MUANDAMO WA MWEZI

MUANDAMO WA MWEZI 0%

MUANDAMO WA MWEZI Mwandishi:
Kundi: Midahalo na majadiliano kielimu

MUANDAMO WA MWEZI

Mwandishi: Juma Muhammad Rashid Al-Mazrui, Al-Zenjibari.
Kundi:

Matembeleo: 59182
Pakua: 4792

Maelezo zaidi:

MUANDAMO WA MWEZI
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 23 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 59182 / Pakua: 4792
Kiwango Kiwango Kiwango
MUANDAMO WA MWEZI

MUANDAMO WA MWEZI

Mwandishi:
Swahili

16

MUANDAMO WA MWEZI

SEHEMU YA KUMI NA TANO

FUNGA YA 'ARAFAH

Katika sehemu hii, ni vyema kwanza nikanukuu yote nilioyasema kuhusu maudhui hii, kisha ndio nikanukuu jawabu niliojibiwa na kuijadili. Kuhusu suala hili nilisema: Anasema Sheikh Nassor Bachoo: "Jambo la kusikitisha ni kwamba ikiwa Waislamu watakubali kuwepo tafauti ya siku na tarehe baina yao, hapana shaka watakuwa wanafunga saumu ya Arafa siku tafauti na inavyotakiwa.

Kwa hivyo lengo na faida ya funga yenyewe litakuwa halikupatikana. Mbali na kukosekana huko Makka jambo baya zaidi ni kwamba watakuwa wanafunga siku ya pili yake ambapo watakuwa wanafunga siku ya 'Idul-Adh-ha'; siku ambayo ni Haramu kufunga.

Ni vyema tuzingatie kwamba funga hii ya Arafa pamoja na Iddi yake ni vitu ambavyo havina mahusiano na kuandama mwezi kutokana na kila nchi inavyoona mwezi wake. Bali chanzo cha funga ya Arafa ni uhusiano wa ile siku ambayo mahujaji wanaposimama katika uwanja wa Arafa. Na jambo la kusimama Arafa linapatikana sehemu moja tu ulimwenguni ambayo ni siku inayosadifu tarehe 9 Dhul-Hijjah huko mji wa Makka; sio tarehe tisa ya nchi nyengine yoyote ile. Kwa uthibitisho zaidi wa funga ya siku ya Arafa tunajifunza kuwa Mtume (s.a.w.) alipotueleza umuhimu wa siku hii, na kila alipotaja siku hii ya Arafa alitumia neno 'siku' wala hakutumia neno 'tarehe'.

Funga ya 'siku' ya Arafa." Mwisho wa kunukuu. Sasa tatizo moja linalowatatiza watu kuhusu suala zima la kuwa na miandamo tafauti ni tatizo hili la funga ya Arafa. Kwa kweli hili si tatizo lakini tatizo tunalo sisi wenyewe katika udha ifu wetu wa kukiweka kila kitu mahala pake na kutoa hukumu kwa mujibu wa misingi inavyotuelekeza. Siisahau kauli ya Dr. Al-zuhailiy yenye maana kwamba makosa mengi ya kifiq-hi yanatokana na kuwacha misingi yake ya kiusuli, na kwamba lau watu walikuwa wanaifata misingi hio, basi makosa yasingelitokea au ingelikuwa nadra sana kutokea.

Sasa suala tunaloulizwa ni kuwa kama muandamo kila watu wawe na wao, itakuwaje ikitokea siku ya Arafa kuwa kwetu ni mwezi nane, ilhali Arafa inakuwa mwezi tisa? Tukifunga tutakuwa tumefunga mwezi nane; tukifunga siku ya pili itakuwa Arafa imeshakwisha?

Jawabu ya suala hili: ni kuwa kwanza inatakiwa tujue kwanini tunafunga siku hio: nini sababu: je sababu ni Arafa au sababu ni mwezi muandamo? Tumeeleza huko nyuma nini illa ambayo, kwa Kiswahili, huwa tunaifasiri kuwa ni Sababu. Tukasema kwamba wengine wanatafautisha baina ya sababu na illa. Sababu - kwao - ni kitu kisicho na uhusiano na kitu chenye kupewa hukumu. Tukatoa mfano wa kutenguka kwa jua kuwa ni sababu ya kuwajibikiwa na Sala. Na illa ni kitu chenye uhusiano na kitu chenye kupewa hukumu, kama kuumwa ndio illa ya kuruhusika kula mchana wa mwezi wa Ramadhani.

Kwa maana hii, utakuwa umefahamu kwamba sababu ya:

1) Kutuwajibikia Sala ya Adhuri na Laasiri - kwa mfano - ni kutenguka jua. Ushahidi wake ni Aya inayosema: (Simamisha sala kwa kutenguka jua).

2) Sababu ya kufunga au kuwajibikiwa na funga ni kuuona mwezi. Kama ilivyo Hadithi inayosema:(Fungeni kwa kuuona) . Sasa hapa tuna mambo mawili: Moja: ni munasaba wa kufunga siku hio ya Arafa. Pili: ni sababu ya kufunga siku hio ya Arafa. Kisimamo cha Arafa ni Munasaba: wa kufunga siku hio: si sababu: Sababu: ya kufunga siku hio, ni muandamo wa mwezi wa mfunguo tatu. Wala usidhani kwamba tarehe tisa ya mwezi huo ndio sababu: "laa" (sio hivyo), bali tarehe tisa ni wakati wa kufunga: si sababu ya kufunga. Na hili linabainishwa zaidi na riwaya tuliotangulia kuinukuu huko nyuma, nayo ni riwaya ya Amiri wa Makka, yenye kusema: "Alituusia Mjumbe wa Allah - rehema na amani ziwe juu yake - tuabudu kwa kuuona, kama h atukuuona na wakashuhudia mashahidi wawili waadilifu, tuabudu kwa (kufata) ushahidi wao." Tumesema huko nyuma kwamba neno Nansuk (tuabudu) wengine wameifasiri ibada hii kuwa ni ibada ya hija nayo ndio tafsiri yenye muelekeo madhubuti zaidi, kwani neno hili hutumika sana kwa maana ya ibada ya hija, kama Allah (S.W.) anavyosema kuhusu ibada ya hija: Mukimaliza Nusuki (ibada) zenu (za hija). Na kwa hivyo imekuja katika "A'WNU AL-MA'ABUDI: SHARHU SUNANI ABI DAUD" kuhusu maana ya Hadithi hio tulioinukuu hapo juu kuwa maana yake inahusiana na ibada za hija. Anasema mwenye kusherehesha: "Na maana yake ni: 'Tuhiji kwa kuuona (mwezi), yaani mwezi muandamo wa mfunguo tatu." Ni wazi kwa maelezo haya au kwa mujibu wa Hadithi hii kwamba sababu ya ibada za hija - ikiwemo funga ya Arafa - ni kuandama kwa mwezi wa mfunguo tatu.

Sasa - tukirudi katika munasaba - ni kuwa munasaba si lazima kuwa mtu ausherehekee siku ile ile ya munnasaba huo. Kwa mfano, tunaposherehekea tokeo fulani lililotokea tarehe fulani katika historia, si lazima kuwa tuifanye sherehe yetu siku na tarehe ile ile: "Laa" tunaweza kuweka sherehe yetu siku nyengine. Sikusudii kufananisha sherehe yetu na mas-ala haya, ninachokusudia ni kukupa mfano utaoweza kufahamu kwawo tafauti baina ya Munasaba na Sababu.

Kwa hivyo, funga imeambatanishwa na muandamo wa mwezi, kama vile sala ilivyoambatanishwa na mtenguko wa jua. Utapolifahamu hili, utakuwa umefahamu kwamba, siku ya kufunga ni tarehe tisa mfunguo tatu, sawa siku hio imeafikiana na Arafa au imetafautiana, kwani sababu tayari imepatikana, na kilichotafauti ni kuafikana wakati wa tarehe ya baadhi ya sehemu na kuafikiana wakati mmoja wa Munasaba. Na Munasaba haufanywi kuw a ni illa wala haufanywi kuwa ni sababu ya hukumu. Hilo ni mosi.

Pili : ni kuwa: hata ikiwa kweli kilicho sahihi ni kwamba watu wakisimama Arafa na sisi tufunge hata ikiwa tarehe nane kwetu kwa mujibu wa muandamo wetu - tumeona kwamba kielimu hili ni kosa lakini tujaalie ni hivyo - basi elewa kwamba hili halijahalalisha kwamba na muandamo wa Ramadhani uwe mmoja. Ukitafakari kidogo hapa, utaona kwamba dai hili ni kujenga hoja juu ya Qiyas baina ya mambo mawili yaliotafauti. Arafa ni tokeo ambalo linatokea Makka tu, wakati Ramadhani ni tokeo la dunia nzima. Kwa hivyo, hata tukisema kwamba kilicho sahihi ni kufunga kwa ajili ya tokeo hilo au munasaba huo wa Arafa, basi itakuwa ni kwa sababu munasaba huo unatokea sehemu moja tu: kwetu hautokei. Kwa lugha nyengine, lau na sisi tulioko nje ya Makka ingelikuwa tunatakiwa tusimame Arafa yetu huko tuliko siku ya tarehe tisa, basi tungefanya hivyo kwa mujibu wa muandamo wetu, kama vile tunavyofunga kwa kufata muandamo wetu, na kusali kwa sababu ya mtenguko wetu wa jua. Wakati Ramadhani ni tokeo la dunia: watu wa Makka wanafunga na sisi tunafunga. Kwa hivyo, haya ni matokeo mawili tafauti huwezi kuyafanyia Qiyas kwani miongoni mwa masharti ya lazima ya Qiyas ni "Kupatikana usawa baina ya Shina na Tawi" na usawa hapa haupo. Kilicho sahihi, ni kufanya Qiyas cha Sala na funga. Kwani:

1) Wajibu wa Sala umefungamanishwa na kutenguka na kuzama kwa jua - kitu cha kimaumbile (Natural phenomenon). Kwa hivyo mtenguko wa jua ni sababu: si munasaba.

2) Wajibu wa funga umefungamanishwa na muandamo wa mwezi - kitu cha kimaumbile (Natural phenomenon). Kwa hivyo kuandama kwa mwezi ni sababu: si munasaba.

3) Jua - ambalo kutenguka kwake ndio sababu ya kuwajibikiwa na sala - likitenguka katika nchi moja, watu wa nchi nyengine hawawajibikiwi na sala. Kwa hivyo, Qiyas sahihi ni kuwa kuonekana kwa mwezi - ambayo ni sababu ya kuwajibika funga - katika nchi moja isiwe sababu ya kufunga kwa watu wa nchi nyengine. Hiki ni Qiyas sahihi. Ama kisimamo cha Arafa si Qiyas sahihi, kwani kisimamo cha Arafa ni Munasaba si Sababu wakati muandamo wa mwezi na kutenguka jua ndio Sababu. Au ukipenda kufanya Qiyas chengine sahihi, basi ni kile tulichotangulia kukinukuu kutoka kwa Sheikh Al-uthaimin, aliposema: "Na wakati wa mwezi ni kama wakati wa siku. Kama vile ambavyo miji inatafautiana katika kuanza kujizuia (na kula n a kunywa na jimai: yaani kuanza kufunga) na (inavyotafautiana katika) kufuturu kwa siku (daily au, basi vivyo hivyo inawapasa watafautiane katika kujizuia na kufuturu kwa mwezi (monthly au). Na (kama) inavyojulikana kwamba tafauti za kisiku zina athari zake kwa makubaliano ya Waislamu. (Watu) waliyo upande wa mashariki, hakika wao wanaanza kufunga kabla ya waliyo upande wa magharibi na wanafuturu kabla yao.

Wala haiwezekani mtu akasema kwamba kauli yake Allah (S.W. inayosema):"Sasa waingiliyeni (wake zenu) na tafuteni kile Allah alichokuandikiyeni, na kuleni na kunyweni mpaka ukubainikieni uzi mweupe kutokana na uzi mweusi wa alfajiri, kisha timizeni saumu hadi usiku." Na kauli yake (Mtume) s.a.w.:"Usiku ukitokeza kutoka hapa na mchana ukaondoka kutokea hapa na jua likatua, basi aliyefunga ameshafungua (au na-afungue)." (Haiwezekani mtu akasema kwamba Aya hio na Hadithi hii) kwamba ni za ujumla wa Wa islamu wote katika miji yote. Basi vivyo hivyo tunasema kuhusu ujumla wa kauli yake Allah (S.W.):﴿ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ (Atayeushuhudia mwezi miongoni mwenu na-aufunge).

Na kauli hii - kama unavyoona - ina nguvu yake kwa mujibu wa lafdhi (yake) na mtazamo sahihi na Qiyas sahihi vile vile: Qiyas cha wakati wa siku kwa (kuulinganisha) na wakati wa mwezi (month). Mwisho wa kunukuu.

Tatu : ni kuwa: kutokukiwahi kisimamo cha Arafa kwa baadhi ya Waislamu wa sehemu nyengine za dunia ni kitu cha lazima. Chukulia - kwa mfano - kuna nchi ambazo siku hio ya mwezi tisa, jua linatua Saudia kwao bado ni usiku au alfajiri ya siku hio hio. Ikiwa watafunga kwa munasaba wa Arafa, inakuwa Arafa haipo tena, labda wawe ni wenye kufata kauli ya wenye kujuzisha kusimama Arafa usiku ndio watakuwa nao wamefunga siku ya Arafa, lakini tatizo bado litabakia katika siku ya Idi.

Siku ya pili - tujaalie ni J/tatu - asubuhi watu wa miji ya Saudia wanasali Idi - wao kwao ni magharibi ya J/pili, na Idi haisaliwi magharibi. Hata wakifika asubuhi - J/tatu kwao - Makka tayari jua limetua, na kwa hivyo ni J/nne. Utaona kwamba mitazamo ya kiakili na hoja za kimaandiko zilizojengeka katika misingi imara ya kifani, inaonesha kwamba kufunga na kufungua - sawa ikiwa Ramadhani au Mwezi tisa mfunguo tatu - basi ni jambo linalofatana na miandamo ya mwezi. Na kilicho sahihi - kama tulivyobainisha - ni kuwa muandamo wa mbali usitendewe kazi mbali. Kwa hivyo, kufunga ni tarehe tisa, sawa imeafikiana na munasaba wa Arafa au haikuafikiana, na kwa kufata tarehe tisa watu wote wa dunia itawezekana kufunga na itawezekana kula Siku Kuu tarehe kumi. Ama tukifata munasaba wa kusimama Arafa, watu wa nchi nyengine hawatoweza kufunga kwani hakuna maafikiano ya wakati wa kufunga baina ya Makka na nchi zao, labda kwa wale wenye kufata kauli ya wenye kujuzisha kusimama Arafa usiku, lakini hata hivyo Idi wataikosa.

Ama tukirudi katika nadharia ya Sheikh Bachoo aliposema: " Ni vyema tuzingatie kwamba funga hii ya Arafa pamoja na Iddi yake ni vitu ambavyo havina mahusiano na kuandama mwezi kutokana na kila nchi inavyoona mwezi wake. Bali chanzo cha funga ya Arafa ni uhusiano wa ile siku ambayo mahujaji wanaposimama katika uwanja wa Arafa." Mwisho wa kunukuu. Tukirudi katika maelezo hayo tunakuta kuwa maelezo hayo yanaifanya ibada ya saumu ianzwe kabla ya kufika sababu yake, kwani Arafa inaanza tarehe tisa baada ya kutenguka jua Adhuhuri, wakati wafungaji huwa tayari wameshafunga tangu kabla ya Alfajiri. Jambo hili la kutangulia "Kilichosababishwa kabla ya kilichosababisha" halipo kamwe katika soko la elimu! Ilivyo ni kutangulia "Kilichosababisha kabla ya kilichosababishwa," kama unavyotangulia mtenguko wa jua au kuzama k wake (ambao ni sababu) halafu ndio ikafatia sala (ambacho ndicho kilichosababishwa).

Ama maneno ya Sheikh Nassor Bachoo aliposema: "Kwa uthibitisho zaidi wa funga ya siku ya Arafa tunajifunza kuwa Mtume (s.a.w.) alipotueleza umuhimu wa siku hii, na kila alipotaja siku hii ya Arafa alitumia neno 'siku' wala hakutumia neno 'tarehe'. Funga ya 'siku' ya Arafa." Mwisho wa kunukuu.

Tunasema kwamba: kuitwa siku hio kuwa ni siku ya Arafa na isiitwe siku ya mwezi tisa si hoja ya kuwa lazima tufunge sawa na Saudia, kwani mtegemezo huu ni kulitegemeza (neno hilo Arafa) kwa ajili ya kuitukuza ile ibada inayofanyika katika eneo hilo." Na hii ni kawaida ya Warabu kuyanasibisha majina ya siku kwa kuyapa majina ya sehemu ambazo kuna matokeo fulani adhimu yaliyotokea au yanatokea katika sehemu hizo. Siku ya vita vya Uhudi - kwa mfano - huiita Yawmu Uhud (Siku ya Uhudi), na Uhudi ni jina la sehemu. Halkadhalika vita vya Hunain: vinaitwa Yawmu H unain (Siku ya Hunain). Anasema Allah kuhusu vita hivyo: "Na siku ya Hunain wingi wenu ulipokupendezesheni." Na Hunain ni jina la mji. Halkadhalika vita vya Badr; Badr ni sehemu. Lakini tunaviita vita hiv yo "Yawmu Badri (Siku ya Badr). Anasema Sahaba Hassan bin Thabit, Mshairi wa Mtume(s.a.w.w):

Nyuso siku ya Badri zilimngojea Mwingi wa rehema alete ushindi. Tazama Sahaba Hassan: ameinasibisha siku hio kwa kuipa jina la sehemu ya Badr, kwa ajili ya utukufu wa yale yaliofanyika hapo. Kwa hivyo kunasibishwa siku ya Arafa na sehemu hio ya Arafa, si kwa sababu tufunge sawa sawa, bali ni kwa utukufu wa yale yanayotendeka. Na yanayotendeka hapo ni Munasaba wa kufunga si Sababu ya kufunga kama tulivyotangulia kubainisha. Na inampasa msomi - mwanachuoni na Talibu Al-ilm (mwanafunzi) - kutafautisha baina ya vitu viwili hivyo. Mwisho wa kunukuu nilioyasema katika kitabu.

JAWABU NILIOJIBIWA NI KAMA IFATAVYO

Baada ya kuyaeleza hayo nilioyaeleza, ndugu zangu walinijibu juu ya maudhui hio kama ifatavyo:

Funga Ya 'Arafah Neno 'Arafah au 'Arafah ni jina linalotokana na uwanja au viwanja maalum vilioko nje kidogo ya Mji Mtukufu wa Makkah. Mahujaji wote ambao wamehirimia kutekeleza Ibada ya Hijja hukusanyika katika viwanja hivyo. Jambo hilo la kwenda kusimama kwenye viwanja hivyo kwa kuomba dua na kumtaja Allaah ni katika nguzo kubwa ya ibada hiyo ya Hijja. Inampasa kila Hajji kusimama au kushiriki hata kwa muda mdogo katika mchana huo. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amebainisha hayo kwa kusema:

(Hijja ni 'Arafah) Jambo hilo linathibitisha kwamba mtu yeyote asiyetekeleza ibada ya kusimama 'Arafah anapokuwa Makkah, atakuwa hakuipata ibada hiyo ya Hijja. Watu humiminika na kusimama kwenye uwanja wa 'Arafah siku ya tarehe 9 - Dhul-Hijjah ya kila mwaka. Ikumbukwe kwamba tarehe 9 hiyo ni ya huko Makkah pahala ambapo inafanyika ibada ya Hijja wala siyo ya pahala pengine popote duniani. Ni vyema kuzingatia kwamba funga hii ya 'Arafah pamoja na 'Iyd yake ni vitu ambavyo havina mahusiano na kuandama kwa mwezi kutokana na kila nchi inavyoona mwezi wake. Chanzo cha funga hii ya 'Arafah ni ule uhusiano wa ile siku ambayo Mahujjaji wanaposimama katika uwanja wa 'Arafah. Ambapo jambo la kusimama 'Arafah linapatikana sehemu moja tu ulimwenguni ambayo ni siku inayosadifu tarehe 9 - Dhul-Hijjah huko mji wa Makkah, sio tarehe 9 ya nchi nyengine yoyote ile.

Kwa maneno mengine ni kuwa tutakapotofautiana katika kufunga Siku ya 'Arafah na 'Iydul-Hajj itakuwa kama kwamba kila nchi ina uwanja wake wa 'Arafah na Makkah yake. Kwa uthibitisho zaidi wa funga ya siku ya 'Arafah tunajifunza kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kila alipokuwa akieleza umuhimu wa siku hii alitumia neno "siku" wala hakutamka neno "tarehe." Ama kwa mujibu wa maelezo ya ndugu yetu Juma, kama kawaida yake yeye anaona kuitwa "Siku ya 'Arafah" haina maana kuwa lazima tufunge sawa na Saudia, bali anaona kuwa hiyo ni "Idhaafatu-Tashriif" (yaani kuitengeneza siku hiyo kwa ajili ya utukufu wa pahala hapo au kwa ajili ya utukufu wa tokeo lenyewe). Sisi kwa upande wetu tunamuuliza ndugu Juma, Je yapo maandiko yoyote ya kilugha au ya kisheria yanayotufunza kuwa pahala pakitumika "Idhaafatu-Tashriif" huwa haparuhusiki tena kutoa mafunzo mengine yaliyomo ndani ya "idhaafa" hiyo? Tujuavyo sisi zipo Aya nyingi za Qur-aan ambazo zimetumika ndani yake hiyo "Idhaafatu-Tashriif" lakini utakuta wanavyuoni wa tafsiri wametoa mafunzo mengine yapatikanayo katika "idhaafa" hizo.

Akaendelea ndugu Juma kutoa kikwazo ambacho anaona kuwa haiwezekani kufunga siku ya 'Arafah sawa na tokeo lenyewe huko Makkah kwa kisingizio cha kuwa kuna nchi zinazotofautiana kwa masaa mengi. Kisha akasema: (Na (kama) inavyojulikana kwamba tafauti za kisiku zina athari zake kwa makubaliano ya Waislamu. Waliyo upande wa mashariki, hakika wao wanaanza kufunga kabla ya waliyo upande wa magharibi na wanafuturu kabla yao). Kama ni hivyo tofauti ni nchi zilizo Magharibi kwa nchi zilizo za Mashariki zinatofautiana, sisi tunamuuliza ndugu Juma vipi tena kwa nchi zilizo jirani kama vile Omani na Dubai , au Omani ya Yemeni, Je! Kuna suala la Mashariki na Magharibi hapa? Au kama ni hivyo basi mbona Juma hakubali uwezekano wa kufunga pamoja nchi zote za Mashariki kwa wakati mmoja na zote za Magharibi kwa wakati mwengine?

JAWABU

Kwanza Kimsingi ni kuwa hamukujibu hoja zangu moja moja kama nilivyoeleza mimi. Mukhtasari wa nilioyaeleza ni kuwa:

a) Ibada za Hija zina Sababu yake.

b) Hadithi imeonesha kuwa sababu ya ibada hizo ni muandamo wa mwezi wa mfunguo tatu. Hadithi imesema: "Alituusia Mjumbe wa Allah - rehema na amani ziwe juu yake - tuabudu kwa kuuona, kama hatukuuona na wakashuhudia mashahidi wawili waadilifu, tuabudu kwa (kufata) ushahidi wao."

Tumesema katika kitabu kwamba neno Nansuk (tuabudu) wengine wameifasiri ibada hii kuwa ni ibada ya hija nayo ndio tafsiri yenye muelekeo madhubuti zaidi, kwani neno hili hutumika sana kwa maana ya ibada ya hija, kama Allah (S.W.) anavyosema kuhusu ibada ya hij a: Mukimaliza Nusuki (ibada) zenu (za hija). Na kwa hivyo imekuja katika "Awnu Al-Ma'abudi: Sharhu Sunani Abi Daud kuhusu maana ya Hadithi hio tulioinukuu hapo juu kuwa maana yake inahusiana na ibada za hija. Anasema mwenye kusherehesha: "Na maana yake ni: 'Tuhiji kwa kuuona (mwezi), yaani mwezi muandamo wa mfunguo tatu." Ni wazi kwa maelezo haya au kwa mujibu wa Hadithi hii kwamba sababu ya ibada za hija - ikiwemo funga ya Arafa - ni kuandama kwa mwezi wa mfunguo tatu.

c) Kwa hivyo, kwa mujibu wa Hadithi hii, sababu ya kuingia ibada ya hijja -funga yake ya mwezi 9 na idi yake mwezi 10, ni muandamo wa mwezi wa mfunguo tatu. Ama kisimamo cha Arafa nimejibu kwamba haiwezekani kuwa ndio sababu ya kufunga kwani, kisimamo kinakuwa baada ya kutenguka jua adhuhuri, wakati wafungaji wameshafunga tangu alfajiri, na sababu hutangulia kwanza kisha ndio kikaja kilichosababishwa; yaani kwa lugha nyengine sababu ya ibada huwa haitanguliwi na ibada yenyewe; bali kwanza hutangulia sababu kisha ndio ikaja ibada ambayo ndio iliosababishwa.

Kwa hivyo, ikiwa sababu ya ibada za hija kikiwemo kisimamo cha Arafa na funga yake ni muandamo wa mfunguo tatu, basi sisi tupo pale pale kwamba Hadithi sahihi ya Ibn Abbaas na Kuraib imethibisha kwamba muandamo wa mbali hautendewi kazi mbali. Kwa hali hii, sisi Afrika Mashariki, na kwangine, hatuwezi kufunga kwa kufata mwezi tisa wa Saudia, kwani muandamo kila mtu ana wake; wala hatuwezi kufanya hivyo kwa kufata kisimamo cha Arafa kwani kisimamo cha Arafa sio sababu ya ibada za Hijja kikiwemo kifungo hicho; bali muandamo wa mwezi ndio sababu kama Hadithi ilivyosema.

MNASEMA

Ndugu Juma ni vyema aelewe kwamba upo uwezekano wa kufunga 'Arafah siku moja dunia nzima kama tulivyoelezea katika kurasa za nyuma za kitabu hichi kwamba dunia nzima inashirikiana katika mchana mmoja na inashirikiana katika usiku mmoja ingawaje kuna nchi zinazotanguliza na nyengine zinazofuatia. Mfano nchi zote za Afrika zinaweza kushirikiana kufunga siku moja kwani baadhi ya nchi za Afrika zinatofuatiana kwa masaa machache tu sio usiku mzima wala mchana mzima. Katika kitabu cha Shaykh Naaswir Bachuu imeandikwa kwamba tofauti iliyopo kwa nchi za Kiislamu zilizo Mashariki ya mbali kama Phillipines na Indonesia na zile zilizo Magharibi ya mbali kama Al-Maghrib yaani Morocco ni tofauti ya masaa 9 tu. Kwa hivyo upo uwezekano wa kitaalamu (Kijiografia) wa kuweza kufunga kwa pamoja katika siku hiyo hiyo moja. Tofauti iliyopo ni ya masaa tu. Tunafunga siku moja sio wakati mmoja wala sio dakika moja. Msisitizo upo katika kufunga siku moja sio kuanza wakati mmoja.

JAWABU

Ama kudai kwamba uko uwezekano wa kufunga Arafa duniani kote siku moja, hilo si da sahihi. Nimekupeni mfano wa mimi mwenye mwezi wa 5 na wa 6 2009 nilikuwa Hong Kong, nikampigia simu ndugu yangu aliye Marekani nikamuuliza ni saa ngapi huko kwenu akanijibu ni saa kumi jioni; wakati huo Hong Kong tumeshali Alfajiri tushatoka Msikiti baina ya saa 11 na nusu mpaka 12 au 12 kasoro kidogo. Tazama tafauti iliokuwepo hapo. Hii ina maana jua likitua U.S.A jioni baada ya masaa mawili, labda na nusu, Hong Kong watu wanaingia makazini asubuhi kweupe na jua liko juu. Utaona kwamba, Kiislamu, ikiingia Ijumaa Hong Kong, Marekani bado ni Alkhamisi. Waislamu walioko Hong Kong wakifunga Arafa mchana wa tarehe 9, Marekani bado ni usiku hawawezi kufunga; Waislamu wa Hong Kong wakifuturu jioni, Marekani ni wakati wa mwisho mwisho wa alfajiri au ni asubuhi. Kwa ufupi ni kuwa baadhi ya States za Amerika na Hong Kong, tafauti haipungui masaa kumi na mbili.

Kwa hivyo, dai hilo si sahihi. Na hapa inabainika kwamba kauli sahihi ni ya kufata tarehe 9 mfunguo tatu kwa mujibu wa muandamo wan chi zetu, kwani tukifanya hivyo Waislamu wote duniani wataweza kufunga tarehe 9 na kula siku kuu tarehe 10. Ama tukifata muandamo mmoja hilo halitowezekana kwani mchana wa mwezi 10 wa nchi moja, tuseme hio Hong Kong, ni usiku katika nchi nyengine tuseme hio Marekani; jua likitua Hong Kong itakuwa tayari Kisharia ni mwezi 11, wakati Marekani ndio kwanza wajitayarisha kwenda kusali idi bado kwao ni mwezi 10. Utaona Al-Nadhar, Athar na migawanyiko ya kijografia, yanatoa jawabu sawa kwamba kilicho sahihi ni kila watu kufata muandamo wao.

Ama baadhi ya nchi kama mulivyosema - Za Africa kwa mfano - sipingi kwamba kuna uwezekano, ninachopinga ni kuwa dalili ni tafauti na kitendo hicho. Kama Ibn Abbas kakataa kuchukua muandamo wa Sham wala tafauti baina yake na Madina haifiki masaa hayo ya masaa 9 na akatoa hoja kwamba "Hivi ndivyo alivyotufunza Mtume s.a.w.", basi vipi itawezekana Kisharia kwamba watu wa Africa nzima wafunge sawa sawa.

MNASEMA

Ndugu Juma anasema: (Utapolifahamu hili, utakuwa umefahamu kwamba, siku ya kufunga ni tarehe tisa mfunguo tatu, sawa siku hio imeafikiana na Arafa au imetafautiana,....) [uk. 141]

JAWABU

Nyinyi ndugu zangu munanukuu maneno "Utapolifahamu hili..?" Bila ya ku nukuu maelezo yenyewe yalionipelekea kusema "Utapolifahamu hili". Sasa msomaji atafahamu nini? Huu sio mjadala wa kielimu wenye lengo la kutafuta natija sahihi. Ilikuwa munukuu jawhari ya maneno yangu kasha ndio muyajibu.

MNASEM

a) Sisi tunamjibu kwamba: Sasa kama anaruhusu kutafautiana, tena kwanini imeitwa (Funga ya 'Arafah) isiitwe "Funga ya tarehe 9"? Kisha ndugu Juma anaamini kwamba: (Arafa ni tokeo ambalo linatokea Makka tu, wakati Ramadhani ni tokeo la dunia nzima.) Kama kawaida yake ndugu Juma anajikanganya kila mara, kama kweli anaamini kila nchi ifunge kwa muandamo wake na 'Arafah, kila nchi ifunge kivyake, inakuaje tena Ramadhaan iwe ni ya dunia nzima, 'Arafah iwe kila mtu na yake?

JAWABU

Ama kwanini imeitwa (Funga ya 'Arafah) isiitwe "Funga ya tarehe 9", nimeshakuelezeeni kwa urefu katika Kitabu. Nimesema: Tunasema kwamba: kuitwa siku hio kuwa ni siku ya Arafa na isiitwe siku ya mwezi tisa si hoja ya kuwa lazima tufunge sawa na Saudia, kwani mtegemezo huu ni kuli tegemeza (neno hilo Arafa) kwa ajili ya kuitukuza ile ibada inayofanyika katika eneo hilo." Na hii ni kawaida ya Warabu kuyanasibisha majina ya siku kwa kuyapa majina ya sehemu ambazo kuna matokeo fulani adhimu yaliyotokea au yanatokea katika sehemu hizo. Siku ya vita vya Uhudi - kwa mfano - huiita Yawmu Uhud (Siku ya Uhudi), na Uhudi ni jina la sehemu. Halkadhalika vita vya Hunain: vinaitwa Yawmu Hunain (Siku ya Hunain). Anasema Allah kuhusu vita hivyo: Na siku ya Hunain wingi wenu ulipokupendezesheni." Na Hunain ni jina la mji. Halkadhalika vita vya Badr; Badr ni sehemu. Lakini tunaviita vita hivyo "Yawmu Badri (Siku ya Badr). Anasema Sahaba Hassan bin Thabit, Mshairi wa Mtume(s.a.w.w) :

Nyuso siku ya Badri zilimngojea Mwingi wa rehema alete ushindi. Tazama Sahaba Hassan: ameinasibisha siku hio kwa kuipa jina la sehemu ya Badr, kwa ajil i ya utukufu wa yale yaliofanyika hapo. Kwa hivyo kunasibishwa siku ya Arafa na sehemu hio ya Arafa, si kwa sababu tufunge sawa sawa, bali ni kwa utukufu wa yale yanayotendeka. Na yanayotendeka hapo ni Munasaba wa kufunga si Sababu ya kufunga kama tulivyotangulia kubainisha. Na inampasa msomi - mwanachuoni na Talibu Al-ilm (mwanafunzi) - kutafautisha baina ya vitu viwili hivyo.

Ama kauli yenu: "Kama kawaida yake ndugu Juma anajikanganya kila mara, kama kweli anaamini kila nchi ifunge kwa muandamo wake na 'Arafah, kila nchi ifunge kivyake, inakuaje tena Ramadhaan iwe ni ya dunia nzima, 'Arafah iwe kila mtu na yake?" Mwisho wa kunukuu. Ninasema: hata hili pia nalo munalifanya kuwa ni hoja ya kielimu!!! Zote mbili - Ramadhani na Arafa - ni za dunia nzima, tafauti ni katika kuingia nyakati zake. Ramadhani ni refu Waislamu ni lazima watakutana kwani hakuna tafauti ya muandamo wa mwezi mzima; kuna tafauti ya siku moja mbili, Arafa ni tokeo la siku moja, inapotafautiana miandamo hupelekea kutafautiana kwa tarehe za kufunga na kula siku kuu.

MNASEMA

Hebu tuangalie hoja nyengine ya ndugu Juma katika uk 142 wa kitabu chake anapodai kunukuu maneno ya Shaykh Al-'Uthayminiy, anaposema: ("Na wakati wa mwezi ni kama wakati wa siku Kama vile ambavyo miji inatafautiana katika kuanza kujizuia (na kula na kunywa na jimai: yaani kuanza kufunga) na (inavyotafautiana katika) kufuturu kwa siku (daily) basi vivyo hivyo inawapasa watafautiane katika kujiz uia na kufuturu kwa mwezi (monthly)

a) Suala linakuja: Je! Kama anavyosema miji inatafautiana kufuturu kwa mwezi kama inavyotafautiana kwa siku. Sasa vipi katika nchi moja iliyo kubwa kama Tanzania ambayo ina mikoa inayotafautiana kuanza k ula na kunywa kama Dar es Salaam na Kigoma? Je! Mbona haitafautiani kwa mwezi? Inafunga kwa muandamo mmoja lakini Dar es Salaam na Kigoma zinatafautiana katika kuanza kula na kunywa (kufuturu) kwa zaidi ya dakika 45?

JAWABU

Hatuzungumzii watu wanatenda nini; tunazungumzia nini kinatakiwa Kisharia kitendwe. Watu wa Kigoma ikiwa muandamo kwao ni tafauti na Dar-es-Salam, basi ilivyo ni kuwa wafunge kwa mujibu wa Muandamo wao kama wanavyosali kwa mujibu wa mtenguko wao na kufuturu kwa mujibu wa kuzama jua kwao. Kinachotazamwa si tangazo au amri ya serikali, bali ni muandamo wa mwezi. Na hili - kama munavyojua - ni jambo ambalo wanavyuoni wamelizungumzia na wako walioeleza kama hivyo. Nchi kama Urusi, hasa kabla ya kugawanyika, vipi utamwambia mtu wa State moja ya mbali na iliotafauti kabisa na State nyengine kwamba wafunge sawa. Kinachozinagatiwa si suala la nchi moja bali ni umbali na tafati za matalai.

Pamoja na hayo, kama nilivyokuelezeni mara nyingi kwamba, suala la umbali gani watu wafunge sawa, linabakia kuwa ni uwanja wa ijtihad kwa kutokuwepo andiko lenye kuonesha umbali gani; ingawa andiko limeonesha kwamba muandamo wa mbali si hoja kwa walio mbali, kilichojificha ni umbali gani. Kwa hivyo, ukweli kwamba muandamo wa mbali si hoja kwa waliombali hili ni andiko ambalo lazima tusallim amri mbele yake; na je umabali huo uwe kiasi gani; hapa wenye elimu wana uwanja mpana wa kujitahidi na kutoa fat-wa na sisi tutatazama ilio na nguvu. Kwa hivyo, ikiwa watu wa Kigoma wamechukua ijtihad ya wanavyuoni wetu wakubwa waliotangulia wa Africa Mashariki, hilo linatoa nafasi kwani hapa uwanja wa ijtihad upo. Ama kutwambia kuwa dunia nzima tuwe na muandamo mmoja: hili ni kinyume na andiko na ni kinyume na maumbile yenyewe ya dunia.

MNASEMA

b) Kwa nini basi nchi kama Omani na Dubai zinatafautishwa katika kuangalia mwezi wakati ambapo nchi hizo hazina tofauti kubwa katika kuanza kula na kunywa? Wala hazina tofauti ya matlai wala masaa ya kuanza na kuingia kwa siku?

JAWABU

Imarati ni maamuzi ya serekali zao kufata Saudia; nalo ni kosa kwani wao na Oman ndio walio karibu zaidi na wana matalai sawa. Na nimekwambieni kuwa mjadala wetu si watu wanafanya nini: bali nini kinatakiwa kitedwe Kisharia. Vyenginevyo na mwengine anaweza kukuulizeni mbona Suudia wanafata muandamo wao; mbona Misr wanafata muandamo wao, n.k. Kwa hivyo, tuko pale pale kwamba hatuzungumzii nini watu wanafanya; bali tunazungumzia nini kinatakiwa kifanywe Kisharia.

MNASEMA

c) Tujuavyo sisi nchi zote za Uarabuni zinapata usiku wao mmoja na mchana wao mmoja, kwa hivyo hakuna shida yoyote katika kufunga 'Arafah siku moja kwa wote.

JAWABU

Sijakwambieni kuwa haiwezekani; nimesema kwamba ushihidi tulio nao ni kuwa:

1) Ibada za Hijja ikiwemo funga hio ya Arafa inategemea muandamo wa mwezi: si kisimamo cha Arafa. Kisimamo cha Arafa ni munasaba na muandamo wa mwezi ndio sababu ya ibada hizo.

2) Muandamo wa mbali si hoja kwa walio mbali.

MNASEMA

Shaykh Naaswir Khamiis 'Abdur-Rahmaan wa Mombasa Kenya ameandika kitabu chake "Mwezi Ko-Ongo" na amethibitisha tofauti ya masaa baina ya nchi mbali mbali mfano: "tofauti ya mji wa Mombasa na nchi ya magharibi ya mbali mwa Afrika kama Algeria ni masaa mawili na dakika ishirini na nane (2:28)" - uk 22. Katika jambo la kuonesha ufinyu aliokuwanao ndugu yetu Juma, ule wa kutokufanya uchunguzi wa kina katika mas-ala haya, yeye anaamini kwamba jambo hili limeanzishwa na Shaykh Naaswir Bachuu na wala halikuwepo ulimwenguni kama anavyodai mwenyewe kwa kauli yake ifuatayo: (Ninasema: Enyi walimwengu wenzangu tazameni hoja za kielimu hizo!!!!!!! Kwani nyinyi Wazanzibari kabla ya kuja fikra hio ya Sheikh Nassor Bachoo ya kufunga kwa muandamo mmoja)

JAWABU

Jambo gani hilo ambalo nimedai kuzushwa na Sheikh Nassor Bachoo? Hebu ninukulieni hilo jambo. Fikra ninayosema kuwa kaja nayo Sheikh Nassor Bachoo Zanzibar ni fikra ya kututaka tufunge kwa muandamo mmoja. Kwa Zanzibar yeye ndiye aliyeitangaza, kuilingania na kuitungia kitabu. Wala sikusema kuwa katika dunia yeye ndiye muasisi wa fikra hio. Ama yale mulioyanukuu kutoka kwa Sheikh Nassor Khamis, sio yalionifanya mimi nikapigwa na mshangao huo: ((Ninasema: Enyi walimwengu wenzangu tazameni hoja za kielimu hizo!!!!!!! Kwani nyinyi Wazanzibari kabla ya kuja fikra hio ya Sheikh Nassor Bachoo ya kufunga kwa muandamo mmoja). Kwa hivyo, musichanganye mambo. Mimi nilishagaa hivyo kwa sababu ya maneno haya ya Sheikh Nassor. Alisema Sheikh Nassor: "Pili kama ingalikuwa hakuna dhana ya kuwa mwezi ukionekana popote watu wafunge, Ibnu Abbas (r.a.) asingekuwa na haja ya kumuuuliza Kurayb juu ya habari za mwezi wa Sham kwa kusema:

"Kis ha (Ibn Abbas) akataja (habari) ya mwezi na akasema: "Ni lini mliuona mwezi?...akasema: "Wewe umeuona?" Hapo ndio nikashanga na nikasema: Hio ndio hoja nyengine ya Sheikh Bachoo, kwamba lau hakuna dhana ya kuwa mwezi ukionekana popote watu wafunge, basi Ibn Abbas asingekuwa na haja ya kumuuliza Kuraib "Lini mumeuona mwezi!!!" Ninasema: Enyi walimwengu wenzangu tazameni hoja za kielimu hizo!!!!!!! Kwani nyinyi Wazanzibari kabla ya kuja fikra hio ya Sheikh Nassor Bachoo ya kufunga kwa muandamo mmoja, mulikuwa hamuwaulizi watu wanaotoka nchi nyengine masuala kama hayo wanapokuja kwenu na nyinyi muko kati kati ya mwezi pamoja na kwamba nyote zamani mukifata muandamo wenu? Sasa kama nyinyi mulikuwa mukiuliza suala hilo hilo kwanini Ibn Abbas na yeye asiulize hata kama dhana hio haipo? Mimi binafsi nina kawaida ya kuwauliza wageni walioko nchi hii ninayoishi suala hilo, na natarajia kwamba pia nimewasikia watu wengi wenye kuwauliza wageni suala hilo. Kwa hakika shubuhati kama hizi hazifai katika kujadili mambo ya kielimu. Kwa ufupi ni kuwa hata kama dhana hio ilikuwepo, dhana hio inabomolewa na kukataa kwake - Ibn Abbas - kuukubali mwezi wa Sham, na kujenga hoja kwa Hadith marfu'u kwamba hayo ndio mafunzo ya Mtume(s.a.w.w) kwao. Sasa uko wapi uhusiano wa maneno yangu na nakala ya Sheikh Nassor Khamis?

MNASEMA

Sasa sisi tunataka kumtihibitishia ndugu Juma kuwa wapo watu wengi ambao pengine hawakuwafikiana na Shaykh Naaswir Bachuu katika baadhi ya mambo au misimamo lakini kwa bakhti nzuri katika hili suala la kufunga 'Arafah na kusali siku ya 'Iydul-Adh-ha wanafuata Makkah na wanaungana na ulimwengu mzima. Mfano mzuri kabisa ni ndugu zetu wa Tarika ya Kadiria, takriban wote wanafunga 'Arafah kwa kufuata tarehe 9 - Dhul-hijjah ya Saudia (Makkah). Hayo yanathibitishwa na aliyekuwa kiongozi wao Mkuu wa Tarika hiyo mwanachuoni maarufu Al-Marhuum Shaykh Muhammad Naaswir Abdulla Al-Qaadiry ambaye aliandika kitabu alichokiita: "Kitabu 'Arafah" na kuandika kwenye gamba la kitabu hicho kwamba: "Nguzo Kubwa Ya Hijjah Ni 'Arafah Tarehe Tisa Mfunguo Tatu Na Kuswali 'Iydul-Hajj Sawa Na Makkah." Katika uk 22 wa kitabu chake hicho pia ameandika kama ifuatavyo: "Waislamu wote ulimwenguni wafunge Sunnah ya 'Arafah sawa na 'Arafah ya Makkah."

Kisha katika uk 74 ameandika Fatwa zifuatazo: "'Arafah ya Makkah tarehe 9 mwezi wa Mfunguo Tatu (Dhul-Hajj) ndiyo 'Arafah ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala) na ndiyo 'Arafah ya Waislamu wote popote walipo ulimwenguni." "Wananaokwenda Hijja, kwao ni haramu kufunga siku hiyo ya 'Arafah huko 'Arafaati (Makkah) na waliobaki majumbani, kwao ni Sunnah kubwa kufunga siku hiyo hiyo ya 'Arafah ya Makkah kokote waliko ulimwenguni." "Tarehe 10 Mfunguo Tatu (Dhul-Hajj) ndiyo siku ya 'Iyd ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala) na 'Iyd ya dunia nzima kwa Waislamu wote. Kufunga siku hiyo yote kamili ni haramu. Anayeswali 'Iyd tarehe 10 ya Makkah amefanikiwa na ole wake yule anayeswali 'Iyd siku atakayo mwenyewe. Kwa ujumla kufunga tarehe 9 Mfunguo Tatu kwa Mahujaji 'Arafah ni Haramu. Na kufunga kwa Waislamu wote ulimwenguni tarehe 10, 11, 12 na 13 Mfunguo Tatu ni Haramu."

"Hivyo ni jambo baya kabisa na lenye kutia huzuni sana kuwaona baadhi ya ndugu zetu Waislamu wanaacha kufunga siku ya 'Arafah Aliyoiteua Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala) na badala yake wanafunga siku ya kuchinja tarehe 10 (ya Makkah) wakisingizia kuwa ndiyo siku yao ya 'Arafah waitakayo wao waliyoichagua wao wenyewe ambayo kufunga siku hiyo ni haramu."

JAWABU

Haya! Hoja iko wapi humu! Je hii ni hoja kwamba alivyosema Sheikh Muhammad Nassor ni sahihi au ni hoja kwamba kuna watu wanaafikiana na nyinyi katika hilo? Ikiwa ndio munatoa hoja kwamba alivyosema Sheikh Muhammad Nassor ni sahihi; nitakutakeni dalili ya usahihi huo; ikiwa munatoa hoja kwamba kuna watu wanaafikiana na nyinyi katika hilo; hapo sikupingini. Lakini suala letu bado lipo: 1) Nini sababu ya kufunga Arafa.

2) Je sababu ni kisimamo cha Arafa.

3) Je ni muandamo wa mwezi wa mfunguo tatu.

4) Je tufate muandamo mmoja au kila mtu wake.

Mimi ushahidi nilio nao ni kuwa:

1) Sababu ya kufunga Arafa ni muandamo wa mfunguo tatu, kama ilivyonena Hadithi ya Amir wa Makka.

2) Kisimamo cha Arafa si sababu kwani sababu hutangulia kisha ndio kikija kilichosababishwa. Kama linavyotenguka jua ndio ukaingia wajibu wa kusali; au unavyoingia mwezi wa Ramadhani ndio ukaja wajibu wa Ramadhani. Ama kisimamo cha Arafa kinaanza baada ya kutenguka jua wakati wenye kufunga wanaanza kufunga tangu Alfajiri. Kwa hivyo, kisimamo cha Arafa ni munasaba ni sababu.

3) Kila watu wafate muandamo wao kwa mujibu wa Hadithi ya Ibn Abbas na Kuraib.