidi huamrisha mema na kukataza maovu katika jamii.

(vi) Husaidia wenye matatizo katika jamii Huwa wepesi wa kutoa msaada kwa hali na mali kwa wanaadamu wenziwe wanaohitajia msaada.

(vii) Hufanya biashara na Allah (s.w) Wanafanya jitihada za makusudi kwa kutumia mali zao na kujitoa muhanga nafsi zao ili kuhakikisha kuwa dini ya Allah inasimama katika jamii. Yaani wanajitahidi kwa jitihada zao zote ili kuzifanya sharia za Allah (s.w) ziwe ndizo zinazotawala harakati zote za maisha ya jamii.

Pia sifa za Waumini zinabainishwa katika Suratul- Muuminuun kama aya zifuatavyo:

﴿قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١﴾ الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ ﴿٢﴾ وَالَّذِينَ هُمْ عَنِ اللَّغْوِ مُعْرِضُونَ ﴿٣﴾ وَالَّذِينَ هُمْ لِلزَّكَاةِ فَاعِلُونَ ﴿٤﴾ وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ ﴿٥﴾ إِلَّا عَلَىٰ أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ ﴿٦﴾ فَمَنِ ابْتَغَىٰ وَرَاءَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْعَادُونَ ﴿٧﴾ وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ ﴿٨﴾ وَالَّذِينَ هُمْ عَلَىٰ صَلَوَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ ﴿٩﴾ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ ﴿١٠﴾ الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ﴾

Hakika wamefuzu Waumini ambao katika swala zao huwa wanyenyekevu.Na ambao hujiepusha na Lagh-wi (mambo ya upuuzi). Na ambao Zaka wanaitekeleza.Na ambao tupu zao wanazihifadhi isipokuwa kwa wake zao au kwa (wanawake) wale iliyomiliki mikono yao ya kuume.Basi hao ndio wasiolaumiwa.Lakini anayetaka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka. Na ambao amana zao na ahadi zao wanaziangalia.Na ambao swala zao wanazihifadhi.Hao ndio warithi.Ambao watarithi Firdaus (Pepo ya daraja ya juu) wakae humo milele. (23:1-11)

Kutokana na aya hizi tunajifunza kuwa waumini wa kweli waliofuzu na watakaostahiki kupata pepo ya Firdaus, ya daraja ya juu kabisa ni wale wanaojipamba na sifa zifuatazo:

(viii) Wenye khushui katika swala Waumini wa kweli waliofuzu huwa na khushui (unyenyekevu) katika swala. Yaani huswali kwa kutulizana kimwili, kimoyo,kiroho na kifikra, huku wakizingatia yale wayasemayo mbele ya Mola wao wakiwa na yakini kuwa anawaona na anawasikia.

(ix) Wenye kuhifadhi swala Waumini wa kweli waliofuzu huhifadhi swala kwa kutekeleza kwa ukamilifu shuruti zote za swala nguzo zote za swala na huswali kama alivyoswali Mtume(s.a.w.w) na hudumu na swala katika maisha yao yote: Rejea Qur-an (70:23).

Zingatio :

Swala husimama kwa kuhifadhiwa na kuswaliwa kwa khushui na kudumu na swala katika maisha yote.

(x) Wenye kuepuka lagh-wi Waumini wa kweli waliofuzu hujiepusha na Lagh-wi. Laghwi ni mambo ya upuuzi yanayomsahaulisha mtu kumkumbuka Mola wake, yanayosababisha ugomvi au bughudha baina ya watu na yanayomsahaulisha mtu kusimamisha swala: Rejea Qur-an (5:91).

Mahala ambapo Allah (s.w) hakumbukwi, shetani huchukua nafasi. Michezo yote ni lagh-wi, isipokuwa ile tu inayochezwa kwa kuchunga mipaka yote ya Allah (s.w) kwa lengo la kukuza ukakamavu na siha.

(xi) Hutoa Zakat na Sadakat Waumini wa kweli waliofuzu hutoa Zakat wakiwa na mali na hutoa misaada na huduma waziwezazo kwa wanaadamu wenziwe kwa kadiri ya haja ilivyojitokeza.Asiyejali kuwasaidia binaadamu wenziwe, huku ana uwezo si Muumini. Rejea Qur-an (107:1-7).

(xii) Huepuka zinaa na tabia za kizinifu Waumini wa kweli waliofuzu hujihifadhi na zinaa au hujiepusha kufanya jimai nje ya mipaka aliyoiweka Allah (s.w). Hatua ya kwanza ya kujilinda na zinaa ni kujiepusha na vishawishi vyote vinavyokurubisha watu kwenye zinaa. Muumini wa kweli hutekeleza pasina kusita ile amri ya Allah (s.w) ya katazo kuwa:

﴿وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَىٰ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا﴾

Wala usiikaribie zinaa; kwa hakika huo ni uchafu na ni njia mbaya kabisa (17:32)

(xiii) Huwa muaminifu Waumini wa kweli waliofuzu huchunga amana. Hutunza amana aliyopewa na kuirejesha au kuitumia kwa mujibu wa maelekezo ya mwenyewe. Amana kuu aliyopewa mwanaadamu na Mola wake ni kule kufadhilishwa kwake kuliko viumbe vingine vyote ili asimamishe Ukhalifa (utawala wa Allah) katika ardhi kama tunavyokumbushwa katika Qur-an:

﴿إِنَّا عَرَضْنَا الْأَمَانَةَ عَلَى السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَالْجِبَالِ فَأَبَيْنَ أَن يَحْمِلْنَهَا وَأَشْفَقْنَ مِنْهَا وَحَمَلَهَا الْإِنسَانُ إِنَّهُ كَانَ ظَلُومًا جَهُولًا﴾

"Kwa yakini Sisi Tulidhihirisha amana kwa mbingu, ardhi na milima,vikakataa kuichukua na vikaiogopa,lakini mwanaadamu aliichukua. Bila shaka yeye ni dhalimu mkubwa, mjinga sana" (33:72)

(xiv) Wenye kutekeleza ahadi Hutekeleza ahadi zao wanapoahidiana na wanaadamu wenziwao maadamu ni katika mipaka ya Allah (s.w). Ahadi kubwa wanayotoa Waislamu mbele ya Allah (s.w) ni shahada; pale wanapo ahidi kuwa hawatamshirikisha Allah (s.w) na chochote na kwamba wataishi maisha yao yote kwa kufuata mwongozo wa Allah (s.w) kupitia kwa Mtume wake, Muhammad(s.a.w.w) . Rejea (6: 162 -163) Katika Suratul-Fur-qaan sifa za Waumini zinabainishwa tena kama ifuatavyo:

﴿وَعِبَادُ الرَّحْمَـٰنِ الَّذِينَ يَمْشُونَ عَلَى الْأَرْضِ هَوْنًا وَإِذَا خَاطَبَهُمُ الْجَاهِلُونَ قَالُوا سَلَامًا ﴿٦٣﴾ وَالَّذِينَ يَبِيتُونَ لِرَبِّهِمْ سُجَّدًا وَقِيَامًا ﴿٦٤﴾ وَالَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا اصْرِفْ عَنَّا عَذَابَ جَهَنَّمَ إِنَّ عَذَابَهَا كَانَ غَرَامًا ﴿٦٥﴾ إِنَّهَا سَاءَتْ مُسْتَقَرًّا وَمُقَامًا ﴿٦٦﴾ وَالَّذِينَ إِذَا أَنفَقُوا لَمْ يُسْرِفُوا وَلَمْ يَقْتُرُوا وَكَانَ بَيْنَ ذَٰلِكَ قَوَامًاوَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ يَلْقَ أَثَامًا ﴿٦٨﴾ يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا ﴿٦٩﴾ إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ يُبَدِّلُ اللَّـهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا﴿٧٠﴾ وَمَن تَابَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَإِنَّهُ يَتُوبُ إِلَى اللَّـهِ مَتَابًا ﴿٧١﴾ وَالَّذِينَ لَا يَشْهَدُونَ الزُّورَ وَإِذَا مَرُّوا بِاللَّغْوِ مَرُّوا كِرَامًا ﴿٧٢﴾ وَالَّذِينَ إِذَا ذُكِّرُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ لَمْ يَخِرُّوا عَلَيْهَا صُمًّا وَعُمْيَانًا ﴿٧٣﴾ وَالَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا ﴿٧٤﴾ أُولَـٰئِكَ يُجْزَوْنَ الْغُرْفَةَ بِمَا صَبَرُوا وَيُلَقَّوْنَ فِيهَا تَحِيَّةً وَسَلَامًا ﴿٧٥﴾ خَالِدِينَ فِيهَا حَسُنَتْ مُسْتَقَرًّا وَمُقَامًا﴾

"Na waja wa Rahmaan; Ni wale wanaokwenda ulimwenguni kwa unyenyekevu; na wajinga wakisema nao (maneno mabaya) huwajibu (maneno ya) salama. Na wale wanaopitisha baadhi ya saa za usiku kwa ajili ya Mola wao kwa kusujudu na kusimama. Na wale wanaosema:"Mola wetu! Tuondolee adhabu ya Jahannam, bila shaka adhabu yake ni yenye kuendelea, Hakika hiyo (Jahannamu) ni kituo kibaya na mahali (pabaya kabisa) pa kukaa".Na wale ambao wanapotumia hawatumii kwa fujo wala hawafanyi ubakhili, bali wanakuwa katikati baina ya hayo .Na wale wasiomuomba mungu mwingine pamoja na Allah, wala hawaui nafsi aliyoiharamisha Allah ila kwa haki, wala hawazini; na atakayefanya hayo atapata madhara (papa hapa ulimwenguni). Na atazidishiwa adhabu siku ya Kiyama na atakaa humo kwa kufedheheka milele. Ila yule atakayetubia na kuamini na kufanya vitendo vizuri, basi hao ndio Mwenyezi Mungu atawabadilishia maovu yao kuwa mema; na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa kurehemu.Na aliyetubia na kufanya wema, basi kwa hakika yeye anatubu kweli kweli kwa Mwenyezi Mungu. Na wale ambao hawashuhudii shahada za uwongo, na wanapopita penye upuuzi, hupita kwa hishima (yao). Na wale ambao wanapokumbushwa aya za Mola wao hawaziangukii kwa uziwi na upofu. Na wale wanaosema: "Mola wetu! Tupe katika wake zetu na wototo wetu yaburudishayo macho (yetu) (nyoyo zetu), na Utujaalie kuwa waongozi kwa wamchao (Mungu). Hao ndio watakaolipwa ghorofa (za Peponi) kwa kuwa walisubiri, na watakuta humo hishima na amani. Wakae humo milele; kituo kizuri na mahali pazuri (kabisa pa kukaa.) (25:63-76).

Kutokana na aya hizi tunajifunza kuwa sifa za Waumini ambao hapa wameitwa "Waja wa Rahman" ni pamoja na:

(xv) Kuishi na watu kwa wema Waumini wa kweli huishi na watu wema kwa kuwathamini na kuwaheshimu; kujizuia na kuwafanyia watu kibri, kujizuia na kujikweza na kujitukuza mbele ya wengine, kujizuia na kuwadhalilisha watu na kuwavunjia heshima.

(xvi) Huepuka ugomvi na mabishano Waumini wa kweli huepuka kabisa tabia ya ugomvi na mabishano. Waumini hufahamu fika kuwa kwenye ugomvi na mabishano shetani huwepo na huchochea faraka baina ya ndugu. (xvii) Hudumu katika kuswali Tahajjud Kuamka usiku na kuswali swala ya "Tahajjud"(kisimamo cha usiku) kwa ajili ya kutafuta radhi za Allah (s.w) na Rehema zake. Swala hii huswaliwa usiku wa manane hususan katika theluthi ya mwisho ya usiku inayokaribiana na Al-fajiri.

(xviii) Huogopa adhabu ya Allah(s.w) Waumini wa kweli huogopa adhabu ya Allah (s.w) aliyowaandalia watu waovu huko akhera kwa kujitahidi kutenda mema na kujiepusha na maovu na kila mara kuomba:

﴿ وَالَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا اصْرِفْ عَنَّا عَذَابَ جَهَنَّمَ إِنَّ عَذَابَهَا كَانَ غَرَامًا﴿٦٥﴾ إِنَّهَا سَاءَتْ مُسْتَقَرًّا وَمُقَامًا﴾

"Mola wetu! Tuondolee adhabu ya Jahannam, bila shaka adhabu yake ni yenye kuendelea.Hakika hiyo (Jahannamu) ni kituo kibaya na mahali (pabaya kabisa) pa kukaa"(25:65-66).

(xix) Hutumia neema kwa insafu Waumini wa kweli hutumia neema walizopewa na Allah kwa insafu. Hawafanyi ubadhirifu au israfu wa neema kama vile kutumia vibaya mali, wakati, vipaji na ujuzi. Waumini daima huzingatia kuwa Allah hawapendi waja wanaofuja neema alizowatunukia. Mubadhirina ni watu wanaofuja neema walizotunukiwa na Allah (s.w). Wasiotumia neema kwa insafu, ni wafuasi wa shetani. Quran inasema:

﴿وَآتِ ذَا الْقُرْبَىٰ حَقَّهُ وَالْمِسْكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ وَلَا تُبَذِّرْ تَبْذِيرًا ﴿٢٦﴾ إِنَّ الْمُبَذِّرِينَ كَانُوا إِخْوَانَ الشَّيَاطِينِ وَكَانَ الشَّيْطَانُ لِرَبِّهِ كَفُورًا﴾

"Na wape jamaa wa karibu haki zao,na mayatima (vilevile) na masikini, wala usifanye ubadhirifu. Hakika wafanyao ubadhirifu ni marafiki wa shetani, na shetani ni mwenye kumkufuru Mola wake" (17:26-27).

(xx) Hawamshirikishi Allah (s.w) Waumini wa kweli hawamshirikishi Allah(s.w). Hujiepusha na aina zote za shirk- shirk katika dhati, shirk katika sifa, shirk katika hukumu na shirk katika mamlaka ya Allah(sw). Kufanya shirk ni dhambi kubwa ya daraja la kwanza. Quran inaonya na kutahadharisha kuwa:

﴿إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا﴾

"Hakika Mwenyezi Mungu hasamehi (dhambi ya) kushirikishwa na kitu na husame yasiyokuwa haya kwa amtakaye. Na anayemshirikisha Allah bila shaka amebuni dhambi kubwa" (4:48)

(xxi) Hulinda na kutetea haki uhai wa nafsi Waumini wa kweli hulinda na kutetea haki ya uhai wa kila nafsi yenye haki ya kuishi. Hivyo, kwa namna yeyote ile ya kisheria, hujitahidi kujiepusha na ushiriki wa kusababisha au kufanya mauwaji ya nafsi ambayo kwa mujibu wa mwongozo wa Allah hustahiki kuishi. Ulinzi na utetezi huu wa haki ya uhai wa nafsi unatokana na mwongozo wa Allah katika Quran kuwa:

﴿مَن قَتَلَ نَفْسًا بِغَيْرِ نَفْسٍ أَوْ فَسَادٍ فِي الْأَرْضِ فَكَأَنَّمَا قَتَلَ النَّاسَ جَمِيعًا وَمَنْ أَحْيَاهَا فَكَأَنَّمَا أَحْيَا النَّاسَ جَمِيعًا ﴾

Mwenye kuiuwa nafsi pasina nafsi (hiyo iliyouliwa kuuwa) au kufanya fisadi katika ardhi,huyo itakuwa kana kwamba ameuwa watu wote. Na atakayeilinda nafsi hiyo, huyo atakuwa kana kwamba amelinda uhai wa watu wote (5:32).

(xxii) Hawafanyi uzinzi Waumini wa kweli hawaikaribii zinaa wala kufanya uzinifu. Na zaidi hawashawishi wala kushiriki kwa namna yoyote ile katika mambo yanayosababisha zinaa kufanyika.

﴿وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَىٰ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا﴾

"Wala usikaribie zinaa.Hakika hiyo ni uchafu (mkubwa) na ni njia mbaya (kabisa)." (17:32).

(xxiii) Husema kweli daima Waumini wa kweli husema kweli daima. Hawatowi ushahidi wa uongo au kutetea batili. Wanapowajibika kutoa ushahidi juu ya jambo, husema ukweli hata kama ni dhidi ya nafsi zao wenyewe au watu wao wa karibu.(rej 4:135, 5:8).

(xxiv) Hawavutiwi na mambo ya kipuuzi Waumini wa kweli ni wale ambao hawavutiwi na mambo ya kipuuzi ambayo wafuasi wa ibilisi huyatumia katika kuwavuta watu kwa lengo la kuwapumbaza na kuwateka akili zao. Muumini huwa hana muda wa kupoteza au fursa ya kuikabidhi akili yake kwa twaghuti aichezee. Hivyo, kwenye mambo ya kipuuzi waumini hupita haraka kwa heshima zao, na ikibidi kuweka jambo m-badala lenye maana na manufaa kwa jamii.

(xxv) Humwitikia Allah(s.w) anapowaita Waumini wa kweli humwitikia Allah (s.w) anapowaita kwa makatazo na maamrisho yake katika Quran. Hivyo hutii kwa unyenyekevu maagizo ya Allah (s.w) kila wanapokumbushwa kwa kusomewa au kusoma wenyewe aya za Kitabu cha Allah (s.w). na Allah (s.w) ananadi katika Quran kuwa:

﴿وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ﴾

Na waja wangu wanapokuuliza kuhusu mimi, basi (waambie) hakika Mimi nipo karibu najibu maombi ya mwombaji pindi anaponiomba. Basi na waniitike na waniamini Mimi ili wapate kuongoka (2:186).

(xxvi) Hujenga familia za kiislamu Waumini hujitahidi kujenga familia za kiislamu kwa kumuongoza mke na kuwalea watoto na wale wote walio chini ya mamlaka yake katika mipaka ya Ucha-Mungu kwa kuwaamrisha kutenda mema na kuwakataza maovu. Pamoja na jitihada hiyo huomba msaada wa Allah kwa kuleta dua ifuatayo:

﴿وَالَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا﴾

"Mola wetu! Tupe katika wake zetu na wototo wetu yaburudishayo macho (yetu) (nyoyo zetu), na Utujaalie kuwa Viongozi kwa wamchao (Mungu). (25:74)

Kwa ujumla waumini wa kweli ni wale wanaojipamba na tabia njema kama iliyoelekezwa katika Qur-an na Sunnah.

ZOEZI

3: 1. Imani ni.................................................................................

2. Pamoja na kudai kwao kuwa ni waumini Allah (s.w) anawakatalia.

"Na katika watu wako wasemao, "Tumemuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na hali ya kuwa wao si wenye kuamini ..." (2:8)

Allah (s.w) anawakatalia kwa sababu.................................................

3. Orodhesha sifa za waumini wa kweli kama zilivyoainishwa katika Qur-an (8:2-4) na (49:15).

4. Orodhesha sifa za waumini kama zilivyo ainishwa katika aya zifuatazo:

(a) Suratul-Muuminuun (23:1-11)

(b) Suratul-Furqaan (25:63-76)

5. Imani ya Kiislamu imejengwa juu ya nguzo sita. Zitaje zote. Kwa mpangilio.