HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU23%

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU Mwandishi:
: AZIZI NJOZI
Kundi: Wanawake

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU
  • Anza
  • Iliyopita
  • 33 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 47726 / Pakua: 5540
Kiwango Kiwango Kiwango
HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

Mwandishi:
Swahili

6

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

DHANA ZA ASILI ZA HAKI YA FAMILIA

Tumesema kwamba mwanadamu hufaidi aina fulani ya heshima ya asili. Asili ya maumbile yake imempa haki kadhaa za msingi zisizoondosheka. Huu ndio msingi wa Azimio la haki za Binadamu kwa wote. Uislamu na falsafa za Mashariki (Asia) zinaunga mkono dhamira hii. Kisichofaa katika Azimio hili na kinachokwenda kinyume ni jinsi mifumo mbali mbali ya falsafa za Kimagharibi inavyoitafsiri asili na maumbile ya mwanadamu. Ni dhahiri kuwa chanzo pekee chenye mamlaka na kisicho na makosa juu ya elimu ya haki za binadamu ni kitabu adhimu na kitukufu cha maumbile. Ni kwa kuzirejea tu kurasa za kitabu hiki ndio tunaweza kuziona haki ambazo zinawahusu watu wote, na kupata hakikisho la nafasi linganishi za haki za mwanaume na mwanamke.

Inastaajabisha kwamba baadhi ya watu wenye mawazo finyu hawakijui chanzo hiki kitukufu. Kwa mujibu wao, chanzo pekee cha kuaminika ni chombo cha wale watu wachache wanaoitawala dunia waliopata nafasi ya kuliandika Azimio hili. Ingawa wao wenyewe wanaweza, kivitendo wasiyazingatie hayo waliyoyaandika lakini wengine hawana haki ya kupinga. Lakini sisi, kwa kutumia hizi hizi haki za binadamu, tunaamini kuwa tuna haki ya kutofautiana. Kwa maoni yetu, chanzo pekee ambacho hakiwezi kupingwa ni maumbile yenyewe ambayo yanaweza kuchukuliwa kuwa ni kitabu cha Mwenyezi Mungu.

Tunawaomba radhi wasomaji wetu, kwa sababu inatupasa tuibue baadhi ya masuala ambayo kwa kiasi fulani ni ya kifalsafa na hivyo yanaonekana makavu. Yanaweza pia kuwa yanakinaisha kwa baadhi ya wasomaji. Tungeweza kuwa tuliyaepuka masuala haya, lakini somo la haki za mwanamke linahusiana sana na masuala hayo hivyo haiwezekani kuyaachilia mbali moja kwa moja. Uhusiano kati ya haki za asili/msingi na malengo ya maumbile.

Kwa mtazamo wetu, haki za asili na za msingi zimeibuka kutokana na mpango wa Mungu, ambapo kwa mujibu wa mpango huu, utaratibu wa kibunifu, kwa kuzingatia malengo yake, huvisukuma mbele vitu vyote kuelekea katika hali ya ukamilikifu, uwezo ambao tayari umefichwa ndani ya maumbile yao. Kila uwezo wa kiasili ni msingi wa moja ya haki za asili na, wakati huo huo, ni mamlaka ya asili ya kuitekeleza haki hiyo. Kwa mfano kila mtoto wa mwanadamu ana haki ya kujifunza na kwenda shule, lakini mtoto wa kondoo hana haki hizo. Kwa nini iko hivyo? Ni kwa sababu mtoto wa binadamu ana uwezo wa kujifunza na kupata busara zaidi wakati mtoto wa kondoo hana uwezo huu. Utaratibu wa kibunifu umeweka mamlaka kwa ajili ya haki hii ndani ya umbile la mwanadamu, lakini mamlaka haya hayakuwekwa ndani ya kondoo. Mambo yako hivi hivi katika haki za kufikiri, kupiga kura na utashi.

Baadhi ya watu wanafikiri kuwa nadharia ya haki za asili na wazo kwamba maumbile yamempatia mwanadamu haki maalum ni madai ya kibinafsi na ya kipuuzi. Kwa kusema kweli hakuna tofauti kati ya haki za wanaadamu na viumbe wasiokuwa wanaadamu. Lakini huu sio uhalisia, vipawa vya kiakili ni tofauti. Maumbile yameiweka kila spishi (kiumbe) iliyopo ulimwenguni katika obiti yake maalum, na inaweza kuwa na mafanikio tu kama itasonga ndani ya mipaka yake. Muumba amefanya hivyo kwa malengo, na mpangilio huu sio wa bahati nasibu.

Msingi wa haki za kifamilia, ambalo ndilo jambo linalojadiliwa hapa, lazima litazamwe kiasili (kimaumbile) kama ilivyo kwa haki nyingine za asili. Kama tukitazama vipaji vya asili vya mwanaume na mwanamke, tunaweza kuona kwa urahisi, iwapo wanaweza kuwa na haki na wajibu unaofanana au la. Lazima ikumbukwe kuwa, kama tulivyoonyesha huko nyuma kuwa nukta inayohisabiwa ni kufanana kwa haki zao sio usawa wa haki zao. Haki za kijamii. Nafasi ya mwanadamu, kuhusiana na haki za kijamii zisizo za kifamilia, siku zote hazinafanani. Katika hali fulani huwa na haki zinazofanana lakini katika hali fulani nyingine haki zao huwa hazifanani lakini huwa na haki sawa. Katika jamii haki zote za msingi huwa sawa kwa watu wote. Kila mtu, kwa mfano, ana haki ya kutumia vipaji vyake kufanya kazi na kushiriki katika mashindano ya maisha, huwa mgombea katika nafasi fulani ya kijamii na kuipata katika njia za halali, kuonyesha uwezo wake kiakili na kivitendo.

Lakini usawa huu huu wa wote juu ya haki za msingi huwaweka katika nafasi zisizo sawa. Kwa mfano, kila mtu ana haki ya kufanya kazi na kushiriki katika ushindani wa maisha, lakini inapokuja katika utendaji wenyewe kivitendo, haiwezekani wote wakafanya kazi vizuri kwa ubora unaolingana. Wengine wanaweza sana na wengine kidogo. Halikadhalika wengine wana ufanisi mkubwa zaidi kuliko wengine. Tena wengine wana elimu zaidi wanamudu zaidi majukumu, wana ufanisi mkubwa zaidi na wanafaa zaidi kuliko wengine. Ni dhahiri kuwa haki zao walizojipatia haziwezi kufanana. Kujaribu kuzifanya haki zao walizojipatia kwa jitihada na vipaji vyao, zifanane haitakuwa kitu kingine isipokuwa dhulma iliyo wazi.

Sababu ambayo ni kwa nini wanaadamu wana haki sawa na zinazofanana ni kuwa uchunguzi wa masuala ya binadamu unathibitisha kuwa hakuna aliyeumbwa akiwa bwana mkubwa, au bwana mdogo. Hakuna aliyezaliwa akiwa mfanyakazi, fundi, mwalimu, ofisa, askari au waziri. Nafasi hizi na madaraja mbali mbali ni sehemu ya haki anazojipatia mtu kwa kipaji na jitihada zake binafsi. Watu wanapaswa kujitafutia haki hizi kwa mujibu wa uwezo, vipaji na jitihada zao.

Hapa ndipo ilipo tofauti kati ya maisha ya kijamii ya wanaadamu na yale ya wanyama wanaopenda kushirikiana kama vile nyuki. Muundo wa maisha ya nyuki ni wa asili/silika kwa asilimia mia moja. Majukumu na kazi mbali mbali zimegawiwa kwa kila mmoja wao na maumbile yenyewe. Baadhi yao wamezaliwa wakiwa machifu na wengine wamezaliwa wakiwa na vyeo vya chini. Baadhi yao huzaliwa wakiwa wahandisi, wengine wakiwa maafisa utawala na wengine wakiwa wafanya kazi wa kawaida. Lakini maisha ya mwanadamu yako tofauti kabisa. Hii ndio sababu baadhi ya wasomi wameikana kabisa ile nadharia ya kale ya kifalsafa inayosema kwamba mwanadamu ni kiumbe wa kijamii kimaumbile na wameonelea kuwa jamii ya wanaadamu ni ya kimkataba (kimaafikiano) kwa asilimia mia moja.

Haki za kifamilia Haya yote yalikuwa yanahusu jamii isiyo ya kifamilia. Sasa vipi kuhusu jamii ya kifamilia? Je, watu wote katika jamii ya familia pia wana nafasi inayofanana na ile ya haki zao wanazojipatia, au je, suala la jamii ya kifamilia, ambayo ina mke na mume, wazazi na watoto na kaka na dada ni tofauti, na je, kuna sheria maalum ya asili inayohusiana na haki za kifamilia? Katika suala hili kuna kuwepo na uwezekano wa mambo mawili. Mojawapo ni kuwa uhusiano kati ya mke na mume au kati ya wazazi na watoto ni kama mahusiano mengine yoyote ya kijamii. Ushirikiano wao ni sawa na ule wa chombo cha watu serikalini na kwenye makampuni. Mahusiano haya hayamaanishi kuwa baadhi ya watu kiasili wana nafasi maalumu.

Ni kutokana tu na sifa binafsi za mtu ndio inatokea kuwa mwingine ni bosi na mwingine ni wa cheo cha chini, mmoja hutoa amri na wengine hutii, mwingine kwa mwezi anapata mshahara mkubwa na mwingine mdogo. Kuwa mume au mke au kuwa baba, mama au mtoto pia haimaanishi kuwa kila mmoja katika hawa ana nafasi maalum. Ni sifa zao wanazojipatia ambazo huamua nafasi zao katika mahusiano yao. Nadharia ya kufanana kwa haki za kifamilia kati ya mwanaume na mwanamke (ambayo kwa makosa inaitwa usawa wa haki) imeegemea katika uwezekano huu.

Kwa mujibu wa nadharia hii, mwanaume na mwanamke hushiriki katika maisha ya kifamilia kwa uwezo sawa, mahitaji sawa na haki sawa za asili. Hivyo, haki zao za kifamilia lazima ziwekwe katika msingi wa kufanana. Kwa mujibu wa uwezekano mwingine, hata haki zao za msingi zinatofautiana. Mume ana haki na majukumu fulani na mke ana haki na majukumu yake fulani. Halikadhalika kwa baba, mama na mtoto.

Katika hali yoyote ile jamii ya kifamilia ni tofauti kabisa na taasisi nyingine za kijamii. Ni uwezekano huu, ambao kwawo dhana ya kutofanana kwa haki kati ya mwanamke na mwanaume imejengwa, na ambayo imekubaliwa na Uislamu. Sasa hebu tuangalie ni uwezekano upi kati ya aina hizi mbili hapo juu ni sahihi, na ni jinsi gani tunaweza kujua usahihi wake. Madai ya asili ya haki za kifamilia. Ili kufikia katika hitimisho sahihi wasomaji wanashauriwa kuzingatia nukta zifuatazo ambazo tayari tumeshazijadili katika suala hili: Haki za asili zimeibuka kutokana na ukweli kuwa maumbile yana lengo lililo wazi, na kuzingatia lengo hilo katika mtazamo, maumbile yamejaalia viumbe vyote hai uwezo fulani na kuweka juu yao haki fulani.

Mwanadamu kama alivyo anafaidi haki fulani zijulikanazo kama haki za binadamu, haki ambazo wanyama hawazifaidi. Ili kuzijua haki za asili na sifa zake, tunapaswa kuyatazama maumbile yenyewe. Kila uwezo wa asili ni mamlaka kwa ajili ya haki ya asili. Wanaadamu wote, kama wanajamii, wana haki za asili sawa na zinazofanana, lakini wanatofautiana katika haki walizojipatia wenyewe ambazo zinategemeana na kazi zao, sifa zao na ushiriki wao katika ushindani wa maisha. Sababu ambayo kwa nini wanaadamu wote katika jamii wana haki sawa na zinazofanana ni kwamba uchunguzi wa masuala ya wanaadamu umeweka wazi kuwa hakuna aliyezaliwa akiwa bwana mkubwa au akiwa na cheo cha chini, akiwa mwajiri au mwajiriwa, akiwa mtawala au mtawaliwa, au akiwa kamanda au askari wa kawaida.

Maisha ya mwanadamu ni tofauti na yale ya wanyama wanaopenda kushirikiana kama vile nyuki. Muundo wa maisha ya mwanadamu haukuamuliwa na maumbile wala maumbile hayakuwapangia watu kazi na vyeo mbali mbali. Nadharia ya kufanana kwa haki za kifamilia za mwanaume na mwanamke imejengwa juu ya dhana kuwa jamii ya kifamilia (wanafamilia) ni kama jamii nyingine ya watu. Wanafamilia wote wanaishi kwa uwezo sawa na mahitaji sawa. Maumbile yamewapa haki zinazofanana. Sheria ya maumbile haijawapangia muundo fulani maalumu, wala haijawapangia kazi na majukumu mbali mbali.

Ama nadharia ya kutofanana kwa haki za familia imejengwa juu ya dhana kuwa jamii ya kifamilia ni tofauti na jamii nyinginezo za kiraia. Mwanaume na mwanamke hawana uwezo na mahitaji sawa. Sheria ya uumbaji imewaweka katika nafasi zinazotofautiana na imepanga majukumu tofauti kwa kila mmoja. Sasa hebu tunagalie ni nadharia gani ni sahihi na kwa nini. Suala hili linaweza kuamuliwa kirahisi tukitumia kigezo ambacho tayari tumeshakitaja na kama tukitazama uwezo na mahitaji ya jinsia zote mbili, ambazo zinajenga mamlaka ya asili ya kudai haki za asili. Je, maisha ya kifamilia ni ya asili au ya kimkataba? Tumeshataja hapo awali kuwa kuna mitazamo miwili juu ya maisha ya kijamii ya mwanadamu. Baadhi wanaamini kwamba kwa asili mwanadamu ni jamii kwa maumbile, ambapo wengine wanashikilia kuwa maisha ya kijamii ni suala la kimkataba na maisha haya yamechaguliwa na mwanadamu kwa hiari yake chini ya ushawishi wa vipengele vinavyolazimisha. Lakini vipengele hivi ni vya nje sio vya ndani.

Hata hivyo, kama ambavyo maisha ya kifamilia yahusikavyo, hakuna mtazamo zaidi ya mmoja. Wote wanakubali kuwa maisha ya kifamilia ni ya asili kwa asilimia mia moja. Mwanadamu amezaliwa akiwa mwanafamilia kwa asili. Hakuwezi kuwa na rai mbili juu ya hili. Hata baadhi ya wanyama, kama vile njiwa na baadhi ya wadudu ambao wanaishi kwa jozi, japo hawaishi maisha ya kijamii kabisa lakini wana aina fulani ya ndoa. Hivyo, suala la maisha ya kifamilia ni tofauti na maisha ya kijamii. Maumbile yamechukua hatua fulani kuhakikisha kuwa mwanadamu na baadhi ya wanyama kwa silika wanakuwa na mwelekeo wa kupenda kuishi maisha ya kifamilia, kuunda familia na kuwa na watoto. Maisha ya mwanadamu wa kale, yawe ni ya kurithi mfumo jike au mfumo dume, lakini wakati wote aliishi maisha ya kifamilia. Nadharia ya vipindi vinne.

Kuhusiana na suala la umiliki wa mali jambo hili linakubaliwa na wote kuwa awali mali ilimilikiwa na jamii nzima (kwa pamoja) na kwamba kumiliki mali mtu mmoja mmoja kulikuja baadaye. Lakini hilo halijawahi kuwa suala la jinsia. Sababu ya umiliki mali binafsi mwanzoni kuwa na kipengele cha kijamii ni kwamba maisha wakati ule yalikuwa ni ya kikabila na kabila zima liliunda familia moja. Wanakabila ambao walikuwa wakiishi pamoja walikuwa na mawazo ya kuishi katika familia moja. Ndio maana mali ilikuwa ikimilikiwa na kabila zima. Katika jamii duni za kale hapakuwa na sheria wala mila ambayo ingeamua jukumu la mwanaume na mwanamke. Yalikuwa ni maumbile tu na hisia za asili ambazo ziliwafanya watekeleze majukumu fulani na waheshimu haki fulani. Hata katika hali hii hawakujiingiza katika ngono holela. Vile vile wanyama wale waliokuwa wakiishi katika jozi, japo hawakuwa na sheria ya kimkataba au kijamii walizingatia sheria ya asili ya haki na majukumu, na hivyo maisha yao ya ngono sio ya holela.

Mrs. Mehr Angiz Manuchehriyan katika dibaji ya kitabu chake, 'Maoni juu ya katiba na sheria ya kiraia ya Iran' anasema: Kwa mtazamo wa kisosholojia maisha ya mwanaume na mwanamke katika sehemu mbali mbali za dunia yanapitia katika moja ya hatua hizi nne. Hatua ya asili Hatua ya mwanaume kumtawala mwanamke hatua ya mwanamke kupinga kutawaliwa na mwanaume Hatua ya usawa wa haki kati ya mwanaume na mwanamke. Anaendelea kusema kuwa katika hatua ya mwanzo mwanamke na mwanaume walikuwa wanachanganyika bila kizuizi chochote. Sosholojia haikubaliani na mtazamo huu kabisa.

Kama kuna kikubwa zaidi sosholojia inachokikubali ni kuwa ilikuwa ni mila katika baadhi ya makabila duni (ya kijima) kwamba makaka kadhaa kwa pamoja walioa madada kadhaa. Na hao makaka wote walikuwa wakiwaingilia madada wote mchanganyiko na watoto walikuwa ni wa wote. Mila nyingine ni kuwa wavulana na wasichana kabla ya ndoa hawana kizuizi. Ni ndoa tu inayowawekea kizuizi. Hizi ni mila mbili tu zinazojulikana. Hata hivyo, kama kuna kabila la kijima linalokwenda zaidi ya mipaka hii na linaruhusu ngono holela basi suala lake ni la kipekee na sio la kawaida.

Will Durant katika kitabu chake, 'History of Civilization' Jalada la kwanza, anasema 'Ndoa ni ugunduzi wa wahenga (mababu) wetu waliokuwa wanyama. Katika baadhi ya ndege inaonekana kuwa ni ukweli kuwa kila ndege hubaki kushikamana na mke/mume wake maalum. Miongoni mwa sokwe na jamii ya nyani wakubwa kujamiiana kati ya dume na jike huendelea hadi mtoto aliyezaliwa anapokuwa mkubwa. Katika mambo mengine uhusiano huu unafanana na uhusiano kati ya mwanaume na mwanamke (watu). Jike linapojaribu kujisogeza kwa dume jingine, hufokewa vikali na lile dume -mume. Jamii ya nyani wanaishi katika familia yenye dume, jike na mtoto.

Ni kawaida kwa sokwe, baba na mama (sokwe) kukaa chini ya mti kula matunda wakati mtoto anakwea miti jirani yao. Historia ya mahusiano ya unyumba ni kongwe kuliko mwanadamu mwenyewe. Kuna jamii chache ambazo hazina mahusiano ya unyumba. Hata hivyo, mtu akijaribu kuzitafuta anaweza kupata chache sana. Tunachosisitiza hapa ni kuwa hisia za kifamilia ni za asili na za silika kwa wanaadamu, na sio zao la ustaarabu na tabia. Kuna wanyama wengi pia wenye hisia kama hizi kisilika. Hii ndio sababu, hakuna wakati wowote katika historia ambapo wanaume na wanawake waliishi pamoja bila kuwekeana mipaka ya ngono.

Hata wale wanaodai kuwepo kwa ukomunisti wa kifedha katika zama za ujima hawadai kuwepo kwa ukomunisti wa ngono. Nadharia ya vipindi vinne vya mahusiano ya mwanaume na mwanamke ni muigizo wa kitoto wa vipindi vinne vya umiliki wa mali, ambavyo wajamaa wanaamini. Wanashikilia kuwa katika suala la kumiliki mali, mwanadamu amepitia vipindi vinne, kipindi cha ujima, ukabaila, ubepari na ujamaa wa kisayansi, ambao ni kurudia kwa ujima lakini katika kiwango cha juu. Inachekesha kuona kuwa Mrs. Manushehriyan anakiita kipindi cha nne uhusiano kati ya mwanaume na mwanamke kuwa ni kipindi cha usawa wa haki na hakiiti kuwa ni kurudi kwa ujima. Katika hili hakufuata mfano wa wajamaa, ingawa anadai kuwa kuna mambo mengi yanayofanana kati ya kipindi cha nne na kipindi cha kwanza. Anasema kuwa kipindi cha nne kinafanana na kipindi cha kwanza kwa sababu katika zama zote hizi mbili mwanaume na mwanamke waliishi bila yeyote kati yao kuwa na madaraka juu ya mwenzake.

Bado hatuelewi anachokimaanisha hasa pale anaposema vipindi hivi (cha kwanza na cha nne) vinafanana kwa kiasi kikubwa. Kama anamaanisha kuwa katika kipindi cha nne vipingamizi vya kuchanganyika kiholela pole pole vitaondoka na familia haitakuwepo tena basi anachomaanisha juu ya usawa wa haki ambao yeye ni mtetezi wake mkubwa, ni tofauti kabisa na kile watetezi wengine wa haki za binadamu wanachokidai na wazo lake hili linaweza hata kuwakera wengine. Sasa hebu tugeuzie macho yetu kwenye asili ya hali za kifamilia za mwanaume na mwanamke. Katika hili lazima tuzingatie mambo mawili kichwani. Moja ni iwapo asili (maumbile) ya mwanamke ni tofauti na mwanaume au la kwa maneno mengine, kuangalia kama tofauti kati ya mwanaume na mwanamke ipo katika mfumo wa uzazi tu, au ina kwenda ndani zaidi.

Nukta ya pili ni kuwa iwapo kuna tofauti nyingine pia, je tofauti hizi zinaathiri haki na majukumu yao au la, au ni kama tofauti ya rangi na utaifa, mambo ambayo hayana uhusiano wowote na asili ya haki za binadamu? Mwanamke katika maumbile Kuhusiana na nukta ya kwanza, hatudhani kwamba ina ubishi. Kila mtu aliyesomasoma juu ya suala hili anajua kuwa tofauti kati ya mwanamke na mwanaume haibakii katika mfumo wa uzazi tu. Suala hapa ni iwapo tofauti hizi zinasababisha katika haki na majukumu yao au la. Wanasayansi na wachunguzi wa kizungu wameifanyia utafiti mkubwa nukta hii, na matokeo ya utafiti wao wa kibailojia, kisaikolojia na kisosholojia hayajaacha chembe yoyote ya shaka juu ya ukweli huu. Lakini ambacho wasomi hawa hawajakitupia macho vya kutosha ni kuwa tofauti hizi kati ya mwanamke na mwanaume zinasababisha kutofanana kwa haki zao na majukumu ya kifamilia, na kuwa tofauti hizi zinawaweka katika nafasi zinazofanana.

Msomi mashuhuri duniani wa kifaransa ambaye ni mwanasaikolojia, daktari wa upasuaji na mwanabaiolojia, Alexis Carrel, katika kitabu chake bora kabisa, 'Man, the Unkown being' (mwanadamu kiumbe asiyefahamika), anakiri kuwa, kwa mujibu wa sheria ya maumbile, mwanaume na mwanamke wameumbwa tofauti na kwamba tofauti zao zinafanya haki na majukumu yao kuwa tofauti. Katika kitabu chake ameweka sura moja yenye jina "Kazi za Kijinsia na Jenetiksi" katika sura hiyo anasema; korodani na ovari zina kazi nyingi sana. Viungo hivi havizalishi mayai na mbegu za uzazi na hivyo muungano wake kusababisha kuzaliwa kwa binadamu mpya peke yake, lakini pia huzalisha uowevu (fluid) ambao humwagwa katika damu na hivyo husababisha tabia za kike na kiume katika hisia zetu na katika tishu na viungo vyetu vya mwili.

Ni uoevu unaozalishwa na korodani ambao husababisha ukakamavu, ushujaa, moyo (thabiti) na kutoogopa. Ni sifa hizi zinazomtofautisha ng'ombe maksai na fahali. Ovari pia humuathiri mwanamke hivyo hivyo. Tofauti zilizopo kati ya mwanaume na mwanamke hazihusiani pekee na sura ya viungo vyao vya uzazi au mwanamke kuwa na tumbo la uzazi na kujifungua watoto na mfumo wao maalum wa elimu, bali ni matokeo ya sababu kubwa zaidi. Inatokana na kemikali zinazozalishwa na tezi za uzazi na kumwagwa katika damu.

Ni kutokana na kuipuuza nukta hii muhimu ndio baadhi ya watetezi wa harakati za wanawake wanafikiri kuwa jinsia zote mbili zinaweza kupata aina moja ya elimu na mafunzo na wanaweza kuchukua elimu na mafunzo ya aina moja na wanaweza kusomea aina moja ya fani/kazi na majukumu yanayofanana. Kwa kusema kweli mwanamke anatofautiana na mwanaume katika mambo mengi. Kila seli ya mwili wa mwanadamu na mifumo yote ya ogani, hasa mfumo wa misuli, ina alama ya jinsia. Sheria za fiziolojia pia, kama za unajimu ni thabiti na hazibadiliki. Tabia za watu haziwezi kuzibadilisha.

Tunapaswa kujaribu kuendeleza vipaji vyao katika mwelekeo unaoafikiana na haiba yao ya ndani, bila kuwaiga wanaume kibubusa. Ni jukumu lao kutoa mchango mkubwa zadi kuliko mwanaume katika maendeleo ya mwanadamu. Wasiyachukulie majukumu yao kiwepesi. Carrel, baada ya kuelezea kukua kwa manii na mayai na jinsi muungano wao unavyotokea anaonyesha kuwa kuwepo kwa mwanamke ni muhimu kwa uzazi lakini sio kuwepo kwa mwanaume.

Anaongeza kuwa mimba huukamilisha mwili na roho ya mwanamke. Mwisho wa sura anasema tusiwatazame/tusiwachukulie wasichana wadogo kwa mtazamo wa kufikiri aina moja ya maisha na namna moja ya ndoto na namna moja ya ukamilifu wao kama wavulana wadogo. Wataalamu wa masuala ya elimu na mafunzo wazingatie tofauti zao za ogani na kifiziolojia na majukumu ya asili ya mwanaume na mwanamke.

Zingatio la nukta hii ya msingi ni muhimu sana kwa mustakabali wa ustaarabu wetu. Kama ulivyoona, mwanasayansi huyu mkubwa anaweka msisitizo katika tofauti nyingi zilizopo kati ya mwanamke na mwanaume na anaamini kuwa tofauti hizi zinawaweka katika nafasi tofauti. Katika sura inayofuata pia, tutanukuu maoni ya wanasayansi juu ya nukta hii, na kisha tutafikia hitimisho kuwa ni maeneo gani ambayo mwanaume na mwanamke wana uwezo na mahitaji sawa na hivyo wanastahili haki na majukumu yanayofanana na ni katika maeneo gani wana nafasi tofauti na hivyo haki na majukumu yasiyofanana. Sehemu hiyo ya kitabu itakuwa muhimu sana kuliko nyingine zote juu ya somo na upangaji wa haki na majukumu ya kifamilia kati ya mwanaume na mwanamke.

7

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

TOFAUTI KATI YA MWANAMKE NA MWANAUME

Hii inaonekana kuwa sentensi isiyofaa. Inaonekana kuwa japo tupo katika karne hii, bado kuna baadhi ya watu, hapa na pale, ambao wana mawazo ya kizamani, na bado wanang'ang'ania wazo lililopitwa na wakati la tofauti kati ya mwanaume na mwanamke. Kama watu wa zama za kati (1500 A.D), watu hawa bado wanamuona mwanamke kuwa wa jinsia ya cheo cha chini na kwamba sio mwanadamu kamili na kamilifu. Yupo katikati si binaadamu wala si mnyama.

Hafai kuishi maisha ya kujitegemea na lazima aishi chini ya uangalizi na udhibiti wa wanaume. Lakini sasa tunajua kuwa mawazo yote haya yamepitwa na wakati na hayafai. Leo hii tunajua fika kuwa dai potofu la kudaiwa kuwa mwanamke sio mkamilifu lilizushwa na mwanaume katika enzi zile ambazo alikuwa anamtawala mwanamke. Sasa, habari iliyothibitishwa ni kwamba mwanamke anatokana na jinsia bora zaidi na mwanaume anatokana na jinsia duni. Haya hi maoni ya baadhi ya wa magharibi wa kisasa.

Kwa ukweli kabisa, maendeleo ya sayansi ya karne ya 20 yamethibitisha wazi wazi kuwepo kwa tofauti kati ya mwanaume na mwanamke. Kuwepo kwao sio uwasilishaji mbaya wa kijicho, bali ni ukweli wa kisayansi, uliotokana na uchunguzi na majaribio. Hata hivyo tofauti hizi hazipo ili kuthibitisha ni jinsia gani ni bora kuliko nyingine. Sheria ya maumbile imeziweka tofauti hizi ili mahusiano ya ndoa yawe imara zaidi na kuufanya msingi wa muungano kati ya mume na mke uwe mkubwa, imara na bora zaidi.

Maumbile yalitaka kugawa haki za kifamilia na majukumu yake baina yao kwa mikono yake (maumbile) yenyewe. Sheria ya maumbile umezifanya tofauti kati ya mwanaume na mwanamke sawa na tofauti ya viungo mbali mbali vya mwili. Imetoa nafasi mbali mbali kwa macho, masikio, mikono, nyayo na uti wa mgongo. Lakini haimaanishi kuwa imefanya dhulma na ubaguzi dhidi ya kiungo chochote.

Je ni uwiano au ukamilifu na kutokamilika? Inashangaza kwamba baadhi ya watu wanasisitiza kuwa tofauti katika nguvu za kimwili na kisaikolojia za mwanaume na mwanamke hutokana na ukamilifu wa mwanaume na kutokamilika kwa mwanamke. Wanashikilia kuwa, kwa sababu fulani nzuri, kwa makusudi kabisa mwanamke ameumbwa akiwa sio mkamilifu. Dhana ya kutokuwa mkamilifu kwa mwanamke imekuwa maarufu zaidi katika nchi za Magharibi kuliko Asia. Watu wa Magharibi wamemuonea. Wakati fulani wamekuwa wakitoa tafsiri mbaya ya maandiko ya kidini juu ya mwanamke, wanasema kwamba mwanamke ajione haya.

Wakati fulani wanasema, 'Mwanamke ni kiumbe mwenye nywele ndefu na ubongo usiofaa,' 'mwanamke ni nusu ya mnyama na nusu ya mtu'n.k. Bado inashangaza zaidi kuona kwamba baadhi ya watu wa Magharibi wamebadilisha mwelekeo wao kwa nyuzi 180, hivi karibuni wameanza kuleta hoja elfu na moja kuthibitisha kwamba kwa mujibu wa maumbile, mwanaume ni duni na sio mkamilifu na kwamba jinsia ya mwanamke ni bora na mkamilifu.

Kama umeshakisoma kitabu, "Woman, the Superior Sex,' cha Ashley Montague, unaweza kuona ni jinsi gani mwandishi huyu, kwa kupotosha ukweli na kuleta hoja zisikubaliana na ukweli alivyojaribu kuthibitisha kuwa mwanamke ni mkamilifu zaidi kuliko mwanaume. Katika fani za utabibu, saikolojia na takwimu za jamii kitabu hiki kinafaa sana, lakini pale mwandishi anapojaribu kutoa hitimisho lake kuthibitisha dai lake, ambalo ndio jina la kitabu anakwenda kwenye upuuzi mkubwa kabisa. Haifahamiki kwa nini ni lazima kwa watu wa Magharibi kwamba siku moja wamuumbue mwanamke na kumuadhiri ili siku ya pili warekebishe yale ya nyuma, wanalazimika kumuondolea mapungufu na udhaifu waliokuwa wamembandikia na badala yake wanambandikia hayo mwanaume.

Kuna umuhimu gani wa kuangalia tofauti kati ya mwanaume na mwanamke kwa matokeo ya ukamilifu wa jinsia mmoja na upungufu wa jinsia nyingine, ili kwamba wakati mwingine tulazimike kumuweka mwanaume upande na wakati mwingine mwanamke? Mwandishi wa kitabu hiki anasisitiza kuwa mwanamke ni bora kuliko mwanaume na anaona kuwa utukufu alionao (mwanaume) ni matokeo ya sababu za kihistoria na kijamii na sio matokeo ya sababu za asili. Kwa kusema kweli, tofauti kati ya mwanaume na mwanamke ni suala la uwiano sio ukamilifu na kutokamilika.

Sheria ya maumbile imeamua kuwa kwa kuwa mwanaume na mwanamke wameumbwa ili waishi pamoja, lazima wawe na uwiano mahususi wa vipaji vyao licha ya tofauti hizi. Nukta hii itafafanuliwa baadaye. Nadharia ya Plato. Suala la tofauti kati ya mwanamke na mwanaume sio jipya ambalo tunaweza kusema kuwa limeibuka katika zama zetu. Lina umri wa miaka zaidi ya 2400. Lilijadiliwa katika sura yake ya sasa, na Plato katika kitabu chake 'The Republic'. Kwa uwazi anaelezea kwamba wanaume na wanawake wana vipaji sawa, na wanawake wanaweza kufanya kazi za kiume na kupata haki kama zile za wanaume. Chanzo cha mawazo yote kuhusu mwanamke, ambayo yameibuka katika karne ya 20, na hata sehemu ya mawazo haya yanayoonekana kuwa ya ovyo na yasiyobadilika kwa watu wa karne ya 20, yamo katika mitazamo ya Plato.

Hii ndio sababu watu wanavutiwa naye sana na kumuita 'Baba wa falsafa'. Plato katika sura ya tano ya kitabu chake, 'The Republic' alizungumzia masuala kama vile ukomunisti wa wanawake na watoto, kuboresha kizazi (breed), kuwa hasi baadhi ya wanaume na wanawake, kuwaruhusu kuzaa wale tu wenye sifa zilizotukuka za kijenetiki, kulea watoto nje ya mazingira ya kifamilia na kuruhusu kuzaa katika miaka fulani tu ya uhai, katika kipindi ambacho nguvu (za uzazi) zipo kileleleni. Plato anaamini kuwa kama ilivyo kwa mwanaume, mwanamke anapaswa kupewa mafunzo ya kijeshi na kama mwanaume anavyoshiriki katika riadha, mwanamke ashiriki pia.

Hata hivyo, kuna mambo mawili ambayo Plato ameyasema. Moja ni kuwa anakiri kuwa kimwili na kiakili wanawake ni dhaifu kuliko wanaume. Kwa maneno mengine anaiona tofauti kati ya mwanaume na mwanamke kuwa ni ya kiasi (ukubwa), sio sifa (ubora) wa vipaji vyao. Anaamini kuwa wote mwanaume na mwanamke wana vipaji. Kitu pekee ni kuwa katika baadhi ya mambo mwanamke ni dhaifu kuliko mwanaume, lakini haoni sababu kwa nini awe na mfumo wa kipekee wa kuendesha mambo. Kwa vile Plato anamuona mwanamke kuwa dhaifu kuliko mwanaume, anamshukuru Mungu kuwa alizaliwa mwanaume. Anasema; "Namshukuru Mungu kwa kuzaliwa kwangu Mgiriki (myunani) na sio vinginevyo, kwa kuzaliwa kwangu nikiwa huru na sio mtumwa na kuzaliwa kwangu mwanume na sio mwanamke." Nukta ya pili ni kuwa yote aliyoyasema Plato ya kuhusu kuboresha ukoo (uzazi), vipaji vya jinsia zote mbili na ukomunisti wa mwanamke na watoto yanahusiana na tabaka tawala, yaani wanafalsafa watawala, kwa sababu kwa mujibu wake, ni tabaka hili tu ndio linafaa kuwa watawala.

Kama tunavyojua kisiasa, Plato alikuwa ni mpinga demokrasia na alikuwa akitetea utawala wa matabaka. Hivyo, alichokisema katika nukta hizo, kinahusiana na tabaka tawala. Kuhusiana na matabaka mengine, ana maoni tofauti. Aristole dhidi ya Plato. Mwanafunzi wa Plato, Aristole ni mwanafikra mwingine wa ulimwengu wa kale, ambaye maoni na mawazo yake tunayo. Ametoa maoni juu ya tofauti kati ya mwanamke na mwanaume na ameyapinga vikali maoni ya mwalimu wake. Anaamini kuwa mwanaume na mwanamke wanatofautiana sio kwa kiasi tu bali hata kwa sifa. Anasema kwamba jinsia hizi mbili zina vipaji vya aina tofauti na majukumu waliyopewa na sheria ya maumbile na haki walizopewa, vyote vinatofautiana sana. Kwa mujibu wa Aristole, kanuni zao za maadili pia zinatofautiana katika mambo mengi. Inawezekana kuwa sifa ya maadili ikawa bora kwa mwanaume lakini isiwe hivyo kwa mwanamke na kinyume chake.

Katika ulimwengu wa kale maoni ya Plato yaliondolewa, yakachukuliwa ya Aristole. Wasomi waliofuatia walipendelea maoni ya Aristole kuliko ya Plato. Mtazamo wa ulimwengu wa sasa. Hayo yalikuwa ya ulimwengu wa kale. Sasa hebu tuangalie ulimwengu wa sasa unavyosema. Ulimwengu wa sasa haubahatishi wala kukadiria. Unatumia njia za kisayansi. Hitimisho zake zimejengwa juu ya ukweli, takwimu na utafiti katika ulimwengu wa sasa.

Kama matokeo ya elimu kubwa na sahihi zaidi katika medani za utabibu, saikolojia na maarifa ya jamii, tofauti nyingi na kubwa, zaidi kati ya mwanamke na mwanaume, zilizokuwa hazijulikani katika ulimwengu wa kale, sasa zimegunduliwa. Watu wa kale walitathimini mwanaume na mwanamke kwa msingi wa kuwa mmoja ni mwenye kukwaruza sana, mrefu ana nywele nyingi zaidi mwilini, ana maungo makubwa zaidi na ana sauti nene zaidi wakati mwingine ana mwili nyororo zaidi, mfupi zaidi, na msafi zaidi, ana sauti nyembamba zaidi na ana maungo madogo zaidi. Waliozama zaidi walizingatia tofauti ya umri wao wa kukua (kubalehe na kuvunja ungo) na tofauti ya akili na hisa zao.

Walimchukulia mwanaume kama alama ya busara, na mwanamke kama alama ya upendo na mihemko. Lakini leo tofauti nyingi zaidi zinajulikana sasa kwamba ulimwengu wa mwanamke ni tofauti na ulimwengu wa mwanaume katika mambo mengi. Kwanza tutasimulia tofauti kati ya mwanaume na mwanamke, kwa mujibu wa tulivyozikusanya kutoka kwa wataalamu mabingwa wa fani hii. Kisha tutaeleza falsafa yake na tutaonyesha tofauti zipi ni za asili na zipi ni matokeo ya kihistoria, kiutamaduni na vipengele vya kijamii. Baadhi ya tofauti hizi ziko wazi mno kiasi cha kuwa huwezi kuzikana. Elimu ya wengine (juu ya hili) inaweza kupatikana kwa kusoma kidogo na uzoefu.

2

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

I- UISLAMU NA MAISHA YA KISASA

Suala la dini na maisha ya kisasa ni moja ya mambo ambayo hayawagusi Waislamu peke yao. Dini nyingine pia zilikumbana na tatizo hili. Watu wengi wenye kupendelea mabadiliko duniani, wameikana dini kwa sababu wanaamini kuwa dini na maisha ya sasa haviendi pamoja. Wanafikiri kuwa kudumaa, kutuama na kutobadilika ni sifa za lazima za mtu mshika dini. Kwa maneno mengine, wanafikiri kuwa kudumaa na ukinaifu unatokana na kutokuwepo kwa mabadiliko na kwamba kudumisha hali ya kizamani ndio tabia za dini.

Marehemu Bwana Nehru aliyekuwa waziri Mkuu wa India alikuwa na mawazo ya kisekula na hakuwa akiamini dini yoyote. Inaoinekana kutokana na kauli zake kuwa kilichomfanya asipende dini ni kutobadilika kwake na ukinaifu unaotokana na kutokuwepo kwa mabadiliko. Kuelekea kipindi cha mwisho cha maisha yake Nehru alihisi kuwa na uwazi moyoni mwake na aliamini kuwa uwazi ule ungezibwa na nguvu ya kiroho tu.

Lakini hakuelekea kuiamini dini yoyote kwa sababu aliamini kuwa hali ya ukinaifu na kutokuwepo kwa mabadiliko ilikuwepo katika dini zote. Mwandishi wa habari wa Kihindi, aitwaye Karanjia, alimhoji Nehru katika kipindi chake cha mwisho mwisho cha uhai wake (Nehru) na alivyoonekana haya yalikuwa ni mahojiano ya mwisho ambapo Nehru alitoa maoni yake juu ya matatizo ya jumla ya ulimwengu.

Alipokuwa akimzungumzia Gandhi, Karanjia alisema, "Baadhi ya wanaopendelea mabadiliko (liberals) na maendeleo wanaamini kuwa Gandhiji, kwa kupitia na kwa kutokana na utatuzi wake wa matatizo kwa hisia kali, unyofu na njia za kiroho, zimedhoofisha na kuitia ubaridi imani yako ya asili ya ujamaa wa kisayansi." Katika kulijibu hili, Nehru alisema; "Ni muhimu na vizuri kutumia fursa ya njia za kimaadili na kiroho.

Mara zote nimekubaliana na Gandhiji juu ya hili. Ninaamini kuwa ni muhimu zaidi kutumia fursa ya njia hizi, kwani sasa, kwa kiasi kikubwa kuliko ilivyokuwa huko nyuma, tunahitaji majibu ya kiroho na kimaadili juu ya maswali yanayotokana na pengo la kimaadili linalosababishwa na tamaduni za kisasa, ambazo zinazidi kuwa maarufu." Kisha Kiranjia aliuliza swali juu ya Ukomunisti.

Nehru alikiri mapungufu yake na katika majibu yake alionyesha baadhi ya mapungufu na ubovu wake (wa ukomunisti). Kwa mara nyingine tena alipendekeza suluhisho la kiroho juu ya matatizo ya dunia. Alipofika hapa Karanjia akasema; "Bwana Nehru, je dhana yako ya utatuzi wa matatizo ya kimaadili na kiroho haikufanyi uwe tofauti na Jawahanal wa jana? (Nehru mwenyewe enzi za ujana wake).

Ulichokisema kinaonyesha kuwa Bwana Nehru, katika kuelekea mwisho wa uhai wake, ameanza kumtafuta Mungu." Nehru alisema; "Ndiyo, nimebadilika. Msisitizo wangu juu ya unyofu na maadili ya kiroho na utatuzi wa matatizo sio wa bahati mbaya." Akaongeza kuwa; "Swali sasa ni jinsi ya kukuza maadili na imani ya kiroho katika daraja la juu zaidi.

Hapana shaka kwamba kwa ajili ya hili, dini zipo, lakini kwa bahati mbaya zimechukua mtazamo finyu na matendo yasiyobadilika na zimebaki kuwa taratibu rasmi lakini duni. Ni umbo lake la nje tu lililobaki, lakini ari na dhana yake ya kweli imetoweka." Uislamu na mahitaji ya wakati. Katika dini zote ni Uislamu tu unaojihusisha zaidi na vipengele vyote vya maisha ya mwanadamu.

Mafundisho yake hayajajikita katika matendo ya ibada na sala na mfumo wa ushauri wa maadili peke yake. Uislamu, kama ulivyoshughulikia uhusiano wa watu na Mwenyezi Mungu, ndivyo hivyohivyo ulivyoshughulikia mahusiano baina ya watu. Katika sura mbali mbali Uislamu umeshughulikia haki za watu binafsi na majukumu yao pia.

Hii ndio sababu swali kwamba mafundisho yake yanafaa kutumika au la katika mazingira yanayozidi kubadilika ni thabiti zaidi katika suala la Uislamu kuliko dini nyingine yoyote. Kwa bahati imetokea kwamba, wasomi wengi na waandishi wasiokuwa Waislamu wamezisoma sheria za kijamii na kiraia (za madai na za jinai) na wamezisifu kuwa ni chombo cha kisheria cha kimaendeleo na endelevu.

Wameusifu Uislamu kwa mapana na marefu, kuwa ni dini hai na itakayodumu milele, na wameuelezea uwezo na sifa za sheria hizi za Kiislamu wa kuweza kutumika nyakati zote na katika hali zote. Mwandishi maarufu sana wa Kiingereza aliyekuwa akipendelea msimamo wa wastani (liberal), Bernard Shaw amesema; "Mara zote nimekuwa nikiipa dini ya Muhammad heshima kubwa (daraja kubwa), kutokana na uhai wake wa ajabu.

Ni dini pekee inayoonekana kwangu kuwa na uwezo wa kunyumbulika na hivyo kuweza kutumika katika dunia inayobadilika na katika zama zote. Nimetabiri kuwa imani ya Muhammad itakubaliwa na Ulaya ya kesho, na dalili za hili zinajionyesha hata sasa. Makasisi wa zama za kati aidha kwa sababu ya ujinga au kwa sababu ya kung'ang'ania bila hoja imani zao waliupaka Uislamu rangi mbaya kabisa. Kwa kusema kweli walifundishwa kumchukia mtu huyu, Muhammad na dini yake. Kwao Muhammad alikuwa mpinga Kristo.

Mimi nimemsoma, mtu huyu wa ajabu, na kwa maoni yangu hakuwa mpinga Kristo kabisa na lazima aitwe mkombozi wa wanaadamu. Ninaamini kuwa kama mtu kama yeye angetwaa madaraka /uongozi wa dunia ya sasa angefanikiwa kutatua matatizo katika namna ambayo ingeleta amani na furaha, vitu ambavyo vinahitajika sana kwa sasa. Dr. Shibli Shama'il ni myakinifu wa Kiarabu wa Lebanoni. Kwa mara ya kwanza alitafsiri kitabu cha 'Darwin Kiitwacho 'Origin of Species' kwenda katika lugha ya Kiarabu, pamoja na sharhe ya mwanasayansi wa kijerumani aitwaye Boucher katika kitabu hicho akakipa jina la 'A weapon against religious belief.' ('Silaha dhidi ya imani za kidini.') Ingawa hamwamini Mwenyezi Mungu, haoni aibu kuusifu Uislamu na muasisi wake mtukuka. Ameusifu Uislamu kwa kusema kuwa ni dini hai inayoweza kutumika katika zama zote.

Mtu huyu, katika juzuu ya pili ya kitabu chake kiitwacho, 'Philosophy of Evolution' ambacho amekichapisha kwa Kiarabu, ameandika makala yenye kichwa cha cha habari 'Uislamu na Ustaarabu'. Ameandika makala hii kukanusha madai ya wasio Waislamu kwa kutoa madai kuwa Uislamu ndio uliosababisha kuporomoka kwa hali ya Waislamu. Shibli Shama'il amejaribu kuthibitisha kuwa jambo hasa lililosababisha kuporomoka kwa hali za Waislamu ni wao Waislamu kuyaacha (kuacha kutekeleza) mafundisho ya kijamii ya Uislamu.

Wale wazungu wanaoushambulia Uislamu aidha hawajui au wanafanya hivyo kwa nia mbaya ya kuwafanya watu wa Mashariki (Asia) wazitilie shaka sheria zao na mfumo wao ili kuwafanya wafuate mfumo wa Kimagharibi. Wakati wa zama zetu, suala la iwapo Uislamu unaafikiana na hali halisi ya maisha ya sasa au la limekuwa likiulizwa sana. Tunapata picha ya ndani ya watu hasa wale wanaotoka katika tabaka la wasomi na tunakuta kuwa swali hili linaulizwa zaidi kuliko maswali mengine.

PINGAMIZI

Wakati fulani watu hawa wanatoa hoja za kifalsafa juu ya suala hili kuwa vitu vyote hapa duniani lazima vibadilike. Hakuna kinachobaki vile vile bila kubadilika, na halikadhalika binadamu wanabadilika. Sasa inawezekanaje sheria za Kiislamu zibaki hivyo bila kubadilika kwa zama nenda rudi? Kama tukilitazama swala hili kwa mtazamo wa kifalsafa kabisa, jibu ni rahisi.

Ni vitu (maada) vinavyobadilika kila mara, ambavyo hukua na kuporomoka na ambavyo hupasika katika kugeuka na kuoza. Lakini sheria za ulimwengu hazibadiliki. Kwa mfano, viumbe vyote hai vimegeuka na vimeendelea kugeuka kwa mujibu wa utaratibu na kanuni fulani zilizoelezwa na wanasayansi. Hapana shaka kwamba viumbe hivi vinageuka na kubadilika lakini kanuni zinazotawala mabadiliko haya hazibadiliki. Na sasa tunazungumzia kanuni (sheria) hizi.

Katika hili, hakuna tofauti yoyote iwapo sheria hizi ni za asili au zimetungwa na kukusanywa, kwani inawezekana kwamba sheria ambazo zimetungwa zinaweza kuwa na asili kama chanzo chao na kuafikiana na mchakato wa mabadiliko ya mtu mmoja mmoja na halikadhalika jamii ya wanadamu kwa ujumla.

Hata hivyo, swali kuhusiana na kuafikina au kutoafikiana kwa Uislamu na mahitaji ya muda halina sura ya kiujumla na kifalsafa peke yake. Swali ambalo huulizwa zaidi ni kuwa kwa vile sheria huundwa kukidhi mahitaji ya wanaadamu na mahitaji yenyewe yanabadilika kila mara inawezekanaje sheria hizo za kijamii zibaki hivyo hivyo bila kubadilika? Ni swali zuri.

Na imetokea kuwa tabia za kimiujiza za Uislamu zimewezesha sheria zisizohitaji kubadilishwa kukidhi mahitaji yasiyobadilika ya mtu mmoja na jamii na sheria zinazobadilika badilika kwa mahitaji ya muda mfupi na yanayobadilika. Hii ni sifa ya kipekee ambayo Waislamu wote wajuzi wa mambo ya sheria za kiislamu na waliozisoma sheria zake wanajivunia. Tutalielezea hili vizuri zaidi baadaye. Je mabadiliko ya kijamii yanakwenda na wakati? Kabla ya kuliendea swali hili tungependa kuibua nukta mbili. Nukta ya kwanza ni kuwa watu wengi wanaoongelea maendeleo na mabadiliko ya hali wanadhani kuwa mabadiliko yoyote ya kijamii, hasa kama yametokea nchi za Kimagharibi, basi ni matokeo ya maendeleo.

Hili ni moja ya mawazo potofu liliyoendekezwa na kizazi hiki. Watu wanadhani kuwa kwa vile njia za maisha hubadilika siku hadi siku, zilizo duni hubadilishwa kwa zilizo bora zaidi na sayansi na viwanda vinaboreka kila siku, mabadiliko yote katika maisha ya binadamu ni aina ya maendeleo na kwa hiyo yanafaa kukaribishwa na kupokelewa kwa mikono miwili. Wanafikiri pia kuwa mabadiliko haya hayaepukiki na huja baada ya muda fulani.

Kwa kusema kweli sio kwamba mabadiliko yote ni matokeo ya maendeleo ya sayansi na viwanda wala sio kwamba hayaepukiki. Huku sayansi ikiendelea kukua, asili ya ubinafsi na unyama wa mwanadamu nayo hubaki bila kubadilika. Ujuzi (elimu) na busara humpeleka mtu katika ukamilifu na asili ya unyama wa mwanadamu humsukumia kwenye ufisadi na upotofu.

Asili ya unyama wa mwanadamu mara zote hujaribu kutumia ujuzi kama njia ya kupatia matamanio yake. Kwa kadiri muda unavyokwenda, kwa kadiri maendeleo na mabadiliko yanavyotokea, ufisadi na upotofu ndivyo unavyozidi kukua na kukomaa. Tunapaswa kwenda na wakati lakini wakati huo huo lazima tupige vita ufisadi pia. Mleta mabadiliko (mema) na mpinga mabadiliko (mema) wote wanapigana dhidi ya muda, tofauti yake ni kuwa mleta mabadiliko mema hupigana dhidi ya upotofu unaoletwa na mabadiliko ya muda na mpinga maendeleo (mabadiliko) hupigana dhidi ya mabadiliko (maendeleo halisi) yanayoletwa na mabadiliko ya muda.

Kama tunauchukulia muda na mabadiliiko yake kama kigezo cha mema yoyote na maovu yote, sasa ni kigezo gani cha kuupimia muda wenyewe? Kama kila kitu kitakwenda na wakati sasa je wakati wenyewe unapaswa kwenda na nini? Kama mwanadamu ataufuata muda na mabadiliko yake kwa utii mkubwa, sasa nini kitafanyika juu ya majukumu na nafasi ya utashi wa mwanadamu? Mwanadamu anaendesha gari la wakati, ambalo liko kwenye mwendo.

Lazima awe mwangalifu na aliongoze vyema gari lake. Vinginevyo atakuwa kama mtu aliyepanda farasi na akamwachia farasi wake aende popote atakapo. marekebisho au kuondoa kabisa? Nukta ya pili inayofaa kutajwa hapa ni kwamba baadhi ya watu wamelitatua tatizo gumu la Uislamu na mahitaji ya wakati kwa namna rahisi sana.

Wanasema kuwa Uislamu ni dini ya milele, na inaweza kurekebishwa ili kuafikiana na mahitaji ya kila zama na wakati. Lakini wanapoulizwa marekebisho haya yanafanyikaje na kanuni yake ni nini, mara moja wanasema kuwa hali ya maisha inapobadilika, sheria zilizopo hubatilishwa na kuwekwa nyingine. Wanatoa hoja kuwa sheria za msimu (muda mfupi) za kidini lazima ziwe na uwezo wa kurekebishwa na ziafikiane na maendeleo ya elimu na sayansi pamoja na kupanuka kwa utamaduni na ustaarabu. Kwa mujibu wao, uwezo huo wa sheria wa kuweza kurekebishwa ili kuafikiana na mahitaji ya wakati haupingani na Uislamu na sio kinyume na mafundisho yake.

Wanadai kuwa, kwa vile mahitaji ya wakati yanabadilika kila mara, basi kila zama huhitaji sheria mpya. Wanaendelea kudai kuwa sheria za kiraia na kijamii za Uislamu zinaafikiana na maisha rahisi ya Waarabu waliokuwa wakiishi kabla ya Uislamu, na ambazo kwa kiasi kikubwa zilikuwa ni kwa mujibu wa mila na desturi zao.

Sasa kwa kuwa haziafikiani na maisha ya zama hizi zinatakiwa ziondolewe na ziwekwe nyingine mpya za kisasa. Watu hawa wanapaswa kuulizwa: Kama uwezo wa sheria kuweza kurekebishwa maana yake ni uwezo wa kubatilishwa na kufutwa, basi ni sheria gani ambayo haina sifa hii? Kuna sheria basi yeyote ambayo haiendi na wakati kwa mtazamo huu?

Tafsiri hii ya uwezo wa sheria kurekebishwa na kuweza kutumika katika zama zote ni sawa na kusema kuwa vitabu vyote na maktaba ndio njia bora kabisa za kufurahia maisha kwa sababu muda wowote mtu atakapotaka starehe, anaweza kuviuza na kutumia fedha zitakazopatikana kwa ajili ya kukidhi matamanio yake. Mwandishi wa Kiirani anasema kuwa mafundisho ya Uislamu yamegawanyika katika sehemu tatu.

Sehemu ya kwanza ina imani za msingi kama vile tauhidi (imani kuwa Mungu ni mmoja tu), Utume, Ufufuo n.k. Sehemu ya pili inahusiana na matendo ya ibada kama vile sala, saumu, udhu, tohara, hija n.k sehemu ya tatu ina sheria zinazohusiana na maisha ya watu. Kwa mujibu wake yeye ni sehemu mbili tu za mwanzo ambazo ni za lazima katika dini na ambazo zinafaa kuhifadhiwa milele.

Lakini sehemu ya tatu sio sehemu ya lazima ya dini kwa kuwa dini haihusiani na maisha ya kila siku ya watu. Mtukufu Mtume mwenyewe hakuamuru kuwa sheria hizi ziwe sehemu ya dini kwa vile hazikuhusiana na ujumbe wake yeye kama Mtume. Ilitokea tu kwamba akawa ni mkuu wa Dola, kwa hiyo akalazimika kuweka sheria pia. Vinginevyo dini haina lolote la kulazimisha katika maisha ya kidunia ya watu. Ni vigumu kuamini kuwa mtu anayeishi katika nchi ya Kiislamu anaweza kuwa mjinga wa mafundisho ya Uislamu kiasi hiki. Je, Qur'ani haijaelezea lengo la kuleta Mitume na Manabii? Je, Qur'ani haisemi wazi wazi kuwa:'Tumewaletea Mitume wetu na dalili za wazi na tumewaleta pamoja nao kitabu na vipimo, ili watu wahukumiane kwa haki. (Suratul Hadidi; 57:25). 35 Qur'ani imeuelezea uadilifu katika jamii kama lengo kuu la Mitume wote.

Kama unataka unaweza usiyafuate mafundisho ya Qur'ani, lakini kwa nini unatenda dhambi kubwa zaidi kwa kuusingizia na kuuzushia Uislamu na Qur'ani? Bahati yetu mbaya zaidi inatokana na ukweli kwamba maadili yetu na sheria vimepoteza chanzo pekee cha nguvu yake, yaani dini. Ni katika nusu karne tu tulipoanza kusikia watu wakipiga kelele kuwa Uislamu ni mzuri, ili muradi tu ubakie ndani ya majumba ya ibada, na usishughulike na jamii.

Kelele hii imepigwa kutoka ndani ya mipaka ya nchi za Waislamu na imeenezwa katika ulimwengu wote wa Kiislamu. Ili kuliweka lengo la kelele hizi wazi tunaweza kusema kuwa nia ni kuufanya Uislamu ubaki kuwa ni kikwazo cha kuzuia kuenea kwa ukomunisti lakini kama huu huu Uislamu utagongana na maslahi ya Magharibi basi upingwe vikali.

Kwa mtazamo wa watu wa Magharibi, matendo ya Uislamu lazima yaendelee, ili pindi ikitokea haja, Waislamu wahamasishwe kuupinga mfumo wa kikomunisti ambao hauamini mambo ya dini na Mungu, lakini sheria za kijamii za Uislamu ambazo zinatoa falsafa ya maisha ya Uislamu lazima ziondoshwe, kwa vile sheria hizi huwapa Waislamu uhuru fulani na kuwafanya wawe watu tofauti wanaojitegemea katika mfumo wao, jambo ambalo litawazuia kumezwa na nchi za Magharibi zenye tamaa kali. Kwa bahati mbaya, watetezi wa hoja kuwa Uislamu haujihusishi na maisha ya kila siku ya watu, wamesahau baadhi ya ukweli wa msingi. Awali miaka 1400 iliyopita, Uislamu ulipinga kanuni kuwa tunaamini baadhi ya mambo (baadhi ya mafundisho ya Uislamu) na tunayakataa mengine, na ukatamka kuwa kanuni na sheria za Uislamu hazibadiliki.

Pili tunaamini kuwa muda umefika ambapo Waislamu hawapaswi kupotoshwa na mbiu za uongo. Watu sasa pole pole wameanza kuamka na wameanza kutofautisha kati ya maendeleo ambayo ni matokeo ya kuchanua kwa vipaji vya kisayansi na kiakili, na kudhihiri kwa ufisadi na upotofu, kutoka nchi za Magharibi. Watu wa ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa, kuliko kipindi kingine chochote, wameanza kufahamu thamani ya mafundisho ya Uislamu na wametambua kuwa wanaweza tu kuishi maisha huru kwa kuyafuata. Hawatayaacha, kwa gharama yoyote.

Waislamu makini wanafahamu kuwa propaganda dhidi ya sheria za kiislamu si chochote bali udanganyifu wa mabepari. Tatu, watetezi wa hoja hii wanapaswa kujua kuwa Uislamu unapokuwa na nguvu, hushinda mifumo mingine yote, iwe ya kikafiri au vinginevyo. Uislamu unataka kutawala maisha ya jamii kama falsafa ya maisha, na hautaki kubakia misikitini tu na sehemu nyingine za ibada. Uislamu ambao utabakia kwenye nyumba za ibada, utaacha nafasi kwa ajili ya mawazo ya Kimagharibi na halikadhalika mawazo yanayopingana na umagharibi na itikadi zake. Adhabu ambazo nchi za magharini zinatumikia, katika baadhi ya nchi za Waislamu ni matokeo ya kutoujua ukweli huu.

3

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

- II UISLAMU NA MAISHA YA KISASA

Mwanadamu sio kiumbe pekee anayeishi maisha ya kijamii. Wanyama wengi, na hususan wadudu hupenda kuishi pamoja na kushirikiana. Wanafuata kanuni za mgawanyo wa kazi, uzalishaji na ugavi na kutoa na kupokea amri. Nyuki, na baadhi ya wadudu jamii ya mchwa wana mfumo huu bora wa maisha, mfumo ambao utamchukua mwanadamu, anayejiona kuwa ni mfalme wa viumbe vyote, miaka au hata karne ili kufikia kiwango hicho cha ufanisi.

Ustaarabu wao (wadudu hawa) haujapitia vipindi kama vile zama za mwituni, zama za mawe na zama za nyuklia. Toka mwanzo wamekuwa na ustaarabu na mfumo wa namna moja kama tu walivyo leo. Ni mwanadamu aliyeanzia sifuri. Tazama : "Mwanadamu aliumbwa dhaifu ."Suratul Nisaa 4:28 Kwa upande wa wanyama, mahitaji yao ya maisha hayabadiliki. Kwao usasa na fasheni mpya havina maana. Ulimwengu wa kale na ulimwengu wa sasa kwao hauna tofauti yoyote.

Kwao sayansi haifanyi ugunduzi wowote ule. Bidhaa mpya kabisa nyepesi na nzito za viwanda hazikuingia katika soko lao; kwa nini? Kwa sababu wanaishi kwa silika na sio kwa akili (mantiki). Maisha ya kijamii ya mwanadamu mara zote yanabadilika. Kila karne ulimwengu unabadilika. Hapo ndio kuna siri ya mwanadamu kuwa mfalme wa viumbe vyote.

Mwanadamu ni mtoto wa maumbile aliyekomaa na kustahili heshima. Amefikia hatua ambayo hahitaji muongozo wa moja kwa moja wa ile nguvu ya ajabu iitwayo silika. Maumbile yanafahamu kuwa mwanadamu ni kiumbe aliyekomaa, na ndio maana yamemuacha huru. Yale ambayo wanyama wanayatekeleza kwa silika na kwa kufuata kanuni za maumbile ambazo hawawezi kuzivunja/kukiuka, wanaadamu wanatakiwa kuyatekeleza kwa kutumia akili na elimu na kwa kufuata sheria zilizopitishwa na zinazoonekana. Mwanadamu akiwa ni mwamuzi wa mwisho wa majaaliwa yake mara zote anaweza kupotoka na kuiacha njia ya maendeleo, na hapa ndio kuna siri ya kuteleza kwake, vipingamizi vyake (anavyokumbana navyo) kupotoka na kushindwa kwake.

Kama tu ilivyo kuwa maendeleo yapo wazi kwake, halikadhalika njia ya kuelekea upotofu, ufisadi na kushindwa haijafungwa. Wanaadamu wamefikia hatua ambayo kwa mujibu wa maneno ya Qur'ani wanaweza kubeba dhamana ambayo mbingu, ardhi na milima haviwezi kubeba; kwa maneno mengine, wanaweza kuishi maisha huru na wanaweza kuchukua majukumu ya kisheria, kitaalamu na mengineyo. Hii ndio sababu hawana kinga ya makosa, ubinafsi, ujinga na dhulma. Pale Qur'ani inapouelezea uwezo huu wa ajabu wa binadamu, mara moja unamtaja kuwa ni 'dhalimu na mjinga'.

Uwezo na sifa hizi mbili za mwanadamu, uwezo wa kuboreka (kuwa bora zaidi) na uwezo wa kupotoka havitenganishiki. Mwanadamu sio kama mnyama ambaye katika maisha yake ya kijamii, huwa haendi mbele wala nyuma, hageukii kulia wala kushoto. Lakini mwanadamu kwa upande wake, katika maisha yake wakati fulani huenda mbele na wakati fulani nyuma. Katika maisha ya wanadamu kama kuna mwendo na kasi, basi kuna kusimama na kupumzika pia. Kama kuna maendeleo na kubadilika kwenda katika hali bora zaidi basi kuna ufisadi na upotofu pia. Kama kuna haki na wema, basi kuna udhalimu na ushari pia.

Kama elimu na busara vimedhihiri basi ujinga na matamanio duni yamedhihiri pia. Inawezekana kwamba mabadiliko yanayotokea na hali mpya zinazoonekana vikawa ni vya kundi la pili (la mabaya). Wasiotaka kubadilishwa na waliopotoshwa. Ni moja ya tabia za mwanadamu kwamba wakati fulani hufanya jambo kupita kiasi na wakati fulani hufanya jambo kwa kiasi kidogo zaidi kuliko inavyohitajika. Kama akichagua kundi la kati na kati hufanya jitihada kutofautisha kati ya mabadiliko ya aina sahihi na mabadiliko ya aina potofu.

Hujaribu na hufanya jitihada kuusukuma muda mbele kwa msaada wa elimu na ubunifu wake na kujinasibisha na maendeleo huku akijaribu kuudhibiti upotofu na kuepuka kutangamana nao. Lakini kwa bahati mbaya, si mara zote mwanadamu huchagua njia hii. Anaandamwa na magonjwa mawili ya hatari, ugonjwa wa kutotaka kubadilika na ugonjwa wa ujinga. Ugonjwa wa kwanza matokeo yake ni kubaki bila mabadiliko na kujiepusha na maendeleo na matokeo ya ugonjwa wa pili ni upotofu wa kuangamia. Asiyetaka kubadilika huchukia kila jambo jipya na hawezi kuafikiana na kitu chochote isipokuwa cha zamani.

Kwa upande wa pili, limbukeni huona kila kitu kipya kuwa ni cha kisasa na maendeleo na hukiaona kuwa ndio hitajio la wakati. Kwa yule asiyetaka mabadiliko (rigid) kila maendeleo mapya kwake anaona ni ufisadi na upotofu wakati limbukeni anaona mambo yote mapya bila kubagua yote yana maana kupanuka kwa utamaduni na elimu. Asiyetaka mabadiliko hatofautishi kati ya pumba na kiini safi na kati ya njia na malengo. Kwa maoni yake kazi ya dini ni kuhifadhi yale yote ya kale na kuukuu hata kama hayatumiki.

Anafikiri kuwa Qur'ani iliteremshwa ili kudhibiti mwendo wa wakati na kuibakiza hali ya dunia iwe vile vile siku zote. Kwa mujibu wa mtazamo huu, mila za zamani na zilizopitwa na wakati, kama vile kuanza kusoma Qur'ani kuanzia mwisho, kuandikia kalamu za matete na wino wa kuchovya kunawia kwenye beseni la kituruki; kula kwa mikono, kutumia taa ya mafuta ya taa na kubakia bila ya kujua kusoma na kuandika ni mambo ya kidini ambayo lazima yahifadhiwe na kudumishwa. Kwa upande mwingine limbukeni huelekeza macho yake yote nchi za Magharibi ili aweze kuiga mtindo wowote mpya utakaotokea na kila mila mpya. Huiita hali hii kuwa ni kisasa na jambo la lazima kufuatwa lililoletwa na wakati. Wote wawili, wasiotaka mabadiliko na waliopotoka (wajinga) wanaamini kuwa mila na desturi zote za zamani ni kanuni/matendo ya kidini, tofauti ni kuwa asiyetaka mabadiliko anataka kuzihifadhi wakati mjinga anaona kuwa dini ni sawa na kudorora (bila mabadiliko yoyote).

Katika karne chache zilizopita suala la migongano kati ya dini na sayansi limekuwa likibishaniwa sana miongini mwa watu wa nchi za Magharibi. Wazo la migongano liliibuka kutokana na mambo mawili. Kwanza kanisa lilikuwa limezikubali baadhi ya dhana za kisayansi na kifalfasa kuwa ni imani za kidini, lakini maendeleo ya sayansi yakathibitisha uongo wa dhana hizo. Pili, sayansi imebadilisha muundo na hali za maisha. Wale wasiotaka mabadiliko, ambao wana muonekano wa kushika dini, wanataka kuufanya muonekano wa nje wa maisha ya kimaada kuwa sehemu ya dini, kama tu, bila ulazima wowote walivyoyapa sura ya kidini baadhi ya masuala ya kifalsafa.

Limbukeni nao wanaamini kuwa dini imeamuru muundo fulani wa maisha ya kimaada, na kwa vile sayansi imeamuru kuwepo kwa mabadiliko katika muundo huu, dini inapaswa kutupiliwa mbali. Kupinga mabadiliko kwa kundi moja, na ujinga wa kundi jingine, kumezua wazo la kubuni la mgogoro kati ya sayansi na dini. Hadith ya mafumbo katika Qur'ani Uislamu ni dini ya kimaendeleo na inataka wafuasi wake waendelee. Qur'ani imetumia hadith ya mafumbo (yenye mafundisho) kuwashawishi Waislamu wasonge mbele, chini ya nuru ya Qur'ani. Inasema kuwa wafuasi wa Mtume Muhammad(s.a.w.w) ni kama mbegu iliyopandwa katika ardhi. Kwanza matawi yake hutokeza kama majani laini ya mbegu. Kisha hukua na kuimarika sana kiasi cha kuweza kusimama katika kikonyo chake. Hakua haraka mno kiasi cha kuwashangaza sana wakulima.

Huu ni mfano wa jamii ambayo Qur'ani inaukusudia. Qur'ani inachokikusudia ni kukua. Qur'ani inataka kuweka msingi wa jamii ambayo mara zote itakuwa ikikua, ikiendelea na kupanuka. Will Durant anasema hakuna dini iliyowataka wafuasi wake kuwa na nguvu kama Uislamu ulivyofanya. Historia ya Uislamu wa awali inaonyesha ni kiasi gani Uislamu ulivyo na nguvu ya kuijenga upya jamii na kuisukuma mbele kimaendeleo. Uislamu unapingana na vyote viwili kutaka mabadiliko na ulimbukeni (ujinga) na unaviona vyote hivi viwili kuwa ni hatari. Uchakavu wa kiakili wa wasiotaka mabadiliko na kung'ang'ania kwao mila za zamani ambazo hazina uhusiano wowote na Uislamu, kumetoa kisingizio kwa limbukeni kuuona Uislamu kuwa unapingana na maisha ya kisasa (usasa).

Kwa upande mwingine kufuatana na kuiga mitindo mipya zaidi na namna za maisha za Magharibi kunakofanywa na limbukeni, imani yao kwamba kufuata utaratibu wa Kimagharibi kimwili na kiroho, kukubali kwao tabia, adabu na desturi za Magharibi, na kuiga kibubusa sheria za kiraia na kijamii kutoka katika nchi za Magharibi, kumetoa kisingizio kwa wasiotaka mabadiliko kukitazama kila kitu kipya kwa mashaka na kukiona kama tishio kwa dini yao, uhuru wao na kwa haiba ya kijamii ya jumuiya yao. Kwa sasa, Uislamu unagharamikia makosa ya makundi yote mawili.

Ung'ang'anizi wa wasiotaka mabadiliko umeacha uwanja wazi kwa limbukeni kufanya uharibifu na ujinga wa limbukeni umewafanya wasiotaka mabadiliko kuwa ving'ang'anizi zaidi katika imani zao. Inashangaza kuona kuwa hawa wanaojiita wameelimika na kustaarabika ingawa kiuhalisia ni watu wajinga, wanafikiri kuwa muda ni maasumu (haubebi dhambi). Ukweli ni kuwa mabadiliko yote yanaletwa na watu, na mwanadamu sio maasumu hata kidogo (hajaepukana na madhambi). Sasa vipi inaweza kufikirika kuwa mabadiliko ya muda mara zote huwa hayana makosa na matatizo. Kama ilivyo tu kuwa mwanadamu ana matakwa ya kupenda sayansi, maadili, sanaa na dini, na mara zote huchukua hatua mpya kwa maslahi ya wanadamu, pia ana baadhi ya tabia mbaya.

Ni mbinafsi, mwenye uchu wa madaraka na mwenye kupenda raha. Anapenda fedha na unyonyaji kama tu alivyo na uwezo wa kugundua mambo mapya na kutafuta njia bora zaidi za kufanya mambo pia ana dhamana ya kutenda makosa. Lakini limbukeni na waliopotoka hawajui mambo hayo. Wanarudia mahadhi yale yale kuwa ulimwengu wa kisasa upo hivi na vile. Kinachoshangaza zaidi ni kuwa wanalinganisha kanuni za maisha na vitu; kama vile viatu, kofia na gauni. Kwa vile vitu hivi hutafutwa na kuhitajika vinapokuwa vipya na kutupwa vinapochakaa, halikadhalika kwa mujibu wao, hali iwe hivyo hivyo kwa ukweli usiobadilika. Kwao, kizuri na kibaya havina maana zaidi ya kipya na cha zamani.

Ukabaila ni mbaya kwa sababu tu ni mfumo wa zamani na umepitwa na wakati. Vinginevyo ulikuwa mzuri kabisa wakati unaanzishwa duniani kwa mara ya kwanza. Halikadhalika unyonyaji wa wanawake ni mbaya tu kwa vile haupendwi na ulimwengu wa kisasa; vinginevyo hadi hivi majuzi, watu hawa hawa walikuwa hawampi mgao wa urithi. Walikuwa hawajaitambua haki yake ya kumiliki mali na walikuwa hawaheshimu ridhaa na maoni yake.

Kwa mujibu wa watu hawa, katika zama hizi, zikiwa ni zama za anga (kuruka na ndege n.k), kama ilivyokuwa tu haiwezekani kusafiri kwa punda na kuacha ndege, kuwasha kibatari na kuacha umeme, kushona nguo kwa mkono na kuandika kwa mkono huku ukiacha mashine kubwa za kisasa za kuchapishia, halikadhalika haiwezekani kuacha kwenda kwenye sherehe za muziki, sherehe ambazo watu wanavaa mavazi ya kuogelea, mialiko ya chakula cha usiku chenye nyama za kubanikwa, kutoshiriki katika vicheko vya ovyo, kutocheza karata, kutovaa visketi vifupu kwani vitu vyote hivi ni mitindo ya karne hii. Wanahofu kuwa wasiposhiriki katika mambo haya watarudi nyuma katika zama za kuendesha farasi. Wanadai kuwa hizi ni zama za nyukilia, zama za sayansi, zama za miezi ya kubuni na zama za makombora ya masafa marefu.

Hili ni jambo zuri! Sisi pia tunamshukuru Mungu kuwa tunaishi katika zama hizi na tunaomba kwamba tufurahie na kufaidika na sayansi na viwanda kwa kiwango cha juu kabisa. Lakini je, mambo yote haya yanasababishwa na sayansi tu? Je, hali zote za karne hii ni matokeo ya maendeleo ya kisasa ya sayansi? Je, sayansi inadai kuwa imedhibiti mambo yote hapa duniani? Sayansi haijawahi kudai hivyo hata siku moja.

Balaa la karne yetu ni kuwa kundi la wanasayansi kwa nia njema kabisa, huitumia sayansi kufanya ugunduzi mpya, lakini kundi jingine la wabinafsi na wenye uchu wa madaraka na wanaoabudu fedha huyatumia vibaya matunda ya jasho la wanasayansi ili kuyafikia malengo yao ya kiovu. Sayansi inalalamika kuwa inatumiwa vibaya na wanaadamu wakorofi na hii ndio bahati mbaya ya kizazi chetu. Sayansi inasonga mbele katika fani za fizikia na inagundua sheria za mwanga na kuakisi na kundi la wakorofi na wabinafsi wanaitumia kutengenezea filamu za bluu (ngono) za uharibifu na uovu. Kemia inaendelea na kugundua tabia za vitu mbali mbali na michanganyiko yake.

Baadhi ya watu wanaamua kutumia ugunduzi huu kutengeneza madawa ya kulevya, heroin ambayo ni laana kwa wanaadamu. Sayansi iligundua chanzo kizuri cha nishati ndani ya atom, lakini kabla ya ugunduzi haujatumika kwa manufaa ya wanaadamu, wenye tamaa ya madaraka walifanya haraka kutengeneza bomu la atomiki, na kuwadondoshea watu wasio na hatia. Mapokezi yalipoandaliwa, kwa ajili ya heshima ya Einstein, mwanasayansi mkubwa wa karne ya 20, yeye mwenyewe alipanda juu ya jukwaa na kusema, "Mnampa heshima mtu ambaye amechangia kwa namna fulani kutengenezwa kwa bomu la atomiki?"

Einsten mwenyewe hakutumia elimu yake kutengeneza bomu. Ni wengine waliotumia ugunduzi wake kwa lengo hili. Matumizi ya heroin, mabomu ya atomiki na filamu za matusi (bluu) haviwezi kuhalalishwa eti kwa madai kuwa ni mambo ya karne hii. Ikiwa ndege za kisasa kabisa za mabomu zinatumika kurushia mambomu bora kabisa kwa watu wa nchi nyingine, na watu walioelimika sana wanaajiriwa kufanya kazi hii, je, usasa huu unaweza kupuguza ushenzi wa kurithi wa tendo hili?

4

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

- III UISLAMU NA USASA

Hoja kuu ya wale ambao wanasema kuwa katika masuala ya haki za kifamilia tunapaswa kufuata mfumo wa Kimagharibi, ni kuwa muda umebadilika na mahitaji ya karne hii yanatutaka tufanye hivyo. Tunaonelea kuwa ni vizuri tuyaweke maoni yetu wazi juu ya nukta hii, kwa sababu bila kufanya hivyo, mjadala juu ya nukta yoyote hautakuwa kamili, ingawa kwa sababu ya uchache wa nafasi haiwezekani kulijadili suala hili kwa mitazamo yake yote, kifalsafa, kisheria, kijamii na kimaadili. Itatosheleza hapa kujadili nukta mbili tu. Nukta ya kwanza ni kwamba kuafikiana kwayo na kukubaliana na mabadiliko ya wakati sio suala rahisi sana kama baadhi ya watu wasiojua wanavyofikiri. Mabadiliko yanayoletwa na wakati, wakati fulani huwa ni ya kurudisha maendeleo nyuma.

Tunapaswa kwenda na mabadiliko ya wakati ya kimaendeleo na tunapaswa kuyapiga vita mabadiliko yanayoletwa na wakati ambayo ni ya kiharibifu. Ili kutofautisha aina hizi mbili za mabadiliko na kujua asili yake, tunapaswa kujua chanzo cha maendeleo (ugunduzi au mabadiliko) haya mapya na yameelekezwa katika mwelekeo gani. Tunapaswa kuangalia ni tabia gani za kibinadamu zimeyaleta (njema au mbaya) na ni matabaka gani ya watu yanatetea mambo haya mapya?

Tunapaswa kuangalia je yameletwa na tabia tukufu za mwanadamu au matamanio duni yanayofanana na wanyama, na kama yamekuja kama matokeo ya uchunguzi usio wa kibinafsi wa wanazuoni na wasomi, au yameletwa na matamanio duni ya wanaotumikia nafsi zao na tabia za kifisadi za jamii.

MNYAMBULIKO WA SHERIA ZA KIISLAMU

Nukta ya pili inayofaa kuwekwa wazi ni kuwa baadhi ya wasomi wa kiislamu wanaamini kuwa Uislamu una uwezo na sifa ambazo zinaupa uwezo wa kutumika zama zote. Kwa mujibu wa wasomi hawa, mafundisho ya Uislamu yanaafikiana na maendeleo ya wakati, kupanuka kwa utamaduni na matokeo ya mabadiliko haya. Hebu tuangalie asili, sifa na uwezo huu ambao Uislamu unao. Kwa maneno mengine hebu tuangalie ni vifaa gani vimewekwa katika jengo hili la dini, na ikiwa vimeipa sifa ya kuafikiana na hali zote zinazobadilika, bila kuwa na haja ya kuacha baadhi ya mafundisho yake na bila mgogoro wowote kati ya mafundisho yake na hali yoyote inayojitokeza ya kupanuka kwa elimu na ustaarabu.

Ingawa suala hili lina sura ya kiufundi, ili kuondoa shaka shaka ya wale wanaotilia shaka ukweli huu kuwa Uislamu una sifa hii, tunalielezea kwa kifupi hapa. Kwa undani zaidi juu ya suala hili, wasomaji wanaweza kusoma kitabu kiitwacho 'Tanbihul Ummah' cha hayati Ayatullah Naini au kitabu kingine kiitacho 'Marjaiyyat Wal Imamat cha mwanazuoni mkubwa wa zama hizi Allamah Tabatabai. Lakini vitabu vyote hivi vipo katika lugha ya kifursi. Kuna nukta nyingi, ambazo zinaunda siri ya Uislamu kuwa na uwezo wa kuafikiana na kupanuka kwa elimu na ustaarabu, na uwezo wa kutumika kwa sheria zake thabiti na imara katika hali mbali mbali za maisha. Hapa tutataja baadhi yake.

Msisitizo katika roho na kutojali sana kiwiliwili. Uislamu haujashughulikia maisha ya nje (kimwili) tu ambayo hutegemea kiwango cha maendeleo ya elimu ya mwanadamu. Mafundisho ya Uislamu hushughulikia roho pia na malengo ya maisha na hutoa njia bora kabisa ya kuyafikia malengo haya. Sayansi haijabadilisha roho na malengo ya maisha wala haijapendekeza njia yoyote nzuri zaidi, fupi zaidi na salama zaidi ya kuyafikia malengo haya. Imetoa tu njia bora zaidi na vifaa vya kukwamisha njia ya kuyafikia malengo haya. Uislamu, kwa kuhifadhi malengo tu katika himaya yake na kuacha muundo na mbinu kwenye himaya ya sayansi na teknolojia, umeepuka migongano dhidi ya utamaduni na ustaarabu.

Sio hivyo tu lakini pia kwa kuhimiza mambo yanayosaidia kupanuka kwa ustaarabu, yaani elimu, kazi, uchamungu, ridhaa, ujasiri na uvumilivu bila kukata tamaa, umejitolea kuwa kigezo kikuu cha kupanua ustaarabu. Uislamu umeweka alama za barabarani katika njia yote ya maendeleo ya mwanadamu. Alama hizi kwa upande mmoja zinaonyesha njia na kituo cha mwisho na kwa upande wa pili zinaonyesha makorongo na sehemu za hatari. Sheria zote za Kiislamu ni alama za barabara, aidha za aina ya kwanza au ya pili. Njia za maisha katika zama hutegemea juu ya kiwango cha elimu ya wanaadamu.

Kwa kadri elimu ya watu inavyopanuka, ndivyo njia bora zaidi za kujipatia kipato zinavyotokea na moja kwa moja zinachukua nafasi ya zile njia duni (za zamani). Mifumo ya nje na ya kimaada ya njia hizi (za kupatia riziki) haina utakatifu katika Uislamu, na Waislamu hawalazimiki kuzidumisha. Uislamu haujasema kifaa hiki na kile kitumike kwa ushonaji, ususi, kilimo, usafiri, vita au kazi nyingine. Hivyo hapawezi kuwa mgogoro wowote kati ya sayansi na Uislamu, pindi kifaa kinapopitiwa na wakati, cha kisasa zaidi kinaweza kutumika badala yake.

Uislamu haujaagiza kutumika kwa mtindo maalum ya viatu au nguo, wala haujapendekeza aina fulani ya ujenzi wa majengo. Halikadhalika hauhimizi juu ya mbinu fulani fulani za uzalishaji na ugavi. Hii ni moja ya sifa hizo za Uislamu, ambazo zimeuwezesha kuweza kutumika katika maendeleo yote ya wakati. Sheria madhubuti kwa mahitaji madhubuti na sheria zinazobadilika kwa mahitaji yanayobadilika. Sifa nyingine ya Uislamu, ambayo ina umuhimu mkubwa ni kuwa umeweka sheria madhubuti (zisizobadilika) kwa ajili ya mahitaji madhubuti (yasiyobadilika) na sheria zinazobadilika kwa mahitaji yanayobadilika. Mbali na mahitaji ya wanaadamu, mahitaji ya mtu mmoja mmoja na vikundi, yote yana asili ya kudumu.

Hayabadiliki kwa mujibu wa wakati. Kanuni za mifumo inayotawala silika za binadamu na mahusiano ya kijamii hazibadiliki. Tunazijua nadharia za 'Maadili husianishi' na 'Uadilifu husianishi' ambazo zina wafuasi wake, na tutatoa maoni yetu kuhusiana nao baadaye. Sehemu nyingine ya mahitaji ya mwanadamu ni ile ya mahitaji yanayobadilika, na hii huhitaji sheria zinazobadilika. Uislamu ulishayaona mahitaji hayo na umeyaunganisha na kanuni fulani ambazo zina sheria ndogo zinazobadilika kila hali inapobadilika. Kufafanua nukta hii hebu tuangalie mifano hii;'Andaeni majeshi kwa ajili yao (maadui)' (Suratul Anfal 8:60.) Wakati huo huo tunasoma hadith kadhaa za Mtume katika vitabu vya sheria za Kiislamu chini ya kichwa cha habari 'Kuendesha farasi na kurusha mishale.' Mtume aliwaelekeza Waislamu wajifunze kuendesha farasi na kurusha mishale na wawafundishe watoto wao pia. Haya yalikuwa ni sehemu ya mafunzo ya Kiislamu katika zama hizo.

Ni dhahiri kabisa hapa kuwa amri ya msingi ni 'Kuandaa majeshi.' Upinde na mshale, jambia na mkuki na farasi sio vya muhimu. Kilicho cha muhimu ni kuwa imara kijeshi dhidi ya maadui. Kuandaa majeshi ni amri ya kudumu ambayo imetokana na hitajio la kudumu. Hata hivyo ulazima wa kupata ujuzi katika kuendesha farasi na kurusha mishale sio wa kudumu, na hubadilika kutokana na wakati.

Kutokana na kubadilika kwa hali, ujuzi wa kufyatua risasi umechukua nafasi ya kurusha mishale. Mfano mwingine ni sheria ya kijamii inayohusu kubadilishana mali, iliyotajwa katika Qur'ani. Uislamu umetambua kanuni ya umiliki wa mali wa mtu binafsi. Hata hivyo umiliki huu unaotambuliwa na Uislamu ni tofauti na ule uliopo katika nchi za kibepari. Tabia ya umiliki wa mali wa watu binafsi katika Uislamu ni kanuni ya kubadilishana. Kwa utaratibu huu Uislamu umeweka sheria fulani.

Mojawapo imeelezwa na Qur'ani Tukufu katika maneno haya'Na msile mali zenu (kila mmoja kula za mwenzake) kwa batili' (Suratul Baqarah, 2:188).

Kwa maneno mengine katika mauzo ya biashara, fedha isitoke mkono mmoja kwenda mwingine isipokuwa kwa kubadilishana na kitu kingine cha halali chenye kuwa na mamlaka ya mwisho juu ya mali hiyo. Imelezwa na kufafanuliwa katika sheria ya Kiislamu mauzo na manunuzi ya vitu fulani yamekatazwa. Vitu hivyo ni pamoja na damu na kinyesi cha binadamu. Sababu ni kuwa vitu hivi havina thamani inayoviwezesha kuhesabika kuwa sehemu ya mali ya mwanadamu. Kanuni hii ni sawa ya mali ya mwanadamu. Kanuni hii ni sawa na ile iliyo katika Aya iliyonukuliwa hapo juu.

Ubatili wa mauzo na manunuzi ya damu na kinyesi cha binaadamu ni sehemu au mfano tu wa matumizi ya kanuni hiyo. Hata kama hakuna ubadilishaji uliofanyika, (wa bidhaa au bidhaa kwa fedha) fedha au mali inayomilikiwa na mtu fulani haiwezi kufujwa au kuliwa bure. Sheria inayokataza kula mali ya mtu mwingine bure (bila kufanya kazi) au kiwizi ni kanuni madhubuti na inatumika zama zote, na imetokana na hitajio la kudumu la jamii.

Lakini kanuni kuwa damu na kinyesi cha binadamu havihesabiki kama mali na haviruhusiwi kuuzwa, inahuisiana na wakati na kiwango cha ustaarabu. Kanuni hii inaweza kubadilishwa kutokana na mabadiliko ya hali, maendeleo ya sayansi na viwanda na uwezekano wa kuzitumia bidhaa hizi katika namna sahihi na yenye manufaa. Mfano mwingine; "Imam Ali(a.s) hakuwahi kuweka dawa kwenye nywele zake hata siku moja, ingawa zilikuwa zimekuwa za mvi katika miaka ya mwisho ya uhai wake.

Siku moja mtu mmoja alimwambia, 'Je Mtume hakuamrisha nywele za mvi ziwekwe dawa?" Ali alijibu 'Ndiyo aliamrisha' Sasa kwa nini huweki dawa kwenye nywele zako? Yule mtu aliuliza. Ali akasema; "Katika wakati ule ambao Mtume alitoa maelekezo haya, idadi ya Waislamu ilikuwa ndogo na kulikuwa wazee wengi waliokuwa wakishiriki vitani. Mtume aliwaamrisha wazipake dawa ili kuficha umri wao halisi, kwani kama adui angeona kuwa anapambana na kundi la wazee tu, hamasa yake ingeongezeka. Kwa kuwa Uislamu umeenea dunia yote, hali imebadilika. Kila mtu yupo huru kupaka dawa nywele zake au kuacha." Kwa maoni ya Imamu Ali, maelekezo ya Mtume hayakuwa ya kudumu wala haikuwa sheria ya kudumu.

Uislamu unajali muonekano wa nje na roho ya ndani pia. Lakini unataka pumba kwa ajili ya punje yenyewe na unataka nguo kwa ajili ya mwili. Suala la kubadilisha herufi Katika siku za hivi karibuni hapa Iran kumekuwa na ubishani juu ya kubadlisha herufi. Suala hili linaweza kuangaliwa katika pande mbili kwa mtazamo wa kanuni za Kiislamu, na kwa sura mbili. Kwanza ni iwapo Uislamu unapendelea herufi fulani na kuzibagua nyingine.

Je Uislamu unaziona herufi za sasa, ambazo ni za Kiarabu, kama zake, na herufi nyinginezo kama zile za kilatini zinazoonekana ni za kigeni? Uislamu ambao ni dini ya ulimwengu mzima unaziona herufi zote duniani kuwa ni sawa. Sura ya pili ni kuwa kiasi gani kubadilika kwa herufi kutachanganya utamaduni wa Taifa la Kiislamu na watu wengine na kutakuwa na madhara gani kwa utamaduni wa taifa hili. Na zaidi ya hayo, katika karne 14 zilizopita, vitabu vya Kiislamu na kisayansi vilivyozalishwa na Irani vimeandikwa katika herufi za sasa (za kiarabu), je kubadilisha herufi si kutazifuta (haribu) kazi zote hizi?

Swali jingine ni, 'Ni akina nani wanaopendekeza mabadiliko haya, na ni akina nani watakaoyatekeleza? Maswali yote haya ni thabiti.' Kuwategemea wengine ndio kumekatazwa, sio kofia ya kizungu Watu kama mimi mara nyingi wanakumbana na maswali, yanayoulizwa kwa dharau au kejeli. "Sheria ya Kiislamu inasemaje kuhusu kula ukiwa umesimama?' Ni vipi kuhusu kula kwa kijiko au uma?' Je kuvaa kofia ya kizungu kumekatazwa?' Je kutumia lugha za kigeni kumekatazwa?'" Katika kujibu maswali haya, tunasema kuwa Uislamu haujatoa maelekezo yoyote mahsusi juu ya hili. Uislamu haujawaelekeza wafuasi wake kula kwa mkono au kijiko. Ulichowaelekeza ni kuzingatia usafi.

Uislamu haujaelekeza matumizi ya mitindo ya aina fulani ya viatu, kofia au nguo. Kwa mtazamo wa Uislamu lugha zote Kiingereza, Kijapani, Kifursi, zina hadhi sawa. Hata hivyo, Uislamu unasema kitu fulani zaidi. Umesema kuwa imekatazwa mtu kupoteza utambulisho wake. Kuwaogopa wengine bila ulazima kumekatazwa, Kuwaiga wengine kumekatazwa, kuchekeshwa na kuvutiwa na wengine kama sungura anavyovutiwa na nyoka, kumekatazwa.

Kumchukulia punda mgeni aliyekufa kuwa ni farasi kumekatazwa. Kuingiza nchini upotofu na ukosefu wa maadili kutoka nje, kwa madai ni mambo ya kisasa ya karne hii, kumekatazwa. Kuamini kuwa Waislamu wanapaswa kufuata mila na utamaduni wa Kimagharibi ndani na nje, kimwili na kiroho, kumekatazwa. Kwenda nchi ya Kimagharibi kwa siku chache na baada ya kurudi, unaanza kutamka maneno yetu kama wao (wazungu) kumekatazwa. Muhimu na muhimu zaidi. Sura nyingine ya Uislamu inayoufanya uende na mahitaji ya wakati ni kukubaliana kwa mafundisho yake na akili/mantiki.

Uislamu umetangaza kuwa sheria zake zimezingatia maslahi makubwa zaidi. Na wakati huo huo, Uislamu wenyewe umetoa madaraja mbali mbali ya umuhimu wa maslahi haya. Hii inarahisisha kazi ya wataalamu wa sheria za Kiislamu katika fani hizo ambapo maslahi tofauti yanaonekana kugongana. Katika hali hizo, Uislamu umewaruhusu wataalamu wa sheria za Kiislamu kupima uzito wa maslahi tofauti, na kuzingatia mwongozo ambao Uislamu wenyewe umetoa, katika kuangalia ni maslahi gani hilo ni muhimu zaidi. Katika fani ya sheria za Kiislamu, hii huitwa suala la "muhimu na muhimu zaidi." Kuna mifano mingi ambapo kanuni hii ya maslahi ya juu na ya juu zaidi imepata kutumika.

Hata hivyo kwa sababu ya uchache wa nafasi, tunairuka sehemu hii Sheria yenye haki ya Turufu. Sifa nyingine ya Uislamu ambayo imeipa dini hii uwezo wa kuhamishika na kutumika katika hali mbali mbali na imeifanya kuwa dini inayoishi na ya kudumu milele ni kuwa ndani yake kuna chombo cha sheria ambacho kazi yake ni kudhibiti na kurekebisha sheria nyingine.

Mafakihi wanaziita kanuni hizi kuwa ni " kanuni za kuongozea." Kanuni ya 'Hakuna madhara' na 'Hakuna hasara' kwamba sheria haitatumika pale ambapo inaweza kusababisha ugumu au madhara kwa maslahi ya mtu asiye na hatia, imeuenea (imeutawala) mfumo mzima wa kisheria. Lengo la kanuni hizi ni kudhibiti na kurekebisha sheria nyingine. Kwa kusema kweli Uislamu umezipa nguvu ya turufu kanuni hizi ambazo hubadilisha kanuni nyingine.

Madaraka ya mtawala Kwa nyongeza kuna mfululizo mwingine wa kanuni za kuweka mambo katika mizania ambazo Mwenyezi Mungu ameipa dini hii ya mwisho. Ayatullah Na'ini na Allamah Tabatabai, juu ya hili, wametegemea madaraka ambayo Uislamu umeipa serikali ongofu ya Kiislamu. Kanuni ya ijtihadi Mshairi na mwanafalsafa wa Kipakistani anasema kuwa Ijtihadi (kuzalisha sheria kutoka vyanzo vyake vya asili) ni nguvu ya hamasa ya Uislamu. Yuko sawa kusema hivyo. Lakini kilicho muhimu zaidi ni kuwa Uislamu una sifa maalum ya kuruhusu Ijtihadi. Hakuna dini nyingine yenye sifa hii katika namna hii hii. Jengo la ndani la Uislamu limejengwa katika namna ambayo kwa msaada wa Ijtihadi, unaweza mara zote kwenda na mahitaji yanayobadilika katika maisha.

Abu Ali Ibn Sina (Avicenna) katika kitabu chake Al-Shifa, ameelezea haja ya Ijtihadi kuwa inatokana na kubadilika kila mara kwa mahitaji. Anasema kuwa hali za maisha mara zote zinabadilika. Matatizo mapya yanaibuka kila mara, lakini misingi ya Uislamu haibadiliki. Hivyo katika hali hii, lazima wawepo watu wanaojua sheria za kiislamu vizuri na mafundisho ya Kiislamu vizuri ili waweze kujibu maswali yote yanayoibuka katika kila zama na hivyo kukidhi mahitaji ya wakati. Katiba ya Iran inaamuru kuwa pawepo chombo cha mujtahidi wasiopungua watano (wanazuoni wakubwa wa Theolojia wanaoweza kufanya ijtihadi) kitakachokuwa kikichunguza sheria zinazopitishwa na serikali kila wakati.

Lengo hapa ni kuwa watu hawa (mujtahidi) kwa vile sio wapinga mabadiliko wala hawapingi maendeleo ya kisasa, wala sio limbukeni wala hawawafuati wengine kibubusa, waangalie na kudhibiti mfumo wa sheria wa nchi. Inapaswa kueleza kuwa ijtihad kwa namna halisi ina maana kubobea na inahitaji uelewa wa ndani sana wa misingi ya Uislamu na nguzo zake na elimu kubwa kabisa ya kanuni za fikihi ya Kiislamu, ambayo si kila mtu aliyesoma Uislamu kwa muda fulani anaweza kudai kuwa mujtahid.

Hapana shaka kuwa hii ni kazi ya umri mzima wa mtu ili kubobea katika kanuni na mafundisho ya Uislamu, na mbali na kipaji, nia na akili, inahitaji pia msaada wa Mungu. Mbali na kubobea (kwenye mchepuo maalum) na Ijtihad, baadhi ya watu wanaweza kupata elimu na kufikia kiasi kwamba maoni yao yanaweza kuchukuliwa kuwa ni fatwa. Historia ya Uislamu inawataja watu hao ambao licha ya elimu yao kubwa na maadili yao ya hali ya juu walikuwa na hadhari kubwa, walipokuwa wakitoa maoni yao, juu ya masuala ya kisheria.

5

6

7

8

9

10

11

12

13