MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU 0%

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU Mwandishi:
Kundi: Vitabu mbali mbali

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

Mwandishi: NDUGU ZETU WA KISUNNI
Kundi:

Matembeleo: 44529
Pakua: 3487

Maelezo zaidi:

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 22 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 44529 / Pakua: 3487
Kiwango Kiwango Kiwango
MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

Mwandishi:
Swahili

4

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

NGUZO ZA IMANI

Tunajifunza katika Qur-an na hadithi sahihi kuwa; Imani ya Kiislamu imejengwa juu ya nguzo sita zifuatazo:

1 Kumuamini Allah (s.w)

2 Kuamini Malaika wake

3 Kuamini Vitabu vyake

4 Kuamini Mitume wake

5 Kuamini Siku ya mwisho

6 Kuamini Qadar yake

Hawi Muumini wa Kiislam yule ambaye amekanusha angalau moja ya nguzo hizi kama inavyobainika katika Qur-an:

﴿وَمَن يَكْفُرْ بِاللَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا﴾

"... Na mwenye kumkanusha Allah (s.w) na Malaika wake na Vitabu vyake na Mitume wake na siku ya mwisho. basi bila shaka amepotea upotofu ulio mbali (kabisa)" (4:136)

Mtu hatakuwa Muumini kwa kutamka tu hizi nguzo sita, bali pale atakapozijua kwa undani na kuendesha maisha yake yote kwa misingi ya nguzo hizi.

Tunazifahamu nguzo hizi sita kutokana na Hadith ya Mtume (s.a.w) iliyosimuliwa na Umar (r.a) kama ifuatavyo: Siku moja tulipokuwa tumeketi pamoja na Mtume(s.a.w.w) alitutokea mtu mmoja ambaye nguo zake zilikuwa nyeupe kama theluji na nywele zake nyeusi sana, hakuwa na dalili zozote za msafiri, ingawa alikuwa mgeni kwetu sote. Halafu alikaa mbele ya Mtume(s.a.w.w) hali magoti yake yakikabiliana na yale ya Mtume na akaweka mikono yake katika mapaja ya Mtume na akasema:"Ewe Muhammad nifahamishe juu ya Uislamu" na Mtume akasema ;

"Ni kushuhudia ya kuwa hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allah, Kusimamisha swalaa, kutoa Zakat, Kufunga Mwezi wa Ramadhani, Kuhiji Makkat kwa mwenye kuweza"

Halafu yule mgeni akasema "umesema kweli".

Tukastaajabu kwa nini aliuliza halafu akasadikisha. Halafu akasema; "Nifahamishe juu ya Iman".

Mtume akasema :

"Ni kumuamini Mwenyezimungu na, Malaika wake , Vitabu vyake, Mitume wake, Siku ya Mwisho na Qadar, Kheri na shari yake . Kisha akasema nifahamishe juu ya Ihsaan" Akasema"Ni Kumuabudu Allah kama kwamba unamuona, ikiwa wewe humuoni yeye anakuona" Halafu akasema nifahamishe juu ya Kiyama" Akasema:"Hajui mwenye kuulizwa juu ya hilo zaidi ya mwenye kuuliza. Akasema: Nifahamishe dalili zake. Mtume akasema: "sNi wakati ambapo mjakazi atamzaa bibi yake, na utakapowaona wachungaji masikini wanaposhindana kujenga maghorofa. "Yule mgeni alipoondoka, Mtume alikaa kimya kwa muda kisha akasema: "eweUmar, unamfahamu muulizaji?' Sote tukamjibu kuwa Allah na Mtume wake wanajua zaidi. Mtume akasema"Huyo ni Jibriil amekuja kuwafundisheni dini yenu" (MUSLIM)

KUMUAMINI ALLAH ( S.W )

Nafasi ya akili katika kumtambua Allah (s.w) Imani ya kweli juu ya Allah (s.w) itathibitika moyoni baada ya kumjua vyema Allah (s.w) na sifa zake zote tukufu. Allah (s.w) hatumuoni kwa macho bali tunamfahamu kwa akili zetu katika kuchunguza dalili mbali mbali zilizotuzunguka. Tunavyojifunza katika Qur-an, matumizi ya kwanza ya akili tulizotunukiwa ni kuyakinisha kuwepo kwa Allah (s.w) na sifa zake. Msisitizo wa matumizi ya akili na fikra zetu katika kazi hii ya kumjua Allah (s.w) na sifa zake tukufu unabainishwa katika aya zifuatazo:

﴿إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ﴾

"Katika kuumbwa mbingu na ardhi na mfuatano wa usiku na mchana ziko hoja (za kuonyesha kuwepo Mwenyezi Mungu-Allah) kwa wenye akili" (3:190)

﴿وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ ﴿٢١﴾ وَمِنْ آيَاتِهِ خَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافُ أَلْسِنَتِكُمْ وَأَلْوَانِكُمْ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّلْعَالِمِينَ ﴿٢٢﴾ وَمِنْ آيَاتِهِ مَنَامُكُم بِاللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَابْتِغَاؤُكُم مِّن فَضْلِهِ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَسْمَعُونَ﴿٢٣﴾ وَمِنْ آيَاتِهِ يُرِيكُمُ الْبَرْقَ خَوْفًا وَطَمَعًا وَيُنَزِّلُ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَيُحْيِي بِهِ الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ﴾

"Na katika ishara zake,(za kuthibitisha kuwepo kwake na uweza wake) ni kuwa amekuumbieni wake zenu katika jinsi yenu ili mpate utulivu kutoka kwao, naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Bila shaka katika haya zimo ishara kwa watu wanaofahamu.Na katika ishara zake (za kuonyesha uwezo wake) ni kuumba mbingu na ardhi na kuhitalifiana lugha zenu na rangi zenu na (mengine yenu na hali ya kuwa muumbaji ndiye huyo huyo mmoja). Kwa yakini katika haya zimo ishara kwa wenye ujuzi. Na katika ishara zake ni kulala kwenu usiku na (kuamka) mchana, na kutafuta kwenu fadhila yake. Hakika katika hayo zimo ishara kwa watu wanaosikia.Na katika ishara zake ni kukuonyesheni umeme kwa (kukutieni) hofu na tamaa (ya kuja mvua), na kuyateremsha (hayo) maji kutoka mawinguni. Kwayo huifufua ardhi baada ya kufa kwake.Bila shaka katika haya zimo ishara kwa watu wanaofahamu" (30:21-24)

Aya hizi chache zatosha kuonesha msisitizo wa Qur-an juu ya kutumia akili na fikara zetu katika kumfahamu vyema Allah (s.w). Kila mtu atakavyozama katika utafiti wa mazingira katika fani yoyote ile ndivyo atakavyoweza kumuona Allah (s.w) na utukufu wake kwa upeo mkubwa zaidi. Allah (s.w) mwenyewe anathibitisha hilo katika aya zifuatazo:

﴿أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ أَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجْنَا بِهِ ثَمَرَاتٍ مُّخْتَلِفًا أَلْوَانُهَا وَمِنَ الْجِبَالِ جُدَدٌ بِيضٌ وَحُمْرٌ مُّخْتَلِفٌ أَلْوَانُهَا وَغَرَابِيبُ سُودٌ ﴿٢٧﴾ وَمِنَ النَّاسِ وَالدَّوَابِّ وَالْأَنْعَامِ مُخْتَلِفٌ أَلْوَانُهُ كَذَٰلِكَ إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ غَفُورٌ﴾

"Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu Ameteremsha maji mawinguni! Na kwayo Tumeyatoa matunda yenye rangi mbali mbali.Na katika milima imo mistari myeupe na myekundu yenye rangi mbali mbali, na (mengine) myeusi sana.Na katika watu na wanyama wanaotambaa na wanyama (wengine), pia rangi zao ni mbali mbali, kwa hakika wanaomcha Allah miongoni mwa waja Wake ni wale wataalamu (wanazuoni): Bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mwenye Nguvu, Msamehevu" (35:27-28)

Wataalamu (wanazuoni) kwa mnasaba wa aya hizi si wale waliobobea kwenye fani ya fiq-h tu na nyinginezo zinazoitwa za "dini" bali ni pamoja na wale walio zama kwenye fani mbali mbali za elimu ya mazingira. Kwa mujibu wa aya hizi, wataalamu waliopigiwa mfano ni wale waliobobea katika taaluma ya hali ya hewa (meteorologists), katika taaluma ya madini (Geologists), katika taaluma ya matunda (horticulturist), katika taaluma ya wanyama (Zoologist) na katika taaluma ya watu na tabia zao (anthropologists).

Wale ambao hawatumii vipawa vyao vya akili katika kumfahamu Mola wao kutokana na mazingira wamefananishwa na wanyama, kama tunavyojifunza katika Qur-an:

﴿وَلَقَدْ ذَرَأْنَا لِجَهَنَّمَ كَثِيرًا مِّنَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ لَهُمْ قُلُوبٌ لَّا يَفْقَهُونَ بِهَا وَلَهُمْ أَعْيُنٌ لَّا يُبْصِرُونَ بِهَا وَلَهُمْ آذَانٌ لَّا يَسْمَعُونَ بِهَا أُولَـٰئِكَ كَالْأَنْعَامِ بَلْ هُمْ أَضَلُّ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْغَافِلُونَ﴾

"Na bila shaka tumewaumbia moto wa Jahannam wengi katika majini na watu (kwa sababu hii) Nyoyo (akili) wanazo, lakini hawafahamu kwazo, macho wanayo lakini hawaoni kwayo na masikio wanayo lakini hawasikii kwayo Hao ni kama wanyama bali wao ni wapotofu zaidi. Hao ndio walioghafilika" (7:179)

﴿إِنَّ شَرَّ الدَّوَابِّ عِندَ اللَّـهِ الصُّمُّ الْبُكْمُ الَّذِينَ لَا يَعْقِلُونَ﴾

"Hakika vinyama viovu mbele ya Mwenyezi Mungu ni hawa wanaojipa uziwi na ububu ambao hawayatii akilini (wanayoambiwa au wanayoyaona)" (8:22).

Vilevile Alla(s.w) anawashutumu wale wanaobishana kuhusu Yeye pasina kuwa na elimu.

﴿أَلَمْ تَرَوْا أَنَّ اللَّـهَ سَخَّرَ لَكُم مَّا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَأَسْبَغَ عَلَيْكُمْ نِعَمَهُ ظَاهِرَةً وَبَاطِنَةً وَمِنَ النَّاسِ مَن يُجَادِلُ فِي اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَلَا هُدًى وَلَا كِتَابٍ مُّنِيرٍ﴾

Je! Huoni ya kwamba Mwenyezi Mungu amekutiishieni vilivyomo mbinguni na ardhini, na Akakukamilishieni neema zake zilizo dhahiri na za siri? Na wako watu wanaobishana katika (mambo) ya Mwenyezi Mungu pasipo elimu wala uwongofu wala Kitabu chenye nuru (31:20)

﴿وَمِنَ النَّاسِ مَن يُجَادِلُ فِي اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَلَا هُدًى وَلَا كِتَابٍ مُّنِيرٍ﴾

Na katika watu wako wanaojadiliana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya ilimu wala uwongozi wala kitabu chenye nuru (22:8)

Kutokana na aya hizi tunabainikiwa kwa uwazi kuwa katika Uislamu suala la kumuamini Allah (s.w) si suala la kibubusa (la kufuata mkumbo tu) bali ni suala la kitaaluma linalohitaji utafiti wa kina wa kisayansi. Kuna maeneo matano makubwa ambayo tukiyazamia vizuri kisayansi, yanatupatia dalili mbali mbali za uwazi zinazotuthibitishia kuwepo kwa Allah (s.w) na utukufu wake usio na mfano wake. Maeneo haya ni:

(i) Umbile la mbingu na ardhi na vyote vilivyomo ndani yake

(ii) Nafsi ya mwanaadamu

(iii) Historia ya mwanaadamu

(iv) Maisha ya Mitume

(v) Mafundisho ya Mitume

Umbile la mbingu na ardhi

﴿إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ﴾

"Katika kuumbwa mbingu na ardhi na mfuatano wa usiku na mchana,ziko alama (hoja) za kuonyesha kuwepo Allah (s.w) kwa wenye akili." (3:190).

Mungu, Muumba wa kila kitu ndiye mmiliki pekee wa viumbe vyote. Ni Yeye anayebadili mielekeo ya upepo, anayekusanya mawingu, anayewasha jua na kuiangazia dunia na kudhibiti sayari zizunguuke katika mihimili yao. Kudai maisha haya ya dunia na ulimwengu mzima yanatokana na bahati nasibu ni kutokitumia kipawa cha busara alichotunukiwa kila mwanaadamu mwenye akili timamu. Mpango bora wa dunia na ulimwengu kwa ujumla unapinga uwezekano wa kutokea kwa bahati nasibu tu, na kinyume chake ni ishara ya wazi ya uwezo wa Allah(s.w)usio na kikomo unaodhihirisha kuwepo kwake.

Wakati ambapo ni muhali hata kwa kitu chepesi kufanya mzunguko wa moja kwa moja katika njia yake bila kwenda kombo, dunia pamoja na ukubwa wake yenye mkusanyiko wa vitu visivyo na idadi hufanya hivyo. Na imekuwa ikifanya hivyo kwa miaka dahari, na dahari, tangu dunia kuumbwa na kuanza mzunguko wake. Allah anasema Yeye ndiye mfanyaji wa mahesabu ya mzunguko huo.

﴿قَدْ جَعَلَ اللَّـهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا﴾

Hakika Mwenyezi Mungu amekwishakiwekea kila kitu kipimo chake (65:3)

Utaratibu huo bora wa ulimwengu unaendeshwa kwa mfumo wa ajabu unaokwenda kwa kutegemea mihimili isiyo na mashiko.Wengine hudhani kuwa baada ya kuumba, Allah(s.w)amekiacha kila kitu kijiendeshe chenyewe tu. La hasha kila tukio litokealo mahala popote pale ulimwenguni hutokea kwa idhini ya Allah(s.w) na chini ya udhibiti wake.

Qur'an inatufahamisha:

﴿أَلَمْ تَعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ إِنَّ ذَٰلِكَ فِي كِتَابٍ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ﴾

Je! Hujui ya kwamba Mwenyezi Mungu anajua yaliyoko mbinguni na ardhini? Bila shaka yote yamo kitabuni mwake.Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni sahali. (22:70)

Kwa ujumla, umbile la mbingu na ardhi pamoja na vyote vilivyomo - jua, mwezi, nyota, sayari mbali mbali, milima na mabonde, maji ya mvua, bahari, mito na maziwa, mimea ya kila namna, wanyama wa kila namna na kadhalika ni hoja kubwa ya kuthibitisha kuwepo Allah (s.w) na utukufu wake kwa kila mwenye kutumia akili yake vizuri. Kila mtu atakavyobobea katika taaluma zinazohusiana na maumbile ya mbingu na ardhi kama vile Jeografia, Elimu ya anga (Astronomy), Elimu ya mimea (Botany), Elimu ya wanyama (Zoology), n.k. ndivyo Imani yake ya kuwepo Allah (s.w) itakavyopea.

﴿إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ غَفُورٌ﴾

Kwa hakika wanaomuogopa Allah (s.w) miongoni mwa waja wake ni wale wataalam..." (35:28)

NAFSI YA MWANAADAMU

﴿وَفِي الْأَرْضِ آيَاتٌ لِّلْمُوقِنِينَ ﴿٢٠﴾ وَفِي أَنفُسِكُمْ أَفَلَا تُبْصِرُونَ﴾

"Na katika ardhi zipo (alama namna kwa namna za kuonyesha kuwepo Allah (s.w) kwa wenye akili.Na katika nafsi zenu (pia zimo ishara hizo) Je, hamuoni?" (51:20-21)

Ukimtafakari mwanaadamu utapata dalili nyingi zinazothibitisha kuwepo kwa Allah (s.w). Maeneo ya kutafakari ni pamoja na:

(I) CHANZO NA MWISHO WA UHAI WA MWANAADAMU

﴿كَيْفَ تَكْفُرُونَ بِاللَّـهِ وَكُنتُمْ أَمْوَاتًا فَأَحْيَاكُمْ ثُمَّ يُمِيتُكُمْ ثُمَّ يُحْيِيكُمْ ثُمَّ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ﴾

"Vipi mnamkanusha Allah (s.w) na hali mlikuwa wafu, akakuhuisheni, kisha atakufisheni, kisha atakurudisheni (tena) kisha kwake mtarejeshwa" (2:28)

﴿فَلَوْلَا إِذَا بَلَغَتِ الْحُلْقُومَ ﴿٨٣﴾ وَأَنتُمْ حِينَئِذٍ تَنظُرُونَ ﴿٨٤﴾ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنكُمْ وَلَـٰكِن لَّا تُبْصِرُونَ ﴿٨٥﴾ فَلَوْلَا إِن كُنتُمْ غَيْرَ مَدِينِينَ ﴿٨٦﴾ تَرْجِعُونَهَا إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ﴾

"Basi mbona (roho) ifikapo kooni,na nyinyi wakati ule mnamtazama. Nasi tunakaribiana naye zaidi (huyo anayetoka roho) kuliko nyinyi,wala nyinyi hamuoni.Kama nyinyi hamumo katika mamlaka (yangu), kwanini hamuirudishi (hiyo roho) ikiwa mnasema kweli?" (56:83-87)

(II) ASILI YA MWANAADAMU

﴿وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَكُم مِّن تُرَابٍ ثُمَّ إِذَا أَنتُم بَشَرٌ تَنتَشِرُونَ﴾

"Na katika ishara zake (za kuonyesha kuwepo kwake) ni huku kukuumbeni kwa udongo kisha mnakuwa watu mnaoenea (kila mahali)" (30:20)

(III) KUUMBWA WANAUME NA WANAWAKE

﴿أَيَحْسَبُ الْإِنسَانُ أَن يُتْرَكَ سُدًى ﴿٣٦﴾ أَلَمْ يَكُ نُطْفَةً مِّن مَّنِيٍّ يُمْنَىٰ ﴿٣٧﴾ ثُمَّ كَانَ عَلَقَةً فَخَلَقَ فَسَوَّىٰ ﴿٣٨﴾ فَجَعَلَ مِنْهُ الزَّوْجَيْنِ الذَّكَرَ وَالْأُنثَىٰ ﴿٣٩﴾ أَلَيْسَ ذَٰلِكَ بِقَادِرٍ عَلَىٰ أَن يُحْيِيَ الْمَوْتَىٰ﴾

"Je! Anafikiri binaadamu kuwa ataachwa bure(asipewa amri za Mwenyezi Mungu wala makatazo yake)? Je, hakuwa tone la manii lililotonwa?.Kisha akawa kidonge cha damu, kisha akamuumba na akamsawazisha,kisha akamfanya namna mbili, mwanamume na mwanamke.Je!Hakuwa huyo ni muweza wa kuhuisha wafu?" (75:36-40).

﴿وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ﴾

"Na katika ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu katika jinsi yenu ili mpate utulivu kwao, naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Bila shaka katika haya ziko alama (za kuwepo Allah) kwa watu wanaofikiri" (30:21)

(IV) TOFAUTI YA LUGHA, RANGI, MAKABILA, MATAIFA

﴿وَمِنْ آيَاتِهِ خَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافُ أَلْسِنَتِكُمْ وَأَلْوَانِكُمْ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّلْعَالِمِينَ﴾

"Na katika ishara zake (za kuonyesha kuwepo kwake na uwezo wake) ni kuumba mbingu na ardhi na kuhitalifiana lugha zenu na rangi zenu.Kwa yakini katika haya zimo ishara kwa wenye ujuzi" (30:22)

﴿يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَأُنثَىٰ وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ ﴾

"Enyi watu! Kwa hakika tumekuumbeni (nyote) kwa (yule) mwanamume (mmoja Adam) na (yule) mwanamke (mmoja Hawwa). Na tumekufanyeni mataifa na makabila (mbali mbali) ili mjuane (tu basi). Hakika aheshimiwaye sana miongoni mwenu mbele ya Allah ni yule amchaye Allah zaidi katika nyinyi. Kwa yakini Allah ni Mjuzi Mwenye habari (za mambo yote)." (49:13)

(V) UMBO NA SURA

﴿ يَا أَيُّهَا الْإِنسَانُ مَا غَرَّكَ بِرَبِّكَ الْكَرِيمِ ﴿٦﴾ الَّذِي خَلَقَكَ فَسَوَّاكَ فَعَدَلَكَ ﴿٧﴾ فِي أَيِّ صُورَةٍ مَّا شَاءَ رَكَّبَكَ﴾

"Ewe mwanaadamu! Nini kikudanganyacho na Mola wako Mtukufu (hata ukamkanusha).Aliyekuumba na akakutengeneza, kisha akakulinganisha sawa sawa. Katika sura yoyote aliyoipenda amekutengeneza" (82: 6-8)

﴿وَفِي خَلْقِكُمْ وَمَا يَبُثُّ مِن دَابَّةٍ آيَاتٌ لِّقَوْمٍ يُوقِنُونَ﴾

Na katika umbo lenu na katika viumbe alivyovitawanya zimo alama kwa watu wenye yakini" (45:4)

(VI) CHAKULA CHA MWANAADAMU

﴿فَلْيَنظُرِ الْإِنسَانُ إِلَىٰ طَعَامِهِ ﴿٢٤﴾ أَنَّا صَبَبْنَا الْمَاءَ صَبًّا ﴿٢٥﴾ ثُمَّ شَقَقْنَا الْأَرْضَ شَقًّا ﴿٢٦﴾ فَأَنبَتْنَا فِيهَا حَبًّا ﴿٢٧﴾ وَعِنَبًا وَقَضْبًا ﴿٢٨﴾ وَزَيْتُونًا وَنَخْلًا ﴿٢٩﴾ وَحَدَائِقَ غُلْبًا ﴿٣٠﴾ وَفَاكِهَةً وَأَبًّا ﴿٣١﴾ مَّتَاعًا لَّكُمْ وَلِأَنْعَامِكُمْ﴾

"Hebu mwanaadam na atazame chakula chake.Hakika Sisi tumemimina maji kwa nguvu(kutoka mawinguni). Tena tukaipasuapasua ardhi.Kisha Tukaotesha humo (vyakula vilivyo) chembe chembe.Na mizabibu na mboga.Na mizeituni na mitende. Na mabustani, (mashamba) yenye miti iliyosongamana barabara.Na matunda na malisho.Kwa ajili ya kukustarehesheni nyinyi na wanyama wenu. (80:24-32)

(VII) UFANYAJI KAZI WA VIUNGO VYA NDANI NA NJE YA MWILI WA MWANAADAMU

﴿فَأَقِمْ وَجْهَكَ لِلدِّينِ حَنِيفًا فِطْرَتَ اللَّـهِ الَّتِي فَطَرَ النَّاسَ عَلَيْهَا لَا تَبْدِيلَ لِخَلْقِ اللَّـهِ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ﴾

"Basi uelekeze uso wako katika dini iliyo sawasawa - ndilo umbile Mwenyezi Mungu alilowaumbia watu; (yaani dini hii ya Kiislamu inawafikiana barabara na umbo la binaadamu).Hakuna mabadiliko katika maumbile ya viumbe vya Mwenyezi Mungu.Hiyo ndiyo dini iliyo haki, lakini watu wengi hawajui." (30:30)

(VIII) USINGIZI

﴿وَمِنْ آيَاتِهِ مَنَامُكُم بِاللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَابْتِغَاؤُكُم مِّن فَضْلِهِ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَسْمَعُونَ﴾

"Na katika ishara zake ni kulala kwenu usiku na kuamka mchana na kutafuta fadhila Yake.Hakika katika hayo zimo ishara kwa wenye kusikia.(30:23)

Mwanadamu japo analala kila siku, hajui chanzo cha usingizi.Mtu anapokuwa usingizini hajui chochote kinachoendelea, Je! ni nani anayeleta usingizi na kuuondoa?

(IX) MWANADAMU KUMKUMBUKA ALLAH (S.W) WAKATI WA MATATIZO

﴿قُلْ مَن يُنَجِّيكُم مِّن ظُلُمَاتِ الْبَرِّ وَالْبَحْرِ تَدْعُونَهُ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً لَّئِنْ أَنجَانَا مِنْ هَـٰذِهِ لَنَكُونَنَّ مِنَ الشَّاكِرِينَ﴾

"Sema: Ni nani anayekuokoeni katika viza (taabu) vya bara na baharini? Mnamuomba kwa unyenyekevu na kwa sauti ndogo (mnasema): Kama akituokoa katika (baa) hii bila shaka tutakuwa miongoni mwa wanaoshukuru (6:63)

Hata Fir'auni, aliyetakabari sana kiasi cha kudai kuwa yeye ni mkubwa kuliko Allah, alimkumbuka Mola wake pale alipokabiliwa barabara na matatizo.

﴿وَجَاوَزْنَا بِبَنِي إِسْرَائِيلَ الْبَحْرَ فَأَتْبَعَهُمْ فِرْعَوْنُ وَجُنُودُهُ بَغْيًا وَعَدْوًا حَتَّىٰ إِذَا أَدْرَكَهُ الْغَرَقُ قَالَ آمَنتُ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا الَّذِي آمَنَتْ بِهِ بَنُو إِسْرَائِيلَ وَأَنَا مِنَ الْمُسْلِمِينَ﴾

"Na tukawapitisha wana wa Israel katika bahari, na Firauni na majeshi yake wakawafuata kwa dhulma na jeuri. Hata kulipomfikia Fir'aun kuzama alisema, "Naamini kwamba hakuna aabudiwaye kwa haki ila yule wanayemuamini wana wa Israel na mimi ni miongoni mwa wanaotii". (10:90)

Historia ya Mwanadamu Historia ya mwanadamu ukiichunguza tangu mwanzo wake utakuta matukio mengi yanayothibitisha kuwepo Allah (s.w) Mmiliki wa kila kitu na mwenye nguvu na uwezo juu ya kila kitu. Mara kwa mara tunatanabahishwa katika Qur-an:

﴿أَفَلَمْ يَهْدِ لَهُمْ كَمْ أَهْلَكْنَا قَبْلَهُم مِّنَ الْقُرُونِ يَمْشُونَ فِي مَسَاكِنِهِمْ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّأُولِي النُّهَىٰ﴾

"Je! Haikuwabainikia tu kama (kaumu) ngapi tuliziangamiza kabla yao? Na hawa (makafiri wa sasa) wanatembeatembea katika maskani yao, (hawaoni alama za kuangamizwa kwao)?Bila shaka katika hayo zimo ishara kwa wenye akili." (20:128)

﴿أَوَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ كَانُوا أَشَدَّ مِنْهُمْ قُوَّةً وَأَثَارُوا الْأَرْضَ وَعَمَرُوهَا أَكْثَرَ مِمَّا عَمَرُوهَا وَجَاءَتْهُمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيَظْلِمَهُمْ وَلَـٰكِن كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ﴾

"Je! Hawatembei katika nchi na kuona jinsi ulivyokuwa mwisho wa wale waliokuwa kabla yao? Walikuwa wenye nguvu zaidi kuliko wao na wakilima ardhi na kuistawisha zaidi kuliko wao walivyostawisha. Na mitume wao waliwajia kwa dalili waziwazi, basi hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwadhulumu,lakini walikuwa wenyewe wakijidhulumu nafsi zao." (30:9)

﴿أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِأَصْحَابِ الْفِيلِ ﴿١﴾ أَلَمْ يَجْعَلْ كَيْدَهُمْ فِي تَضْلِيلٍ ﴿٢﴾ وَأَرْسَلَ عَلَيْهِمْ طَيْرًا أَبَابِيلَ ﴿٣﴾ تَرْمِيهِم بِحِجَارَةٍ مِّن سِجِّيلٍ ﴿٤﴾ فَجَعَلَهُمْ كَعَصْفٍ مَّأْكُولٍ﴾

"Je!Huoni Mola wako alivyo wafanya watu wenye ndovu?Hakujaalia vitimbi vyao kuharibika?Na akawapeleka ndege makundi kwa makundi, wakawapiga kwa mawe ya udongo wa kuchoma, Akawafanya kama majani yaliyotafunwa." (105:1-5)

Tukio hili la watu wenye ndovu lilitokea mwaka 570.A.D. miezi michache kabla ya kuzaliwa Mtume Muhammad(s.a.w.w). Mnamo mwaka wa 570 A.D. Abraha, gavana wa Yemen, chini ya himaya ya Kikiristo ya Uhabeshi alikusanya jeshi lenye askari 60,000 na ndovu (tembo) kumi na tatu (13) kwa nia ya kuibomoa na kuisambaratisha Al-Ka'abah, nyumba takatifu ya Allah (s.w) iliyopo Makka. Walinzi wa Ka'abah, kabila la Quraish waliongozwa na Abdul-Muttalib, Babu yake Mtume (s.a.w), walimfahamisha Abraha kuwa wao hawana uwezo wa kupambana na jeshi lake hilo bali mwenye Ka'abah ndiye atakayeilinda. Abraha alipokaidi na kusisitiza kutekeleza azma yake ya kuivunja Ka'abah, Abdul- Muttalib aliwaamuru wakazi wa Makka wampishe na akaingia ndani ya Ka'abah na kumuomba Allah (s.w) kwa unyenyekevu kama ifuatavyo:

"O Allah, mtu hulinda nyumba yake, nawe ilinde nyumba yako. Usiuachie msalaba na hila zao kesho kushinda hila zako. Kama utaamua kuwaachia waifanye watakavyo Qibla yetu, Basi wewe ni muweza wa kufanya upendavyo. Wanusuru leo watumishi wako dhidi ya watumishi wa Msalaba na waabudu wake. Ewe Mola wangu, sina matumaini yoyote toka kwa yeyote dhidi yao isipokuwa kwako. Ewe Mola wangu, ilinde nyumba yako dhidi yao. Adui wa nyumba hii ni adui yako. Wazuie wasiiharibu nyumba yako"

Kesho yake, Abraha na jeshi lake kabla hawajapiga hatua kutoka kwenye kambi yao, kilometa tano (5) tokea Makka, walizingirwa na jeshi la ndege wadogo wadogo walioitwa "Ababil" waliokuwa na silaha ya vijiwe. Kila ndege alimlenga askari wake na kijiwe hicho kilichomchakaza na kumfanya kama majani yaliyotafunwa na kutemwa. Tukio hili la "watu wa ndovu" ni kielelezo tosha kutokana na historia ya binaadamu kuwa Allah (s.w) yupo na anauwezo ulio juu ya hila zote za binaadamu na juu ya kila kitu.

Maisha ya Mitume Ukiyachunguza maisha ya mitume mbalimbali kama yalivyoelezwa katika Qur-an utabaini kuwa wao kweli walikuwa ni wajumbe wa Allah (s.w). Tunayoyaona katika maisha ya Mitume ambayo yanatuhakikishia kuwepo kwa Allah (s.w) ni pamoja na:

(i) Kuwepo kwao na kujieleza kwa watu wao kuwa ni Mitume wa Mwenyezi Mungu (s.w)

(ii) Msimamo wao katika kujieleza kwa jamii zao kuwa wao ni Mitume wa Allah (s.w)

(iii) Mwenendo wao mwema kutoathiriwa na (mazingira) jamii

(iv) Miujiza waliyoionesha katika kuthibitisha utume wao (v) Kuhimili kwao mateso na kujitoa kwao muhanga kwa ajili ya Allah (s.w)

(vi) Ujasiri wao katika kuwakabili viongozi wa jamii zao.

(vii) Ushindi wao dhidi ya maadui wa Mwenyezi Mungu

(viii) Mitume kutohitaji malipo yoyote kwa ajili ya kazi yao.

(i) Kuwepo kwao na kujieleza kwa watu wao kuwa ni Mitume wa Mwenyezi Mungu (s.w) Mitume walijieleza kwa uwazi kuwa wao ni mitume wa Allah (s.w) kama tunavyojifunza katika mifano ifuatayo:

﴿لَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا إِلَىٰ قَوْمِهِ فَقَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ إِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿٥٩﴾ قَالَ الْمَلَأُ مِن قَوْمِهِ إِنَّا لَنَرَاكَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٦٠﴾ قَالَ يَا قَوْمِ لَيْسَ بِي ضَلَالَةٌ وَلَـٰكِنِّي رَسُولٌ مِّن رَّبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٦١﴾ أُبَلِّغُكُمْ رِسَالَاتِ رَبِّي وَأَنصَحُ لَكُمْ وَأَعْلَمُ مِنَ اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٦٢﴾ أَوَعَجِبْتُمْ أَن جَاءَكُمْ ذِكْرٌ مِّن رَّبِّكُمْ عَلَىٰ رَجُلٍ مِّنكُمْ لِيُنذِرَكُمْ وَلِتَتَّقُوا وَلَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٦٣﴾ فَكَذَّبُوهُ فَأَنجَيْنَاهُ وَالَّذِينَ مَعَهُ فِي الْفُلْكِ وَأَغْرَقْنَا الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا إِنَّهُمْ كَانُوا قَوْمًا عَمِينَ ﴿٦٤﴾ وَإِلَىٰ عَادٍ أَخَاهُمْ هُودًا قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ أَفَلَا تَتَّقُونَ ﴿٦٥﴾ قَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن قَوْمِهِ إِنَّا لَنَرَاكَ فِي سَفَاهَةٍ وَإِنَّا لَنَظُنُّكَ مِنَ الْكَاذِبِينَ ﴿٦٦﴾ قَالَ يَا قَوْمِ لَيْسَ بِي سَفَاهَةٌ وَلَـٰكِنِّي رَسُولٌ مِّن رَّبِّ الْعَالَمِينَ﴾

"Tulimtuma Nuhu kwa watu wake naye akasema: 'Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Hakika mimi ninakuhofieni adhabu ya siku iliyo Kuu. Wakuu wa watu wake wakasema: "Sisi tunakuona uko katika upotofu uliodhahiri.Akasema (Nuhu):"Enyi kaumu yangu mimi simo katika upotofu lakini mimi ni Mtume nitokaye kwa Mola wa walimwengu wote. Na kwa Adi (tulimpeleka) ndugu yao Hudi akasema: "Ewe kaumu yangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu nyinyi hamna Mungu ila Yeye Hamuogopi? Wakasema wakuu waliokufuru katika kaumu yake:"Sisi tunakuona umo katika upumbavu na tunakuona u miongoni mwa waongo.Akasema: "Enyi kaumu yangu! Mimi sina upumbavu.Lakini mimi ni Mtume niliyetoka kwa Mola wa walimwengu.(7:59-67)

Pamoja na Mitume kujieleza kuwa wanatoka kwa Allah (s.w) mwenyewe Allah (s.w) anatufahamisha kuwa ametuma Mitume:

﴿وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ فَمِنْهُم مَّنْ هَدَى اللَّـهُ وَمِنْهُم مَّنْ حَقَّتْ عَلَيْهِ الضَّلَالَةُ فَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَانظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُكَذِّبِينَ﴾

Na bila shaka tulimpeleka Mtume katika kila umma ya kwamba,"muadubuni Mwenyezi Mungu na mwepukeni muovu (twaaghuut) (16:36)

﴿إِنَّا أَرْسَلْنَاكَ بِالْحَقِّ بَشِيرًا وَنَذِيرًا وَإِن مِّنْ أُمَّةٍ إِلَّا خَلَا فِيهَا نَذِيرٌ﴾

Bila shaka Sisi tumekutuma (tumekuleta) kwa haki ili ubashirie na uonye. Na hakuna taifa lolote ila alipita humo muonyaji (Mtume kuwaonya). (35:24)

﴿وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلًا مِّن قَبْلِكَ مِنْهُم مَّن قَصَصْنَا عَلَيْكَ وَمِنْهُم مَّن لَّمْ نَقْصُصْ عَلَيْكَ وَمَا كَانَ لِرَسُولٍ أَن يَأْتِيَ بِآيَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ فَإِذَا جَاءَ أَمْرُ اللَّـهِ قُضِيَ بِالْحَقِّ وَخَسِرَ هُنَالِكَ الْمُبْطِلُونَ﴾

Na kwa yakini tuliwatuma Mitume kabla yako.Wengine katika hao tumekusimulia (majina yao na habari zao) na wengine hatukusimulia na haikuwa kwa Mtume yoyote kuleta muujiza wowote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na itakapokuja hukumu ya Mwenyezi Mungu kutahukumiwa kwa haki, na wafanyao mambo ya batili watapata hasara wakati huo. (40:78).

Hivyo, kuwepo kwa Mitume kunatuthibitishia kuwepo kwa Mwenyezi Mungu (s.a.w) kwa namna mbili, kwanza, kama Mwenyezi Mungu (s.w) asingelikuwepo asingelileta Mitume kwa wanaadamu. Pili, Mitume wote waliotokea katika nyakati mbali mbali za historia wasingelitoa dai moja linalofanana kwa wote kuwa wao ni Mitume wa Mwenyezi Mungu (s.w) kama Mwenyezi Mungu hayupo.

(ii) Mwenendo wao mwema kutoathiriwa na jamii Mitume wote takriban walizaliwa na kulelewa katika jamii za kijahili zilizozama katika kumshirikisha Mwenyezi Mungu (s.w) na miungu chungu nzima. lakini jambo la ajabu na kushangaza ni kwamba, Mitume wote tangu utotoni waliepukana na tabia za kijahili na walijiepusha mbali na kumshirikisha Mwenyezi Mungu (s.w). Walikuwa na mwenendo wa kiutu (wa Kiislamu) uliowavutia watu wote wa jamii zao na walikuwa ni nyota katika jamii. Kwa mfano, Nabii Ibrahim(a.s) alizaliwa na kuhani Mkuu.

Yaani baba yake Nabii Ibrahim alikuwa ni kiongozi au msimamizi wa ibada ya masanamu. Lakini Nabii Ibrahim kamwe hakuvutiwa na ibada hiyo ya masanamu bali akiwa angali kijana mdogo aliona kuwa ni kinyume kabisa na akili ya mwanaadamu kuwaabudu miungu wengine kinyume na kumuabudu Allah (s.w) aliye mpweke. Mfano wa pili ni ule wa Nabii, Musa(a.s) aliyelelewa katika nyumba ya Firaun aliyetakabari na kujiita mungu. Malezi hayo ya kifalme kamwe hayakumuathiri Nabii Musa(a.s) .Aliinukia kuwa na mwenendo mwema wa kumpwekesha Allah (s.w).

Mfano mwingine ni ule wa Mtume Muhammad(s.a.w.w) ambaye alizaliwa katika jamii ya Maquraysh iliyobobea katika ujahili na iliyozama katika ushirikina kiasi kwamba kila kitu kwao kiliweza kufanywa mungu na kuabudiwa. Katika wakati huo masanamu ya watu, ndege na wanyama yaliuzwa sokoni kama miungu wa kuabudiwa na hata tende zilifinyangwa na kuabudiwa. Lakini tunavyojifunza katika historia, Mtume(s.a.w.w) tangu utotoni mwake hakuathiriwa kamwe na ibada za masanamu na mwendo wa ujahili. Bali tunajifunza kuwa aliinukia katika kumtambua na kumpwekesha Allah (s.w) na aliwazidi watu wote kwa tabia njema kiasi kwamba watu wake walimtegemea sana kwa ushauri na kuwatunzia amana zao na walimwita "mkweli", "mwaminifu" na majina mengine kama haya yaliyodhihirisha tabia yake njema katikati ya jamii ya kijahili. Ni kitu gani kilichowafanya Mitume kuwa tofauti na watu wa jamii zao?

Je, hakuna aliyewatayarisha na kuwalea katika mwenendo huo ili wawe viigizo vyema katika jamii zao? Bila shaka Mwenyezi Mungu (s.w) ndiye aliwewaleta Mitume ili wafikishe ujumbe wake na wawe viigizo vyema katika kuutekeleza Uislam kama inavyobainishwa katika Qur-an:

﴿لَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا بِالْبَيِّنَاتِ وَأَنزَلْنَا مَعَهُمُ الْكِتَابَ وَالْمِيزَانَ لِيَقُومَ النَّاسُ بِالْقِسْطِ﴾

Kwa hakika tuliwapeleka Mitume wetu kwa dalili wazi wazi na tukaviteremsha Vitabu na uadilifu pamoja nao, ili watu wasimamie uadilifu. (57:25)

(iii) Dalili (miujiza) za kuthibitisha Utume wao Mitume wameletwa pamoja na alama mbali mbali za kuwathibitisha Utume wao kwa watu wao.

﴿لَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا بِالْبَيِّنَاتِ﴾

"Kwa hakika tumewapeleka Mitume wetu kwa dalili wazi wazi" (57:25)

Kila Mtume alipewa dalili za kuwathibitishia watu wake kuwa yeye ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Alama za Utume wa Nabii Musa(a.s) ni fimbo yake kugeuka kuwa nyoka wa kweli na mkono wake kutoa mwan ga mkali kama tunavyojifunza katika Qur-an. (Rejea 28:29-32)

Dalili za Utume wa Nabii Issa(a.s) zilikuwa ni kuwafufua wafu, kuwaponyesha vipofu na wenye mbaranga, kulifanya sanamu la ndege kuwa ndege wa kweli kama inavyobainishwa katika Quran (5:110).

Dalili aliyopewa Mtume Muhammad(s.a.w.w) ya kuthibitisha kuwa yeye ni Mtume wa Allah (s.w) ambayo itabakia mpaka mwisho wa ulimwengu ni Qur-an. Qur-an tofauti na vitabu vingine vya Allah (s.w) imehifadhiwa na uharibifu wa aina yoyote. Qur-an yenyewe inatukumbusha:

﴿أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ وَلَوْ كَانَ مِنْ عِندِ غَيْرِ اللَّـهِ لَوَجَدُوا فِيهِ اخْتِلَافًا كَثِيرًا﴾

Hawaizingatii nini,hii Qur-an? Na kama ingelitoka kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu bila shaka wangelikuta ndani yake khitilafu nyingi. (4:82).

(iv) Kuhimili mateso na kujitoa kwao muhanga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (s.w)

Jambo jingine linalopatikana katika historia ya Mitume ni uvumilivu waliokuwa nao dhidi ya mateso mbali mbali waliyofanyiwa na watu wao na bado wakaendelea kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu bila ya kukata tama. Tukirejea katika Qur'an tunapata mifano mbali mbali ya mateso waliyofanyiwa na jamaa zao. Kwa mfano tunajifunza katika Qur-an kuwa ilikuwa ni tabia ya Wayahudi (kizazi cha Israil) kuwauwa Mitume yao pasina haki:

﴿إِنَّ الَّذِينَ يَكْفُرُونَ بِآيَاتِ اللَّـهِ وَيَقْتُلُونَ النَّبِيِّينَ بِغَيْرِ حَقٍّ وَيَقْتُلُونَ الَّذِينَ يَأْمُرُونَ بِالْقِسْطِ مِنَ النَّاسِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ﴾

Wale (Mayahudi) wanaozikataa Aya za Mwenyezi Mungu, na wakawaua manabii pasina haki, na wakaua watu wanaoamrisha kusimamisha haki, wapashe habari ya adhabu kali. (3:21)

Nabii Yahya(a.s) (Yohana mbatizaji) ni miongoni mwa Mitume wa Mwenyezi Mungu waliochinjwa na Mayahudi, kwa sababu tu eti walisimama kidete kufikisha neno la Mwenyezi Mungu, kwa watu wao ili wasimamishe haki katika jamii kwa kufanya mema na kuacha maovu.Pia Mayahudi walikula njama za kumuua Nabii Isa(a.s) . Lakini Mwenyezi Mungu (s.w) alimuokoa na kumnyakuwa kwake kama tunavyojifunza katika Qur-an:

﴿وَقَوْلِهِمْ إِنَّا قَتَلْنَا الْمَسِيحَ عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ رَسُولَ اللَّـهِ وَمَا قَتَلُوهُ وَمَا صَلَبُوهُ وَلَـٰكِن شُبِّهَ لَهُمْ وَإِنَّ الَّذِينَ اخْتَلَفُوا فِيهِ لَفِي شَكٍّ مِّنْهُ مَا لَهُم بِهِ مِنْ عِلْمٍ إِلَّا اتِّبَاعَ الظَّنِّ وَمَا قَتَلُوهُ يَقِينًا ﴿١٥٧﴾ بَل رَّفَعَهُ اللَّـهُ إِلَيْهِ وَكَانَ اللَّـهُ عَزِيزًا حَكِيمًا ﴿١٥٨﴾ وَإِن مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ إِلَّا لَيُؤْمِنَنَّ بِهِ قَبْلَ مَوْتِهِ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكُونُ عَلَيْهِمْ شَهِيدًا﴾

"Na kwa (ajili ya) kusema kwao: Sisi tumemuua Masihi Isa, mwana wa Maryam Mtume wa Mungu", hali hawakumuua wala hawakumsulubu, bali walibadilishiwa (mtu mwingine wakamdhani Nabii Issa). Na kwa hakika wale waliokhitilafiana katika (hakika) hiyo (ya kumuua Nabii Isa) wamo katika shaka nalo (jambo hilo la kusema kauawa).Wao (kabisa) hawana yakini juu ya (jambo) hili (la kuwa kweli wamemua Nabii (Isa). Isipokuwa wanafuata dhana tu. Na kwa yakini hawakumua.Bali Mwenyezi Mungu alimnyanyua kwake, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima. (4:157-158)

Naye Nabii Ibrahim alitupwa motoni na jamaa zake, Mwenyezi Mungu (s.w) aliuamrisha moto kuwa baridi na salama kwake:

﴿قُلْنَا يَا نَارُ كُونِي بَرْدًا وَسَلَامًا عَلَىٰ إِبْرَاهِيمَ﴾

"Tukasema: 'Ewe moto! Kuwa baridi na salama juu ya Ibrahim". (21:69)

Mitume pia walitiwa vifungoni na vizuizini (kutengwa na jamii) kama ilivyokuwa kwa Nabii Yusufu(a.s) na Nabii Muhammad(s.a.w.w) . Baadhi ya Mitume na wafuasi wao walifukuzwa nchini mwao na kuhamia ugenini kama ilivyokuwa kwa Mtume(s.a.w.w) na Muhajirina:

﴿لِلْفُقَرَاءِ الْمُهَاجِرِينَ الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِن دِيَارِهِمْ وَأَمْوَالِهِمْ يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانًا وَيَنصُرُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ أُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ﴾

"(Basi) wapewe (mali hayo) mafakiri wa Kimuhajiri ambao walifukuzwa katika nyumba zao na mali zao; (wakakhiari kuyaacha hayo) kwa ajili ya (kutafuta) fadhila za Mwenyezi Mungu na radhi (yake) na kuinusuru (dini ya) Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Basi hao ndio waislamu wa kweli. (59:8).

Mitume pia walinyanyaswa kwa matusi na kejeli. Kwa mfano Mtume Muhammad(s.a.w.w) aliitwa mwendawazimu, mchawi, mtunga mashairi, abtair (mkiwa) na matusi mengineyo. Pamoja na kufanyiwa madhila yote hayo, bado Mitume walisimama kidete kuufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu (s.w) kwa watu wao na wala hawakukata tamaa.Ni nguvu gani iliyowapa Mitume ustahimilivu kiasi hicho? Je,kuna malipo yoyote ya hapa duniani waliyoyapata ndiyo yakawafanya kuwa wastahamilivu kiasi hicho? Je, Mitume hawakuwa na tegemeo la kulipwa na mwenye uwezo juu ya kila kitu anayestahiki kutegemewa na kuogopwa kuliko yeyote yule? Bila shaka uvumilivu na subira ya hali ya juu waliyokuwa nayo Mitume ni alama kuwa yuko mwenye nguvu na uwezo juu ya kila kitu waliyekuwa wakimtegemea na kutaraji ujira mkubwa kutoka kwake.

(v) Ujasiri wa Mitume mbele ya Viongozi wa jamii ya kishirikina Mitume hawakumchelea yeyote katika kuwafikishia watu ujumbe waliotumwa kuufikisha.Hawakufikisha ujumbe wao kwa watu wa kawaida tu bali waliwaendea Wafalme na watawala wa jamii waliokuwa wapinzani wakubwa wa ujumbe wa Mwenyezi Mungu (s.w). Mitume waliwaelekea wakuu hao wa jamii pamoja na takaburi zao na vitisho vingi walivyovitoa dhidi yao. Kwa mfano Nabii Ibrahiim hakumchelea baba yake katika kumfikishia ujumbe wa kumpwekesha Mwenyezi Mungu (s.w) kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:

﴿إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ يَا أَبَتِ لِمَ تَعْبُدُ مَا لَا يَسْمَعُ وَلَا يُبْصِرُ وَلَا يُغْنِي عَنكَ شَيْئًا ﴿٤٢﴾ يَا أَبَتِ إِنِّي قَدْ جَاءَنِي مِنَ الْعِلْمِ مَا لَمْ يَأْتِكَ فَاتَّبِعْنِي أَهْدِكَ صِرَاطًا سَوِيًّا ﴿٤٣﴾ يَا أَبَتِ لَا تَعْبُدِ الشَّيْطَانَ إِنَّ الشَّيْطَانَ كَانَ لِلرَّحْمَـٰنِ عَصِيًّا ﴿٤٤﴾ يَا أَبَتِ إِنِّي أَخَافُ أَن يَمَسَّكَ عَذَابٌ مِّنَ الرَّحْمَـٰنِ فَتَكُونَ لِلشَّيْطَانِ وَلِيًّا ﴿٤٥﴾ قَالَ أَرَاغِبٌ أَنتَ عَنْ آلِهَتِي يَا إِبْرَاهِيمُ لَئِن لَّمْ تَنتَهِ لَأَرْجُمَنَّكَ وَاهْجُرْنِي مَلِيًّا﴾

(Wakumbushe) alipomwambia baba yake: "Ewe baba yangu! Kwanini unaabudu visivyosikia na visivyoona na visivyo kufaa chochote?Ewe baba yangu!Kwa yakini imenijia ilimu isiyokujia. Basi nifuate nitakuongoza njia iliyosawa.Ewe baba yangu! Usimuabudu shetani, hakika shetani ni mwenye kumuasi (Mwenyezi Mungu) Mwingi wa rehma.Ewe baba yangu! Hakika naogopa kukupata adhabu inayotoka kwa Mwingi wa Rehma (Mwenyezi Mungu), ukifanya hivyo) utakuwa mwenziwe shetani".Akasema (yule baba yake):"Je, unaichukia miungu yangu, ewe Ibahimu? Kama huachi (haya unayoyasema) lazima nitakupiga mawe.Na niondokelee mbali, kwa muda mchache (huu). (19:42-46)

Nabii Ibrahim hakuishia kuufikisha ujumbe kwa baba yake tu, bali aliufikisha pia kwa vitendo kwa jamii nzima kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:

﴿وَتَاللَّـهِ لَأَكِيدَنَّ أَصْنَامَكُم بَعْدَ أَن تُوَلُّوا مُدْبِرِينَ ﴿٥٧﴾فَجَعَلَهُمْ جُذَاذًا إِلَّا كَبِيرًا لَّهُمْ لَعَلَّهُمْ إِلَيْهِ يَرْجِعُونَ ﴿٥٨﴾ قَالُوا مَن فَعَلَ هَـٰذَا بِآلِهَتِنَا إِنَّهُ لَمِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٥٩﴾ قَالُوا سَمِعْنَا فَتًى يَذْكُرُهُمْ يُقَالُ لَهُ إِبْرَاهِيمُ ﴿٦٠﴾ قَالُوا فَأْتُوا بِهِ عَلَىٰ أَعْيُنِ النَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَشْهَدُونَ ﴿٦١﴾ قَالُوا أَأَنتَ فَعَلْتَ هَـٰذَا بِآلِهَتِنَا يَا إِبْرَاهِيمُ ﴿٦٢﴾ قَالَ بَلْ فَعَلَهُ كَبِيرُهُمْ هَـٰذَا فَاسْأَلُوهُمْ إِن كَانُوا يَنطِقُونَ ﴿٦٣﴾ فَرَجَعُوا إِلَىٰ أَنفُسِهِمْ فَقَالُوا إِنَّكُمْ أَنتُمُ الظَّالِمُونَ ﴿٦٤﴾ ثُمَّ نُكِسُوا عَلَىٰ رُءُوسِهِمْ لَقَدْ عَلِمْتَ مَا هَـٰؤُلَاءِ يَنطِقُونَ ﴿٦٥﴾ قَالَ أَفَتَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُكُمْ شَيْئًا وَلَا يَضُرُّكُمْ ﴿٦٦﴾ أُفٍّ لَّكُمْ وَلِمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿٦٧﴾ قَالُوا حَرِّقُوهُ وَانصُرُوا آلِهَتَكُمْ إِن كُنتُمْ فَاعِلِينَ﴾

"Na wallahi (kwa haki ya Mungu) nitayafanyia mabaya masanamu yenu haya baada ya kunipa mgongo mkenda zenu." Basi akayavunja (masanamu yote yale) vipande vipande isipokuwa lile kubwa lao (aliliacha), ili wao (hao makafiri) walirudie. Wakasema: "Nani aliyeifanya hivi miungu yetu? Hakika huyo yu miongoni mwa madhalimu (wakubwa).Wakasema: "Tulimsikia kijana mmoja akiwataja anayeitwa Ibrahim.Wakasema: Basi mleteni mbele ya macho ya watu, wamshuhudie (kwa ubaya wake huyo)" Wakasema: "Je!Wewe umeifanya hivi miungu yetu, Ee Ibrahim? Akasema: Siyo,bali amefanya (hayo) huyu mkubwa wao, basi (muulizeni na) waulizeni (pia hao waliovunjwa) kama wanaweza kusema! Basi wakajirudi nafsi zao, (wakafikiri udhalilifu wa waungu hao walio nao, wasioweza kujipigania) na wakasema: "Hakika nyinyi mlikuwa madhalimu (wa nafsi zenu kwenda kuwaabudu wasiokuwa na maana)." Kisha wakainamishwa vichwa vyao, (wakarejea ujingani, ukafirini, wakasema): "Hakika umekwishajua ya kwamba hawasemi, (kwa nini unatucheza shere?).Akasema: "Je! Mnaabudu badala ya Mwenyezi Mungu (miungu) isiyokufaeni chochote(mnapowaabudu) wala kukudhuruni (chochote mnapoacha kuwaabudu? Kefule (udhalilifu) yenu na ya hivyo mnavyoviabudu kinyume na Mwenyezi Mungu. Je! hamfikiri? (21:57- 67)

Pia Nabii Ibrahim(a.s) alimkabili mfalme na kuhojiana naye. - Rejea Qur-an (2:258)

(vi) Ushindi wa Mitume dhidi ya maadui Jambo jingine tunalojifunza katika historia ya Mtime ambalo ni miongoni mwa dalili kubwa za kuonyesha kuwepo kwa Mwenyezi Mungu (s.w) ni ushindi waliokuwa wakiupata Mitume na wafuasi wao wachache dhidi ya maadui zao. Mara zote walikuwa wapinzani wakubwa wa ujumbe wa Mwenyezi Mungu (s.w) walikuwa watawala wa walioshikilia dola na matajiri waliokuwa na wafuasi wengi na majeshi yenye nguvu kubwa. Kwa upande mwingine, katika jamii zote, walioamini Mitume walikuwa wachache na wengi wao wakiwa wanyonge wa jamii. Pamoja na hivyo Mitume na waumini wachache wanyonge waliwashinda maadui zao walikuwa na nguvu kwa kiasi kikubwa.

Hebu turejee mifano michache ifuatayo: Nabii Nuhu(a.s) aliwalingania watu wa jamii yake kwa miaka 950. Lakini watu wake pamoja na kutishia kumuua, walimtaka awaletee kutoka kwa Mola wake hiyo adhabu aliyokuwa akiwatahadharisha kwayo ikiwa anasema kweli kuwa yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.w). Mwishowe adhabu kweli ililetwa na wakawa ni wenye kugharikishwa kama tunavyojifunza katika Qur-an: Basi kwa ajili ya makosa yao waligharikishwa wakaingizwa motoni wala hawakuwapata wa kuwanusuru mbele ya Mwenyezi Mungu (s.w). (71:25) Nabii Hud(a.s) alitumwa kwa watu wa Ad na kuwafikishia ujumbe wa Mwenyezi Mungu (s.w). Lakini wengi wao wakiongozwa na watawala na matajiri walitakabari na kukataa na kuwa dhidi yake na wafuasi wachache walioamini pamoja naye. Kisha Mwenyezi Mungu (s.w) alimnusuru Mtume wake na walioamini pamoja naye kutokana na madhalimu kama tunavyojifunza katika Qur-an:

﴿٧٢فَأَنجَيْنَاهُ وَالَّذِينَ مَعَهُ بِرَحْمَةٍ مِّنَّا وَقَطَعْنَا دَابِرَ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَمَا كَانُوا مُؤْمِنِينَ﴾

Basi tukamuokoa yeye na waliokuwa pamoja naye kwa rehema zetu, na tukakata mizizi ya wale waliozikadhibisha aya zetu, na (ambao) hawakuwa wenye kuamini. (7:72).

Nabii Musa(a.s) na wana wa Israil waliokolewa kutokana na makucha ya dhalimu Firaun na majeshi yake kama tunavyojifunza katika Qur-an:

﴿فَأَتْبَعُوهُم مُّشْرِقِينَ ﴿٦٠﴾فَلَمَّا تَرَاءَى الْجَمْعَانِ قَالَ أَصْحَابُ مُوسَىٰ إِنَّا لَمُدْرَكُونَ ﴿٦١﴾ قَالَ كَلَّا إِنَّ مَعِيَ رَبِّي سَيَهْدِينِ ﴿٦٢﴾ فَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ مُوسَىٰ أَنِ اضْرِب بِّعَصَاكَ الْبَحْرَ فَانفَلَقَ فَكَانَ كُلُّ فِرْقٍ كَالطَّوْدِ الْعَظِيمِ ﴿٦٣﴾ وَأَزْلَفْنَا ثَمَّ الْآخَرِينَ ﴿٦٤﴾ وَأَنجَيْنَا مُوسَىٰ وَمَن مَّعَهُ أَجْمَعِينَ ﴿٦٥﴾ ثُمَّ أَغْرَقْنَا الْآخَرِينَ ﴿٦٦﴾ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ ﴿٦٧﴾ وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ﴾

Basi (watu wa Firaun na mwenyewe nafsi yake Firaun) wakawafuata (Nabii Mussa na watu wake) lilipotua jua. Na yalipoonana majeshi mawili (haya, watu wa Nabii Musa wanakimbia, na Firauni na watu wake wanawafuatia). Watu wa Musa walisema: "Hakika tutakamatwa. (Musa) akasema: "La, kwa yakini Mola wangu yu pamoja nami, bila shaka ataniongoza (tuokoke sote)". Mara tulimpelekea Wahyi Musa (tukamwambia): "Piga bahari kwa fimbo yako". Basi ikatengana, na kila sehemu ikawa kama jabali kubwa. Na tukawaleta hapo wale wengine (nao ni firauni na watu wake). Na tukamuokoa Musa na wale waliokuwa pamoja naye wote.Kisha tukawagharikisha hao wengine. Hakika katika hayo muna mazingatio: lakini wengi katika wao si wenye kuamini. Na kwa yakini Mola wako ndiye Mwenye Nguvu, mwenye Rehema. (26:60-68)

Mfano wa mwisho ni ule unaopatikana katika historia ya Mtume Muhammad(s.a.w.w) na wafuasi wake. Vita vya kwanza vikubwa alivyopigana Mtume (s.a.w) na wafuasi wake dhidi ya maadui wa Mwenyezi Mungu ni vita vya Badr. Katika vita hivyo jeshi la makafiri wa Kiquraish lililojizatiti barabara lilikuwa na watu 1000 ambapo jeshi la Waislamu lisilojiandaa vizuri kivita lilikuwa na wanajeshi 300 tu hivi. Pamoja na udogo na uduni wa jeshi, Waislamu walipata ushindi mkubwa kwa msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w) kama tunavyojifunza katika Qur-an:

﴿إِذْ تَسْتَغِيثُونَ رَبَّكُمْ فَاسْتَجَابَ لَكُمْ أَنِّي مُمِدُّكُم بِأَلْفٍ مِّنَ الْمَلَائِكَةِ مُرْدِفِينَ ﴿٩﴾ وَمَا جَعَلَهُ اللَّـهُ إِلَّا بُشْرَىٰ وَلِتَطْمَئِنَّ بِهِ قُلُوبُكُمْ وَمَا النَّصْرُ إِلَّا مِنْ عِندِ اللَّـهِ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴾

(Kumbukeni) mlipokuwa mkiomba msaada kwa Mola wenu, naye akakujibuni kuwa:"Kwa yakini Mimi nitakusaidieni kwa malaika elfu moja watakaofuatana mfululizo (wanaongezeka tu)". Na mwenyezi Mungu hakufanya haya ila iwe bishara (habari ya furaha) na ili nyoyo zenu zituwe kwayo. Na hakuna msaada (wa kufaa) ila utokao kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu (na) Mwenye hikima. (8:9-10).

Ushindi wa Mitume na wafuasi wao haukupatikana ila kwa msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w). (vii) Mitume kutohitajia malipo kutoka kwa watu wao:

Mitume, tofauti na viongozi wengine waliojitokeza katika jamii mbalimbali, hawakuifanya kazi yao ya kuwaongoza watu katika njia ya Mwenyezi Mungu (s.w) kwa kutarajia maslahi yoyote si ya hali wala ya mali, kutoka kwa watu wao. Waliifanya kazi hiyo kama watumishi wa Mwenyezi Mungu (s.w) na ni yeye pekee waliyemtegemea awalipe kwa kazi hiyo. Daima walikuwa wakiwakumbusha watu wao jambo hili kama tunavyorejea katika Qur-an:

﴿وَمَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَىٰ رَبِّ الْعَالَمِينَ﴾

"Wala sikutakini juu yake ujira, ujira wangu hauko ila kwa (Mwenyezi Mungu) Mola wa walimwengu wote"(26:127)

Mitume wasingelikuwa wajumbe wa Mwenyezi Mungu (s.w) wenye uhakika wa kupata ujira mkubwa kwake kwa kazi yao, kitu gani kingeliwazuia wasitake malipo kutoka kwa watu wao, kama viongozi wa kawaida wa jamii za wanaadamu wanavyotaka malipo kutoka kwa watu wao?