ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI

ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI 0%

ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI Mwandishi:
Kundi: Midahalo na majadiliano kielimu

ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI

Mwandishi: TIJANI SAMAWI
Kundi:

Matembeleo: 35342
Pakua: 3141

Maelezo zaidi:

ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 21 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 35342 / Pakua: 3141
Kiwango Kiwango Kiwango
ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI

ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI

Mwandishi:
Swahili

3

ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI

UIMAMU KISHIA NA KISUNNI

ITIKADI INAYOHUSU UIMAMU KWA PANDE MBILI

Makusudio ya Uimamu katika mlango huu ni ule Uimamu mkuu kwa ajili ya Waislamu, yaani nakusudia Ukhalifa, utawala, kuongoza na kusimamia.

Na kwa kuwa kitabu changu katika uchambuzi wake kimetegemea kulinganisha baina ya madhehebu ya Kisunni na yale ya Shia Imamiyyah, basi hapana budi kwanza nitoe misingi ya Uimamu kwa pande zote mbili ili imbainikie msomaji na mwenye kuchunguza ni ipi misingi na mafunzo ambayo kila upande unayategemea, na pia afahamu kukinaika kwangu ambako kulinilazimisha kukubali kugeuka na kuacha vile nilivyokuwa hapo kabla. Uimamu kwa Mashia ni msingi miongoni mwa misingi ya dini kutokana na umuhimu mkubwa ulionao na ni daraja tukufu ya kuuongoza umma bora uliotolewa kwa watu. Pia uongozi huo unazo sifa kadhaa na mambo maalumu ya kipekee yanayouhusu nami ninataja baadhi yake tu.

Miongoni mwa sifa hizo ni: Elimu, Ushujaa, Upole, Utakatifu, Kutosheka, Uchamungu, kuipa nyongo dunia na Mashia wanaitakidi kwamba Uimamu ni cheo akitoacho Mwenyezi Mungu kumpa aliyemteua miongoni mwa waja wake wema ili aweze mtu huyo kusimamia suala nyeti ambalo ni kuongoza ulimwengu baada ya Mtume (s.a.w.), na kwa msingi huu Imam Ali bin Abi Talib alikuwa ndiye kiongozi wa Waislamu kwa kuchaguliwa na Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu alimpelekea wahyi Mtume wake ili amtawalishe (Ali) kuwa kiongozi wa watu. Bila shaka Mtume wa Mwenyezi Mungu alimtawalisha na akaujulisha umma baada ya hija ya kuaga katika bonde la Khum, Waislamu nao walikula kiapo cha utii. Hivi ndiyo wasemavyo Mashia.

Ama Masunni wao pia wanasema kuwa ni lazima kuwepo Uimamu ili kuuongoza umma, lakini wao wanaupa umma haki ya kumchagua kiongozi wake, na ndiyo maana Abubakar bin Abi Quhafah alipokuwa Imam wa Waislamu kwa kuchaguliwa na Waislamu wenyewe baada ya kufariki Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) ambaye (kama wasemavyo) alilinyamazia jambo la ukhalifa na wala hakuubainishia umma kitu chochote kuhusiana na suala hilo na akaliacha liwe ni mashauriano baina ya watu. Ukweli uko wapi?

Mtu anayechunguza, akizingatia kauli za pande mbili na akafikiri kwa makini juu ya hoja za makundi haya mawili bila ya chuki basi huenda akaukaribia ukweli bila shaka yoyote. Nami hapa nitakuonesheni ukweli ambao mimi niliufikia kwa njia ifuatayo:

1. Uimamu ndani ya Qur'an Tukufu:

Mwenyezi Mungu Anasema:

"Na kumbukeni Ibrahim alipofanyiwa mtihani na Mola wake kwa amri nyingi naye akazitimiza, (Mwenyezi Mungu) akamwambia hakika mimi nitakufanya uwe kiongozi wa watu wote. Ibrahim akasema; na miongoni mwa kizazi changu (wafanye wawe viongozi) akasema, ahadi yangu haiwafikii madhalimu". (Qur'an, 2:124) Ndani ya aya hii Tukufu, Mwenyezi Mungu anabainisha kwamba Uimamu ni cheo kitokacho kwa Mwenyezi Mungu, na humpa cheo hicho yule amtakaye miongoni mwa waja wake pale aliposema: "Nitakufanya kiongozi (Imam) wa watu." Kama aya ilivyobainisha kwamba Uimamu ni ahadi toka kwa Mwenyezi Mungu hawaipati isipokuwa waja wema ambao Mwenyezi Mungu amewateua kwa ajili ya lengo hili, na hii hutokana na kuwakanusha kwake madhalimu ambao hawastahiki ahadi hiyo ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Mwenyezi Mungu amesema:

"Na tumewafanya kuwa Maimamu wanaoongoza kwa amri yetu na tukawapelekea wahyi wa kufanya mambo ya kheri na kusimamisha sala na kutoa zaka na wakawa ni wenye kutunyenyekea". Qur'an, 21:73)

Pia amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na tukawafanya miongoni mwao kuwa Maimamu wanaoongoza kwa amri yetu, (hii ni kwa kuwa) walisubiri na walikuwa wakiziamini aya zetu". (Qur'an, 32:24)

Vile vile amesema:

"Na tunataka kuwafanyia ihsani wale waliodhoofishwa katika ardhi na kuwafanya kuwa Maimamu na kuwafanya kuwa warithi". (Qur'an, 28:5)

Huenda baadhi ya watu wakafikiri kwamba aya hizi zilizotajwa zinajulisha kwamba Uimamu uliokusudiwa hapa ni Utume na Unabii, (kufikiri) hivyo ni kosa katika maana ya ujumla ya Uimamu, kwani kila Mtume ni Nabii na ni Imam, na siyo kila Imam ni Mtume au Nabii!!

Na kwa lengo hili basi Mwenyezi Mungu ameweka wazi ndani ya kitabu chake kitukufu kwamba, waja wake wema inawezekana kwao kumuomba yeye Mwenyezi Mungu cheo hiki kitukufu ili wasimamie jukumu la kuwaongoza watu, ili wapate malipo makubwa. Mwenyezi Mungu amesema:

"Na wale ambao hawashuhudii ushuhuda wa uongo na wanapopita penye upuuzi hupita kwa heshima, na wale ambao wanapokumbushwa aya za Mola wao hawaziangukii kwa uziwi na upofu, na wale wanaosema, Mola wetu tupe miongoni mwa wake zetu na watoto wetu yaburudishayo macho yetu na utujaalie kuwa Maimam wa wachamungu". (Qur'an, 25:72-74)

Kama ambavyo Qur'an vile vile imelitumia tamko la Imamah ili kujulisha viongozi na watawala madhalimu ambao wanawapoteza wafuasi na raia wao na kuwaelekeza kwenye maovu na mateso duniani na akhera.

Imekuja ndani ya Qur'an simulizi juu ya Firauni na majeshi yake pale Mwenyezi Mungu aliposema: "Basi tukamtesa yeye na majeshi yake na tukawatumbukiza baharini basi angalia ulikuwaje mwisho wao, na tuliwafanya kuwa Maimamu waitao kwenye moto na siku ya Qiyama hawatasalimishwa, na tukawafuatishia laana katika dunia hii na siku ya Qiyama watakuwa miongoni mwa wenye hali mbaya mno." (Qur. 28:40-42)

Na kwa msingi huu, kauli ya Mashia iko karibu na kile ambacho Qur'an imekithibitisha, kwa kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ameweka wazi kwa maelezo ambayo hayatoi nafasi yoyote ya mashaka, kwani Uimamu ni cheo kitokacho kwa Mwenyezi Mungu na hukiweka pale atakapo. Na cheo hicho ni ahadi ya Mwenyezi Mungu ambayo amekataa wasiipate madhalimu, na kwa kuwa mtu asiyekuwa Ali miongoni mwa masahaba wa Mtume bila shaka yoyote kuna kipindi kabla ya Uislamu alifanya ushirikina, Hapana shaka kwa ajili hiyo wanakuwa miongoni mwa madhalimu, hivyo hawastahiki ahadi ya Mwenyezi Mungu ya Uimamu na Ukhalifa, na hapo inabakia kauli ya Mashia ya kwamba Imam Ali bin Abi Talib peke yake ndiyo alistahiki ahadi ya Mwenyezi Mungu ya Uimamu kuliko Masahaba wengine, kwani yeye Ali (a.s.) hakuabudia sanamu, bali Mwenyezi Mungu ameutukuza uso wake kinyume cha Masahaba, kwani Ali hakupata kusujudia sanamu.

Na iwapo patasemwa kuwa Uislamu unafuta yaliyotendeka hapo kabla, sisi tutasema ndiyo lakini bado inabakia tofauti kubwa kati ya yule aliyekuwa mshirikina kisha akatubu na yule aliyekuwa mtakatifu na hakumtambua Mola mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu.

2. Uimamu katika Sunna ya Mtume:

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) amesema kauli nyingi kuhusu Uimamu, kauli ambazo zimenakiliwa na Mashia na Masunni ndani ya vitabu vyao na Musnad zao, kuna wakati alizungumza juu ya Uimamu kwa tamko la "Al-Imamah" na wakati mwingine kwa tamko la "Al-Khilafah" na kuna wakati alitumia tamko la "Al-Wilayah" au Al-Imarah." Kuhusu tamko la Al-Imamah imekuja kauli ya Mtume kama ifuatavyo:

"Maimamu wenu bora ni wale munaowapenda nao wanakupendeni, na mnaowaombea nao wanakuombeeni, na Maimamu wenu waovu ni wale munao wachukia nao wanakuchukieni na munawalaani nao wanakulaanini". Wakasema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu je, tuwapige upanga?

Mtume akasema, "Hapana madam wanasali sala miongoni mwenu". Taz: Sahih Muslim Juz. 6 uk. 24 Babu Khiyaril-Aimati wa Shirarihim. Na amesema Mtume (s.a.w.):

"Baada yangu watakuwepo Maimamu ambao hawatafuata muongozo wangu na wala hawatafuata suna yangu, na watakuja simama miongoni mwao watu ambao nyoyo zao ni nyoyo za shetani zikiwa ndani ya miili ya watu". Taz: Sahih Muslim Juz. 6 uk. 20 Babul-Amri Biluzumil-Jamaah Inda Dhuhuril-Fitan. Na kuhusu tamko la "Al-Khilafah" imekuja kauli yake Mtume kama ifuatavyo:

"Dini haitaacha kuwa imara mpaka kiama kitakaposimama hadi wakufikieni Makhalifa kumi na mbili na wote watatokana na Makuraishi".

Na imepokewa toka kwa Jabir bin Samurah amesema, "Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu akisema: Uislamu hautaacha kuwa na nguvu kupitia kwa Maimamu kumi na wawili, kisha alisema neno ambalo sikulifahamu, nikamwambia baba yangu,Mtume amesemaje? Akasema wote ni kutokana na Makuraishi". Na imekuja kauli ya Mtume kuhusu tamko la "Al-Imarah" kama ifuatavyo:

"Itakuwepo aina fulani ya Maamiri ambao mtawatambua na mtawapinga, mwenye kuwatambua amejitakasa na mwenye kuwapinga amesalimika, lakini yeyote atakayewaridhia na kuwafuata... Wakasema Je, tuwapige, akasema, hapana maadamu wanasali".

Taz: Sahih Muslim Juz. 6. uk. 23 Babu Wujubil-Inkari Alal-Umarai. Na amesema tena Mtume kuhusu tamko la "Al-Imarah ": "Watakuwepo Maamiri kumi na wawili wote ni Makuraishi" Taz: Sahih Bukhar Juz. 8 uk. 127. Na imekuja toka kwa Mtume (s.a.w.) akiwatahadharisha Sahaba wake: "Mtaupupia Uamiri na kutakuwa na majuto siku ya Qiyama, mwenye kunyonya ameneemeka, na aliyeacha kunyonya ameathirika." Taz: Sahih BukhariJuz, 8 uk. 106. Kama ambavyo Mtume amezungumza tena kwa tamko la "Wilayah" "Mambo ya watu hayataacha kuwa na mafanikio maadamu watakuwa wanatawaliwa na watu kumi na wawili wote ni Maquraishi". Taz: Sahih Muslim Juz. 6 uk. 3.

Na baada ya maelezo haya mafupi juu ya maf-humu ya Al-Imamah na Al-Khilafah ambayo nimeitoa ndani ya Qur'an na Sunna sahihi ya Mtume bila ya tafsiri wala taawili, bali nimetegemea vitabu vya Kisunni bila ya (kutegemea)vitabu visivyokuwa vyao miongoni mwa (vitabu vya) Mashia, kwani jambo hili (yaani la Ukhalifa wa Makhalifa kumi na wawili na wote ni Makuraishi) kwa Masunni ni katika mambo yanayokubalika na wala hakuna utata juu yake, wala hawatofautiani wawili kuhusiana nalo na hiyo ni pamoja na kufahamu kwamba baadhi ya wanachuoni wa Kisunni wanabainisha kwamba Mtume (s.a.w.) amesema: "Kutakuwepo na Makhalifa kumi na wawili wote ni katika bani Hashim." Taz: Yanabiul-Mawaddah Juz. 3uk. 104.

Na imepokewa toka kwa Shaabi, naye toka kwa Mas-Rooq, amesema: "Wakati fulani sisi tulikuwa kwa ibn Mas-ud tunaaridhi Misahafu yetu kwake basi kijana fulani akamwambia, hivi Mtume wenu alikuusieni kuwa watakuwepo Makhalifa wangapi baada yake, akasema hakika wewe ni mdogo kwa umri na jambo hili hajaniuliza mtu kabla yako, ni kweli alituusia Mtume wetu (s.a.w.) kwamba baada yake watakuwepo Makhalifa kumi na wawili kwa idadi ya Mabwana wa kizazi cha Israeli... Taz: Yanabiul-Mawaddah Juz. 3 uk. 105.

Na baada ya haya, hebu basi na tuangalie juu ya kusihi kwa madai ya kila upande kwa kuyapitia maandiko yaliyowazi kama ambavyo tutajadili taawili ya kila moja ya pande mbili hizi kuhusu suala hili muhimu ambalo limewagawa Waislamu tangu siku aliyofariki Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) mpaka leo hii, na kutokana na kutengana huko kukawa kumetokea Madh-hebu mengi na makundi mengi na mafundisho mengi ya kifikra na maneno, wakati hapo zamani Waislamu walikuwa ni umma mmoja. Basi kila tofauti iliyotolewa baina ya Waislamu sawa sawa iwe ni ya Fiqhi au tafsiri ya Qur'an au katika kuifahamu Sunna tukufu ya Mtume, basi asili yake na sababu yake ni Ukhalifa.

Ni kitu gani basi kitakujulisha huo Ukhalifa ni jambo gani? Ukhalifa ambao baada tu ya Saqifah limekuwa ni jambo ambalo kwa sababu yake hadithi sahihi na aya zilizo wazi zimekuwa zikipingwa na (badala yake) kutengenezwa hadithi nyingine zisizokuwa na msingi ndani ya sunna ya Mtume ili tu kuuthibitisha na kuupa usahihi Ukhalifa ulio patikana ndani ya Saqifa? Jambo hili linanikumbusha namna ilivyo Israel na hali halisi iliyopo, nayo ni kuwa, Wafalme na Maraisi wa (Mataifa ya) Waarabu walikutana na wakaafikiana kuwa wasiitambue nao wala amani, kwa maana kwamba kilicho chukuliwa kwa nguvu kisirudishwe ila kwa nguvu. Baada ya miaka michache (Waarabu) wakakutana upya, mara hii kwa ajili ya kuvunja uhusiano wao na Misri ambayo imetambua kuwepo kwa Wazayoni, na baada ya miaka michache wakarejesha uhusiano wao na Misri na hawakuilaani kuhusu uhusiano wake na Israel pamoja na kuwa Israel haikubaliani na haki za Taifa la Wapalestina na haikubadilisha chochote kutoka kwenye msimamo wake, bali ilizidisha kero zake na ikaongeza kuwakandamiza wananchi wa Palestina. Basi historia inajirudia yenyewe kwani Waarabu wamezoea kukubaliana na matokeo yalivyo.

MJADALA WA UKHALIFA

MAONI YA MASUNNI KUHUSU UKHALIFA NA MJADALA JUU YA HILO

Maoni yao juu ya Ukhalifa yanaeleweka, nayo ni kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alificha na hakumbainisha yeyote kushika Ukhalifa, lakini watu wenye hekima miongoni mwa Masahaba walikusanyika ndani ya Klabu ya bani Saidah na wakamtawalisha Abubakr ashike mahala pa Mtume (s.a.w.), na hiyo ni kwa sababu Mtume (s.a.w.) alimuachia kusalisha wakati wa maradhi yake, basi wakasema: Mtume wa Mwenyezi Mungu alimridhia Abubakar kwa ajili ya jambo la dini yetu basi ni kwa nini sisi tusimridhie kwa mambo ya dunia yetu?

Hivyo basi kauli ya Masunni kwa ufupi imefungamana na vifungu vifuatavyo:

1). Mtume (s.a.w.) hakumbainisha yeyote.

2). Ukhalifa hauwezi kusihi isipokuwa kwa njia ya mashauriano.

3). Kumtawalisha Abubakr ni jambo lililotendeka kupitia Masahaba wakubwa.

Bila shaka haya ndiyo yalikuwa maoni yangu wakati nilipokuwa nikifuata Madhehebu ya Malik, na nikiyatetea kwa nguvu zote nilizopewa na nikiyatolea dalili ya aya zinazohusu kushauriana, na nilikuwa nikijaribu kwa uwezo wangu kueleza kuwa dini ya Kiislamu ni dini yenye demokrasi katika maamuzi na kwamba yenyewe ndiyo iliyoanza kuweka msingi huu wa kibinaadamu, msingi ambao mataifa yaliyoendelea yanajivunia.

Zaidi ya hapo nilikuwa nikisema, "Ikiwa mataifa ya Magharibi hayakupata kuutambua utaratibu huu wa jamhuri mpaka katika karne ya kumi na tisa, basi bila shaka Uislamu umeyatangulia mataifa hayo na kuufahamu utaratibu huo tangu karne ya sita. Lakini baada ya kukutana kwangu na wanachuoni wa Kishia na kusoma vitabu vyao na kuzichunguza hoja zao zenye kukinaisha, hoja ambazo zimo ndani ya vitabu vyetu nilibadili maoni yangu ya mwanzo pale nilipopambanukiwa na hoja zilizo wazi, kwani haiwezekani kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kuuacha umma bila ya Imam (kiongozi) kwani yeye Mwenyezi Mungu ndiye asemaye: "Bila shaka wewe ni muonyaji, na kila kaumu inaye muongozaji".

Kama ambavyo haistahiki kabisa kwa mujibu wa huruma yake Mtume kuuacha umma wake bila mchungaji na hasa tutakapofahamu ya kwamba Mtume alikuwa akichelea utengano[23] wa umma wake na kurudi kinyume nyume[24] na kushindania dunia[25] kisa cha kuuana wao kwa wao[26] na kufuata nyendo za Mayahudi na Wakristo[27] Na Iwapo Ummul-Muuminina Aisha binti Abubakr alimtumia ujumbe Umar bin Al-Khattab wakati alipopigwa dharuba ya upanga (iliyopelekea kifo chake) akamwambia:

"Mtawalishe mtu juu ya umma wa Muhammad (kabla hujafa) na usiwaache watu hivi hivi tu, hakika mimi nachelea fitina juu yao." Taz: Al-Imamah wa Siyasah. Na iwapo Abdallah bin Umar naye anaingia ndani kwa baba yake alipokuwa kapigwa dhoruba hiyo ya upanga na kumwambia: "Hakika watu wanadai kwamba wewe humtawalishi mtu (baada yako) basi waonaje lau ungekuwa na mchungaji wa ngamia au mchungaji wa mbuzi kisha akaja kwako na akaiacha mifugo hiyo bila shaka itapotea, basi usimamizi wa watu ni jambo muhimu zaidi." Taz: Sahih Muslim Juz. 6 uk. 5, Baabul-Istikhlafi wa Tarkih.

Na kama Abubakr mwenyewe naye ndiye yule Waislamu walimtawalisha kwa mashauriano yeye ndiye anayebomoa msingi huo na haraka anamtawalisha Umar baada yake ili kwa tendo hilo akate mizizi ya utengano wa hitilafu na fitna. jambo hili la Abubakr kumtawalisha Umar baada yake, Imam Ali (a.s.) alilitambua mapema wakati ule Umar alipomlazimisha Imam Ali ampe Baia Abubakar, basi Imam Ali alisema kumwambia Umar: "Niandae nafasi ili wewe uwe na hisa, na leo hii nimuimarishe ili kesho akurudishiye"! Taz: Al-Imamah Was-Siyasah cha ibn Qutaibah Juz.l uk.18.

Basi mimi nasema, "Ikiwa Abubakr hayaamini mashauriano, ni vipi sisi tutaamini kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) aliliacha jambo hili bila kumuweka mtu, na je tuseme Mtume alikuwa hakijui kile walichokuwa wakikijua kina Abubakr, bibi Aisha na Abdallah bin Umar? Na ni kitu ambacho watu wote

wanakitambua moja kwa moja nacho ni kutokea hitilafu ya maoni na kila mmoja kutamani namna yake iwapo suala la kuamua lingeachwa mikononi mwao na hasa pale jambo lenyewe litakapohusu uongozi na kukalia madaraka ya Ukhalifa". Na hali hiyo ndiyo iliyotokea kwa vitendo hata kwenye uchaguzi wa Abubakr siku hiyo ya Saqifah, kwani tumeona kupinga kwa Bwana mkubwa wa Kiansar Saad bin Ubbadah na mwanawe Qais bin Saad, Ali bin Abi Talib, Zubair bin Al-Awwam,[28] Abbas bin Abdil-Mutalib, Bani Hashim wengine na baadhi ya Masahaba ambao walikuwa wakiona kuwa Ukhalifa ni haki ya Ali (a.s.) na walipinga baia hiyo na wakabakia nyumbani kwa Ali mpaka wakatishiwa kuchomwa moto.[29]

Kwa kulinganisha hayo tunaona Mashia wanathibitisha kinyume cha usemi wa Masunni na wanasisitiza ya kwamba Mtume (s.a.w.) alimbainisha Ali kuwa ni Khalifa na akatamka hili katika matukio mengi na lililo mashuhuri ni lile la Ghadir Khum. Na iwapo uadilifu unakulazimisha kumsikiliza mgomvi wako ili naye alete maoni yake na hoja zake kuhusu jambo fulani mlilohitilafiana wewe na yeye, basi hali itakuwaje iwapo mgomvi wako atatoa hoja kupitia kitu ambacho wewe mwenyewe unashuhudia kuwa kilitokea?

Na dalili za Mashia siyo dalili za kipuuzi au dhaifu mpaka uwepo uwezekano wa kuzipuuza na kujisahaulisha kirahisi, bali mambo wanayotolea ushahidi yanafungamana na aya za Qur'an Tukufu zilizoshuka kuhusu jambo hili (la Ukhalifa), naye Mtume (s.a.w.) alizipa umuhimu na udhibiti muda wote wa uhai wake, na zikanakiliwa na pande zote mbili mpaka zikavijaza tele vitabu vya historia na vile vya hadithi, nao wapokezi wakazisajili zama baada ya zama.

1. Uongozi wa Ali (a.s.) ndani ya Qur'an:

Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:

"Mtawala wenu ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wale walioamini ambao husali sala na hutoaza kahali ya kuwa wamerukuu, na yeyote atakayemtawalisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wale walioamini, bila shaka kundi laMwenyezi Mungu ndilo litakaloshinda" (Qur'an, 5:55-56)

Ameandika Abu Is-haq At-Thalabi ndani ya tafsiri yake iitwayo At-Tafsir-rul Kabir kwa Isnad ya Abu Dharri Al-Ghifari amesema: "Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa (masikio) haya mawili vinginevyo yazibe, na nilimuona kwa (macho) haya mawili vinginevyo na yapofuke akisema:"Ali ni kiongozi wa watu wema, na muangamizaji wa kufru, basi atasaidiwa atakayemsaidia, na atadhalilishwa atakayemdhalilisha.Kwa yakini mimi siku moja nilisali pamoja na Mtume, basi akaomba muombaji ndani ya Msikiti, hakuna mtu yeyote aliyempa kitu, na Ali alikuwa amerukuu basi akamnyooshea yule muombaji kidole chake kilichokuwa na pete, yule muombaji akaja akaichukua ile pete kidoleni mwa Ali, hapo Mtume (s.a.w.) akamnyenyekea Mwenyezi Mungu Mtukufu akamuomba akasema:

Ewe Mwenyezi Mungu, hakika ndugu yangu Musa alikuomba akasema: Mola wangu kifungue kifua changu na uniwepesishie jambo langu na ukifungue kifundo cha ulimi wangu ili kauli yangu ifahamike, na uniwekee waziri kutoka miongoni mwa jamaa zangu ndugu yangu Harun, ziimarishe kwake nguvu zangu ili tupate kukutakasa sana na tukutaje kwa wingi bila shaka wewe kwetu sisi ni mwenye kutuona,kisha ukampa habari (Musa) kuwa, Umepewa maombi yako Ewe Musa. Ewe Mwenyezi Mungu nami mja wako na Mtume wako nikunjulie kifua changu na uniwepesishie jambo langu na uniwekee waziri kutoka miongoni mwa jamaa zangu Ali ziimarishe kwake nguvu zangu".

Abu Dharri amesema:"Wallahi Mtume hakukamilisha maneno yake ila aliteremka Jibril na aya hii "Mtawala wenu ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wale walioamini ambao husali sala na hutoa zaka hali ya kuwa wamerukuu, na yeyote mwenye kumtawalisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wale walioamini basi bila shaka kundi la Mwenyezi Mungu ndilo litakaloshinda". Taz: Al-Jams-u Baina Sihahis-Sittah, Sahihun-Nasai, Musnad Ahmad bin Hanbal ibn Hajar ndani ya Sawaiq yake pia ameisimulia ibn Abil-Hadid ndani ya Shar-h ya Nahjul-Balagha.

Hapana ikhtilafu yoyote kwa Mashia kwamba aya hii ilishuka kwa ajili ya Ali bin Abi Talib kwa mapokezi yatokayo kwa Maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) nayo ni miongoni mwa khabari zinazokubalika kwao kwani imesimuliwa aya hii ndani ya vitabu vingi vya Kishia vinavyotegemewa kama vile:

1). Biharul-Anwar cha Majlisi 2). Ithbatul-Hudat cha Al-Hurru Al Amili 3). Tafsirul-Mizan cha Allamah Tabatabai 4). Tafsirul-Kashif cha Muhammad Jawad Mughiniyah 5). Al-Ghadir cha Al-Allamah Al-Amini na wengine wengi. Kama ambavyo imesimuliwa juu ya kushuka kwa aya hii kumuhusu Imam Ali bin Abi Talib toka kwa wanachuoni wengi wa Kisunni nitataja miongoni mwa hao wale wa Tafsiri tu:

1). Tafsirul-Kash-Shaf ya Zamakhari Juz.l uk. 649

2). Tafsirut-Tabari Juz. 6. uk. 288.

3). Zadul-Masirifill-Mit-Tafsir cha ibn Jauzii Juz.2uk. 383.

4). Tafsirul-Qur-Tibii Juz. 6 uk. 219

5). Tafsirul-Fakhrir-Razi Juz. 12 uk. 25,

6). Tafsirubni Kathir Juz. 2 uk. 71.

7). Tafsirun-Nasfii Juz. 1 uk. 289. X

8). Shawahidut-Tanzil ya Al-Haskani Al-Hanafi Juz.l uk!61.

9). Ad-Durul-Manthur Fi Tafsir bil-Maathur ya Suyuti Juz. 2

uk.293.

10). Asbabun-nuzul cha Al-Imamul-Wahidi uk. 148. 11). Ahkamul-Qur'an cha Aljas-Sas Juz. 4 uk. 102. 12). At-Tas-hilu Liulumit-Tanzil cha Alkalbii Juz.l uk. 181.

Na vitabu vya Kisunni ambavyo sikuvitaja ni vingi zaidi kuliko vile nilivyovitaja. 2. Ayatul-Balagh pia yahusika na utawala wa Ali:

Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:

"Ewe mtume fikisha uliyoteremshiwa toka kwa Mola wako, na kama hukufanya basi hukufikisha ujumbe wake, na Mwenyezi Mungu atakulinda kutokana na watu". (Qur'an, 5:67) Baadhi ya wafasiri wa Kisunni wanasema kwamba aya hii ilishuka mwanzoni mwa wito wa Uislamu pale Mtume (s.a.w.) alipokuwa akiweka walinzi wa kumlinda kwa kuchelea kuuawa, na iliposhuka kauli hii isemeyo, "Mwenyezi Mungu atakulinda kutokana na watu" Mtume akasema: "Nendeni zenu bila shaka Mwenyezi Mungu amekwisha kunilinda". Ibn Jarir na ibn Mardawaih wamethibitisha toka kwa Abdallah bin Shaqiq kuwa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu amesema: "Hakika kulikuwa na watu miongoni mwa Masahaba wake wakikaa nyuma yake (kumlinda) basi iliposhuka aya isemayo "Mwenyezi Mungu atakulinda kutokana na watu Mtume alitoka akasema:

"Enyi watu nendeni zenu, bila shaka Mwenyezi Mungu amekwisha nilinda kutokana na watu" Taz: Ad-Durul-Manthur Fit-Tafsir Bil-Maathur Juz. 3 uk. 119.

Naye ibn Hibban na ibn Mar-dawaih wamethibitisha toka kwa Abu Hurairah amesema: "Tulikuwa tukisafiri pamoja na Mtume safarini tunamuachia sehemu kubwa ya kivuli naye huketi chini yake, basi siku moja akaketi chini ya mti na akauning'iniza upanga wake kwenye mti, kuna mtu fulani alikuja akachukua upanga ule kisha kasema, Ewe Muhammad ni nani atakulinda kutokana nami? Mtume akasema, Mwenyezi Mungu ndiye atakayenilinda kutokana nawe uweke upanga huo, yule mtu akauweka na ndipo iliposhuka aya hii ya "Mwenyezi Mungu atakulinda kutokana na watu" Taz: Rejea iliyotangulia.

Ni kama ambavyo Tirmidhi na Al-Hakim na Abu Nuaim wao wametoa mapokezi toka kwa bibi Aisha amesema: "Mtume (s.a.w.) alikuwa akilindwa mpaka iliposhuka aya isemayo "Mwenyezi Mungu atakulinda kutokana na watu", akatoa kichwa chake kwenye Qubbah akasema "Enyi watu nendeni zenu hakika Mwenyezi Mungu amekwisha kunilinda". Naye Tabrani na Abu Nuaim ndani ya Ad-Dalail na ibn Mar-Dawaih na ibn Asakir wamethibitisha kutoka kwa Ibn Abbas amesema: "Mtume (s.a.w.) alikuwa akilindwa na ammi yake bwana Abu Talib ambaye alikuwa akimtumia kila siku mtu miongoni mwa Bani Hashim ili kumlinda, basi Mtume akasema ewe ammi yangu hakika Mwenyezi Mungu amekwisha kunilinda sina haja na hao unaowatuma".

Nasi tunapofanya mazingatio kuhusu hadithi hizi na taawili hizi, tunazikuta hazikubaliani na mafuhumu ya aya tukufu wala mtiririko wake, kwani riwaya zote hizi zinafidisha kwamba aya hii ilishuka mwanzoni mwa daawa hata baadhi yake zinaonyesha wazi kwamba ilikuwa ni kipindi cha uhai wa Abu Talib yaani kabla ya Hijra kwa miaka mingi, na hasa riwaya ya Abu Hurairah ambayo ndani yake anasema kuwa: "Tulikuwa tukifuatana na Mtume wa Mwenyezi Mungu safarini tunamuachia kivuli kikubwa..." Riwaya ni dhahiri kabisa kwamba ni ya kuzua, kwani Abu Hurairah hakuujua Uislamu wala kumjua Mtume (s.a.w.) isipokuwa katika mwaka wa saba wa Hijra ya Mtume kama anavyoshuhudia yeye mwenyewe[30] jambo hilo, basi ni vipi riwaya hiyo itakubalika na hali ya kuwa wafasiri wote wa Kisunni na Kishia wamekubaliana kwamba Suratul-Maidah imeshuka Madina nayo ndiyo ya mwisho kushuka katika Qur'an?

Hapana shaka Ahmad amethibitisha, naye Abu Ubaid ndani ya Fadail yake, An-Nasai, Ibnul-Mundhir, Al-Hakim, Ibnu Mar-Dawaih na Baihaqi ndani ya Sunan yake, kutoka kwa Jubair Bin Nufair amesema: "Nilihiji na kisha nikaingia kwa Aisha akasema: Ewe Jubair unaisoma Suratul-Maidah? Nikasema ndiyo, akasema bila shaka hiyo ni sura ya mwisho kushuka basi mtakacho kikuta ndani yake kuwa ni halali kihalalisheni, na mtakachokikuta ndani yake kuwa ni haramu basi kiharamisheni.[31]

Kama ambavyo wamethibitisha Ahmad, Tirmidhi, Al-Hakim, ibn Mar Dawaih na Baihaqi ndani ya Sunani yake kutoka kwa Abdallah bin Amri amesema: "Sura ya mwisho kushuka ni "Al-Maidah". Taz: Ad-Durrul-Manthur Juz. 3 uk. 3. Na amethibitisha Abu Ubaid toka kwa Muhammad bin Kaab Alqurtubi amesema: "Suratul-Maidah iliteremka kwa Mtume katika Hijja ya kuaga (akiwa) kati ya Maka na Madina hali yakuwa Mtume yuko juu ya ngamia wake, bega la ngamia yule likavunjika na Mtume (s.a.w.) akashuka."

Taz: Ad-Durrul-Manthur Juz. 1 Tafsir Bil-Maathur Juz. 3 uk. 4. Naye ibn Jarir amethibitisha toka kwa Rabii bin Anas amesema: Suratul-Maidah ilishuka kwa Mtume (s.a.w.) njiani wakati wa Hija ya kuaga Il-Hali Mtume yuko juu ya kipando chake, basi kipando hicho kikapiga magoti kutokana na uzito wa sura hiyo". Taz: Ad-Durrul-Manthur Fitafsir Bil-Maathur Juz. 3 uk.4.

Pia amethibitisha Abu Ubaid toka kwa Damrah bin Habib na A'tiyyah bin Qais wamesema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) amesema: Sura ya Maidah ndiyo ya mwisho kushuka katika Qur'an, basi ihalalisheni halali yake na muiharamishe haramu yake". Taz: Rejea iliyotangulia.

Basi ni vipi iwe kwa mtu mwenye akili, tena muadilifu atakubaliana baada ya yote haya na madai ya yule asemaye kwamba sura hiyo ilishuka mwanzoni mwa Utume? Na sababu ya kufanya hivyo ni kutaka kuigeuza toka kwenye maana yake halisi. Zaidi ya hivyo Maisha hawahitilafiani kuwa kama Suratul-Maidah ndiyo sura ya mwisho kushuka katika Qur'an na kwamba aya hii isemayo: "Ewe Mtume fikisha yale uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako...." ndiyo aya iitwayo kuwa ni aya ya 'Kufikisha' (Ayatul-Balagh) iliteremka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) siku ya kumi na nane ya mfunguo tatu baada ya Hijja ya kuaga huko kwenye bonde la Khum kwa mnasaba wa Mtume kumsimika Imam Ali bin Abi Talib mbele za watu ili awe ni Khalifa wake baada yake na hiyo ilikuwa ni siku ya Al-Khamis, Jibril alishuka na sura hiyo baada ya kupita saa tano za mchana akasema: "Ewe Muhammad Mwenyezi Mungu anakutakia amani na anakuambia: Ewe Mtume fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako na ikiwa hukufanya, basi hujafikisha ujumbe wake na Mwenyezi Mungu atakulinda kutokana na watu .

Kwa kuwa kauli ya Mwenyezi Mungu inasema: "Ikiwa hukufanya basi hujafikisha ujumbe wake" Hii inajulisha dalili iliyo wazi kwamba ujumbe (aliotumwa) umefikia mwisho au ukingoni, na kilichobakia ni jambo muhimu ambalo dini haikamiliki isipokuwa kwa jambo hilo. Kama ambavyo aya hii inavyoonesha kwamba Mtume anachelea kufanywa muongo na watu pindi atapowalingania jambo hili muhimu, lakini Mwenyezi Mungu anamtaka aitumie fursa hiyo kwani wakati umeshafika na hiyo ndiyo fursa nzuri mno na mahala pake ni mahala panapostahiki mno, kwa sababu watu. waliokusanyika pamoja na Mtume walikuwa zaidi ya laki moja ambao walifuatana naye katika Hijja ya kuaga. Isitoshe nyoyo zao zilikuwa bado zimeshikamana na mambo matukufu ya Mwenyezi Mungu na ziko tayari kupokea agizo lolote la Mtume wa Mungu naye akatangaza katika fursa hiyo habari za kwisha umri wake.

Kauli ya Mtume alipowaambia kwamba, "Huenda mimi nisikutane nanyi baada ya mwaka huu, kwani karibu atanijia mjumbe wa Mola wangu nami nitaitwa na nitaitika", watu hawa watatawanyika baada ya mkusanyiko huu unaotisha na warejee majumbani kwao na huenda wasipate fursa ya kukutana kwa mara nyingine kwa idadi hii kubwa. Na hapo Ghadir Khum ndiyo njia panda, hivyo haiwezekani kwa Muhammad (s.a.w) kuikosa fursa hii kwa namna yoyote ile.

Basi iweje imkose hali ya kuwa Wahyi umekwishamfikia kwa njia inayofanana kama onyo ya kwamba, ujumbe wote umefungwa kwenye kufikisha hili (litakiwalo hapo) naye Mwenyezi Mungu amemdhamini ulinzi kutokana na watu, hapana cha kumfanya achelee kupingwa na watu hao kwani ni Mitume wangapi kabla yake waliopingwa na hilo halikuwarudisha nyuma katika kufikisha yale waliyoamrishwa kwa kuwa ni juu ya Mtume kufikisha tu, japokuwa Mwenyezi Mungu yuwafahamu kwamba wengi wa watu hao wanaichukia haki[32] na japokuwa anafahamu kuwa wengi wao ni wapinzani,[33] hiyo haiwi sababu kwa Mwenyezi Mungu kuwaacha bila kusimamisha hoja juu yao ili watu wasije pata hoja dhidi ya Mwenyezi Mungu baada ya kufika Mitume na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu tena mwenye hekima.[34]

Na kwa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) anacho kiigizo chema kwa ndugu zake miongoni mwa Mitume waliomtangulia ambao walipingwa na watu wao. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: "Na kama wakikupinga, bila shaka walipinga kabla yao watu wa Nuhu na watu wa Adi na watu wa Thamud na watu wa Lut na watu wa Madyan, na Musa pia alikadhibishwa nikawapa muda makafiri kisha nikawatia mikononi, basi ilikuwaje adhabu yangu". (Qur'an, 22:42-44)

Nasi tutakapoacha chuki mbaya na kuacha kutetea madhehebu, bila shaka tutakuta ufafanuzi huu unakubaliana na akili na unakwenda sambamba na mtiririko wa aya na matukio yaliyoitangulia na kuifuatia. Na kwa hakika wengi wa wanachuoni wetu (wa Kisunni) wamethibitisha kwamba sura hiyo ilishuka huko kwenye bonde la Khum kuhusiana na kusimikwa kwa Imam Ali (a.s.) kuwa Khalifa, na riwaya hizo zinazohusu sura hiyo wamezithibitisha kuwa ni sahihi ndugu zao miongoni mwa wanachuoni wa Kishia na wameafikiana nao juu ya hilo nami nitataja kuonesha mfano wa wanachuoni wa(kisuni) waliolithibitisha hilo kama ifuatavyo:

1). Al-Hafidh AbuNuaim ndani ya Kitabu chake kiitwacho:

"Nuzulul-Qur 'an.

2). Al-Imamul-Wahidi ndani ya kitabu chake kiitwacho; Asbabun Nuzul uk. 150.

3). Al-Imam Abu Is-haq Ath-Thalabi ndani ya Tafsirul-Kabir.

4). Al-Hakim Al-Haskani ndani ya kitabu chake kiitwacho As-Shawahidut-TanzilLiqawaidit TafdhilJuz. 1 uk. 187.

5). Jalalud-Din As-Suyuti ndani ya kitabu chake kiitwacho Ad Durrul-Manthur Fitafsir Bil-Maathur Juz. 3 uk. 117.

6). Al-Fakhrur-Razi ndani ya Tafsirul-Kabir Juz. 12 uk. 50.

7). Muhammad Rashid Rida ndani ya Tafsir Al-Manar Juz. 2 uk. 86 Juz. 6uk. 463.

8). Tarikh Dimishq cha Abu Asakir Ash-Shafi Juz. 2 uk. 86.

9). Fat-Hul-Qadir cha Shaukani Juz. 2 uk. 60.

10). Matalibus-Suul cha Ibn Tal-hah Ashqfi Juz. 1 uk. 44

11). Al-Fusulul-Muhimmah cha IbnAs-Sabbagh Al-Maliki uk. 25

. 12). Yanabiul-Mawaddah cha Al-Qanduzi Al-Hanafi uk. 120.

13).Al-Milal Wan-Nihal cha As-Shahir Stani Juz.luk. 163.

14). Ibn Jarir A'tabari ndaniya Kitabul-Wilayah. 15). Ibn SaidAs-Sajistani ndaniya Kitabu chake Al-Wilayah.

16). Umdatul-Qarii Fit Shark Al-Bukhari cha Badrud-Din Al-Hanafi Juz. 8 uk.584.

17). Tafsirul-Qur'an cha Abdul-Wahhab Al-Bukhari.

18). Ruhul-Maani cha Al-Alusi Juz.2 uk.384.

19). Faraidus-Simtain cha Al-Hum-wayni Juz. 1 uk.185.

20). Fat-Hul-Bayan Fi Maqasidil-Qur'an cha Al-Allamah As-Sayyid Siddiq Hasan Khan Juz.3 uk.63.

Hii ni sehemu ndogo miongoni mwa vitabu vyao nilivyonavyo, lakini wako zaidi ya hawa miongoni mwa wanachuoni wa Kisunni ambao Al-Allamah Al-Amin amewataja ndani ya Kitabu cha Al-Ghadir. Basi ni jambo gani Ewe bwana alilolifanya Mtume wa Mwenyezi Mimgu (s.a.w.) pindi Mwenyezi Mungu alipomuamrisha kufikisha yale aliyoteremshiwa?

Mashia wanasema kwamba: "Mtume aliwakusanya watu kwenye uwanja huo mahala hapo paitwapo Ghadir Khum, na akawahutubia hotuba ndefu yenye kina kisha akawashuhudisha nafsi zao na wakashuhudia kwamba yeye Mtume (s.a.w.) ni bora kwao kuliko nafsi zao, na hapo ndipo alipounyanyua mkono wa Imam Ali bin Abi Talib akasema "Yeyote ambaye mimi ni mtawala wake basi huyu Ali ni mtawala wake, Ewe Mwenyezi Mungu mtawalishe atakayemtawalisha Ali na umpinge atakayempinga Ali, na umsaidie atakayemsadia na umdhalilishe atakayemdhalilisha na uipeleke haki iwe pamoja na (Ali) popote atakapokuwa." Hii ndiyo ile hadithi iitwayo Hadithul-Ghadir na wameithibitisha wanazuoni wa Kishia na wale wa Kisunni kwa maelezo ya namna moja.

Kisha Mtume alimvalisha Ali kilemba chake na akamtengenezea mahali kisha akawaamuru Masahaba wampongeze kwa kuwa kwake Amiri wa Waumini, nao wakafanya kama walivyoamriwa na Mtume (s.a.w.). Watu wa mwanzo kumpongeza walikuwa ni Abubakar na Umar na wakamwambia "Hongera Ewe mwana wa Abu Talib umekuwa mtawala wa kila Muumini mwanamume na mwanamke". Taz: Musnad Ahmad bin Hanbal Juz. 4 uk. 281. At-Tabari katika Tafsiri yake, Ar-Razi ndani ya Tafsiri yake Juz. 3 uk. 636, Ibn Hajar ndani ya As-Sawaiq, Daraqutni, Al-Bayhaqi na Al-Khatibul-Baghdadi n.k.

Walipokwisha kumpongeza, Mwenyezi Mungu akamteremshia Mtume kauli yake isemayo "Leo nimekukamilishieni Dini yenu na nimekutimizieni neema yangu na nimekuridhieni Uislamu kuwa ndiyo dini yenu". Hivi ndivyo wasemavyo Mashia, na kauli hii kwao ni katika mambo ambayo wote wanaafikiana. Basi Je, tukio hili kwa Masunni limeelezwa ili tusibakie tunaegemea kwao na tunafurahishwa na kauli yao? Bila shaka Mwenyezi Mungu ametutahadhirisha kwa kusema:

"Na miongoni mwa watu kuna ambaye kauli yake inakufurahisha hapa duniani, naye humshuhudisha Mwenyezi Mungu yale yaliyomo moyoni mwake na hali ya kuwa yeye ni mgomvi mkubwa kabisa" (Qur'an, 2:204) Basi ni wajibu tufanye tahadhari na tuichunguze maudhui hii kwa hadhari na kuzitazama dalili za pande zote mbili kwa uadilifu hali ya kuwa tukitaka radhi za Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Jawabu ni ndiyo, (tukio hili limetajwa kwa Masunni) na kwa hakika wengi miongoni mwa wanachuoni wa Kisunni wanalitaja tukio hili kwa namna lilivyo na ufuatao ni ushahidi kutoka katika vitabu vyao:

1) Imam Ahmad bin Hanbal amethibitisha kutoka kwenye hadithi ya Zaidi bin Ar-Qam amesema: " Tulishuka pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kwenye bonde liitwalo Khum, basi Mtume akaamuru paswaliwe, Mtume akaswali mchana wa joto kali,kisha akatuhutubia, na alitengenezewa kivuli kwa kutumia nguo kwenye mti kutokana na jua kisha Mtume akasema: Je, hivi hamjuwi, au je, hivi hamshuhudii kwamba mimi ni bora mno kwa kila muumini kuliko nafsi yake? Watu wakasema, kwa nini (tusishuhudie hilo) Mtume akasema, basi yeyote ambaye mimi ni mtawala wake Ali ni mtawala wake, Ewe Mwenyezi Mungu msaidie atakayemsaidia (Ali) na umfanye adui atakaye mfanya Ali kuwa niadui..."

Taz: Musnad Ahmad bin Hanbal Juz. 4 uk. 3 72. 2) Imam An-Nasai amethibitisha katika Kitabul-Khasais kutoka kwa Zaid bin Ar-Qam amesema, "Pindi Mtume (s.a.w.) aliporudi kutoka kwenye Hijja ya kuaga na akafika Ghadir Khum, aliamuru kutengenezwe vivuli na mara vikaaandaliwa kisha akasema: "Kama kwamba mimi nimeitwa na nimeitika na kwa hakika ninaacha kwenu vizito viwili, kimojawapo ni kikubwa kuliko kingine nacho kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu watu wa yumba yangu, kwa hiyo angalieni ni vipi mtanifuata ndani ya viwili hivyo, kwani havitatengana mpaka vinifikie kwenye birika, kisha akasema, bila shaka Mwenyezi Mungu ndiye mtawalia mambo yangu nami mtawalia mambo ya kila muumini, halafu akaushika mkono wa Ali akasema: "Yeyote ambaye mimi ni mtawalia mambo yake huyu (Ali) ni mtawalia mambo yake, Ewe Mwenyezi Mungu msaidie atakayemsaidia (Ali) na mfanye adui atakayemfanya adui". Abu Tufail amesema, "Nikamwambia Yazid, Je uliyasikia haya kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu" akasema, "Ndiyo, hapana aliyekuwako katika vivuli hivyo ila alimuona kwa macho yake na alimsikia kwa masikio yake". Taz: An-Nasai katika Kitabul-Khasais, uk. 21.

3) Al-Hakim An-Nishaburi amethibitisha toka kwa Zaidi Bin Ar-Qaam kwa njia mbili zilizo sahihi tena kwa sharti za Bukhari na Muslim amesema: "Wakati Mtume aliporejea toka Hijja ya kuaga alifika kwenye bonde laKhum akaamuru atengenezewe vivuli,akaandaliwa kisha akasema: "Kama kwamba mimi nimeitwa na nimeitika, na kwa hakika nimeacha kwenu vizito viwili, kimojawapo ni kikubwa kuliko kingine navyo ni kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu, basi angalieni namna gani mutanifuata katika viwili hivyo, kwani havitaachana mpaka vinifikie kwenye Haudh. Kisha akasema, hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mtawalia mambo yangu nami ni mtawalia mambo ya kila muumini, halafu akaushika mkono wa Ali akasema,Yeyote ambaye mimi ni mtawalia mambo yake basi huyu hapa (Ali) ni mtawalia mambo yake, Ewe Mwenyezi Mungu msaidie atakayemsaidia na umfanye adui atakayemfanyia uadui". Taz: Mustadrak Al-Hakim Juz. 3 uk. 109.

4) Kama ambavyo ameithibitisha hadithi hii Muslim ndani ya Sahih yake na kuitegemezea kwa Zaid bin Ar-Qam, lakini Muslim ameifupisha akasema, "Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) siku moja alisimamaakatuhutubia tulipokuwa katika bonde liitwalo Khum lililokobaina ya Maka na Madina akamtukuza Mwenyezi Mungu na kumsifu, akatoa mawaidha na akakumbusha kisha akasema, Ammabaad, fahamuni enyi watubila shaka mimi ni kiumbe, karibu atanijia mjumbe wa Mola wangu na nitaitika, naminakuachieni vizito viwili, cha kwanza ni kitabu cha Mwenyezi Mungu ndani yake kuna uongofu na kuna nuru, kishikeni kitabucha Mwenyezi Mungu namshikamane nacho, akahimiza juu ya kitabu cha Mwenyezi Mungu na akasisitizia kisha akasema, Na watu wa nyumba yangu nakukumbusheni MwenyeziMungu juu ya watu wanyumba yangu, nakukumbusheni Mwenyezi Mungu juu ya watu wa yumba yangu,nakukumbusheni Mwenyezi Mungu juu ya watu wa yumba yangu ...." Taz: Sahih Muslim Juz. 7 uk. 122 Babu Fadhail Ali ibn Abi Talib, pia hadithi hii wameitaja Imam Ahmad, Tirmidhi, ibn Asakir na wengineo.