• Anza
  • Iliyopita
  • 2 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 6024 / Pakua: 1767
Kiwango Kiwango Kiwango
MFALME WA UVUMILIVU

MFALME WA UVUMILIVU

Mwandishi:
Swahili

MFALME WA UVUMILIVU

(Imamu Hasan Al-Mujtaba A.S.)

KIMEANDIKWA NA: Maulana Sayyid Ali Naqi Saheb

KIMETAFSIRIWA NA: Bwana L.W. Hamisi Kitumboy

KIMETOLEWA NA KUCHAPISHWA NA

BILAL MUSLIM MISSION OF TANZANIA

P.O. BOX 20033

DAR ES SALAAM - TANZANIA

TEL: 2120111 / 2112420 FAX: 2116550

EMAIL: bilal@cats-net.com / bilal@raha.com

WEB: bilaltz.org

Haki ya kunakili imehifadhiwa na

Bilal Muslim Mission of Tanzania

ISBN 9976 956 56 8

Toleo la Kwanza: 1979, Nakala 2000

Toleo la Pili: 1990, Nakala 2500

Toleo la Tatu: 2007, Nakala 1000

Kimetolewa na Kimechapishwa na

BILAL MUSLIM MISSION OF TANZANIA

P.O. BOX 20033

DAR ES SALAAM - TANZANIA

TEL: 2120111 / 2112420 FAX: 2116550

MWENYEZI MUNGU ANASEMA:

(Ewe mwanadamu! Ikumbuke) siku Tutakapowaita kila watu pamoja na Imamu wao; basi atakayepewa kitabu (chake cha Amali) kwa mkono wa kulia, hao watavisoma vitabu vyao (kwa furaha); (Bani Israil, 17:71)

MTUKUFU MTUME (S.A.W.W.) AMESEMA:

Yeyote yule afaye pasi na kumjua Imamu wa zama zake, atakuwa kafa kifo cha ujinga.

MTUKUFU MTUME (S.A.W.W.) AMESEMA:

Hao (Ulul Amr watajwao kwenye Qur’ ani 4:59) ni Makhalifa wangu na Maimamu wa Waislamu baada yangu. Wa kwanza ni Ali, kisha ni Hassan, kisha ni Husayn, kisha ni Ali bin Husayn, kisha ni Muhammad bin Ali, kisha ni Jaafar bin Muhammad, kisha ni Musa bin Jaafar, kisha ni Ali bin Musa, kisha ni Muhammad bin Ali, kisha ni Ali bin Muhammad, kisha ni Hassan bin Ali, kisha ni Muhammad bin Hassan (Mahdi)...

(Kifayatul Athar na Rawdhatul Ahbab, vya Hafidh Jamaluddin Muhaddith).

SHUKRANI

Kitabu hiki kimeandikwa kwa lugha ya Urdu na Mtukufu Sayadul Ulama Maulana Sayyid Ali Naqi Saheb, Mujtahidi wa Chuo Kikuu cha Lucknow, Uhindi.

Kimetafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza na Sayyid Hashim Riza Rizvi, B.A., B.T. Yadgar-e-Husaini H.S. School Allahabad, Uhindi, na kutolewa na Imamia Mission Lucknow, U.P., Uhindi.

Kimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili kutoka katika hiyo ya Kiingereza na Marehemu Bwana L.W. Hamisi Kitumboy (aliyekuwa Mubalighi Mkaguzi, wetu) na kikachekiwa na kusahihishwa na Mwalimu Dhikiri (Zakir Ali) U.M. Kiondo, Edita wa Sauti ya Bilal.

UTANGULIZI

Maisha ya mwanadamu yamejaa matukio ya kila namna ya kufurahisha na ya kuchukiza. Na sifa nzuri zaidi kwa roho ya mtu ni kuhisi kwamba yu alazimika kutimiza wajibu wake, na kiwango cha juu zaidi kwa heshima ya mtu ni kutimiza wajibu wake bila ya kujali gharama ya utimizaji wa wajibu huo. Ili kuijenga fikara hiyo katika akili zetu, ni lazima kujifunza maisha ya wale watu waliokuwa na madaraka katika mioyo yao na akili zao na ambao kila mara walifanya mambo huku wakiwa na fikara za kutimiza wajibu, ambazo hazikuingiliwa na maoni yao wala silika zao. Maisha ya familia ya Mtukufu Mtume (s.a.w.) yalikuwa ni mfano mzuri wa fikara za kiheshima na mtu kujiona kuwa yuna wajibu fulani. Tunaona maishani mwao aina mbali mbali za msingi huu muhimu sana. Kwa vile hali za maisha yao waliyokiishi hapa duniani zinatofautiana, kutoka mtu hadi mwingine, hali za maisha yao hutofautiana pia. Maisha ya mjukuu wa kwanza wa Mtume (s.a.w.), Imamu Hasan (a.s.) yalikuwa, peke yake, mfano wa uvumilivu, huruma, na ustahimilivu.

JINA LAKE:

Jina lake ni HASAN. Jina lake la heshima lilikuwa Al-Mujtaba (aliyechaguliwa) na Kunyat (jina la utoto) wake ni Abu Muhammad. Alikuwa mtoto wa Sayyidina Ali (a.s.) na Bibi Fatimah (a.s.), bintiye Mtukufu Mtume (s.a.w.).

KUZALIWA KWAKE:

Alizaliwa tarehe 15 mwezi wa Ramadhani katika mwaka wa tatu wa Hijiriya (mnamo mwaka 625 Miladiya). Kuzaliwa kwake kulikuwa tukio la kwanza la neema ya aina ya pekee nyumbani mwa Mtukufu Mtume (s.a.w.). Mtume (s.a.w.), alipokuwa Maka alipoteza wanawe wote mmoja hadi mwingine na alibakia na binti mmoja (Bibi Fatimah a.s.) tu. Makafiri wakaanza kumdhihaki na kumwita Abtar (mtu ambaye kizazi chake chote kimemalizika.

Mtume (s.a.w) alihuzunika sana kuambiwa hivyo, hivyo Mwenyezi Mungu akateremsha Sura ya Kauthar (Sura ya 108) ambayo ndani yake alineemeshwa kwa habari njema kuwa Mwenyezi Mungu atampa furaha ya kuwa na dhuria wengi na kuwa adui yake ndiye atakayekuwa Abtar. Hivyo kuzaliwa kwa Imamu Hasan (a.s.) kulikuwa kutimilika kwa bishara ya Sura hii. Ulimwengu unafahamu kwamba: ingawa maadui wa Imamu Hasan (a.s.) na Imamu Husain (a.s.) wamejaribu kila waliloliweza ili wasiwe na dhuria, vivyo bado dhuria wao wanapatikana katika kila pembe ya ulimwengu. Hivyo, kwa Mtume (s.a.w.), kuzaliwa kwa mjukuu huyu kulikuwa uthibitisho wa kwanza wa kudumu udhihirishao kuwa Qurani Tukufu inatoka kwa Mwenyezi Mungu, na makafiri waliona kuwa Mwenyezi Mungu aliitimiza ahadi yake.

Mtoto alipotimiza umri wa siku saba, Mtume (s.a.w.) alifanya Aqiqah (sherehe ya kunyolewa nywele alizozaliwa nazo mtoto). Kufuatana na Amri ya Mwenyezi Mungu, akamwita mtoto huyo Hasan jina hili hakulipata mtu ye yote kabla. Hali kadhalika jina la Husain.

KULELEWA KWAKE:

Alikuwa chini ya ulezi wa babu yake Mtukufu (s.a.w.) kwa muda wa miaka minane. Hakuna mtu ye yote yule aliyempenda mjukuu wake kama Mtukufu Mtume (s.a.w.) alivyompenda mjukuu wake Hasan (a.s.). Kuna hadithi kadha wa kadha zilizopokewa juu ya wajukuu wawili wa Mtukufu Mtume (s.a.w.) zikionyesha mapenzi yake kwao na heshima wanayoistahili, kwa mfano hadithi hizi za Mtume (s.a.w.) zisemazo:-

(i) Hassan na Husain ni viongozi wa vijana wa Peponi.

(ii) Hawa wawili (Hasan na Husain) ni johari za Pepo ya Mwenyezi Mungu.

(iii) Wao (Hasan na Husain) ni mashada.

(iv) Ewe Mwenyezi Mungu, (mimi) nawapenda (Hasan na Husain); basi uwe mwenye huruma kwao.

Zaidi ya hayo, Mtukufu Mtume (s.a.w.) alisisitiza kutowaita vijana hawa wajukuu zake, bali watoto wake hasa.

Kuna hadithi ya Mtukufu Mtume (s.a.w.) iliyoandikwa katika vitabu vyote vya hadithi za Mtume (s.a.w.) isemayo kuwa Mtume (s.a.w.) alisema, Mwenyezi Mungu kampa kila mwanaume wana aliowazaa yeye mwenyewe, lakini mimi kanipa wana waliozaliwa na Ali. Zaidi ya hapo, wana hao walikuwa wale wana ambao asili ya tabia zao ilikuwa ule utakatifu wenyewe na mfano mzuri wa mkono wa malezi ya Mtume (s.a.w.). Kwa hakika, tangu utotoni mwao walikuwa mfano mzuri wa tabia za Mtukufu Mtume (s.a.w.). Yeye Mtume (s.a.w.) mwenyewe alisema, Hasan ana ustahimilivu wangu mzuri na Husain ana ukarimu na ushupavu wangu. Ustahimilivu bora ni fungu dogo la maneno lakini kwa hakika ni muhtasari wa sifa nzuri sana. Mtukufu Mtume (s.a.w.) wakati wa Utume wake alikuwa akimchukua Imamu Hasan (a.s.) kwenda naye kazini kwake tangu utotoni mwake, jambo lionyeshalo kuwa Mtume (s.a.w.) alitaka kuiacha kazi ya kuuhami Uislamu mikononi mwa watu wa nyumba yake. Moja ya matukio kama hayo ni lile la Mubahila ambapo Imamu Hasan (a.s.) alifuatana na wazazi wake, babu yake na nduguye kuonyesha kuwa wao walikuwa wameuchukua ujumbe wa Mwenyezi Mungu.

Mnamo tarehe 2 Rabiul-Awwal (Mfunguo Sita) mwaka wa 11 Hijiriya Mtukufu Mtume (s.a.w.) alifariki dunia Imamu Hasan (a.s.) aliondokewa na chanzo cha furaha yake na amani ya akili. Baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.) Imamu Hasan (a.s.) alimpoteza mamie katika muda wa miezi michache tu tangu kufariki kwa Mtume (s.a.w.) na alibakiwa na babie tu. Alipitisha ujana wake katika muda mrefu alioupitisha babie katika kujitenga. Miaka ishirini na mitano ya maisha ya kujitenga mwishoni mwao ilimleta kupewa ukhalifa Imamu Ali (a.s.). Hivyo Imamu Hasan (a.s.) ilimbidi afuatane na baba yake katika vita vya Jamal, Siffin na Nahrawan.

UKHALIFA WAKE:

Mnamo tarehe 21 ya mwezi wa Ramadhani, mwaka wa 40 Hijiriya Hadhrat Ali (a.s.) alifariki. Waislamu wote waliukubali Ukhalifa wa Imamu Hasan (a.s.), naye katika hotuba yake kwa Waislamu alizungumzia kuhusu tabia za baba yake na maisha yake ya kawaida tu kwa maneno yaliyomshtua hata yeye mwenyewe na watu wote waliokuwepo hapo walilia. Kisha alizungumzia kuhusu kustahiki kwake kuwa Khalifa, sifa zake na jamii yake. Bwana Abdallah Ibn Abbas alitoa hotuba na aliwataka watu kula kiapo cha utii (Baiat) kwa Imamu (a.s.). Watu wote waliitikia kwa furaha. Kisha Imamu Hasan (a.s.) aliwauliza watu, Je, mtanitii ninapopigana au ninapofanya amani? Watu wote walikubali. Kisha alichukua utawala mikononi mwake, akawateua maofisa, akatoa amri zake na akaanza kuhukumu kesi.

Wakati huo Muawiyah (Gavana wa Shamu) alinyakua Kiti cha enzi na kujitangazia kuwa yu mtawala aliyehuru kutokana na serikali ya Khalifa wa Mtume (s.a.w.). Kwa upande mwingine kila aina ya upinzani mkali na kutoaminiana vilionekana kila mahali katika nchi ambayo Imamu Hasan (a.s.) alichaguliwa kuwa Khalifa wake. Hata wakati wa baba yake kulikuwepo kikundi ambacho hakikuupenda mwenendo wake wa kuifuata barabara misingi ya Uislamu na ambacho kiliikataa kabisa misingi hiyo.

Ingawa Khawarij (waliojitenga) walishindwa katika vita ya Nahrawan, lakini wanachama wa kikundi hicho walisambaa katika pembe zote za nchi kuvuruga amani ya watu na mtu aliyemwua Sayyidina Ali (a.s.) alikuwa mtu wa kikundi hiki.

Wakati nchi ingali bado katika msiba wa Sayyidna Ali (a.s.), na Imamu Hasan (a.s.) bado hajafanya mipango yote ya serikali, gavana wa Shamu (aitwaye Muawiyah) alianza kupeleka majambazi ya kisirisiri nchini Iraq. Mmoja wa majambazi hao alikamatwa na akafungwa mjini Kufa (Iraq) na mwingine akafungwa mjini Basrah (Iraq). Watu hao walikuja kumvurugia mambo Hasan (a.s.). Kisha Imamu Hasan (a.s.) alimwandikia barua Muawiyah akimwambia wewe hutaki kuacha uchokozi wako na umetuma majasusi wako hapa. Inaonyesha kwamba wewe unataka vita. Basi jitayarishe, kwa maana hali hii ya kuzuka kwa vita baina yetu haiko mbali. Zaidi ya hapo nimesikia kuwa ulitumia maneno ya matusi kwa baba yangu alipokufa. Hivyo sivyo wafanyavyo watu wenye busara. Kifo kitatufika sote; ninaweza kufa leo na wewe ukafa kesho. Kwa hakika hatumfikirii mtu aliyekufa kuwa kafa kweli. Yeye kaenda tu kwenye mapumziko yake kutoka sehemu fulani kwenda kwenye sehemu nyingine.

Imamu Hasan (a.s.) na Muawiyah waliandikiana barua nyingi baada ya barua hii. Muawiyah akijua barabara tamaa za watu wa Kufa na kutoafikiana kwao baina yao na upungufu wao katika kutenda mambo yao, alifikiria kuwa huo ndio wakati mzuri kuishambulia Iraq. Alipofika mpakani, Imamu Hasan (a.s.) alijitayarisha kwenda kupambana naye. Alimtuma Bwana Hajar ibn-i-Adi kwenda kukusanya watu kwenda vitani. Lakini matokeo yake ni kama yalivyotegemewa. Watu wachache tu ndio walioitikia mwito huo. Idadi hii ni pamoja na watu wa kikundi cha Khawarij na wengine wachache waliopendelea kupata nyara za vita na wengine wamekuja kwa ajili ya kulazimishwa na wakuu wa makabila yao. Wachache tu ndio waliokuwa waaminifu kweli.

Muawiyah alimpeleka Abdullah ibn-i-Aamir ambaye alipiga hema mahali paitwapo Ambar. Imamu Hasan (a.s.) aliondoka kwenda kupambana naye na akasimama mahali paitwapo Saabat karibu na mji wa Dair-i-Kaab. Ili kupata kujua fikara za watu wake, Imamu (a.s.) aliwakusanya na akawahutubia akisema, Sina mfundo. Ninakujalini sawa kabisa na vile ninavyojijali mimi mwnyewe. Ninajaribu kupata wazo lenu. Ninategemea kuwa mtakubali kunipa wazo lenu. Ninaona kuwa wengi wenu mmekuwishavunjika mioyo na sioni kuwa nikulazimisheni kwa vyo vyote vile kufanya jambo fulani kinyume na mapenzi yenu. Baada ya hotuba yake kulizuka makelele kutoka kwa wasikilizaji (askari) wake. Baadhi yao walipiga kelele wakipinga kupigana katika vita hiyo. Kama kingelikuwa kikundi cha adui zake tu hali isingelikuwa mbaya sana kwa mwana shujaa wa Sayyidina Ali (a.s.). Lakini kundi hili lilikuwa mchangonyiko (wa maadui na marafiki) na watu wachache kutoka miongoni mwa makafiri walimshambulia na wakanyakua zulia alilolikalia Imamu (a.s.) na mtandio wake kutoka begani mwake. Mara moja Imamu Hasan (a.s.) alimpanda farasi wake na kuuliza, Wako wapi (watu wa makabila ya) Rabiah na Hamdan? Mara moja watu wa makabila haya walikusanyika na kuwasogeza mbali wale watu watovu wa adabu. Kutoka hapo Imamu (a.s.) aliondoka kwenda Madina. Alipokuwa njiani, Khawarij mmoja aliyeitwa Jurah wa kabila la Asad aliyekuwa kajificha alimshambulia Imamu (a.s.) kwa upanga na kumjeruhi katika nyonga yake. Jurah alitiwa nguvuni na kuadhibiwa. Kidonda hicho kiliuguzwa mjini Madina na kilipopona Imamu (a.s.) alijitayarisha tena kupambana na Muawiyah.

MAPATANO:

Muawiyah alijua kutokuwa na moyo wa kupigana, wa jeshi la Imamu Hasan (a.s.) na alijua kuwa Imamu Hasan (a.s.) mwenyewe hakuwa na nia ya kupigana; lakini vile vile alijua kwamba kwa vyo vyote vile iwavyo, mjukuu wa Mtume (s.a.w.) hatakubali kufanya mapatano ya muda chini ya masharti yaliyo kinyume na misingi ya Uislamu. Hivyo kwanza aliwapelekea ujumbe watu wa Imamu Hasan (a.s.) akiwataka wasihatarishe maisha yao na kumwaga damu na akawahonga baadhi yao na kuwatisha wengine kwa kuwatajia idadi kubwa ya askari wa jeshi lake; kisha akampelekea ujumbe Imam Hasan (a.s.) kuwa yeye (Muawiyah) alikuwa tayari kufanya mapatano ya muda chini ya masharti yo yote yale atakayoyapenda Imamu (a.s.).

Kwa hakika Imamu Hasan (a.s.) hakupenda kuanzisha vita yo yote ile kwa sababu ya utovu wa uaminifu wa watu wa kikundi chake. Lakini wakati huo huo alitaka kuondoa hali yo yote ile itakayoleta kutoeleweka kwa msimamo wake. Sasa Muawiyah alipodhihirisha kupendelea kwake kufanya mapatano ya muda chini ya masharti yatakayotolewa na Imamu (a.s.), hakukuwepo tena uwezekano wa Imamu (a.s.) kukataa. Ingawa Imamu alifahamu kabisa kuwa mtawala wa Shamu asingeliweza kuyafuata barabara masharti ya mapatano hayo ilimbidi akubali kufanya mapatano hayo ya muda, kwa maana hakutaka kutoa nafasi kwa kikundi cha Muawiya kupata sababu ya kuanzisha vita. Kabla ya kumpelekea Muawiyah jibu lake la mwisho aliwaita watu wake na akawaambia akisema, Mmepigana vita mbili zilizo kali. Baadhi ya watu wenu wameuawa katika vita ya Siffin, ambao bado mungali mkiwalilia. Wengine wameuawa katika vita ya Nahrawan, ambao bado damu yao mwaitakia fidia. Kama mko tayari kufa basi na tuyakatae mapatano haya na kama mnayapenda maisha yenu zaidi (kuliko ukweli) basi natuyakubali.

Watu walianza kupiga kelele kutoka kila upande wakisema, Tunapenda kuishi, na tufanye mapatano. Matokeo yake ni kwamba Imamu Hasan (a.s.) alitayarisha masharti ya mapatano hayo na kuyapeleka kwa Muawiyah:-

Masharti ya Mapatano:

Masharti ya Mapatano hayo yalikuwa haya:-

1. Kwamba Muawiyah atawale kwa mujibu wa Quran Tukufu na Hadithi za Mtukufu Mtume (s.a.w.).

2. Kwamba Muawiyah hatakuwa na haki ya kuweka mrithi wa Ufalme wake.

3. Kwamba maisha ya watu wote nchini Shamu, Iraq, Hijaz, Yemen, na sehemu zote nyinginezo yatakuwa salama.

4. Kwamba wafuasi wa Hadhrat Ali (a.s.) watakuwa katika usalama na kwamba mali zao na familia zao zitatetewa po pote pale walipo.

5. Kwamba Muawiyah hatajaribu kumuuwa Imamu Hasan (a.s.) wala nduguye Husain au mtu ye yote wa nyumba ya Mtukufu Mtume (s.a.w.) au hata kuwadhuru waziwazi au kwa kisirisiri wala kuwatishia kwa jinsi yo yote ile au mahali po pote pale.

6. Maneno ya Matusi yaliyokuwa yakitumika hadi sasa katika Msikiti wa Jamia na katika Sala, kumtukana Hadhrat Ali (a.s.) lazima yaachwe.

Muawiya alisita kulikubali sharti hili la mwisho. Hivyo Imamu Hasan (a.s.) alilibadili kidogo na kuwa matusi hayo yasitolewe mbele ya Imamu Hasan (a.s.)

Mapatano haya yalifikiwa katika mwezi wa Rabi-ul-awwal (Mfunguo Sita) au Jumadal-Ula (Mfunguo Nane) katika mwaka wa 41 Hijiriya.

Baada ya mapatano:

Baada ya mapatano haya kufikiwa, majeshi yalirudi nyumbani. Ufalme wa Muawiya ukadumishwa na zaidi ya kuwa na Shamu tu, Muawiyah alipata Misri, Iraq, Hijaz, Yemen na Iran pia. Baada ya mapatano haya Imamu Hasan (a.s.) alikuwa akisikia maneno ya matusi kutoka vinywani mwa watu wale waliokuwa wakimwita, hadi jana yake tu, Amiri wa Wenye kuamini lakini sasa walikuwa wakimwita Mwenye kuifedhehesha dini. Lakini Mfalme wa Uvumili (a.s.) alinyamaza kimya.

Mara baada ya Muawiyah kujiona kuwa matatizo yake yamemalizika aliingia Iraq na kupiga kambi mahali paitwapo Nakhilah karibu na mji wa Kufah, na alisema katika hotuba yake ya Ijumaa, Kusudi langu la kupigana katika vita hii si kukuoneni mkisali, mkifunga, mkienda hija, au mkiyafuata mambo mengine ya dini; kwa sababu mlikuwa mkiyafanya yote hayo. Nilitaka tu, kuendeleza utawala wangu juu yenu, jambo ambalo nimefaulu kulipata baada ya mapatano haya ingawa ninyi hamkupenda. Na kuhusu masharti ya mapatano, ni nani basi anayeyajali? Ninaweza kuyajali au kutoyajali kufuatana na mapenzi yangu. Watu wote walinyamaza kimya, lakini hakuna aliyeweza kumpinga. Jambo la haya zaidi lilikuwa kwamba, mjini Kufa, mbele ya Maimamu Hasan (a.s.) na Husain (a.s.) Muawiyah alimtukana Hadhrat Ali (a.s.) na Imamu Hasan (a.s.). Imamu Husain (a.s.) aliposikia hivyo alisimama badala ya kakie ili kuzungumza. Lakini Imamu Hasan (a.s.) alimkalisha na akamjibu Muawiyah kwa kifupi sana lakini kwa maneno makali mno.

Hivyo Muawiyah alikataa kuyafuata masharti yote ya mapatano. Ingawa Imamu alikuwa akiishi katika hali ya kujitenga (peke yake) na kwa maisha ya usalama hakuachwa atulie. Watu wa ukoo wa Bani Ummayah walianza kumfanyia propaganda dhidi yake.

Basi ubaya wao wa mara kwa mara, matusi na masingizio yalipofikia kiwango ambacho kiasi chake kinaweza kuonekana kutokana na maneno aliyoyasema Imam Husain (a.s.) akimwambia Marwan, wanafiki walipokuwa wakilia katika maziko ya Imamu Hasan (a.s.), Leo mnalia. Lakini ni ninyi mliompa (Imamu Hasan (a.s.) mishtuko hii ambayo ni sisi tu tunaoweza kuitambua. Kisha Marwan akasema Ndio, hiyo ni kweli kabisa. Lakini hayo yote nimemtendea yule mtu aliyekuwa na uvumilivu mkubwa kuliko mlima huu

TABIA YAKE:

Tabia yake ilikuwa ni uvumilivu wa kimya kimya. Hii ilikubaliwa na marafiki na maadui zake kwa pamoja. Mfano wa tabia yake hiyo umetolewa hapo juu sasa hivi na maneno ambayo kwayo Marwan alikubali hivyo, yanaonyesha wazo lisilofutika ambalo tabia za Imamu Hasan(a.s.) zililijenga moyoni mwa adui huyo mkubwa kabisa.

Kila mara wafuasi wa serikali ya Shamu walikuwa na kawaida ya kutumia maneno mabaya kwa Imamu Hasan (a.s.) kwa nia ya kumkasirisha ili kumfanyia jambo fulani litakaloweza kuwasababisha kuyaachilia mbali yale masharti ya mapatano baina yake na Muawiyah. Lakini katika matukio yote hayo Imamu Hasan (a.s.) alionyesha uwezo wa kuwa na furaha na kuzizuia hasira zake, na uvumilivu ambao hauna kifani chake ila katika nyumba ya Mtukufu Mtume (s.a.w.) tu.

Ukarimu wake na upole wake, vilijulikana mahali pote Uarabuni. Mara tatu aligawanya pesa zake zote miongoni mwa maskini, na mara mbili alitoa nusu ya mali yake yote ikiwa ni pamoja na vyombo vya nyumbani na hata nguo zake.

Kufuatana na habari zilizoandikwa na baadhi ya wanahistoria ni kwamba, lilikuwepo sharti katika mapatano na Muawiyah kuwa kiasi fulani cha pesa kipelekwe na Muawiyah kila mwaka kwa Imamu Hasan (a.s.). Sababu ya kifungu hiki inaweza kuwa tu kwamba Imamu (a.s.) alitaka kuhakikisha kutolewa kwa japo sehemu ya pesa za serikali kupewa wenye kustahiki, kile wanachokistahiki.

Kila mara alikuwa akitoa pesa zote alizokuwa nazo, bila ya kujali ukubwa wa kima hicho. Siku moja aliulizwa kwa nini hakujisamehe hata kidogo katika kuzidi kuitikia maombi ya wale watu waliokuja kuomba pesa hata alipokuwa yeye mwenyewe yu mhitaji wa pesa? Imamu (a.s.) alijibu, Mimi mwenyewe nikiwa mwombaji mlangoni pa Mwenyezi Mungu, vipi nitaweza kuwakatalia wale wanaonijia? Kama nikiwakatalia basi vipi nitamtegemea Mwenyezi Mungu kunikidhia haja zangu?

Hivyo kila mtu ilimbidi akubali ubora wake wa kiasilia wa jamii ya Mtukufu Mtume (s.a.w.) katika elimu na ujuzi. Bwana mmoja aliyeitwa Abdallah ibn-i-Abbas aliyekuwa akijipatia jina na umaarufu kwa kutumia elimu aliyojipatia kutoka kwa Imamu Ali bin Abi Talib (a.s.) alikuwa kila mara akiinamisha kichwa chake kwa mwana wa Hadhrat Ali (a.s.). Siku moja mtu mmoja alikuja katika Msikiti wa Mtume (s.a.w.) ulioko mjini Madina) na kuomba aelezwe aya fulani ya Qurani Tukufu. Kwanza alimuomba Bwana Abdallah ibn-i-Abbas, kisha, Abdallah ibn-i-Umar, na mwishoni alimwuliza Imamu Hasan (a.s.). Kama ilivyotegemewa mtu huyo alikubali kuwa jibu la mwisho lilikuwa bora zaidi. Mara nyingi katika Mahakama ya Muawiyah, katika hali hiyo mbaya, (ya uadui kati ya Imamu (a.s.) na Muawiyah), Muawiyah alitoa hotuba za kuvutia sana akithibitisha ubora wa jamii ya Mtukufu Mtume (s.a.w.) na ile ya Hadhrat Ali (a.s.), na baba yake (Hadhrat Ali (a.s.), Bwana Abi Talib) ambao hata maadui waliutambua.

Imamu Hasan (a.s.) alikwenda Maka kuhiji kwa miguu karibuni mara 25. Kila alipofikiria kifo, kabri, siku ya Kiyama au Hesabu ya mwisho ya maisha ya mtu, alikuwa akitetemeka kwa kumuogopa Mwenyezi Mungu na alikuwa akilia na kuzirai. Kila aliposimama kusali alikuwa akitetemeka.

KIFO CHAKE:

Ingawa Imamu Hasan (a.s.) aliishi maisha ya amani, silaha ya Siri iliyokuwa ikitumiwa kila mara na wana wa Umayyah ilitumiwa dhidi yake. Muawiyah alimuuwa Imamu Hasan (a.s.) kwa sumu kupitia kwa mkewe (Imamu a.s.) aitwae Jadah bint wa Ashath kwa kumuahidi kuwa atampa dirhamu laki moja na ataolewa na mwanawe Yazid. Imamu Hasan (a.s.) alimwita nduguye Husain (a.s.) na kumtaka amzike karibu na kaburi la Mtukufu Mtume (s.a.w.) kama ikiwezekana. Lakini ama kukitokea upinzani basi asiruhusu kumwagika kwa damu, hivyo amzike katika Jannatul-Baqi. Mnamo tarehe 28 ya mwezi wa Safar (Mfunguo Tano) mwaka wa 50 wa Hijiriya, Imamu Hasan (a.s.) alifariki na Imamu Husain (a.s.) alichukua maiti yake kuelekea kwenye kaburi la Mtukufu Mtume (s.a.w.), lakini kile kilichofikiriwa kuwa kitatokea, kweli kilitokea.

Aisha (mkewe Mtume s.a.w.), Marwan na wengineo walipinga na mwishowe wale watu waliokuwa wameibeba maiti ya Imamu (a.s.) walitupiwa mishale hata baadhi ya mishale hiyo ikampiga maiti. Bani Hashim walichukizwa sana lakini mrithi wa Mfalme wa uvumilivu, nduguye Imamu Husain (a.s.) aliwatuliza na kuipeleka maiti hiyo Jannatul-Baqi na kumzika hapo.

MWISHO

YALIYOMO UKURASA

MFALME WA UVUMILIVU 1

(Imamu Hasan Al-Mujtaba A.S.) 1

MWENYEZI MUNGU ANASEMA: 2

MTUKUFU MTUME (S.A.W.W.) AMESEMA: 2

MTUKUFU MTUME (S.A.W.W.) AMESEMA: 2

SHUKRANI 2

UTANGULIZI 2

JINA LAKE: 3

KUZALIWA KWAKE: 3

KULELEWA KWAKE: 4

UKHALIFA WAKE: 5

MAPATANO: 6

TABIA YAKE: 9

KIFO CHAKE: 10

MWISHO 10