MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU 0%

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU Mwandishi:
Kundi: Vitabu mbali mbali

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

Mwandishi: NDUGU ZETU WA KISUNNI
Kundi:

Matembeleo: 44527
Pakua: 3487

Maelezo zaidi:

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 22 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 44527 / Pakua: 3487
Kiwango Kiwango Kiwango
MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

Mwandishi:
Swahili

6

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

KUAMINI MALAIKA WA ALLAH (S.W.)

Malaika ni nani? Malaika ni katika waja na viumbe wa Allah(SW) walioumbwa kutokana na nuru. Tunafahamishwa katika hadithi ifuatayo kuwa: Aysha (r.a.) amesimulia kuwa Mtume(s.a.w.w) amesema:

Malaika wameumbwa na nuru na majini wameumbwa kutokana na ndimi za moto na Adamu ameumbwa kwa udongo kama ilivyoelezwa kwenu (katika Qur'an). (Muslim)

Na katika Qur'an tukufu,Allah(SW) anatubainishia kuwa, katika maumbile yao halisi, malaika ni viumbe wenye mbawa.

﴿الْحَمْدُ لِلَّـهِ فَاطِرِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ جَاعِلِ الْمَلَائِكَةِ رُسُلًا أُولِي أَجْنِحَةٍ مَّثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ يَزِيدُ فِي الْخَلْقِ مَا يَشَاءُ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴾

"Sifa zote njema ni za Allah,Muumba wa mbingu na ardhi. Aliyewafanya malaika kuwa wajumbe wenye mbawa mbili-mbili,na tatu tatu, na nne nne.Huzidisha katika kuumba apendavyo.Bila shaka ni mwenye uweza juu ya kila kitu" (35:1)

JE MALAIKA WANAISHI WAPI?

Katika Qur,an tunafahamishwa kuwa Malaika wanayo makazi maalumu lakini si hapa duniani. Allah(SW) anawanukuu malaika wakisema:

﴿وَمَا مِنَّا إِلَّا لَهُ مَقَامٌ مَّعْلُومٌ ﴿١٦٤﴾ وَإِنَّا لَنَحْنُ الصَّافُّونَ ﴿١٦٥﴾ وَإِنَّا لَنَحْنُ الْمُسَبِّحُونَ﴾

Hakuna yoyote miongoni mwetu ila anapo mahali pake mahususi. Na kwa yakini katika sisi wapo wajipangao safu. Na wako katika sisi wamtukuzao (Mwenyezi Mungu) (37:164-166)

Kutokana na kazi zao, Malaika wengi tunaishi nao humu humu duniani na wako nasi muda wote.Kila mtu ana malaika wawili wenye kuandika amali zake. Hakika juu yenu kuna wenye kuwatunza, malaika watukufu wenye kuandika.Wanayajua yote mnayoyatenda (82:10-12) Aidha, tunafahamishwa katika Qur,an kuwa kila mmoja wetu ana kundi la malaika mbele na nyuma yake. Ana (kila mtu) kundi (la malaika) mbele yake na nyuma yake.Wanamlinda kwa amri ya Mwenyezi Mungu. (13:11)

KWANINI HATUWAONI MALAIKA?

Pengine mtu aweza akauliza kuwa kama tumezungukwa na malaika mbele na nyuma, kulia na kushoto, kwanini basi hatuwaoni?

Jibu ni kwamba, mwanadamu yupo kwenye mtihani. Mtihani wenyewe ni kufanya mema kwa kutaraji malipo ya Allah(SW) na kuacha maovu kwa kuogopa adhabu zake.

﴿تَبَارَكَ الَّذِي بِيَدِهِ الْمُلْكُ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿١﴾ الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا وَهُوَ الْعَزِيزُ الْغَفُورُ ﴾

Ametukuka yule ambaye Mkononi mwake umo ufalme(wote); naye ni mwenye uweza juu ya kila kitu. Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni; ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Naye ni Mwenye nguvu na Mwenye msamaha (67:1-2)

Malaika ndio wasimamizi wa mtihani huu, na wamefanywa wasionekane machoni petu ili kila mtu atumie uhuru wake wa ama kumuogopa Allah(SW) kwa kutenda mema au kumkufuru Allah(SW) kwa kumuasi.

Lau malaika wangelionekana, watu wengi wangelitenda mema kinafiki(ria) badala ya kufanya kwa ikhilaswi. Mfano wake, ingekuwa kama vile watu wenye dhamira za kufanya uhalifu wanavyojidai watu wema pale wanapokuwepo askari waliovalia rasmi. Utendaji kazi wa malaika ni kama mashushushu au askari kanzu. Mtu muovu anapanga na kutenda maovu akidhani yupo peke yake,kumbe malaika wapo wanaandika.Na ndiyo maana muovu atakapoona kila jambo lake limerikodiwa, atashangaa siku ya kiama kuwa alijulikanaje?

﴿وَوُضِعَ الْكِتَابُ فَتَرَى الْمُجْرِمِينَ مُشْفِقِينَ مِمَّا فِيهِ وَيَقُولُونَ يَا وَيْلَتَنَا مَالِ هَـٰذَا الْكِتَابِ لَا يُغَادِرُ صَغِيرَةً وَلَا كَبِيرَةً إِلَّا أَحْصَاهَا وَوَجَدُوا مَا عَمِلُوا حَاضِرًا وَلَا يَظْلِمُ رَبُّكَ أَحَدًا﴾

Na madaftari yatawekwa mbele yao.Utawaona wabaya wanayaogopa kwasababu ya yale yaliyomo; na watasema: "Ole wetu! Namna gani madaftari haya! Haliachi dogo wala kubwa ila yamelidhibiti.Na watakuta yote yale waliyoyafanya yamehudhuria hapo; na Mola wako hamdhulumu yeyote(18:49)

Siku mtu atakapowaona malaika Kuna siku na muda maalumu ambapo kila mtu binafsi ataanza kuwaona malaika katika umbile lao halisi.

(a) Siku ya kukata roho Hii ni siku na saa ambayo dakika chache baada ya hapo mtu hukata roho na kuiaga dunia. Kwa watu wema, watakuja malaika wa kuwaliwaza:

﴿تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ﴿٣٠﴾ نَحْنُ أَوْلِيَاؤُكُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ﴾

......Hao huwateremkia Malaika "msigope wala msihuzunike, na furahini kwa pepo mliyokuwa mkiahidiwa. Sisi ni vipenzi vyenu katika maisha ya dunia na (huku) katika Akhera......"(41:30-31)

Watu wanaotenda maovu watapata mshituko mkubwa na kujawa na huzuni kubwa mno pale watakapowaona Malaika. Watasikitika sana kwa jinsi walivyokuwa wakijidanganya nafsi zao, wakatenda maovu kwa kudhania kuwa hakuna Malaika wanaorekodi matendo yao waliyokuwa wakiyafanya hadharani na mafichoni. Watafadhaika na kusema:

﴿حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ رَبِّ ارْجِعُونِ ﴿٩٩﴾ لَعَلِّي أَعْمَلُ صَالِحًا فِيمَا تَرَكْتُ كَلَّا إِنَّهَا كَلِمَةٌ هُوَ قَائِلُهَا ﴾

....Mola wangu! Nirudishe(duniani). Ili nifanye mema sasa badala ya yale niliyoyaacha. (Malaika watamwambia): "Hapana! Hakika hili ni neno tu analosema yeye(mtu muovu)....(23:99-100)

(b) Siku ya kiyama Kuanzia pale mtu anapowaona malaika hakutakuwa tena na kizuizi cha kutowaona kama ilivyokuwa hapa duniani. Kuonekana Malaika siku ya kiama itakuwa ni ishara mbaya kwa watu waovu kuwa umeshafika wakati wa wao kuhukumiwa na Allah (s.w) na kuanza kutumikia adhabu za kudumu katika Moto wa Jahannam. Qur'an inatufahamisha kuwa: Siku watakayowaona Malaika haitakuwa furaha siku hiyo kwa wenye makosa; na watasema:

﴿يَوْمَ يَرَوْنَ الْمَلَائِكَةَ لَا بُشْرَىٰ يَوْمَئِذٍ لِّلْمُجْرِمِينَ وَيَقُولُونَ حِجْرًا مَّحْجُورًا ﴾

"(Mungu) atuepushie mbali adhabu hii iliyotukabili (lakini haitawafaa kitu dua hiyo)(25:22)

(c) Motoni na Peponi Malaika watahudhuria katika uwanja wa hukumu siku ya Kiyama. Kila mtu atawaona wamejipanga safu wakisubiri amri ya Mwenyezi Mungu:

﴿يَوْمَ يَقُومُ الرُّوحُ وَالْمَلَائِكَةُ صَفًّا لَّا يَتَكَلَّمُونَ إِلَّا مَنْ أَذِنَ لَهُ الرَّحْمَـٰنُ وَقَالَ صَوَابًا﴾

Siku ambayo zitasimama Roho na Malaika safu safu; hatasema siku hiyo ila yule ambaye (Allah) Mwingi wa rehema amempa idhini, na atasema yaliyo sawa (78:38)

Wakipewa amri na Allah(s.w) malaika watawakamata waovu na kuwachungachunga kuelekea motoni kuadhibiwa.

﴿وَسِيقَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ جَهَنَّمَ زُمَرًا حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوهَا فُتِحَتْ أَبْوَابُهَا وَقَالَ لَهُمْ خَزَنَتُهَا أَلَمْ يَأْتِكُمْ رُسُلٌ مِّنكُمْ يَتْلُونَ عَلَيْكُمْ آيَاتِ رَبِّكُمْ وَيُنذِرُونَكُمْ لِقَاءَ يَوْمِكُمْ هَـٰذَا﴾

Na waliokufuru watapelekwa katika Jahannam makundi makundi mpaka watakapoifikia; itafunguliwa milango yake; walinzi wake(malaika) watawaambia: Je! hawakukujieni Mitume miongoni mwenu wakikusomeeni aya za Mola wenu na kukuonyeni juu ya makutano ya siku yenu hii(39: 71)

﴿وَسِيقَ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ إِلَى الْجَنَّةِ زُمَرًا حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوهَا وَفُتِحَتْ أَبْوَابُهَا وَقَالَ لَهُمْ خَزَنَتُهَا سَلَامٌ عَلَيْكُمْ طِبْتُمْ فَادْخُلُوهَا خَالِدِينَ﴾

Watu wema watasindikizwa na malaika mpaka kwenye pepo tukufu, na malaika wa huko watawakaribisha. Na walinzi wake(malaika) watawaambia: Amani juu yenu, furahini, na ingieni humu mkae milele(39:73)

SIFA ZA MALAIKA

Malaika Ni viumbe watiifu wasiomuasi Allah(SW) Malaika ni viumbe watiifu kwa Allah(SW). Wakipewa amri ya kumuadhibu mtu muovu,hawagomi wala kumuonea huruma mtu huyo.

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَائِكَةٌ غِلَاظٌ شِدَادٌ لَّا يَعْصُونَ اللَّـهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ﴾

Enyi mlioamini! Ziokoeni nafsi zenu na nafsi za watu wenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Juu yake kuna Malaika wakali wenye nguvu.Hawamuasi Allah(SW) katika yale anayowaamuru, na wanatekeleza vile walivyoamrishwa.(66:6)

WANA ELIMU YA KUTOSHA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO

Malaika wana elimu inayowawezesha kutekeleza majukumu yao bila ya kubabaisha. Elimu waliyopewa malaika ni sehemu ndogo sana katika ujuzi wa Allah (SW). Na wenyewe walikiri mbele ya Allah (SW):

﴿قَالُوا سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا إِنَّكَ أَنتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ﴾

Wakasema: Utukufu ni wako! Hatuna elimu ila ile uliyotufundisha, bila shaka wewe ndiye mjuzi na mwenye hekima (2:32)

HAWANA JINSIA

Malaika hawana jinsia ya kike wala ya kiume.Qur'an inawakosoa watu wanaodhani kuwa malaika ni wanawake. Inahoji:

﴿وَجَعَلُوا الْمَلَائِكَةَ الَّذِينَ هُمْ عِبَادُ الرَّحْمَـٰنِ إِنَاثًا أَشَهِدُوا خَلْقَهُمْ سَتُكْتَبُ شَهَادَتُهُمْ وَيُسْأَلُونَ﴾

Na wamewafanya malaika ambao ni waja wa Mwingi wa Rehma kuwa ni wanawake. Je wameshuhudia kuumbwa kwao (43:19).

NI VIUMBE WENYE MBAWA

﴿الْحَمْدُ لِلَّـهِ فَاطِرِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ جَاعِلِ الْمَلَائِكَةِ رُسُلًا أُولِي أَجْنِحَةٍ مَّثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ يَزِيدُ فِي الْخَلْقِ مَا يَشَاءُ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴾

"Sifa zote njema ni za Allah, Muumba wa mbingu na ardhi.Aliyewafanya malaika kuwa wajumbe wenye mbawa mbili-mbili, na tatu tatu, na nne nne. Huzidisha katika kuumba apendavyo.Bila shaka Allah ni mwenye uweza juu ya kila kitu". (35:1)

HUWEZA KUJIMITHILISHA UMBILE LA MWANADAMU

Malaika huweza kujimithilisha kuwa kama wanadamu. Hufanya hivyo pale wanapotumwa na Allah (SW) kuleta ujumbe kwa watu maalumu. Kwa mfano, Bibi Maryam, mama yake nabii Isa(a.s) , alijiwa na malaika katika umbo mithili ya mwanaume:

﴿وَاذْكُرْ فِي الْكِتَابِ مَرْيَمَ إِذِ انتَبَذَتْ مِنْ أَهْلِهَا مَكَانًا شَرْقِيًّا ﴿١٦﴾ فَاتَّخَذَتْ مِن دُونِهِمْ حِجَابًا فَأَرْسَلْنَا إِلَيْهَا رُوحَنَا فَتَمَثَّلَ لَهَا بَشَرًا سَوِيًّا﴾

Na mtaje katika kitabu, Maryam, alipojitenga na watu wake katika upande wa mashariki. Tukampelekea Muhuisha sharia Yetu (Jibril) akajimithilisha kwake kwa sura ya binaadamu aliye kamilifu. (19:16-17)

LENGO LA KUUMBWA MALAIKA

Lengo la kuumbwa malaika ni kumtumikia Allah(SW). Katika kutekeleza lengo la kuumbwa kwao, malaika hawana hiyari katika kutekeleza amri za Allah(SW), hufanya mambo yote vile anavyotaka Allah(SW).

﴿لَّا يَعْصُونَ اللَّـهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ﴾

..Hawamuasi Allah(SW) katika yale anayowaamuru, na wanatekeleza vile walivyoamrishwa.(66:6)

KAZI ZA MALAIKA

Malaika wamepewa kazi ya kumtumikia Allah(SW) kwa kumtukuza na kumtakasa, kama wanavyosema wenyewe:

﴿وَمَا مِنَّا إِلَّا لَهُ مَقَامٌ مَّعْلُومٌ ﴿١٦٤﴾ وَإِنَّا لَنَحْنُ الصَّافُّونَ ﴿١٦٥﴾ وَإِنَّا لَنَحْنُ الْمُسَبِّحُونَ﴾

Hakuna yoyote miongoni mwetu ila anapo mahali pake mahususi. Na kwa yakini katika sisi wapo wajipangao safu. Na wako katika sisi wamtukuzao (Mwenyezi Mungu) (37:164-166)

MALAIKA PIA HUSHUGHULIKIA MAMBO YA WANADAMU KATIKA MAISHA YA DUNIANI NA AKHERA

Miongoni mwa mambo hayo ni:

(1) KULETA UJUMBE KWA WANAADAMU KUTOKA KWA ALLAH (SW)

Kazi ya kwanza ya malaika ni kuleta ujumbe wa Allah(SW) kwa wanadamu. Ujumbe huo huweza kuwa ni mwongozo wa maisha(Wahy) au habari juu ya jambo fulani. Malaika hupeleka ujumbe wa Allah(SW) kwa mitume au watu wa kawaida. Huteremka Malaika na wahy kwa amri yake juu ya anaowataka katika waja wake kuwa

﴿ أَنْ أَنذِرُوا أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاتَّقُونِ﴾

"onyeni kuwa hakuna wa kuabudiwa isipokuwa Mimi, basi niogopeni" (16:2)

Jibril, ambaye ndiye mkuu wa Malaika, ndiye mjumbe mkuu aliyekuwa akiwaletea Mitume wote Wahyi. Yeye ni mwalimu mkuu aliyeteuliwa na Allah(SW) kuwafunza mitume namna ya kuwalingania watu Uislamu kwa maneno na matendo.

﴿إِنَّهُ لَقَوْلُ رَسُولٍ كَرِيمٍ ﴿١٩﴾ ذِي قُوَّةٍ عِندَ ذِي الْعَرْشِ مَكِينٍ﴾

Hakika hii Quran ni neno lililoletwa na mjumbe mtukufu, malaika mwenye nguvu na hadhi kubwa kwa Mwenyezi Mungu.(81:19-20)

(2) KUANDIKA AMALI ZA WANAADAMU NJEMA NA MBAYA

Kila mtu ana malaika waandishi wawili, kulia na kushoto kwake. Unaposema au kutenda jema au baya hadharani au umejificha peke yako, malaika hawa wanakuona na kurekodi jambo hilo.

﴿إِذْ يَتَلَقَّى الْمُتَلَقِّيَانِ عَنِ الْيَمِينِ وَعَنِ الشِّمَالِ قَعِيدٌ ﴿١٧﴾ مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ﴾

Wanapopokea wapokeaji wawili, anayekaa kuliani na anayekaa kushotoni. Hatoi (mtu)kauli yoyote isipokuwa karibu naye yupo mngojeaji(malaika) tayari (kuandika.) (50:17-18).

(3) KUWALINDA WANAADAMU

Qur'an inatufahamisha Kazi ya tatu ya malaika ni kumchunga na kumlinda kila mtu na vitu vya hatari vilivyo nje ya uwezo wake.

﴿لَهُ مُعَقِّبَاتٌ مِّن بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ يَحْفَظُونَهُ مِنْ أَمْرِ اللَّـهِ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ وَإِذَا أَرَادَ اللَّـهُ بِقَوْمٍ سُوءًا فَلَا مَرَدَّ لَهُ وَمَا لَهُم مِّن دُونِهِ مِن وَالٍ﴾

Ana (kila mtu) kundi (la malaika) mbele yake na nyuma yake. Wanamlinda kwa amri ya Mwenyezi Mungu.Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko nafsini mwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo katika nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu anapowatakia watu adhabu, hakuna cha kuzuia wala hawana mlinzi yeyote badala yake Mwenyezi Mungu (13:11)

Kwa ulinzi huu wa malaika utokao kwa Allah(SW), mtu hata kama atachukiwa na dunia nzima na kwahiyo wakafanya njama za kutaka kumdhuru, hawataweza mpaka Allah(SW) aondoe ulinzi wake.Vivyo hivyo, kama Allah(SW)atauondoa ulinzi wake huu kwa mtu, hakuna wa kumkinga na shari hata kama atalindwa na mitambo madhubuti ya kisasa pamoja na wataalamu wa ulinzi wa ulimwengu mzima.

(4) KUWAOMBEA WAUMINI MSAMAHA KWA ALLAH (S.W.)

Malaika pia wana kazi ya kumwomba Allah(SW) awasamehe wale watu wanaotubia na kufuatisha vitendo vyema.Humwomba Allah (SW) awasamehe, afute makosa yao, awarehemu kwa kuwalipa pepo na kuwaepusha na adhabu ya Moto.

"Wale wanaokichukua kiti cha enzi (cha Mwenyezi Mungu) na wale wanaokizunguka, wanamtukuza Mola wao na kumsifu na wanamuamini na wanawaombea msamaha waliaomini (Wanasema):

﴿رَبَّنَا وَأَدْخِلْهُمْ جَنَّاتِ عَدْنٍ الَّتِي وَعَدتَّهُمْ وَمَن صَلَحَ مِنْ آبَائِهِمْ وَأَزْوَاجِهِمْ وَذُرِّيَّاتِهِمْ إِنَّكَ أَنتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ﴾

"Mola wetu! Umekienea kila kitu kwa rehema na Elimu. Basi wasamehe waliotubu na kufuata njia yako na waepushe na adhabu ya Jahannam"(40:8)

Na Mwenyezi Mungu anaahidi kuwa wale wanaotubu kwa kujuta juu ya maovu waliyofanya, wakamuamini Yeye ipasavyo, kwa kujizuia kuyaendea maovu na badala yake wakashikamana na mwenendo mwema; Atabadilisha maovu yao kuwa mema! Qur'an inathibitisha hili katika aya ifuatayo, inasema:

﴿إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ يُبَدِّلُ اللَّـهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا﴾

Ila yule atakayetubia na kuamini na kufanya vitendo vizuri; basi hao ndio Mwenyezi Mungu atawabadilishia maovu yao kuwa mema, na mwenyezi Mungu ni mwingi wa kusamehe na Mwingi wa kurehemu.(25:70)

(5) KUWASAIDIA WAUMINI VITANI KATIKA KUPAMBANA NA MADHALIMU

Miongoni mwa kazi tukufu za malaika ni kuwasaidia waislamu kupambana na maadui wenye nguvu kubwa kijeshi katika vita. Qur'an inatueleza kuwa:

﴿بَلَىٰ إِن تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا وَيَأْتُوكُم مِّن فَوْرِهِمْ هَـٰذَا يُمْدِدْكُمْ رَبُّكُم بِخَمْسَةِ آلَافٍ مِّنَ الْمَلَائِكَةِ مُسَوِّمِينَ﴾

Naam.Kama mtasubiri na kujilinda na makatazo yake(Allah) na maadui wakakufikieni kwa ghafla, hapo Mola wenu atakusaidieni kwa Malaika elfu tano washambuliao kwa nguvu(3:125)

(6) KUWAANGAMIZA WATU WAOVU WALIOPINDUKIA MIPAKA

Malaika pia wana kazi ya kuwaangamiza watu waovu waliokubuhu na kupindukia mipaka. Watu wa nabii Lut waliangamizwa na Malaika baada ya kubobea katika maovu na kukataa kwao kujirekebisha. Tunafahamishwa hili pale malaika walipomjibu nabii Ibrahiimu(as) Wakasema:

﴿قَالُوا إِنَّا أُرْسِلْنَا إِلَىٰ قَوْمٍ مُّجْرِمِينَ ﴿٥٨﴾ إِلَّا آلَ لُوطٍ إِنَّا لَمُنَجُّوهُمْ أَجْمَعِينَ﴾

"Hakika sisi tumetumwa kwa wale watu wakosa (tuwaangamize) Isipokuwa waliomfuata Lut.Bila shaka sisi tutawaokoa wote hao (15:58-59)

(7) KUTOA ROHO ZA WATU

Kuna malaika wengi wanaohusika na utoaji wa roho za wanadamu wakati muda wao wa kuishi duniani unapokamilika. Malaika mkuu wa kazi hii ni Malakul-mauti:

﴿قُلْ يَتَوَفَّاكُم مَّلَكُ الْمَوْتِ الَّذِي وُكِّلَ بِكُمْ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُمْ تُرْجَعُونَ﴾

Atakufisheni Malaika wa mauti aliyewakilishwa kwenu, kisha mtarejeshwa kwa Mola wenu (32:11)

(8) KUWALIWAZA NA KUWAKARIBISHA WATU WEMA PEPONI KABLA YA KUTOLEWA ROHO

kila mtu aliyetenda mema na kutofanya maovu atashukiwa na malaika wa kumliwaza. Watamwambia:

﴿يَا أَيَّتُهَا النَّفْسُ الْمُطْمَئِنَّةُ ﴿٢٧﴾ ارْجِعِي إِلَىٰ رَبِّكِ رَاضِيَةً مَّرْضِيَّةً ﴿٢٨﴾ فَادْخُلِي فِي عِبَادِي ﴿٢٩﴾ وَادْخُلِي جَنَّتِي﴾

Ewe nafsi yenye kutulia! Rudi kwa Mola wako hali ya kuwa utaridhika Naye amekuridhia. Basi ingia katika kundi la waja (wazuri) uingie katika pepo yangu.(89:27-30).

﴿وَسِيقَ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ إِلَى الْجَنَّةِ زُمَرًا حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوهَا وَفُتِحَتْ أَبْوَابُهَا وَقَالَ لَهُمْ خَزَنَتُهَا سَلَامٌ عَلَيْكُمْ طِبْتُمْ فَادْخُلُوهَا خَالِدِينَ﴾

Na siku ya Kiama watawapokea na kuwakaribisha kwenye pepo ya Allah (SW) yenye neema za kudumu. Watawaambia: Amani juu yenu, furahini, na ingieni humu mkae milele (39:73)

(9) KUWAADHIBU WATU WAOVU MOTONI

Watu wanaotenda maovu watakuwa katika adhabu kali kwenye Moto wa Jahannam. Mwenyezi Mungu amewaweka malaika maalumu kwa ajili ya kuwaadhibu watu waovu wasiotaka kutubia, kujirekebisha wala kutenda mema. Allah (SW) anamtangazia kila mtu mwenya tabia hizi kuwa:

﴿سَأُصْلِيهِ سَقَرَ ﴿٢٦﴾ وَمَا أَدْرَاكَ مَا سَقَرُ ﴿٢٧﴾ لَا تُبْقِي وَلَا تَذَرُ ﴿٢٨﴾ لَوَّاحَةٌ لِّلْبَشَرِ ﴿٢٩﴾ عَلَيْهَا تِسْعَةَ عَشَرَ﴾

Karibuni hivi nitamtia katika Moto.Na ni nini kitakachokujulisha Moto huo? Haubakizi wala hausazi, unababua ngozi mara moja.Juu yake wako malaika (walinzi) kumi na tisa.(74:26-30).

Mkuu wa malaika hawa wa adhabu katika Jahannam ni Malik. Kutokana na machungu ya adhabu watakayopata, watu waovu watalia na kutamani mauti, watamtaka Malik amwombe Allah (SW) awafishe kuliko hiyo adhabu inayowakabili:

﴿ وَنَادَوْا يَا مَالِكُ لِيَقْضِ عَلَيْنَا رَبُّكَ قَالَ إِنَّكُم مَّاكِثُونَ﴾

Nao watapiga kelele: watasema: "Ewe Malik!Na atufishe Mola wako! (Maliki) atasema: "Kwa hakika mtakaa humu humu"(43:77)

Na Mwenyezi Mungu anasifu kuwa adhabu watakayotoa malaika hao kutokana na uwezo aliowapa haitakuwa na mfano wake katika adhabu hizi za duniani.

Siku hiyo mwanadamu atakumbuka, lakini kukumbuka huko kutamfaa nini.Atasema:

﴿وَجِيءَ يَوْمَئِذٍ بِجَهَنَّمَ يَوْمَئِذٍ يَتَذَكَّرُ الْإِنسَانُ وَأَنَّىٰ لَهُ الذِّكْرَىٰ ﴿٢٣﴾يَقُولُ يَا لَيْتَنِي قَدَّمْتُ لِحَيَاتِي ﴿٢٤﴾ فَيَوْمَئِذٍ لَّا يُعَذِّبُ عَذَابَهُ أَحَدٌ ﴿٢٥﴾ وَلَا يُوثِقُ وَثَاقَهُ أَحَدٌ﴾

"Laiti ningalitanguliza(wema) kwa ajili ya uhai wangu (huu wa leo). Basi adhabu ya(Allah) siku hiyo, haitolingana na adhabu aitoayo yeyote (katika wanadamu).Wala hatafunga yeyote jinsi ya kifungo chake (Allah) (89:23-26).

Taathira ya Imani ya Malaika katika maisha ya kila siku Kuamini Malaika ni imani ambayo pindi ikithibiti vema moyoni, huleta taathira kubwa sana katika maisha ya kila siku na hivyo kubadili kabisa tabia na mwenendo wa Muumini. Hii ni kwa sababu:

1. Imani ya kweli juu ya Malaika humuepusha Muumini na kumshirikisha Allah (s.w) na viumbe vyake, hasa vile visivyoonekana, miongoni mwa hivyo ni Malaika na Majini.

2. Muislamu anaamini kuwa Malaika ni viumbe watukufu ambao wametakasika na dhambi na kila aina ya uchafu, lakini binaadamu amepewa daraja ya juu zaidi pindi atakapotimiza wajibu wake kama Khalifa wa Allah (s.w) hapa duniani. Imani hii humpelekea mtu kujitahidi upeo wa uwezo wake kuishi maisha yanayolingana na cheo hiki kikubwa, cheo ambacho Malaika walikitamani (Rejea Qur-an, 2:30)..

3. Muislam anaamini kuwa kila wakati na kila alipo yu pamoja na Malaika watukufu.Imani hii peke yake inatosha kumfanya mtu abadili tabia yake. Hii ni kwa sababu binaadamu ameumbwa na haya, kwa hiyo huhuzunika akifanya mambo maovu mbele ya watu na hasa mbele ya watu anaowaheshimu.

4. Muislamu anaamini kuwa Malaika hao sio tu kuwa wapo naye daima bali wanahudhurisha mbele ya Allah (s.w) kila anachokitenda. Imani hii ikithibiti moyoni humfanya Muislam ajitahidi kufanya mambo mema na ajitahidi kuepuka maovu.

5. Muislamu anajua kuwa Malaika sio tu hupendezwa na mema, bali pia humuombea mtu huyo anayefanya mema, maghfira kwa Allah (s.w) jambo ambalo humzidishia Muislamu hima ya kutenda mema daima na kujiepusha na maovu hata akiwa peke yake.

KUAMINI VITABU VYA ALLAH (S.W)

Mtu hawi Muumini wa kweli mpaka awe na yakini juu ya vitabu vya Allah (s.w). Vitabu vya Allah (s.w) vimeshushwa kupitia kwa Mitume mbali mbali.

﴿لَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا بِالْبَيِّنَاتِ وَأَنزَلْنَا مَعَهُمُ الْكِتَابَ وَالْمِيزَانَ لِيَقُومَ النَّاسُ بِالْقِسْطِ﴾

"Kwa hakika tuliwapeleka Mitume wetu kwa dalili wazi wazi na tukaviteremsha Vitabu na uadilifu pamoja nao, ili watu wasimamie uadilifu..." (57:25).

Vitabu vya Allah (s.w) ni vingi lakini tunavyovifahamu ni vile vilivyotajwa katika Qur-an kama ifuatavyo:

(1) Suhufi kwa Ibrahimu(a.s)

(2) Taurati kwa Mussa(a.s)

(3) Zabri kwa Daud(a.s)

(4) Injili kwa Issa(a.s)

(5) Qur-an kwa Muhammad(s.a.w.w)

Lengo la kushushwa Vitabu vya Allah (s.w) Iimebainishwa wazi katika Qur-an kuwa vitabu vya Allah (s.w) vimeshushwa kupitia kwa Mitume wake ili kuwaongoza wanaadamu katika njia iliyonyooka. Njia iliyonyooka ni ile inayomuwezesha mwanaadamu kumuabudu Allah (s.w) katika kila kipengele cha maisha yake kwa kipindi chote cha uhai wake hapa ulimwenguni. Allah (s.w) amechukua ahadi ya kuwaletea watu mwongozo tangu awali pale alipowashusha wazazi wetu, Adamu(a.s) na mkewe (Hawwah) hapa ardhini kama tunavyojifunza katika Qur-an:

﴿قُلْنَا اهْبِطُوا مِنْهَا جَمِيعًا فَإِمَّا يَأْتِيَنَّكُم مِّنِّي هُدًى فَمَن تَبِعَ هُدَايَ فَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ ﴿٣٨﴾ وَالَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ﴾

"Tukasema, shukeni humo nyote, na kama ukikufikieni uwongozi utokao kwangu, basi watakaoufuata uwongozi wangu huo haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika. Lakini wenye kukufuru na kuyakadhibisha maneno yetu, hao ndio watakaokuwa watu wa Motoni, humo watakaa milele". (2:38-39).

Ahadi hii ameitekeleza Allah (s.w) kwa kuwaleta Mitume mbali mbali baada ya Adamu (a.s) na kuwashushia vitabu vyenye Uongozi na nuru. Qur-an inasisitiza:

﴿إِنَّا أَنزَلْنَا التَّوْرَاةَ فِيهَا هُدًى وَنُورٌ﴾

"Hakika tuliteremsha Taurat yenye Uongozi na Nuru.." (5:44)

﴿وَقَفَّيْنَا عَلَىٰ آثَارِهِم بِعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ مُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ مِنَ التَّوْرَاةِ وَآتَيْنَاهُ الْإِنجِيلَ فِيهِ هُدًى وَنُورٌ﴾

"Na tukawafuatishia (Mitume hao) Issa bin Maryam kuyahakikisha yaliyokuwa kabla yake katika Taurat, na tukampa Injili iliyomo ndani yake Uongozi na nuru." (5:46)

﴿شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ﴾

"Ni mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa katika (mwezi) huo (hii) Qur-an ili iwe Uongozi kwa watu na hoja zilizo wazi za Uongozi wa upambanuizi..." (2:185)

Haja ya Mwongozo kutoka kwa Allah (s.w) Mwanaadamu pamoja na elimu aliyotunukiwa, hana uwezo pasina msaada wa muumba wake, kupata majibu sahihi ya maswali ya msingi ya maisha yake hapa duniani na huko akhera. Maswali haya ya msingi ni:

1. Nani chanzo cha maumbile yote?

2. Ni lipi lengo la mwanaadamu hapa ulimwenguni?

3. Atalifikiaje lengo hilo?

4. Ni ipi nafasi halisi ya mwanaadamu hapa ulimwenguni?

5. Ni ipi hatma yake baada ya kufa, je kufa ndio mwisho wa maisha yake?

Mwanaadamu bila ya mwongozo kutoka kwa muumba wake hana uwezo wa kutoa majibu sahihi ya maswali haya. Elimu ya mazingira aliyonayo mwanaadamu ni finyu mno kiasi kwamba haimuwezeshi hata kuijua roho yake kama tunavyokumbushwa katika Qur-an:

﴿وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الرُّوحِ قُلِ الرُّوحُ مِنْ أَمْرِ رَبِّي وَمَا أُوتِيتُم مِّنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا﴾

"Na wanakuuliza habari ya roho.Sema: "Roho ni jambo lililohusika na Mola wangu. Nanyi hamkupewa katika elimu ila kidogo kabisa" (17:85)

Maana ya Kuamini Vitabu vya Allah Imani ya kweli katika Uislamu haishii moyoni tu bali ni lazima idhihirishwe katika matendo ya kila siku. Hivyo, waumini wa kweli wa vitabu vya Allah (s.w) ni wale wanaoendesha maisha yao ya kila siku katika kila kipengele kwa kufuata bara bara maongozi ya vitabu vya Allah (s.w). Kabla ya Qur-an kushushwa, waumini wa kweli wa vitabu vya Allah vilivyotangulia, vikiwemo Taurat, Injili, Zaburi, n.k. ni wale walioishi kwa mujibu wa maongozi ya vitabu hivyo kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:

﴿إِنَّا أَنزَلْنَا التَّوْرَاةَ فِيهَا هُدًى وَنُورٌ يَحْكُمُ بِهَا النَّبِيُّونَ الَّذِينَ أَسْلَمُوا لِلَّذِينَ هَادُوا وَالرَّبَّانِيُّونَ وَالْأَحْبَارُ بِمَا اسْتُحْفِظُوا مِن كِتَابِ اللَّـهِ وَكَانُوا عَلَيْهِ شُهَدَاءَ فَلَا تَخْشَوُا النَّاسَ وَاخْشَوْنِ وَلَا تَشْتَرُوا بِآيَاتِي ثَمَنًا قَلِيلًا وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ﴾

"Hakika tuliteremsha Taurati yenye uwongozi na nuru; ambayo kwayo Manabii waliojisalimisha (kwa Allah) waliwahukumu Mayahudi; Watawa na Maulamaa pia (walihukumu kwa hiyo Taurat); kwa sababu walitakiwa kuhifadhi kitabu hicho cha Allah; Nao walikuwa mashahidi juu yake. Basi, msiwaogope watu, bali niogopeni (Mimi). Wala msibadilishe Aya zangu kwa thamani chache (ya maslahi ya dunia).Na wasiohukumu kwa yale aliyoteremsha Allah, basi Hao ndio makafiri." (5:44)

﴿وَلْيَحْكُمْ أَهْلُ الْإِنجِيلِ بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فِيهِ وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ﴾

"Watu wa Injili wahukumu kwa yale aliyoteremsha Allah ndani yake.Na wasiohukumu kwa (kufuata) yale aliyoteremsha Allah, basi hao ndio mafasiki (maasi)" (5:47)

Baada ya Qur-an kushushwa kupitia kwa Mtume Muhammad(s.a.w.w) kwa ajili ya walimwengu wote, Waumini wa kweli wa vitabu vya Allah (s.w) ni wale wanaoishi kwa kufuata maongozi ya Qur-an na Sunnah ya Mtume Muhammad(s.a.w.w) katika maisha yao yote. Si muumini yule anayeikataa Qur-an na Mtume aliyeshushiwa hatakama anadai kuwa anaiamini Taurat, Zabur, Injili, n.k. na Mitume walioshushiwa vitabu hivyo kwa mujibu wa aya ifuatayo:

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا آمِنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِي نَزَّلَ عَلَىٰ رَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِي أَنزَلَ مِن قَبْلُ وَمَن يَكْفُرْ بِاللَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا﴾

"Enyi mlioamini! Mwaminini Allah na Mtume wake na kitabu alichokiteremsha juu ya Mtume wake,na vitabu alivyoviteremsha zamani. Na mwenye kumkanusha Allah na Malaika wake na vitabu vyake, na Mitume wake na siku ya mwisho, basi bila shaka amepotea upotofu uliombali (na haki)" (4:136)

Hivi sasa, katika vitabu vya Allah (s.w) vilivyoshushwa hapa ulimwenguni, ni Qur-an pekee iliyobakia katika lugha yake ya asili (Kiarabu fasaha) na katika usahihi wake wa asili. Vitabu vilivyoitangulia Qur-an vinakabiliwa na matatizo makubwa mawili yafuatayo:

1. Lugha zilizotumika katika vitabu hivyo zimekufa (zimetoweka). Kwa mujibu wa Qur-an kila Mtume alilepewa wahay kwa lugha ya watu wake

﴿وَمَا أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا بِلِسَانِ قَوْمِهِ لِيُبَيِّنَ لَهُمْ﴾

"Na hatukumpeleka Mtume yeyote isipokuwa kwa lugha ya watu wake ili apate kuwabainishia..." (14:4).

Tunajua kutokana na historia kuwa lugha hukua na kufa. Hivi sasa kwa mfano Allah (s.w) akituletea kitabu alichoshushiwa Nabii Adam(a.s) katika lugha aliyozungumza Adam(a.s) na wanawe wa karibu wa wakati ule, hatuwezi kupata ujumbe wake.

2. Vitabu vilivyoitangulia Qur-an viliingizwa mikono ya watu, vikabadilishwa na kupotoshwa ili kukidhi matashi ya watu waliodai kufuata vitabu hivyo kinyume na Allah (s.w). Taurat, Zabur, Injili, n.k. Vilikumbwa na tatizo hili.

Qur-an imeepukana na matatizo haya kwani hivi leo, Lugha ya Kiarabu, ni miongoni mwa lugha kubwa zinazokua kwa kasi; pia Kiarabu ni lugha fasaha na tajiri kwa maneno kuliko lugha zote duniani. Pia Qur-an tofauti na vitabu vingine vya Allah (s.w), haitaingiliwa na mkono wa mtu, kwani imepewa hifadhi na Allah (s.w) mwenyewe:

﴿نَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ﴾

Hakika sisi ndio tulioteremsha mawaidha haya (hii Qur-an) na hakika Sisi ndio tutakao yalinda" (15:9).

﴿لَّا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِ تَنزِيلٌ مِّنْ حَكِيمٍ حَمِيدٍ﴾

"Haitakifikia batili mbele yake wala nyumba yake; kimeteremshwa na Mwenye Hikma Ahimidiwaye." (41:42).

Hivyo hivi sasa, Muumini wa kweli wa vitabu vya Allah (s.w) ni yule:

1. Anayeamini pasi na tone la shaka kuwa Qur-an yote kama msahafu ulivyo kuanzia sura ya kwanza (Al-Faatiha) mpaka sura ya mwisho (An-Naas) ni maneno kutoka kwa Allah (s.w). Muumini anayakinisha kuwa:

﴿ذَٰلِكَ الْكِتَابُ لَا رَيْبَ فِيهِ هُدًى لِّلْمُتَّقِينَ﴾

"Hiki ni kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake, ni uwongozi kwa wamchao Allah" (2:2)

2. Anayaongoza maisha yake ya kila siku kwa kufuata Qur'an na mwenendo au sunnah ya mfasiri wa Qur-an, Mtume Muhammad(s.a.w.w). Qur-an yenyewe inasisitiza:

﴿وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا﴾

"Haiwi kwa mwanamume aliyeamini wala kwa mwanamke aliyeamini, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapokata shauri, wawe na hiari katika shauri lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hakika amepotea upotofu ulio wazi (kabisa)." (33:36)

﴿وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ﴾

"...Na wasiohukumu kwa yale aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri". (5:44)

﴿وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ﴾

"... Na wasiohukumu kwa yale aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio madhalimu" (5:45) lengo-2 166 1/18/10, 12:28 PM 167

﴿وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ﴾

"... Na wasiohukumu kwa yale aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio mafasiki (maasi)" (5:47)

KUAMINI MITUME WA ALLAH (S.W)

Mtu hawi Muumini wa kweli mpaka awe na yakini juu ya Mitume wa Allah (s.w) kama tunavyojifunza katika Qur-an: "Semeni nyinyi (Waislamu kuwaambia Mayahudi na Wakristo kuwa):"Tumemwamini Mwenyezi Mungu na yale tuliyoteremshiwa, na yale yaliyoteremshwa kwa Ibrahimu, na Ismail na Is-haqa na Yaaqubu na kizazi (chake Yaaqubu); na waliyopewa Manabii (wengine) kutoka kwa Mola wao; hatutafautishi baina ya yoyote katika hao.(Wote tunawaamini), na sisi tumenyenyekea kwake." (2:136) Kuamini baadhi ya Mitume wa Mwenyezi Mungu na kuwakanusha wengine kama walivyo fanya mayahudi na Wakristo ni Ukafiri kama tunavyojifunza katika Qur-an:

﴿إِنَّ الَّذِينَ يَكْفُرُونَ بِاللَّـهِ وَرُسُلِهِ وَيُرِيدُونَ أَن يُفَرِّقُوا بَيْنَ اللَّـهِ وَرُسُلِهِ وَيَقُولُونَ نُؤْمِنُ بِبَعْضٍ وَنَكْفُرُ بِبَعْضٍ وَيُرِيدُونَ أَن يَتَّخِذُوا بَيْنَ ذَٰلِكَ سَبِيلًا ﴿١٥٠﴾ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ حَقًّا وَأَعْتَدْنَا لِلْكَافِرِينَ عَذَابًا مُّهِينًا ﴿١٥١﴾ وَالَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَرُسُلِهِ وَلَمْ يُفَرِّقُوا بَيْنَ أَحَدٍ مِّنْهُمْ أُولَـٰئِكَ سَوْفَ يُؤْتِيهِمْ أُجُورَهُمْ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا﴾

"Hakika wale wanaomkanusha Mwenyezi Mungu na Mitume yake, na wanataka kutenga baina ya Mwenyezi Mungu na Mitume yake, kwa kusema: "Wengine tunawaamini na wengine tunawakataa," na wanataka kushika njia iliyo kati kati ya haya (si ya Kiislamu khasa wala ya Kikafiri).Hao ndio Makafiri kweli.Na tumewaandalia makafiri adhabu idhalilishayo.Na waliomwamini Mwenyezi Mungu na Mitume yake wala wasimfarikishe yoyote katika wao (bali wamewaamini wote), hao atawapa ujira wao.Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa kurehemu." (4:150-152).

Mitume wa Allah (s.w) ni wengi sana kama inavyobainishwa katika Qur-an:

﴿وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلًا مِّن قَبْلِكَ مِنْهُم مَّن قَصَصْنَا عَلَيْكَ وَمِنْهُم مَّن لَّمْ نَقْصُصْ عَلَيْكَ﴾

"Na kwa yakini tuliwatuma mitume kabla yako (Muhammad).Wengine katika hao tumekusimulia (majina yao na habari zao) na wengine hatukukusimulia..." (40:78)

Mitume waliosimuliwa katika Qur-an ni hawa ishirini na tano (25) wafuatao:

1. Adam(a.s)

2. Idrisa (Enock)(a.s)

3. Nuhu (Noah)(a.s)

4. Hud (Heber)(a.s)

5. Salih (Metheusaleh)(a.s)

6. Ibrahim (Abrahim)(a.s)

7. Lut (Lot) (a.s)

8. Ismail (Ismael)(a.s)

9. Is-haq (Isaac)(a.s)

10. Yaaqub (Jacob)(a.s)

11. Yusuf (Joseph)(a.s)

12. Shu'aib (Jethro)(a.s)

13. Ayyub (Job)(a.s)

14. Mussa (Moses)(a.s)

15. Harun (Aaron)(a.s)

16. Dhul kifl (Ezekiel)(a.s)

17. Daud ( David)(a.s)

18. Sulayman (Solomon)(a.s)

19. Ilyaas (Elias)(a.s)

20. Al - Yassa' (Elisha)(a.s)

21. Yunus (Johah)(a.s)

22. Zakariya (Zechariah)(a.s)

23. Yahya (John the Baptist)(a.s)

24. Isa (Jesus)(a.s)

25. Muhammad(s.a.w.w)

LENGO LA KULETWA MITUME WA ALLAH (S.W)

Mitume wameletwa kuwa Waalimu na viongozi wa kuwafundisha watu Uislamu na kuwaelekeza kuusimamisha Uislamu katika jamii kinadharia na kimatendo kama tunavyojifunza katika Qur-an:

﴿ لَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا بِالْبَيِّنَاتِ وَأَنزَلْنَا مَعَهُمُ الْكِتَابَ وَالْمِيزَانَ لِيَقُومَ النَّاسُ بِالْقِسْطِ﴾

"Kwa hakika Tuliwapeleka Mitume wetu kwa dalili wazi wazi na Tukaviteremsha vitabu na Uadilifu (mizani) pamoja nao, ili watu wasimamie uadilifu. (57:25)

﴿ هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ﴾

"Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na kwa dini ya haki ili kuifanya ishinde dini zote, ijapokuwa washirikina watachukia." (9:33, 61:9)

MWISHO WA UTUME

Maswali ambayo huweza kuulizwa ni: Kwa nini wahyi ukatike?Kwa nini Mitume wasiendelee kuletwa hadi kiyama? Kwa nini Muhammad(s.a.w.w) afunge mlango wa Utume? Ili kulielewa vizuri suala hili la mwisho wa Utume yafaa kwanza tuzingatie kuwa kilicho muhimu na cha msingi kabisa kwa Mtume yeyote si kule kuwepo kimwili bali ni kule kuufikisha kwake ujumbe aliopewa na Mwenyezi Mungu (s.w) ili watu wake wasiwe na hoja tena iwapo watachagua kupotea. Na lau ingekuwa lililo muhimu kwa Mtume ni kule kuwapo kimwili basi Mwenyezi Mungu angelimpeleka Mtume mara tu baada ya kufariki Mtume aliyetangulia.

Kilicho cha msingi ni mafundisho aliyokuja nayo.Maadamu ujumbe aliouleta uko hai basi Mtume huyo yu hai. Hivyo kifo halisi cha Mtume ni kule kupotea kwa mafundisho aliyoyaleta. Mitume wote waliomtangulia Muhammad(s.a.w.w) mafundisho yao yalipotea, kwani yalichanganyika na hekaya mbali mbali. Katika vitabu vilivyoitangulia Qur-an, kwa mfano Taurat, Injil, na Zaburi hakuna hata kimoja ambacho kipo katika hali ya usahihi wake wa asili. Hata wafuasi wa vitabu hivyo wanakiri kuwa nakala walizonazo leo si zile walizopewa Mitume. Si hivyo tu bali hata historia za maisha ya Mitume waliomtangulia Muhammad(s.a.w.w) zimechanganywa na ngano za kushtusha kabisa, hata inakuwa vigumu kupambanua haki na batili.

Kinyume chake mafundisho aliyokuja nayo Muhammad(s.a.w.w) yako hai kabisa na hayajaharibiwa na katu hayawezi kuharibiwa.Qur-an, kitabu alichoteremshiwa kipo tena katika lugha ile ile ya asili bila ya kupunguza wala kuzidisha japo nukta moja. Historia kamili ya maisha yake, maneno yake, maagizo yake, vitendo vyake, vyote vimehifadhiwa kwa usahihi kabisa kiasi ambacho karne 14 zimepita lakini bado historia yake ni ya wazi na kamili kama kwamba tunamuona kwa macho yetu. Katika kila kipengele cha maisha yetu tunaweza kupata muongozo na mafundisho kutoka kwa Muhammad(s.a.w.w) . hii ndio sababu hakuna haja ya kuletwa Mtume mwingine baada yake.

Zaidi ya hayo yapo mambo matatu ambayo husababisha kuhitajika kuja kwa Mtume mwengine baada ya yule aliyetangulia:

(1) Iwapo mafundisho ya Mtume aliyetangulia yamechanganywa na hekaya za nzushi, kuharibiwa na kupotea. Katika hali kama hiyo Mtume anahitajika ili aje aifundishe dini katika usahihi wake wa awali.

(2) Iwapo mafundisho ya Mtume aliyeondoka hayakukamilika na hivyo kukawa na haja ya kuyakamilisha, kuyarekebisha, au kuongeza jambo fulani.

(3) Iwapo Mtume aliyetangulia alipelekwa kwa watu wa taifa fulani maalum au nchi fulani maalum na hivyo kuwepo haja ya kuletwa Mtume kwa watu wa taifa au nchi nyingine. Au pengine Mtume anaweza kuletwa ili amsaidie Mtume mwingine, lakini kwa kuwa hii si kanuni ya kawaida, hatujaita kama sharti la nne. Katika Qur-an ipo mifano miwili ya hali kama hiyo. Nabii Haruni(a.s) alikuwa msaidizi wa Nabii Musa(a.s) . Nabii Lut (a.s) Ismail(a.s) na Is-haq(a.s) walikuwa wasaidizi wa Nabii Ibrahim(a.s).

Haya matatu ndiyo masharti makuu ya kimsingi yanayohitajika ili aletwe Mtume mwingine. Kati ya hayo hakuna hata sharti moja lililopo leo.

Kwanza : mafundisho ya Mtume wa mwisho, Muhammad(s.a.w.w) yako hai, yamehifadhiwa na yatadumu hadi siku ya Kiyama. Mwongozo aliouleta kwa walimwengu wote ni sahihi na kamili na umehifadhiwa katika Qur-an humo kuna ahadi ya ulinzi wa Allah (s.w) kama tunavyofahamishwa:

﴿نَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ﴾

"Hakika sisi ndio tulioteremsha mawaidha (haya hii Qur-an); na Hakika sisi ndio tutakaoyalinda." (15:9).

Pia sunnah zake zimehifadhiwa kikamilifu kiasi ambacho mtu anaweza kujua pasi na shaka yoyote nini mafundisho ya Mtume juu ya jambo fulani.Hivyo sharti la kwanza linaondoka.

Pili : Mwenyezi Mungu amekamilisha mwongozo wake kwa Nabii Muhammad(s.a.w.w) na hivyo Uislamu ni dini kamilifu kwa ulimwengu wote. Allah (s.w) anasema katika Qur-an:

﴿الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا ﴾

"Leo nimekukamilishieni dini yenu, na kukutimizieni neema yangu juu yangu na nimekupendeleeni Uislamu uwe dini yenu (5:3)

Na tukiutafiti Uislamu kwa makini kama mfumo kam ili wa maisha tunaona unadhihiri ukweli wa aya hii ya Qur-an. Uislamu unatoa mwongozo wa maisha haya na ya akhera na hakuna jambo lililo muhimu katika kumuongoza mwanaadamu lisilokuwemo katika mwongozo aliokuja nao Muhammad(s.a.w.w) . Hivyo hoja ya kuhitaji Mtume ili aje kukamilisha dini pia inaondoka. Hata hivyo kuna baadhi ya watu wanaosema kwamba kupita tu kwa muda mrefu ni sababu ya kuhitaji Mtume mwingine. Hii ni kwa sababu wanasema mwongozo ulioletwa karne 14 zilizopita ni wa kale mno kiasi kwamba hauwezi kukidhi mahitaji ya watu wa leo. Mawazo haya hayana msingi kabisa, kwa sababu zifuatazo:

(i) Mafunzo ya Uislamu ni ya milele, kwa sababu ni ufunuo utokao kwa Mwenyezi Mungu mjuzi wa yote ya kale, ya sasa na yajayo, tena basi mwenye uhai wa milele. Elimu ya binaadamu ndiyo yenye ukomo, na ni jicho la binaadamu ambalo haliwezi kuona hata kesho achilia mbali miaka milioni mmoja ijayo. Elimu na hikima ya Mwenyezi Mungu imesalimika na upungufu kama huo.

(ii) Uislamu umeegemeza mafundisho yake juu ya umbile la binaadamu. Na umbile la binaadamu limesalia vile vile katika zama zote. Watu wote wamejengwa kwa majengo yale yale yaliyowajenga watu wa kale kabisa na hivyo umbile lao kimsingi ni lilelile.

(iii) Katika maisha ya binaadamu kuna mizani inayoridhisha kabisa baina ya mambo yanayodumu na mambo yanayobadilika. Misingi muhimu na maadili makuu hayabadiliki na sura ya nje ndiyo inayoweza kubadilika kutokana na kupita kwa muda. Qur-an na sunna zinatoa kanuni au misingi ya kudumu na kwa kutumia ijitihadi misingi hiyo inaweza kutekelezwa kadri hali itakavyobadilika. Uislamu ndio dini pekee iliyoweka utaratibu madhubuti unaoweza kuoanisha maendeleo ya binaadamu na misingi ya Kitabu cha Allah (s.w) na Sunnah ya Mtume wake Muhammad(s.a.w.w).

Na tukirudi katika lile sharti letu la tatu kuhitajia kuletwa Mtume mwingine, tunaona kuwa Muhammad(s.a.w.w) hakuletwa kwa taifa au watu maalum bali kwa walimwengu wote. Qur-an inasema:

﴿قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعًا﴾

"Sema (Ewe Nabii Muhammad): "Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu nyinyi nyote". (7:158)

﴿وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِّلْعَالَمِينَ﴾

"Nasi hatukukutuma ila uwe rehema kwa walimwengu wote" (21:107)

Labda itaulizwa: Kwanini Mtume Muhammad(s.a.w.w) awe Mtume wa walimwengu wote? Ama kuhusu suali hili, hapana jibu lolote lililotolewa katika Qur-an wala katika hadithi za Mtume(s.a.w.w) . Hivyo ni Allah (s.w) pekee anayejua ni kwanini alimleta kwa ulimwengu mzima. Lakini tunaweza kutumia akili zetu finyu tukajaribu kuona hikima iliyopo kwa Mtume(s.a.w.w) kuwa Mtume wa ulimwengu mzima jambo ambalo halikuwezekana kwa Mitume waliotangulia. Hapo awali, kabla ya Mtume(s.a.w.w) , Mitume walikuwa wakitokea kwa kila nchi au kila taifa. Sababu ya msingi tunayoweza kuona kirahisi ni kwamba katika wakati huo wa historia njia za usafiri na mawasiliano yalikuwa finyu sana kwa kiasi ambacho mawasiliano kati ya watu na nchi moja na nyingine yalikosekana kabisa. Kila nchi au ukanda wa jiografia ulikuwa ni ulimwengu wa peke yake.

Katika hali hii ilikuwa ni vigumu mno kuwa na Mtume mmoja kwa ulimwengu wote. Ndio tunakuta kila nchi au kila ukanda wa jiografia ukatumiwa Mtume wake. Sote tunashuhudia kuwa katika umma huu wa mwisho wa Mtume Muhammad(s.a.w.w) pamekuwa na maendeleo makubwa sana ya mawasiliano kiasi kwamba dunia inakuwa kama kijiji. Suala la "Globalization" (utandawazi) kwa Waislamu sijambo geni. Tunafahamishwa katika Qur-an kuwa umma huu wa Mtume Muhammad(s.a.w.w) ni umma mmoja na unawajibika kuufanya Uislamu utawale ulimwengu mzima.

Kutokana na hoja hizi tatu itaonekana wazi ni kwanini hakuna haja ya Mtume mwingine baada ya Muhammad(s.a.w.w) . Na ndivyo Allah (s.w) anavyotufahamisha katika Qur-an kuwa yeye Muhammad(s.a.w.w) ni "Khataman-Nabiyyina" - yaani mwisho wa Mitume:

﴿مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ وَكَانَ اللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا ﴾

Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali yeye ni Mtume wa Allah na mwisho wa Mitume na Allah ni mjuzi wa kila kitu. (33:40)

Na Mtume Muhammad(s.a.w.w) mwenyewe pia anasema:

Palikuwa na Mitume waliowaongoza Banii Israil katika njia sahihi. Kila Mtume alipokufa, alifuatiwa na Mtume mwingine. Lakini hapana Mtume atakayekuja baada yangu.Kazi hii (ya kuufundisha Uislamu na kuusimamisha) inaweza kufanywa na makhalifa (viongozi wa Kiislamu). (Bukhari)

Na katika Hadithi nyengine Mtume(s.a.w.w) amesema:

"Uhusiano wangu na (msururu mrefu) wa Mitume unaweza kueleweka vizuri kwa mfano wa nyumba nzuri ya kifalme. Nyumba hii ikawa imejengwa vizuri sana na ikawa inapendeza lakini pakawa na nafasi moja iliyobakia. Watu wakawa wanaizungumza nyumba hii nzuri na wakawa wanauliza kwa mshangao.Kwanini hii sehemu isiwe imejazwa! Nimejaza pengo hili na ni Mtume wa mwisho". (Bukhari)

Mitume wa Uongo Wafuatao ni baadhi ya wale waliodai utume wakati Mtume (s.a.w) akiwepo na baada yake. Aswad Aus: Alijitangazia Utume wakati wa Mtume(s.a.w.w) na aliuawa kwa amri ya Mtume mwenyewe.

Musailama (Al-kadhaab) Alijitangazia Utume wakati wa Abubakari (Khalifa wa kwanza wa Mtume(s.a.w.w) . Waislamu walimpiga vita na kumuua. Bahau'lla Alijitokeza huko Iran katika karne ya 19 na aliuawa na Waisalmu.

Mirza Gulam Ahmed Alizaliwa huko India katika kitongoji cha Kadiani katika karne ya 19. Japo alilindwa na serikali ya Kikoloni ya Kiingereza, alipigwa vita na Waislamu kwa maneno na kalamu mpaka uwongo wake ukawa dhahiri kwa waislamu pamoja na kutumia kwake Qur-an hii wanayoifuata Waislamu. Pia kwa kukosekana mtu aliyekuja na kitabu cha mwongozo kinachofanana na Qur'an angalau kwa mbali, inazidi kutudhibitishia kuwa Mtume Muhammad(s.a.w.w) ni Mtume wa mwisho na Qur'an ni ujumbe wa mwisho wa Allah (s.w) utakaobakia mpaka mwisho wa ulimwengu. Maana ya Kuamini Mitume wa Allah (s.w) katika maisha ya kila siku.

Waumini wa kweli wa Mitume wa Allah (s.w) ni wale wenye tabia ifuatayo:

1. Kuwatii Mitume ipasavyo kwa kufanya yale yote waliyoamrisha na kuacha yale yote waliyoyakataza kama Qur'an inavyosisitiza:

﴿وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا﴾

"... Na anachokupeni Mtume basi pokeeni, na anachokukatazeni jiepusheni nacho..." (59:7)

﴿قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٣١﴾ قُلْ أَطِيعُوا اللَّـهَ وَالرَّسُولَ فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْكَافِرِينَ ﴾

Sema: "Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu, basi nifuateni; (hapo)Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakughufirieni madhambi yenu.Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghufira, mwenye rehema. Sema: "Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume. Na kama mkikengeuka,(Mwenyezi Mungu atakutieni adabu),kwani Mwenyezi Mungu hawapendi Makafiri" (3:31-32)

2. Kuwafanya Mitume vigezo vya maisha yao kibinafsi, kifamilia na kijamii kama inavyosisitizwa katika Qur-an:

﴿ لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا﴾

"Bila shaka mnao mfano mwema (wa kuiga) kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwa mwenye kumuogopa Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, na kumtaja Mwenyezi Mungu sana". (33:21)

3. Kuwapenda Mitume kuliko nafsi zao kama Qur-an inavyosistiza:

﴿قُلْ إِن كَانَ آبَاؤُكُمْ وَأَبْنَاؤُكُمْ وَإِخْوَانُكُمْ وَأَزْوَاجُكُمْ وَعَشِيرَتُكُمْ وَأَمْوَالٌ اقْتَرَفْتُمُوهَا وَتِجَارَةٌ تَخْشَوْنَ كَسَادَهَا وَمَسَاكِنُ تَرْضَوْنَهَا أَحَبَّ إِلَيْكُم مِّنَ اللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَجِهَادٍ فِي سَبِيلِهِ فَتَرَبَّصُوا حَتَّىٰ يَأْتِيَ اللَّـهُ بِأَمْرِهِ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْفَاسِقِينَ ﴾

"Sema "Kama baba zenu na wana wenu na ndugu zenu na wake zenu na jamaa zenu na mali mlizozichuma na biashara mnazoogopa kuharibikiwa,na majumba mnayoyapenda; (ikiwa vitu hivi) ni vipenzi zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kupigania dini yake, basi ngojeni mpaka Mwenyezi Mungu alete amri yake; na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu maasi" (9:24)

Kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume si jambo lingine zaidi ya kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa unyenyekevu na upendo.

Muumini wa kweli hatakuwa tayari kuifurahisha nafsi yake au kumfurahisha yeyote awaye kinyume na kumfurahisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Ni katika maana hii Mtume(s.a.w.w) anasema:

"Hatakuwa mmoja wenu ni Muumini wa kweli mpaka anipende zaidi kuliko chochote kile ikiwa ni pamoja na familia yake, mali yake na watu wote" .(Sahihi Muslim)

"Yeyote yule anayependa Sunnah yangu ananipenda, na yeyote yule anayenipenda atajikuta yuko ubavuni kwangu huko Peponi" (Tirmidh)

4. Kuwafanya Mitume kuwa Mahakimu wao pale wanapohitilafiana katika jambo lolote lile kama tunavyojifunza katika Qur-an:

﴿فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا﴾

"Naapa kwa (haki ya) Mola wako (Ewe Muhammad); wao hawawi wenye kuamini mpaka wakufanye hakimu katika yale wanayokhitalifiana, kisha wasione uzito nyoyoni mwao juu ya hukumu uliyopitisha, na wanyenyekee kabisa." (4:65)

﴿وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا﴾

"Haiwi kwa mwanamume aliyeamini wala kwa mwanamke aliyeamini, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapokata shauri, wawe na hiyari katika shauri lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake hakika amepotea upotofu (upotevu) ulio wazi." (33:36)

5. Kuwa na yakini kuwa Mtume Muhammad(s.a.w.w) ndiye Mtume wa mwisho kama Qur-an inavyosisitiza:

﴿مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ وَكَانَ اللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا﴾

"Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na mwisho wa Mitume, na Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu." (33:40)

6. Kumswalia Mtume(s.a.w.w) mara kwa mara katika swala na kila anapotajwa. Kumswalia Mtume(s.a.w.w) ni amri ya Allah (s.w) kama inavyotuelekeza ifuatavyo:

﴿إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا﴾

Hakika Mwenyezi Mungu anamteremshia Rehema Mtume;na Malaika wake. Basi; Enyi mlioamini, msalieni Mtume na muombeeni amani. (33:56)

ZOEZI 2:2

1. Malaika ni......................................................................

2. Toa tofauti nne (4) zilizopo kati ya Malaika na binaadamu.

3. Orodhesha kazi kumi (10) za malaika zenye mahusiano na binaadamu.

4. Muumini wa kweli wa Malaika ni yule anayefanya yafuatayo:-

(a) ..........................(b) ......................(c) .....................(d) .........................

5. Taja vitabu vinne (4) vya Allah (s.w) vilivyohadithiwa katika Qur-an na Mitume walioshushiwa.

6. Lengo la kushushwa vitabu vya Allah (s.w) ni..................................

7. "Hakika ni juu yetu kutoa mwongozo." (92:12) Pamoja na binaadamu kupewa akili na elimu hana uwezo wa kujiundia njia sahihi ya maisha kwa sababu zifuatazo:

(a)...............................................

(a)..............................................

(b)..............................................

8. Toa tofauti nne (4) zilizopo kati ya Qur-an na vitabu vingine vya Allah (s.w). 9. Muumini wa kweli wa Qur-an ni yule anayefanya yafuatayo:

(a).............................................

(b)..................................................

10. (a) Mitume wa Allah (s.w) ni ..................................................

(b) Mitume wameletwa ili..................................................

(c) Waumini wa kweli wa Mitume wa Allah (s.w) ni wale wenye tabia zifuatayo:

(i)..........................

(ii)..........................

(iii)..........................

(iv)..........................

(v)..........................