• Anza
  • Iliyopita
  • 11 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 3843 / Pakua: 1956
Kiwango Kiwango Kiwango
SHAHADA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S)

SHAHADA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S)

Mwandishi:
Swahili

SHAHADA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S)

FATIMA (A.S) KWA MUHTASARI.

Hakika Mwenyeezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu watu wa nyumba (ya Mtume), na anataka kukutakaseni sana sana.{33:33)

Mwenyeezi Mungu (s.w) amewataja Ahlul-bayt (a.s) kwa kuwakirimu na kuwanyanyua hadi katika daraja ya juu kabisa,kisha Mtume (s.a.w) akamchukua Fatima,kisha Ali,kisha Hassan,kisha Husein (a.s) akasema:

"Hawa ni Ahlul-bayt wangu". Fatima (a.s) alikuwa ni bint mdogo sana kati ya mabinti wa Mtume (s.a.w) na anayependwa zaidi na Mtume (s.a.w) kuliko yeyote yule kati yao.Na alikuwa ni mbora wa wanawake wote wa ulimwenguni,na Mtume (s.a.w) amezungumza kuhusiana na Fatima (a.s) kwa kusema:

{{Hakika Fatima ni sehemu ya nyama yangu, kinanitia wasi wasi (shaka) kinachomtia wasi wasi (au shaka), na kinaniudhi kinachomuudhi}} Na hili ni moja kati ya yale mambo yanayoonyesha utukufu wa Sayyidat Fatima (a.s) na daraja yake ya juu kabisa.Ama wema wake,ubora wake,mazuri yake na Fadhila zake ni nyingi sana na kubwa,na Baba yake s.a.w) amemwambia kwa kusema: "Hakika ya Mwenyeezi Mungu huridhia unaporidhia,na hughadhibika unapoghadhibika".

SEHEMU YA KWANZA.

KUZALIWA KWA SAYYIDAT FATIMA (A.S).

Sayyidat Fatima (a.s) amezaliwa katika mji wa Makka mwezi wa sita ambao ni Jamaadul-a'khir (Yaani Jamaaduth-thaaniy) siku ya Ishirini (20) ya mwezi huu,mwaka wa arobaini na tano (45) wa kuzalizliwa Mtume (s.a.w) na ilikuwa ni mwaka wa tano baada (ya Mab-ath) ya Mtume (s.a.w) kutumwa na Mola wake (s.w) akiwa ni Mjumbe wake kwa walimwengu wote.Na mimba ya kwanza kwa Bi Khadija (a.s) ilikuwa ni mimba ya Sayyidat Fatima (a.s).

Mtume (s.a.w) baada ya kupandishwa mpaka mbinguni,alikunywa maji ya peponi na akala katika matunda ya peponi,yenye harufu nzuri,matamu kupindukia na kila aina ya sifa,kisha Mwenyeezi Mungu (s.w) akayabadilisha matunda hayo kuwa maji katika mgomgo wa Mtume (s.a.w),baada ya Mtume (s.a.w) kushuka kutoka Mbinguni kuja Ardhini,kabla hajala kitu chochote cha humu duniani,akakutana kimwili na mkewe Bi Khadija (a.s),kisha baada ya hapo Bi Khadija akapata Mimba ya Sayyidat Fatima (a.s),haya ndiyo mazingira ya mimba ya Sayyidat Fatima (a.s) yalivyokuwa,kwa hakika mimba yake ilitokana na chakula au matunda bora ya peponi ambayo hayapatikani katika Uliwemwengu huu ispokuwa Peponi tu.

Na pindi Mtume (s.a.w) alipokuwa na hamu ya (kutaka kujikumbushia harufu nzuri ya peponi) harufu ya peponi alikuwa akimnusa Mwanaye kipenzi Sayyidat Fatima (a.s),na kupata kutoka kwake harufu ya Peponi na harufu ya Mti mzuri.Na alikuwa akizidisha kumbusu mwanae Fatima (a.s),na hii ni kwa sababu ya ubora wake na sehemu yake aliyokuwa nayo mbele ya Mtume (s.a.w).

1

SHAHADA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S)

SEHEMU YA PILI:

IDADI YA MAJINA YA FATIMA (A.S).

Imepokewa kutoka kwa Yuunus bin Dhab-yaan amesema:

Amesema Abu Abdillah (a.s):

Kwa Fatima kuna majina tisa (9) kutoka kwa Mwenyeezi Mungu (s.w),(jina la kwanza): 1-Fatima

2-Swiddiyqa

3-Al-mubaarak

4-Atw-twaahira

5-Az-zakiyya

6-Ar-raadhia

7-Al-mardhiyya

8-Al-muhad-ditha

9-Az-zahraa.

Kisha akasema:

Unajua tafsiri ya (jina hili la) Fatima?

Nikasema (yaani Yuunus bin Dhab-yaan): Nijulishe Ewe Bwana wangu:Akasema:

Maana yake: "Ametenganishwa na kumuweka mbali na mto wa jahannam",akasema(Yuunus):Kisha akasema:

"Lau kama si Amirul Muuminina Ali (a.s) kumuoa Fatima (a.s),basi asingelikuwepo anayefaa na anayestahiki kumuoa katika uso wa Ardhi hii katika wanaadam na wasiokuwa wanaadam mpaka siku ya Kiyama."

Na katika Musnadur-ridhaa, imekuja hadithi hii kwamba Mtume (s.a.w) amesema: "Mtoto wangu Fatima ameitwa Fatima kwa sababu Mwenyeezi Mungu (s.w) amemtenganisha na kumtenganisha yule atakayempenda (Fatima -a.s-) na moto wa Jahannam." Na majina yote nane yaliyobaki kila jina lina maana yake,hatukuweza kutaja tafsiri ya kila jina kutokana na ufinyu wa muda.

2

SHAHADA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S)

SEHEMU YA TATU:

LAQABU ZA SAYYIDAT FATIMA (A.S)

Kuhusiana na Laqab za Sayyidat Fatima (a.s) ni kwamba alikuwa akiitwa: 1-Ummul-Hassan

2-Ummul-Husein

3-Ummul-Muhsin

4-Ummul-AIMMA. (MAMA YA MAIMAM 12)

5-UMMU-ABIYHA

6-UMMUL-MUUMININA

Na laqab hizi utazikuta katika Ziyaara yake (a.s), inayoitwa:{Ziyaarat Fatimatuz-zahraa (a.s). Na Mbinguni Fatima (a.s) huitwa:

1-An-nuuriyya.

2-As-samaawiyya.

3-Al-haaniya.

Laqab hii ya tatu yaani (Al-haaniya) maana yake ni:

Mwenye kumhurumia Mume wake na Watoto wake. Ama huruma yake kwa mume wake, inathibiti na inatosha kwa yale yaliyomfika Sayyidat Fatima (a.s) baada kupigwa,kudhalilishwa na athari za mijeredi katika mwili wake kama vile bangili au pingu au kingaja au kilinzi.Yote hayo ilikuwa ni katika kumhami na kumlinda Mume wake (Yaani Imam Ali -a.s-) mpaka alipokufa shahidi.

Lakini pamoja na hayo Sayyidat Fatima (a.s) mauti yalipomfika alilia sana, Amirul Muminina Ali bin Abi Twalib (a.s) akamuuliza: Ewe Kipenzi changu! Ni kipi kinacho kuliza? Fatima (a.s) akasema: Ninalia kwa sababu ya yale utakayokuja kukutana nayo baada yangu, Imam Ali (a.s) akamwambia: Usilie! Nakuapia kwa Mwenyeezi Mungu (s.w), hakika ya hayo (yatakayonifika baada yako) ni madogo sana kwangu katika Dhati ya Mwenyeezi Mungu (s.w).

3

SHAHADA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S)

SEHEMU YA NNE:

FADHILA ZA SAYYIDAT FATIMA (A.S).

Sayyida Fatima (a.s) alikuwa ni miongoni mwa Watu wa Kisaa,na miongoni mwa watu wa Mubaahala ambao (tarehe ishirini na nane (28) mfungo tatu mwaka wa kumi (10) Hijria) waliongozwa na Mtume (s.a.w) kwenda kukutana na ujumbe wa kikristo kutoka Najran ili kujadiliana kuhusiana na Nabii Isa (a.s) ambapo maudhui ilikuwa ni kuhusu:

{Kuzaliwa kwa Nabii Isa bila Baba},Wakristo wao walikidai na kudhani kuwa Nabi Isa (a.s) Baba yake ni Mwenyeezi Mungu (s.w),siku hii ilikuwa ni siku maalum kwa ajili ya kuwarekebisha imani yao watu hao ambapo mtume (s.a.w) aliwasomea aya inayosema:

"Hakika mfano wa Isa mbele aya Mwennyeezi Mungu ni kama mfano wa Adam,aliumbwa kwa udongo kisha akamwambia kuwa naye akawa". Wakristo baada ya kug'ang'ania imani yao na itikadi yao hii batili ndipo Mwenyeezi Mungu (s.w) alipomwamrisha Mtume wake (s.a.w) katika aya ya 61 ya Suurat Aali Imraan,ambapo alimtaka afanye nao maombi kwa unyenyekevu,kisha waiweke laana ya Mwenyeezi Mungu (s.w) iwe ni yenye kuwashukia wenye kusema uongo.Ujumbe huo wa Wakristo uliokuja kukutana na Kundi la Mtume (s.a.w) ulikuwa ukiongozwa na Makasisi watatu:Ambao ni:

1-Ahtam

2-Al'aaqib

3-Sayyid.

Lakini wakristo baada ya kuona Nyuso alizokuja nazo Mtume (s.a.w) si Nyuso za kawaida wakaamua kuishia mitini!! Mmoja wa viongozi wa wakristo hao aliyekuwa akiitwa Sayyid, aliwashauri wakiristo hao wabishi kupindukia wenye itikadi dhaifu kwa kuwambia namna hii:

"Enyi Wakristo! Mimi naziona Nyuso hizi (yaani kundi hili la Mtume -s.a.w-) kama zitamuomba Mwenyeezi Mungu auondoe mlima mahala pake,wallah atauondoa.Msiapizane naye mtaagamia,na hatabaki mkristo hata mmoja hapa duniani mpaka siku ya kiyama" Askofu Ahtam naye baada ya kuziona Nyuso zile zikiwaka na kun'gara,hakuamini macho,akashindwa kuvumilia kwa mshangao ikabidi awambie wakristo na maaskofu wenzake:Niacheni nikamuulize Muhammad kuhusiana na hawa watu!! Alipomkaribia Mbora wa Mitume (s.a.w) akamuuliza:

"Ewe Abulqaasim! Unatoka na kina nani kwa ajili ya maapizano haya"? Mtume (s.a.w) akamjibu:Ninaapizana nanyi nikiwa na watu bora hapa duniani na watukufu mno mbele ya Mwenyeezi Mungu (s.w) nao ni:Mtume akaaza kuwataja kwa majina yao mmoja baada ya mwingine: 1-Ali

2-Fatima

3-Hasan {a.s}

4-Husein.

Yule Askofu wa tatu Al-aaqib aliyekuwa ndiye mwenyekiti wa ujumbe huo,wakristo walimuuliza na akajibu namna hii:

"Enyi Wakristo wallah nyinyi mnajua kuwa Muhammad ni Nabii aliyeletwa na amekuja na ushahidi uliowazi kuhusiana na Nabii Isa (a.s),wallah hakuna watu walioapizana na Nabii wakasalimika,ikiwa mtaamua kuapizana naye basi mtaangamia."

Utakuta maulamaa na watunzi wa vitabu hivi wametaja kisa hiki kama inavyotakiwa na kama kilivyokuwa,ambapo wametaja kuwa wakristo hao waliogopa kufanya maapizano,wakaamua kuomba sulhu kwa kutoa Dirhamu Elfu Arobaini. Tukio hili linadhihirisha ukubwa wa Mwenyeezi Mungu,Mwenye nguvu na Hekima.

Pia tukio hili linadhihirisha ubora wa Sayyidat Fatima (a.s) ambaye alichukua nafasi ya wanawake wote wa uliwmenguni siku hiyo ya Mubaahala kwani mpangilio wa kikosi cha Mtukufu Mtume (s.a.w) ulikuwa katika mfumo alioutaka na alioukusudia Mwenyeezi Mungu (s.w) katika aya hiyo ya 61 ya suurat Aali Imraan.aya, aya hiyo inasema hivi: * "Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu" Mtume (s.a.w) akamuita Hasan na Husein (a.s).

* "Na wanawake wetu na wanawake wenu" Mtume (s.a.w) akamuita Fatima (a.s).

* "Na nafsi zetu na nafsi zenu" Mtume (s.a.w) akamuita Ali (a.s).

Sayyidat Fatima (a.s) pia alikuwa ni miongoni mwa wale ambao A'yatut-tat-hiir imeshuka kwao ikisema: "ona kwamba naye miongo mwao (au yuko pamoja nao) chini ya Kisaa (Shuka). Sayyidat Fatima (a.s) pia ni Mama wa Maimam kumi na Wawili (a.s),wote hao asili yao ni Sayyidat Fatuma (a.s) na wote hao ni wajukuu wa Mtume (s.a.w).Pia Sayyidat Fatima (a.s) ni Mbora wa wanawake wote wa ulimwengu mzima tangu mwanzo wa ulimwengu mpaka mwisho wake.

Na alikuwa (a.s) ndiye anayemfanana sana Mtume (s.a.w) katika mazungumzo kuliko watu wote,desturi yake,mwenendo wake na tabia yake vilikuwa vinahadithia na kusimulia desturi,mwenendo na tabia ya mtume (s.a.w).Matembezi yake (a.s) {alipokuwa akitembea} ndiyo yale yale ya Mtume (s.a.w), na alikuwa kila anapoingia kwa Mtume (s.a.w),basi Mtume (s.a.w) alikuwa akimkaribisha na kubusu mikono yake na kumkarisha sehemu yake ile aliyokuwa amekaa kabla ya Fatima (a.s) kuingia.Na Mtume alipokuwa akiingia kwa Fatima (a.s),basi Fatima (a.s) alikuwa anasimama na kumkaribisha na kumbusubu mikono yake (s.a.w).

Mtume (s.a.w) alikuwa mara nyingi {zisizohesabika} akimbusu Fatima (a.s), na alipokuwa akihitajia na kuitamani harufu nzuri ya peponi, basi alikuwa akinusa harufu yake na alikuwa (s.a.w) akisema: "Fatima ni sehemu ya Nyama yangu, atakaye mfurahisha atakuwa kanifurahisha mimi na atakayemfanyia ubaya atakuwa kanifanyia ubaya mimi, Fatima ni mbora wa watu kwangu"

Na kuna mengine mengi sana ambayo yanadhihirisha mahaba kibao ya Mtume (s.a.w) kwa mwanae Fatima (a.s), kama vile kumuita Fatima (a.s) kwa jina hili: {Ya Habiybat Abiyha}-yaa ni:

{Ewe Habibi (Kipenzi)wa Baba yake}.

4

SHAHADA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S)

SEHEMU YA TANO:

KATIKA WINGI WA IBADA ZA SAYYIDAT FATIMA (A.S):

Hakuna katika Umma huu aliyekuwa ni mwenye kumuabudu sana Mwenyeezi Mungu (s.w) kuliko Fatima (a.s),alikuwa anasimama katika (swala zake) mpaka miguu yake inatuna na kuvimba. Mtume (s.a.w) alimuuliza Fatima (a.s):

Ni kitu gani ambacho ni kheri (kuliko vitu vyote) kwa Mwanamke? Fatima akasema, ni: ((Mwanamke asimuone Mwanaume na Mwanaume asimuone Mwanamke)). Mtume (s.a.w) akamkumbatia kisha akasema:

"Kizazi wao kwa wao" Na Imam Hasan bin Ali (a.s) amesimulia akisema:

Nilimuona Mama yangu Fatima (a.s) akiwa amesimama katika Mihrab (yaani sehemu yake ya kusalia) yake usiku wa Ijumaa,alibaki akiwa ni mwenye kurukuu na kusujudu mpaka asubuhi,na nilimsikia akiwaombea Waumini wa kiume na Waumini wa kike na akizidisha kuwaombea dua,na hajiombei yeye binafsi kitu chochote,nikamuuliza mama yangu: Ewe Mama yangu!: "Kwanini Hujiombei wewe mwenyewe nafsi yako kama unavyomuombea asiyekuwa wewe"? Akasema mama yangu: Ewe Mwanangu: "Jirani kisha Nyumbani"

5

SHAHADA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S)

SEHEMU YA SITA

KISA KINACHOONYESHA FADHILA ZA FIDH-DHA ALIYEKUWA MHUDUMU WA SAYYIDAT FATIMA (A.S).

Abul Qaasim Al-qash-ariy katika kitabu chake amenukuu kauli hii au kisa hiki kutoka katika kauli za baadhi ya watu wenye kufuatilia fisa na mikasa, ambapo amesema namna hii:

Wamesema baadhi yao;{Kuhusiana na alivyosimulia msimulizi mwenyewe wa kisa hiki}:Nilitengana {au niliachana} na msafara wangu {niliokuwa pamoja nao} kijijini, {Nikiwa kwenye kipando-yaani Farasi} nikakutana na Mwanamke {ambaye naye alikuwa na msafara,lakini msafara huo ukamuacha na hatimaye akapotea njia}, nikamuuliza:

Wewe ni nani? ,Yule Mwanamke akasema:

*Na uwambie maneno ya amani (yaani salam):Hivi karibuni watajua*. Nikamsalimia kisha nikamuuliza:Unafanya nini hapa? Yule Mwanamke akasema:

*Na ambaye Mwenyeezi Mungu anamuongoza hakuna awezaye kumpoteza.* Nikamuuliza;wewe ni katika Majini au ni katika wanaadam?

Yule Mwanamke akasema:

*Enyi Wanaadam! Chukueni pambo lenu* Nikamuuliza,umetokea sehemu gani? Yule Mwanamke akasema:

"Wanaitwa kutoka mahala pa mbali." Nikamuuliza:Unakusudia sehemu gani?

Yule Mwanamke akasema:

*Na ni haki ya Mwenyeezi Mungu juu ya watu kuhiji Nyumba hiyo* Nikamuuliza:Nilini umeachana na msafara wako? Yule Mwanamke akasema:

*Na bila shaka tumeziumba mbingu na Aradhi na vilivyomo kati yake kwa muda wa siku sita* Nikasema:Unahitajia chakula? Yule Mwanamke akasema:

*Wala hatukuwafanya miili isiyokula chakula*, Nikampatia chakula (akawa akila chakula ile huku tukiedelea na mwendo).Kisha nikasema:Tembea kwa haraka na ufanye haraka.

Yule mwanamke akasema:

(katika jambo loloye) ispokuwa lile iliwezalo* Nikamuuliza:Nikupandishe (pia juu ya farasi)? Yule Mwanamke akasema:

*Lau kama wangelikuwako humo (Mbinguni na Ardhini) waungu wengine ispokuwa Mwenyeezi Mungu,lazima zingeliharibika* Nikashuka na kumpandisha yeye,kisha akasema yule Mwanamke:

*Atukuzwe yeye aliyetutiisha haya* Hapa Mwanamke huyo alikusudia mnyama yule aliyempada kwamba:Kwa uwezo wa Mwenyeezi Mungu (s.w) mnyama yule (na viumbe wengine mfano wake ) kamfanya awe ni mwenye kumtii Mwanaadam,kutokana na hilo Mwenyeezi Mungu (s.w) anastahiki kutukuzwa sana maana yeye ndiye aliyetutiisha haya na lau kama si yeye basi tusingeliweza kutenda haya au tusingeliweza kuwafanya wanyama hao sisi wenyewe wawe ni wenye kututii.Na ndio maana Mwanamke huyo baada ya kupandishwa juu ya kipando kile au farasi yule,alisema kauli hii:

*Atukuzwe yeye aliyetutiisha haya* Baada ya kuufikia Msafara wa Mwanamke huyo,nikamuuliza mwanamke huyo: Kuna mtu yeyote katika msafara huu unayemfahamu? Yule mwanamke akasema: *Ewe Yahya! Shika Kitabu kwa nguvuYule Mwanamke akajibu:

*Mali na watoto ni pambo la maisha ya dunia* Baada ya vijana wale kumfikia Mama yao,Mama yao (yaani ni Mwanamke yule) akasema:

*Ewe baba!Muajiri hakika mbora uwezaje kumuajiri ni yule mwenye nguvu,mwaminifu* Mara wale vijana wakanipa baadhi ya vitu (ikiwa ni sehemu ya ujira ya kumuongoza njia Mwanamke huyo). Kisha yule Mwanamke akasema (baada ya kuwa nimeisha pokea vitu vile):

*Na Mwenyeezi Mungu humzidishia amtakae* Vijana (wale) wakaniongezea,kisha nikawauliza vijana wale kuhusiana na mwanamke yule:wakasema: "Huyu ni mama yetu,FIDH-DHA,mtumishi wa Fatimatuz-Zahraa (a.s),hajawahi kuzungumza kwa muda wa miaka ishirini ispokuwa kwa Qur'an tu."

Huyu ndiye alikuwa mtumishi wa Fatima (a.s),ambaye kuzungumza kwake ilikuwa ni Qur'an tupu,swali: Ikiwa Mtumishi anaijua Qur'an namna hii kiasi kwamba kila ukimuuliza swali anakupatia jibu kutoka ndani ya Qur'an Tukufu kwa haraka hakara kama radi vile,je itakuwa kwa Fatima (a.s) kuhusiana na Qur'an Tukufu ambaye ndiye mmiliki wa Mtumishi huyo?

Jawabu lake ni kwamba Fatima (a.s) alikuwa akiijua Qur'an Tukufu kuliko Mtu yeyote yule maana Qur'an hii imeshuka katika Nyumba ya Mtume (s.a.w) na Fatima (a.s) ni mmoja kati ya watu nyumba ya Mtume (s.a.w), hivyo (watu wa Nyumba ya Mtume -s.a.w-) Ahlul Bayt (a.s) ndio wanaoijua Qur'an Tukufu kwa maana ya kuijua, na yeyote anayejikurubisha au anayekaa karibu na Ahlul-bayt (a.s) au anaye bahatika kuipata Elimu ya Ahlul-bayt (a.s),au anayewafuata Ahlul-bayt (a.s) na kujifunza kila kitu kutoka kwao,kwa bara ya watu hawa wema waliotwaharishwa,na waliozama zaidi katika elimu,na wanaolijua jina kubwa la Mwenyeezi Mungu (s.a.w),mtu huyo atakuwa na elimu iliyo sahihi katika kila kitu,mfano mzuri ni FIDH-DHA aliyekuwa mtumishi wa Bi Fatima (a.s).

6

SHAHADA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S)

SEHEMU YA SABA

TUKIO LA KUCHOMWA MOTO NYUMBA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S).

Historia ya Kiislaam inasema kwamba, Abubakri watu walimpa (BAIA) au kiapo cha kumkubali kuwa khalifa siku ile ile aliyoaga dunia Mtume wa Mwenyeezi Mungu (s.a.w) katika sehemu moja inayoitwa SAQIYFAT BANIY SAAD; kisha wakampa baia kwa ujumla siku ya Jumatatu ambayo ilikuwa ni siku inayofuatia baada ya siku ile aliyoaga dunia Mtume (s.a.w).Lakini Saad bin Ubaada,alikataa kata kata kumbai na kumkubali Abubakri kuwa ni khalifa wa Mtume (s.a.w),pia watu wengine baadhi kwa upande wa Khazraj,na upande wa ma-Qurayshi,nao kama Saad walikataa kumbai Abubakri.wakawa upande wa Imam Ali (a.s).

Lakini watu waliowengi walikwenda upande wa Abubakri ambapo baadhi yao walilazimishwa kufanya hivyo kwa kutishiwa maisha yao kwamba endapo watapinga na kukataa kumkubali Abubakri kuwa ni khalifa wa Mtume (s.a.w) basi upanga utaangusha shingo zao,na wengine bila hata ya kulazimishwa wakambai Abubakri na kusahau au kujisahaulisha kauli ya Mtume (s.a.w) na usia wake aliokuwa akiukariri kila mara na kila sehemu mbalimbali kwamba:Ali bin abi Twalib (a.s) ni "Wasii wangu,na ni Khalifa wangu baada yangu".

Watu hao walisahau (na si kusahau bali kujisahaulisha) hata kwenda kumzika Mtume (s.a.w) siku hiyo, wakakimbilia eneo hilo la Saqiyfat Bani Saad wakiongozwa na Umar pamoja na Abubakri ili kujichagua na kugawana vyeo!!,(utadhani walikuwa wamepanga kwamba Mtume (s.a.w) akisha kufa tukapata habari basi bila kupoteza hata sekunde,tujikusanye katika eneo hili kwa uchaguzi)!.{Na hivi bila shaka yoyote ndivyo ilivyokuwa}!!.

Siku hiyo ndugu msomaji haitasahaurika madamu ulimwengu huu bado upo,Mtume (s.a.w) alizikwa na watu wachache sana siku hiyo wanaohesabika kwa vidole vya mikono.Mtu ambaye hakuna mfano wake katika Ulimwengu huu, si mwanzo wake wala mwisho wake ukampata aliyekuwa kama yeye!!,anazikwa na idadi ya kusikitisha kama hiyo!!.

Imam Ali (a.s) alipoona watu wanamkimbia, wamekuwa madhalili, hawako tiyari kumnusuru, wameacha usiwa wa mtu, wameacha kutumia elimu na kuamua kutumia matamanio yao, akawaona pia neno lao wote liko pamoja na Abubakri na Umar, wakawa wakimtukuza Abubakri, kiufupi akajihisi upweke baada ya kuondoka Mtume (s.a.w), watu wote wamemgeuka ispokuwa wachache tu, ikabidi ajikalie zake nyumbani.

Umar ambaye kipindi hicho alijikabidhi cheo cha kuwa mshauri wa Abubakri, akatoa wazo kumwambia Abubakri: Ni kitu gani kinakuzuia usimtumie mtu mtu huyu (yaani Ali a.s) ili akupe Baia (yaani kiapo cha kwamba wewe ni khalifa wa Mtume s.a.w)? Kwa hakika hajabaki mtu yeyoye ambaye hakumpa baia Abubakri ispokuwa akina Abuudhar, Salmaan Al, Faarsiy,Mikidad,Bilal Muslim na maswahaba wengine wachache sana waliokuwa waaminifu na ambao imani ilikuwa imeingia katika nafsi zao.

Abu bakri akamuuliza Umar: Tumtume mtu gani kwa Ali -(a.s)-? Umar akasema: Tumtumie Qanfadha, maana Qanfadha ni mtu mmoja mbabe sana, na ni katika (Matulaqaau-yaani wale ambao Mtume (s.a.w) aliwaachia huru baada ya kutekwa mateka siku hiyo ya Fat-hi Makka ili waende zao-).Umaru akasema: Mtu huyu pia ni mmoja kati ya kizazi cha Bani Adiyyu bin Kaabi.

Abubakri akamtuma bwana huyo Qanfadha kwa Imam Ali (a.s) akiwa na wasaidizi kadhaa, wakaenda na baada ya kufika kwa Imam Ali a.s) wakamuomba kuingia ndani, Imam (a.s) akakataa kuwaruhusu, wale wasaidizi wa Qanfadha wakaamua kurudi kwa Abubakri na Umar ambao wakati huo walikuwa wamekaa msikini, wakiwa wamezungukwa na watu,wale wasaidizi wa Qanfadha wakasema:

"Hajaturuhusu (yaani Imam Ali -a.s-) tuingie ndani" Umar bin Khattaab akasema: "Rudini! Akiwaruhusu ingineni na asipowaruhusu kuingia ingineni bila ruhusa (yake)" Wakarudi,na walipofika katika nyumba ya Fatima (a.s) wakaomba ruhusa kuingia,Sayyidat Fatima (a.s) akasema: "Nawazuia kuingia katika Nyumba yangu pasiana Idhni (yangu)" Wale wasaidizi wa Qanfadha wakarudi kwa Abubakri na Umar na Qanfadha (Aliyelaaniwa) akaganda pale pale mlangoni hataki kutoka, utadhani nyumba yake kajenga yeye!!!!!!

Walipofika kwa Umar na Abubakri wakasema: "Kwa hakika Fatima amesema kadha wa kadha na katuwekea ngumu au katuzuia kuingia katika nyumba yake pasina idhni yake." Umar akakasirika sana na akasema: "Sisi ni akina nani na wanawake ni akina nani"!! Kisha Umar mtoto wa Khattaab akatoa amri kwa watu waliokuwa wamemzunguka wakusanye kuni (popote pale watakapoziona), baada ya watu wale kukusanya kuni za kutosha, wakabeba kuni zao huku wakiongozwa na Umar wakaelekea katika nyumba ya Fatima (a.s) ambaye ni Mwanamke bora kuliko Wanawake wote wa ulimwenguni tangu kuumbwa kwa ulimwengu huu mpaka mwisho wake, walipofika katika nyumba ya Fatima (a.s) wakaziweka kuni hizo kuzunguka nyumba mzima, nadani yake kuna Imam Ali (a.s), kuna mkewe Fatima (a.s),na kuna watoto wao Hasan na Husein (a.s),kisha Umar akaita kwa sauti ya kushiba mpaka Ali na Fatima (a.s) wakasikia sauti hiyo.

"Wallah! Wewe Ali utoke nje utoe Baia Kwa Khalifa wa Mtume, kinyume chake nitawasha moto katika nyumba hii." Fatima (a.s) akasimama na akasema: Ewe Umar unanini wewe na sisi? Umar akasema: "Fungua mlango, na usipofungua mlango nitaichoma moto nyumba yenu mkiwa ndani yake" Fatima (a.s) akasema:

"Ewe Umar! Humuogopi Mwenyeezi Mungu (s.w) unataka kuingia katika nyumba yangu kwa nguvu"? Umar akakataa kuondoka na akawataka watu wake wamletee moto, moto ukaletwa, Umar akachukua moto ule na kuuwasha moto Mlango wa nyumba ya Fatima (a.s), kisha Umar akaupiga teke mlango huo na akaingia zake ndani (kwa nguvu bila ruhusa), alipoupiga teke mlango huo,Fatima (a.s) ambaye kipindi hicho alikuwa na mimba ya Muhsin (a.s) alikuwa nyuma ya mlango huo akijaribu kumzuia Umar na wenzake wasiingie ndani,hivyo akawa amezaburiwa na mlango huo baada ya kupigwa teke lililoshiba na Umar;mlango huo ukamjeruhi na kumuumiza Fatima (a.s) tumboni,Umar baada ya kuingia ndani akakumbana na Fatima (a.s) nyuma ya mlango,kisha Fatima (a.s) akapiga ukulele akiita kwa kusema:

"Ewe Baba yangu! Ewe Mjumbe wa Mwenyeezi Mungu (s.w)! Umar akainua upanga wake uliokuwa kwenye ala yake (Scabbard) na kuuweka upande wa shingo ya Sayyidat Fatima (a.s), Fatima (a.s) akapiga tena ukelele kwa sauti ya juu kabisa akiita: "Ewe Baba yangu". Basi Umar akaona afanyeje ili kumnyamazisha Fatima (a.s) aachane na ukelele huo wa Kumuita Baba yake Mtume (s.a.w).akawaza na kuwazua, likamjia wazo! Akaamua kunyanyua mjeredi wake na kumchapa nao Sayyidat Fatima (a.s) sehemu ya mgongo wake. Fatima (a.s) akaita kwa sauti ya juu:

"Ewe Mjumbe wa Mwenyeezi Mungu,ni mabaya sana waliyoyatenda nyuma yako Abubakri na Umar" Kisha Umar akawaamrisha watu wake waingie ndani na kmkamata Imam Ali (a.s) lakini Imam Ali (a.s) akawa akikumbuka wasia wa Mtume (s.a.w) aliomhusia na ahadi zake kwake.Watu hao walipoingia ndani wakamkuta Imam Ali (a.s) akiwa ameketi chini akiwa na upanga wake pembeni, Qanfadha akaogopa kumgusa Imam Ali (a.s) na akarudi nje kwa Abubakri maana alifua wazi kuwa ikiwa Imam Ali (a.s) atakasirika na kutoa upanga wake,basi eneo hilo litakuwa halitoshi na hakuna mtu atake salimika na upanga huo maana ulikuwa ni ule upanga aliopewa na Mtume (s.a.w) mkali kupindukia,Abubakri akwambia Qanfadha:

"Rudi ndani akitoka bahati yake Na asipotoka nje, basi vamia hiyo nyumba yake, Na akiendelea kukataa kutoka nje, ichome moto nyumba yao" Yule Qanfadha (Aliyelaaniwa) na wasaidizi wake wakarudi, wakaivamia nyumba yake (a.s) na kuingia ndani bila idhni. Imam Ali (a.s) akasimama ulipokuwa upanga wake, wakamuwahi waovu wale kuuzingira upanga ule, na wakazidi kuwa wengi wote wakielekea ulipo upanga ule ili kuuzingira kisawasawa na ili Imam Ali (a.s) asiweze kuuchukua na kubadilisha hali ya hewa ya pale!! Na watu hao walikuwa wengi kupingdukia.Imam Ali (a.s) akakutana na panga zao, na wakaweza kumzingira na kutupa kamba katika shingo yake, Sayyidat Fatima (a.s) akazunguka baina yao na baina ya Imam Ali (a.s) katika mlango wa nyumba yake, akijaribu kuwazuia wasiweze kumtoa nje mumewe Imam Ali (a.s), Yule bwana muovu wa waovu aliyelaaniwa, kwajina Qanfadha akampiga Fatima (a.s) kwa Mjeredi, mpaka pale Bibi Fatima (a.s) alipofariki dunia,alikuwa na alama ya mijeredi hiyo (kama vile alama za bangili au pingu) kwenye sehemu ya bega lake na sehemu ya juu ya mgongo wake karibu na shingo kwa nyuma, aliyochapwa na Umar pamoja na Qanfadha.

Kisha wakweza kumtoa nje Imam Ali (a.s) huku wakimburuza chini mpaka kwa Abubakri aliyejivalisha vazi la Ukhalifa au Uongozi wakati anajua mia kwa mia kuwa hastahiki uongozi huo,huku Umar bin Khattaab akiwa amesimama na Upanga wake katika kichwa chake (yaani pembeni kwa Abubakri),na Khaalid bin Waliid, na Abu Ubaida bin Jarraah,na Saalim bin Maula,na Abi Hudhaifa, na Maadhi bin Jabal,na Mughiira bin Shu-u-ba, na Asiidu bin Hudhairi, na Bashiiru bin Saad,na watu wengine waliokuwa wamemzunguka Abubakri wakiwa wamebeba Panga zao.

Baadae Sayyidat Fatima (a.s) akaenda moja kwa moja mpaka kwa Abubakri, akawakuta wakiwa wamemzingira Imam Ali (a.s) katika sehemu hiyo, akwamwambia Abubakri:

Ewe Abubakri! Unataka kunifanya mjane sio! kwa kuniulia Mume wangu? Wallah! Nakuapia kwa jina la Mwenyeezi Mungu (s.w)! Usipoacha kufanya hivyo, Mimi nitatawanya tawanya nywele zangu, Na kuzichana chana nguo zangu, na nitaelekea katika Kaburi Tukufu la Baba yangu (Kumshitakia haya mnayotufanyia na kumfanyia Mume wangu), na nitapiga ukelele kwa Mwenyeezi Mungu (s.w)"

Basi wakadhani labda anatania, mara Fatima (a.s) akatoka nje akiwa amewashika mikono Hasan, na Husein (a.s) akitaka kulielekea Kaburi Tukufu la Baba yake Mtume (s.a.w), Imam Ali (a.s) akasema kumwambia Salmaan:

"Mfuate na umuombe Binti ya Mtume (s.a.w) asielekea katika kaburi la Baba yake, kwa hakika mimi ninaona sehemu (yaani pande) mbili za Madina (zinagongana na) zinapinduka (endapo atafika kaburini na kumshitakia Mtume -s.a.w-), Wallah! Ikiwa atazitawanya tawanya nywele zake (Kama alivyosema), na kuvuruga vuruga na kucha chana nguo zake, na akaelekea katika kaburi la Baba yake (s.a.w), na kapiga ukelele akimshitakia Mola wake (s.w),basi Mji huu wa Madina (utageuka kichwa chini miguu juu) utaangamia na vyote vilvyokuwemo ndani ya Mji huu vitaangamia."

Salmaan radhi za Allah (s.w) ziwe juu yake, akamfuata Sayyidat Fatima (a.s) na akasema kwambia Fatima (a.s): "Ewe Bint ya Muhammad (s.a.w), Kwa hakika Mwenyeezi Mungu (s.w) amemtuma Baba yako akiwa ni Rehema, nakuomba urudi (usielekee huko unakotaka kuelekea)" Fatima (a.s) akasema: "Ewe Salmaan! Watu hao wanataka kumuua Ali (a.s) na mimi nimeshindwa kuvumilia, niacheni nielekee katika kaburi la Baba yangu, kisha nitawanye tawanye nywele zangu, na nichane chane nguo zangu, na nipige ukelele nikimlilia Mola wangu".

Salmaan akasema: "Hakiki Mimi naogopa Mji huu wa Madina usije kupatwa, na Ali (a.s) amenituma kwako akikutaka urudi Nyumbani na uachane na azimio lako." Sayyidat Fatiama (a.s) akasema: "Basi narudi, Na ninasubiri, Na ninasikia kauli, na ninamtii mume wangu"

Hivyo Fatima (a.s) akatii amri ya Mumewe Imam Ali (a.s), ambapo alikuwa kaisha likaribia kaburi la Baba yake (s.a.w),ikabidi yeye na watu wote katika kizazi cha Bani Hashim waliokuwa wametoka nje na kuandamana wakiongozwa na Sayyidat Fatima (a.s) baada ya Imam Ali (a.s) kupelekwa kwa Abubakri,wakarudi Nyumbani.

Tangu siku hiyo baada ya Bi Fatima (a.s) kuvamiwa na watu hao nyumbani kwake na kufanyiwa yote hayo waliyomfanyia mpaka kusababisha mimba yake kutoka, akaanza kuumwa, hakuweza kupona Sayyidat Fatima (a.s) kutokana na uchungu wa maumivu aliyoyapata katika tukio hilo la kihistoria na baya kuliko, maradhi hayo yakapelekea Bi Fatima (a.s) kufa Shahidi na kuiaga dunia hii.Kwa hiyo kipigo hicho namadhara ya siku hiyo aliyoyapata,ndio sababu ya Kifo cha Kishahidi cha Mbora wa wanawake wa ulimwengu mzima wa mwanzo na wa mwisho,Bi Fatima (a.s).

Laana ya Mwenyeezi Mungu (s.w) daima iko juu ya wale waliosababisha kifo chake, waliomdhulumu Mwanamke huyu (a.s), waliomuudhi Sayyidat Fatima (a.s),waliomfanya Bi Fatima (a.s) kughadhibika na kumuongezee huzuni baada ya kuwa kamkosa Baba yake (s.a.w) na kubaki Yatima,waliomvunjia heshima Mwanamke huyu ambaye ni sehemu ya Nyama ya Mtume wa Mwenyeezi Mungu (s.a.w), waliosababisha mpaka leo kaburi lake lisijulikane ni kaburi lipi kati ya yale makaburi matukufu ya Maimam (a.s) waliozikwa pale katika sehemu ya Baqii.

7

SHAHADA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S)

SEHEMU YA NANE:

USIA WA SAYYIDAT FATIMA (A.S) KWA MUMEWE ALI (A.S).

Imepokewa kutoka kwa Raudhat Al-waaidhiina na wengine, kwamba: Sayyidat Fatima (a.s) aliumwa maradhi makali sana,na alibaki muda wa siku arobaini (40 tu) katika maradhi yake mpaka alipokufa (a.s).Baada ya kujihisi kuwa hawezi kupona kutokana na maumivu makali yaliyotokana na maradhi hayo, akamuita Ummu Ayman,na Asmaau bint Amiysi wakakaa karibu naye,na Imam Ali (a.s) akiwa kando ya mkewe Fatima (a.s),kisha Fatima (a.s) akasema:

Ewe Mtoto wa Ami yangu! Kwa hakika Nafsi yangu imesha pata tangazo la kifo (Death announcement), na hakika mimi sioni mbele yangu kilichobaki ila (karibuni hivi) nitakutana na Baba yangu saa baada ya saa, na mimi nakuusia (Mume wangu) mambo kadhaa kutoka katika Roho yangu; Imam Ali (a.s) akamwambia:

"Niusie chochote kile utakachokitaka Ewe Bint ya Mtume (s.a.w)", akakaa karibu sana na Kichwa cha Bi Fatima (a.s),kisha akawatoa wote waliokuwa mahala pale katika nyumba ile,wakabaki wawili tu,kisha Faatima (a.s) akaanza kumuusia Mumewe Imam Ali (a.s) namna hii:

Ewe Mtoto wa Ami yangu! Hujanihaidi kitu chochote ukiwa ni mwenye kusema uongo au kunifanyia khiyana,na sijawahi kukukhaalif u au kwenda kinyume na kauli yako tangu tuanze kuishi pamoja;Imam Ali (a.s)akasema:Najikinga kwa Mwenyeezi Mungu,wewe ni mjuzi zaidi wa kumjua Mwenyeezi Mungu,na ni Mchamungu,Mkarimu pia na mnyenyekevu,na wewe ni mwenye Kumuogopa sana Mwenyeezi Mungu kiasi kwamba siwezi kuthubutu hata sekunde kukushakia kwamba kuna siku ulikwenda kinyume na kauli yangu (na kunikhaalif),ninasikitika sana kutengana na wewe,ispokuwa ni jambo ambalo lazima liwe,na Mwenyeezi Mungu (s.w) kaufanya msiba wa Mtume (s.a.w) kuwa mpya,na kifo chako na kutenga na wewe ni pigo kubwa sana kwangu,kwa hakika sisi wote ni wa Mwenyeezi Mungu (s.w) na sisi kwake yeye tutarejea,ni msiba mkubwa ulioje na wenye kusikitisha zaidi,Wallah! Msiba huu ni msiba usiokuwa na fanaka (yaani kitulizo au liwazo),na ni masaibu yasiyokuwa na mfano wake,kisha wote wawili wakalia kwa muda wa saa zima hivi,Kisha Imam Ali (a.s) akakichkua kichwa cha Sayyidat Fatima (a.s) na kukikumbatia katika kifua chake,kisha akasema:

Niusie chochote kile utakachokitaka, kwa hakika utanikuta ni mwenye kutekeleza yote kama ulivyoniamrisha nifanye,na nitachagua jambo lako kuliko jambo langu,kisha Fatima (a.s) akasema: Mwenyeezi Mungu (s.w) akulipe kheri ya malipo Ewe Mtoto wa Ami yangu.

Kisha akamuusia amuoe baada yake Amaama ambaye ni binti ya Dada yake Zainab,na amuandalie jeneza.na kwamba ahakikishe hashuhudii yeyote yule miongoni mwa wale waliomdhulumu na kuchukua haki yake,na ahakikishe pia hamsalii mtu yeyote miongoni mwao wala yule ambaye ni miongoni mwa wafuasi wao,na kwamba amzike usiku macho yatakapo pumzika na kulala.

Kisha alimuusia Imam Ali (a.s) awe ndiye mwenye kumuosha, na kumvisha sanda, na kumsalia, na kumshusha kabrini, na kumlaza kwenye Lahdi, Kisha akasema kumwambia Imam Ali (a.s):Na uweke udongo juu yangu,kisha ukae sehemu ya kichwa changu kuelekea uso wangu,kisha usome na uzidishe kusoma Qur'an Tukufu na Dua,hakika wakati huo ni saa {au ni muda ambao } ambayo Maiti anahitaji msaada kutoka kwa aliyekuwa hai,na mimi ninakuaga kwa Mwenyeezi Mungu (s.w) na ninakuusia kwa (watoto wangu) kizazi changu yaliyokuwa ya kheri.Kisha baada ya hapo Ummu Kulthuum akaja mahala pale alipokuwa Imam Ali (a.s) akaungana na Fatima (a.s) na baada ya Sayyidat Fatima (a.s) kuaga Dunia,Imam Ali (a.s) akafanya yote hayo aliyousiwa na Mkewe Fatima (a.s).

Pia kuna Riwaya nyingine imepokelwa kwamba: Pindi mauti yalipomfika Sayyidat Faatuma (a.s), akamwambia Imam Ali (a.s): Nitakapo kufa,basi asijue yeyote kuhusiana na kifo changu ispokuwa Ummu Salama,na Ummu Ayman,na Fidh-dha,na Wanangu,na Abbaas,na Abdullah bin Abbaas,Hakika Mimi nimekuhalalishia uweze kuniona baada ya mauti yangu, hivyo kuwa Na wanawake wale watakaoniosha, wala usinizike ispokuwa usiku na mtu yeyote asijue kabri langu" Kwa ufupi hivi ndivyo "Shahada" ya Sayyidat Fatima (s.a.w) ilivyokuwa, ambapo hakukaa muda mrefu mbora huyu baada ya kifo cha Baba yake (s.a.w) ispokuwa siku tisini na tano (95 tu).

Na siku ya kifo chake (a.s) ilikuwa ni siku ya tatu (3) ya mwezi wa Jamaadul-A'khir (yaani Jamaaduth-thaaniy), mwaka wa kumi na moja (11) baada ya Hijra.na sababu kuu ya kifo chake,ni yale mabaya walimfanyia siku ile wabaya walipoamua kuivamia nyumba yake ambapo Umar alimpiga kwa Mjeredi wake na kumbamiza kwa mlango,kisha Qanfadha aliyelaaniwa,naye akampiga kwa mjeredi wake na kumuumiza kwa amri ya Umar bin Khattaab,ambapo kutokana na masaibu hayo akapata bibi Fatima (a.s) Mimba yake ya Muhsini ikatoka na kuharibika,na akaumwa maradhi makubwa sana kuazia siku hiyo,maradhi ambayo baada ya muda mfupi mno yalipelekea Bi Fatima (a.s) kuiga dunia.Kwa hakika Bi Fatima (a.s) hakumruhusu mtu yeyote yule aliyeshiriki kumfanyia maudhi na kumdhuru aingine tena katika nyumba yake na hakuzungumza nao tena wote kuanzia siku hiyo waliomfanyia ubaya huo mpaka mwisho wa maisha yake ya hapa duniani.

Napenda kuchukua nafasi hii kuwapeni pole waislaam wote ulimwengu wenye kupemnda haki na kupinga batili,wale ambao ni maadui wa dhulma,wenye kuwapenda Ahlul-Bayt (a.s) kama Mwenyeezi Mungu (s.w) alivyotuamrisha tuwapende katika Kitabu chake Kitukufu.Hakika Msiba wa Fatima (a.s) ni msiba unaozigonga nyoyo za Waumini,ni msiba unaowafanya waumini kusikitika.Ni mazito alioyofanyiwa kiasi kwamba Baba yake (s.a.w) laiti angelikuwa hai siku ya tukio basi asingelikuwa radhi na watu hao waofu.Kwa hakika Mwenyeezi Mungu (s.w) ni Mwokozi na Mwenye kuwanusuru wale wenye kuonewa na kudhulumiwa katika Ardhi hii,na ni Mwenye Nguvu na nguvu zake zimeshinda kila kitu.Siku yaja wabaya hao watapata malipo ya mchezo wao mbaya na haramu walioucheza wa kumuua Binti na kipenzi wa mjumbe wake Muhammad (s.a.w).

MWISHO

VYANZO

Tazama: Bihaarul-Anwaar: Juzu ya 43: Ukurasa wa 10: Hadithi ya 1.

Kisha tazama: Dalaailul-Imaama: Ukurasa wa 10.

Tazama:Bihaarul-An-waar:Juzu ya 43:Ukurasa wa 218.

Tazama kisa hiki katika vitabu hivi:

1-Ruuhul-Maaniy:Juzu ya 3.Ukurasa wa 301.

2-Tafsirul-Kabiir:Juzu ya 8.Ukurasa wa 81.

3-Tafsiir Kurtubi:Juzu ya 4 .Ukurasa wa 104.

Tazama hadithi hii katika: Bihaarul-An-waar: Juzu ya 43: Ukurasa wa 23.Hadithi ya 17.

Rejea katika kitabu kiitwacho: Rabiul-Abraal: Cha Zamakhshariy utakuta habari hizi.

Tazama:Al-manaaqib:Juzu ya 3:Ukurasa wa 341.

Tazama:Ilalush-sharaayiu:Juzu ya 1.Ukurasa wa 182.

Kisha Tazama:Bihaarul-An-waar:Ukurasa wa 82.

Suuratuz-zukh-ruf:Aya ya 89.

Suuratuz-zumar:Aya ya 37.

Suuratul-Aa'raf:Aya ya 31.

Suurat Fusw-swilat(Haa Mym):Aya ya 44.

Suurat Aali Imraan:Aya ya 97.

Suuratul-Anbiyaa:Aya ya 8.

Suuratul Baqarah:Aya ya 286.

Suuratul-Anbiyaa:Aya ya 22.

Suuratuz-zukhruf:Aya ya 13.

SuuratuSwaad:Aya ya 26.

Suurat Aali Imraan:Aya ya 144.

Suurat Maryam:Aya ya 12.

Suurat Twaha:Aya ya 11 na 14.

Suuratul-Kahfi:Aya ya 46.

Suuratul-Qasas:Aya ya 26.

Suuratul-Baqarah:Aya ya 261.

Tazama Kisa hiki katika sehemu hii:

Al-manaaqib: Juzu ya 3.Ukurasa wa 343.

* Maasuudiy katika kitabu chake (ITHBAATUL-WASWIYYA) Ukurasa wa 123:Amesema:

Mara wakamvamia (yaani Imam Ali a.s), na wakauchoma moto mlango wake (mlango wa nyumba yake).

*Na Sheikh Mufiid katika kitabu chake (AL-IKHTISWAASWU) Ukurasa wa 185 mpaka 186,amesema:

"Baada ya kufika (yaani Umar na watu wake waliokuwa wamebeba kuni wakielekea katika nyumba ya Bi Fatima -a.s-) mlangoni, Umar akaupiga mlango kwa mguu wake na kuuvunja

*Ukitaka kupata habari hizi za Kushambuliwa kwa nyumba ya Fatima na kuchomwa moto mlango wa nyumba yake na kumfanyia Binti ya Mtume (s.a.w) kila aina ya Maudhi soma kitabu hiki kiitwacho:

{KITABU SULEIMU BIN QAISI}: Ukurasa wa 83 mapaka ukurasa wa 84.

Kisha soma: {BIHAARUL-ANWAAR}:Juzu ya 28.Ukurasa wa 269.

* Tazama tukio hili katika kitabu hiki kiitwacho:

{AL-IYAASHIY}: Juzu ya 2.Ukurasa wa 67.

*Pia tazama :{ BIHAARUL-ANWAAR}: Juzu ya 28: Ukurasa wa 227.

Tazama: Bihaarul-Anwaar: Juzu ya 43.Ukurasa wa 191.

Kisha tazama: Rawdhatul-waaidhiina: Juzu ya 1: Ukurasa wa 151.

Kisha tazama: Awaalimul-Uluumi: Juzu ya 6.Ukurasa wa 274.

Tazama: Bihaarul-Anwaar: Juzu ya 82: Ukurasa wa 27.

Tazama riwaya hii: Bihaarul-Anwaar: Juzu ya 43: Ukurasa wa 218.

Tazama: DALAAILUL-IMAAMA: Ukurasa wa 45.

*Mwandishi ni: Taqee Zacharia.

Anayekukaribisheni nyote katika website hii inayotumia lugha ya Kiswahili Sanifu:

FAHARASA

SHAHADA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S) 1

FATIMA (A.S) KWA MUHTASARI 1

SEHEMU YA KWANZA 2

KUZALIWA KWA SAYYIDAT FATIMA (A.S) 2

SHAHADA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S) 3

SEHEMU YA PILI: 3

IDADI YA MAJINA YA FATIMA (A.S) 3

SHAHADA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S) 4

SEHEMU YA TATU: 4

LAQABU ZA SAYYIDAT FATIMA (A.S) 4

SHAHADA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S) 5

SEHEMU YA NNE: 5

FADHILA ZA SAYYIDAT FATIMA (A.S) 5

SHAHADA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S) 7

SEHEMU YA TANO: 7

KATIKA WINGI WA IBADA ZA SAYYIDAT FATIMA (A.S): 7

SHAHADA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S) 8

SEHEMU YA SITA 8

KISA KINACHOONYESHA FADHILA ZA FIDH-DHA ALIYEKUWA MHUDUMU WA SAYYIDAT FATIMA (A.S) 8

SHAHADA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S) 10

SEHEMU YA SABA 10

TUKIO LA KUCHOMWA MOTO NYUMBA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S) 10

SHAHADA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S) 15

SEHEMU YA NANE: 15

USIA WA SAYYIDAT FATIMA (A.S) KWA MUMEWE ALI (A.S) 15

MWISHO 17

VYANZO 18