HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU0%

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU Mwandishi:
: AZIZI NJOZI
Kundi: Wanawake

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

Mwandishi: Allamah Shahid Murtaza Mutahhari
: AZIZI NJOZI
Kundi:

Matembeleo: 45410
Pakua: 3154

Maelezo zaidi:

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 33 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 45410 / Pakua: 3154
Kiwango Kiwango Kiwango
HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

Mwandishi:
Swahili

17

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

V- TALAKA

Tumeshasema hapo awali kuwa kuna hali mbili za talaka zinazosababisha matatizo yote. Mojawapo ni kuwa kuna baadhi ya kesi za talaka ambazo zinatokana na tabia ya kutokuwa mwaminifu na kutochangamka kwa upande wa wanaume. Nyingine ni kuwa, hata kunapokuwa hakuna uwezekano wa kufikia maelewano kati ya mume na mke, baadhi ya wanaume hukataa kutoa talaka sio kwa nia ya kutaka kuendelea kuishi naye bali kwa nia ya kumnyanyasa.

Tumeshaeleza hapo awali kuwa Uislamu unakaribisha jambo lolote litakalozuia talaka za aibu (udhalilishaji) na umechukua hatua kuliondosha kabisa tatizo hili. Hata hivyo Uislamu haukubaliani na matumizi ya nguvu kwa lengo la kudumisha mahusiano ya ndoa. Uislamu unaiona familia kama taasisi yenye uhai na (Uislamu) unafanya jitihada kuifanya iendelee kuwa hai. Lakini ikifa, hukumu ya Uislamu ni kuwa inapaswa kuzikwa. Uislamu hautaki familia iliyotiwa mumiani na ibakie kuwa na uhai bandia. Tumejifunza kwamba sababu ya kwa nini mwanaume ana haki ya kutoa talaka ni kuwa mahusiano ya kinyumba (ndoa) yamejengwa juu ya uhusiano wa asili ambao una kanuni zake. Maumbile yamezikabidhi funguo za uimarishaji wake au ubomoaji wake mikononi mwa mwanaume.

Mwanaume na mwanamke, kila mmoja, kwa asili ana nafasi yake, ambayo haiwezi kubadilishwa wala nafasi zao haziwezi kuunganishwa na kufanywa kuwa nafasi moja. Hizi nafasi maalumu za kila mmoja huibua haki na majukumu maalumu, haki ya talaka ikiwa ni mojawapo. Kwa maneno mengine haki hii inatokana na jukumu na mchango mahususi na maalumu ambao mwanaume na mwanamke kila mmoja huutoa katika kutafuta mwenzi katika maisha. Haki ya kutoa talaka inatokana na mchango maalumu wa mwanaume na si kutokana na umiliki wake.

Sasa unaweza kirahisi kupima thamani ya propaganda zinazoendeshwa na wanaoupinga Uislamu. Wanadai kuwa Uislamu umempa mwanaume haki ya talaka, kwa sababu hamtambui mwanamke kuwa ni mwenye utashi huru au kuwa ana matamanio au dhamira. Wanasema kuwa Uislamu unamuweka mwanamke katika kundi la vitu visivyo na uhai, umempatia mwanaume haki ya umiliki dhidi ya mwanamke.

Kiasili haki hizo zinajumuisha haki ya ukombozi. Tumeshaonyesha kuwa sheria ya familia ya Kiislamu haikujengwa juu ya umiliki (umwinyi) wa mwanaume na utwana wa mwanamke.

Falsafa ya Uislamu ni ya kina na ya juu mno kuliko uwezo wa kiakili wa waandishi hawa. Kwa kupitia muongozo wa Mwenyezi Mungu, Uislamu unaelewa asili ya msingi na muundo wa mfumo wa familia. Hivi sasa sayansi inabainisha baadhi ya mambo ya ajabu yaliyotatuliwa na Uislamu karne 14 zilizopita. Talaka inatolewa kwa namna maalum. Wanaoupinga Uislamu wanasema kuwa talaka inapaswa kuwa na muundo wa kimahakama na sio wa kuachia huru au kutoa nafuu. Ukweli ni kwamba talaka ina kipengele cha kuachia huru kwa sababu ndoa ina kipengele cha kutwaa.

Haiwezekani kubadilisha sheria ya kumtafuta mwenzi, ambayo imetoa majukumu ya kufanya kwa mwanaume na mwanamke katika mchakato huu (wa kutafuta mwenzi), na hali ya asili ya ndoa inafanana na kutwaa (kujinyakulia). Kuhusiana na uhusiano wa ngono (jimai), maumbile yameweka majukumu tofauti kwa mwanaume na mwanamke, kwa wanaadamu na wanyama. Talaka ingeweza kunyang'anywa kipengele chake cha kuachia huru kama tu ingewezekana kubadili sheria ya maumbile.

Mkosoaji mmoja anasema kuwa kwa ujumla mafakihi wa Kishia wanautafsiri mkataba wa ndoa kuwa ni wa kudumu, lakini inaonekana kuwa kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu, ni wa kudumu kwa mke tu, kwani mume anaweza kuubatilisha muda wowote kwa utashi na raha zake. Anaongeza kuwa ni jambo la aibu kumpa mume haki ya kutoa talaka katika zama hizi za atom, miezi bandia na demokrasia.

Inaelekea kuwa bwana huyu na wengine, wenye fikra kama zake, hawatofautishi kati ya kubatilisha ndoa na talaka. Tunaposema kuwa mkataba wa ndoa ni mkataba wa kudumu, tuna maana kuwa si mume wala mke mwenye haki ya kuubatilisha.

Ikiwa ndoa imebatilishwa (kama ambavyo huwa inatokea japo mara chache sana) huchukuliwa kana kwamba haikuwahi kufungwa na hakuna mtiririko wowote wa kisheria katika hilo. Mwanamke hawezi kudai mahari yake.

Mwanaume hana jukumu la kumtunza katika kipindi cha eda. Lakini kwa upande mwingine wa talaka, mkataba wa ndoa iliyofungwa kihalali huvunjwa, lakini athari zake za kisheria hazifutwi (hazibatilishwi) kabisa. Kwa mfano, ikiwa mwanaume atamtaliki mke wake baada ya kuishi naye hata kwa siku moja, anapaswa kulipa mahari yote na anawajibika kumtunza katika kipindi chote cha eda. Ikiwa atampa talaka mara tatu baada ya ndoa kufungwa lakini kabla ya kuingiliana naye, anapaswa kulipa nusu ya mahari na kumtunza mke wake. Kwa vile hapa hakuna suala la eda hivyo hakuna suala la matunzo.

Hivyo ni wazi kuwa talaka haibatilishi athari zote za kisheria za mkataba wa ndoa. Ni dhahiri pia kuwa talaka ni tofauti na kubatilisha ndoa na kwamba haki ya ndoa haipingani na ukweli kwamba mkataba wa ndoa ni wa kudumu. Kuna vipengele viwili vilivyo bainishwa katika Uislamu, ubatilisho wa ndoa na talaka.

Ndoa inaweza kubatilika ikiwa kuna upungufu mkubwa wa kimwili uliogundulika ama kwa mume au mke, katika hili wote wana haki sawa ya kubatilisha ndoa. Talaka tu ndiyo haki ya mume peke yake. Ukweli kwamba kuna kanuni tofauti kwa ajili ya talaka kwa upande mmoja na kanuni tofauti za ubatilisho wa ndoa kwa upande mwingine unaonyesha kuwa Uislamu haukumpa mwanaume haki ya kutoa talaka kwa sababu ulitaka kumpa upendeleo maalum.

Adhabu kwa mtu anayetoa talaka. Kwa nia ya kuzuia talaka, baadhi ya mifumo ya sheria imeweka adhabu kwa mtu anayempa mkewe talaka. Hatuna hakika kama sheria kama hii bado ipo sehemu yoyote ile duniani kwa sasa. Hata hivyo, wanahistoria wanasema kuwa Wafalme wa Kikristo wa Urumi waliwatoza faini wale wote ambao waliwataliki wake zao bila sababu ya maana. Ni wazi kuwa huu ni muundo mwingine wa matumizi ya nguvu katika kudumisha maisha ya ndoa, na hivyo haiwezi ikawa na manufaa (msaada) makubwa. Kumpa mke haki ya kutoa talaka. Mpaka sasa tumejadili haki ya asili ya kutoa talaka ambayo ni ya mume peke yake.

Lakini anaweza kumpa mke wake haki ya kutoa talaka. Utoaji huu wa mamlaka haya kwa mke unaweza kuwa wa jumla au unaoweza kutumika katika mazingira fulani. Ili kuhakikisha kuwa haibatilishwi huingizwa katika mkataba wa ndoa kama sharti la kudumu, ambapo kwa mujibu wa sharti hilo mke hupewa mamlaka fulani ambayo tayari watakuwa wameshakubaliana. Imekuwa ni kawaida tokea zamani kwamba wanawake wanaohisi kwa namna yoyote kuwa na shaka na mwenendo wa waume zao huhimiza kuwekwa kwa sharti hili katika mikataba yao ya ndoa na hutumia mamlaka waliyopewa, pindi kukiwa na haja ya kufanya hivyo.

Hivyo, sio sawa kusema kuwa haki ya talaka ni haki ya mtu mmoja tu na kwamba Uislamu umempa haki hiyo mwanaume tu. Talaka ya Kimahakama. Talaka ya kimahakama ina maana uvunjaji wa ndoa kwa mamlaka ya jaji na si kwa mamlaka ya mume. Katika nchi nyingi ni mahakama tu yenye mamlaka ya kutoa talaka na kuvunja ndoa. Kwa mujibu wa mfumo huu, kila talaka ni talaka ya kimahakama., Tumeshabainisha hapo awali kuwa ikiwa asili ya ndoa, lengo la kuundwa kwa familia na nafasi inayoshikiliwa na mwanamke katika familia, talaka ambayo hujiendesha itakavyo haiwezi kutegemea uamuzi wa jaji.

Sasa tungependa kuona ikiwa, kwa mtazamo wa Uislamu, jaji hana mamlaka ya kutoa talaka au ikiwa kuna hali zozote ambazo, zikiwa sio za kawaida jaji anaweza kufanya hivyo. Talaka ni haki ya asili ya mume, ikiwa uhusiano wake na mke wake ulikuwa wa kawaida. Kwa kawaida, kama anataka kuishi na mke wake anapaswa kumjali, kumpatia haki zake zote anazostahili na kuishi naye kwa wema. Kama akiona kuwa hawezi kuishi naye kwa wema anapaswa kumlipa haki zake zote na kutengana (kuachana) naye. Mbali na kumlipa haki zake anapaswa kumlipa kiasi kingine cha fedha au mali cha ziada kama shukrani kwa wema wake.

Qur'ani Tukufu inasema:

"Wapatieni cha kuwaliwaza, mwenye wasaa kwa kadri ya uwezo wake, na maskini kwa kadiri ya uwezo wake, riziki nzuri." (Suratul Baqara, 2:236). Lakini kunaweza kuwa na hali ambapo maisha ya ndoa hayaendi kama kawaida. Kunaweza kuwa na mwanaume ambaye hataki kuishi kwa wema na mkewe wala hataki kumpa talaka. Talaka ya asili inaweza kufananishwa na mtoto anapozaliwa kwa njia ya kawaida. Lakini talaka ya mwanaume ambaye hayuko tayari kutekeleza wajibu wake na hataki kutoa talaka, kwa hiari yake ni kama uzazi usio wa kawaida ambao huhitaji upasuaji wa daktari.

Je, baadhi ya kesi za ndoa hazitibiki kama kansa? Katika hali hizo talaka haitegemei ridhaa na mapenzi ya mume. Ikiwa mwanaume huyo hayuko tayari kutoa talaka, mwanamke hawezi kuachwa aendelee kuvumilia maumivu bila kupata dawa. Uislamu hauwi mtazamaji mkimya katika hali hizi. Baadhi ya watu wana fikra potofu kuwa kwa mtazamo wa Uislamu hali hizi hazitibiki. Wanafikiri kuwa ni aina ya kansa inayowatesa watu wenye bahati mbaya lakini haiwezi kutibika na hivyo mwanamke hana namna isipokuwa kustahamili hadi atakapokufa. Kwa maoni yetu fikra hii haikubaliki katika kanuni za Uislamu. Uislamu ni dini ambayo mara zote hutetea uadilifu.

Kujenga jamii adilifu imekuwa ni lengo kuu la Mitume wote. Qur'ani Tukufu inasema;

"Kwa hakika Tuliwapeleka Wajumbe Wetu na dalili zilizo wazi na Tuliwateremshia pamoja nao Kitabu na Mizani, ili wanaadamu wahukumiane kwa haki (usawa)." (57:25).

Uislamu hauwezi kuvumilia uvunjaji wa maadili wa wazi namna hii, wala ukafikiriwa kuwa utatoa sheria itakayotoa suluhisho linalofananishwa na kansa. Inasikitisha kwamba baadhi ya watu ambao wanakiri kuwa Uislamu ni dini ya uadilifu, bado wanashikilia mtazamo huu.

Ikiwa 'sheria moja nyeusi' itapachikwa kwenye Uislamu na ikakubaliwa kuwa ni kansa, hakuwezi kuwa na kizuizi cha maana cha kuzuia sheria nyingine 'za kikatili' kuitwa tetenasi, kifua kikuu, polio n.k. Madai haya ni kinyume cha kanuni ya uadilifu ambayo ndio msingi mkuu wa sheria za Kiislamu.

Aidha, kama inawezekana kuondoa kansa kwa upasuaji mdogo. Je haitakuwa busara kuharakisha tiba na kumpa mgonjwa nafuu? Hebu chukua mfano wa mwanamke anayekwenda kwa mwanaume kwa moyo na nia safi akijua ni mwenzi wake maishani, lakini ghafla mwanaume huyo anapoteza mapenzi naye.

Ikiwa mwanaume atatumia vibaya madaraka yake, hampi talaka wala hataki kukaa naye kwa wema, kwa maneno ya Qur'ani anamning'iniza, sio kwa sababu anataka kuishi naye kama mkewe bali kwa nia ya kumzuia asitafute mume mwingine anayefaa, mwanamke huyu kwa hakika anataabishwa na kansa. Lakini kansa hii inaweza kuponyeshwa kirahisi kwa upasuaji, na baada ya upasuaji mgonjwa anatarajiwa kupona kabisa. Upasuaji huu unaweza kufanywa na jaji mwenye ujuzi tu.

Kama ilivyoelezwa awali, ni tatizo kubwa la jamii yetu kwamba baadhi ya waume wasio na huruma hukataa kutoa talaka na hivyo kufanya dhulma kubwa. Wanatumia dini kuhalalishia mienendo yao isiyokubalika kabisa. Wanaposema kuwa mwanamke avumilie kwa subira ukatili wao kama kansa isiyotibika kwa hakika wanalichafua jina la Uislamu. Ingawa somo hili ni la kiufundi, hata hivyo tunataka kulijadili kwa kifupi ili kuondoa shaka ya watu waovu na kufafanua mafundisho ya Uislamu juu ya hili. Kushindwa kabisa kufikia maafikiano.

Baadhi ya hali za kushindwa kufikia maafikiano sio za kipekee kwenye masuala ya ndoa na talaka. Hutokea pia katika maeneo mengine pia, kama vile yanayohusiana na matatizo ya kifedha. Sasa hebu tuangalie jinsi Uislamu ulivyoshughulikia mikwamo katika maeneo haya. Je umeiondoa mikwamo hii au umeikubali kama hali zisizotibika?

Jaalia watu wawili, kwa kupitia mirathi au njia nyingine wanatokea kumiliki mali isiyogawanyika kama vile almasi, pete au gari na hawako tayari kutumia mali hiyo pamoja au kwa zamu. Pia kila mmoja wao hayuko tayari kuuza sehemu yake kwa huyu mwenzake.

Pia hawakubaliani juu ya namna nyingine ya kuitumia mali hiyo. Mali hiyo inakaa bila kutumiwa, kwa sababu ni dhahiri hakuna yeyote kati yao anayeweza kuitumia bila idhini ya mwenzake. Nini kifanyike katika hali hiyo. Je tatizo hilo libakie hivyo bila kutatuliwa na mali ibaki bila kutumiwa? Je Uislamu umetafuta suluhisho la utata huu? Ukweli ni kuwa Uislamu hauchukulii suala hili kuwa lisiloweza kutanzuliwa. Haukiri kuwa haki ya kumiliki inaweza kuzuia kutumiwa kwa mali yoyote.

Unaziruhusu mahakama za sheria kuingilia kati na kuyaweka mambo sawa. Hata kama pande zinazohusika hazitaki suala hilo liamuliwe, bado mahakama inaweza kuamuru mali hiyo ikodishwe au iuzwe. Mapato yatakayopatikana yatagawiwa baina ya wamiliki, lakini mahakama inaweza kuchukua hatua kwa idhini au bila idhini yao. Katika hali hizo, haki ya umiliki haizingatiwi kwa sababu ya kuhusika kwa kanuni nyingine, kanuni ya kuzuia kitu kukaa bila kutumika.

Haki ya umiliki inapaswa kupuuzwa katika hali hii, kwa sababu inapaswa kuheshimiwa tu ikiwa haitasababisha hasara kabisa au kitu kukaa bila kutumiwa. Jaalia watu wawili wanaolimiki almasi, jambia au kitu kinginecho. Hakuna aliye tayari kumuuzia mwenzake sehemu yake (gawio lake la mali) lakini wote wawili wanakubaliana kuikata na kila mtu kupata kipande (nusu).

Ni wazi kuwa almasi, jambia au gari likikatwa vipande viwili huwa haiwezi kutumika tena na hupoteza thamani yake. Uislamu hauruhusu uharibifu huo. Fakihi (mjuzi wa sheria za Kiislamu) mkubwa, Allamah Hilli, anasema kuwa mamlaka za kisheria hazipaswi kumruhusu yeyote kuchukua uamuzi kama huu. Ukweli kwamba wamiliki wa mali hiyo wamekubaliana juu ya uamuzi huu, hautazingatiwa wala kuheshimiwa katika hali hizi.

Mkingamo wa talaka. Sasa hebu tuangalie nini kinapaswa kufanywa juu ya suala la talaka. Ikiwa mume hataki maelewano na hatekelezi majukumu yake yote au baadhi ya kifedha (matunzo), kimaadili kuishi naye kwa wema na jimai (ngono) kama ilivyoamrishwa na Uislamu na wakati huo huo hayuko tayari kumtaliki mkewe, je ni hatua gani ichukuliwe? Je kuna sababu inayotosheleza hapa kuiruhusu mamlaka ya kisheria kuingilia kati?

Maoni ya Ayatullah Hilli. Fakihi mkubwa wa zama hizi, Ayatullah Sheikh Husein Hilli wa Najaf Iraq, amelijadili suala hili katika tashifu (makala) yake iitwayo 'Haki za unyumba'. Huu hapa ni mukhtasari wa maoni yake: "Ndoa ni mkataba mtakatifu na wakati huo huo ni aina fulani ya ushirika (ubia) kati ya watu wawili ambao kila mmoja anawajibika kwa mwenzake, na ambao utekelezaji wa majukumu hayo huwasababishia furaha. Huu sio mwisho.

Kwa kweli, mafanikio na furaha ya jamii nzima hutegemea mafanikio ya uhusiano wao. Haki kuu za mke ni matunzo, unyumba na kuishi naye kwa wema. Ikiwa mume ataacha kutekeleza majukumu yake na pia atakataa kumtaliki mke wake, je mwanamke afanye nini na amwelekee vipi mume wake? Hapa kuna njia mbili. Aidha mamlaka ya kisheria ya kiislamu iingilie kati na kuitangaza ndoa kuwa imevunjika au mke naye akatae kutekeleza majukumu yake. Njia ya kwanza inaungwa mkono na Aya hizi za Qur'ani.

"Talaka inaweza kutolewa mara mbili; kisha mwanamke arejeshwe na kukaa naye kwa wema au aachiliwe aende kwa wema (Suratul Baqarah, 2:229). Kwa maneno mengine, haki ya talaka na kutanguliwa kwake ni mara mbili tu. Baada ya hapo kuna njia mbili tu zinazobaki, ama kukaa na mke kwa wema au kumwacha kwa wema. Katika Suratul Baqarah tena (2:232), Qur'ani inasema:"Mnapokuwa mmewataliki wake zenu, na wamemaliza eda zao, ama kaeni (warejeeni) nao kwa wema au waacheni kwa wema. Msiwashikilie kwa nguvu ili muwatese, hamuwarejei wala hamuwaachi.

Yeyote anayefanya hivyo anajidhulumu nafsi yake. Kutokana na Aya hizi, tunaweza kupata kanuni ya jumla. Mume anapaswa ama kumrejea mke wake na kutekeleza majukumu yake kikamilifu au kumwacha na kukata uhusiano wa unyumba. Kwa mtazamo wa Uislamu, hakuna njia ya tatu. Maneno 'Msiwang'ang'anie kwa nguvu ili muwatese' yanakataa njia (suluhisho) ya tatu mbali na kuwarejea na kukaa nao kwa wema au kuwaacha kwa wema. Kwa maana ya kijumla zaidi, maneno haya yanajumlisha hali zote, kumtesa mwanamke kwa makusudi na kupuuzia haki na maslahi yake kwa kukataa kumtaliki.

Aya hizi zinaeleza wazi wazi suala la kubatilisha talaka na zinaweka wazi kuwa ubatilishaji wa talaka unapaswa kufanywa kwa nia njema ya kutaka kuendelea kuishi na mwanamke kwa wema kama mwenzi maishani na sio kwa nia ya kumtesa. Lakini kwa upana wake, Aya hizi hazizungumzi suala hili tu. Zinaweka kanuni ya jumla kutumika katika haki za mke wakati wote na katika hali zote. Kama kanuni ya jumla, mume anapaswa kuchagua moja kati ya njia mbili katika maisha yake yote ya ndoa.

Hakuna njia ya tatu. Baadhi ya mafakihi, kwa makosa wamezibana Aya hizi. Wana maoni kuwa zinawahusu wale waume tu wanaotaka kuzibatilisha talaka zao katika kipindi cha eda. Kwa kusema kweli mtazamo huu sio sahihi. Mbali na muktadha wa Aya hizi, Maimamu wa Ahlul Bait ambao maoni yao ni hukumu moja kwa moja, wamezitumia Aya hizi katika hali nyingine pia.

Kwa mfano Imam Baqir(a.s) amesema kuwa:Mume anayeapa kuwa hamtaki mke wake na kwa kufuatana na kiapo hicho akajitenga naye, ana njia mbili tu za kufanya baada ya kipindi cha miezi mine kuisha. Ama avunje kiapo chake na kutoa kafara kwa tabia yake isiyofaa au mara moja amtaliki mkewe, kwani Mwenyezi Mungu anasema; "Ama mrejeshe na kukaa naye kwa wema au muache kwa wema (Suratul Baqara 2:229).

Katika tukio jingine ambapo mtu mmoja alikuwa amemteuwa mtu mwingine kupanga mahari na kufunga naye ndoa kwa niaba yake, lakini baadaye alikana kuwa hakuagiza hivyo, Imam Sadiq(a.s) alisema kuwa mwanamke angejichagulia mume mwingine. Mwanaume huyo atakapojua kuwa alikuwa amemteuwa mtu na kumpa madaraka ya kupanga mahari na kufunga ndoa kwa niaba yake lakini baadaye akakana, basi ni lazima atoe talaka ili moyo wake (dhamira) uwe safi, kwa kuwa Allah amesema; "Ama kaa na mwanamke kwa wema au muache kwa wema" Mifano hii inaonyesha kuwa Maimamu waliamini kuwa Aya hii ilikuwa ni kanuni ya jumla.

Na iwapo mume hatekelezi jukumu lake la unyumba wala hamtaki mke wake, mahakama ya kidini inapaswa kumwita na kumtaka atoe talaka. Akikataa, mahakama yenyewe inaweza kutangaza kuwa ndoa imevunjika. Kwa mujibu wa hadith, Abu Basir amesimulia kuwa Imam Sadiq(a.s) alisema: "Ikiwa mume hamtunzi mke wake ni jukumu la mahakama kuvunja ndoa yao, kwa kulazimisha talaka." Hii kwa kifupi ni maoni ya fakihi wa cheo cha juu wa zama hizi.

Anayetaka kujua undani wake asome kitabu kiitwacho 'Huquq-uz-Zawjiyyah' ambacho kina maelezo marefu ya mwanazuoni huyu. Kama ulivyoona, Aya, "Ama kaa naye kwa wema au muache kwa wema' ni kanuni ambayo Uislamu umeitumia kuwajibisha haki za mke. Kwa mujibu wa kanuni hii na amri kali iliyomo katika sentensi msiwarejeshe ili kuwadhuru', Uislamu hautaki mwanaume yeyote mwovu kuyatumia madaraka yake vibaya na kumbana mwanamke asiolowe na mtu mwingine. Mbali na hoja hizo zilizonukuliwa kutoka kwenye makala ya 'Haki za Unyumba', kuna hoja nyingine pia ambazo zinaunga mkono mtazamo kuwa Aya "Ama kaa naye kwa wema au muache kwa wema' kwa mtazamo wa Uislamu ni kanuni ya jumla inayohusu haki zote za mke. Kwa kadri mtu anavyozitazama pande mbali mbali za kanuni hii, ndivyo anavyozidi kuutambua ubora wa mafundisho ya Uislamu.

Katika kitabu, al-Kafi, Jalada la tano, Imam Sadiq(a.s) ameripotiwa kusema kuwa:Mtu anapotaka kumuoa mwanamke anatakiwa asema; "Ninakiri kiapo kilichochukuliwa na Allah' "Ama kaa naye kwa wema au muache kwa wema' Qur'ani Tukufu inasema; "Vipi mnaweza kunyang'anya mahari (mliyowapa) na hali mmeshaingiliana nao, na wamechukua kwenu ahadi thabiti (ya kuwalipa mahari kamili) (Suratul Nisaa, 4:21). Wafasiri wa Qur'ani, wote Shia na Sunni wanakubali kuwa hapa 'ahadi thabiti' inazungumziwa Aya, "Ama kaa naye kwa wema au muache kwa wema'. Hii ndio ahadi ambayo Imam Sadiq(a.s) aliimaanisha alipowataka watu kuikubali ahadi ya Allah wakati wa ndoa.

Vyanzo vyote vya Kishia na Kisunni vinaripoti kuwa katika Hija ya mwisho Mtukufu Mtume alisema; "Muogopeni Allah juu ya wanawake kwani hiyo ni dhamana ya Allah, na mmeruhusiwa kustarehe nao kwa neno lake." Mwanahistoria maarufu na mwanatheolojia Ibn al-Athir anaandika kuwa 'neno la Allah' katika kauli hii ya Mtume linamaanisha Aya ya Qur'ani;"Ama kaa naye kwa wema au muache kwa wema' Maoni ya Sheikh Tusi. Sheikh Tusi akitoa maoni yake juu ya suala la kukosa nguvu za kiume (uhanithi), anasema kuwa baada ya kuthibitika kuwa mume ni hajiwezi (kiunyumba), mke ana hiari ya kuvunja ndoa. Anasema kuwa mafakihi wote wamekubaliana juu ya hili na kwa kutetea hoja yao wanatumia Aya "Ama kaa naye kwa wema au muache kwa wema' Mwanaume huyu, kwa vile hana uwezo wa kutekeleza jukumu lake la unyumba, hawezi kukaa na mke wake kwa wema, hivyo anapaswa kumwacha. Maoni yote yaliyonukuliwa hapo juu, yanathibitisha kuwa Uislamu haumruhusu mwanaume yeyote kuitumia haki yake ya talaka vibaya na kumweka mke wake kama mfungwa. Hata hivyo, ifahamike kuwa si kila jaji ana ujuzi wa kutosha kuingilia masuala haya.

Uislamu umeweka vigezo vigumu sana vya mtu kuwa kadhi. Inafaa pia ieleweke kuwa talaka zinazotolewa na jaji zinatarajiwa kuwa chache sana, kwani Uislamu unapenda familia zidumu kwa kadri inavyowezekana, Uislamu hauwezi kuruhusu talaka ichukue sura kama ile ya Ulaya na Marekani, mambo tunayoyasoma kila siku kwenye magazeti. Kwa mfano mwanamke mmoja alidai talaka kwa kuwa mume wake hakuipenda filamu ambayo yeye alikuwa anaipenda. Mwanamke mwingine alitaka talaka kwa kuwa mume wake hakumbusu mbwa wake kipenzi, vijisababu vingine vingi vya ovyo ambavyo ni vituko vinaripotiwa kila siku. Vyote hivi vinaashiria kuporomoka kwa ubinadamu. Katika sura hii, tumejadili nadharia tano za talaka kwa mtiririko huu: Haifai kuwepo kwa vizuizi vya kimaadili na kijamii vya talaka.

Ndoa ni mkataba wa milele. Talaka inapaswa kupigwa marufuku kabisa (maoni ya kanisa Katoliki). Ndoa inaweza kuvunjwa na mwanaume sio mwanamke. Ndoa inaweza kuvunjwa na wote wawili, mume na mke lakini kwa masharti fulani. Taratibu za uvunjaji wake zinafanana bila kujali aliyeamua kuvunja ni mume au mke (maoni ya watetezi wa usawa wa haki). Njia ya talaka iko wazi kwa wote mume na mke lakini taratibu zake ni tofauti (kutegemea ni nani, mume au mke, anayeamua kuvunja ndoa).

Kama tulivyosema hapo awali, Uislamu unaunga mkono nadharia ya mwisho. Kutokana na tuliyoyasema juu ya kutoa madaraka kwa mke ya kuvunja ndoa kama sharti la lazima na mkataba wa ndoa na uwezekano wa talaka ya kimahakama, ni dhahiri kuwa japo Uislamu hautambui kuwa mke ana haki ya asili ya talaka, lakini haujamfungia moja kwa moja mlango wake wa kutokea. Suala la talaka ya kimahakama linaweza kujadiliwa zaidi, hasa kwa kurejea maoni ya mafakihi wa matapo mbali mbali ya sheria, lakini tunafikiri kuwa kwa matumizi na haja yetu ya sasa, hatuhitaji kwenda ndani zaidi.