MUANDAMO WA MWEZI

MUANDAMO WA MWEZI 0%

MUANDAMO WA MWEZI Mwandishi:
Kundi: Midahalo na majadiliano kielimu

MUANDAMO WA MWEZI

Mwandishi: Juma Muhammad Rashid Al-Mazrui, Al-Zenjibari.
Kundi:

Matembeleo: 59180
Pakua: 4789

Maelezo zaidi:

MUANDAMO WA MWEZI
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 23 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 59180 / Pakua: 4789
Kiwango Kiwango Kiwango
MUANDAMO WA MWEZI

MUANDAMO WA MWEZI

Mwandishi:
Swahili

19

MUANDAMO WA MWEZI

SEHEMU YA KUMI NA NANE

KUFUNGWA KWA MASHETANI

MUNASEMA

18. Kufungwa Kwa Mashetani Katika kejeli zake ndugu Juma kwenye hoja za Kidini, hata katika maneno ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anathubutu kuyaumbua kwa kusema kama ifuatavyo: ((Hoja nyengine - ya mitaani - inasema kwamba Ramadhani inapoingia hupatikana rehema fulani. Miongoni mwa hizo ni kuwa mashetani wote hufungwa kama Bwana Mtume(s.a.w.w) alivyosema: "Ramadhani ikiingia, milango ya mbingu (na katika riwaya ya pili) milango ya pepo hufunguliwa, na milango ya jahannam hufungwa na mashetani hutiwa minyororo." Na Hadithi nyengine inasema: "Inapoingia siku ya kwanza ya Ramadhani upepo hupiga chini ya Arshi kutoka katika majani ya pepo (kuwapiga upepo huo) Mahuru-Al-ain.)

Maneno kama haya ya kuyakejeli na kuyabeza maneno matukufu ya Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuyafanya kama kwamba ni maneno ya mitaani au kuifanya haki kuwa batil ni katika mambo yanayompelekea mtu kuingia katika kufru. Kitu cha msingi ni vyema kukumbuka kwamba Shaykh Naaswir Bachuu hakuonesha lugha za kashfa na kejeli hata katika yale maeneo ambayo hakukubaliana nayo basi pia alitumia lugha ya kistaarabu.

JAWABU

Kejeli iko wapi hapa? Je mimi niliyaita maneno ya Mtume(s.a.w.w) kuwa ndio hoja ya mitaani au niliita kule Sheikh Nassor Bachoo kutoa hoja kwa Hadithi hio kuwa ndio hoja ya mitaani? Ebu Soma yote niliosema. Nilisema: Hoja nyengine - ya mitaani - inasema kwamba Ramadhani inapoingia hupatikana rehema fulani. Miongoni mwa hizo ni kuwa mashetani wote hufungwa kama Bwana Mtume(s.a.w.w) alivyosema: "Ramadhani ikiingia, milango ya mbingu (na katika riwaya ya pili) milango ya pepo hufunguliwa, na milango ya jahannam hufungwa na mashetani hutiwa minyororo." Na Hadithi nyengine inasema: "Inapoingia siku ya kwanza ya Ramadhani upepo hupiga chini ya Arshi kutoka katika majani ya pepo (kuwapiga upepo huo) Mahuru-Al-ain."

Tunachojifunza kutokana na Hadithi hizi ni kuwa:

1) Ramadhani ni moja!!!

2) Neema hizo za kufungwa mashetani na nyenginezo hupatikana siku ya mwanzo ya Ramadhani. Sasa je:

a) Rehema hizi watazipata dunia nzima au wale waliouona mwezi tu?!!!

b) "Inapotokea nchi fulani kama Saudia (Makka & Madina) imeingia katika Ramadhani, Tanzania wanangoja mwezi wao.

Je inaaminika kwamba wale mashetani walioko nchini S. Arabia yatakuwa yamefungwa na mashetani yalioko Tanzania watabaki huru bado? Au tudhani mashetani yalioko S. Arabia yatakimbilia huku Tanzania mbio kuja 'kuvunja jungu' kwa kuwa Ramadhani haijaingia huku bado?"

c) Je mtu aliyeanza kufunga S. Arabia siku ya mwanzo, siku ya pili akaja Tanzania wakati bado watu hawajaanza kufunga, vipi ile rehema ya kufungiwa mashetani ataipata, au watafungwa kwa ajili yake tu?!!!

d) Je mtu huyu aliyeanza kufunga Ramadhani S. Arabia kisha alipokuja Tanzania Ramadhani bado je ataambiwa kaja kufunga Ramadhani au kafunga Ramadhani Saudia na kaja kufunga Shaabani huku Tanzania.

e) Nini hukumu ya saumu ya mtu huyu?!

Masuala haya nimeyanukuu kimaana kutoka katika kitabu cha Sheikh Bachoo , nayo ni masuala ya kuchekesha na kustaajabisha!!! Lau tutakwenda mahala kama Al-azhar au chuo chochote kile kikubwa tukatoa hoja hizi, basi hata yule anayeona kwamba kauli sahihi ni kauli ya kufunga kwa muandamo mmoja basi atacheka sana!!!

Ama kuhusu suala la kwanza kwamba Hadithi hizi zinathibitisha kuwepo Ramadhani moja, Jawabu yake ni kuwa Ramadhani kweli ni moja. Na kwani ni nani kasema kwamba kuna Ramadhani mbili katika mwaka? Ramadhani ni moja katika mwaka isipokuwa inatangulia kuingia katika miji fulani na kuchelewa katika miji myengine, kama vile ambavyo - katika Ramadhani moja hio hio, tunatangulia kufunga katika baadhi ya miji kwa kutangulia kuchomoza alfajiri na tunachelewa kufunga katika miji myengine kwa kuchelewa kuingia alfajiri. Na tunatangulia kufuturu katika miji myengine kwa kutangulia kutua kwa jua na tunachelewa katika miji myengine kwa kuchelewa kutua kwa jua. Na hii haina maana kwamba kuna Ramadhani tano au kumi.

Ramadhani zingelikuwa mbili lau ingelikuwa tunafunga mwezi huo wa Ramadhani, na mwezi mwengine, mathalan tunafunga na mfunguo sita, lakini tunafunga mwezi mmoja, tafauti ni katika kutangulia na kuchelewa tu, basi vipi mtu atatoa hoja kama hio!!! Tazama ukweli kwamba, pia kuna watu wanatangulia kusali Adhuhuri na wengine wanachelewa kwa masaa mengi, wala haisemwi kwamba kuna Adhuhuri tatu au nne. Kwa hivyo, dai hili halina muelekeo kabisa wala halifai kuzungumzwa na wanavyuoni wala wanafunzi, dai hili linafaa kuzungumzwa na watu wasiojua Dalili za Kisharia.

Pili : ni kuwa Hadithi mbili hizo alizozinukuu Sheikh Bachoo hazitoi ushahidi huo kamwe wa kuwa na Ramadhani moja, kwani mantiki ya kusemwa "Ikiingia Ramadhani" ni sawa sawa na kusemwa: "Ikiingia J/tatu" au kusemwa "Ukiingia usiku" na hii haina maana kwamba J/tatu ikianza kuingia sehemu moja huwa imeingia dunia nzima: bali ikianza kuingia sehemu moja - yaani baada ya kutua jua magharibi - sehemu nyengine bado ni J/pili asubuhi. Halkadhalika kusemwa "Ukiingia usiku" kama Allah alivyosema: Usiku ulipomuingilia: haina maana kwamba usiku ukiingia sehemu moja ndio umeingia dunia nzima. Kwa ufupi ni kuwa hii ni hoja ambayo haina faida yoyote ya kielimu, lakini tunaijadili kwa ajili ya watu wa mitaani tu.

Ama suala linalosema: "Je mtu huyu aliyeanza kufunga Ramadhani S. Arabia kisha alipokuja Tanzania Ramadhani bado je ataambiwa kaja kufunga Ramadhani au kafunga Ramadhani Saudia na kaja kufunga Shaabani huku Tanzania Nini hukumu ya saumu ya mtu huyu?!" Jawabu yake ni kuwa: je mtu aliyepanda ndege siku ya J/pili - mathalan - ikamkuta magharibi humo katika ndege katika sehemu fulani ya anga ya dunia akafuturu, kisha baada ya saa moja au mbili akaingia katika anga ya nchi nyengine bado ni saa 9 za jioni ya siku hio hio ya J/pili, funga yake itakuwaje: je ataambiwa kafunga huyu siku ya J/pili au kafunga nusu ya siku hio katika sehemu moja ya dunia na kala katika sehemu nyengine ya dunia?

Tena mara ya pili: je mtu aliyepanda ndege akaanza kusali Adhuhuri humo katika sehemu ambayo jua tayari limetenguka au akasali magharibi katika sehemu ambayo jua tayari limezama na kabla ya kumaliza ikawa ndege imeingia katika sehemu ambayo jua bado halijatenguka au halijazama, je yule aliyesali Adhuhuri ataambiwa kasali Adhuhuri au kasali nusu adhuhuri na nusu Dhuha?! Na yule aliyesali magharibi atakuwa kasali magharibi au kasali sala ambayo nusu yake ni magharibi na nusu yake ni laasiri kipande: yenye rakaa tatu? Jawabu yako hapa ndio jawabu yetu kule. Utaona kwamba masuala yote haya si yenye kima katika soko la elimu, bali ni masuala ya kuwababaisha watu wasiojua nini cha kujadiliwa katika mas-ala haya ya funga.

Sasa cha muhimu kujua ni kuwa Dini ya Kiislamu imeyagawa mambo katika sehemu nne kuu. Moja ni kitu ambacho kimeelezwa katika Qur-an kwa uwazi. Pili ni kitu ambacho kimeelezwa katika Sunnah (Hadithi) kwa uwazi. Tatu ni kitu ambacho Umma umekubaliana juu ya kitu hicho. Mambo matatu haya hayafai kupingwa: ni lazima tufanye vile vile ilivyoelezwa kwa uwazi. Sasa mambo mengine (ambayo ndio ya nne) ni yale ambayo hayakuelezwa kabisa au hayakufafanuliwa nayo ni kama hayo:

1) Aliyefunga katika nchi fulani kisha akaja katika nchi nyengine watu wako katika Shaabani.

2) Kama tulivyosema: "Aliyepanda ndege siku ya J/pili - mathalan - ikamkuta magharibi humo katika ndege katika sehemu fulani ya anga ya dunia akafuturu, kisha baada ya saa moja au mbili akaingia katika anga ya nchi nyengine bado ni saa 9 za jioni ya siku hio hio ya J/pili ya tarehe hio hio alioiwacha katika nchi alioondoka, funga yake itakuwaje: je ataambiwa kafunga huyu siku ya J/pili au kafunga nusu ya siku hio katika sehemu moja ya dunia na kala katika sehemu nyengine ya dunia?"

3) Aliyesali Magharibi katika ndege baada ya kutua jua kabla ya kumaliza sala yake ndege imeingia katika anga ambayo jua lake bado halijatua, je itakuwaje sala yake.

Mas-ala haya na yalio mfano wa haya hayana andiko maalumu lililo wazi, kwa hivyo huitwa mas-ala ya ijtihadi. Kila aliyefikia daraja ya kuitwa Mujtahid atatoa fikra yake akijiongozea kwa dalili za Kisharia (Qur-an, Sunna, Ijmaa (makubaliano ya Umma) au Qiyas (analogy). Kwa hivyo, utaona kwamba bado tuna tatizo la kutokufahamu tafauti baina ya mas-ala ya ijtihadi na yale yasio ya ijtihadi. Mas-ala ya kutokufata muandamo wa mbali yamethibiti kwa Hadithi ya Mtume (s.a.w.) katika riwaya hio ya Ibn Abbas na Kuraib, kwa hivyo haya si mas-ala ya ijtihadi, lakini furui (matawi) tunazozipata katika mas-ala haya na ambazo hazikuelezwa kwa uwazi, ndizo za kufanyiwa ijtihadi.

Sasa kwa ufupi ni kuwa jawabu ya suala "Nini hukumu ya saumu ya mtu huyu" aliyefunga Ramadhani S. Arabia na alipokuja Tanzania akakuta watu wanakula bado ni Shaabani, jawabu ya suala hili ni jawabu ya masuala mawili tulioyatoa, nayo ni masuala ya aliyefuturu na aliyesali kwenye ndege. Na hii ni kuwa:

1) Ima aliyesali basi sala yake aliosali mwanzo aitupilie mbali na aanze upya kwani katika sehemu alio bado wakati wa Sala haujaingia. Halkadhalika aliyefuturu. Ukichukua msingi huu, basi na aliyefunga Saudia Ramadhani na alipokuja Tanzania akaikuta Shaabani bado imo, basi saumu yake asiizingatie na aanze upya kwani katika sehemu alio bado wakati wa kufunga haujaingia.

2) Au asirejee tena sala yake kwani kasali kwa mujibu wa wakati sawa huko alikotoka. Halkadhalika aliyefuturu. Basi na huyu aliyetoka Saudia naye aendelee kufunga kwa kuzingatia kwamba kafunga sawa kwa mujibu wa kule anakotoka. Kwa hivyo, chagua jawabu unayotaka katika mas-ala haya mawili ya aliye kwenye ndege, kisha jawabu yako hio utayoichagua ndio jawabu yetu kwako kwa yule aliyefunga S. Arabia na akaja Tanzania hali ya kuwa bado ni Shaabani.

Ama masuala ya kufungwa mashetani hayana uhusiano kabisa na masuala ya kuthibiti muandamo wa mwezi katika miji pasi na kuthibiti katika miji myengine. Na kipi kinatujuilisha sisi kwamba mwezi ukiandama sehemu moja hufungwa mashetani wa dunia nzima au kila mahala hufungwa mashetani kwa mujibu wa muandamo wa mwezi wa mahala hapo? Kipi kitatujuilisha mas-ala haya. Haya ni mas-ala ya ghaibu wala hayatakiwi kabisa kuhusishwa na mas-ala ya dhahiri. Hadithi inatueleza kwamba mashetani hufungwa. Vipi wanafungwa: hakuna ufafanuzi. Na mas-ala haya ni mas-ala ya itikadi haitakiwi kusema kwa ijtihadi na rai wala kwa kusukuma. Bali Hadithi hio inabidi itazamwe, ikiwa ni Hadithi sahihi na ni mutawatir basi tuikubali; ikiwa sahihi lakini ni Ahadi basi tutatazama ikiwa Umma umekubaliana juu ya maana yake, itakuwa imepata nguvu kwa Ijmaa (makubaliano) ya Umma; ikiwa kuna khilafu nayo ni Hadithi Ahadi basi tuiache kama ilivyo, kwani Hadithi Ahadi haijengewi hoja katika mambo ya itikadi, kama Jumhuri ya Umma ilivyosema. Mwisho wa kunuu nilioyasema katika kitabu.

Hayo ndio nilioyasema. Haya nionesheni hapa wapi nimeyakejeli maneno ya Mtume(s.a.w.w) . Mimi ninachokipinga ni kuzichukua Hadithi hizo za kufungwa kwa mashetani kama ni ushahidi wa kuwepo kwa muandamo mmoja: sio kuzikejeli Hadithi hizo. Bali nimesema katika maelezo ya chini: "Ibn Hajar ana maelezo mazuri kuhusu Hadithi ya kufungwa mashetani. Tazama Al-Fat-Hu katika sherehe ya Hadithi na. 1899". Sasa tuseme ndio mumekuwa hamufahamu kiasi hiki au muna lengo lenu?!

Munasema Tukirudi katika mafunzo ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya kufungwa kwa mashetani tunazingatia juu ya kuingia kwa mwezi wa Ramadhaan, kwani maneno ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) yamekuja katika matamko yasemayo: (Inapoingia siku ya mwanzo ya Ramadhaan mashetani hufungwa)

Ndugu Juma akiendelea kudai kwamba: (Ikiingia Ramadhani" ni sawa sawa na kusemwa: "Ikiingia J/tatu" au kusemwa "Ukiingia usiku" na hii haina maana kwamba J/tatu ikianza kuingia sehemu moja huwa imeingia dunia nzima: bali ikianza kuingia sehemu moja - yaani baada ya kutua jua magharibi - sehemu nyengine bado ni J/pili asubuhi.)

Hayo ndio kama yale tunayomueleza ndugu Juma kila mara kwamba Suala la kutangulia mchana au usiku sio hoja katika mas-ala ya muandamo wa mwezi. Hilo ni jambo lisilowezekana kutumia "Qiyaas" cha mwezi na jua. Hapawezekani kutumiwa "Qiyaas" cha Swala, kuanza kufutari wakati wa magharibi au nyakati za kula daku kabla ya alfajiri hata katika nchi moja kuna kutafautiana katika kuingia mchana na usiku pia kuna kutafautiana katika kuingia "siku." Tuchukulie mfano Dar es Salaam inaingia katika siku ya Jumapili pale jua linapotua, wakati huo huo Kigoma bado iko katika siku ya Jumamosi jioni. Lakini kumbuka kwamba wanafunga siku moja ya muandamo wa mwezi mmoja. Tukichukua mfano mwengine wa nchi kubwa kama Canada au Urusi, ndani ya nchi hizo kuna tafauti ya masaa mengi kutoka mashariki hadi magharibi zake.

JAWABU

Haya yote nimeshayaeleza - mas-ala ya Qias, mas-ala ya kuwa na nyakati tafauti za kufuturu katika nchi moja yote mumeyakariri mara elfu na tumeshayaeleza sana. Lakini pamoja na hayo, hayana uhusiano na maudhui iliopo hapa. Maudhui ya hapa ni kufungwa kwa mashetani na hili pia nimeshakufafanulieni kwamba si hoja ya kuwa tuwe na muandamo mmoja wala mas-ala hayo hayapo kamwe katika uwanja wa elimu.

MNASEMA

Akiendelea kutoa hoja zake ndugu Juma juu ya kufungwa kwa Mashetani anahoji: (Na kipi kinatujuilisha sisi kwamba mwezi ukiandama sehemu moja hufungwa mashetani wa dunia nzima au kila mahala hufungwa mashetani kwa mujibu wa muandamo wa mwezi wa mahala hapo?) Hapa Ndugu Juma amekuja na dhana kwamba mashetani hufungwa pale tu ilipoingia Ramadhaan. Na sisi tunamuuliza ni wapi ameona kuwa ikiingia Ramadhaan hufungwa mashetani wa sehemu hiyo tu iliyoandama mwezi?

JAWABU

Hilo suala jijibuni wenyewe kwani mimi sijasema hivyo wala sijaja na dhana hio, ingawa nadai kwamba inawezekana ikawa hivi na inawezekana ikawa hivi: hakuna ushahidi wa mkato juu ya vipi mashetani wanafungwa. Na mimi nilichokisema ni hiki: Ama masuala ya kufungwa mashetani hayana uhusiano kabisa na masuala ya kuthibiti muandamo wa mwezi katika miji pasi na kuthibiti katika miji myengine. Na kipi kinatujuilisha sisi kwamba mwezi ukiandama sehemu moja hufungwa mashetani wa dunia nzima au kila mahala hufungwa mashetani kwa mujibu wa muandamo wa mwezi wa mahala hapo? Kipi kitatujuilisha mas-ala haya.

Haya ni mas-ala ya ghaibu wala hayatakiwi kabisa kuhusishwa na mas-ala ya dhahiri. Hadithi inatueleza kwamba mashetani hufungwa. Vipi wanafungwa: hakuna ufafanuzi. Na mas-ala haya ni mas-ala ya itikadi haitakiwi kusema kwa ijtihadi na rai wala kwa kusukuma. Bali Hadithi hio inabidi itazamwe, ikiwa ni Hadithi sahihi na ni mutawatir basi tuikubali; ikiwa sahihi lakini ni Ahadi basi tutatazama ikiwa Umma umekubaliana juu ya maana yake, itakuwa imepata nguvu kwa Ijmaa (makubaliano) ya Umma; ikiwa kuna khilafu nayo ni Hadithi Ahadi basi tuiache kama ilivyo, kwani Hadithi Ahadi haijengewi hoja katika mambo ya itikadi, kama Jumhuri ya Umma ilivyosema.

MNASEMA

Tujuavyo sisi ni kuwa tamko la "Ashshayaattwiinu" kwa hapa lina maana ya mashetani wote dun ia nzima. Tamko lililokuja katika Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu kufungwa kwa mashetani inapoingia siku ya mwanzo ya Ramadhaan yaani, lina "Alif na Laam" ambayo linaonesha ni tamko la umumi ('aam). Neno ni na kawaida ya neno "Ismul-jinsi" linawakilisha maana ya ('aam) yaani linazungumzia "ujumla" au "wote". Baadhi ya vitabu vilieleza kwamba "Ismul-jinsi" kuwa ni ('aam)

Ni vyema kuelewa kuwa msimamo wa Shaykh Naaswir Bachuu katika kitabu chake ni kuwataka Waumini wote wafunge na kufungua kwa "Siku moja" na msimamo wake huo unatokana na Hadiyth sahihi ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo na watu wote kwamba: ((Fungeni kwa kuonekana mwezi - muandamo.)) Maneno hayo ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) yanawajumuisha Waumini wote, popote walipo kama tulivyokwisha elezea hayo katika kurasa zilizopita. Kwa upande wa utekelezaji wa kufunga na kufungua kwa dunia nzima siku moja, uwezekano huo pia upo kama tulivyokwisha elezea kwa urefu.

JAWABU

Madai yenu: "Tujuavyo sisi ni kuwa tamko la "Ashshayaattwiinu" kwa hapa lina maana ya mashetani wote dunia n zima. Tamko lililokuja katika Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu kufungwa kwa mashetani inapoingia siku ya mwanzo ya Ramadhaan yaani, lina "Alif na Laam" ambayo linaonesha ni tamko la umumi ('aam). Madai haya yanaonesha hamujui mukisemacho. Huu sawa ni ujumla lakini kwa mujibu wa qarina (context) ya Hadithi hakuna ulazima wa kuwa iwe ni ujumla wa dunia nzima. Sababu ni kama ilivyo katika Hadithi: "Ikiingia siki ya kwanza ya Ramadhani" na Ramadh ani haiingii dunia nzima kwa wakati mmoja. Bali kuna sehemu imeingia yaani kwa kuingia magharibi na kuna sehemu ni asubuhi - Ramadhani haijaingia. Ni sawa na kusema "Ikiingia J/tatu", J/tatu huwa haiingi dunia nzima wakati mmoja. Kwa hivyo, ujumla uliomo katika mashetani si lazima uwe ujumla wa dunia, bali inawezekana ikawa hivyo, na inawezekana ikawa pale ilipoingia Ramadhani tu, kwani tamko ikiingia siku ya kwanza ya Ramadhani haliuhusu ulimwengu wote. Kwa hivyo, hili ni suala la ghaib na halina ufafanuzi bali lina ihtimalat uwezekano huu na ule. Kwa hivyo, hii si hoja inayokubalika Kisharia.

MNASEMA

Baada ya maelezo kama hayo: Ndugu Juma anatoa hoja za kutokuwepo uwezekano huo kwa kutoa mifano tofauti kama ifuatayo: ((je mtu aliyepanda ndege siku ya J/pili - mathalan - ikamkuta magharibi humo katika ndege katika sehemu fulani ya anga ya dunia akafuturu, kisha baada ya saa moja au mbili akaingia katika anga ya nchi nyengine bado ni saa 9 za jioni ya siku hio hio ya J/pili, funga yake itakuwaje: je ataambiwa kafunga huyu siku ya J/pili au kafunga nusu ya siku hio katika sehemu moja ya dunia na kala katika sehemu nyengine ya dunia? Tena mara ya pili: je mtu aliyepanda ndege akaanza kusali Adhuhuri humo katika sehemu ambayo jua tayari limetenguka au akasali magharibi katika sehemu ambayo jua tayari limezama na kabla ya kumaliza ikawa ndege imeingia katika sehemu ambayo jua bado halijatenguka au halijazama, je yule aliyesali Adhuhuri ataambiwa kasali Adhuhuri au kasali nusu adhuhuri na nusu Dhuha?!))

JAWABU

yetu kwa ndugu Juma ni pale pale kwamba: a). Hayo ni mas-ala ya Ijtihaad kama alivyotaja mwenyewe ndugu Juma kwenye uk 168 wa kitabu chake. Ndio maana hakuna kauli moja ya Wanavyuoni katika mas-ala hayo.

JAWABU

Kwani mimi nilisema hivi kujibu nini. Tafadhali rejeeni mjadala kamili: musikate maneno vipande bila kutimaza maana. Nukta hii ilikusudiwa kujibu kitu maalumu nayo ni kuwa Sheikh Nassor aliuliza masuala haya:

1) Je mtu huyu aliyeanza kufunga Ramadhani S. Arabia kisha alipokuja Tanzania Ramadhani bado je ataambiwa kaja kufunga Ramadhani au kafunga Ramadhani Saudia na kaja kufunga Shaabani huku Tanzania.

2) Nini hukumu ya saumu ya mtu huyu?!

Hayo ndio masuala yake. Nami nikamjadili kwa kusema: Ama suala linalosema: "Je mtu huyu aliyeanza kufunga Ramadhani S. Arabia kisha alipokuja Tanzania Ramadhani bado je ataambiwa kaja kufunga Ramadhani au kafunga Ramadhani Saudia na kaja kufunga Shaabani huku Tanzania Nini hukumu ya saumu ya mtu huyu?!" Jawabu yake ni kuwa: je mtu aliyepanda ndege siku ya J/p ili - mathalan - ikamkuta magharibi humo katika ndege katika sehemu fulani ya anga ya dunia akafuturu, kisha baada ya saa moja au mbili akaingia katika anga ya nchi nyengine bado ni saa 9 za jioni ya siku hio hio ya J/pili, funga yake itakuwaje: je ataambiwa kafunga huyu siku ya J/pili au kafunga nusu ya siku hio katika sehemu moja ya dunia na kala katika sehemu nyengine ya dunia?

Tena mara ya pili: je mtu aliyepanda ndege akaanza kusali Adhuhuri humo katika sehemu ambayo jua tayari limetenguka au akasali magharibi katika sehemu ambayo jua tayari limezama na kabla ya kumaliza ikawa ndege imeingia katika sehemu ambayo jua bado halijatenguka au halijazama, je yule aliyesali Adhuhuri ataambiwa kasali Adhuhuri au kasali nusu adhuhuri na nusu Dhuha?! Na yule aliyesali magharibi atakuwa kasali magharibi au kasali sala ambayo nusu yake ni magharibi na nusu yake ni laasiri kipande: yenye rakaa tatu? Jawabu yako hapa ndio jawabu yetu kule. Utaona kwamba masuala yote haya si yenye kima katika soko la elimu, bali ni masuala ya kuwababaisha watu wasiojua nini cha kujadiliwa katika mas-ala haya ya funga. Kwa hivyo, huu ndio mnasaba wa mimi kusema hayo mulioyanukuu. Ama ikiwa hamukujilazimisha kunukuu kitu kwa ukamilifu, mutamfanya msomaji asijue nini hasa kimezungumzwa.

MNASEMA

b). Ndugu Juma anapenda kutumia "Qiyaas" cha Sala na Funga (Swaum) ambapo tumeshaeleza kwamba ni jambo lisilokubaliana kabisa. Hayo tumeyaeleza sana , tatizo sio muandamo mmoja au mingi, hata katika nchi moja inatokea, unaweza kusafiri kwa ndege ukasali katika anga la Dar-es-salaam Adhuhuri ukafika Kigoma bado haijaingia Adhuhuri. Je utasema Dar-es-salaam na Kigoma kila moja iangalie mwezi wake? Au kama utaondoka Dar es Salaam umeshafuturu ukafika Kigoma jua halijatua bado utafanyaje?

JAWABU

Ni kweli: hayo mumeyaeleza sana nami nimekujibuni sana nanyi munakariri yayo kwa yao. Suala la miandamo nimekwambieni haitazamwi nchi moja; inatazamwa tafauti za matalai na umbali wa masafa. Kwa hivyo, hii hoja yenu munayoikariri "Hata nchi moja; hata nchi moja" hii si hoja ya kuzingatiwa, kwani kinachotazamwa ni tafauti za matala na umbali: si nchi moja au nchi tafauti. Ama huyu aliyetoka Dar baada ya kufuturu akafika Kigoma bado jua halijatua, sijui kenda kwa chombo gani, maana Unguja na Pemba kwa ndege - nadhani - haipungui nusu saa; sasa Kigoma yenye tafauti ya dakika 40 kwa mujibu wa maneno yenu na masafa ni marefu mno, sijui kapanda chombo gani!

MNASEMA

Kabla ya kuendelea na ufafanuzi zaidi ni vyema kumnukuu ndugu Juma katika maelezo yake anaposema: (Sasa cha muhimu kujua ni kuwa Dini ya Kiislamu imeyagawa mambo katika sehemu nne kuu. Moja ni kitu ambacho kimeelezwa katika Qur-an kwa uwazi. Pili ni kitu ambacho kimeelezwa katika Sunnah (Hadithi) kwa uwazi. Tatu ni kitu ambacho Umma umekubaliana juu ya kitu hicho. Mambo matatu haya hayafai kupingwa: ni lazima tufanye vile vile ilivyoelezwa kwa uwazi. Sasa mambo mengine (ambayo ndio ya nne) ni yale ambayo hayakuelezwa kabisa au hayakufafanuliwa) Kwa maelezo hayo mazuri aliyoyaeleza ndugu Juma tungependa kumuuliza:

Je suala la kufunga na kufungua kwa muandamo mmoja ataliweka wapi katika mafungu hayo? Bila shaka suala hili litawekwa katika kifungu cha pili. Yaani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amelieleza jambo hili kwa uwazi. Riwaya zote zilizokuja katika agizo hili ni sahihi na zenye kukubalika mbele ya Wanazuoni wote wa Kiislamu. Na riwaya zote hizo zimekuja kwa Waumini wote popote walipo watekeleze agizo hilo Mwanachuoni maarufu Al-Jassas katika kitabu chake Ahkamul-Qur-aan J. I uk 305 katika kuielezea kauli hii ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema hivi:- "Ni jambo linaloeleweka kuwa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo: (Fungeni kwa kuonekana mwezi na fungueni kwa kuonekana mwezi), ni ya jumla inawahusisha watu wa pande zote za dunia na kwamba haihusu watu wa nchi moja peke yao pasi na wengine."

JAWABU

Tunaendelea kukariri. Suala la kufunga kwa miandamo tafauti limefafanuliwa na Hadithi ya Ibn Abbaas, kilichojificha ni masafa. Ama Hadithi munazosema nyinyi ni Hadithi Aam. Lakini suala ni kuwa je ujmla wenyewe ni ujmla gani. Tumeshakubainishieni kuwa ujmla wenyewe ni kuwa watu wote wanaamrishwa kuwa wasifunge ila kwa kuuona. Ndio maana katika riwaya nyengine ikaja "Musifunge mpaka muuone". Hakuna katika riwaya zote hizo ufafanuzi juu ya suala la kuwa je tufunge kwa muandamo mmoja au kila watu wawe na muandamo wao. Ufafanuzi huu unapatikana katika Hadithi ya Kuraib na Ibn Abbaas ambayo munaikimbia: hamuitaki. Kwa hivyo, maneno ya Al-Jassas si sahihi, na kama mulivyosema, maneno ya mwanachuoni hayana kima ikiwa yatakwenda kinyume na dalili. Madai hayo yanaifanya Hadithi ya Kuraib na Ibn Abbaas isizingatiwe: iwachwe wakati kanuni ni kutokuliacha andiko lolote litapowezekana kutendewa kazi. Kwa ufupi ni kuwa, hoja hio niliijibu kama ifatavyo: Jambo la pili: la kutazamwa katika Hadithi hii ni kuwa Khitabu (Agizo: kama alivyofasiri Sheikh Nassor Bachoo) ya Hadithi hii ni Aam (ya ujumla), kama Sheikh alivyon ukuu kutoka katika kitabu cha Al-sayyid Saabiq.

Na sisi tunajibu kwa jawabu mbili. Ya kwanza ni kuwa: Ujumla wa agizo hilo, umehusishwa na Hadithi ya Ibn Abbas, na kanuni ya kiusuli inaeleza kwamba Al-khaas (Andiko maalumu au specific) ndio inayotangul izwa kuliko Al-aam (Andiko la ujumla), kwa kuwa kwake (hio Khaas) ni ya uhakika kinyume na Aam hakika yake ni (kitu) cha dhana. Kwa hivyo kanuni hapa inatutaka kuitanguliza Hadithi ya Ibn Abbas. Na natija ni kuwa ujumla jamala uliobakia katika Had ithi "Fungeni kwa kuonekana mwezi na fungueni kwa kuonekana mwezi" na ambacho tunachotakiwa sote tukifanye kwa mujibu wa Hadithi hii, ni kuwa sote tufunge kwa kuuona mwezi. Ama je muandamo ni mmoja au kila watu wana muandamo wao, Hadithi hii haitoi jawabu hio.

Jawabu ya pili: ni ile tuliotangulia kuinukuu kutoka kwa Sheikh Ibn Uthaimin aliponukuu jawabu ya wale wenye kusema kwamba kila mji una muandamo wake, ambapo walisema kwamba ujumla uliomo katika Hadithi hio, ni sawa na ujumla uliomo katika Aya inayosema:

﴿ فَالْآنَ بَاشِرُوهُنَّ وَابْتَغُوا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَكُمْ ۚ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ ۖ ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ ۚ ﴾

"Sasa waingiliyeni (wake zenu) na tafuteni kile Allah alichokuandikiyeni, na kuleni na kunyweni mpaka ukubainikieni uzi mweupe kutokana na uzi mweusi wa alfajiri, kisha timizeni saumu hadi usiku."

Je hapa Allah anazungumza na watu wote au na watu maalumu? Je kuzungumza huku na watu wote inamaanisha kwamba alfajiri ya nchi moja ikichomoza watu wa nchi zote wajizuie, au kila watu na alfajiri yao? Jawabu yako hapa ndio jawabu yetu kwa maneno ulioyanukuu kutoka katika kitabu cha Al-sayyid Saabiq kwamba Hadithi hiyo "Fungeni kwa kuuona" ni: "Agizo la ujumla linalojumuisha umma wote (wa Kiislamu) kwa hivyo; yeyote miongoni mwao atakayeuona (mwezi) popote pale; kuonekana huko ku takuwa ni kuonekana kwa wote." Halkadhalika tunajibu ujumla huo kwa Hadithi inayosema:"Usiku ukitokeza kutoka hapa na mchana ukaondoka kutokea hapa na jua likatua, basi aliyefunga ameshafungua (au na-afungue)." Na sisi tunauliza je hapa walikuwa wakiambiwa watu wa Makka tu, au wakiambiwa watu wa nchi zote? Kama walikuwa wakiambiwa watu wa nchi zote, je jua likitua Makka au katika mji wowote ule sote tufuturu? Kwa hakika kila aliyejaaliwa kuwa na mtazamo sahihi, anaona kwamba kujenga hoja kwa ujumla wa Hadithi "Fungeni kwa kuuona" kwamba ni ushahidi wa kuwepo muandamo mmoja, ni kujenga hoja juu ya msingi dhaifu sana. Na kwa maana hio, Ibn Uthaimin (Mwanachuoni wa Kiwahabi) akasema kwamba kauli ya kuwa kila watu wana muandamo wao: "Ina nguvu yake kwa mujibu wa lafdhi (yake) na mtazamo sahihi na Qiyas sahihi vile vile: Qiyas cha wakati wa siku kwa (kuulinganisha) na wakati wa mwezi (month). Mwisho wa kunukuu.

Kwa ufupi ni kuwa, ujumla wa Hadithi inayosema "Fungeni kwa kuuona" ni - kama tulivyotangulia kusema - kwamba watu wote ni lazima wafunge kwa kuuona: si kwa kalenda wala kwa jengine lolote. Huu ndio ujumla unaokusudiwa katika Hadithi hio, au ndio ujumla uliobakia baada ya kuhusishwa au kuvuliwa sehemu ya ujumla huo na Hadithi ya Ibn Abbas na Kuraib.

Jambo la tatu: la kutazamwa katika Hadithi hii, ni kuwa Hadithi hii ni Mutlaq (isiofungamanishwa na kitu) wakati Hadithi ya Ibn Abbas ni muqayyad (iliofungamanishwa). Kanuni ni kuitanguliza muqayyad kuliko mutlaq kama usuli unavyoeleza. Kwa hivyo, kila msingi utaoufata utaona kwamba Hadithi ya Ibn Abbas ndio inayotakiwa itangulizwe.

Ama waliosema kwamba tufunge kwa muandamo mmoja, ukweli ni kuwa wao waliitanguliza rai kuliko kanuni za tafsiri. Walitazama wakaona kuwa mwezi ni mmoja na unakamilisha safari yake mara moja na kwa hivyo muandamo utakuwa mmoja. Lakini tumeona kwamba huu si muandamo wa Kisharia bali ni muandamo wa Kifalaki: muandamo wa Kisharia tunaupata katika kuzijumisha Hadithi tafauti. Pili ni kuwa hio ni rai, na ya Ibn Abbas ni Hadithi; na rai haina uwezo wa kuipinga Hadithi. Kama walivyosema: "Rai haina nafasi mbele ya Andiko."

20

MUANDAMO WA MWEZI

SEHEMU YA KUMI NA TISA

HITIMISHO

19. Hitimisho Kuna milango katika kitabu alichoandika ndugu Juma ambayo hatukupenda kuizungumza, kwani ukichunguza utakuta maneno yake yote yamejengeka katika dhana mbili. Moja ni ile kauli aipendayo kuikariri kwamba (Penye andiko huwa hakuna ijtihadi:) Bila shaka andiko alilokusudia ni ile kauli ya Ibnu 'Abbas (Radhiya Allaahu 'Anhu) alipokataa mwezi wa Sham kwa kusema: (La! Hivi ndivyo alivyotuamuru Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)?.) Kwa upande wetu tumejaribu kuilezea kifani kauli hii na tumeonesha kwa kutumia ushahidi mbali mbali juu ya udhaifu unaopatikana katika kuitegemea kauli hiyo katika mas-ala haya.

JAWABU

Ni fani gani mulioitumia kubainisha Hadithi hio? Pili ni kosa kusema kuwa hio ni kauli ikiwa munakusudia kuwa ni ijtihad tu; hio si kauli kwa maana ya ijtihad bali ni Hadithi. Nakukumbusheni maneno yenu muliposema: "Isipokuwa Sahaba akisema: "Tumeamrishwa kadha" au "Tumekatazwa kadha." Jambo hilo hupewa hukumu ya "Rafii" yaani hio inazingatiwa kuwa ni Hadithi ya Mtume(s.a.w.w) . Kwa bahati mbaya, maneno yenu haya - ambayo ni sahihi kwani ndivyo ilivyo katika elimu ya Hadithi - ni kinyume na matendo yenu. Tazama kwamba hamuiti hio kuwa ni Hadithi bali munasema "Kisa" au "Kauli"; wakati muitakayo nyinyi ndio munaita "Hadithi". Hii inaashiria kwamba hamuutaki ukweli bali munataka kulazimisha rai hata kama ni kinyume na fani za elimu.

MNASEMA

Dhana ya pili ya ndugu Juma imejengeka katika msingi dhaifu wala haina nafasi katika uwanja wa fani (kitaalamu) nao ni kule kusukuma kwake juu ya elimu ya Jiografia. Umeonekana udhaifu wake hasa pale alipokuwa akijaribu kuelezea tofauti iliyopo baina ya nchi na nchi katika suala zima la kutofautiana kwa masaa na kuingia kwa usiku na mchana kwa baadhi ya nchi. Kwa upande wa suala hilo pia tumeshalieleza na kulitolea mifano mbali mbali.

JAWABU

Udhaifu munao nyinyi, kwa kudai kwenu kwamba inawezekana kwa ulimwengu mzima kufunga sawa sawa na kwamba wote wanakutana katika usiku na mchana, ilhali kuna sehemu nyingi ambazo zimepishana kwa masaa mengi: huku usiku kule mchana; jua likitua kule huku ni asubuhi. Sasa vipi watafunga sawa sawa na kukutana kwa usiku na mchana. Nyinyi hamuoni haya munavyosukuma kwa kunukuu kanuni za kiusuli halafu hata kuzifasiri hamujui licha ya kuzitumia?! Kanuni nyengine munazinukuu kutolea hoja nazo ni dhidi yenu, yote hayo nyinyi hamuyajui na munasukuma na wenyewe mumeridhia!

MNASEMA

Mwisho tunachukua fursa hii kumuonya ndugu Juma kuwa amuogope Mwenyezi Mungu hususan katika mas-ala ya kielimu. Akumbuke kuwa Mwenyezi Mungu Ameonya juu ya mtu kusema jambo au kufanya asilolijua. Aelewe kwamba ataulizwa juu ya hilo Lingekuwa jambo la busara kama ndugu Juma angalikubali kuuliza na kufanya utafiti zaidi juu ya mas-ala haya kama agizo la Mwenyezi Mungu linavyotutaka.

Wala usifuate (ukipita ukiyasema au kuyafanya) usiyo na ilimu (ujuzi) nayo. Hakika masikio na macho na moyo, hivyo vyote vitaulizwa. (17: 36)

Jawabu

Hii ni nasaha nzuri kwa ndugu kumpa nduguye. Nami nakupeni nasaha yangu kwa udhati: si kwa kukejeli. Tafadhali chukueni vitabu vya fani hususan usulu-fiqhi, usulul-hadith, balagha, nahau na sarfu. chukueni vitabu hivyo, nendeni kwa mtu kama Sheikh Aliyani akusaideni. Au kwa wale walio Pemba nawende kwa mtu kama Sheikh Kabi. Hawa wataweza kukusaidieni kwani wana uwezo mzuri. Vyenginevyo mutakuwa siku zote munasukuma mukinukuu kitu ambacho kukifasiri hamujui wala hamujui mahala pa kukiweka.

Muogopeni Mwenyezi Mungu hususan katika mas-ala ya kielimu. Kumbukeni kuwa Mwenyezi Mungu Ameonya juu ya mtu kusema jambo au kufanya asilolijua. Aeleweni kwamba mutaulizwa juu ya hilo Lingekuwa jambo la busara kama ndugu zetu mungelikubali kuuliza kwani Allah anasema:

﴿ وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ ۚ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَـٰئِكَ كَانَ عَنْهُ

مَسْئُولًا﴾

Wala usifuate (ukipita ukiyasema au kuyafanya) usiyo na ilimu (ujuzi) nayo. Hakika masikio na macho na moyo, hivyo vyote vitaulizwa. (17: 36)

21

MUANDAMO WA MWEZI

SEHEMU YA ISHIRINI NA MOJA

MUKHTASARI WA MJADALA

Ndugu msomaji bila shaka umejionea kwamba, katika sehemu zake nyingi, huu si mjadala wa kielimu, bali ni mjadala wa hoja za mitaani safi. Ingawa ndugu zetu wamejaribu kunukuu huku na kule, lakini mara nyingi huwa hicho walichokinukuu hawajui hata tafsiri yake licha ya kujua wapi pa-kukiweka. Sasa baada ya hayo, ningependa kukupa maelezo kwa ufupi kuhusu ikhtilafu hizi za miandamo ya mwezi.

Waislamu wametafautiana juu ya suala la mwezi muandamo: je muandamo mmoja wa mwezi unatosha kwa dunia nzima au kila watu wa matalai fulani wawe na muandamo wao. Wengine wakasema kuwa muandamo mmoja wa mwezi unatosha kwa dunia nzima; wengine wakasema kila watu wa matalai fulani wawe na muandamo wao. Wanaosema kwamba tufunge kwa muandamo mmoja wanatoa hoja kwa Hadithi isemayo: "Fungeni kwa kuuona". Hoja yao katika Hadithi hii ni kuwa Hadithi hii ni ya ujmla: haamrishwi kwayo Muislamu pasi na Muislamu; wala watu wa nchi moja pasi na wengine.

Sisi tunaosema kuwa kila watu na muandamo wao, tumekuwa na jawabu tafauti juu ya maana ya Hadithi hio kama ifatavyo: 1) Ujumla uliomo ndani ya Hadithi hio haurejei katika nchi za dunia; bali unarejea katika uoni wa mwezi muandamo. Yaani maana ya Hadithi ni kuwa watu wote wasifunge ila kwa kuuona mwezi. Huu ndio ujumla uliomo katika Hadithi hio. Ama suala je watu wote wafunge kwa muandamo mmoja au vipi? Hadithi hio haitoi ufumbuzi juu ya suala hilo. Bali hilo linapatika katika Hadithi ya Kuraib na Ibn Abbaas.

2) Pili ni kuwa Hadithi hio - katika baadhi ya mazingatio yake - ni 'Aam ya ujumla. Na Hadithi ya Ibn Abbaas na Kuraib Khaas. Kanuni ya kufasiria mandiko inasema kwamba Khaas inatangulizwa kabla ya 'Aam.

3) Hadithi hio - katika baadhi ya mazingatio yake - ni mujmal (isiofafanuliwa). Wakati Hadithi ya Ibn Abbaas na Kuraib ni mubayyan (iliofafanuliwa). Kanuni ya kufasiria maandiko inasema kwamba mubayyan ndio yenye kutangulizwa kabla ya mujmal; yaani andiko mujmal hurejeshwa katika andiko mubayyan. Tumeiita Hadithi "Fungeni kwa kuuona" kuwa ni mujmal kwa kuzingatia kwamba Hadithi hii haikubainisha je muandamo ni mmoja au kila watu wana muandamo wao? Bali imesema kwa ujumla tu "Fungeni kwa kuuona mwezi" kama Qur-an ilivyosema "Simamisha sala kwa kutenguka jua." Na tumeiita Hadithi ya Kuraib na Ibn Abbaas kuwa ni mubayyan kwani - katika qadri hii - imebainisha kwamba muandamo wa mbali hautendewi kazi mbali.

4) Hadithi hio - katika baadhi ya mazingatio yake - ni mutlaq (isiofungamanishwa na sehemu) wakati Hadithi ya Kuraib na Ibn Abbaas muqayyad (iliofungamanishwa na sehemu pasi na nyengine). Kanuni ni kulirejesha andiko mutlaq katika andiko muqayyad, yaani muqayyad ndio inayotangulizwa. Na kwa hivyo, Hadithi hio ni lazima ifungamanishwe na Hadithi ya Ibn Abbaas ili kufikia maana sahihi. Tumeiita Hadithi hio kuwa ni mutlaq kwa kuwa lafdhi yake haikufungamanishwa na sehemu yoyote, na tukaiita Hadithi ya Ibn Abbaas kuwa ni muqayyad kwani lafdhi yake imefungamanishwa na sehemu moja pasi na nyengine. Kwa hivyo, kwa mujibu wa kanuni zote za tafsiri, natija ni kuwa Hadithi ya Ibn Abbaas na Kuraib ni lazima itangulizwe. Jambo jengine ni kuwa ujumla uliomo katika Hadithi hio, ni sawa na ujumla uliomo katika Aya inayosema

﴿أَقِمِ الصَّلَاةَ لِدُلُوكِ الشَّمْسِ

Simamisha sala kwa kutenguka jua .

Hapa pia haamrishwi mtu maalumu, lakini pamoja na hayo nyakati za sala za watu duniani haziungani. Kwa hivyo, ujumla uliopo hapa ni kuwa watu wote kila watu ni lazima wasali adhuhuri kwa kutenguka jua.

Pia ujumla huo, ni kama Hadithi isemayo:"Usiku ukitokeza kutoka hapa na mchana ukaondoka kutokea hapa na jua likatua, basi aliyefunga ameshafungua (au na-afungue)." Na bila shaka ujumla huu maana yake ni kuwa kila watu wafuturu kwa kuzama jua: wala haina maana ya kuungana nyakati za kufuturu. Halkadhalika, ujumla uliomo katika Hadithi: "Fungeni kwa kuuona", utaona - hususan baada ya kuzikusanya dalili zote mbili: Hadithi hio na ya Kuraib - kwamba ujumla uliomo ndani yake ni kuwa watu wote kila watu ni lazima wafunge kwa kuuona: si ujumla wa kuwa watu wote wafunge sawa sawa. Vyenginevyo, itabidi tulitendee kazi andiko moja; na tuliwache jengine na hili ni kinyume na minhaj (methodology) ya tafsiri.

Wanaosema kuwa kila watu na muandamo wao, wanatoa hoja kwa:

1) Hadithi ya Ibn ya Ibn Abbaas na Kuraib isemayo :"Kutoka kwa Kurayb (kasema) kwamba Ummu Al-fadhli bint Al-harith alimtuma Sham (Syria) kwa Muawiya. Akasema: 'Basi nikaenda Sham nikamkidhia haja yake.' Na ukaniindamia (mwezi wa) Ramadhani na mimi niko Sham. Basi nikauona mwezi usiku wa (kuamkia) ijumaa. Kisha nikaja Madina mwishoni mwa mwezi. Basi Abdullahi bin Abbas (r.a.) akaniuliza. Kisha akataja (habari za) mwezi muandamo akasema: 'Lini mumeuona mwezi muandamo?' Nikasema: 'Tumeuona usiku wa (kuamkia) Ijumaa.' Akasema: 'Wewe umeuona?' Nikasema: 'Ndio. Na Watu wameuona na wakafunga na Muawiya akafunga.' Akasema: 'Lakini hakika ya sisi tumeuona usiku wa (kuamkia) Juma Mosi, basi hatuachi kuendelea kufunga mpaka tutimize (siku) thalathini au tuuone.' Nikasema: 'Kwani wewe hutosheki na kuonekana na Muawiya na kufunga kwake?' Akasema: 'Laa' (Sio): Hivi ndivyo alivyotuamrisha Mtume(s.a.w.w) ."

Hoja yao humu ni kuwa Ibn Abbaas alipopewa habari za muandamo wa mwezi uliotokea Sham usiku wa Ijumaa, alikataa kuufata na akasema "Hivi (ninavyofanya mimi) ndivyo alivyotuamuru Mtume s.a.w.". Ikafahamika kwa mujibu wa nakala hii kwamba mafunzo ya Mtume(s.a.w.w) ni kutokuuzingatia muandamo wa mbali. Ama wanaosema kuwa tufunge kwa muandamo mmoja wakajibu kwa hoja tafauti, muhimu zao ni hoja sita za Al-Imamu Al-Shawkani ambazo nimezijadili katika kitabu. Na muhimu katika hizo ni kuwa hii ilikuwa ni ijtihad ya Ibn Abbaas. Hoja hii ikajibiwa kwamba Ibn Abbaas katika riwaya hii kasema: "Hivi ndivyo alivyotuamuru Mtume(s.a.w.w) ". Na lafdhi kama hii inaifanya hadithi ihukumiwe kuwa ni marfu'u yaani hukumu yake ni kuwa hio ni Hadithi ya Mtume (s.a.w.). Hivi ndivo elimu ya Hadithi inavyosema.

2) Hoja ya pili ya wale wenye kusema kuwa kila watu na muandamo wao, ni Qiyas cha nyakati za funga na nyakati za Sala na kufuturu kama tulivyoeleza juu. Ubainifu wa hili ni kuwa: a) Wajibu wa Sala umefungamanishwa na kutenguka na kuzama kwa jua - kitu cha kimaumbile (Natural phenomenon). Kwa hivyo mtenguko wa jua ni sababu ya kuwajibika sala.

b) Wajibu wa funga umefungamanishwa na muandamo wa mwezi - kitu cha kimaumbile (Natural phenomenon). Kwa hivyo kuandama kwa mwezi ni sababu ya kuingia kwa wajibu wa funga.

c) Jua - ambalo kutenguka kwake ndio sababu ya kuwajibikiwa na sala - likitenguka katika nchi moja, watu wa nchi nyengine hawawajibikiwi na sala. Kwa hivyo, Qiyas sahihi ni kuwa kuonekana kwa mwezi - ambayo ni sababu ya kuwajibika funga - katika nchi moja isiwe sababu ya kuwajibikiwa na funga kwa watu wa nchi nyengine. Hiki ni Qiyas sahihi kama alivyosema Sheikh Ibn

'Uthaimin. Huu ndio mukhtasar wa suala hili la kuonekana mwezi na anayetaka kwa urefu na arudi katika kitabu Ufafanuzi Wa Mgogoro Wa Kuandama Kwa Mwezi cha Sheikh Nassor Bachoo na kitabu Ushahidi Uliowekwa Wazi cha Juma Mazrui. Ahsanteni

Ndugu yenu katika dini

Juma Muhammad Rashid Al-Mazrui

Tel: 92213669 Al-Qurm, Muscat Oman

E-Mail: jumamazrui@hotmail.com

Jumamazrui@yahoo.com

Tarehe 6/8/2009

MWISHO