HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU0%

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU Mwandishi:
: AZIZI NJOZI
Kundi: Wanawake

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

Mwandishi: Allamah Shahid Murtaza Mutahhari
: AZIZI NJOZI
Kundi:

Matembeleo: 45427
Pakua: 3166

Maelezo zaidi:

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 33 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 45427 / Pakua: 3166
Kiwango Kiwango Kiwango
HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

Mwandishi:
Swahili

19

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

NDOA YA MITALA (MKE ZAIDI YA MMOJA)

Ndoa ya mke mmoja ndio muundo wa asili zaidi wa ndoa. Hali ya kumiliki kitu peke yako, au uhusiano ambao wewe tu ndio unashikilia nafasi hiyo na umiliki binafsi umejikita katika aina hii ya ndoa, japo umiliki huu ni tofauti na umiliki wa mali au utajiri. Katika mfumo huu mume na mke, kila mmoja huhisi hisia za moyoni na faida za ngono za mwenzake kuwa ni zake peke yake. Kinyume na ndoa ya mke mmoja ni ndoa ya mke zaidi ya mmoja (mitala) kwa wakati mmoja na Ukomonisti wa ngono. Jimai ya ngono, kimaana pia inaweza kuitwa mitala.

Ukomonisti wa ngono. Ujimai wa ngono maana yake hakuna kuwa peke yako. Kwa mujibu wa nadharia hii, hakuna mwanaume ambaye anapasa kuwa mali ya mwanamke mmoja tu wala mwanamke kuwa mali ya mume mmoja tu. Maana yake ni kupinga (kuikana) kuwepo maisha ya familia. Historia na nadharia zinazohusiana na zama za kale kabla ya kuanza kuandikwa kwa historia haionyeshi kipindi chochote ambapo mwanadamu hakuwa na familia na ambapo Ukomonisti wa ngono ulikuwa umestawi.

Kinachodaiwa kuwepo katika baadhi ya makabila ya kishenzi (yasiyo na ustaarabu na utamaduni) ilikuwa ni hali ya kati na kati, kati ya maisha ya familia (yaani kila mtu na mke wake au mume wake) na Ukomonisti wa ngono. Inasemekana kwamba katika baadhi ya makabila ilikuwa ni jambo la kawaida kwamba wavulana kadhaa kwa pamoja waliwaoa wasichana kadhaa, au wanaume kadhaa wa ukoo mmoja waliwaoa kwa ushirikiano wanawake kadhaa wa ukoo mwingine.

Will Durant katika kitabu chake, 'History of Culture' Jalada la 1, anaandika kwamba katika baadhi ya maeneo ndoa za ushirikiano zilikuwa mashuhuri kwa maana kuwa wanaume kadhaa wa ukoo mmoja walishirikiana kuwaoa wanawake kadhaa wa ukoo mwingine, kwa mfano imekuwa ni mila huko Tibet kwamba ndugu kadhaa wa kiume wana idadi sawa ya madada (ambao ni ndugu) kama wake zao. Kila kijana huingiliana na yeyote katika wale akina dada anayempenda.

Hapa kuna aina fulani ya Ukomonisti wa ngono. Mila kama hii ilipata kuwepo huko Uingereza enzi za kale. Mila ambayo ilikuwa maarufu miongoni mwa Wayahudi na makabila mengine ya zamani na ambapo kwa mujibu wa mila hiyo, baada ya kufa ndugu mmoja wa kiume, ndugu yake mwingine wa marehemu alimuoa mjane wake, ilikuwa ni masazo ya mila ya kale.

Maoni ya Plato Inaelekea kwamba wakati akiitangaza nadharia yake ya 'wanafalsafa watawala' Plato amependekeza katika kitabu cha 'The Republic,' aina fulani ya ujamaa wa kifamilia kwa tabaka hili. Viongozi kadhaa wa kikomunisti wa karne ya 19 pia walitoa pendekezo kama hilo, lakini kama ilivyoripotiwa na mwandishi wa kitabu, 'Freud and the Prohibition of consanguineuous marriage,' baada ya machungu mengi, dola nyingi za kikomunisti zenye nguvu, zilitangaza rasmi kuitambua sheria ya mke mmoja mume mmoja mwaka 1938. Kuwa na mume zaidi ya mmoja (polyandry).

Muundo mwingine wa mitala ni hali ya mke kuwa na mume zaidi ya mmoja (polyandry) kwa wakati mmoja. Kwa mujibu wa Will Durant mila hii inapatikana miongoni mwa makabila fulani ya Tibet na kwingineko. Al-Bukhari katika mkusanyiko wake maarufu wa hadithi, as-Sahihi, anamripoti Aisha kuwa alisema kuwa miongoni mwa Waarabu wa kabla ya Uislamu kulikuwa aina nne za mahusiano ya ngono.

Mojawapo ni ndoa sahihi ambayo bado ipo hadi sasa. Katika muundo huu mwanaume hutoa pendekezo kwa msichana kupitia kwa baba yake na baada ya kupanga mahari, humbeba mke wake. Hapawezi kuwa na utata juu ya watoto waliozaliwa katika ndoa hii. Kulikuwa na aina nyingine ya ndoa, ambayo ilikuwa ikiitwa Istibza. Ili kuzaa (kupata) kizazi kizuri, mume alimchagua mwanaume na kumuomba mke wake aingiliwe na huyo mwanaume kwa muda fulani.

Yeye mwenywe alijitenga na mke wake hadi mwanamke alipopata mimba. Ilikuwa ni ndoa ndani ya ndoa iliyofanywa ili kuboresha kizazi. Kwa mujibu wa mila nyingine, kundi la wanaume kumi au pungufu ya hapo, walishirikiana kufanya mapenzi na mwanamke mmoja. Baada ya kuwa mjamzito, mke aliwaita wote, na kwa mujibu wa mila ya enzi hizo, wote walipaswa kwenda. Hapo alimteua mwanaume mmoja kuwa baba wa mtoto wake na kuwaacha wale wengine ambao nao pia walikuwa tayari kukubali jukumu hilo. Mwanaume huyo baada ya kuchaguliwa, hakuwa na hiari ya kukubali au kukataa kuwa baba wa mtoto.

Aina ya nne ya mahusiano ya unyumba ni umalaya. Malaya walikuwa na bendera juu ya nyumba zao. Hii ilitumika kama alama ya kuwatambulisha. Mwanaume yeyote alikuwa anaweza kuwaingilia wanawake hawa. Mwanamke yule alipozaa, aliwaita wanaume wote waliomwingilia, na kwa msaada wa mtaalamu wa kutambua tabia kwa kuangalia uso, alimteua baba wa mtoto. Mwanaume mhusika alipaswa kukubali uamuzi wa mtaalamu huyu na kummiliki mtoto. Hizi ni aina za mahusiano ya kinyumba zilizokuwepo Arabuni kabla ya Uislamu. Mtume alizipiga marufuku zote na kubakiza moja iliyopo sasa.

Hii inaonyesha kuwa mila ya mke kuwa na mume zaidi ya mmoja ilikuwepo miongoni mwa Waarabu wa kabla ya Uislamu pia. Montesquieu anaripoti kuwa Mwarabu mtembeaji wa dunia nzima, Abu Zahir al-Hassan, aliikuta mila hii China na India alipozitembelea nchi hizi katika karne ya 19 na aliichukulia kama aina ya ufisadi. Pia anaandika: "Katika Pwani ya Malabar kuna kabila liitwalo Nair.

Waume wa kabila hili hawawezi kuwa na mke zaidi ya mmoja lakini wanawake wanaruhusiwa kuchagua waume wengi. Labda sababu ni kuwa Wanair ni jamii ya wapiganaji na wawindaji. Kama tunavyowazuia kuoa askari wetu wa Ulaya ili ndoa isiingiliane na kazi zao za kupigana, makabila ya Malabar pia yameamua kuwa, wanaume wa Nair wajitahidi kadri wawezavyo kuepukana na majukumu ya familia.

Kutokuwa na hali na tabia ya kitropiki ya eneo hili, haiwezekani kuzuia ndoa kabisa, imeamuliwa kuwa wanaume wengi wawe na mke mmoja ili wasielemewe na majukumu ya kifamilia na hivyo kuathiri ufanisi wao." Kasoro za mke mmoja kuwa na waume zaidi ya mmoja. Kasoro kubwa na ya msingi ya mfumo huu wa mke kuwa na mume zaidi ya mmoja ni kuwa ukoo wa baba wa mtoto hubakia haujulikani kwa uhakika (yaani baba halisi wa mtoto huwa hajulikani). Katika mfumo huu uhusiano kati ya baba na mtoto haueleweki na hii ndio sababu mfumo huu hau jafanikiwa kama ilivyo Ukomonisti wa ngono haujaweza kujikita sehemu yeyote, mfumo huu pia haujakubalika katika jamii yoyote ya maana.

Kama tulivyosema awali, maisha ya familia, ujenzi wa nyumba (makazi) ya kizazi kijacho na muunganiko maalumu kati ya vizazi vya zamani na vijavyo ni moja ya mahitaji ya silika za binadamu. Kuwepo kwa mifano michache ya mke kuwa na waume wengi katika baadhi ya jamii hakuthibitishi kuwa uundaji wa familia sio silika ya mwanadamu. Halikadhalika utawa na useja kabisa (kuepuka kufanya tendo la ndoa), kama inavyofanywa na wanaume na wanawake kadhaa, pia ni aina ya upotofu. Mfumo huu si tu kwamba hauafikiani na asili ya mwanaume ya kuhodhi na upendo wake wa mfumo dume, bali pia unapingana na maumbile ya mwanamke pia. Uchunguzi wa kisaikolojia umebaini kuwa mwanamke anapenda zaidi kuwa na mume mmoja kuliko mwanaume anavyopenda kuwa na mke zaidi ya mmoja.

MITALA (MKE ZAIDI YA MMOJA)

Muundo mwingine wa mitala ni mtu kuwa na mke zaidi ya mmoja. Mfumo huu umezoeleka na kuwa na mafanikio zaidi kuliko ule wa mke kuwa na waume wengi na ujima wa ngono. Sio tu kwamba umekuwepo miongoni mwa makabila ya kishenzi, bali pia umetumiwa na watu wengi wastaarabu. Mbali na Waarabu, umetumiwa pia na Wayahudi, Wairani wa zama za Sasania na jamii nyinginezo.

Montesquieu anasema kuwa huko Malaya ilikuwa inaruhusiwa kuwa na wake watatu. Pia anasema kuwa mfalme wa Urumi, Valentinian II aliwaruhusu watu wake kuoa wake wengi, lakini kwa sababu sheria hii ilikuwa haiafikiani na hali ya hewa (tabia) ya Ulaya, ilifutwa na wafalme wengine kama Theodore n.k. Uislamu na mitala. Tofauti na ilivyokuwa kwa mfumo wa mke kuwa na mume zaidi ya mmoja, Uislamu haukukataza moja kwa moja ndoa ya mke zaidi ya mmoja (mitala). Badala yake uliweka idadi maalumu, pia umeweka masharti mengine pia na haukumruhusu kila mtu kujiingiza katika kuoa wake wengi.

Tutaeleza baadaye masharti yaliyowekwa na Uislamu na tutaeleza kwa nini Uislamu haukupiga marufuku ndoa za mitala moja kwa moja. Inashangaza kwamba katika zama za kati, ambapo propaganda za kuupinga Uislamu zilikuwa katika kilele chake, wapinzani wa Uislamu walikuwa wakisema kuwa ni Mtume wa Uislamu ambaye kwa mara ya kwanza alianzisha ndoa ya mitala. Walidai kuwa mila hii ilikuwa msingi wa Uislamu na kwamba kuenea kwa Uislamu kwa haraka haraka sehemu mbalimbali duniani kulitokana na mila hii. Wakati huo huo walidai kuwa mitala hii ilikuwa ndio sababu ya kuporomoka kwa watu wa Mashariki.

Will Durant katika kitabu chake "History of Culture" juz. 1, anasema kuwa mapadri na makasisi wa zama za kati waliamini kuwa ndoa za mitala zilianzishwa na Mtume wa Uislamu, ambapo sio kweli. Kama tunavyojua maisha ya ndoa katika jamii nyingi za kijima yalifuata utaratibu huu wa mitala. Kuna sababu nyingi za kuzuka kwa mfumo huu.

Katika jamii za kijima, sehemu kubwa ya wanaume walikuwa zaidi wakijishughulisha na uwindaji na upiganaji, hivyo kiwango chao cha vifo kilikuwa juu miongoni mwao. Kwa vile idadi ya wanawake ilizidi ya wanaume, hivyo ilikuwa ni lazima kutumia mfumo huu. Haikuwa inawezekana kuwaacha baadhi ya wanawake bila kuolewa, hasa ikizingatiwa kuwa, kwa vile idadi ya vifo katika jamii za kijima ilikuwa juu, kila mwanamke alitarajiwa kuzaa watoto.

Hapana shaka kwamba mfumo huu ulizifaa jamii hizo, sio tu kwa sababu ya uwingi wa wanawake kuliko wanaume, bali pia mfumo huu uliongeza idadi yao na kuwafanya kuwa na nguvu. Katika zama hizi wanaume wengi wenye nguvu na afya huchelewa kuoa na huzaa watoto kidogo tu. Lakini zamani wanaume wenye nguvu walikuwa na nafasi ya kuoa wake bora kabisa na walikuwa wakizaa idadi kubwa ya watoto. Hii ndio sababu desturi hii iliendelea kwa muda mrefu sana si tu miongoni mwa jamii za kijima bali hata katika jami zilizoendelea. Ni hivi karibuni tu kuwa pole pole desturi hii imeanza kutoweka katika nchi za Mashariki. Kilimo kimeimarisha maisha ya wanaume na kimepunguza ugumu wa taabu za kale, ambapo matokeo yake ni kuwa na idadi ya wanaume na wanawake imeanza kulingana.

Hivi sasa mitala imekuwa ni fahari ya kundi dogo la matajiri, hata katika jamii za kijima, na walio wengi wanalazimika kuridhika na mke mmoja, na kwa burudani ya ziada, wanaweza kujiingiza katika zinaa, kila inapowezekana. Gustav Leabeon katika kitabu chake, 'History of Culture' anasema kuwa hakuna mila isiyopendwa Ulaya kama ndoa za mitala, wala Ulaya haijaihukumu kimakosa mila nyingine yoyote kama ilivyofanya kwa ndoa hii.

Waandishi wa kizungu wameamini kuwa ndoa za mitala ni msingi wa Uislamu na ndio sababu kubwa ya kuenea kwake. Pia wanashikilia kuwa mila hii ndio sababu ya kuanguka kwa watu wa mashariki. Pingamizi nyingine mbali na hizi, zinazoonyesha huruma kwa wanawake wa Mashariki, zinadai kuwa wanawake hawa walionenepeana wanafungiwa ndani ya kuta nne za nyumba zao chini ya matowashi (wanaume waliohasiwa) wenye mioyo migumu.

Pia wanadai kuwa kosa dogo ambalo wanaweza kumuudhi mkuu wa familia linaweza kuwafanya waadhibiwe adhabu ya kifo. Fikra kama hizi hazina msingi wowote. Wazungu wasio na upendeleo wanapaswa kujua kuwa ni mila ya ndoa ya mitala ambayo imeyapa nguvu mahusiano ya kifamilia na kuinua maadili ya watu hawa. Ni kutokana na mila hii kwamba mwanamke wa Mashariki anaheshimika zaidi kuliko wa ulaya. Kabla ya kuthibitisha nukta hii, lazima tuweke wazi kuwa mila hii haihusiani na Uislamu.

Hata kabla ya Uislamu, mila hii ilikuwa inafuatwa na watu wa Mashariki wakiwamo Wayahudi, Wairani, Waarabu n.k. Watu waliosilimu huko Mashariki hawakunufaika na lolote katika mila hii. Juu ya hayo, hakuna dini yoyote yenye nguvu kama hii iliyobuni au kuzuia mila hii ya mitala. Mila hii haikuanzishwa na dini yoyote. Ilitokana na hali ya hewa na sababu nyingine zilizohusiana na mfumo wa maisha ya Mashariki. Hata Magharibi, ambako hali ya hewa haiendani na kuweko kwa desturi kama hiyo, lakini ndoa ya mke mmoja inapatikana katika vitabu vya sheria tu.

Katika maisha halisi hakuna dalili ya ndoa ya mke mmoja. Haifahamiki ni kwa namna gani mitala ya halali ya Mashariki ni ya hadhi ya chini kuliko ndoa za mitala ya siri za watu wa Magharibi. Watu wa mashariki, wanapotembelea nchi za Ulaya na kukumbana na shutuma kali za Wazungu dhidi ya mila zao hushangazwa na kuona wameonewa. Ni ukweli kwamba Uislamu haukuanzisha ndoa za mitala. Ulichokifanya ni kuidhibiti tu. Umepanga idadi ya mwisho. Umeweka masharti magumu juu yake.

Mila tayari ilikuwepo katika jamii nyingi ambazo zilikuja baadaye kusilimu. Walilazimika tu kufuata masharti yale yaliyowekwa na Uislamu. Katika kitabu chake 'Iran During the Sassanian Period,' Christenson ameandika: "Ndoa za mitala zilichukuliwa kuwa ni msingi wa familia. Kimsingi, idadi ya wake ambao mtu angependa kuwa nao ilitegemea na uwezo wake.

Watu maskini hawakuwa wanamudu kuwa na mke zaidi ya mmoja. Mkuu wa familia alikuwa na haki maalum. Mmoja wa wake alichukuliwa kuwa ni mke kipenzi na alipata haki zote. Wake wengine waliwatendea kama wafanyakazi tu. Haki za kisheria kati ya makundi haya mawili zilitofautiana sana. Watumwa wa kike (masuria) walijumuishwa katika kundi la wake wafanyakazi. Haifahamiki ni wake vipenzi wangapi mume angeweza kuwa nao. Lakini limetajwa suala la wake wawili vipenzi katika maandishi ya kisheria.

Kila mmoja wao aliitwa malkia wa nyumba (mama mwenye nyumba). Waliishi katika nyumba tofauti. Mume alipaswa kumhudumia mke wake kipenzi katika maisha yake yote. Kila mtoto wa kiume hadi anapobalehe na kila mtoto wa kike hadi alipoolewa walikuwa na haki sawa. Lakini ni watoto wa kiume tu (wa wake wafanyakazi) walioingizwa katika ukoo wa baba." Katika kitabu, "Social History of Iran from tha fall of the Sassanians to the fall of Umayads", marehemu Sa'id Nafisi anaandika kuwa, "Idadi ya wanawake ambao mwanaume angeoa haikuwa na mpaka na wakati fulani inavyoonekana katika kumbukumbu za Kigiriki mwanaume alikuwa anaweza kuwa na mamia ya wanawake katika nyumba yake."

Montesquieu, akimnukuu mwanahistoria wa Kirumi, anasema kuwa wanafalsafa wengi wa Kirumi ambao walikuwa wanateswa na Wakristo kwa sababu walikataa kuwa wakristo walikimbia Roma na kwenda kwa Mfalme wa Iran, Khusro Parviz. Walishangazwa kuona kwamba huko si tu kwamba ndoa za mitala zilikuwa zinaruhusiwa bali pia wanaume wa Kifarsi walikuwa wakiingiliana na wake za watu wengine pia. Lazima ieleweke hapa kwamba wanafalsafa wa Kirumi walikimbilia kwenye kasri la Mfalme wa Iran, Anushirwan na sio kwenye kasiri la Khusro Parviz. Montesquieu amechanganya majina kutokana na kutoelewa vizuri. Kabla ya Uislamu, Waarabu walikuwa na uwezo wa kuwa na idadi isiyo na mipaka ya wake.

Ni Uislamu ulioweka mipaka. Hii bila shaka iliwasababishia usumbufu wale waliokuwa na wake zaidi ya wanne. Kuna baadhi walikuwa na wake kumi. Walilazimika kuwaacha sita. Kutokana na haya ni wazi kuwa si Uislamu ulioanzisha ndoa za mitala. Uislamu uliziwekea udhibiti tu. Hata hivyo haukuzipiga marufuku kabisa, katika sura zinazofuatia tutataja sababu zilizosababisha mila hii, na tutaelezea sababu ambazo zimewafanya wanaume na wanawake wa zama hizi walazimike kuipiga vita mila hii. Sababu za kihistoria za mitala.

Ni sababu zipi za kihistoria na kijamii zilizosababisha mitala? Kwa nini mataifa mengi ya ulimwengu, hasa mataifa ya mashariki yamekubali mila hii na kwa nini mataifa ya Magharibi, kamwe hayakupata kuitumia mila hii? Imekuwaje kwamba katika miundo mitatu ya mitala ni huu muundo mmoja tu wa mume kuwa na wake wengi ndio uliopata umaarufu? Mke kuwa na waume wengi na Ukomonisti wa ngono ama hazikupata kutumiwa kabisa, au zimetumika kidogo sana na katika maeneo machache sana. Mpaka tuyajadili maswali haya ndio tutaweza kulijadili suala la ndoa za mitala katika Uislamu na kwa mujibu wa mahitaji ya sasa ya mwanadamu.

Tusipoyatumia na kuyazingatia matokeo ya uchunguzi wa kijamii na kisaikolojia yaliyopatikana juu ya mada hii, sisi pia, kama walivyokuwa waandishi wengine wa juu juu, tunaweza kuangukia na kuanza kuimba nyimbo za zamani za kudai kuwa sababu za mitala ziko wazi. Yaani, mila hii imetokana na ukatili wa mwanaume na utawala wake kwa mwanamke. Ni matokeo ya mfumo dume.

Kwa kuwa mwanaume amemtawala mwanamke, ametunga sheria na mila ambazo zitamnufaisha yeye. Hivi ndivyo alivyoipa nguvu mila hii yenye manufaa kwake na madhara kwa mwanamke, na amekuwa akiitumia kwa karne nyingi. Mwanamke alikandamizwa, hakuweza kuutekeleza mfumo wa yeye kuwa na waume wengi. Na sasa muda wa uonevu wa mwanaume umekwisha, mila ya ndoa za mitala lazima iondoke kama ilivyokuwa kwa fursa nyingine za uongo ili kuleta haki sawa kwa wanaume na wanawake. Kufikiri kwa namna hii ni kwa kitoto na kwa juu juu sana.

Sababu ya mitala sio ukandamizaji wa mwanaume kwa mwanamke wala kushindwa kwa mfumo wa mke kuwa na waume wengi sio ukandamizaji wa mwanamke. Kama kivitendo mfumo huu umekufa, hii sio kwa sababu muda wa uonevu wa mwanaume umefikia kikomo. Mwanaume hajapoteza fursa yoyote, kimsingi amepata fursa juu ya mwanamke. Hatukatai kuwa ukandamizaji ni moja ya mambo yaliyobadilisha historia. Pia hatukatai kuwa katika kipindi chote cha historia mwanaume ameyatumia vibaya madaraka yake dhidi ya mwanamke. Lakini tunaamini kuwa ni mawazo finyu kuyaelezea mawazo ya kifamilia kwa kigezo cha dhulma peke yake.

Tukikubali mtazamo huu, lazima pia tukubali kuwa katika kipindi ambacho ndoa za mke kuwa na wanaume wengi zilikuwa maarufu miongoni mwa Waarabu wa kabla ya Uislamu, au kama alivyoripoti Montesquieu, miongoni mwa Wanair katika pwani ya Malabar mwanamke alipata fursa ya kumtawala mwanaume na akawa anakaa na wanaume wengi. Lazima ikubaliwe pia kuwa kipindi hicho kilikuwa ni cha dhahabu kwa mwanamke.

Awali tulimnukuu Montesquieu akisema kuwa mila ya mke kuwa na waume wengi miongoni mwa Wanair haikutokana na utawala wa mwanamke au heshima aliyokuwa akipewa, bali ilikuwa ni uamuzi wa jamii wa kuwaepusha askari dhidi ya mzigo wa majukumu ya familia.

Aidha, kama Mfumo dume ndio ulisababisha mitala, kwa nini mfumo huu haukupata umaarufu Ulaya (Magharibi)? Hata hivyo, mfumo dume haukuwepo Mashariki peke yake. Je, watu wa Magharibi tokea awali wamekuwa Wakristo wachamungu wanaoamini juu ya usawa kati ya mwanaume na mwanamke? Je, kigezo cha kumiliki kimemnufaisha mwanaume wa mashariki na kukuza uadilifu huko Magharibi?

Mpaka kufikia nusu karne iliyopita mwanamke wa Magharibi alikuwa miongoni mwa wenye bahati mbaya kabisa duniani. Hata mali yake ilidhibitiwa na mume wake. Wazungu wenyewe wanakiri kuwa katika zama za kati, nafasi ya mwanamke wa mashariki ilikuwa bora sana ikilinganishwa na mwanamke wa Magharibi.

Gustav Leabeon anasema kuwa Uislamu, katika kipindi cha mwanzo kabisa, ulimpa mwanamke nafasi (hadhi) ambayo mwanamke wa kizungu alipata baada ya muda mrefu sana, yaani baada ya uungwana na ustaarabu wa Waarabu wa Andolusia kuingia Ulaya. Tabia njema kwa mwanamke ni sehemu kubwa ya uungwana ambao Wazungu walijifunza kutoka kwa Waislamu. Ilikuwa ni Uislamu (na sio dini ya Kikristo kama inavyoaminiwa na watu wengi wa kawaida), ulioinyanyua hadhi ya mwanamke. Katika zama za kati machifu wa makabila, licha ya kuwa Wakristo kamwe hawakumpa mwanamke heshima anayostahili.

Uchambuzi wa historia ya kale unaonyesha kuwa tabia ya 235 wafalme na viongozi wengine wa Ulaya ilikuwa ni ya kishenzi sana. Waandishi wengine wa Kizungu, pia wametoa maelezo kama haya kuhusiana na nafasi ya mwanamke katika zama za kati. Japo mfumo dume ulikuwa umeenea sana Ulaya katika kipindi hiki, bado ndoa za mitala hazikuweza kuwa ni desturi. Ukweli ni kuwa ni mfumo wa mke kuwa na waume wengi (popote ulikotumika) hautokani na utawala au nguvu ya mwanamke juu ya mwanaume wala kushindwa kwa mfumo huu hakukutokana na udhaifu wa mwanamke wala ukandamizaji wa mwanaume dhidi yake. Halikadhalika mitala katika nchi za Mashariki haikusababishwa na udikteta na uonevu wa mwanaume wala si kwamba haujaenea huko magharibi kwa sababu ya kuwepo usawa kati ya mwanaume na mwanamke.

20

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

SABABU ZA KUSHINDWA KWA MFUMO WA MKE KUWA NA WAUME WENGI

Sababu kubwa ya kushindwa kwa mfumo huu ni kuwa ulikuwa haufai kwa maumbile ya mwanaume wala ya mwanamke. Haufai kwa maumbile ya mwanaume, kwa sababu, kwanza hauafikiani na asili yake ya kupenda umiliki pekee (yaani awe wake peke yake) na pili kwa sababu haukubaliani na kanuni ya kwamba baba aweze kujiamini juu ya ubaba wake. Ni maumbile ya mwanadamu kuwa na mafungamano maalumu na wanawe. Kila mwanadamu kwa asili anatamani kuzaa watoto na anataka uhusiano na kizazi chake kilichopita na kijacho uwe unaeleweka na wa uhakika. Anataka kujua yeye ni mtoto wa nani na ni baba wa nani. Mfumo wa mke kuwa na waume wengi haukubaliani na silika hii ya mwanadamu. Kwa upande mwingine mfumo wa mume kuwa na wake wengi (mitala) hausababishi matatizo haya, si kwa mwanaume, wala mwanamke.

Imeelezwa kuwa wakati fulani wanawake wapatao arobaini walimwendea Imam Ali(a.s.) na kumuuliza kwa nini Uislamu umewaruhusu wanaume kuoa wake wengi lakini haujaruhusu wanawake kuwa na waume wengi. Wakamuuliza kama huu sio ubaguzi wa wazi. Imam Ali(a.s.) aliagiza viletwe vikombe vya maji na akampa kila mwanamke kikombe kimoja cha maji. Kisha akawaamuru wamwagie maji yote yale katika chombo kimoja kikubwa kilichokuwa katikati yao. Baada ya kutekeleza agizo hilo, Imam Ali(a.s.) aliwaamuru kila mmoja wao achukue maji yale tu yaliyokuwa kwenye kikombe chake. Wanawake wote walisema kuwa hilo lilikuwa haliwezekani kutokana na ukweli kwamba maji yote yalikuwa yamechanganyika.

Imam Ali(a.s.) alisema kuwa:kama mwanamke mmoja angeolewa na wanaume wengi, ni wazi kuwa angeingiliana nao. Akipata mimba na kuzaa, haitafahamika mtoto yule ni wa baba yupi. Kwa upande wa mwanamke, mfumo huu pia hauafikiani na maumbile yake. Mwanamke hamhitaji mume kwa ajili ya kukidhi silika yake ya ngono tu. Ingekuwa hivyo tungesema kuwa 'Wanaume wengi zaidi, raha zaidi'.

Mwanamke anataka mwanamume ambaye yeye mwanamke ataudhibiti moyo wake, atakayekuwa mlinzi na mwangalizi wake, atakayejitoa mhanga kwa ajili ya mkewe na atakayefanya kazi kwa bidii na kumletea fedha. Fedha anazojitafutia mwanamke huwa hazitoshi kukidhi mahitaji yake wala huwa hazina thamani sawa na zile alizopewa na mwanaume anayempenda. Mume hukidhi mahitaji ya kifedha ya mke wake kwa moyo wa kujitolea. Mke na watoto ni hamasa kubwa na bora kabisa kumhamasisha mwanaume kufanya kazi.

Katika mfumo wa mke kuwa na waume wengi mwanamke hawezi akadai na kupata mapenzi ya kweli na kujitolea kutoka kwa yeyote kati ya wanaume hawa. Hii ndiyo sababu, kama ilivyo tu kwa umalaya, huu umekuwa ni mfumo unaochukiza kwa mwanamke. Hivyo mfumo huu wa mke kuwa na waume wengi haukidhi wala kukubaliana na asili na mahitaji ya mwanaume wala mwanamke.

KUSHINDWA KWA UKOMONISTI WA NGONO

Katika mfumo huu si mwanaume wala mwanamke anayeweza kudai au kujinasibisha na mke au mume maalumu kuwa ni wake na hii ndiyo sababu mfumo huu kamwe haukupata kuwa maarufu sehemu yoyote ile. Ilipendekezwa na Plato ambaye aliliruhusu jambo hili kwa tabaka la watawala au 'wanafalsafa watawala.' Lakini pendekezo lake halikuwa kama la wengine na yeye mwenyewe baadaye ilibidi abadilishe maoni yake. Katika karne iliyopita, Frederick Engels, baba wa pili wa ukomunisti alitoa wazo hili na akalitetea kwa nguvu. Lakini halikukubaliwa hata katika ulimwengu wa kikomunisti.

Inasemekana kuwa Urusi ilijaribu kutekeleza nadharia ya familia ya Engels, lakini kufuatia machungu waliyayopata yaliyotokana na mfumo huu walilazimika kuutambua mfumo wa mume mmoja mke mmoja kuwa ndio sera rasmi. Mitala inaweza kuonekana kuwa ni jambo la fahari kwa mwanaume lakini kamwe suala la mke kuwa na waume wengi halijawahi na halitapata kuwa ni jambo la fahari kwa mwanamke. Sababu ni kuwa mwanaume anataka mwili wa mwanamke na mwanamke anataka moyo wa mwanaume. Mwanaume anachojali ni kuumiliki mwili wa mwanamke, haijalishi hata kama haumiliki moyo wake.

Hii ndio sababu mwanaume huwa hajali hata kama mmoja wa wake zake atapunguza upendo kwake, lakini kwa mwanamke, kitu muhimu kabisa ni moyo wa mwanaume na hisia zake za moyoni. Akivipoteza hivyo, huwa amepoteza kila kitu. Kwa maneno mengine, kuna vitu viwili katika maisha ya unyumba, mwili na hisia za moyoni. Mwili unahusiana na ngono, ambayo hamu yake huwa kileleni katika kipindi cha ujana na baadaye hupungua polepole. Hisia za moyoni huhusiana na hisia za upendo, upole na kujitoa. Hisia hizi hukua na kukomaa kwa kadri muda unavyokwenda.

Kwa vile maumbile ya mwanamke ni tofauti na ya mwanaume, mwanamke hujali zaidi hisia za moyoni katika maisha yake ya ndoa. Lakini kwa mwanaume, ama mwili ndio muhimu zaidi au vyote viwili, mwili na hisia za moyoni vina umuhimu sawa. Huko nyuma, tulimnukuu mwanasaikolojia wa kike ambaye ana maoni kuwa mwanamke ana tabia za kipekee za akili. Mtoto hukua katika tumbo lake na kunyonyeshwa na kulelewa katika mapaja yake. Anahitaji sana kujitolea na upendo wa dhati wa mumewe kama baba wa mtoto. Hata kiasi cha upendo kwa wanawe kinategemeana na kiasi cha upendo anachokipata kutoka kwa baba yao.

Ni ndoa ya mume mmoja tu ndiyo inaweza kukidhi mahitaji haya. Ni kosa kubwa sana kulinganisha ndoa ya mke mmoja kuwa na waume wengi na ndoa ya mume mmoja kuwa na wake wengi na kudai kuwa hakuna tofauti yoyote kati ya aina hizi mbili za ndoa. Pia ni makosa kusema kuwa ndoa za mitala zilikuwa mashuhuri katika baadhi ya sehemu za dunia kwa sababu mwanaume ana nguvu zaidi, na kwamba ndoa za mke kuwa na waume wengi zilishindwa kutokana na mke kuwa ni jinsia dhaifu.

Mwandishi wa zama hizi, ambaye ni mwanamke anasema: "Tunaweza kusema kuwa kwa vile mwanaume anaweza kuwa na wake wanne, basi mke pia anapaswa kuwa na haki hiyo kwani wote ni binadamu. Hitimisho hili la kimantiki ni la kuudhi, zaidi kwa wanaume. Wanakasirishwa kusikia hoja hii na wanapiga kelele: 'Inawezekanaje mwanamke akawa na waume zaidi ya mmoja?' Kujibu hilo sisi kwa sauti ndogo tunasema: Inawezakanaje mwanaume akawa na mke zaidi ya mmoja?" Pia anasema: "Hatukusudii kupalilia ufisadi au kupuuzia umuhimu wa maisha ya usafi wa kimaadili. Tunataka tu wanaume waelewe kuwa maoni yao juu ya wanawake hayakujengwa juu ya hoja za maana.

Mwanaume na mwanamke ni sawa kama wanaadamu. Kama mwanaume ana haki ya kuwa na wake wanne, basi mwanamke pia lazima awe na haki kama hiyo. Hata kama tukichukulia kwamba mwanamke kiakili sio bora kuliko mwanaume, lakini ni hakika kwamba kiroho mwanamke sio dhaifu kuliko mwanaume." Kama ambavyo utakuwa umebaini kauli hiyo haioneshi tofauti yeyote kati ya mitala na ndoa za mke kuwa na waume wengi, isipokuwa kwamba kwa kuwa mwanaume ni wa jinsia yenye nguvu zaidi basi amechukuwa mfumo wa mitala kwa manufaa yake, na mwanamke kwa kuwa ni wa jinsia dhaifu hakuweza kuutumia utaratibu huo.

Mwandishi huyo pia anasema kuwa mwanaume anamuona mwanamke kuwa ni mali yake, na ndio maana anataka kuwa na wake wengi. Kwa maneno mengine ni kuwa mwanaume anataka kujikusanyia mali nyingi kwa kadri inavyowezekana. Kwa vile mwanamke yupo katika nafasi ya mtumwa, hawezi kuwa anamilikiwa na bwana zaidi ya mmoja.

Kinyume na maoni ya mwandishi huyu, ukweli kwamba mfumo wa mke kuwa na waume wengi haujawahi kukubaliwa na idadi yoyote kubwa ya watu popote pale duniani unathibitisha kuwa mwanaume hamchukulii mke wake kuwa ni mali yake, kwani katika mali, ni mashuhuri duniani kote kuwa mali humilikiwa kwa ubia na wamiliki wote hunufaika na mali hiyo kwa ubia. Kama mwanaume angekuwa anamchukulia mwanamke kuwa ni mali, ni wazi kuwa asingekuwa na pingamiza katika kuichangia na wengine.

Hakuna sheria duniani inayolazimisha kuwa mali imilikiwe na mtu mmoja tu. Inasemwa kwamba mume ni mtu mmoja na mke ni mtu mmoja. Wanapaswa kuwa na haki sawa. Kwa nini mume awe na haki ya kufurahia mitala na mke anyimwe haki hiyo ya kuwa na waume wengi? Tunasema kuwa hapa ndio kuna makosa. Unadhania kwamba mitala ni sehemu ya haki za mume, na mke kuwa na waume wengi ni sehemu ya haki za mke. Ukweli ni kwamba mitala ni sehemu ya haki za mwanamke, na ndoa ya mke kuwa na waume wengi sio sehemu ya haki za mwanaume wala mwanamke. Ni mfumo usio na faida kwa wote wawili, mwanamke na mwanaume.

Tutathibitisha baadaye kuwa mfumo wa mitala umewekwa na Uislamu kwa nia ya kulinda maslahi ya mwanamke. Kama nia ingekuwa kumpendelea mwanaume, Uislamu ungemruhusu mwanaume kufanya mapenzi na mwanamke mwingine mbali na mke wake na usingeweka uwajibikaji juu yake kuhusiana na mke wake wa halali na watoto wake wa halali. Mfumo wa mke kuwa na waume wengi kamwe haujapata kuwa na maslahi yoyote kwa mwanamke. Sio haki aliyonyimwa.

Mwandishi ambaye tumenukuu maoni yake anasema: "Tunataka wanaume waelewe kuwa maoni yao juu ya wanawake hayajajengwa juu ya hoja ya maana." Kwa bahati sisi pia hicho ndicho tunachokusudia kukifanya. Katika sura zinazofuata tutaeleza msingi wa mtazamo wa Uislamu juu ya mitala. Tunawaalika watu wote wanaofikiri kuutazama na kuona kama mtazamo wa Uislamu umejengwa au haukujengwa juu ya hoja zozote za maana. Tunaahidi kuwa tutayabatilisha yale yote, tuliyoyasema ikiwa mtu yeyote atathibitisha kuwa msingi wa mtazamo wa Uislamu ni mbovu.

21

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

SABABU ZA KIHISTORIA ZA MITALA (11)

Tamaa ya mwanaume katika ngono na utawala wake wa kibabe peke yake sio sababu tosha za kuibuka kwa mitala. Lazima ziwepo sababu nyingine zilizochangia katika mwanaume muasherati kukidhi hamu yake ya kuwa 241 na wanawake wa aina mbalimbali. Ni rahisi zaidi kujiingiza katika ngono holela kuliko kuwa na mwanamke wa chaguo lake kama mke wake wa halali na kujitwisha jukuma la kutunza watoto wake wa baadaye. Mitala huwa mashuhuri katika jamii zile tu ambazo zinajali maadili na zinazuia ngono holela na mwenye kiu ya uasherati hulazimika kulipa gharama ya kutaka aina mbalimbali za wanawake kwa kumkubali mwanamke anayehusika kuwa mke wake wa halali na kubeba jukumu la kuwa baba wa watoto wa mwanamke huyo. Sasa hebu tuangalie kama kuna sababu zozote za kijografia, kiuchumi au kijamii zilizochangia kuibuka na kuwepo kwa ndoa za mitala.

SABABU ZA KIJIOGRAFIA

Montesquieu na Gustav Leobeon wanasisitiza kuwa hali ya hewa na tabia za nchi ndio sababu kuu za maendeleo ya mitala. Wasomi hawa wanaamini kuwa tabia ya nchi na hali ya hewa ya nchi za Mashariki zinaifanya mila hii isiepukike huko. Katika nchi za Mashariki, wanawake hupevuka na kuzeeka haraka zaidi, hivyo mwanaume huoa mke wa pili na wa tatu. Pia wanafikiri kuwa mwanamke mmoja hawezi kukidhi kiu ya ngono ya mwanaume aliyekulia katika tabia ya nchi za Mashariki.

Gustav Leobeon katika kitabu chake "History of Islamic and Arab Culture" (Historia ya utamaduni wa Kiislamu na kiarabu) anasema: "Mila ya ndoa za mitala haikuanzishwa na dini. Ni matokeo ya tabia za nchi, tabia ya watu wa huko na sababu nyingine zinazohusiana na maisha ya Mashariki. Haihitajiki kusisitiza sana kuwa hizi ni sababu zenye nguvu sana. Pia tabia zao za kimwili na kimhemko, unyoyeshaji wao wa watoto na magonjwa yao mara nyingi huwalazimisha wanawake wa Mashariki kujitenga na waume zao. Kwa kuzingatia tabia za nchi za Mashariki (Hali ya Hewa) pamoja na tabia za kitaifa za wanaume wa Mashariki, huwa haiwezekani kwa wanaume kustahamili kutengana na wake zao japo kwa muda mfupi, hivyo ndoa za mitala zimekuwa ni mila.

"Montesquieu katika kitabu chake, "The Spirit of Law" anasema: "Katika nchi za kitropiki wanawake hupevuka wakiwa na umri wa miaka nane, tisa au kumi na baada ya kuolewa punde huwa wajawazito. Tunaweza tukasema kuwa katika nchi za kitropiki, mimba hushika mara moja tu baada ya ndoa." Predo, alipokuwa anayaelezea maisha ya Mtume wa Uislamu, anasema kuwa alimuoa Khadija akiwa na umri wa miaka mitano na alianza kumwingilia akiwa na umri wa miaka nane. Kwa sababu ya ndoa za mapema, wanawake katika nchi za kitropiki huzeeka wakiwa na umri wa miaka ishirini. Anasema kuwa huanza kuzeeka hata kabla ya kupevuka. Katika nchi zenye tabia ya vuguvugu, wanawake hubaki na ujana na uzuri wao kwa muda mrefu zaidi.

Huchelewa kupevuka na huwa wamekomaa zaidi na wanakuwa na uzoefu zaidi wakati wanapoolewa. Hupata watoto katika umri mkubwa zaidi, na mume na mke huzeeka takribani kwa wakati mmoja. Hivyo ndivyo usawa kati ya mwanamke na mwanaume unavyopatikana na wanaume huwa hawahitaji kuwa na mke zaidi ya mmoja. Hivyo ni kwa sababu ya tabia ya nchi ndio maana sheria imekataza mitala huko Ulaya lakini ikairuhusu huko Asia. Maelezo haya sio sahihi. Mila ya mitala haiko katika nchi za kitropiki tu huko Asia.

Katika kipindi cha kabla ya Uislamu mila hii ilikuwa mashuhuri sana nchini Iran, ambapo tabia ya nchi ni ya vuguvugu. Ni uzushi kabisa kusema kuwa katika nchi za Mashariki wanawake huzeeka wakiwa na umri wa miaka ishirini, kama ilivyodaiwa na Montesquieu. Inashangaza pia kusikia kuwa Mtume wa Uislamu, alimuoa Khadija akiwa na umri wa miaka mitano na kwamba alianza kumwingilia akiwa na umri wa miaka nane. Kila mtu anaelewa kuwa Mtume alimuoa Khadija, wakati yeye Mtume, alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano na Bibi Khadija alikuwa na umri wa miaka ishirini na nane, ingawa baadhi ya vyanzo vya kihisto ria vyenye makosa vinasema kuwa Khadija wakati huo alikuwa na umri wa miaka arobaini.

Pili, ikikubaliwa kuwa kuwahi kwa umri wa uzee kwa wanawake na nguvu nyingi za urijali kwa wanaume ndizo sababu ya mila hii, kwa nini watu wa Mashariki hawakujiingiza katika ngono holela na ufuska kama wenzao wa Magharibi ambao walifanya ngono holela na ufuska katika zama za kati na za sasa. Kama alivyoonyesha Gustav Leabeon, suala la mume kuwa na mke mmoja limebakia katika vitabu vya sheria lakini halionekani katika maisha halisi ya kila siku. Tena, katika nchi za Mashariki, mitala ipo katika muundo wake wa Kisheria. Mwanamume humkubali mwanamke mhusika kama mke wake wa kisheria na halali na anapaswa kubeba jukumu la kuwa baba wa watoto wa mwanamke huyo. Mitala iliyopo Ulaya ni ile haramu na isiyokuwa ya kisheria pamoja na ndoa za siri. Mwanaume wa Magharibi hujiingiza katika ngono holela na hukwepa majukumu yanayohusiana na ndoa.

MITALA HUKO MAGHARIBI

Tunaona kuwa ni muhimu kutoa maelezo mafupi ya mitala huko Ulaya katika zama za kati kama yalivyoelezewa na mwana historia mashuhuri wa kimagharibi. Maelezo haya yanapasa kuwafunua shuka jeusi wale wanaozikosoa nchi za mashariki kwa mitala kwamba licha ya dosari zinazodaiwa, mitala zilikuwa ni ndoa zenye heshima zaidi kuliko kile kilichokuwepo Ulaya. Will Durant katika kitabu chake, History of Civilization, Juz.17, anatoa maelezo ya kuvutia juu ya hali ya maadili nchini Italia katika kipindi cha uamsho. Hapa chini tunatoa muhtasari wa yale aliyosema chini ya kichwa "Morals in sexual Relations".

Katika utangulizi wake mfupi anasema kuwa kabla ya kuelezea maadili ya Italia, tunaweza kusema kuwa kwa asili mwanamume ni mwenye asili ya kuoa wake wengi. Ni vikwazo vikali vya kimaadili, kazi nyingi ngumu na umaskini na uwajibikaji wa hali ya juu wa mke, kwa pamoja ndio vinaweza kumlazimisha kubaki na mke mmoja. Kisha anasema kuwa uzinifu haukuwa jambo geni katika zama za kati kabla ya zama za uamsho. Kama ilivyokuwa kwamba katika zama za kati dhambi ya zinaa ilishutumiwa na watu walihimizwa kuishi maisha ya usafi, halikadhalika katika kipindi cha uamsho (Renaissance), vijana, wasomi walifundishwa kuwa na tabia njema na kutunza ubikra kwa wanawake.

Wasichana waliokuwa wanatoka katika familia zinazoheshimika walikuwa kwa kiasi fulani wakitengwa na wanaume wasiokuwa na familia yao na walifundishwa faida za kutunza ubikra wao hadi watakapoolewa. Wakati fulani mafundisho haya yalikuwa yanawaingia kichwani na kusaidia. Inaripotiwa kuwa ilikuwa kwamba ikitokea msichana akinajisiwa alikuwa akijizamisha majini na kufa.

Haya lazima yatakuwa ni matukio haba sana, kwa sababu askofu alikuwa akichukua taabu ya kujenga mnara baada ya kifo chake ili kukumbuka usafi wake wa kimaadili. Idadi ya waliokuwa wakifanya mapenzi kabla ya ndoa lazima itakuwa ilikuwa kubwa, kwa sababu kulikuwa na idadi kubwa ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa katika kila mji wa Italia. Lilikuwa ni jambo la fahari kwamba mtu alikuwa hana mtoto wa nje ya ndoa, lakini kuwa naye mmoja halikuwa ni jambo la aibu.

Kwa kawaida mume alimshawishi mke wake wakati wa ndoa kuja kwa mumewe pamoja na mtoto wake (wa huyo mwanamke) aliyemzaa nje ya ndoa. Ili alelewa pamoja na watoto wa ndani ya ndoa. Kuzaliwa nje ya ndoa halikuwa ni doa katika utukufu wa yeyote. Isitoshe cheti cha uthibitisho kuwa mtoto husika ni wa ndani ya ndoa kilikuwa kinaweza kupatikana kirahisi kwa kumpa rushwa kiongozi wa kanisa. Iwapo watoto wa ndani ya ndoa wenye haki ya kurithi walikuwa hawapo, basi watoto wa nje ya ndoa walikuwa wakirithi mali na hata kiti cha ufalme kama ilivyokuwa kwa Frante - I ambaye, alimrithi Alfonso - I, Mfalme wa Naples. Pius - II alipokuja Bavaria mwaka 1459, alipokelewa na wana wa mfalme saba, ambapo wote walikuwa ni watoto wa nje ya ndoa.

Uhasama na uadui kati ya watoto wa nje ya ndoa na wale wa ndani ya ndoa ndio ilikuwa sababu muhimu ya migogoro katika zama za uamsho. Liwati nayo ilikuwa ni kufufuliwa tu kwa desturi ya kale ya kigiriki. San Bernardino aliikuta aina hii ya upotofu na uchafu ikiwa imeenea sana huko Naples akahisi kuwa hali hiyo inahatarisha kutokea kwa adhabu waliyopewa watu wa Sodoma. Artino aliikuta hali hii chafu huko Roma pia. Umalaya pia ulikuwa katika kiwango cha juu. Mwaka 1490, kati ya wtu wote 90,000 wa Roma, wanawake 6,800 walikuwa wamesajiliwa kama malaya. Idadi hii haihusishi mahawara na malaya ambao hawajasajiliwa. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 1509, kati ya watu laki tatu wa mji huo, kulikuwa malaya 11,654.

Katika karne ya 15, msichana ambaye alikuwa amefikisha umri wa miaka 15 hali ya kuwa hana mume alionekana kama doa katika jina zuri la familia. Katika karne ya 16 "umri wa mkosi" ulisogezwa mbele hadi miaka 17, ili kumuwezesha msichana kupata elimu ya juu. Wanaume, ambao walikuwa wanafurahia huduma za malaya waliokuwa wameenea kila sehemu, walikuwa wanavutiwa kuoa ikiwa tu mwanamke mhusika aliahidi kumpatia mahari ya kuvutia.

Kwa mujibu wa mfumo wa zama za kati, mke na mume walitarajiwa kupendana na kushirikiana katika huzuni na furaha. Inavyoonekana matarajio haya kwa kiasi fulani yalifikiwa, lakini bado uzinifu ulikuwa umejikita mizizi. Ndoa nyingi za watu wa tabaka la juu zilikuwa ni za kidiplomasia zilizofungwa kwa maslahi ya kisiasa na kiuchumi. Waume wengi waliona kuwa ni haki yao kuwa na bibi pembeni. Mke alikuwa anakasirika sana lakini alikuwa analazimika kuizoea hali hiyo. Miongoni mwa watu wa tabaka la kati uzinifu ulionekana kuwa ni mila halali. Machiavelli, na rafiki zake inaonekana hawakujisikia vibaya juu ya hadithi za kutokuwa kwao waaminifu ambapo walikuwa wakibadilishana wake. Ilikuwa mke naye akifuata nyendo za mumewe za kutokuwa mwaminifu, kwa kawaida alikuwa anaipuuzia tabia yake wala hakuona wivu wala kukereka.

Hii ndio hali ya maisha ya watu ambao wanaona kuwa mitala ni uhalifu usiosameheka wa watu wa Mashariki na wakati mwingine wamekuwa wakiilaumu hali ya hewa (tabia ya nchi) kwa kusababisha mila hii isiyokuwa ya kibinadamu. Lakini hali ya hewa ya huko kwao haiwaruhusu kutokuwa waaminifu kwa wake zao na kuvuka mipaka ya mke mmoja! Pia inafaa ieleweke kuwa kutokuwepo kwa mitala ya halali miongoni mwa wazungu, iwe mizuri au mibaya, hakutokani na dini ya Kristo, ambaye kamwe hakuikataza. Kinyume chake, dini ya Kristo inazithibitisha kanuni za Agano la kale ambalo waziwazi linazitambua ndoa za mitala. Hivyo tunaweza kusema kuwa dini ya Kristo inaruhusu mitala na Wakristo wa kale walikuwa wakioa na kuolewa mitala. Hivyo kujiepusha kwa wazungu kisheria na mitala lazima kutakuwa kumetokana na sababu nyinginezo, sio dini.

22

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

HEDHI

Baadhi wanasema kuwa ndoa za mitala zimetokana na hedhi za mwanamke na mchoko anaoupata baada ya kuzaa na kutopenda kwake kufanya ngono wakati wa kunyonyesha. Will Durant anasema kuwa katika jamii za kijima wanawake huzeeka haraka. Hiyo ndiyo sababu kwamba ili wawanyonyeshe watoto wao kwa muda mrefu na ili warefushe tofauti ya umri kati ya mtoto mmoja na mwingine bila kuziziba kiu za wanaume zao za kupata watoto, na ili kuwawezesha waume zao kukidhi hamu yao ya ngono huwahimiza waume zao kuoa mke mpya. Mara nyingi imeonekana kuwa mke wa kwanza, kwa nia ya kupunguza uzito wa majukumu yake, humshawishi mume wake kuoa mke wa pili ili apate watoto zaidi na mali zaidi.

Hapana shaka kwamba hedhi ya mwanamke na uchovu wake baada ya kuzaa, kijimai, huwaweka mwanaume na mwanamke katika nafasi tofauti. Sababu hizi humfanya mwanaume amgeukie mwanamke mwingine, lakini hizi peke yake haziwezi kuwa sababu ya mitala isipokuwa tu kama kuna vikwazo vya kijamii na kimaadili vinavyozuia ngono holela, sababu hizo zinaweza kuwa na nguvu tu ikiwa mwanaume hayuko huru kufanya ngono holela.

KIKOMO CHA KIPINDI CHA KUZAA KWA WANAWAKE

Baadhi wanaamini kuwa kikomo cha kipindi cha kuzaa kwa wanawake ni moja ya sababu zilizoibua ndoa za mitala kwani inaweza kutokea kwamba mwanamke anafikia umri huu kabla hajazaa watoto wa kutosha. Inawezekana pia kwamba watoto wameshakufa. Katika hali hizo, kama mume hataki kumtaliki mke wake wa kwanza na wakati huo huo anataka watoto zaidi, basi anakuwa hana namna isipokuwa kuongeza mke wa pili, au wakati fulani hata mke wa tatu. Halikadhalika utasa wa mke wa kwanza unaweza kuwa ni sababu ya mume kuoa mke wa pili.

SABABU ZA KIUCHUMI

Sababu za kiuchumi zimetajwa pia kuwa ni sababu ya mitala. Inasemekana kuwa katika zama za kale wake wengi na idadi kubwa ya watoto vilikuwa vinachukuliwa kuwa ni rasilimali ya kiuchumi. Alikuwa akiwatumikisha wake na watoto wake na wakati mwingine alikuwa akiwatendea kama watumwa. Wakati mwingine aliamua hata kuwauza. Wengi wa watumwa hawakutekwa vitani bali waliuzwa na baba zao.

Hii inaweza kuwa sababu ya mitala. Kwa sababu mwanaume anaweza kupata watoto tu kwa kumkubali mwanamke kuwa ni mke wake wa halali. Ngono holela haiwezi kufanikisha jambo hili. Hata hivyo hii sio sababu ya ndoa zote za mitala. Baadhi ya jamii za kijima zilikuwa zikioa wake wengi zikiwa na wazo hili kichwani. Lakini si watu wote walioa wake wengi kwa lengo hili. Katika zama za kale, mitala ilikuwa ni mila iliyozoeleka katika matabaka mbalimbali. Wafalme, wana wa wafalme, machifu, mitume na wafanya biashara walikuwa na wake wengi. Kama tunavyojua, matabaka haya, kamwe hayakuwanyonya kiuchumi wake zao wala watoto wao.

IDADI YA WANAFAMILIA

Kupenda idadi kubwa ya watoto na kupanuka kwa familia, kumekuwa ni moja ya sababu za mitala. Mitazamo ya mwanamke na mwanaume juu ya idadi ya watoto wanayoihitaji inaweza kutofautiana. Idadi ya watoto ambayo mwanamke anaweza kuzaa ni ndogo sana, awe na mume mmoja au waume wengi. Lakini idadi ya watoto ambayo mwanaume anaweza kuzaa inategemeana na idadi ya wanawake alionao. Kinadharia inawezekana mwanaume akawa na maelfu ya watoto kwa kupitia mamia ya wanawake alionao. Tofauti na ulimwengu wa sasa, katika ulimwengu wa kale idadi ya wanafamilia iilikuwa inahesabika kuwa ni sifa muhimu ya kijamii. Makabila na koo zilifanya kila linalowezekana kuongeza idadi yao, ilikuwa ni fahari ya ukoo kuwa na kabila kubwa. Ni wazi kuwa ndoa za mitala ndio ilikuwa ni njia pekee ya kufikia lengo hili.

UWINGI WA WANAWAKE

Sababu ya mwisho na muhimu zaidi ambayo ilichangia kuibuka kwa ndoa za mitala ni kuwa mara zote wanawake huwa ni wengi kuliko wanaume. Sio kwamba idadi ya wanawake wanaozaliwa ni kubwa kuliko ya wanaume. Ikitokea katika sehemu fulani wanawake zaidi wamezaliwa katika sehemu nyingine wanaume zaidi watazaliwa. Lakini bado idadi ya wanawake wanaofaa kuolewa ni kubwa kuliko idadi ya wanaume wanaofaa kuoa. Sababu ni kuwa idadi ya vifo vya wanaume mara zote imekuwa kubwa kuliko wanawake. Inawezekana kwamba ikiwa ndoa ya mke mmoja mume mmoja itazingatiwa kikamilifu, idadi kubwa ya wanawake itabaki bila waume wa halali, watoto wa ndani ya ndoa na maisha ya familia.

Hakuna shaka kwamba kwa uchache hii ndio ilikuwa hali ya mambo katika jamii za kijima. Tayari tumeshanukuu maoni ya Will Durant anayesema kuwa katika jamii za kijima, uhai wa mwanaume mara zote ulikuwa hatarini kwa sababu mara zote alikuwa akishughulika katika kuwinda na kupigana na hii ndio sababu kwamba idadi ya vifo vya wanaume ilikuwa kubwa kuliko wanawake. Kwa kadri idadi ya wanawake ilivyozidi kuongezeka, kulikuwa na mambo mawili tu ya kuchagua ama kuruhusu mitala au kuilazimisha idadi kubwa ya wanawake kuishi maisha yao yote bila kuolewa.

HITIMISHO

Hapo juu tumejadili sababu zote ambazo zinaweza kudhaniwa kuwa ndio chanzo cha mitala. Kama ambavyo tumeona, baadhi ya sababu hizi kama vile tabia ya nchi (hali ya hewa) ilivyo sio sababu halisi. Hivyo tunazipuuza. Sababu nyingine zinaweza kuwa zile zenye nguvu ya kumshawishi mwanaume kuoa wake wengi lakini hazitoi uhalali juu ya kitendo chake. Zina sura ya ukandamizaji, ubabe na ukatili. Sababu za kiuchumi zinaingia katika kundi hili.

Ni dhahiri kuwa uuzaji wa watoto ni moja ya vitendo vya kikatili na kishenzi kabisa. Kuamua kuoa wake wengi kwa ajili ya lengo hili ni haramu kama kitendo chenyewe kilivyo haramu. Kundi la pili linajumuisha sababu ambazo zinaweza kuonekana kuwa ni sababu thabiti kwa upande wa mume au jamii. Ugumba wa mke wa kwanza, kufikia kikomo cha uzazi wakati bado mume anahitaji watoto au kama kabila au taifa linahitaji idadi kubwa ya watu. Kama kanuni ya jumla, sababu zote ambazo zinatokana na kutofautiana kati ya mume na mke kuwiana na mahitaji ya jimai na nguvu ya uzazi, zina uthabiti. Kundi la tatu linajumuisha sababu ambazo kama ikikubaliwa kuwa zilikuwepo au bado zipo, sio tu kwamba huruhusu mitala bali pia huzifanya kuwa ni wajibu.

Katika hali hii, mitala ni haki ya mwanamke ambayo mwanaume na jamii wanapaswa kuitoa. Sababu hii ni uwingi wa wanawake kuwazidi wanaume, ikiwa idadi ya wanawake wanaopaswa kuolewa ni kubwa kuliko idadi ya wanaume wanaofaa kuoa, mitala huwa ni wajibu wa wanaume na haki ya mwanamke, kwani ikiwa itaamuriwa kuwa mume mmoja akae na mke mmoja tu, idadi fulani ya wanawake itakuwa imenyimwa haki ya kuishi maisha ya kifamilia. Haki ya ndoa ni haki ya msingi ya binadamu na hakuna anayepaswa kunyimwa haki hii kwa kisingizio chochote.

Jamii haiwezi ikachukua hatua yoyote ambayo inaweza ikawanyima baadhi ya watu haki hii. Haki ya ndoa ni haki ya asili kama ilivyo kwa haki ya uhuru, haki ya kufanya kazi na haki ya kupata chakula, malazi na elimu. Hivyo, sheria ya kuwa na mke mmoja inapingana na haki za binadamu pindi inapokuwa wanawake wanaopaswa kuolewa ni wengi kuliko wanaume wanaofaa kuoa. Kwa uchache, hii ndiyo imekuwa ni hali ya mambo huko nyuma. Katika sura zifuatayo tutaangalia ikiwa bado kuna mazingira ambayo sio tu kwamba yanahalalisha mitala bali pia yanaijenga haki hii kwa ajili ya mwanamke. Na kama mazingira haya bado yapo, sasa ni nini nafasi ya haki hii dhidi ya haki ya mke wa kwanza.