• Anza
  • Iliyopita
  • 13 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 6780 / Pakua: 3671
Kiwango Kiwango Kiwango
JAWABU KWA WAPINGA MAULIDI

JAWABU KWA WAPINGA MAULIDI

Mwandishi:
Swahili

JAWABU KWA WAPINGA MAULIDI

MWANZO WA KITABU

MUANDISHI NI: SEHIKH ABILLAHI NAASIR

MAULIDI NI MOJA KATI YA SHEREHE ZA KITAMADUNI ZA KIISLAMU. SHEREHE ZA MAULIDI NI ZENYE KUPEWA KIPAU MBELE SANA NA WATU WA MUAMBAO WA AFRIKA YA MASHARIKI, SABABU KUU ILIYO WAFANYA WAO KUWA NA SHAUKU YA MAULIDI KILA IFIKAPO MFUNGUO SITA, NI KULE KUWA WAO, NI WAISLAMU WENYE MAPENZI NA MTUME WAO.

KATIKA ZAMA ZA MIAKA KAMA ISHIRINI AU KUMI NA TANO ILIYOPITA, KULIANZA KUINGIA VURUGU LA BAADHI YA WAISLAMU WENYE SIASA KALI, LILILOWATANGAZIA WENGINE UHARAMU WA MAULIDI, HAIDHURU KATIKA USEMI WAO HUO, HUWA WANATOA DALILI MBALI MBALI, LAKINI WAKATI MWENGINE DALILI ZAO HUWA HAZIKUBALIKI KIMANTIKI.

KITABU HIKI KILICHOKO MIKONONI MWENU NI KITABU KILICHO KUSANYA JUMLA YA MAKALA MABALI MBALI ZILIZITAYARISHWA NA SHEIKH ABDILLAHI NAASIR, KWA AJILI YA KUJIBU HOJA MBALI MBALI ZA WAPINGAJI WA MAULIDI. NA MIMI KWA UPANDE WANGU NIMEAMUA KUUWEKA UTANGULIZI HUU, ILI TU NIWEZE KUTOA MTAZAMO WA SUALA HILI LILIVYO INGAWAJE NI KWA UFUPI KABISA. NINATARAJI WAISLAMU WENZETU WATAFAIDIKA NA MAELEZO HAYA, NA WATALITUMIA JICHO LA KUTAFAKARI KATIKA KUYAANGAZA YALIOMO NDANI YA MAKALA HIZI. NINAMUOMBA MOLA MTUKUFU ATUNUSURU NA SHARI ZA UJINGA WETU, NA ATUPE UFUNUO WA ELIMU ITOKAYO MBINGUNI. KWANI YEYE TU NDIYE MJUZI NA KIONGOZI WA WACHA MUNGU.

AAMIN YAA RABBAL AALAMIIN.

MKUSANYAJI WA MAKALA:

SALIM SAID AL-RAJIHIY

SHEREHE ZA MAULIDI:

Maulidi ni Kiswahili cha neno la Kiarabu, mawlid. Neno hili lina maana ya "mazazi" au "kuzaliwa kwa" (birthday). Kwa kawaida, linapotumiwa na Waislamu, huwa na maana ya siku aliyozaliwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.), au hafla ya kuisherehekea siku hiyo.

Waislamu wa ulimwengu mzima, ifikapo tarehe 12 ya Mfungo Sita (Rabiul Awwal), husoma maulidi na kuisherehekea siku hiyo kwa furaha kubwa. Sherehe hizo, kwa dasturi, haziishii tarehe hiyo tu, bali huendelea hata kwa miezi miwili mitatu baada ya hapo. Hili huwa ni kwa sababu ya Waislamu wa kila nyumba, kila mtaa, kila mji na kila nchi kutaka kushiriki katika sherehe hizo na kupata baraka zake. Vile vile huwapa Waislamu nafasi ya kutembeleana na kushirikiana katika sherehe hizo - jambo ambalo lisingewezekana lau watu wote wangeliamua kuzifanya sherehe hizo siku hiyo hiyo moja tu.

Kwa nini kusoma maulidi?

Waislamu husoma maulidi kwa sababu mbalimbali. Kati ya hizo ni: (i) kuikumbuka na kuitukuza siku aliyozaliwa mbora wa viumbe vyote, aliyetutoa vizani na kututia kwenye nuru;

(ii) ni njia moja ya kutoa shukrani zetu kwa neema hiyo;

(iii) katika sherehe hizo, hupatikana fursa ya kukumbushana maisha ya bwana mkubwa huyo na mafunzo yake;

(iv) hupatikana fursa ya Waislamu wa madhihabi na mataifa mbalimbali kushirikiana na kuziweka kando hitilafu zao; na

(v) mikusanyiko hiyo huleta athari kwa wasio Waislamu ya kuupenda Uislamu, na hata kusilimu.

Wanaopinga na sababu zao

Lakini, hata hivyo, kuna baadhi ya Waislamu -- japokuwa wao si wengi kama wanaoyasoma -- ambao hupinga kusomwa maulidi; na hutoa sababu zao. Kati ya sababu hizo ni:

(i) maulidi hayakuwako zama za Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Basi kwa nini yazuliwe sasa?

(ii) hayakusomwa na maswahaba wala waandamizi wao. Kama kweli yangelikuwa ni sawa kuyasoma, bila shaka mabwana wakubwa hao wangelikuwa ni wa mbele kufanya hivyo;

(iii) kuweka ada ya kusoma maulidi ni kuigiza Wakristo walioweka siku ya Krismasi; na Mwislamu haruhusiwi kufanya hivyo;

(iv) kwenye sherehe za maulidi hufanywa baadhi ya mambo ambayo ni ya munkar (yanayochukiza, bali ni haramu kamwe, katika sharia ya Kiislamu);

(v) hakuna ushahidi wowote, wa Qur'ani wala Hadithi za Mtume Muhammad (s.a.w.w.), unaothubutisha usawa wa kuyasoma maulidi, sikwambii kuyatilia nguvu.

Kwa nguvu ya hujja hizo, mara nyingi viongozi wa wanaopinga maulidi huwaonyesha wafuasi wao kuwa wale wanaosoma maulidi ni watu waliopotea kwa "kuzua" mambo yasiyo na msingi katika dini yetu hii. Jambo hili limeleta mchafuko -- unaofufuka aghalabu kila ifikiapo miezi ya kusoma maulidi -- ambao unahatarisha umoja na masikizano, sio baina ya Waislamu wa madhihabi mbalimbali peke yao, bali hata wale wa madhihabi mamoja!

Mchafuko huu huzidi kukua kwa sababu ya lugha kali inayotumiwa na pande zote mbili -- za wanaounga na wanaopinga maulidi -- katika kutetea misimamo yao; na hilo haliwezi kusaidia katika kutatua usawa uko wapi. Liwezalo kutatua hitilafu hii ni kuijadili ki-ilimu na kwa lugha nzuri ya kuhishimiana. Na hilo ndilo nililokusudia kulifanya, kuanzia makala yanayofuatia haya, Inshallah.

ABDILAHI NASSIR

P.O. BOX 84603

MOMBASA

4 Rabiul Awwal, 1423

17 Mei, 2002

1

JAWABU KWA WAPINGA MAULIDI

MAKALA NO: 1

MUANDISHI NI: SEHIKH ABILLAHI NAASIR

WANAVYOSEMA WAPINGA MAULIDI NA MAJIBU YETU

Katika makala yetu ya kwanza tuliahidi kuzijadili ki-ilimu, moja baada ya moja, hujja zinazotolewa na wanaopinga maulidi. Kwa hivyo leo tunaanza:

Hujja yao ya kwanza ni kwamba: maulidi hayakuwako zama za Mtume Muhammad (s.a.w.w.) Kwa hivyo, kuyaleta baada ya yeye kufariki dunia, ni bid'a (uzushi). Na kila bid'a, kwa maneno yake mwenyewe Bwana Mtume (s.a.w.w.), ni upotevu. Kwa hivyo, kila anayesoma maulidi amepotea!

MAJIBU YETU:

Ni kweli kwamba maulidi, hivi tunavyoyasoma, hayakuwako zama za Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Lakini si kweli kwamba, kulifanya kila ambalo halikuwako zama hizo, ni upotevu. Kama ni hivyo, basi bila shaka Waislamu wote leo -- wakiwamo wanaopinga maulidi -- wangelikuwa wamepotea kwa kuwa (katika zama zao mbalimbali) wamefanya, na wanaendelea kufanya, mambo ambayo hayakuwako zama za Bwana Mtume (s.a.w.w.)!

Kwa mfano, katika zama za Bwana Mtume (s.a.w.w.), misikiti haikuwa ikitandikwa chochote (watu wakisujudu juu ya mchanga); lakini leo inatandikwa majamvi, busati na mazulia! Kiwanja kitakatifu cha Al-Kaaba kilikuwa ni mchanga mtupu na mawe; lakini leo kimetandikwa marumaru! Watu walikuwa wakenda kuhiji kwa kupanda ngamia au majahazi; lakini leo wanakwenda kwa ndege, meli za kisasa na mabasi ya anasa (luxury)! Watu, walipokuwa wengi msikitini, walikikhutubu kwa kupaza sauti zao; lakini leo wanatumia vipaza sauti (loud speakers)! Misahafu ilikiandikwa kwa mkono, juu ya ngozi na mifupa, na kutolewa nakala chache; lakini leo inachapwa kwa mashini, juu ya karatasi za fakhari, na kutolewa nakala mamilioni kwa mamilioni!

Lakini hakuna anayesema -- hata hao wanaopinga maulidi hawasemi -- kwamba Waislamu waliobuni mambo hayo wametuletea bid'a au wamepotea. Kwa nini? Kwa sababu kwao wao, na kwa wanaosoma maulidi, uzushi wa aina hiyo si bid'a; sio alioukusudia Bwana Mtume (s.a.w.w.). Alioukusudia yeye ni ule wa kuzua jambo katika dini hii ambalo halitokani nayo (maa laysa minhu). Hilo ndilo lililo wazi kutokana na Hadithi mashuhuri ya Bwana Mtume (s.a.w.w.) inayosema: "Yoyote atakayezua, katika dini yetu hii, jambo ambalo halitokani nayo, litarudishwa (litakataliwa)."

Ukiitaamali vizuri Hadithi hiyo, itakudhihirikia kwamba Bwana Mtume (s.a.w.w.) hakutuzuia kuzua (kubuni), katika dini hii, kila ambalo halikuwako zama zake. Kama angelitaka kutuzuia hivyo, Hadithi hiyo isingelisema hivyo, bali ingelisema hivi: "Yoyoye atakayezua jambo katika dini yetu hii, litakataliwa." Na lau ingelisema hivyo, basi yote yale tuliyoyataja hapo juu yasingeliruhusiwa; yangelikuwa bid'a.

Lakini Hadithi haikusema hivyo. Ilivyosema ni: " Yoyote atakayezua ambalo halitokani nayo, litakataliwa." Kwa kuongeza kifungu cha maneno tulichokichapa kwa italiki (yaani "ambalo halitokani nayo"), ni wazi kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.w.) hakukusudia kuwazuia Waislamu kufanya kila ambalo halikuwako zama zake. Alilolikusudia ni kutuachia wazi mlango wa kubuni mambo katika dini hii bora tu yawe yanatokana nayo.

Sasa suali hapa ni: jee, maulidi si katika mambo yanayotokana na "dini hii", hata kama hayakuwako zama za Bwana Mtume (s.a.w.w.)?

Majibu yetu ni: Maulidi, na yaliyomo maulidini, si mageni na "dini hii", bali yanatokana nayo, kama tutakavyobainisha kwa urefu zaidi katika majibu yetu ya hujja Na. (v) ya wapinzani wake inshallah.

Kwa hivyo, kuwa tu jambo halikuwako zama za Mtume Muhammad (s.a.w.w.) si hujja ya kuwazuia Waislamu kulifanya. Wanalozuiliwa Waislamu kulifanya ni kuzua jambo na kulifanya ni dini hali ya kuwa halina asili na dini. Na maulidi si hivyo!

Inshallah, katika makala yanayofuatia, tutaijadili hujja yao ya pili.

ABDILAHI NASSIR

P.O. BOX 84603

MOMBASA

13 Rabiul Awwal, 1423

26 Mei, 2002

2

JAWABU KWA WAPINGA MAULIDI

MAKALA NO: (2)

MUANDISHI NI: SEHIKH ABILLAHI NAASIR

WANAVYOSEMA WAPINGA MAULIDI NA MAJIBU YETU

Katika makala yetu kabla ya haya, tulijibu hujja ya kwanza ya wanaopinga maulidi. Leo tunaendelea na hujja yao ya pili. Katika hujja yao ya pili wanasema: Maulidi hayakusomwa na maswahaba wala waandamizi wao (taabi'in). kama kweli yangelikuwa ni sawa kuyasoma, bila shaka mabwana wakubwa hao wangelikuwa ni wa mbele kufanya hivyo.

MAJIBU YETU:

Hakuna Mwislamu yoyote anayekataa kuwa maswahaba ni watu watukufu. Wala hakuna anayekataa kuwa wao ndio kiungo chetu sisi na Bwana Mtume (s.a.w.w.). Lakini, pamoja na utukufu wote huo, wao walikuwa ni binadamu; hawakuwa ni ma'asumin. Walikiweza kufanya jambo, wakaswibu (wakapata); kama ambavyo walikiweza kufanya jambo, wakakosea. Na mifano ya yote mawili hayo ni mingi katika historia yao.

Kwa hivyo, kuwa tu jambo fulani halikufanywa na maswahaba, haliwi ni hujja sahihi ya kuwazuilia Waislamu kulifanya jambo hilo. Hujja ya pekee iliyo sahihi ni iwapo lile ambalo hawakulifanya wao, waliacha kulifanya kwa sababu ndivyo alivyoamrisha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w.), au waliacha kulifanya kwa sababu linapingana na maamrisho ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w.). Ikiwa walifanya hivyo ndipo jambo hilo litakapokuwa ni hujja; lakini si kwa sababu ya kuwa halikufanywa na maswahaba, bali ni kwa sababu tu ya kuwa ndivyo alivyoamrisha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w.), au ni kwa sababu tu ya kuwa linapingana na mafunzo ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w.) -- na hivyo ndivyo Kiislamu.

Kwa hivyo si sawa kuyapinga maulidi kwa sababu tu hayakusomwa na maswahaba na waandamizi wao. La sawa ni kuyapinga kwa sababu tu yamekatazwa na Mwenyezi Mungu au Mtume Wake (s.a.w.w.), au yanapingana na maamrisho yao. Na hilo, mpaka hivi sasa, wapinzani wa maulidi hawajaweza kulithubutisha.

Tunasema hivyo kwa sababu, mmoja kati ya misingi muhimu ya sharia ya Kiislamu, inyaokubaliwa na wanazuoni wa wanaosoma maulidi na wale wa wanaopinga maulidi, ni kwamba -- tunapokuja kwenye mambo kama ya maulidi, ujenzi wa msikiti, mavazi, na kadhaalika -- kila kitu ni halali mpaka kithubutishwe kuwa ni haramu. Kwa hivyo, kwa msingi huu, uharamu wa maulidi haitaki uthubutishwe na wanaoyasoma, bali inataka uthubutishwe na wanaoyapinga. Wala wasilithubutishe hilo kwa vichwa vyao (Sura 16:116), bali kwa kutoa ushahidi wa maneno ya Mwenyezi Mungu au Mtume Wake s.a.w.w. (Sura 4:59). Na hilo pia, mpaka dakika hii, wapinzani wa maulidi hawajaweza kulifanya.

Mwanzo mwanzo wa kuzuka madhihabi haya ya kupinga maulidi, wafuasi wake waliyapinga mambo mengi yaliyozuka katika zama zao. Kati ya mambo hayo ni kuvuta sigara, kupiga simu ya mdomo (telephone), kujiwekea kashida mbele ya mtu anaposwali, kumwamkia mtu kwa: "Umeamkaje?", kupana mikono baada ya swala, kutandika busati misikitini, na hata kuvaa nguo yenye thamani inayozidi dirhamu 100 (mia)!

Yote hayo waliyapinga kwa hujja ya kuwa hayakuwako zama za Mtume (s.a.w.w.), na kwamba hayakufanywa na maswahaba na waandamizi wao! Lakini, baada ya kutambua walikosea wapi, walirudi nyuma, wakayakubali yote hayo. Kwa maneno mengine, yakawa sio bid'a tena!

Leo, kwa hujja hizo hizo, waandamizi wao wameanza kusema vibula vivunjwe! Kesho watasema na minara nayo ivunjwe! Kesho kutwa watasema mimbari za mbao au za mawe, nazo pia ziondolewe, zirudishwe zile za vigogo vya mtende; hata vya mnazi havitafaa! Baada ya hapo ni nini kitakachowazuia wasitwambie tuondoe banka (panka) misikitini, turudi kujipepea kwa nguo zetu kama ilivyokuwa zama za Bwana Mtume (s.a.w.w.)? Au twende hijja kwa ngamia au farasi badali ya ndege? Au ni lipi litakalowazuia kutuamrisha kuisoma Qur'ani katika ngozi na mbao, kama ilivyokuwa zama za Bwana Mtume (s.a.w.w.) na maswahaba, badali ya hii miswahafu mizuri mizuri tuliyonayo?

Ni matumaini yetu kwamba, kama ambavyo watangulizi wao walirudi nyuma na kuyakubali yale waliyoyafanya ni bid'a mwanzo, wao nao watafuata nyayo zao, wayaone maulidi, na mengine kama maulidi, kuwa sio bid'a iliyokatazwa na Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Alhamdulillaah, baadhi yao wameanza kuona hivyo na kufanya sherehe za mazazi ya Bwana Mtume (s.a.w.w.). Lakini badali ya kuyaita maulidi, huyaita seera!

Inshallah, katika makala yanayofuatia, tutazijadili hujja zao nyengine.

ABDILAHI NASSIR

P.O. BOX 84603

MOMBASA

25 Rabiul Awwal, 1423

7 Juni, 2002

13 Rabiul Awwal, 1423

26 Mei, 2002

3

JAWABU KWA WAPINGA MAULIDI

MAKALA NO: (3)

MUANDISHI NI: SEHIKH ABILLAHI NAASIR

WANAVYOSEMA WAPINGA MAULIDI NA MAJIBU YETU

Bado tunaendelea na hujja za wanaopinga maulidi.

Hujja yao ya tatu ni kuwa: kuweka ada ya kusoma maulidi ni kuigiza Wakristo walioweka siku ya Krismasi; na Mwislamu haruhusiwi kufanya hivyo.

MAJIBU YETU:

Mwislamu hazuiliwi kufanya jambo kwa sababu tu linafanywa na Mkristo au kafiri yoyote mwengine. Analozuiwa ni kufanya jambo kama linalofanywa na Mkristo, au kafiri yoyote mwengine, linapokuwa linakwenda kinyume na mafunzo ya Kiislamu; na hilo sio linapofanywa na Mkristo au kafiri yoyote tu, bali hata linapofanywa na Mwislamu mwenziwe; haruhusiwi kulifanya.

Tunaposoma historia, kwa mfano, tunaona jinsi Bwana Mtume (s.a.w.w.) -- katika Vita vya Handaki -- alivyokubali shauri la Salman Farisi la kuchimba handaki kama walivyokifanya Wafursi kwao. Na Wafursi, wakati huo, hawakuwa ni Waislamu, bali walikuwa ni makafiri waliokiabudu moto! Jee, kwa kuwaigiza makafiri hao katika uchimbaji wa handaki, Bwana Mtume (s.a.w.w.) alikosea?

Hali kadhaalika, tukija kwenye hijja mathalan, tunaona jinsi mahujaji wanavyokwenda baina ya Swafaa na Marwa, na jinsi wanavyochinja wanyama mwisho wa hijja yao. Lakini vitendo kama hivyo, kabla ya Uislamu, vilikuwa vikifanywa na makafiri! Basi kama kuigiza Wakristo hakuruhusiwi, kwa nini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w.) wakatuamrisha kufanya mambo ambayo dhahiri yake ni sawa na kuwaigiza makafiri?

Ukivizingatia vizuri vitendo hivyo utaona kwamba, japokuwa kwa dhahiri vinafanana na vile vya makafiri, kwa kweli huwezi kusema kuwa ni sawa na kuwaigiza makafiri. Kwa nini? Kwa sababu waliyokuwa wakiyafanya makafiri mwahali humo, walikuwa wakiyafanyia masanamu yao, waliyoyaweka humo. Kwa hivyo yao ilikuwa ni shirk (ushirikina). Lakini tunayoyafanya sisi Waislamu, baada ya kuondolewa mbali masanamu hayo, huwa tunamfanyia Mwenyezi Mungu Mmoja tu, asiye na mwenziwe (mshirika). Kwa hivyo yetu ni tawhid (kumpwekesha Mwenyezi Mungu).

Hali kadhaalika tunapokuja kwenye Krismasi. Japokuwa Krismasi, kama maulidi, hufanywa kwa kusherehekea mazazi ya Mitume ya Mwenyezi Mungu (Nabii Muhammad s.a.w.w. na Nabii Isa a.s.), lakini sherehe mbili hizo -- kama ambavyo kila mtu anajua -- si sawa. Sherehe zinazofanywa Krismasi ni tafauti kabisa na zinazofanywa maulidini, kama ambavyo Wakristo wanavyomchukulia Nabii Isa a.s. (Yesu Kristo) ni tafauti kabisa na vile Waislamu wanavyomchukulia Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Kwa mfano, Waislamu hawamchukulii Mtume Muhammad (s.a.w.w.) kuwa ni Mungu, wala ni Mtoto wa Mungu, wala ni Roho Mtakatifu.

Kwa hivyo kuwa tu jambo fulani lilitangulia kufanywa na makafiri -- wawe ni Wakristo ama ni wengineo -- haiwi ni hujja ya kuwazuilia Waislamu kulifanya jambo hilo maadamu watayatoa yote ya ukafiri yaliyokuwamo humo. Na hivyo ndivyo maulidi yalivyo. Zaidi ya kuwa zote mbili -- Krismasi na maulidi -- ni sherehe za mazazi ya Mitume ya Mwenyezi Mungu, hakuna jengine linalofanana katika sherehe hizo.

Kama tutashikilia kuwa ni haramu Waislamu kuwaigiza Wakristo, au makafiri wowote kwa jumla, katika jambo lolote -- hata kama halipingani na dini yetu -- basi sio wanaosoma maulidi tu, bali hata wanaoyapinga pia watakuwa makosani. Kwani ni nani kati yao aliyeacha gari au ndege, akaendelea kupanda punda, farasi au ngamia? Ni nani, anayejimudu, aliyeacha kutumia umeme (spaki), akaendelea na kuni au mafuta ya taa? Ni nani anayeradhiwa kujipepea kwa kipepeo au nguo yake, akaacha -- ikiwa anayo nafasi -- kutumia banka au AC (Air Conditioner)? Ni nani anayepanda kwa miguu mpaka ghorofa ya 15, au ya 10, akaacha lifti? Kwa nini hawayaachi yote hayo ili wasiwe wanawaigiza Wakristo au makafiri wengine, maana yote hayo yameanzishwa na wao.

Kwa hivyo si sawa kuwazuilia Waislamu kusoma maulidi kwa sababu tu ya kuwa, kufanya hivyo, ni kuwaigiza Wakristo katika sherehe zao za Krismasi.

Inshallah, katika makala yanayokuja, tutaijadili hujja yao ya nne.

ABDILAHI NASSIR

P.O. BOX 84603

MOMBASA

2 Rabiuth Thani, 1423

14 Juni, 2002

4

JAWABU KWA WAPINGA MAULIDI

MAKALA NO: (4)

MUANDISHI NI: SEHIKH ABILLAHI NAASIR

WANAVYOSEMA WAPINGA MAULIDI NA MAJIBU YETU

Tunaendelea na hujja za wanaopinga maulidi na majibu yetu.

Katika hujja yao ya nne wanasema: Kwenye sherehe za maulidi hufanywa baadhi ya mambo ambayo ni ya munkar (yanayochukiza, bali ni haramu kamwe, katika sharia ya Kiislamu).

MAJIBU YETU:

Hiyo si hujja madhubuti. Kwa nini maulidi yote yatupwe kwa sababu tu ya kufanywa baadhi ya mambo ambayo ni ya munkar katika sherehe zake? Kwa nini hayaondolewi hayo ya munkar, kama yako, yakabakishwa yasiyo ya munkar? Kwani tunda likiwa limeoza kidogo hutupwa lote, au hukatwa pale palipooza likaliwa pale pazuri palipobaki?

Katika hili tuna funzo zuri kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Yeye aliondoa tawafu ya Al-Kaaba, na Swafaa na Marwa, kwa sababu mwahali humo mulikuwa na munkar (masanamu) au aliamrisha yaondolewe hayo masanamu na watu waendelee kutufu? Tutaona kuwa Mwenyezi Mungu hakutuzuia kufanya jambo zuri lililokuwako (kutufu na kusa'yi) kwa sababu tu katika ibada hizo palikuwa na munkar (masanamu). Alilolifanya ni kuondoa munkar uliokuwako, akatuacha tuendelee na mazuri yaliyobaki (tawafu).

Kwa hivyo, kama katika maulidi kuna munkar wowote, la sawa ni uondolewe munkar huo, na maulidi yaachwe yaendelee. Si kumtupa jongoo na ung'ongo (ujiti) wake.

Kidokezo

Baada ya kutoa makaratasi yetu kwa wiki tatu, makundi mawili ya wanaopinga maulidi yamejitokeza. La kwanza limejita "Ahlu-Tawheed"; na la pili linajita "Wakereketwa wa Sunna Malindi". Na yote mawili hayakutoa anwani zao!

Ahlu-Tawheed wametoa makaratasi yenye jina la "Uzushi na Shirk Ndani ya Barzanji na Vitabu Vyengine vya Maulid". Katika makaratasi hayo, wamenukuu baadhi ya madondoo ambayo -- kwa maoni yao -- ni shirki. Lakini hawakutueleza vipi kuwako madondoo hayo katika vitabu hivyo, hata kama yatakuwa ni shirki kweli, yanafanya maulidi yoyote mengine (yasiyo na hayo wanayoyaona wao kuwa ni shirki) hayafai kusomwa.

Wakereketwa wa Sunna Malindi, kwa upande wao, wametoa makaratasi yenye jina la "Chapa ya Kwanza (1): Majibu ya Abdillah Nassir". Katika makaratasi hayo, ambayo wameahidi kuendelea nayo, hawajazungumzia maulidi. Walilolifanya ni kunizungumza mimi binafsi -- kwa ya kweli na ya uwongo! Lakini na wao pia, kama wenzi wao, hawajatueleza vipi vyovyote vile vitakavyokuwa mimi binafsi -- iwe ni kwa wema ama kwa uovu -- ni hujja tosha ya kuyafanya maulidi yawe hayafai kusomwa! Pengine watalieleza hilo katika makala yao yatakayofuatia.

Hata hivyo si nia yangu, kwa sasa, kuyajibu makaratasi hayo kwa sababu kutatutoa nje ya mfululizo wetu huu. Nia yangu inshallah ni kuendelea kuzijibu hujja zao zote nilizozidondoa katika makaratasi yetu ya kwanza ya tarehe 4 Rabiul Awwal, 1423 / 17 Mei, 2002. Baada ya hapo ndipo nitakapojibu hayo yaliyomo katika makaratasi yao hayo.

Kwa hivi sasa, napenda kuwahakikishia wanaosoma maulidi kwamba yote waliyoyataja katika makaratasi yao mawili hayo tutayajibu kiilimu na kistaarabu, kama ilivyo dasturi yetu, na kama tulivyofanya mpaka sasa, pamoja na kuonyesha kwamba hayana mashiko.

Kwa hivyo, tunawaomba wale walionayo makaratasi hayo wayaweke, wangojee majibu yetu inshallah.

ABDILAHI NASSIR

P.O. BOX 84603

MOMBASA

9 Rabiuth Thani, 1423

21 Juni, 2002

5

JAWABU KWA WAPINGA MAULIDI

MAKALA NO: (5)

MUANDISHI NI: SEHIKH ABILLAHI NAASIR

WANAVYOSEMA WAPINGA MAULIDI NA MAJIBU YETU

Tunaendelea na hujja za wanaopinga maulidi na majibu yetu.

Katika hujja yao ya tano wanasema: Hakuna ushahidi wowote, wa Qur'ani wala Hadithi za Mtume Muhammad (s.a.w.w.), unaothubutisha usawa wa kuyasoma maulidi, sikwambii kuyatilia nguvu.

MAJIBU YETU:

Katika majibu yetu ya hujja yao ya pili, tulieleza kwamba -- kwa mujibu wa msingi mmoja kati ya misingi muhimu ya sharia ya Kiislamu -- anayetakikana kuthubutisha kuwa maulidi hayafai kusomwa si anayesema yasomwe; ni anayesema yasisomwe. Kwa hivyo ushahidi wa Qur'ani na Hadithi unaotakikana si wa kutolewa na sisi tunaosema ni sawa kusoma maulidi, bali ni wa kutolewa na wao wanaoyakataza. Jee, wanao ushahidi huo? Kama wanao, twaukaribisha.

Hata hivyo, kama ushahidi wanaoutaka wapinga maulidi, wa Qur'ani na Hadithi, ni unaosema kwa kutasua (nassun qat'iyy / categorically), "Enyi mlioamini! Someni maulidi"; basi ushahidi huo hakuna. Lakini tunauliza, kwa sharia ya Kiislamu, ni lazima jambo litasuliwe katika Qur'ani au Hadithi ya Bwana Mtume (s.a.w.w.) ndipo liruhusiwe kufanywa? Jee, hakuna mambo ambayo Waislamu -- wakiwamo wanaopinga maulidi -- huyafanya pamoja na kuwa hawana ushahidi wa Qur'ani wala Hadithi zilizoyataja mambo hayo?

Kwa mfano, ni nani kati ya wanaopinga maulidi anayeweza kututolea ushahidi wa kutasua -- wa Qur'ani au Hadithi ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) -- wa Waislamu kuruhusiwa kujenga vyuo (colleges) na vyuo vikuu? Au kutoa digrii? Au kujenga hospitali na zahanati? Au kujenga nyumba za mayatima (orphanages)? Au kuunda vyama vya ushirika? Au kuweka mashindano ya kusoma Qur'ani na kuyatolea zawadi, na mengine mengi kama hayo? Jibu ni: hakuna! Kama uko, tunaomba tutolewe. Jee, kwa kuwa hauko, ndio watakuwa Waislamu wote -- wakiwamo wanaosoma maulidi -- wanakosea kwa kuyafanya mambo hayo kwa sababu tu hakuna aya au Hadithi inayoyataja? Kama ni hivyo, basi kwa nini wao wanayafanya? Kama sio hivyo, basi kwa nini wanatukataza kuyasoma maulidi kwa sababu hiyo hiyo?

Katika Qur'ani na Hadithi kuna mambo ambayo uhalali wake umetasuliwa (specified). Mfano wa hayo ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu, kuswali, kufunga (saumu), kutoa zaka, kuhiji, kuowa, kufanya biashara, kufanya uadilifu, na kadhaalika. Kuna na ambayo uharamu wake pia umetasuliwa; kama kumshirikisha Mwenyezi Mungu, kuzini, kula riba, kuiba, kudhulumu, kusema uwongo, kusengenya, na kadhaalika. Yote hayo ni mambo ambayo ushahidi wake -- wa kuyatasua khaswa -- unaweza kutolewa katika Qur'ani na / au Hadithi za Bwana Mtume (s.a.w.w.).

Kuna na ambayo hayakutasuliwa isipokuwa yametajwa kwa jumla (generally) tu. Hayo, kinyume na yale yaliyotasuliwa tuliyoyataja hapo juu, yana uwanja mkubwa wa jinsi ya kuyatekeleza maadamu hayatachanganywa na ya haramu. Hebu tuangalie mifano miwili mitatu:

1. Mayatima: Tunaposoma Qur'ani na / au Hadithi, tunaona kwamba tunahimizwa kwa jumla tuwatizame, tusiwatupe; tuwahurumie, tusiwatese. Vipi? Hilo hatukutajiwa tafsili zake isipokuwa tumeachiwa sisi, bora tu tusitie la haramu. Kwa sababu hii ndio ukaona hakuna aliyezuia kujengwa nyumba za mayatima (orphanages) japokuwa hazikutajwa kwa jina katika Qur'ani wala Hadithi za Mtume Muhammad (s.a.w.w.)!

2. Ilimu: Tunaposoma Qur'ani na / au Hadithi, tunaona jinsi tunavyohimizwa, bali kufaradhiwa, kusoma na kuitafuta ilimu popote ilipo. Hatukupawa tafsili ya namna ya kulitekeleza hilo. Kwa hivyo, maadamu hatulitii la haramu, tuko huru kusoma kwa ubao, kitabu, tepu, video, redio, runinga, mtandao, na kadhaalika; kama ambavyo tuko huru kusoma madrasa, nyumbani, msikitini, chuoni (college) au kwenye vyuo vikuu; na kama ambavyo tuko huru kukaa majamvini, vitini au madeskini. Hakuna hata mmoja wa mashekhe wa wanaopinga maulidi anayewazuia watu kuyafanya hayo, na tuliyoyataja hapo juu yanayohusu mayatima, kwa sababu tu hayakutajwa kwa jina katika Qur'ani wala Hadithi za Mtume Muhammad (s.a.w.w.)!

Basi kwa nini kuyapinga maulidi?

Inshallah, katika makala yanayofuatia haya, tutazidondoa aya za Qur'ani na Hadithi za Bwana Mtume (s.a.w.w.) ambazo, japokuwa hazikutaja maulidi kwa jina, zinaunga kwa jumla yale yanayofanywa na yanayofanyika maulidini.

ABDILAHI NASSIR

P.O. BOX 84603

MOMBASA

16 Rabiuth Thani, 1423

28 Juni, 2002

6

JAWABU KWA WAPINGA MAULIDI

MAKALA NO: (6)

MUANDISHI NI: SEHIKH ABILLAHI NAASIR

WANAVYOSEMA WAPINGA MAULIDI NA MAJIBU YETU

Kama tulivyoeleza katika makala yetu ya wiki iliyopita, sio kila kitu kimetajwa kinaga ubaga katika Qur'ani na / au Hadithi. Kuna yaliyotajwa hivyo; kuna na yaliyotajwa kwa jumla, kama maulidi. Lau Waislamu (wanazuoni wao) wangekataa kila jambo ambalo halikutajwa kwa jina katika Qur'ani na / au Hadithi, wangelibaki nyuma kwa karne 14, na wasingekuwa na maendeleo yoyote.

Sasa tuje kwenye maulidi.

Japokuwa -- kama tulivyoeleza katika makala yetu ya wiki iliyopita -- maulidi hayakutajwa kwa jina katika Qur'ani wala Hadithi, lakini yamekusanya mengi yaliyoamrishwa au yaliyopendekezwa na Qur'ani na / au Hadithi. Hapa chini tutayataja baadhi yake tu:

1. Kusoma na kusikiliza Qur'ani: Tunaposoma Qur'ani (k.m. Sura 73:4 na 20), tunaona jinsi Mwenyezi Mungu anavyotuamrisha tuisome. Na tunapokuja kwenye Hadithi zake, tunaelezwa kwamba Bwana Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akipenda sana mtu amsomee yeye Qur'ani, na yeye akisikiliza.

Jee, pale tunapoyafungua maulidi yetu kwa mmoja wetu kuisoma Qur'ani, na wengine tukawa tunamsikiliza, huwa -- kama hatukufanya la sunna -- tumefanya lipi la bid'a?

2. Kumswalia Mtume (s.a.w.w.): Katika Qur'ani Tukufu (Sura 33:56), Mwenyezi Mungu anatuamrisha tumswalie Mtume Wake (s.a.w.w.) baada ya kutwambia kuwa Yeye na Malaika Wake hufanya hivyo pia. Isitoshe! Na kila Ijumaa, khatibu hutukumbusha juu ya mimbari, kwa kututajia Hadithi ya Mtume (s.a.w.w.), kuwa yoyote atakayemswalia yeye mara moja, Mwenyezi Mungu atamswalia (atamrehemu) mtu huyo mara kumi!

Jee, katika kikao kimoja tu cha maulidi, waliohudhuria humswalia Mtume (s.a.w.w.) mara ngapi? Zidisha mara hizo kwa kumi ujue Mwenyezi Mungu hukurehemu wewe mara ngapi katika kikao hicho. Jee, ni lipi hapo -- kama halitakuwa sunna -- lililo bid'a?

3. Kumhishimu na kumtukuza Bwana Mtume (s.a.w.w.): Katika Qur'ani Tukufu (Sura 7:157), Mwenyezi Mungu anawasifu, na kuweta "wenye kufaulu", wale ambao humtukuza na kumhishimu Mtume Wake (s.a.w.w.), wakamsaidia na kuyafuata yale aliyoyaleta. Lakini tutawezaje kuyafanya hayo kama mtu mwenyewe hatumjui vilivyo?

Waswahili husema: "Jambo usilolijua ni usiku wa kiza"; na "asiyekujua hakuthamini". Kwa hivyo, bila ya kumjua Mtume (s.a.w.w.) vilivyo -- historia yake, sifa zake, cheo chake, utukufu wake, na kadhaalika -- vipi tutaweza kumthamini na kumtukuza? Ndipo wanazuoni, kwa kuwa si kila mtu aweza kusoma vitabu, wakabuni maulidi ili yawe ni chombo cha kumjulisha Bwana Mtume (s.a.w.w.) apate kuhishimiwa na kutukuzwa. Hivyo katika maulidi, watu hupata fursa ya kuelezwa yote ya Mtume (s.a.w.w.). Na kwa kuyajua hayo, watu humpenda; na kama ilivyo dasturi ya kila apendaye kumfuata yule anayempenda, watu humfuata.

Jee, kama maulidi yanasaidia watu kumjua Mtume (s.a.w.w.), kumkumbuka na kumpenda, ni lipi hapo la bid'a?

4. Kumsifu Bwana Mtume (s.a.w.w.): Tunaposoma maisha yake, tunaambiwa kwamba, miongoni mwa maswahaba, walikuwako waliotunga mashairi ya kumsifu Bwana Mtume (s.a.w.w.) ambayo walikwenda nayo mbele zake na kumsomea. Bwana Mtume (s.a.w.w.) hakuwafukuza watu hao wala hakuwakataza, bali aliwasikiliza na kuyafurahia yote waliyomsomea. Kwa kitendo hicho kwa hivyo, Bwana Mtume (s.a.w.w.) alitufungulia mlango wa kumsifu. Tafauti ya pekee iliyoko baina ya maswahaba na sisi ni kwamba wao walimsifu machoni mwake, hali sisi tunamsifu akiwa hayuko na sisi kimwili. Sasa, kwa kitendo hiki, tunafanya jambo gani ambalo halikufanywa na maswahaba na kukubaliwa na mwenyewe Bwana Mtume (s.a.w.w.)?

Kama kufanya hivyo ni bid'a, basi sunna ni ipi?

Kwa leo tukomee hapa. Inshallah wiki ijayo tutaendelea na yaliyobaki.

ABDILAHI NASSIR

P.O. BOX 84603

MOMBASA

23 Rabiuth Thani, 1423

5 Julai, 2002

7

JAWABU KWA WAPINGA MAULIDI

MAKALA NO: (7)

MUANDISHI NI: SEHIKH ABILLAHI NAASIR

WANAVYOSEMA WAPINGA MAULIDI NA MAJIBU YETU

Wiki iliyopita tulidondoa baadhi ya mambo yanayofanywa maulidini ambayo, ama Qur'ani na / au Hadithi zimeyaamrisha, au zimeyapendekeza. Leo tunaendelea na yaliyobaki:

5. Kutoleana waadhi: Katika Qur'ani Tukufu (Sura 16:125) Mwenyezi Mungu anatuamrisha tulinganiane kwa hikima na mawaidha mema. Na vivyo hivyo ndivyo Bwana Mtume (s.a.w.w.) anavyotuhimiza katika Hadithi zake nyingi.

Jee, maulidini hatutoleani mawaidha na kulinganiana mema? Hayo nayo kama ni bid'a, sunna ni ipi?

6. Kumpenda Mtume (s.a.w.w.): Hadithi zake (s.a.w.w.) zatuhimiza tumpende, bali zinatueleza waziwazi kwamba hatuwi ni waumini mpaka tumpende yeye kuliko nafsi zetu, kuliko mali yetu na ahli zetu, bali kuliko watu wote.

Jee sifa zote zile anazosifiwa Mtume (s.a.w.w.) maulidini, furaha zote na nderemo zinazoonyeshwa maulidini, haziwi ni ushahidi wa mapenzi yetu kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.)? Mambo kama hayo hufanyiwa asiyependwa?

Kama kuonyesha mapenzi yetu kwa Mtume wetu ni bid'a, sunna ni ipi?

7. Kujumuika na kushikamana: Qur'ani Tukufu (Sura 3:103) inatuhimiza tushikamane na tusifarikiane. Na Mtume naye (s.a.w.w.) anatuhakikishia, katika Hadithi zake, kwamba popote ambapo tutajumuika kwa kheri -- na sidhani kuwa maulidi ni shari -- basi Malaika watatuzunguka, rehema za Mwenyezi Mungu zitufinike, na utulivu wa nyoyo utushukie.

Jee, tunapokusanyika maulidini, hatuyaoni hayo? Ule umoja na mshikamano unaopatikana maulidini, wa wafuasi wa madhihabi mbalimbali kusahau hitilafu zao na kuwa kitu kimoja, ni rehema ndogo?

8. Kutembeleana na kukirimiana: Bwana Mtume (s.a.w.w.), katika Hadithi zake, ametunasihi tuwe tukifanyiana hayo; na hayo huyapata kwa ukubwa siku za maulidi. Waislamu wa mtaa mmoja, au mji mmoja, au hata nchi moja -- kwa kuhudhuria sherehe za maulidi ya wenzi wao -- hupata fursa ya kutembeleana na kukirimiana. Kwa njia hii hujuana hali, wakasaidiana na kupanana (peana) moyo. Hilo huleta mapenzi na mshikamano baina yao. Na iwapo pale pasomwapo maulidi Waislamu ni wachache, kutembelewa kwao na ndugu zao wanaotoka sehemu nyengine huwatia moyo, na pia huwafanya wahishimiwe na wale jirani zao wasio Waislamu.

Katika hayo, ni lipi la bid'a, kama hapana la sunna?

9. Kutangaza Uislamu na kusilimisha wengine: Katika Qur'ani Tukufu (Sura 5:67) Mwenyezi Mungu anamwamrisha Mtume Wake (s.a.w.w.) awafikishie watu Ujumbe aliompa. Na katika khutba yake ya mwisho, Bwana Mtume (s.a.w.w.) alituamrisha sisi wafuasi wake tuufikishe Ujumbe huo kwa yule ambaye haujamfikia. Na hilo limepatikana -- na linaendelea kupatikana -- maulidini kwa ushahidi wa rikodi ya wengi waliosilimu baada ya kuhudhuria maulidini na kusikiliza kaswida na khutba zinazotolewa huko.

Jee, bid'a ni ipi hapo?

10. Kumkumbuka Mtume Muhammad (s.a.w.w.): Qur'ani Tukufu (Sura 41:34) inatwambia kuwa jema na ovu si sawa. Ukitaka kuliondoa ovu, liondoe kwa jema ndipo ovu litakapofutika. Na Mtume (s.a.w.w.) naye ametwambia vivyo hivyo. Hali kadhaalika wazee nao wanatwambia kwamba tukitaka kumpokonya mtoto wembe ili asijikate, tusimwache mikono mitupu maana ataurudia. Badali yake tumpe kitu chengine kisicho na madhara (k.m mpira) ashike. Kwa njia hii tutamwokoa na madhara.

Katika zama kama hizi zetu ambapo Waislamu kwa jumla, na watoto wao khaswa, wanayajua zaidi ya viongozi wasio Waislamu, bali hata ya walio maadui wa Uislamu, katika nyanja mbalimbali, na husherehekea mazazi yao -- ni lipi bora? Tuwaache waendelee vivyo hivyo? Au tuwaambie waache kufanya hivyo bila ya kuwawekea badali yake? Au tuwawekee badali iliyo nzuri (ya sherehe za mazazi ya Mtume (s.a.w.w.) na viongozi wengine wa Kiislamu) ili tuwaachishe hayo waliyoyashika? Jawabu hapo ninakuachia wewe, ndugu Mwislamu.

Mpaka hapa tumemaliza majibu yetu ya hujja zinazotolewa na wanaopinga maulidi; na kuwafikiwa ni kwa Mwenyezi Mungu. Inshallah wiki ijayo, kama tulivyoahidi katika makala yetu ya 9 Rabiuth Thani, 1423 / 21 Juni 2002, tutaanza kuyajibu ya Ahlu-Tawheed waliyoyasema katika makaratasi yao, "Uzushi na Shirk Ndani ya Barzanji na Vitabu Vyengine vya Maulidi".

ABDILAHI NASSIR

P.O. BOX 84603

MOMBASA

1 Jamaadal Uulaa, 1423

12 Julai, 2002

8

JAWABU KWA WAPINGA MAULIDI

MAKALA NO: (8)

MUANDISHI NI: SEHIKH ABILLAHI NAASIR

WANAVYOSEMA WAPINGA MAULIDI NA MAJIBU YETU

Kama tulivyoahidi wiki iliyopita, leo tunaanza kuwajibu Ahlu-Tawheed kwa waliyoyaandika katika makaratasi yao waliyoyapa jina la "Uzushi na Shirk Ndani ya Barzanji na Vitabu Vyengine vya Maulidi".

Katika makaratasi yao hayo, ndugu zetu hao wamenukuu baadhi ya maneno yaliyomo katika Barzanji na Burdah (vitabu viwili vinavyoeleza sifa za Mtume Muhammad s.a.w.w.) na kujaribu, kadri ya ujuzi na uweza wao, kuonyesha kwamba kusema maneno hayo ni shirki. Lakini, kabla ya kutoa majibu yetu, tuanze kwa kuyanukuu maneno yenyewe. Nayo ni mane yaliyotolewa katika Barzanji, na mawili katika Burdah.

Katika Barzanji wameyatoa yanayofuata:

1. "Na kama si yeye (Mtume s.a.w.) asingekuwa Alkhalilu (Ibrahim) na Adam. Na Musa (asingekuwepo) na Issa, bali hata Mulku Suleimani (usingekuwepo)."

2. "Ilisemekana alipotaka Mwenyezi Mungu, Mwenye Ezzi na Alietukuka, kumdhihirisha Mbora wa viumbe vyake, Muhammad, Rehma na Amani za Mwenyezi Mungu zimfikie. Akamuamrisha Jibril achukue Udongo wake (wa kumuumbia nao) kwenye mahali pa kaburi lake karimu".

3. "Alikuwa Mtume akikua mchana mmoja kama anavyokua mtoto mwengine kwa mwezi mzima kwa ajili ya kushughulikiwa na Mwenyezi Mungu".

4. "Akamwonyesha kwa haya macho ya kichwani (ya usoni) aliyomwonyesha. Nayo ni yeye mwenyewe Mwenyezi Mungu."

Na katika Burdah wameyatoa yanayofuata:

5. "Kama si yeye (Mtume s.a.w.w.) usingetoka ulimwengu (usingeumbwa)."

6. "Haukupata kunipiga vita Ulimwengu, nikataka nusra kwa Mtume, ila huipata tu."

Hayo ndiyo maneno waliyoyanukuu ndugu zetu wa Ahlu-Tawheed kuthubutisha kwamba, katika vitabu hivyo, muna shirki. Wakayaandamiza, pia, na hujja zao za kuyabatilisha hayo.

MAJIBU YETU :

Kwanza; tukumbuke kwamba tunalojadiliana si kuwa, katika vitabu vya maulidi, muna shirki au hamuna; la! Tunalojadiliana ni: maulidi ni bid'a au si bid'a; ni haramu au si haramu? Sisi, kwa upande wetu, katika makala yetu sabaa yaliyopita, kwa kujibu hujja zinazotolewa na wapinga maulidi, tumeonyesha kwamba maulidi si bid'a wala si haramu. Kwa hivyo sasa tunalolingojea kwa wapinga maulidi, wakiwamo Ahlu-Tawheed, ni majibu yao ya hujja tulizozitoa -- kiilimu na kimantiki, kama tulivyofanya sisi.

Pili; hata kama itakubaliwa kuwa hayo maneno waliyoyanukuu ni shirki -- na hilo hatulikubali kwa hujja tunayoitoa hapa chini -- hilo haliwi ni hujja ya kuharamishia maulidi au kuyasusia. La sawa kufanywa hapo ni kuyatoa hayo yanayoonekana ni shirki na / au kuyasahihisha; si kuzuia watu kuyasoma. Hivyo, kwa mfano, ndivyo alivyofanya marehemu Sheikh Abdulla Swaleh Farsy katika Wasila wa Nabahani. Yeye alipoona kwamba "Lawlaahu maa kunnaa walaa baaqiina" si sawa, hakuzuia watu, wala yeye hakuacha kuusoma. Alichofanya ni kukibadilisha kipande hicho na kukisoma alivyoona yeye ni sawa: "Lawlal ilaahu" Hakuutupa wasila wote, wala hakuzuia watu kuusoma kwa sababu tu muna kipande cha maneno asiyoyakubali.

Tatu; tunapoyataamali yote madondoo sita waliyoyanukuu Ahlu-Tawheed, ambayo nasi tumeyanukuu hapo juu, hakuna hata moja liwezalo kusemwa ni shirki kwa hujja ifuatayo:

Shirki ni kusema / kuamini kuwa Mwenyezi Mungu ana mwenziwe, au ana aliye sawa naye, au ana mfanowe, au ana anayetokana naye. Pia kusema / kuamini kuwa yuko muumbaji mwengine wa ulimwengu asiyekuwa Yeye, au muendeshaji (mudabbir) ulimwengu asiyekuwa Yeye, au mwenye haki ya kuweka sharia asiyekuwa Yeye, au anayelazimika kutwiiwa asiyekuwa Yeye, au kuna mtawala (haakim) asiyekuwa Yeye, au kuna mwenye haki ya kuabudiwa asiyekuwa Yeye.

Kwa kuwa hakuna hata moja, ya madondoo sita waliyoyanukuu Ahlu-Tawheed kutoka katika Barzanji na Burdah, linalosema hivyo, vipi basi mutakuwa muna shirki? Kama lipo, tunaomba watwambie ni dondoo lipi kati ya hayo waliyotutajia, na linaingia wapi katika hiyo taarifa ya shirki tuliyoieleza sisi hapo juu. Kama taarifa yetu imeacha mengine yaliyo shirki, basi tunaomba tukumbushwe. Kwa hakika haikuwa nia yangu kuingia katika masiala ya shirki kwa sababu hilo li nje ya maudhui yetu. Maudhui yetu ni maulidi ni bid'a au si bid'a; ni haramu au si haramu. Na hilo tushalijibu vya kutosha. Lakini, kwa kuwa wafuasi wa madhihabi ya wapinga maulidi hupenda kukibandika jina la bid'a au shirki kila wanachokipinga wao, nimeona japo kwa ufupi niwaeleze wasomaji wangu jamaa zetu hao hupotelea wapi katika kuielewa shirki ni nini, na si nini! Hilo, inshallah, tutalishughulikia wiki ijayo, kabla ya kuwajibu "Wakereketwa wa sunna Malindi".

ABDILAHI NASSIR

P.O. BOX 84603

MOMBASA

8 Jamaadal Uulaa, 1423

19 Julai, 2002

9

JAWABU KWA WAPINGA MAULIDI

MAKALA NO: (9)

MUANDISHI NI: SEHIKH ABILLAHI NAASIR

WANAVYOSEMA WAPINGA MAULIDI NA MAJIBU YETU

Wiki iliyopita tuliyataja maneno ambayo Ahlu-Tawheed wameyatoa katika Barzanji na Burdah ambayo, kwa maoni yao, ni shirki. Tukaahidi kuyajadili maoni hayo leo, baada ya kuieleza shirki ni nini.

Kwa taarifa tuliyoitoa sisi (na tumeomba tuelezwe kama tumeacha kitu katika taarifa hiyo), kati ya madondoo sita yaliyonukuliwa na ndugu zetu hao, matano yametushinda kuelewa vipi yaweza yakawa ni shirki. Kwa hivyo hatutashughulika nayo kwa leo mpaka hapo tutakapofafanuliwa inshallah. Tutakaloshughulika nalo leo ni moja tu lililobaki ambalo, kwa hujja walizozitoa kulipingia, tumeweza kulifahamu lililowafikirisha wao kuwa ni shirki. Nalo ni lile la Buswiri kusema katika Burdah: "Haukupata kunipiga vita Ulimwengu nikataka nusra kwa Mtume ila huipata tu."

Kulikosoa hilo, Ahlu-Tawheed wameitaja Sura 3:126 ambayo wameifasiri hivi: "Na msaada hautoki (kwa mwengine yoyote) isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye Nguvu na Mwenye hikima". Kwa kuitaja aya hii, kwa hivyo, tumeelewa kwamba ndugu zetu hao wameyaelewa maneno ya Buswiri hivi: "Kwa kuwa msaada (nasr) hautoki isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu, kuuomba kwa mtu mwengine yoyote asiyekuwa Mwenyezi Mungu, hata awe ni Mtume (s.a.w.w.), ni sawa na kumfanya mtu huyo ni Mwenyezi Mungu! Na kufanya hivyo ni shirki; kwa hivyo katika Burdah muna shirki!"

MAJIBU YETU :

Kwanza; katika tafsiri yao ya hiyo Sura 3:126 wameongeza maneno katika pinde, tuliyoyachapa kwa italiki, ambayo hayamo katika aya hiyo, wala hayaipunguzii maana lau yasingeongezwa.

Pili; kama maana ya "msaada hautoki isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu" ni kwamba haturuhusiwi kutafuta msaada kwa asiyekuwa Yeye, au asiyekuwa Yeye hana msaada wa kuutoa, basi ilikuwaje watu wa Madina wakaitwa answaar (wasaidizi)? Walimsaidia nani? Huyo aliyesaidiwa, aliukosa msaada wa Mwenyezi Mungu hata wakaingia kati wao? Na sisi Waislamu, pamoja na Mtume wetu (s.a.w.w.), tunamshirikisha Mwenyezi Mungu kwa kuwaita answaar watu wa Madina?

Tunaposoma Sura 3:81 tunaona jinsi Mwenyezi Mungu alivyochukua ahadi kwa Mitume Yake kwamba itamsaidia / itamnusuru (latansurunnahuu) Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Jee, kama "msaada hautoki (kwa mwengine yoyote) isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu," ilikuwaje hapo, Yeye Mwenyewe, akautaka kwa asiyekuwa Yeye? Jee, kwa kitendo hicho, Mwenyezi Mungu -- Mwenyezi Mungu apishe mbali! -- alikusudia kuifanya Mitume Yake ni miungu?

Katika Sura 7:157, kati ya sifa za waumini ambao "ndio wenye kufaulu", ni wale ambao wamemsaidia / wamemnusuru (wanaswaruuhu) Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Jee, kama "msaada hautoki (kwa mwengine yoyote) isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu", kwa nini akawaagiza waumini wamsaidie Mtume Wake? Kwa sifa hiyo hapo, ndio Mwenyezi Mungu amewafanya waumini kuwa ni miungu? Mwenyezi Mungu -- Mwenyezi Mungu apishe mbali -- hapo amefanya shirki?

Hali kadhaalika; tunaposoma Sura 28:15 tunaona jinsi jamaa yake Nabii Musa (a.s) "alivyomuomba msaada" (fastaghaathahuu) juu ya adui yake. Jee, Nabii Musa (a.s) alimrukia jamaa yake huyo, na kumwambia asilete shirki kwa kumuomba yeye msaada badali ya Mwenyezi Mungu? La! Alimsaidia; na siku ya pili (Sura 28:18) yule aliyeomba msaada jana (istanswarahuu) akamuomba tena! Jee, kama "msaada hautoki (kwa mwengine yoyote) isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu", kwa kutoa msaada wake huo, Nabii Musa (a.s) alikuwa Mwenyezi Mungu, au hakujua kuwa "msaada hautoki isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu"?

Kwa kutaja mifano hiyo hapo juu, sisi tusomao maulidi hatukusudii kukanusha yaliyomo katika aya iliyotajwa na wapinga maulidi, kuwa "msaada hautoki isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu"; hasha! Tunalokusudia ni kufahamisha kwamba: maneno yanapofanana, si lazima na maana yafanane (yawe mamoja). Kwa hivyo, msaada ambao Buswiri aliuomba kwa Bwana Mtume (s.a.w.w.), na sisi huukariri tunapoisoma hiyo Burdah, sio msaada ambao huombwa kwa Mwenyezi Mungu. Ni majina tu kufanana -- kama ulivyokuwa ule ambao Mwenyezi Mungu alimtakia Mtume Wake kwa Mitume mengine, na aliotutaka sisi waumini tumpatie Mtume Muhammad (s.a.w.w.), na ambao watu wa Madina walimpatia Bwana Mtume (s.a.w.w.) hata wakaitwa answaar (wasaidizi wake), na ule ambao Nabii Musa (a.s) alimpatia jamaa yake.

Msaada wa Mwenyezi Mungu unatokana na Yeye Mwenyewe; hakupawa na yoyote uweza huo wa kusaidia. Lakini wa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, akiwamo Mtume Muhammad (s.a.w.w.), si wake mwenyewe; ni wa kupawa (kuwezeshwa na Mwenyezi Mungu). Na hapo ndipo palipo na tafauti baina ya shirki ni nini, na si nini.

Ukiamini kwamba Mtume (s.a.w.w.) -- yeye mwenyewe, bila ya kupawa uweza huo na Mwenyezi Mungu -- aweza kusaidia; hiyo ni shirki. Na hilo silo alilokuwa akiliamini Buswiri, wala silo tunaloliamini sisi tusomao maulidi. Lakini ukiamini kuwa msaada uwezao kupawa na Mtume (s.a.w.w.) ni ule aliowezeshwa yeye na Mwenyezi Mungu; hiyo si shirki. Na hilo ndilo alilokusudia Buswiri katika Burdah, na ndilo tunaloliamini sisi tunaosoma maulidi. Kwa hivyo kubwa ambalo wapinga maulidi waweza kutwambia sisi ni kuwa Mtume (s.a.w.w.) hakuwa / hana uweza huo; kwa hivyo ni kazi bure kumuomba hivyo -- jambo ambalo hatulikubali kwa sababu ya hujja tulizonazo. Lakini hawawezi kutwambia ni shirki, kwa mifano mingi tuwezayo kuwatolea katika Qur'ani Tukufu.

Inshallah wiki ijayo tutaeleza kwa urefu ni wapi ambapo wapinga maulidi hupotea na kukosea kuielewa shirki. Nataraji baada ya hapo wataweza kuyaelewa yaliyomo katika Barzanji na Burdah.

ABDILAHI NASSIR

P.O. BOX 84603

MOMBASA

15 Jamaadal Uulaa, 1423

26 Julai, 2002

10

11

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KWANZA

AL - BAQARAH (NG’OMBE)

﴿ يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ اذْكُرُوا نِعْمَتِيَ الَّتِي أَنْعَمْتُ عَلَيْكُمْ وَأَنِّي فَضَّلْتُكُمْ عَلَى الْعَالَمِينَ ﴾

47.Enyi wana wa Israil, ikumbukeni neema Yangu niliyowaneemesha, na nikawatukuza kuliko viumbe wengine.

﴿ وَاتَّقُوا يَوْمًا لَّا تَجْزِي نَفْسٌ عَن نَّفْسٍ شَيْئًا وَلَا يُقْبَلُ مِنْهَا شَفَاعَةٌ وَلَا يُؤْخَذُ مِنْهَا عَدْلٌ وَلَا هُمْ يُنصَرُونَ﴾

48.Na iogopeni siku ambayo nafsi haitafaa nafsi kwa lolote.Wala hayatakubaliwa kwake maombezi (shufaa), wala hakitapokelewa kikomboleo; wala hawatanusuriwa.

WANAWA ISRAIL TENA!

Aya 47 - 48

MAELEZO

Enyi wana wa Israil ikumbukeni neema Yangu.

Aya hii inatilia mkazo Aya iliyotangulia, na ni maandalizi kwa yatakayokuja baada yake. Tutaonyesha katika sehemu itakayofuatia hekima ya kukaririka. Makusudio ya kukumbuka hapa ni kushukuru; yaani zishukuruni neema zangu kwa usikizi na twaa. Na nikawatukuza kuliko viumbe wengine.

Mwenyezi Mungu aliwafadhilisha kuliko mataifa mengine ya wakati huo. Herufi lam katika neno Alamin ni ya kuenea kwa kawaida, sio kuenea kwa kiuhakika. Inatosha kuwa ubora ni katika upande mmoja na sio pande zote. Upande ambao Waisrail wamepambanuka na watu wengine ni kwamba Mwenyezi Mungu aliwapelekea idadi ya Mitume; kwa mfano Musa, Harun, Yoshua, Zakaria na Yahya na wengineo. Wote hao ni Waisrail. Vyovyote ilivyo, kuwa bora kwao kwa watu wa zama zao kwa upande fulani, hakufahamishi kuwa bora katika kila upande kwa watu wa wakati huo; wala sio kwamba mtu wao ni bora kuliko mtu mwingine. Bali kule kuwa Mitume wengi wamekuja kutokana na kabila lao ni hoja juu yao na wala sio hoja yao, kwa sababu hilo linafahamisha kwamba wao walikuwa katika upotevu sana, ikawa kuna haja sana wapate waonyaji na wahadharishaji. Na ogopeni siku mbayo nafsi haitaifaa nafsi nyingine kwa lolote. Yaani kila mtu na lake hakuna dhahiri wala batini, hakuna kusaidiana wala kuoneana huruma.

﴿ يَوْمَ يَفِرُّ الْمَرْءُ مِنْ أَخِيهِ ﴾

Siku ambayo mtu atamkimbia ndugu yake. (80:34).

Wala hayatakubaliwa kwake (hiyo nafsi) maombezi (shufaa), wala hakitapokelewa kikomboleo; wala hawatanusuriwa. Yaani Kiyama ni sawa na mauti, haufai usaidizi wowote, haitafaa fidiya yoyote, hata ikiwa ghali, wala haitazuia nguvu yoyote hata iwe kubwa kiasi gani. Hakuna chochote isipokuwa Rehema ya Mwenyezi Mungu:

﴿ لَئِن لَّمْ يَرْحَمْنَا رَبُّنَا وَيَغْفِرْ لَنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴾

Kama hataturehemu Mola wetu na kutusamehe, bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliopata hasara. (7:149)

KUKARIRIKA KATIKA QURAN

Mara ya pili Mwenyezi Mungu anawaku-mbusha wana Israil neema Zake na amerudia baada ya Aya tano. Hiyo siyo Aya peke yake iliyorudiwa katika Quran, zimeka-ririka Aya nyingi hasa zile zinazofungamana na wana wa Israil pamoja na Musa(a.s.) . Wengi hujiuliza sababu ya kukaririka Aya.Wameafikiana wafasiri kwamba hekima ya kukaririka ni kutilia mkazo. Baada ya kupita siku, wakuu wa vyama, wanasiasa, wafanyibiashara na wenye mashirika wamegundua kwamba, kukar-irika jambo ndio njia nzuri ya kulipendekeza, kulikinaisha na kulifanyia propaganda. Kwa ajili hiyo ndio wakaweka mitindo mbali mbali ya matangazo, kukawa na watu maalum wa kuhusika nayo na yakawa ghali sana.

Gustave Lebon anasema katika kitabu chake kiitwacho The man and his work: Mwenye kulikariri tamko mara kwa mara hulibadilisha kuwa itikadi. Dr Gibson katika kitabu kilichotarjumiwa kwa kiarabu kayfa tufakkir (Vipi utafikiri) anasema Ibara zina sumaku zinapokaririka mara kwa mara mbele ya macho yetu na masikio yetu, zinapumbaza akili zetu kabisa. Kwa hivyo basi Quran inakariri kwa mfumo mwingine pamoja na kuzidisha makemeo na mengineyo kwa kiasi cha hekima inavyotaka.

SHUFAA (UOMBEZI)

Hapana budi shufaa iwe na pande tatu: Mwenye kuombwa, mwenye kuombewa na muombezi ambaye anakuwa kati ya hao wawili, anaomba kwa yule wa kwanza ili amsaidie wa pili ni sawa apate idhini ya yule mwenye kuombwa au la. Hiyo ndiyo Shufaa kwa viumbe. Ama shufaa mbele ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) maana yake ni msamaha na maghufira kwa mwenye dhambi; haitakuwa shufaa mbele ya Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa idhini yake.

Amesema mwenye Majmaul-Bayan Shufaa kwetu ni yenye kuhusika na kuondoa madhara na kuondoa mateso kwa mumin mwenye dhambi. Muutazila na Khawarij wamekanusha Shufaa ya Muhammad(s.a.w.w) kwa wenye madhambi makubwa katika umati wake, kwa maana hii tuliyoinakili kutoka kwa mwenye Majmaul-Bayan, lakini Imamiya na Ashaira wameithibitisha kwamba iko.Akili haihukumu kutokea Shufaa au kutotokea, lakini haioni pingamizi yoyote ya kupatikana. Kwa hiyo, kusihi kwake na kuthibiti kwake kutategemea kunakili kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Ambaye kumemthibitikia kunakili huko, basi ni wajibu kwake kuamini Shufaa, na kama hakuthibitikiwa basi atasamehewa. Kwa hali hiyo inatubainika kuwa shufaa si msingi wa dini na kwamba mwenye kuikanusha na huku anamwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi huyo ni Mwislamu bila shaka.

Tukirudi kwenye Aya za Quran tunakuta nyingine zinakanusha; kama ile inayosema:

﴿ يَوْمٌ لَّا بَيْعٌ فِيهِ وَلَا خُلَّةٌ وَلَا شَفَاعَةٌ ﴾

...Siku ambayo hapatakuwa na bishara wala urafiki wala Shufaa (uombezi).... (2:254)

Hapo inaonyesha kukanusha Shufaa kabisa.Na Aya nyingine zinathibitisha kwa sharti; kama ile inayosema:

﴿لَا تُغْنِي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا إِلَّا مِن بَعْدِ أَن يَأْذَنَ اللَّـهُ لِمَن يَشَاءُ وَيَرْضَىٰ ﴾

....Hautafaa chochote uombezi (shufaa) wao isipokuwa baada ya Mwenyezi Mungu kutoa idhini kwa amtakaye na kumridhia. (53:26)

Tukiziunganisha Aya mbili hizi na tukazikusanya pamoja, natija itakuwa, Mwenyezi Mungu atakubali Shufaa kutoka kwa mwombezi baada ya kumpa idhini. Sio lazima kupatikana idhini ya Mwenyezi Mungu kwa jina la mmoja mmoja, bali inatosha tu kwa Mtume kujua kwamba Shufaa ni halali ikiwa yule mwenye kuombewa si katika wenye kuwakandamiza watu na kunyanganya riziki zao; bali ni katika watu wa kawaida tu, ambao wanafanya madhambi ya kawaida.

Kwa maneno mengine ni kwamba makusudio ya idhini ya Mwenyezi Mungu kwa Shufaa ni kumpa wahyi Mtume wake kwamba Mimi nimekuruhusu kuwaombea uwatakao katika Umma wako ambao wamefanya mad- hambi maalum. Hapo basi mambo ya hao wenye madhambi yatakuwa mikononi mwa Mtume(s.a.w.w) ; naye atamwombea yule mwenye kustahiki kuombewa. Imethibiti kwamba yeye amesema: Nimeuweka akiba uombezi wangu kuwaombea wenye madhambi makubwa katika Umma wangu.

Sisi tuna yakini kuthibiti Shufaa katika Uislamu.Lakini hatujui kwa ufafanuzi; wakati huo huo tunaamini kwa imani ya mkato, kwamba mwombezi bora wa mtu ni matendo yake, na kwamba kitakachowaombea wenye dhambi ni toba. Hakika Mwenyezi Mungu haweki kizuizi kwa mwenye kutaka kuokoka akiwa na ikhlasi na akakimbilia kwenye ukarimu wa Mwenyezi Mungu hali ya kunyenyekea.

﴿وَإِذْ نَجَّيْنَاكُم مِّنْ آلِ فِرْعَوْنَ يَسُومُونَكُمْ سُوءَ الْعَذَابِ يُذَبِّحُونَ أَبْنَاءَكُمْ وَيَسْتَحْيُونَ نِسَاءَكُمْ وَفِي ذَٰلِكُم بَلَاءٌ مِّن رَّبِّكُمْ عَظِيمٌ ﴾

49.Na tulipowaokoa kwa watu wa Firaun waliowapa adhabu mbaya; wakiwachinja watoto wenu wakiume na kuwaacha hai wakike; na katika hayo ulipatikana mtihani mkubwa uliotoka kwa Mola wenu.

﴿وَإِذْ فَرَقْنَا بِكُمُ الْبَحْرَ فَأَنجَيْنَاكُمْ وَأَغْرَقْنَا آلَ فِرْعَوْنَ وَأَنتُمْ تَنظُرُونَ﴾

50.Na tulipoitenga bahari kwa ajili yenu na tukawaokoa, na tukawazamisha watu wa Firaun na hali mwatizama.

NA TULIPOWAOKOA

Aya 49 - 50

LUGHA

Neno: Aal, lina maana ya kurudi; kwa hiyo kila mwenye kurudiwa kwa nasaba, rai au itikadi basi yeye ni Aal wa wale wanaomrudia, kisha likawa linatumiwa zaidi kwa maana ya watu wa nyumba ya huyo mtu atakayetajwa, lakini hawezi kuitwa mtu Al mpaka awe na utukufu fulani. Makusudio ya Al-Firaun hapa ni wafuasi wake ambao walikuwa wakiwatesa wana wa Israil kwa amri yake. Abu-Hayan Al-Andalusi (Mhispania) amesema: Katika tafsir yake kubwa Al-Bahrul Muhit; Firaun ni lakabu (msimbo) ya wafalme wa Misri wakati huo; kama vile Kisra wa Fursi, Kaizari wa Roma, Najashi wa Uhabeshi, Tubba wa Yemen na Khaqani wa Uturuki.

Lakini alhamdulillah misimbo hii yote imebakia kuwa ni vigano tu!

MAELEZO

Baada ya Mwenyezi Mungu kuwakumbusha neema zake kwao kwa ujumla, sasa anawakumbusha kwa ufafanuzi. Bora zaidi ya neema aliyoidokeza ni kuwaokoa na Firaun na wafuasi wake ambao waliwapa Mayahudi adhabu kali. Mwenyezi Mungu ameifasiri adhabu hiyo kwa kusema: wakiwachinja watoto wenu wakiume na kuwaacha hai wakike. Yaani wanawaua watoto wanaume na kuwaacha wanawake waje kuwafanya watumishi.

* 18 Mwenye Majmaul Bayan anasema: Firaun aliota mambo yaliyomtisha. Wakamfasiria makuhani kuwa atazaliwa kijana wa kiume kutoka kwa wana wa Israil ambaye atakuja muua, ndipo Firaun akawafanyia hivyo wana wa Israil. Zaidi ya hayo Wamisri walikuwa wakiwadhalilisha Wayahudi kwa kuwatuma kazi za kuvunja mawe, kuchimba mifereji na kazi nyinginezo za sulubu. Msemo umewaelekea Mayahudi waliokuwepo zama za Mtume Muhammad(s.a.w.w) , kwa sababu wao walikuwa kwenye dini ya mababu zao na waliridhia amali zao. Na,mwenye kupenda amali ya watu wengine anakuwa ameshirikiana nao.

Na katika hayo ulipatikana mtihani mkubwa uliotoka kwa Mola wenu: Yaani, Enyi wana wa Israil, Mwenyezi Mungu amewatahini katika shida na raha, ili ijulikane kuwa je mtapigana jihadi na kuwa wavumilivi katika shida? Na je,mtashukuru raha? Au mtasalimu amri katika shida na mkufuru katika neema? Kwa hakika Mwenyezi Mungu hamtahini mtu ili ajue, la! Yeye anajua lenye kuwa kabla ya kuwa; isipokuwa yeye anamtahini mtu kwa ajili ya kusimamisha hoja juu yake. Kwani hakuna madai kwa asiyekuwa na hoja, hata kama yenye kudaiwa yanathibiti katika elimu ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.). Mwenyezi Mungu amewaonyesha Waisrail neema ya pili aliposema: Na tulipoitenga bahari kwa ajili yenu na tukawaokoa, na tukawazamisha watu wa Firaun

Yaani tulitenga bahari na tukafanya njia kumi na mbili kwa hisabu ya wajukuu. Wajukuu katika wana wa Israil ni koo katika kizazi cha Yaqub(a.s) Kwa ufupi Wayahudi walikuwa katika unyonge na udhalili wa hali ya juu; na adui yao alikuwa na nguvu za hali ya juu. Lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akabadilisha hali hiyo kupitia mikononi mwa Mtume wake Musa(a.s) , wao wakawa ndio wenye nguvu; na adui yao akawa dhalili, hilo wakaliona kwa macho yao; kama inavyosema Aya: Na hali nyinyi mnaangalia. Mwenyezi Mungu alimdhalilishia yule aliyewadhalilisha na akamwangamiza yule aliyetaka kuwaangamiza. Kwa hivyo basi wamelazimiana na hoja na imewalazimu kuwaidhika na kuzingatia, wala wasiwafanyie wengine yale waliyofanyiwa na wengine.

Lakini hivi leo mfano ule ule waliokuwa wakifanyiwa na Firaun ndio wanawafanyia Wapelestina. Na waendelee hivyo, lakini wajue hali itakuja wabadilikia tu, na yatawafika yale yaliyompata Firaun. Na waangalie ilivyokuwa kwa Nebukadnezzar na Warumi; na kwamba shujaa huvuma kisha akaisha. Jambo la kustaajabisha sana kwa mtu ni kwamba anapokuwa kwenye shida, kisha akaokolewa na Mwenyezi Mungu, basi hupetuka mipaka akafanya uovu na kusahau kila kitu. Wafasiri wengi wamesema, kwamba bahari iliyotajwa ni Bahari nyekundu (Red Sea).

﴿وَإِذْ وَاعَدْنَا مُوسَىٰ أَرْبَعِينَ لَيْلَةً ثُمَّ اتَّخَذْتُمُ الْعِجْلَ مِن بَعْدِهِ وَأَنتُمْ ظَالِمُونَ﴾

51. Na tulipomwahidi Musa masiku arobaini mkafanya ndama (kuwa Mungu) badala ya Mwenyezi Mungu mkawa madhalimu (wa nafsi zenu).

﴿ثُمَّ عَفَوْنَا عَنكُم مِّن بَعْدِ ذَٰلِكَ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴾

52.Kisha tukawasamehe baada ya hayo ili mpate kushukuru.

﴿وَإِذْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ وَالْفُرْقَانَ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ﴾

53.Na tulipompa Musa kitabu na upambanuzi ili mpate kuongoka.

NA TULIPOMWAHIDI

Aya 51 - 53

LUGHA

Neno: Musa kwa lugha ya Kiarabu lina maana ya: kifaa cha kunyolea nywele kilichotengezwa kutokana na chuma; lakini maana yanayokusuduwa kwa Musa bin Imran siyo ya Kiarabu, bali ni ya Kikibti ambayo ni matamko mawili: Mu lenye maana ya maji na Sa lenye maana ya mti. Kwa hiyo maana ya Musa ni maji ya mti, Ama maana ya kuitwa Maji ya mti, kama ilivyoelezwa katika Majmaul-Bayan, ni kwamba wajakazi wa Asiya(mke wa Firaun), walitoka kwenda kuoga wakakuta sanduku lililokuwa na Musa ndani yake baina ya maji na mti; wakawa naye.

MAELEZO

Baada ya Firaun kuangamizwa na Mwenyezi Mungu na waliokuwa pamoja naye, Waisrail Walipumua, wakarudi Misri wakiwa salama; kama livyoelezwa katika Majmau.Wakati huo, Tawrat ilikuwa bado haijateremshwa, wakamtaka Musa awaletee kitabu kutoka kwa mola wao. Basi Mwenyezi Mungu akamwahidi kumteremshia Tawrat na akamwekea wakati. Musa akawaambia: Hakika Mola wangu ameniahidi kitabu ambacho ndani yake mna ubainifu wa ambayo ni wajibu kwenu kuyafanya na kuyaacha. Akawambia wakati wake ambao ni masiku arobaini, na masiku hayo - kama ilivyosemwa - ni mwezi wa Dhul-Qaada, na siku kumi za mwezi wa Dhul- Hijja.

Musa akenda kwa Mola wake ili awachukulie watu wake kitabu; ndugu yake Harun akawa naibu wake. Kabla ya kwisha muda wa kuja Musa, walianza kuabudu ndama badala ya Mwenyezi Mungu, wakajidhulimu wao wenyewe.

Hiyo ndiyo maana ya dhahiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

Na tulipomwahidi Musa masiku arobaini mkafanya ndama (kuwa Mungu) badala ya Mwenyezi Mungu mkawa madhalimu ( wa nafsi zenu).

Baada ya Musa kurejea kwa watu wake, walitubia na wakarudi kwa Mola wao; Mwenyezi Mungu akawakubali toba yao, na hii ni neema ya tatu ambayo imeelezewa katika Aya:Kisha tukawasamehe baada ya hayo .

Ama neema ya nne ni; kitabu cha Mwenyezi Mungu:Na tulipompa Musa kitabu na upambanuzi ili mpate kuongoka. Kitabu chenyewe ni Tawrat; yenye kukusanya kila kitu kwa ajili ya kubainisha haki na batili, na halali na haramu.

Kunganisha kati ya neno, kitabu na kupambanua, ni kuunganisha sifa kwenye kile kinashosifiwa. Kwa muhtasari ni kwamba: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewakumbusha Waisrail katika Aya zilizotangulia, neema nne, Kuwaokoa kuchinjiwa watoto wao wa kiume na kuachwa wa kike wawe watumwa, kuangamia kwa Firaun, kusamehewa na kuletewa Tawrat.

Maelezo mazuri zaidi niliyoyasoma kuhusu maudhui haya, ni kauli ya Abu Hayan Al-Andulusi katika Tafsir Al -Bahrul Muhit; namnukuu: Tazama uzuri wa safu hizi ambazo zimepangika kwa mpango wa mtungo wa lulu na wa sayari katika falaki zake, kila safu katika hizo, yaani neema, imeishia kwa mnasaba wake na ikafikia daraja ya juu ya ufasaha ukitoka kwa Mwenyezi Mungu kupitia mdomoni mwa Muhammad mwaminifu wake, bila ya kusoma kitabu chochote kabla yake, wala kuandika kwa mkono wake.

Abu Hayan anaonyesha kuwa mpangilio huo wenye kupangika vizuri ni katika miujiza ya Muhammad; kwamba yeye anauelezea bila ya kujifundisha. Mwenyezi Mungu awarehemu wahenga, awasamehe na awape neema nyingi. Kwani hakika wao hawakuona chochote chenye harufu ya kuitilia mkazo dini hii na Mtume wake mtukufu isipokuwa walikinyooshea shingo kwa pupa na shauku; wakafanya haraka kukisherehesha, kukifafanua na kukitolea dalili. Lakini tuko wapi sisi wanavyuoni wa sasa ambao twapupia zaidi dunia; hatuoni umuhimu wowote isipokuwa umuhimu wetu tu; wala matatizo isipokuwa matatizo ya watoto wetu tu! Tuko wapi sisi na hao watukufu waliojitolea kila kitu kwa ajili ya kuutukuza Uislamu na Mtume wa Uislamu? Mwenyezi Mungu awasamehe na awainue, na kila mwenye kuitumikia dini, kwenye daraja ya juu.

﴿وَإِذْ قَالَ مُوسَىٰ لِقَوْمِهِ يَا قَوْمِ إِنَّكُمْ ظَلَمْتُمْ أَنفُسَكُم بِاتِّخَاذِكُمُ الْعِجْلَ فَتُوبُوا إِلَىٰ بَارِئِكُمْ فَاقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ عِندَ بَارِئِكُمْ فَتَابَ عَلَيْكُمْ إِنَّهُ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ ﴾

54.Na Musa alipowaambia watu wake: Enyi watu wangu! Hakika nyinyi mmejidhulumu kwa kufanya kwenu ndama (kuwa ni Mungu). Basi tubuni kwa Muumba wenu na jiueni; hilo ni bora kwenu mbele ya Muumba wenu.Basi akapokea toba yenu.Hakika Yeye ndiye apokeaye toba Mwenye kurehemu.

﴿وَإِذْ قُلْتُمْ يَا مُوسَىٰ لَن نُّؤْمِنَ لَكَ حَتَّىٰ نَرَى اللَّـهَ جَهْرَةً فَأَخَذَتْكُمُ الصَّاعِقَةُ وَأَنتُمْ تَنظُرُونَ ﴾

55.Na mliposema: Ewe Musa! Hatutakuamini mpaka tumwone Mungu waziwazi.Ukawanyakua ukelele na hali mwatizama.

﴿ثُمَّ بَعَثْنَاكُم مِّن بَعْدِ مَوْتِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ﴾

56.Kisha tukawafufua baada ya kufa kwenu ili mpate kushukuru.

﴿وَظَلَّلْنَا عَلَيْكُمُ الْغَمَامَ وَأَنزَلْنَا عَلَيْكُمُ الْمَنَّ وَالسَّلْوَىٰ كُلُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا رَزَقْنَاكُمْ وَمَا ظَلَمُونَا وَلَـٰكِن كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴾

57.Tukawatilia kivuli kwa mawingu na tukawateremshia Manna na Salwa: Kuleni katika vitu vizuri tulivyowaruzuku.Na hatukuwadhulumu, lakini wamejidhulumu wenyewe.

MUSA ALIPOWAAMBIAWATU WAKE

Aya 54 - 57

LUGHA

Manna ni kitu fulani kinachonata mithili ya asali, na Salwa ni tombo (aina ya ndege wa jamii ya kware, kama kuku).

MAELEZO

Na Musa alipowaambia watu wake: Enyi watu wangu! Hakika nyinyi mumejidhulumu kwa kumfanya kwenu Ndama (kuwa ni Mungu). Basi tubuni kwa Muumba wenu. Maana yoyote inayofahamika kwa kusikia tu haihitaji tafsiri, bali kuifasiri na kuisherehesha ni ufedhuli tu! Na Aya hii iko katika hali hiyo.

Na jiueni Makusudio ya kujiua yako wazi, ni kujitoa roho: wala hapana haja ya kufasiri vingine, kwa maana ya kuhalifu mapenzi na kuidhalilisha nafsi kwa kukiri dhambi na makosa au kumwabudu sana Mwenyezi Mungu; kama ilivyosemwa. Makusudio ya kujiua hapa, ni baadhi wawaue wengine. Kwa hivyo yule ambaye hakurtadi dini yake kwa kuabudu ndama ndio atamuua yule aliyertadi dini yake. Sawa na kusema kwake Mwenyezi Mungu:

﴿فَإِذَا دَخَلْتُم بُيُوتًا فَسَلِّمُوا عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ ﴾

...Mnapoingia katika majumba jitoleeni salamu.... (24:61).

Na vile vile kusema kwake

﴿وَلَا تَلْمِزُوا أَنفُسَكُمْ ﴾

...Wala msijikejeli: yaani msikejeliane (49:11)

Amesema Tabrasi katika Majmaul-Bayan kwa upande wa Shia, na Razi katika Tafsir Al-Kabir, kwa upande wa Sunni, kuwa Mwenyezi Mungu aliijaalia toba yao ni huko kujiua, sio kwamba wajiue baada ya kutubia. Hukumu hii ina mfano wake katika sharia ya Kiislamu, pale ulipozingatia kuua kuwa ni hadi na adhabu ya kosa la kurtadi.Hilo tutalieleza katika kifungu cha kurtadi kinachofuatia. Zinaendelea Aya kueleza maovu ya Waisrail: Na mliposema: Ewe Musa! Hatutakuamini mpake tumwone Mungu waziwazi Wakati Musa alipowaendea na Tawrat, baadhi yao walisema: Hatuamini kuwa kitabu hiki kinatoka kwa Mungu mpaka tumwone kwa macho; bila ya kizuwizi chochote kati yetu sisi na Yeye; na atueleze ana kwa ana kuwa Yeye amekutuma na kitabu hiki.

Sijui kama wale wanaokanusha kuwepo Mwenyezi Mungu wakati huu, kwa kuwa tu hawajamuona kwa wazi, wanategemea Waisrail na inadi yao? Au vipi? Mayahudi walimwambia Musa: Hatutakuamini mpaka tumwone Mungu. Hawa wa sasa nao wanasema: Hakuna chochote chenye kupatiana isipokuwa kile tunachoweza kukiona kwa jicho, kukigusa kwa mkono, kukinusa kwa pua au kukionja kwa mdomo. Hivyo ndivyo inavyokaririka historia ya picha ya upinzani wa haki katika kila kizazi.

Yakawanyakua mauti ya ghafla na hali mwalizania Yaani adhabu kutoka mbinguni iliwapata wale waliomwambia Musa hatukuamini mpaka tumwone Mungu wazi wazi, wakaangamizwa mbele ya macho ya wale wasiopinga. Kisha tukawafufua baada ya kufa kwenu ili mpate kushukuru. Baadhi ya wafasiri kama vile Muhamad Abduh, katika tafsiri Al-Manar, amesema: Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakuwarudishia uhai mara ya pili baada ya kuchukuliwa na ukelele; na kwamba makusudio ya kufufuliwa kwao ni kizazi chao kuwa kingi. Wengine wakasema kuwa sio hivyo, hayo hayafahamiki kutokana na dhahiri yake ilivyo, na kwamba waliorudishwa ni wale wale waliouliwa na ukelele.Na hii ndiyo sawa, kwani hapana sababu inayolazimisha taawil, madamu kurudishwa kuwa hai kunawezekana kiakili. Na hilo lilimtokea Uzair, kama inavyofahamisha Aya:

﴿قَالَ أَنَّىٰ يُحْيِي هَـٰذِهِ اللَّـهُ بَعْدَ مَوْتِهَا فَأَمَاتَهُ اللَّـهُ مِائَةَ عَامٍ ثُمَّ بَعَثَهُ﴾

Akasema: Mwenyezi Mungu atauhuisha vipi (mji) huu baada ya kufa kwake? Mwenyezi Mungu Akamfisha kwa miaka mia, kisha akamfufua.... (2:259)

Kimsingi,lililotokea haliwezi kuwa muhali. Kwa hakika inaonyesha kwamba makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: Yakawanyakua mauti ya ghafla, na kauli yake tukawafufua ni wale waliokuwa wakati wa Musa waliosema: Mpaka tumwone Mungu waziwazi Kwa hiyo, kauli haiwahusu Mayahudi waliokuwa na mtume, msemo umeele-kezwa kwao kwa kuangalia kuwa wanatokana na kizazi kilichosema hivyo.

Tukawatilia kivuli cha mawingu na tukawateremshia Manna na Salwa. Hayo yaliyotokea wakati Waisrail walipotoka Misri wakahangaika katika jangwa la Sinai, kusikokuwa na majengo; wakamlalamikia Musa kwa joto la jua; Mwenyezi Mungu akawaneemesha kwa wingu lililowafunika na kuwakinga na joto la jua kali. Vile vile Mwenyezi Mungu akawaneemesha kwa Manna na Salwa ili wale. Yatakuja maelezo katika tafsiri ya Aya ya 60 kuwa maji yaliwabubujikia kutoka katika jiwe alilolipiga Musa kwa fimbo yake. Inashangaza kuona baadhi ya wafasiri, wakifasiri yale aliyoyanyamazia Mwenyezi Mungu kuyabainisha; kama vile idadi ya waliojiua kwa toba ya kuabudu ndama, kuwa ni watu elfu moja; vile vile walionyakuliwa kuwa ni watu sabini. Ama kuhusu Manna, wanadai kila mtu alikuwa akipata pishi moja na kwamba Salwa ilikuwa ikishuka kutoka mbinguni ikiwa moto moto huku ikifuka moshi, na mengineyo ambayo hayana kauli yoyote iliyopokewa au kudhaniwa.

Imethibiti Hadith kutoka kwa Mtume mtukufu(s.a.w.w) :Hakika Mwenyezi Mungu amenyamazia mambo si kwa kusahau, ni kwa kuwaonea huruma, kwa hiyo msijikalifishe nayo.

Katika Nahjul-Balagha amesema Imam Ali(a.s) :Hakika Mwenyezi Mungu amewafaradhisha faradhi msizipoteze, na amewawekea mipaka msipetuke; na ameyakataza mambo basi msifanye; na ameyanyamazia mambo si kwa kusahau, basi msijikalifishe (nayo).

Na hawakutudhulumu sisi, lakini wamejidhulumu wenyewe .Kukanusha dhulma kwa Mwenyezi Mungu ni sawa na kukanusha kuwa na watoto na mshirika; yaani kumwepusha kabisa na hilo; sawa na kumwambia mseja kuwa hana mtoto. Ama kujidhulumu kwa Mayahudi ni kwa sababu ya usafihi wao na kuzikanusha neema za Mwenyezi Mungu ambaye hanufaiki na twaa ya mwenye kumtii wala hayamdhuru maasi ya mwenye kuasi na madhara ya uasi yanamrudia mwasi. Anasema Ali bin Abu Twalib (a.s.):Ewe mwanadamu ukiona Mola wako anaendelea kukuneemesha nawe unamwasi, basi mhadhari.

Kwa ufupi Aya hizi zinaonyesha ibada ya Waisrail kwa ndama, kutubia kwao kwa kujiua na kutaka kwao kumwona Mwenyezi Mungu. Vile vile kuangamia kwao na kufufuliwa kwao, kufunikwa na kiwingu na kulishwa Manna na Salwa.. Tutaelezea kisa cha Nabii Musa na Waisrail katika surah ya Maida (5) Inshallah. Waliposema kumwambia Musa:

﴿فَاذْهَبْ أَنتَ وَرَبُّكَ فَقَاتِلَا إِنَّا هَاهُنَا قَاعِدُونَ﴾

...Basi nenda wewe na Mola wako mkapigane sisi tutakaa hapa (5:24).

Hilo ni tamko linaloonyesha ukhabithi na uduni wa Mayahudi. Wa kwanza waliogundua uhabithi na uduni wao ni watu wa Firaun ambao waliwachinja watoto wao wa kiume na kuwaacha wa kike. Kumwona Mungu Kutokana na Aya tukufu:Mpaka tumwone Mungu waziwazi.

Tutaonyesha mzozo uliopo katika madhehebu ya Kiislamu na tofauti zao kuwa akili inajuzisha kuonekana Mwenyezi Mungu kwa macho au la?!

Wamesema Ashari (Sunni): Hakika kuonekana Mungu kwa macho kunawezekana kiakili, kwa sababu Yeye yupo na kila kilichopo kinawezekana kuonekana.

Imamiya na Mu’utazila wamesema; Haijuzu kuonekana Mwenyezi Mungu kwa macho katika hali yoyote ile, si duniani wala akhera, kwa sababu Yeye si umbo hata akaonekana, wala haingii katika umbo wala upande fulani.

Baada ya akili kuthibitisha kutoonekana, wamechukulia kwamba ataonekana kiakili sio kwa macho na kwa hakika ya imani sio ya viungo vya mwili, kwa mujibu wa alivyosema mwanafalsafa mkubwa na mashuhuri, Muhammad bin Ibrahim Shirazi, maarufu kwa jina la Mulla Sadra. Katika aliyoyatolea dalili Mulla Sadra kuhusu kutoonekana, ni kauli yake: Kuhisi kitu ni hali inayozuka kwa kile kinachohisi kikikutanishwa na kinachohisiwa kilichozuka. Hivyo basi, kulazimisha kitu ambacho hakikuzuka kuwa kinahisiwa ni kama kulazimisha kitu kisicho na upande kuwa kina upande.

Kauli yake hii - kama ninavyoona - ni kwamba jicho haliwezi kuona kitu isipokuwa kwa sharti mbili:

Liwe linaweza kuona na kiwe kile kinachoangaliwa kinaweza kuonekana kwa jicho. Hilo ni jambo la msingi; likikosa jicho uwezo wa kuona, au kikiwa kitu hakina uwezo wa kuonekana; itakuwa kuona hakuko. Jicho ni dogo na duni zaidi kuweza kuona dhati tukufu; kama vile ambavyo, Mwenyezi Mungu ni mkubwa wa kuonekana na jicho. Nilipokuwa nasoma ibara hii, tukufu akili yangu ilienda kwa mwanafalsafa wa Kiingereza John Luk, anayesema kuwa: kitu kina sifa yake ya kwanza yenye kukithibitikia, ambayo haipambanuki nayo, ni sawa mtu aitambue au asiitambue; kama vile vitu vinavyosimamisha kitu hicho.

Vile vile kuna sifa ya pili ambayo haiwezi kuepukana na kuhisiwa au kujulikana; kama rangi, sauti na ladha. Rangi siyo sifa ya kitu, kama inavyoonekana, isipokuwa ni mawimbi ya kimwangaza yanayohusika kati ya kitu na jicho; kama wasemavyo wataalamu. Vile vile sauti ni mawimbi ya kihewa; na ladha isingekuweko kama si mdomo. Kwa hiyo ladha inahitilafiana kwa uzima wa mdomo na ugonjwa.Kwa ufupi anataka kueleza kuwa hakuna rangi bila ya jicho; wala sauti bila ya sikio; au ladha bila ya mdomo. Hakuna mwenye kutia shaka kwamba nuru ya Mwenyezi Mungu imezidi mawimbi ya kimwanga na mengineyo.Kwa hivyo yakikosekana mawimbi haya, ndio kumekosekana kuona.