ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI

ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI 0%

ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI Mwandishi:
Kundi: Midahalo na majadiliano kielimu

ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI

Mwandishi: TIJANI SAMAWI
Kundi:

Matembeleo: 35347
Pakua: 3141

Maelezo zaidi:

ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 21 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 35347 / Pakua: 3141
Kiwango Kiwango Kiwango
ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI

ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI

Mwandishi:
Swahili

9

ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI

QADHAA NA QADAR (KWA MASUNNI)

Katika maisha yangu yaliyopita Qadhaa na Qadar lilikuwa ni fumbo gumu, kwani sikulipatia tafsiri inayotosheleza ambayo itaipumzisha fikra yangu na kuukinaisha moyo wangu, hivyo nilibakia mwenye kuchanganyikiwa baina ya mafunzo niliyoyasoma katika madarasa ya Masunni ya kwamba mtu ni mwenye kuendeshwa (hana hiyari) katika matendo yake yote kwa yale yanayowafiki, "Kila mtu amefanyiwa wepesi kutenda aliloumbiwa" Ni kwamba (inasemwa) Mwenyezi Mungu Mtukufu huwatuma Malaika wawili miongoni mwa Malaika kwenda kwa mtoto aliye tumboni mwa mama yake na humo huandika muda wake na rizki yake na kazi yake, na kama atakuwa muovu au mwema,[90] (nilibaki ndani ya itikadi hii hali ya kuwa nimechanganyikiwa hivyo) na baina ya kile ambacho kinashinikizwa na akili yangu na nafsi yangu katika uadilifu wa Mwenyezi Mungu Mtukufu na kutokuwa kwake dhalimu kwa viumbe wake. Itakuwaje awashinikize kwenye matendo fulani kisha awaadhibu kwa ajili ya makosa aliyowaandikia na akawashinikiza wayafanye?

Hapana shaka nilikuwa kama wengine miongoni mwa vijana wa Kiislamu nikiishi katika fikra hizo zinazogongana katika mtazamo wangu kwamba, Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye yeye mwenye nguvu mwenye uwezo ambaye haulizwi yale ayatendayo nao viumbe wataulizwa (Qur'an 21:23). Naye ni mwenye kufanya alitakalo (Qur'an 85:16). Amewaumba viumbe akawagawa, sehemu fulani miongoni mwao itakuwa peponi na sehemu nyingine motoni, kisha yeye ni mwingi wa rehma mpole mwenye kurehemu waja wake, hadhulumu kiasi hata cha chembe ndogo (Qur'an, 4:40). "Na Mola wako si mwenye kuwadhulumu waja" (Qur'an Fus-silat, 46). "Bila shaka Mwenyezi Mungu hawadhulumu watu chochote lakini watu wanajidhulumu nafsi zao (Qur'an. 10:44).

Kisha yeye Mwenyezi Mungu ni mwenye huruma mno kuliko mwanamke alivyo na huruma kwa mwanawe kama ilivyokuja ndani ya hadithi tukufu. BukhariJuz. 7 uk. 75. Na ni mara nyingi kulikuwa kukijitokeza kupingana ndani ya akili yangu kuhusu aya za Qur'an Tukufu, kwani wakati mwingine nilikuwa nikifahamu kwamba mtu anafahamu ndani ya nafsi yake naye peke yake ndiye mwenye jukumu la matendo yake. "Basi yeyote atakayetenda wema wenye uzito wa chembe (ndogo) atauona (wema huo) na yeyote mwenye kutenda uovu wenye uzito wa chembe (ndogo) atauona (uovu huo)." (Qur'an, 99:7-8)

Na wakati mwingine nilikuwa nikifahamu kwamba, mtu ni mwenye kuendeshwa na hana ujanja wala nguvu, hana mamlaka ya nafsi yake kujinufaisha, na au kukinga madhara wala namna ya kutafuta rizki. "Wala hamtataka (kitu) isipokuwa atake Mwenyezi Mungu" (Qur'an, 76:30). "Mwenyezi Mungu humpotoa amtakaye na humuongoa amtakaye" (Qur'an 35:8). Na siyo mimi peke yangu bali Waislamu wengi wanaishi katika hali hii ya kupingana kifikra na ndiyo maana utawakuta Masheikh wengi na wanachuoni pindi unapowauliza juu ya maudhui ya Qadhaa na Qadar huwa hawapati jawabu la kukinaisha nafsi zao wenyewe kabla ya kuwakinaisha wengine bali wao husema, "Maudhui hii si lazima kuingia kwa undani". Kuna baadhi yao huharamisha kuichimbua kwa undani na husema: "Inapasa kwa Muislamu kuamini Qadhaa na Qadar za kheri na shari, na kwamba zote zinatoka kwa Mwenyezi Mungu."

Na pindi mpinzani anapowauliza: "Ni vipi Mwenyezi Mungu atamshinikiza mja wake kutenda maovu kisha amtupe motoni"? Basi Masheikh hao humtuhumu kukufuru na uzandiki na kuwa eti ametoka katika dini, na tuhuma nyinginezo mbaya zisizokuwa hizo. Na kwa sababu hiyo akili (za watu) zimepooza na kutindia, imani (zao) zinaamini kwamba kuoa (hakupatikani ila) kama umeandikiwa, na talaka ( nayo haituki ila) kama imeandikwa, na hata kuzini (nalo ni suala la) kuandikiwa kwani wanasema, "Kila utupu umeandikiwa jina la yule utakayemuoa. Si hivyo tu,bali hata kunywa pombe, kuua nafsi na hata kula na kunywa huwezi kula wala kunywa isipokuwa kile alichokuandikia Mwenyezi Mungu!

Niliwaambia baadhi ya wanachuoni wetu (wa Kisunni) baada ya kuyaaridhi mas-ala haya kwamba, "Qur'an inapinga madai haya na wala haiwezekani kwa hadithi kuipinga Qur'an!! Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema kuhusu jambo la kuoa "Waoweni muwapendao katika wanawake" (Qur'an, 4:3) Aya hii inajulisha juu ya kuwa na hiyari, na amesema Mwenyezi Mungu kuhusu talaka, "Talaka ni mara mbili, kisha ni kukaa kwa wema au kuachana kwa wema" (Qur'an, 2:229). Hii nayo pia ni hiyari. Na kuhusu zinaa amesema, "Musiikurubie zinaa hakika ni jambo chafu na ni njia mbaya (Qur'an, 12:32).

Hii nayo ni dalili ya kuwa na hiyari. Kuhusu pombe amesema, "Hakika shetani anataka kukutilieni uadui na bughdha baina yenu kwa ajili ya pombe, na kamari, na anataka kukuzuwieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali basi komeni (kunywa pombe) (Qur'an5:91). Nayo pia inakataza kwa maana ya kuwa na hiyari. Amma kuua nafsi Mwenyezi Mungu amesema kuhusiana na jambo hilo,"Na msiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharamisha (kuiua) isipokuwa kama kuna haki (ya kuuawa)" (Qur'an, 6:151) Na amesema tena Mwenyezi Mungu: "Na yeyote atakayemuua Muumini kwa kukusudia, basi malipo yake ni motoni, ataishi humo milele, na Mwenyezi Mungu amemkasirikia,amemlaani na amemuandalia adhabu kali" (Qur'an, 4:93) Aya hii pia inaonyesha hiari kuhusu kuua. Na hata mambo yanayohusu kula na kunywa, Mwenyezi Mungu ametuwekea mipaka akasema: "Na kuleni na mnywe lakini msivuke mipaka hakika yeye Mwenyezi Mungu hawapendi wanaovuka mipaka" (Qur'an 7:31). Kadhalika hii inaonyesha hiyari.

Basi ni vipi ewe Bwana wangu baada ya dalili zote hizi za Qur'an ninyi (bado) mwasema kwamba kila kitu kinatokana kwa Mwenyezi Mungu na mja yeye ni mwenye kuendeshwa katika matendo yake yote? Alinijibu akasema kwamba, "Mwenyezi Mungu Mtukufu yeye peke yake ndiye ambaye anauendesha ulimwengu na akatolea ushahidi kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: "Sema: Ewe Mola uliyemiliki ufalme wote, humpa ufalme umtakaye, humuondolea ufalme umtakaye, humtukuza umtakaye, na humdhalilisha umtakaye, kheri imo mkononi mwako bila shaka wewe ni mwenye uwezo juu ya kilakitu".(Qur'an,3:26) Mimi nikasema: "Hapana hitilafu yoyote baina yetu juu ya kutaka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na pindi anapotaka kufanya jambo, mtu au jini wala viumbe wengineo hawana uwezo wa kupinga kutaka kwake, bali hitilafu iliyopo ni kuhusu matendo ya waja, je, matendo hayo yanatokana na waja au yanatokana kwa Mwenyezi Mungu"?

Akanijibu: "Ninyi muna dini yenu nami nina dini yangu" Hapo akaufunga mlango wa majadiliano kutokana na usemi huo. Basi hizi mara nyingi ndizo hoja za wanachuoni wetu, na ninakumbuka kwamba nilirejea baada ya siku mbili nikamwambia "Ikiwa itikadi yako ni kwamba Mwenyezi Mungu ndiye atendaye kila kitu na waja hawana hiyari ya kufanya chochote, basi ni kwa nini husemi kuhusu Ukhalifa kama hivi usemavyo, ya kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu yeye ndiye mwenye kuumba na kuchagua na wao (waja) hawana hiyari"? Akasema: "Ndiyo hivyo ndivyo nisemavyo, kwani Mwenyezi Mungu ndiye aliyemchagua Abubakar na Umar na Uthman kisha Ali, lau Mwenyezi Mungu angelimtaka Ali awe ndiye Khalifa wa kwanza, basi watu na majini wasingeweza kulizuwia jambo hilo." Mimi nikasema:"Sasa umenasa." Akasema, "Kwa vipi nimenasa?" Nikasema: "Basi imma useme kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliye wachagua hao Makhalifa wanne kisha baada ya hapo akawaachia watu uamuzi wa yule wamtakaye, na imma useme kwamba Mwenyezi Mungu hakuwaachia watu uamuzi wa kumchagua wamtakaye bali yeye ndiye humchagua kila Khalifa tangu kufariki Mtume mpaka siku ya Qiyama"

Akajibu: "Nasema tena mara ya pili, "Sema, Ewe Mola uliyemiliki ufalme wote, unampa ufalme (mtu) umtakaye na unamuondolea ufalme umtakaye " Nikamwambia, "Kwa hiyo kila upotofu na kila maovu yaliyotokea katika Uislamu kutokana na wafalme na watawala yote yanatokana kwa Mwenyezi Mungu, kwani yeye ndiye aliyewatawalisha watu hawa juu ya shingo za Waislamu? Akajibu: "Ndivyo ilivyo na miongoni mwa wema wako waliosoma hivi, "Na tukitaka kuangamiza kijiji tunawapa amri watu wa kijiji wanaishi kwa raha yaani tunawafanya maamiri" Nikasema hali ya kushangazwa:"Kwa hiyo kuuawa kwa Ali kwa mkono wa Ibn Mul-Jam na kuuawa Husein bin Ali ni kutaka kwake Mwenyezi Mungu"?

Akasema katika hali ya kujitetea: "Naam, moja kwa moja, je, hukupata kuisikia kauli ya Mtume kumwambia Ali, "Mtu muovu mno katika watu wa hapo baadaye ni yule atakayekupiga juu ya hiki mpaka zilowane hizi, na akaashiria kichwa chake (Ali) na ndevu zake, na hivyo hivyo Imam Husein, Mtume (s.a.w.) aliyafahamu mauaji yake huko Karbala na alimsimulia mama Ummu Salama juu ya mauaji hayo, kama ambavyo Mtume alifahamu kwamba Sayyidna Hassan Mwenyezi Mungu ataleta upatanishi kupitia kwake kati ya makundi mawili makubwa miongoni mwa Waislamu. Basi kila kitu kimeandaliwa na kuandikwa tangu hapo zamani na mtu hana njia ya kukwepa, na kwa hali hii wewe ndiyo umenasa na siyo mimi."

Nilinyamaza kidogo na kumuangalia hali ya kuwa anatamba kwa maneno haya, akidhani kwamba ameninyamazisha kwa dalili madhubuti, (nikitafakari) ni vipi nitamkinaisha ya kwamba kujua kwa Mwenyezi Mungu juu ya kitu fulani haimaanishi moja kwa moja kwamba yeye ndiye aliyekadiria na kuwashinikiza watu juu ya kitu hicho, nami natambua tangu hapo mwanzo kwamba fikra yake haiwezi kuzingatia nadharia kama hii. Nilimuuliza tena mara nyingine: "Kwa hiyo marais na wafalme waliopita na waliopo sasa ambao wanaupiga vita Uislamu na Waislamu, Mwenyezi Mungu ndiye aliyewatawalisha? Akasema, "Bila shaka". Nikamwambia, "Hata wakoloni wa Kifaransa walioitawala Tunisia, Al-geria na Morocco nao ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu". Akasema: Ndiyo, kwani pindi ulipofika wakati maalum Wafaransa waliondoka kwenye nchi hizo". Mimi nikasema: Sub-hanallah!! Basi ni vipi ulikuwa ukiitetea nadharia ya Masunni kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alikufa na kuliwacha jambo la Ukhalifa liwe la mashauriano baina ya Waislamu ili wamchague wamtakaye"? Akasema:"Mpaka sasa bado niko kwenye msimamo huo na nitabakia hivyo kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu".

Nikasema: "Basi ni vipi unakubaliana na kauli mbili, uchaguzi wa Mwenyezi Mungu na uchaguzi wa watu kwa mashauriano"? Akasema:"Hiyo ni kwa kuwa Waislamu walimchagua Abubakar basi bila shaka Mwenyezi Mungu kishamchagua"! Nikasema: "Aliwateremshia Wahyi (ufunuo) hapo Saqifah kuwajulisha juu ya kumchagua Khalifa"? Akasema:Astaghfirullah!!(Mwenyezi Mungu anisamehe) hapana Wahyi baada ya Muhammad kama wanavyoamini Mashia. (Mashia kama inavyofahamika hawaitakidi jambo hili bali hizo ni tuhuma zilizoambatanishwa kwao na maadui zao). Mimi nikasema: "Hebu tuachane na Mashia na uzushi wao, na ututosheleze kwa maelezo uliyonayo, ni vipi wewe umefahamu kwamba Mwenyezi Mungu alimchagua Abubakar"?

Akasema "Lau Mwenyezi Mungu angetaka kinyume cha hivyo basi, Waislamu na walimwengu wote wasingeweza kwenda kinyume cha vile atakavyo Mwenyezi Mungu". Basi hapo nilikumbuka kisa kingine nilipokuwa nikitembea katika shamba fulani pamoja na rafiki yangu, shamba ambalo lilikuwa na Mitende mingi nami nilikuwa nikimsimulia juu ya Qadhaa na Qadar, basi ghafla ilidondoka tende mbivu juu ya kichwa changu, nami nikaichukua toka kwenye majani ili niile na nikaiweka kinywani mwangu. Rafiki yangu alishangaa hali ya kuwa anasema: "Huwezi kula ila kile alichokuandikia Mwenyezi Mungu tende hii imedondoka kwa ajili yako". Mimi nikasema:"Maadamu wewe unaamini kwamba tende hiyo nimeandikiwa basi mimi sitaila" nikaitema. Akasema,"Subhanallah!! Ikiwa kitu hakikuandikwa kwa ajili yako, Mwenyezi Mungu atakitoa hata kama kimo tumboni mwako." Nikasema:"Kama ni hivyo basi nitaila" nikaiokota tena na kuimeza.

Hapo akasema:"Wallahi tende hiyo imeandikwa kwa ajili yako (akiwa na maana Mwenyezi Mungu amekuandikia) akawa amenishinda kwa njia hiyo kwani siwezi tena kuitoa tende hiyo tumboni mwangu. Naam, basi hiyo ndiyo itikadi ya Masunni kuhusu Qadhaa na Qadar au (ukipenda) sema hii ndiyo iliyokuwa itikadi yangu nilipokuwa sunni. Na kwa mujibu wa hali halisi ni kwamba (hali hii) inatufanya tuishi kutokana na itikadi hii tukiwa ni wenye kuchanganyikiwa kifikra baina ya mambo yanayopingana, na moja kwa moja tutabakia hivyo hivyo tunasubiri Mwenyezi Mungu atubadilishie mambo yetu, badala ya sisi wenyewe kubadili ili Mwenyezi Mungu atubadilishie, na tunakwepa majukumu ambayo tumeyabeba na tunamtupia majukumu hayo yeye Mwenyezi Mungu. Iwapo utamshutumu mzinifu au mwizi au hata muovu ambaye kamteka msichana asiyejiweza na akamuua baada ya kumaliza matamanio yake basi atakujibu kwa kusema "Mwenyezi Mungu ndiye mwenye nguvu, Mola wangu amenikadiria.

Nashangazwa, Mola huyu huyu anamuamuru mtu amzike binti yake akiwa hai kisha atamuuliza ni kwa kosa gani binti. huyu aliuawa? Umetakasika Ewe Mwenyezi Mungu, bila shako, huu ni uzushi mkubwa (uliozushwa). Ni jambo la kawaida wataalamu wa kimagharibi wanavyotudharau na kutucheka kutokana na akili yetu mbovu, bali wanatupachika majina na kutuita; "Waarabu walioandikiwa " na huifanya kuwa ndiyo sababu ya msingi ya ujinga wetu na kutokuendelea kwetu. Pa ni kawaida watu wenye kuchunguza wafahamu kwamba itikadi hii ilianza toka kwenye dola ya Banu Umayyah ambao walikuwa wakieneza uzushi kwamba, Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye aliyewapa ufalme na akawatawalisha juu ya watu, basi ni wajibu kwa watu kuwatii na kutokuwapinga, kwani yeyote mwenye kuwatii kamtii Mwenyezi Mungu, na mwenye kuwapinga basi kampinga Mwenyezi Mungu na ni lazima auawe.

Na kuhusu jambo hili tunao ushahidi mwingi kutoka katika historia ya Kiislamu: Huyu hapa Uthman bin Affan alipotakiwa ajiuzulu anapinga na kusema, "Siwezi kuivua kanzu aliyonivalisha Mwenyezi Mungu " Taz: Tarikh Tabari Hisar Uthman, pia Tarikh Ibn Athir. Basi kwa mtazamo wake (Uthman) Ukhalifa ni vazi la Mwenyezi Mungu kamvalisha, haipasi kwa yeyote miongoni mwa watu kumvua isipokuwa Mwenyezi Mungu, yaani kwa labda afe. Huyu hapa naye Muawiyyah pia anasema: "Kwa hakika mimi sikuwapigeni ili mfunge na mtoe zaka, bali nimewapigeni ili niwatawaleni, na bila shaka Mwenyezi Mungu amenipa hilo hali ya kuwa hamtaki". Taz: Maqatilut-Talibin uk. 70, Ibn Kathir Juz. 8 uk. 131 Ibn Abil-Hadid Juz. 3 uk. 16.

Na hata kumchagua mwanawe Yazid na kumtawalisha juu ya watu bila ridhaa yao, Muawiya alidai kwamba Mwenyezi Mungu ndiye aliyempa Ukhalifa mwanawe Yazid juu ya watu, na hilo wamelisimulia wanahistoria pale Muawiyah alipoandika baia yake na kuisambaza sehemu mbali mbali, na Gavana wake huko Madina alikuwa Mar-wan bin Al-Hakam, akamuandikia kile ambacho Mwenyezi Mungu (kwa mujibu wa madai yake) amekipitisha kupitia ulimi wake kuhusu baia ya Yazid. Taz: Al-Imamah Was-Siyasah Juz. 1 uk. 151 Baiatu Muawiya Liyazid Bis-Sham. Hivyo hivyo ndivyo alifanya yule muovu ibn Ziyad, pale walipomuingiza Imam Ali Zainul-Abidin kwa huyo ibn Ziyad hali yakuwa (Imam Zainul Abidin) kafungwa kwa minyororo basi aliuliza akasema:"Ni nani huyu" wakasema, "Ni Ali bin Husain" Akasema, Je, Mwenyezi Mungu hajamuua Ali bin Husayn"? Bibi Zainab shangazi yake Imam Zainul-Abidin akamjibu, "Sivyo bali waliomuua ni maadui wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake".

Ibn Ziyad akamwambia bibi Zainab: "Waonaje ni jinsi gani Mwenyezi Mungu alivyowafanya watu wa nyumba yako". Bibi Zaynab akasema:"Sikuona isipokuwa wema tu, hawa ni watu ambao Mwenyezi Mungu amewafaradhishia kuuawa, walitoka hadi kwenye malazi yao, na Mwenyezi Mungu atakukutanisheni wewe na wao kisha muhojiane na kusutana, basi zingatia ni nani atakayeshindwa siku hiyo, mama yako akuhuzunikie ewe mwana wa Mar-Janah". Taz: Maqatilut-Talibin, Maq-Talul-Husayn. Basi hivi ndivyo ilivyoenea itikadi hii itokayo kwa Bani Ummayyah na wasaidizi wao na wakaisambaza ndani ya umma wa Kiislamu isipokuwa Mashia (Wafuasi) wa watu wa Nyumba ya Mtume (s.a.w.).

ITIKADI YA MASHIA KUHUSU QADHAA NA QADAR

Tangu nilipowafahamu wanachuoni wa Kishia- k.m. Shahid Muhmmad Baaqir As-sadri aliyenitosheleza mambo mengi kuhusu maudhui hii (Mwenyezi Mungu amrehemu) pia Sayid Al-khui na Al-allaamah Muhammad Ali Tabatabai na Sayid Hakiim na wengineo na kusoma vitabu vyao niligundua elimu mpya inayohusu Qadhaa na Qadar. Na bila shaka Imam Ali alikwisha kuifafanua kwa ubainifu mkubwa mno unaoenea pale alipomwambia mtu aliyemuuliza juu ya Qadhaa na Qadar. "Ole wako huenda wewe umedhania Qadhaa ya lazima na Qadar iliyokwishapitishwa, basi lau ingekuwa hivyo, thawabu na adhabu vingebatilika na ahadi na maonyo vingeporomoka. Bila shaka Mwenyezi Mungu amewaamuru waja wake kwa kuwahiyarisha na akawakataza kwa kuwatahadharisha, na akakalifisha mambo mepesi wala hakukalifisha mambo mazito, na hakuasiwa eti kwa kuwa ameshindwa na wala hakutiiwa hali ya kukarahisha, na hakuwatuma Manabii kwa ajili ya mchezo na wala hakuwateremshia waja vitabu kwa ajili ya upuuzi, na wala hakuumba mbingu na ardhi bure bure, hiyo ni dhanna ya wale waliokufuru, basi ole wao wale waliokufuru (wataadhibiwa adhabu ya) moto".

Taz: Sharh Nahjul-Balaghah ya Sheikh Mohammad Abdooh Juz. 4 uk. 673. Basi ubainifu ulioje, sijapata kusoma maneno yenye ufafanuzi wa kina na hoja inayojulisha ukweli kuliko maneno hayo (ya Ali), basi Muislamu hutosheka (na akafahamu) kwamba matendo yake yanatokana na kutaka kwake halisi na uamuzi wake, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu ametuamuru lakini akatuachia uhuru wa kuamua nayo ndiyo ile kauli ya Imam Ali aliposema, "Bila shaka Mwenyezi Mungu amewaamrisha waja wake kwa kuwahiyarisha ". Kama ambavyo Mwenyezi Mungu ametukataza na akatutahadharisha kutokana na adhabu iwapo tutamkhalifu, basi maneno yake yakajulisha ya kwamba mtu anao uhuru wa kutenda na anao uwezo wa kwenda kinyume na amri za Mwenyezi Mungu, na katika hali hii inamuwajibikia adhabu na hiyo ndiyo ile kauli ya Imam Ali (a.s.) aliposema, "Na akawakataza kwa kuwatahadharisha ". Zaidi ya hapo Imam Ali (a.s.) aliongeza kuyafafanua mas-ala haya akasema kwamba, "Mwenyezi Mungu Mtukufu hakuasiwa eti kwa kuwa amezidiwa". Na maana ya hayo ni kwamba lau Mwenyezi Mungu angetaka kuwashinikiza waja wake na kuwalazimisha kufanya kitu, basi wote wasingekuwa na uwezo wa kumshinda kuhusu amri yake. Hapo (Imam Ali) amejulisha ya kuwa Mwenyezi Mungu amewaachia (waja wake) uhuru wa kuamua kutii au kuasi, na (kauli hii) inathibitisha kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema, "Wambie huu ni ukweli utokao kwa Mola wenu, atakaye na aamini na atakaye akufuru." (Qur'an, 18:29)

Kisha baada ya hayo Imam Ali (a.s.) anaielekeza dhamira ya mtu ili iweze kufikia undani wa hali yake halisi, analeta dalili madhubuti na isemayo,"Lau mtu angekuwa ni mwenye kulazimishwa juu ya matendo yake kama wanavyoitakidi baadhi ya watu, basi kutumwa kwa Mitume na kuteremshwa vitabu ni aina ya mchezo na upuuzi, jambo ambalo Mwenyezi Mungu ametakasika nalo, kwani nafasi ya Manabii wote na kuteremshwa vitabu vyote ni kwa ajili ya kuwarekebisha watu na kuwatoa kwenye kiza, kuwapeleka kwenye nuru na kuwapa tiba yenye manufaa juu ya maradhi yao ya kinafsi na kuwabainishia njia bora ya maisha mazuri, Mwenyezi Mungu anasema, "Bila shaka hii Qur'an inaongoza katika njia iliyonyooka mno." (Qur'an, 17:9).

Imam Ali (a.s.) anakamilisha kwa kubainisha kwamba, itikadi ya watu kuwa ni wenye kulazimishwa katika matendo yao ni itikadi inayomaanisha kuwa, "Mwenyezi Mungu ameumba mbingu na ardhi na vyote vilivyomo bure bure tu." Hii ni kufru na Mwenyezi Mungu amewaonya wasemao hivyo kwa adhabu ya moto. Na tunapoichambua kauli ya Mashia kuhusu Qadhaa na Qadar tunaikuta kuwa ni kauli ya sawa na ni rai muafaka. (Ni vema ifahamike kwamba), wakati kikundi fulani kilipochupa mpaka na kikaitakidi itikadi ya "Jabri" (kutenzwa nguvu) kmgine nacho kikachupa mpaka kikaamini kuwa kuna "Taf-widh"(uhuru usiyo na mipaka). Hapo watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) wakaja kusahihisha Maf-hum (ufahamu) wa itikadi na kuwakosoa jamaa hawa na wale wao wakasema: "Hapana Jabri (kutenzwa nguvu) wala Taf-widh (uhuru usiyo na mipaka) lakini liko jambo baina ya mawili hayo". Taz: Itikadi za Mashia Juu ya Qadhaa na Qadar.

Naye Imam Jaafar As-Sadiq amepiga mfano ulio wazi juu ya jambo hilo, mfano ambao watu wote wanaweza kuufahamu kwa kadiri ya akili zao, nao ni pale alipomwambia muulizaji aliyeuliza: "Ni nini maana ya kauli yako kwamba hapana Jabr wala Taf-widh lakini liko jambo baina ya mawili hayo"? Imam Jaafar alimjibu muulizaji huyo (akasema) "Kutembea kwako juu ya ardhi siyo sawa na kuanguka kwako juu ya ardhi hiyo". Na maana ya maneno hayo ni kuwa, sisi tunatembea juu ya ardhi kwa hiyari yetu, lakin pindi tunapoanguka ardhini hilo siyo kwa hiyari yetu, kwani ni nani basi miongoni mwetu apendaye kuanguka jambo ambalo huenda likasababisha kuvunjika kwa baadhi ya viungo katika miili yetu na hatimaye kuwa vilema?

Hapo ndipo Qadha na Qadar inapokuwa ni jambo moja baina ya mambo mawili, yaani sehemu fulani inatokana nasi na kwa utashi wetu nasi ndiyo tuitendayo kwa kutaka kwetu kikamilifu, na sehemu ya pili iko nje ya matakwa yetu nasi ni wenye kuikubali tu (kuitii) na wala hatuwezi kuizuwia, basi tutaulizwa kwa ile sehemu ya kwanza na hatutaulizwa kwa hii sehemu ya pili. Hivyo basi katika hali hii na ile mja ni mwenye kuhiyarishwa na ni mwenye kuendeshwa kwa wakati huo huo. A. Ni mwenye kuhiyarishwa katika matendo yake ambayo yanatokana naye baada ya kufikiri na kutambua, kwani hapo huwa anapita katika nyanja za hiyari na upinzani baina ya kutenda au kujizuwia kutenda, na mwishoni mwake mambo huwa ni imma atende au asitende, na hiki ndicho alichokiashiria Mwenyezi Mungu Mtukufu aliposema: "Na (ninaapa) kwa roho na aliyeitengeneza, kisha akaifahamisha uovu wake na wema wake, bila shaka amefaulu aliyeitakasa nafsi yake". (Qur'an, 91:7-9).

Kuitakasa nafsi na kuichafua ni matokeo ya hiyari ya dhamira ipatikanayo kwa kila mtu, kama yalivyo mafanikio na kutofanikiwa vitu ambavyo moja kwa moja ni matokeo yanayokwenda sambamba na utashi. B. Mtu ni mwenye kuendeshwa katika kila yale ambayo yamzungukayo miongoni mwa siri za ulimwengu na nyendo zake zote ambazo zinatii atakavyo Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kila sehemu zake (hizo siri za ulimwengu) na maumbile yake, sayari zake na nguvu zake. Basi hapo mtu hana hiyari kuchagua jinsi yake kuwa mwanamume au mwanamke wala (hawezi) kuchagua rangi yake ukiachilia mbali kuchagua wazazi wawili ili tu awe katika malezi ya wazazi wawili matajiri badala ya kuwa na wazazi masikini, wala hawezi kuchagua hata urefu wa kimo chake na umbo la mwili wake.

Hivyo mtu ni mwenye kuyatii mambo mengi yenye kutenza nguvu (kama vile maradhi ya kurithi) na kanuni za kimaumbile zinazofanya kazi kwa faida yake bila ya yeye kulazimika, kwani yeye anapochoka hulala na huamka baada ya kupumzika, anakula anapohisi njaa, anakunywa anapohisi kiu, na hucheka na kuchangamka pale anapofurahi, hulia na kunyongea pale anapohuzunika hali ya kuwa ndani yake (mwanadamu) muna vitendea kazi na viwanda vya kutengeneza Hormone, chembechembe za uhai na maji yenye uwezo wa kubadilika. Vyote hivi kwa wakati huo huo huwa vinauweka mwili wake kwenye uwiano wa kufanya kazi kwa njia ya ajabu kabisa, hali ya kuwa yanapotendeka yote haya hana habari wala hafahamu kwamba uangalizi wa kiungu umemzunguka wakati wote katika nyakati za uhai wake bali hata baada ya kufa kwake.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema kuhusu maana hii (iliyoelezwa hapo kabla): "Je, hivi mtu anadhani kuwa ataachwa hivi hivi tu, je, hivi yeye hakuwa ni tone la manii lililotonwa? Kisha akawa pande la damu, hatimaye (Mwenyezi Mungu) akamuumba na akamsawazisha (akawa mwanadamu kamili) kisha akamfanya namna mbili (akawepo) mwanaume na mwanamke, basi je, (aliyefanya hayo) hakuwa ni muweza wa kuhuisha na kufisha?" (Qur'an, 75:36-40) Hapana shaka Mwenyezi Mungu ni muweza, umetakasika na umetukuka Ewe Mola wetu wewe ndiwe uliyeumba na kusawazisha, nawe ndiwe ambaye umekadiria (kila kitu) na umekiongoza, nawe ndiwe ambaye umefisha kisha ukahuisha, utakatifu ni wako na utukufu ni wako, hakika ameangamia na amepotea yeyote mwenye kukupinga na kujitenga nawe na hakukutukuza vilivyo. Basi hebu tukamilishe uchambuzi huu kwa maneno aliyoyasema Imam Ali bin Musa Ar-Ridhaa ambaye ni Imam wa nane miongoni mwa Maimam wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) naye kwa hakika alikuwa mashuhuri kwa elimu katika zama za Maamuni (Khalifa wa Banu Abbas) na kabla hata hajafikia umri wa miaka kumi na minne alikuwa kesha kuwa ndiye mtu mjuzi mno wa watu wa zama zake.

Taz: Al-iqdul-Farid cha ibn Abdi Rabih Juz. 3, uk. 42. Kuna mtu alimuuliza Imam Ridhaa kuhusu maana ya maneno ya babu yake Al-Imam Jaafar As-Sadiq aliposema kuwa: "Hapana Jabr wala Taf-widh, bali kuna jambo baina ya mambo mawili" Basi Imam Ar-Ridhaa alimjibu mtu huyo (akasema): "Yeyote mwenye kudai kwamba Mwenyezi Mungu anatenda matendo yetu kisha hutuadhibu juu ya matendo hayo, basi huyo atakuwa anazungumzia juu ya Jabr, na yeyote adhaniye kwamba Mwenyezi Mungu ameachia mambo ya viumbe na riziki kwa Maimamu wake, basi bila shaka huyo atakuwa amezungumzia Taf-widh, na asemaye kuhusu Jabr ni kafiri na asemaye kuhusu Taf-widh ni mshirikina."

Amma maana ya jambo baina ya mambo mawili ni kule kuwepo njia ya kuyatenda aliyoyaamuru Mwenyezi Mungu, na kuacha aliyoyakataza, yaani Mwenyezi Mungu amempa(mwanaadamu) uwezo wa kutenda maovu na kuyaacha kama ambavyo amempa uwezo wa kufanya mema na kuyaacha na akamuamuru kufanya hili la wema na kuacha la uovu." Naapa kuwa huu ndiyo ubainifu uliowazi unaotosheleza, ambao uko kwenye kiwango cha akili na unaofahamika kwa watu wote wenye taaluma na wasio na taaluma. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) amesema kweli pale alipozungumza juu ya haki inayowastahiki Maimamu wa nyumba yake (Amani ya Mwenyezi Mungu iwashukie) akasema: "Musiwatangulie mtaangamia na wala musiwapuuze pia mtaangamia, wala musiwafundishe kwani bila shaka wao ni wajuzi mno kuliko ninyi." Taz: 1) Ibn Hajar katika Sawaiq Al-Muhriqah uk. 148

2) Maj-mauz-zawaid Juz. 9 uk. 163.

3) Yanabiul-Mawaddah uk. 41.

4) Ad-Durrul-Manthoor cha Suyuti Juz. 2 uk. 60.

5) Kanzul-UmmalJuz. 1 uk. 168.

6) Usudul-Ghabah Juz. 3 uk. 137.

7) Abaqatul-An-war Juz. 1 uk. 184.