HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU0%

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU Mwandishi:
: AZIZI NJOZI
Kundi: Wanawake

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

Mwandishi: Allamah Shahid Murtaza Mutahhari
: AZIZI NJOZI
Kundi:

Matembeleo: 45197
Pakua: 2960

Maelezo zaidi:

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 33 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 45197 / Pakua: 2960
Kiwango Kiwango Kiwango
HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

Mwandishi:
Swahili

10

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

-II MAHARI NA MATUNZO

Katika sura hii tumeelezea falsafa na asili ya mahari. Tumeonyesha kuwa sheria ya maumbile imeweka mahusiano kati ya jinsia hizi mbili na imeweka majukumu tofauti ya watu wa jinsia hizi mbili katika maisha. Ilionyeshwa pia kuwa mahari ilitokana na hisia za upendo na upole wa mwanaume, na sio kutokana na hisia zake za kutawala na ukatili. jukumu la mwanamke katika jambo hili limetokana na utambuzi wake wa pekee wa kujizuia, (yaani kujizuia kujitoa kirahisi kwa mwanaume) na sio kwa sababu ya udhaifu wowote au kutokuwa na uwezo wowote. Malipo ya mahari ni zana iliyoamuriwa na sheria ya maumbile ili kuonyesha thamani ya mwanamke. Thamani yake ya kimaadili ni kubwa sana kuliko thamani yake ya kimwili.

Mila za kabla ya Uislamu ziliondolewa na Uislamu. Qur'ani iliondoa mila nyingi za Waarabu zilizokuwepo kabla ya Uislamu zilizokuwa zikihusiana na mahari, na ikairejesha mahari katika nafasi yake ya asili na inayostahili. Katika kipindi cha kabla ya Uislamu wazazi walifkiri kuwa mahari ni mali yao wanayopewa kama hadiya ya taabu walizopata katika kumlea na kumkuza msichana. Imetajwa katika Kashshaf (Tafsiri ya Qur'ani inayosikifa sana) n.k kuwa pindi msichana alipozaliwa na mtu alipotoka kumpongeza baba wa msichana huyo basi alitoa pongezi hizo kwa kusema, "Mkoba huu unaonukia uzuri uwe na manufaa kwako", msemo wenye maana, "Mungu ajalie umuozeshe na upokee mahari yake".

Katika kipindi cha kabla ya Uislamu, akina baba au kama wao hawakuwepo makaka, kama walinzi na walezi wa asili wa msichana walimuozesha kwa mwanaume waliyemtaka wao sio ambaye msichana mwenyewe alimtaka. Na wakati huo huo waliona mahari yake kuwa ni mali yao. Wakati mwingine walibadilishana mabinti. Mwanaume alikuwa akimtoa binti yake au dada yake na kumpa mwanaume mwingine kwa matarajio ya yeye pia kupewa binti au dada wa huyo ambaye yeye amemuozesha. Katika ndoa ya aina hii iliyokuwa ikiitwa ndoa ya Shighar, waolewaji wote wawili walikuwa hawapokei mahari yoyote.

Uislamu ulipiga marufuku aina hii ya ndoa. Mtukufu Mtume alisema;"Hakuna Shighar (kubadilishana mabinti au akina dada) katika Uislamu." Kwa mujibu wa desturi ya Kiislamu, sio tu kwamba baba hapaswi kudai chochote katika sehemu ya mahari ya binti yake, lakini pia hairuhusiwi kuingiza katika mkataba wa ndoa sharti la kwamba mbali na mahari, malipo mengine ya ziada yatalipwa kwa baba wa binti.

Kwa maneno mengine, baba haruhusiwi kunufaika kifedha kwa namna yeyote kutokana na ndoa ya binti yake. Uislamu pia ulipiga marufuku mila ambayo ilimlazimisha muoaji kufanya kazi kwa baba mkwe mtarajiwa kama mahari katika kipindi ambacho kulikuwa hakuna fedha. Mila hii haikuja tu kuwepo kwa sababu mababa walitaka kunufaika kupitia kwa mabinti zao. Kulikuwa na sababu nyingine pia, ambazo zilikuwa ndio ada ya zama hizo ambazo kiumuhimu hazikuwa za uonevu.

Hata hivyo, hakuna shaka yeyote juu ya kuwepo kwa mila hii katika zama za kale. Kisa cha Musa na Shu'aib, kilichosimuliwa katika Qur'ani kinaonyesha kuwepo kwa mila hiyo. (Nabii) Musa alipokuwa akitoroka kutoka Misri, alipofika katika kisima cha Madyan aliwahurumia binti zake Shuayb, waliokuwa wamesimama pembeni na kondoo zao na hakuna aliyekuwa akiwajali. Musa aliwachotea maji.

Wasichana wale walimsimulia baba yao kisa hicho (cha kusaidiwa na Nabii Musa) na baba yao alimtuma mmoja wao kwenda kumwita Musa nyumbani kwake. Baada ya kujitambulisha, Shuaib alimwambia Musa; "Ningependa nikuozeshe binti yangu mmoja kwa sharti kwamba utanifanyia kazi kwa miaka minane. Ukipenda unaweza kunifanyia kwa miaka miwili zaidi na hivyo jumla kuwa miaka kumi." Musa aliikubali ofa hiyo na akawa mkwe wa Shuaib.

Mila hiyo ndio ilikuwa utamaduni wa zama hizo. Kulikuwa na sababu mbili zilizosababisha mila hii. Kwanza, fedha hazikuwepo wakati huo na huduma pekee ambayo bwana harusi angeweza kuitoa kwa mke wake au baba mkwe wake ilikuwa ni kuwafanyia kazi. Sababu ya pili ilikuwa ni kuwepo kwa mila ya mahari.

Wanasosholojia wanaamini kuwa mila ya kumpa baba (mkwe) mahari ni moja ya desturi ya zamani sana. Ili kutoa mahari, imma baba mkwe alimpa muoaji kazi za kufanya au alichukua fedha kutoka kwake. Kimsingi alichokichukua kutoka kwa mume wa binti yake ilikuwa ni kwa ajili ya manufaa ya binti yake. Hata hivyo, tayari Uislamu umeshapiga marufuku mila hiyo, na sasa baba wa mwanamke hapaswi kudai chochote katika mahari ya binti yake, hata kama anataka aitumie kwa ajili ya binti yake. Ni mwanamke mwenyewe tu ndiye mwenye haki ya kuitumia apendavyo. Katika zama za kabla ya Uislamu, kulikuwepo mila nyingine pia, ambazo kimsingi zilimnyima mwanamke mahari yake.

Moja ya mila hizo ilikuwa ni kurithi haki za unyumba. Ilikuwa mwanaume akifa, mtoto wake wa kiume au kaka yake alirithi haki za unyumba (yaani alimrithi mke wa marehemu) pamoja na mali za marehemu. Mtoto au kaka wa marehemu alikuwa na haki ya ama kumuozesha mjane kwa mwanaume mwingine na mahari kuichukua yeye au yeye mwenyewe kujitangaza kuwa ni mume wa mjane tena kwa kutumia mahari ile ile aliyoitoa marehemu. Qur'ani Tukufu ilipiga marufuku mila hii pia. Inasema:

"Enyi mlioamini! Sio halali kwenu kuwarithi wanawake kwa nguvu." (Suratul Nisaa; 4:19). Katika Aya nyingine, Qur'ani Tukufu imepiga marufuku kabisa ndoa ya kumuoa mke wa baba (mama wa kambo) hata kama ataridhia. Qur'ani inasema;

"Msiwaoe wanawake waliopata kuolewa na baba zenu." (Suratul Nisa; 4:22).

Qur'ani Tukufu ilipiga marufuku mila zote zilizomnyima mwanamke mahari yake. Moja ya mila hizo ilikuwa ni kwamba mwanaume alipomchoka mke wake, alimtesa kwa matarajio kuwa mwanamke huyo atakubali kupewa talaka kwa sharti la kurudisha mahari yote au nusu aliyopewa. Qur'ani Tukufu inasema;

"Wala msiwazuie wanawake kuolewa ili mpate kuchukua sehemu ya yale mliyowapatia." (Suratul Nisaa, 4:19) 125 Mila nyingine mbaya ilikuwa mwanaume alimuoa mwanamke na hata kulipa mahari kubwa, lakini baada ya kumchoka alikuwa akimchafulia jina lake, kwa kumshutumu kwa uzinifu na kudai arudishiwe mahari yake. Mila hii pia ilipigwa marufuku na Uislamu. Uislamu una mfumo wake wa mahari. Ni kanuni ya Uislamu isiyo na ubishi wowote kuwa mwanaume hana haki yoyote juu ya mali au fedha ya mke wake, wala hana haki ya kumlazimisha kumfanyia chochote.

Mapato ya mke anayefanya kazi hayawezi kutumiwa na mume wake bila ruhusa yake ( ya mke). Katika hili hakuna tofauti kati ya mwanaume na mwanamke. Kinyume na mila ya kikristo iliyoenea huko Ulaya hadi mwanzoni mwa karne ya 20, mwanamke kwa mtazamo wa Uislamu, hayuko chini ya udhibiti wa mume wake katika masuala ya kifedha. Ana uhuru kamili na fedha zake. Ingawa Uislamu umempa mwanamke uhuru kamili wa kiuchumi na umezuia mume wake asimuingilie mke wake katika mali zake bado umebakisha mfumo wa mahari.

Hii inaonyesha kuwa kwa mtazamo wa Uislamu mahari hailipwi kwa mwanamke ili mwanaume aje kunufaika na nishati yake ya mwili au kumnyonya kiuchumi. Uislamu una mfumo wake wa mahari, ambao hautakiwi kuchanganywa na mfumo mwingine wowote. Vipingamizi vinavyotolewa dhidi ya mifumo mingine, havina mwanya wowote katika mfumo wa Kiislamu. Kama ilivyoelezwa katika sura hii, Qur'ani Tukufu imelezea mahari kama, 'hadiya.' Kwa mujibu wa Qur'ani, mahari ni wajibu (lazima). Qur'ani imezingatia kwa uangalifu tabia zote za maumbile ya mwanadamu, na ili kuhakikisha kuwa si mwanaume wala mwanamke anayepewa nafasi ya kusahau majukumu na mchango wao wa asili, imehimiza umuhimu wa kupanga mahari.

Mchango au jukumu la mwanamke ni kuitikia penzi la mwanaume. Ni vizuri ikiwa atampenda mwanaume lakini upendo wake unatakiwa kuwa ni mwitikio wa hatua za mwanzo zilizochkuliwa na mwanaume. Ikiwa atampenda mwanaume ambaye tangiapo hampendi, basi atakumbana na matatizo mengi ikiwa ni pamoja na kushindwa kulimiliki pendo hilo na hili litakuwa ni pigo kubwa sana kwa haiba yake. Lakini ikiwa upendo wake ni mwitikio wa upendo wa mwanaume, hapa kunakuwa hakuna suala la kushindwa au pigo kwa haiba yake.

Je, ni kweli kwamba mwanamke sio mwaminifu, kwamba hana msimamo katika penzi lake, na kwamba hawezi kutumainiwa? Ni kweli na pia sio kweli. Ni kweli kama atakayelianzisha penzi ni mwanamke. Kama yeye ndio wa kwanza kuanguka katika penzi, basi hilo sio la kuaminika. Muda si mrefu atapoteza penzi lake. Lakini sio kweli ikiwa penzi la mwanamke ni mwitikio wa penzi la dhati la mwanaume, katika hali hii, penzi halielekei kudumaa, isipokuwa kama mwanaume mwenywe atapoteza penzi lake kwa mwanamke huyo.

Hapo ndio penzi litadumaa. Hili ndio penzi la asili la mwanamke. Ni kutokana na penzi la aina ya kwanza ambapo mwanamke anabobea katika kutokuwa mwaminifu, na ni kutokana na aina ya pili ya penzi ambalo amepewa katika uaminifu. Ikiwa jamii inataka uimara wa familia, basi haina budi kuifuata Qur'ani ambayo imeweka kanuni tofauti kwa mwanaume na mwanamke. Sheria ya mahari inaafikiana na maumbile, kwa sababu ni ishara kwamba penzi lilianzishwa na mwanaume, na mwanamke aliitikia tu. Mwanaume hutoa zawadi kama ishara ya upendo na heshima kwa mwanamke.

Hivyo sio jambo la maana kuifuta sheria hii ambayo huunda sehemu muhimu ya sheria iliyoundwa na maumbile yenyewe. Kama tulivyoona, Qur'ani Tukufu ilipiga marufuku mila nyingi zilizokuwepo kabla ya Uislamu pamoja na desturi zilizokuwa zinahusiana na mahari, ingawa watu wa zama hizo walikuwa wamezizoea sana. Qur'ani ilichokiamrisha ni tofauti na mila zilizokuwepo katika siku hizo. Hivyo haiwezi ikadaiwa kuwa Qur'ani haijasisitiza kuwepo au kutokuwepo kwa mahari. Ingeweza kuwa ilipiga marufuku kabisa suala la mahari lakini haikuona kuwa ni jambo la busara kufanya hivyo.

Ukosoaji wa wanaopinga kuwepo kwa Mahari Sasa baada ya kuona maoni ya Uislamu juu ya mahari, hebu tuangalie ukosoaji unaotolewa na wale wanaopinga sheria hii ya Uislamu. Mkosoaji mmoja anasema; "Kama ilivyo kwa mtu anavyotumia fedha kupata bustani, nyumba, au farasi, halikadhalika fedha lazima itumike katika kumnunua mwanamke. Na kama ilivyo kuwa bei ya nyumba, bustani au farasi hutegemea ukubwa, uzuri na ubora wa matumizi yake halikadhalika bei ya mwanamke hutegemea uzuri au ubaya wake na mali au umasikini wake. Hio ndio falsafa ya mahari. Hakuna unyumba bila kutoa pesa na kutoa kulipa bei ya manunuzi." Kama ingekuwa ni mila ya Kimagharibi, je, watu wangezusha fitna za chuki dhidi yake? Ikiwa mtu mmoja atampa pesa mtu mwingine, je, hii ina maana kuwa amemnunua? Je mila ya kupeana zawadi ipigwe marufuku?

Qur'ani inaeleza wazi wazi kuwa mahari si chochote zaidi ya zawadi. Na zaidi ya hili Qur'ani imeweka sheria za uchumi ambazo haziruhusu mwanaume kumnyonya mwanamke kiuchumi. Unaweza kusema kuwa wanaume wengi wa Asia wanawanyonya wake zao kiuchumi. Hilo tunakubali. Lakini hakutokani na mahari. Wanaume hawa hawasemi kuwa wanafanya hivyo kwa kuwa waliwalipia wake zao mahari. Kuna sababu nyingine zilizosababisha kuwa mara nyingi wanaume wanawatawala wanawake.

Kwanini sheria ya maumbile ichafuliwe badala ya kuwabadilisha wanaume wanaohusika? Lengo kuu la hoja zote hizi ni kuwafanya watu wa Mashariki wasahau falsafa yao ya maisha na kanuni za kibinadamu, ili waweze kumezwa kirahisi na wageni. Mkosoaji huyu anaendelea kusema kuwa; "Ikiwa kuna usawa kamili wa kiuchumi kati ya mwanaume na mwanamke, hakuna sababu kwanini mwanaume ashikwe shati kumtunza mke wake na kumpatia chakula, mavazi na mahari.

Hapa mwanamke analipwa mara mbili, jambo ambalo mwanaume hajawahi kufikiriwa kufanyiwa." Tukiichambua hoja hii kwa uangalifu, tutaona inamaanisha kuwa katika kipindi ambapo mwanamke hakuwa na haki ya kumiliki mali na hakuwa na uhuru wa kiuchumi, mahari na matunzo vilihalalishwa kwa kiasi fulani.

Lakini katika hali ambazo mwanamke amepewa uhuru wa kiuchumi, kama Uislamu ulivyompa, hakuna uhalali wa kumtunza na kumpa mahari. Mkosoaji huyu anaonekana kuwa na imani potofu kuwa mahari ilikuwa ikilipwa ili kufidia dhulma ya kiuchumi aliyokuwa akifanyiwa mwanamke. Ukweli ni kinyume chake.

Tukiitazama Qur'ani falsafa halisi ya mahari inaweza kuthibitika. Mkosoaji mwingine ameandika; "Kwa vile mwanaume na mwanamke wameumbwa sawa, mmoja kumlipia gharama au kumpa marupurupu mwingine hakuna sababu ya kiakili. Kama ilivyo mwanaume anavyomhitaji mwanamke, halikadhalika ndivyo mwanamke anavyomhitaji mwanaume. Hivyo katika hili wote wawili wanahitajiana.

Hivyo itakuwa sio haki kumuamrisha mmoja wao kulipa gharama za mwenzake. Lakini kwa vile mwanaume alikuwa na haki ya kutoa talaka na mwanamke hakuwa na uhakika wa kuishi na mwanaume huyo kama mume wake katika uhai wake wote, hivyo alipewa haki ya kudai aina fulani ya usalama (kinga) kutoka kwa mwanaume." Anaongeza kuwa; "Katika mazingira ambapo mwanaume hana haki kabisa kutoa talaka, basi hakuna uhalali kabisa wa kuendelea kwa desturi hii." Ni dhahiri kuwa kutokana na tulivyoyasema hoja hizi hazina msingi wowote. Mahari sio bei wala mshahara. Hapana shaka kwamba mwanaume na mwanamke wanahitajiana, lakini nafasi zao hazifanani. Maumbile yamewaweka katika nafasi tofauti.

Pia ni upuuzi kuielezea mahari kuwa ni kinga ya kifedha dhidi ya haki ya talaka, na juu ya hilo, kudai kuwa hii ndio sababu iliyoufanya Uislamu uiamrishe, ni kilele cha upuuzi. Tungependa kuwauliza watu hao kuwa kwanini awali Uislamu ulimpa mwanaume haki ya kutoa talaka? Kama haki hii ya talaka isingekuwepo je kusingekuwa na haja ya usalama (kinga)? Na zaidi ya haya sentensi hii ina maana kuwa Mtukufu Mtume(s.a.w.w) alipopanga mahari kwa ajili ya wake zake wenyewe, alikuwa na nia ya kuwapa kinga dhidi yake mwenyewe.

Halikadhalika alipopanga mahari ya Bibi Fatima wakati wa ndoa yake kwa Imam Ali alifanya hivyo kwa sababu alitaka kuweka kinga kwa bibi Fatima dhidi ya Imam Ali. Ikiwa, kwa ajili ya kujenga hoja tu, tutakubali kuwa mahari ni aina ya kinga, sasa swali linaloibuka ni kuwa, kwa nini Mtume(s.a.w.w.) aliwashauri wanawake kusamehe mahari yao kwa waume zao kama ishara ya wema. Kwa nini alikielezea kitendo hicho kuwa ni cha heri na kina thawabu nyingi?

Kwa nini alihimiza kuwa mahari iwe ndogo kwa kadiri inavyowezekana? Je hii haionyeshi kuwa Mtume aliichukulia mahari kuwa ni zawadi na alichukulia kuwa kuisamehe ilikuwa ni njia ya kuimarisha mapenzi baina ya mume na mke? Kama Uislamu uliitazama mahari kuwa ni kinga, kwa nini basi Qur'ani inasema:"Wapeni wanawake mahari yao kama hadiya; kwa nini haikusema wapeni wanawake mahari yao kama kinga."

Aidha, inaonekana kuwa mkosoaji huyu ana imani potofu kuwa, katika siku za awali za Uislamu, mahari ilikuwa na muundo sawa na wa sasa.

Hivi sasa utaratibu uliozoeleka ni kuwa hulipa kiasi fulani cha mahari, lakini mke huwa hapati mahari yote, isipokuwa kunapokuwa na ubishani. Aina hii ya mahari huchukua sura ya kinga. Lakini katika kipindi cha awali cha Uislamu, utaratibu ulikuwa ni kulipa fedha ya mahari yote iliyokubaliwa. Katika mazingira haya haiwezi kudaiwa kuwa mahari ni mfumo fulani wa kinga.

Historia inaonyesha kuwa Mtume Mtukufu hakuwa akikubali kufungisha ndoa yoyote bila mahari kupangwa. Kisa kifuatacho kilichotajwa katika vitabu vya Shia na Sunni ni mfano wa desturi ya Mtume: Mwanamke alikuja kwa Mtume akasema;"Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Nikubali niwe mke wako." Mtume Mtukufu alinyamaza kimya na hakusema kitu. Mwanamke alikaa chini. Mmoja wa masahaba wa Mtume aliinuka na kusema; "Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Kama hauko tayari, mimi niko tayari kumuoa." Mtume akauliza ni mahari gani utakayotoa?" "Sina kitu."

Mtume akasema:"hiyo haitafaa. Nenda nyumbani kwako. Labda unaweza kupata kitu cha kumpa mwanamke huyu kama mahari yake. Mwanamume yule alienda kwenye nyumba yake. Mara akarudi na kusema; "Sikupata chochote." Mtume akasema nenda tena ukatafute, hata pete ya chuma itafaa." Mwanaume yule alienda tena. Alirudi na kusema kuwa hakuweza kupata pete ya chuma. Alisema kuwa alikuwa tayari kutoa nguo alizovaa kama mahari kwa mwanamke yule. Mmoja wa masahaba wa Mtume, aliyekuwa akimjua mtu huyo vizuri, alisema kuwa anafahamu kuwa mtu huyo alikuwa hana nguo nyingine.

Hivyo alimuomba Mtume ampangie zile zile nguo alizovaa ndio ziwe mahari ya mwanamke huyo. Mtume alisema; "Ikiwa nusu ya nguo zake zitapangwa kuwa mahari nani atakayezivaa? Yeyote kati ya hawa wawili atakayevaa nguo hizi atamuacha mwenzake bila nguo. Hilo haliwezekani." Mchumbiaji alikuwa amekaa kwenye sehemu yake. Mwanamke pia alikuwa akisubiri uamuzi wa mwisho. Wakati huo, Mtume na masahaba wake wengine walikuwa wamejishughulisha katika kuzungumza juu ya jambo jingine. Muda mrefu ulipopita, mwanaume yule aliinuka ili aondoke. Mtukufu Mtume alimwita kwa kumwambia, "'Njoo hapa' Akaja.

Mtume akamuliza"Unaikumbuka Qur'ani? "Ndiyo ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu!" Ninaikumbuka sura hii na ile." "Je unaweza kuzisoma kutoka kichwani (bila kitabu)?" "Ndiyo, ninaweza" Mtume akasema; "Vizuri sana. Sasa ni sawa. Ninakuozesha mwanamke huyu na mahari yake ni kuwa umfundishe Qur'ani." Mwanaume yule aliushika mkono wa mwanamke yule na wote wawili wakaondoka! Kuna nukta nyingine, pia zinazohusiana na suala la mahari kwa sasa tunaziacha.

11

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

-III MAHARI NA MATUNZO

Tumeelezea mtazamo wa Uislamu juu ya mahari na falsafa yake. Sasa hebu tuliangalie suala la matunzo. Lazima ieleweke kuwa kama ilivyo kwa mahari, matunzo pia yana muundo wake katika sheria ya Kiislamu na isichanganywe au kufananishwa na utaratibu wa wasiokuwa Waislamu. Kama Uislamu ungemruhusu mwanaume amtumikishe mwanamke na yeye mwanaume achukue mapato ya jasho la mke wake, sababu ya kwa nini mume anapaswa kutoa matunzo kwa mke wake ingekuwa dhahiri, kwani ni wazi kuwa ikiwa mtu anamyonya mtu (au mnyama) mwingine kiuchumi ni lazima amgharamie gharama zote za maisha yake (maisha ya huyo anayenyonywa). Ikiwa mfugaji hatamlisha farasi wake, basi farasi huyo hatambebea mizigo. Lakini Uislamu haujamruhusu mwanaume kumnyonya mwanamke.

Kwa upande mwingine mwanamke ana haki ya kumiliki mali na kujipatia fedha, na mume hana haki ya kutenga mikono kwa kile alichojichumia mwanamke. Na wakati huo huo ni wajibu wa mume kubeba gharama zote za matunzo ya familia. Anapaswa kumtunza mkewe, watoto wake pamoja na wafanyakazi wa ndani na kununua vyombo vya ndani n.k. kwa sababu gani? Kwa bahati mbaya, watu wenye akili za Kimagharibi hawako tayari kufikiri hata kidogo juu ya vitu hivi. Wanarudia maoni yale yale ya chuki dhidi ya muktadha wa sheria ya Kiislamu, ambayo wazungu wanayatumia kuhalalishia mfumo wao wa kisheria.

Ni sawa kusema kuwa matunzo kwa mke katika nchi za Magharibi, hadi kufika karne ya 19, ilikuwa ni ishara ya utumwa wa mwanamke, kwa sababu huko mwanamke alipaswa kuendesha kazi zote za ndani za nyumba ya mumewe bure tena bila kuwa na haki ya kumiliki chochote. Ni dhahiri kuwa chakula, mavazi, n.k alivyokuwa akipewa mwanamke havikuwa na tofauti na mgao wa kila siku wa mfungwa au mgao wa chakula anachopewa mnyama mbeba mizigo. Lakini suala la Uislamu ni tofauti kabisa.

Ni mfumo wa kipekee duniani ambao humuondoa mwanamke katika majukumu ya kuendesha maisha ya familia ya mwanaume, humpa uhuru kamili wa kiuchumi na wakati huo huo humuondoa katika kuchangia chochote katika bajeti ya familia. Hapa tuna falsafa tofauti ambayo inahitaji maelezo yetu maalumu. Kumuweka mwanamke wa kizungu katika kizuizi hadi katika nusu ya karne ya 19. Dr. Shayagan anasema; "Uhuru wa kiuchumi wa mwanamke ambao umetambuliwa na sheria ya Shia toka awali kabisa, haukuwepo Ugiriki (Uyunani), Urumi na Japan hadi hivi karibuni katika nchi zilizo nyingi. Mwanamke kama mtu mdogo tu na kichaa alizuiwa kuingia katika malipo yoyote ambayo yangesababisha yeye kumiliki mali. Huko Uingereza ambako mwanamke alionekana kuwa si mtu kamili bali ni sehemu ya mume wake, sheria mbili zilipitishwa, moja mwaka 1870, na nyingine mwaka 1882, ambazo ziliondoa kizuizi hicho cha mwanamke kumiliki mali.

Huko Italia, sheria ilipitishwa mwaka 1919 ili kuondoa kizuizi dhidi ya mwanamke. Sheria ya kiraia ya mwaka wa 1900 nchini Ujerumani na ile ya Uswisi ya mwaka 1907 zilimpa mwanamke haki sawa na zile alizokuwanazo mwanaume. Hata hivyo, Wareno na Wafaransa waliendelea kuweka kizuizi kwa wanawake walioolewa kumiliki mali katika sheria zao hadi mwaka 1938 ambapo Ufaransa ilibadilisha sheria yake kwa kiasi fulani.

Kama ulivyoona ni karne moja tu imepita tangu sheria ya kwanza ya uhuru wa kiuchumi wa mwanamke ilipopitishwa huko Uingereza mwaka wa 1882 na hicho kilichoitwa kizuizi kwa mwanamke aliyeolewa kiliondolewa. Kwa nini Ulaya ilimpa mwanamke uhuru wa kiuchumi ghafla? Sasa hebu tuangalie nini kilitokea katika karne iliyopita kiasi cha tukio hili muhimu kutokea? Je, utambuzi wa wazungu uliamka ghafla na hivyo kuwafanya watambue udhalimu wa nyendo zao? Will Durant katika kitabu chake, 'Pleasure of Philosophy" anajibu swali hili.

Humo tunakutana na ukweli wa kushtusha. Tunagundua kuwa mwanamke wa kizungu kwa kusema kweli anapaswa kuzishukuru mashine na siyo mtu yeyote kwa ukombozi alioupata pamoja na haki ya kumiliki mali. Anapaswa kulishukuru Bunge la Uingereza kwa kupitisha sheria ya uhuru wa kiuchumi wa mwanamke na sio wamiliki wa viwanda waliotaka kupata faida zaidi kwa kulipa mishahara midogo. Will Durant anasema; "Mabadiliko ya haraka katika tabia na mila, kongwe zaidi kuliko historia ya Ukristo, yanaelezewa na uwingi na aina tofauti tofauti za mashine.

Ukombozi wa mwanamke ni matokeo ya mapinduzi ya viwanda." Katika karne moja iliyopita ilikuwa ni vigumu sana kwa wanaume wa Uingereza kupata kazi. Lakini matangazo ya biashara yaliwataka wao wawapeleke wake zao na watoto viwandani. Waajiri walikuwa na shida ya faida viwandani na mgao, na hawakushughulishwa na maadili. Walikuwa ni mabepari wamiliki wa viwanda wa karne ya 19 ambao bila kujua walikula njama ya kuvuruga maisha ya familia ya watu. Hatua ya kwanza ya kuwakomboa bibi zetu ilikuwa ni sheria ya mwaka 1882.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, wanawake wa Uingereza waliweza kufurahia fursa ambayo haikupata kutokea kabla. Walipewa haki ya kukaa na fedha zao wenyewe. Sheria hii iliyokuwa inawakilisha maadili yaliyotukuka ya Kikristo ilipitishwa na wamiliki wa viwanda katika Bunge la Uingereza. Tokea mwaka huo wanawake wamekombolewa kutokana na kazi ngumu za ndani na badala yake wanamenyeka kutokana na sulubu za madukani na viwandani.

Kama unavyoona walikuwa ni wamiliki wa viwanda wa Uingereza ambao kwa ajili ya kutaka faida kubwa zaidi, walichukua hatua hii kwa manufaa ya mwanamke. Qur'ani na Uhuru wa kiuchumi wa mwanamke. Uislamu miaka 1425 iliyopita uliweka sheria hii;"Wanaume wana sehemu ya walichochuma na wanawake wana sehemu ya walichochuma," (Suratul Nisa; 4:32). Katika Aya hii Qur'ani imetambua nyadhifa za wote wawili mwanaume na 135 wanamke juu ya matunda ya jasho lao. Katika sehemu nyingine Qur'ani inasema:"Wanaume wana sehemu ya waliyoyaacha wazazi (wao) na wanawake wana sehemu ya waliyoaacha wazazi (wao)." (Suratul Nisa; 4:7). Aya hii inathibitisha kustahiki kwa mwanamke kupata urithi, jambo ambalo lilikuwa halitambuliwi na Waarabu wa kabla ya Uislamu.

Ulinganishaji Qur'ani Tukufu ilitoa uhuru wa kiuchumi karne 13 kabla ya Ulaya, na kukiwa na tofauti hizi: Sababu zilizoufanya Uislamu utoe uhuru huo wa kiuchumi zilikuwa ni ubinadamu, maadili na maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Hapakuwepo sababu kama vile tamaa ya wenye viwanda wa Uingereza ambao kwa kutaka kujaza matumbo yao, walipitisha sheria na kisha wakapiga kelele kubwa dunia nzima kuwa wamezitambua rasmi haki za wanawake, na kwamba walikuwa wameweka usawa kati ya mwanaume na mwanamke. Uislamu ulitoa haki sawa kwa mwanamke, lakini haukuvuruga msingi wa familia yake, wala haukuwahamasisha wanawake na mabinti kuwaasi waume zao na baba zao. Uislamu ulileta mapinduzi makubwa, lakini ulifanya hivyo kwa utulivu na usalama.

Kwa mujibu wa Will Durant, nchi za Magharibi zilichokifanya ilikuwa ni kumnusuru mwanamke na sulubu za kazi za ndani na badala yake kumtwisha sulubu za madukani na viwandani. Kwa maneno mengine, Ulaya ilimfungua mwanamke pingu moja na kwa kutumia pingu nyingine ikamfunga mikono na miguu. Uislamu ulimuokoa mwanamke kutoka katika utumwa (kwa mwanaume), ndani ya nyumba na shambani, na ulimuondolea mzigo wa kugharamia gharama za familia.

Kwa mujibu wa mtazamo wa Uislamu, mwanamke ana haki ya kuchuma mali (fedha), kuzitunza na kuziendeleza mali zake, lakini wakati huo huo haifai alazimishwe kufanya kazi ngumu ambazo zinaweza kuharibu uzuri na fahari yake. Lakini wapi! cha ajabu ni kuwa macho na masikio ya baadhi ya waandishi wetu yameziba kiasi cha kuwa hawawezi kuzitambua taarifa za kihistoria na ukweli wa kifalsafa. Shutuma za wakosoaji na majibu yetu.

Mwanamke mmoja anaikosoa sheria ya matunzo kwa kusema kuwa sheria hii inamtaka mume atoe chakula, mavazi na malazi kwa mke wake sawa tu na mfugaji anavyopaswa kumpa chakula na malazi mnyama wake. Tungependa kumuuliza mkosoaji huyu ni kwa namna gani amefikia hitimisho kuwa mume anammiliki mke wake au ni namna gani umiliki huu umekuwa sababu ya mwanaume kumtunza mke wake.

Ni umiliki gani huo ambao mmiliki hana haki hata ya kuomba huyo anayemmiliki kumpa glasi ya maji. Ni umiliki gani huo ambao unampa haki mmilikiwa anachokichuma kuwa ni chake mwenyewe na sio cha mmiliki wake? Ni umiliki gani huo ambao anayemilikiwa akipenda anaweza kuomba malipo kutoka kwa mmiliki hata kwa kazi ndogo aliyoifanya? Ni aina gani hii ya umiliki ambapo mmiliki hana haki ya kumzalimisha huyo anayemmiliki hata kumnyonyesha mtoto wake ambaye pia ni mwanaye pia?

Pili, je, ni kweli kwamba mtu ambaye gharama zake zinalipiwa na mtu mwingine huwa mtumwa wa huyo mmiliki? Kwa mujibu wa sheria ya kila nchi ni wajibu wa baba au baba na mama kubeba gharama za watoto wao. Je, inaweza kudaiwa kuwa watoto wanamilikiwa na wazazi? Uislamu umefanya kuwa ni wajibu kwa watoto kuwasaidia wazazi wao pindi wanapohitaji msaada huo. Je hii ina maana kuwa kwa mujibu wa Uislamu, wazazi wanamilikiwa na watoto wao? Aina tatu za matunzo.

Uislamu unazitambua aina tatu za matunzo: Mtu anayemiliki wanyama lazima awatunze. Msingi wa matunzo haya ni umiliki. Mwanaume anapaswa kubeba gharama za watoto wake kama ni wadogo au kama ni maskini. Halikadhalika anapaswa kuwatunza wazazi wake ikiwa wao ni maskini. Msingi wa matunzo haya sio umiliki. Ni haki za asili. Watoto wana haki kwa wazazi wao waliowaleta duniani. Halikadhalika wazazi wana haki kwa watoto wao waliowazaa. Aina hii ya matunzo inakuwepo tu pindi kunapokuwepo na haja (yaani inapokuwa wazazi au watoto ni maskini).

Mume anapaswa kumtunza mke wake. Msingi wa aina hii ya matunzo sio umiliki wala haki za asili kama ilivyo hapo juu. Wala hautegemei uhitaji (wa mke), hali ya uzee au vinginevyo. Hata ikitokea kuwa mke ni milionea mwenye kipato kikubwa na mume wake ana kipato kidogo, bado ni jukumu la mume kubeba gharama za matunzo kwa mke wake. Na sifa ya pekee ya aina hii ya matunzo, tofauti na zile mbili za mwanzo, ni kuwa ina ulazima wa kisheria, yaani mwanaume anaweza kulazimishwa na mahakama kutekeleza jukumu hili. Ni nini msingi wa aina hii ya matunzo? Tutajadili hili katika sura inayofuatia.

Je mwanamke wa kisasa hataki mahari na matunzo? Tumeshaeleza kuwa kwa mtazamo wa Uislamu, ni jukumu la mwanaume kubeba gharama za familia yote ikiwa ni pamoja na za mke wake, mke ambaye yeye hana jukumu kama hili. Hata kama utajiri wa mwanamke ni mkubwa mara nyingi kuliko wa mwanaume, mwanamke halazimiki kuchangia chochote katika bajeti ya familia. Akiamua kuchangia basi ni kwa hiari yake. Kwa upande mwingine, mwanaume analazimika kubeba gharama za mke wake, lakini Uislamu haumruhusu yeye kumnyonya mke wake kiuchumi.

Katika hili matunzo ya mke yanafanana na wazazi, ambayo katika baadhi ya hali, huwa ni wajibu. Lakini mtoto hana haki ya kuwatumikisha wazazi ili apate kuwatunza, jukumu ambalo ni lake. Kulinda maslahi ya kiuchumi ya mwanamke. Uislamu, kwa namna bora isiyo na mfano umeyalinda maslahi ya kiuchumi na kifedha ya mwanamke. Kwa upande mwingine umempa uhuru wa kiuchumi na umemzuia mwanaume kuingilia fedha zake au kuidhibiti mali yake na wakati huo huo umemuondolea jukumu la kusimamia gharama za familia.

Hivyo hana haja ya kukimbizana na fedha. Watu wa Magharibi, ambao wanataka kuikosoa sheria ya matunzo walikosa cha kusema hivyo wakaamua kuzusha uongo mkubwa. Wanasema kuwa falsafa ya matunzo ni kwamba mwanaume hujiona kuwa ni mtawala wa mwanamke na humfanya amtumikie. Kama ilivyo kwa mfugaji anavyopasa kubeba gharama za mnyama wake ili mnyama huyo aendelee kumtumikia ndiyo kwa msingi na lengo hilo hilo kwamba sheria ya matunzo imefanya kuwa ni wajibu kwa mwanaume kutoa japo mkate na siagi kwa mke wake. Kwa kusema kweli, ikiwa mtu anataka kuishambulia sheria ya Kiislamu, anaweza kufanya hivyo kirahisi kwa kulaumu kuwa kwa nini mwanamke amependelewa kiasi hicho na kumtwisha mwanaume mzigo wa majukumu makubwa kiasi hicho, badala ya kuikosoa kwa kutumia jina la kumtetea mwanamke.

Ukweli ni kuwa Uislamu haujakusudia kumpendela mwanaume wala mwanamke. Uislamu haukukusudia mafanikio ya mwanaume na mwanamke peke yao bali hata kwa watoto watakaozaliwa na wanaadamu wote. Uislamu unaamini kuwa njia pekee ya kutoa hakikisho la mafanikio ya mwanaume, mwanamke, watoto wao na wanaadamu wote ni kutopuuza sheria za maumbile na amri za Muumba Mwenye Nguvu Zote. Kama tulivyoonyesha tena na tena, Uislamu umelizingatia hili mara zote kuwa mwanaume ni alama ya kuhitaji, matamanio na kushughulika na mwanamke ni alama ya kutojali. Uislamu umemuonesha mwanaume kama mteja na mwanamke kama mmiliki wa mali.

Kwa mtazamo wa Uislamu, mwanaume anapaswa ajione kama mfadhiliwa na anapaswa awe tayari kubeba gharama zake za msingi. Mwanaume na mwanamke wanapaswa wasisahau kuwa wamepangiwa nafasi tofauti na maumbile katika suala la mapenzi. Ndoa inaweza kuwa imara na ya furaha ikiwa kila mmoja atatekeleza kikamilifu jukumu alilopangiwa na maumbile. Sababu ya pili inayofanya mume awajibike kumtunza mke wake ni kuwa, ni mwanamke anayetaabika na maumivu yote ya uzazi wa mtoto. Mchango wa mwanaume katika hili ni kwa muda mfupi tu na ni yenye kuleta starehe. Ni mwanamke anayestahamili taabu za mimba, kujifungua, kunyonyesha na kulea mtoto. Kazi zote hizi zinatumia nishati (nguvu) yake na kupunguza uwezo wake wa kufanya kazi. Kama itaamuliwa kwamba sheria haitatoa kinga kwa mwanamke na ikaamuru kuwa wote mume na mke wachangie bajeti sawa katika kuendesha familia basi bila shaka mzigo wa mwanamke utakuwa mzito mno. Kama tunavyojua, wale wanyama wanaoishi kwa jozi, mara zote dume hutoa ulizi kwa jike na husaidia jike wakati wa kuzaa kwa kuleta chakula.

Aidha, kutokana na mtazamo wa kiwango cha kufanya kazi na uwezo wa kufanya kazi ngumu na zinazohitaji nguvu nyingi, zenye kuzalisha zaidi na za kiuchumi zaidi, haulingani kati ya mume na mke (sio sawa). Ikiwa mahusiano baina yao yatabadilika na mwanaume akakataa kutoa hata senti kwa ajili ya mkewe, mwanamke hataweza kushindana naye. Isitoshe, mwanamke huhitaji fedha zaidi kuliko mwanaume. Kujipamba na kujirembesha ni sehemu ya maisha ya mwanamke, na moja ya mambo ya lazima kabisa. Fedha anazotumia kujipamba katika maisha yake ya kawaida ni nyingi mno zikilinganishwa na anazotumia mwanaume. Tabia yake ya kujirembesha imemfanya apende aina mbali mbali za manukato.

Kwa mwanaume, suti inaweza kuvaliwa kwa muda wote hadi hapo itakapokwisha, lakini mwanamke huivaa nguo tu pale inapoonyesha upya. Mara nyingi nguo au pambo hupoteza thamani yake baada ya kuvaliwa mara moja tu. Uwezo wa mwanamke wa kuzalisha ni mdogo kuliko wa mwanaume lakini yeye ndiye mwenye matumizi makubwa zaidi. Uwanamke wa mwanamke, yaani uzuri wake, urembo wake, fahari yake na uchangamfu huhitaji raha zaidi na jitihada kidogo.

Ikiwa mazingira yatamlazimisha kufanya kazi kwa bidii na kufanya jitihada mara zote katika kujipatia fedha, fahari yake huondoka/huharibika. Mashaka ya kifedha yatamsabashia makunyazi katika uso wake kama yanavyosababisha katika uso wa mwanaume. Inasikika mara nyingi kwamba wale wanawake maskini wa kimagharibi, wanaolazimika kufanya kazi viwandani au katika karakana ili kujipatia riziki wanatamani kuwa wangeishi maisha ya mwanamke wa Mashariki (Asia). Ni dhahiri kuwa mwanamke ambaye akili yake haijatulia (haijaridhika) hawezi akajitunza vizuri wala hawezi akawa chanzo cha furaha kwa mume wake.

Hivyo sio kwa maslahi ya mwanamke bali kwa maslahi ya mwanaume na familia pia kuwa mwanamke asilazimishwe kubeba mzigo mzito wa kujitafutia riziki yake. Mwanaume pia anataka mazingira ya nyumbani yawe katika hali ambayo yeye atajisikia kupumzika na kusahahu mashaka yake yote. Mazingira kama haya yanaweza kuandaliwa na mwanamke tu, ikiwa yeye mwenyewe hajachoka wala hana mashaka. Ni huzuni iliyoje kwa mwanaume anayekuja nyumbani akiwa amechoka na kumkuta mke wake akiwa amechoka kuliko yeye! Hivyo utulivu wa mwanamke, uzuri na kuridhika kwake ni mambo ya muhimu hata kwa mwanaume pia. Sababu inayowafanya wanaume wawe tayari kuwakabidhi wake zao fedha walizozipata kwa jasho na taabu nyingi na kuwaruhusu wazitumie kwa uhuru na kwa raha zao ni kuwa wanajua kuwa wanawahitaji wake zao kwa ajili ya utulivu wao wa kiakili. Wanafahamu kuwa Mwenyezi Mungu amemfanya mwanamke kuwa chanzo cha furaha na utulivu kwa mwanaume.

Qur'ani inasema:"Yeye ndiye aliyekuumbeni katika nafsi moja na katika (nafsi) hiyo alimuumba mwenzi ili apate utulivu kutoka kwake." (Suratul A'raf, 7:189).

Mwanaume anafahamu kuwa chochote anachotoa ili kumridhisha mke wake, hutoa kwa kupitia mlango wa pili kujihakikishia furaha yake mwenyewe na kung'arisha maisha ya familia yake.

Anajua kuwa ili waridhishane na kupeana utulivu na raha inatakiwa angalau mmoja wao asielemewe na uchovu, na katika mgawanyo huu wa majukumu, ni mwanaume anayefaa zaidi kushiriki katika mapambano ya maisha na mwanamke anafaa zaidi kuchukua nafasi ya mliwazaji. Mwanaume na mwanamke wameumbwa katika namna ambayo mwanamke humtegemea mwanaume kifedha na mwanaume humtegemea mwanamke ili kupata msaada wa kiroho na kimaadili. Mwanamke hawezi kujitosheleza kifedha na kimali bila msaada wa mwanaume na ndio maana Uislamu umemuamrisha mume wake wa halali (mume wa halali tu) kumsaidia mke wake.

Ikiwa mwanamke anataka kuishi kifahari kama anavyotaka basi lazima apate msaada wa mume wake wa ndoa. Vinginevyo itambidi awategemee wanaume wengine, hali ambayo imekuwa ya kawaida kabisa na kwa bahati mbaya inazidi kuongezeka. Propaganda dhidi ya matunzo. Wapotoshaji wa kijinsia wamegundua kuwa ikiwa mahitaji ya kifedha ya mwanamke hayatakidhiwa na mume wake, basi wao wanaweza kumnasa kirahisi.

Hiyo ni moja ya sababu zinazosababisha kuwapo propaganda nyingi dhidi ya mume kumtunza mkewe. Ukichunguza falsafa ya wanawake kulipwa mishahara minono na makampuni ya kibiashara, unaweza kuelewa kirahisi tunachomaanisha. Hakuna shaka yeyote kuwa kufuta mfumo wa mume kumtunza mkewe kutamfanya mwanamke kuwa malaya. Inawezekanaje kwa mwanamke anayejitegemea mwenyewe bila msaada wa mume akakidhi mahitaji yake ya asili yeye mwenyewe?

Wazo hili la kupiga marufuku matunzo ya mume kwa mkewe linaungwa mkono na wanaume waliochoshwa na israfu (ufujaji) wa wake zao. Wanataka kulipiza kisasi kwa wanawake wafujaji na wapenda mitindo kwa ujumla kupitia wanawake wenyewe na kulipa jina (wazo hili) la uhuru na usawa.

Will Durant, baada ya kufafanua maana ya 'neo-marriage' (ndoa mambolea) kama aina ya ndoa ya kisheria yenye uzuiaji mimba wa kisheria, talaka kuhitaji ridhaa ya pande zote mbili, na kutokuwepo na watoto (kutozaa watoto) na kutokuwepo matunzo anasema kuwa, "Wanawake wapenda mitindo wa tabaka la kati punde watasababisha kisasi cha wanaume wachapa kazi kuishia juu ya jinsia yote ya kike. Ndoa itapata mabadiliko makubwa kiasi cha kuwa wanawake wasiokuwa na kazi, ambao ni wapenda mapambo na manukato ghali watatoweka.

Wanaume watawaomba wanawake wabebe gharama zao wenyewe. Ndoa za kirafiki au ndoa mamboleo humtaka mwanamke afanye kazi hadi mimba inapokuwa kubwa kabisa. Kuanzia sasa na kuendelea atapaswa kubeba gharama zake zote yeye mwenyewe na hivyo ukombozi wake utakuwa umekamilika. Mapinduzi ya viwanda yanadhihirisha madhara yake ya kikatili. Mwanamke analazimika kufanya kazi pamoja na mumewe viwandani. Mwanamke, badala ya kukaa chumbani na kumlazimisha mumewe kufanya kazi mara mbili kufidia kutozalisha kwake, atapaswa kuwa sawa na mumewe katika kazi, adhabu, haki na majukumu.

Kisha kwa kejeli, Will Durant anasema; "Hii ndio maana ya ukombozi wa mwanamke." Dola badala ya mume. Ni ukweli usiopingika kuwa kuzaa ni jukumu la asili la mwanamke na kwa sababu hiyo analazimika kumtegemea mwanaume kwa ajili ya msaada wake wa kiuchumi na kifedha. Baadhi ya watu katika Ulaya ya sasa, katika kutetea kwao ukombozi wa mwanamke, wamekwenda mbali zaidi mpaka kufikia kuunga mkono kurejeshwa kwa mfumo jike (matriachal System).

Wanaamini kuwa baada ya mwanamke kupata uhuru kamili na kupata usawa wake na mwanaume katika mambo yote, huko baadaye baba ataonekana kama nyongeza/kiambata kisicho cha lazima na hatimaye ataondolewa katika orodha ya wanafamilia. Wakati huo huo, watu wanatoa wito kwa serikali kuchukua nafasi ya baba na kutoa ruzuku kwa wanawake ambao hawako tayari kubeba mzigo wa kuanzishsa familia peke yao, ili wasiache kuzaa watoto na ili wanaadamu wasitoweke duniani.

Kwa maneno mengine, mwanamke ambaye huko nyuma alikuwa tegemezi na kwa mujibu wa wakosoaji wengine, alikuwa mtumwa wa mwanaume, huko baadaye atakuwa tegemezi na mtumwa wa serikali. Majukumu na haki za baba yatahamishiwa serikalini. Mtu anaweza kutamani kuwa watu hawa ambao wamedhamiria kwa upofu wao kuudondosha muundo huu mtukufu wa familia uliojengwa kwa sheria za Mwenyezi Mungu, laiti wangekaa na kutafakari madhara ya kitendo chao.

Bertrand Russel katika kitabu chake kiitwacho, 'Marriage and morals' (Ndoa na maadili) anajadili suala la uingiliaji wa serikali kiutamaduni na kiafya katika suala la watoto, anasema: "Inavyoonekana baba anapoteza umuhimu wake kama sababu ya kibaiolojia. Sababu nyingine yenye nguvu inayomuondoa katika nafasi yake ni mwelekeo wa wanawake katika uhuru wa kiuchumi. Wanawake wanaoshiriki kupiga kura, wengi wao hawajaolewa. Wanawake walioolewa wana matatizo zaidi kuliko wale ambao bado hawajaolewa licha ya kinga ya kisheria bado wako nyuma katika kufanikiwa kupata kazi.

Ikiwa wanawake walioolewa wanataka kudumisha uhuru wao wa kiuchumi, wanapaswa kuchagua moja kati ya haya mawili, ama washikilie kazi zao na kuacha jukumu la malezi ya watoto kwa mayaya wanaolipwa, au kupokea ruzuku wanayolipwa na serikali ili kuwawezesha kuwatunza watoto wao na wao wenyewe. Katika chaguo la kwanza, idadi ya vituo vya kulelea watoto wachanga na chekechea itaongezeka sana, na kwa mtazamo wa kisaikoloji, madhara ya asili ya hali hii yatakuwa kwamba watoto hawa hawatatambua kuwepo kwa baba wala mama.

Chaguo la pili peke yake halitoshi. Lazima liongezewe nguvu ya kisheria ya kuwaajiri tena kwa lazima akina mama, umri wa watoto wao unapofika umri fulani. Njia hii ina faida moja. Mwanamke anaweza kumlea mtoto wake mwenyewe bila kumtegemea mwanaume. Ikiwa sheria hii itapitihswa, itatupasa tusubiri kuona matokeo yake katika maadili ya familia.

Inawezekana sheria ikaamua kuwa mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa hana haki ya kupata ruzuku au ikiwa kuna dalili kuwa mama alizini, ruzuku hiyo atapewa baba wa mtoto. Katika hali hii polisi wa kila eneo watapaswa kuwachunguza wanawake ambao hawajaolewa. Matokeo ya sheria hii hayatakuwa mazuri sana na yanaweza kuwafadhaisha wazazi (waliozini na kuzaa). Kwa sababu licha ya kinga ya kisheria, bado wazo la polisi kuwachunguza wanawake ambao hawajaolewa litaachwa na ruzuku itatolewa hata kwa akina mama waliozaa watoto nje ya ndoa.

Katika hali hii, jukumu la kiuchumi la baba litatoweka kabisa miongoni mwa wafanya kazi na umuhimu wake kwa watoto wake hautakuwa zaidi ya ule wa mbwa au paka Ustaarabu kwa jumla au huu ustaarabu ambao kwa sasa hivi umezuka unaelekea kuzidhoofisha hisia z a kimama.

Ili kuulinda ustaarabu huu, ambao tayari umeshaendelea sana, inaweza kuonekana kuwa ni muhimu kuwapa wanawake fedha nyingi ili waone kuwa mimba zina faida. Katika hali hii, haitakuwa muhimu au lazima kwa wanawake wote kuzaa. Itakuwa ni kazi ya kitaalamu kama kazi nyingine na itachaguliwa na wanawake kwa sifa zao. Lakini zote hizi ni dhana.

Tunachomaanisha ni kuwa harakati za ukombozi wa wanawake zinasababisha kuporomoka kwa mfumo dume (patriarchy system), ambao toka zama za kabla ya kuandikwa kwa historia, ulikuwa ni alama ya ushindi wa mwanaume dhidi ya mwanamke. Katika nchi za Magharibi inaaminika kuwa ni alama ya ustaarabu kuwa serikali inachukua nafasi ya baba" Kama ilivyo dhahiri kutokana na maelezo hayo hapo juu (ya Bertrand Russel), k ufuta matunzo ya mwanamke, au kama mabwana hawa wanavyopenda kuuita uhuru wa mwanamke wa kiuchumi, kutakuwa na madhara yafuatayo: Baba ataondolewa katika orodha ya wanafamilia au kwa uchache atapoteza umuhimu wake.

Mfumo jike utafufuliwa. Serikali itachukua nafasi ya baba. Akina mama watasaidiwa na serikali. Hisia za kimama zitadhoofika. Kuzaa/kubeba mimba kutapoteza hisia za asili na sasa kutakuwa ni kazi ya kuajiriwa kama kazi nyingine. Ni wazi kuwa, matokeo ya maendeleo yote haya yatakuwa ni kubomoka kwa familia ambako kutamaanisha kuanguka kwa ubinadamu. Katika hali hiyo kila kitu kitakwenda vizuri isipokuwa kitu kimoja tu ndio kitakosekana nacho ni furaha na utulivu wa kiakili, vitu vinavyopatikana katika familia tu.

Hata hivyo, tunachomaanisha ni kuwa hata wanaounga mkono uhuru kamili wa mwanamke na kumuondoa baba katika orodha ya wanafamilia wanashikilia kuwa jukumu la asili la mwanamke la kuzaa watoto linampa haki ya kupata ruzuku na katika baadhi ya mazingira mshahara, au marupurupu na kwa mujibu wao, malipo haya yalipwe na serikali. Kwa upande mwingine mchango wa mwanaume katika uzazi (kutunga mimba) haumpi haki hiyo (ya kulipwa ruzuku n.k).

Sheria za kazi duniani, zinapopanga mshahara wa chini wa mfanyakazi wa kiume, huzingatia mahitaji ya mke wake na watoto pia, jambo linalomaanisha kuwa sheria za kazi duniani zinatambua rasmi kuwa mwanaume anawajibu kumtunza mke wake na watoto. Je azimio la haki za binadamu kwa mwanamke? wote limemdhalilisha Azimio la Haki za Binadamu kwa wote (kifungu cha 23, ibara iii) linasema;"Kila mtu ambaye anafanya kazi ana haki ya kupata malipo ya haki na yanayofaa, ili kumhakikishia yeye mwenyewe mwanaume na familia yake maisha yenye heshima na kukiwa na haja apewe kinga nyingine ya ziada." Ibara ya (i) kifungu cha 25 kinasema;"Kila mmoja ana haki ya kuishi maisha mazuri, yanayofaa kwa afya na siha yake yeye mwenywe (mwanaume) na familia yake, ikiwa ni pamoja na chakula, mavazi nyumba, matibabu na mahitaji mengine yote ya lazima ya kijamii na kinga sahihi wakati mtu anapopoteza ajira, ugonjwa, kupata ulemavu, kufa na kuacha mjane, uzee au hali nyinginezo ambazo ziko nje ya udhibiti wake.

Vifungu hivi viwili vinamaanisha kuwa kila mwanaume, anayeanzisha familia anapaswa kubeba gharama za mke wake na watoto na kwamba gharama zao zinahesabika kuwa sehemu ya gharama zake mwenyewe.

Ingawa Azimio la haki za Binadamu limeeleza wazi wazi kuwa mwanaume na mwanamke wana haki sawa halijaona kuwa mwanaume kumtunza mwanamke kuwa ni matusi kwa mwanamke au kuwa ni doa kwa usawa wake. Hivyo wale wanaolinukuu azimio hili kama rejea yao muhimu wanapaswa kuliangalia suala la matunzo ya mume kwa mkewe kuwa limewekwa wazi katika azimio hili.

Je, wale wenye akili za Kimagharibi wanaokiita kila kitu cha Kiislamu kuwa ni cha kupinga maendeleo watalikasirikia pia hili azimio na kuliezea kuwa linarejesha utumwa wa mwanamke?

Aidha, Azimio la Haki za Binadamu linaposema kuwa kila mmoja ana haki ya usalama au kinga pindi anapopoteza kazi anapougua, anapopata ulemavu, anapokufa na kuacha mjane, uzee au kukosa njia ya kujipatia riziki katika hali ambazo yeye hana udhibiti nazo, sio tu kwamba zinauelezea ujane kuwa ni pigo kwa riziki lakini linautaja sambamba na ukosefu wa ajira, maradhi na ulemavu.

Hivyo linawaweka wanawake katika kundi la wasio na ajira, wagonjwa, walemavu na wazee. Je, hili sio tusi kubwa kwa mwanamke? Kama maelezo haya yangekutwa katika vitabu au sheria za nchi ya Mashariki (Asia), bila shaka kelele kubwa ingekuwa imeshapigwa mpaka sasa kulilaani hilo. Lakini wale wanaotazama mambo kwa uhalisia wake kiasi cha kutorubuniwa kirahisi na propaganda za uwongo wanaelewa fika kuwa sheria ya maumbile na hata Azimio la Haki za Binadamu, zilizoweka ujane katika kundi la wasio na ajira haiwadhalilishi. Halikadhalika, sheria ya Kiislamu ambayo imefanya matunzo ya mwanamke kuwa wajibu kwa mwanaume, haijamshusha hadhi mwanamke. Ni ukweli kwamba ameumbwa hivyo kwamba anamhitaji mwanaume na anamtegemea.

Mwanaume na mwanamke wameumbwa katika hali ya kutegemeana kwa nia ya kuufanya muungano wao uwe na nguvu na imara na kuyafanya mahusiano ya kifamilia ambayo ni muhimu kwa furaha ya mwanadamu kuwa thabiti zaidi, ikiwa mwanamke atamtegemea mwanaume kifedha mwanaume naye humtegemea mwanamke kwa utulivu wa akili. Hivyo kutegemeana huwaleta karibu zaidi na huwaunganisha vizuri zaidi.