TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NANE Juzuu 8

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NANE0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NANE Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NANE

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 11505
Pakua: 1949


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 17 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 11505 / Pakua: 1949
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NANE

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NANE Juzuu 8

Mwandishi:
Swahili

14

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NANE

لَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا إِلَىٰ قَوْمِهِ فَقَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ إِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿٥٩﴾

59. Hakika tulimtuma Nuh kwa watu wake. Akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu, hamna Mungu mwingine zaidi yake. Hakika mimi ninawahofia na adhabu ya siku iliyo kuu.

قَالَ الْمَلَأُ مِن قَوْمِهِ إِنَّا لَنَرَاكَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٦٠﴾

60. Wakasema wakuu wa watu wake: Hakika sisi tunakuona umo katika upotofu ulio wazi.

قَالَ يَا قَوْمِ لَيْسَ بِي ضَلَالَةٌ وَلَـٰكِنِّي رَسُولٌ مِّن رَّبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٦١﴾

61. Akasema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika upotevu, lakini mimi ni Mtume nitokaye kwa Mola wa walimwengu wote.

أُبَلِّغُكُمْ رِسَالَاتِ رَبِّي وَأَنصَحُ لَكُمْ وَأَعْلَمُ مِنَ اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٦٢﴾

62. Nawafikishia ujumbe wa Mola wangu na nawanasihi; na ninajua kwa Mwenyezi Mungu msiyoyajua.

أَوَعَجِبْتُمْ أَن جَاءَكُمْ ذِكْرٌ مِّن رَّبِّكُمْ عَلَىٰ رَجُلٍ مِّنكُمْ لِيُنذِرَكُمْ وَلِتَتَّقُوا وَلَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٦٣﴾

63. Je, mnastaajabu kuwafikia mawaidha kutoka kwa Mola wenu kupitia mtu anayetokana na nyinyi ili awaonye na ili muwe na takua, na ili mpate kurehemiwa? ”

فَكَذَّبُوهُ فَأَنجَيْنَاهُ وَالَّذِينَ مَعَهُ فِي الْفُلْكِ وَأَغْرَقْنَا الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا إِنَّهُمْ كَانُوا قَوْمًا عَمِينَ ﴿٦٤﴾

64. Basi walimkadhibisha. Nasi tukamwokoa yeye na waliokuwa pamoja naye katika jahazi, na tukawazamisha waliozikadhibisha ishara zetu, Hakika wao walikuwa watu vipofu.

NUH

Aya 59 – 64

MAANA

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kusema, katika Aya 35 ya Sura hii:“Enyi Wanadamu! Watakapowafikia Mitume kutoka miongoni mwenu” Anaashiria, katika Aya hii na zinazofuatia, kisa cha Mitume Nuh, Hud, Swaleh, Nabii Lut, na Shuaib(a.s) .

Mwenyezi Mungu amekifupisha sana hapa kisa cha Nuh, ambapo ametosheka tu na kutaja majibizano kati yake na jamaa zake na namna walivyoepuka mwito na jinsi walivyostaajabu kuchagua Mwenyezi Mungu Mtume kutokana na wao.

Na kwamba yeye (s.w.t) aliwagharikisha wakadhibishaji na kuwaokoa waumini.

Hakika tulimtuma Nuh kwa watu wake.

Tabrasi anasema katika Majamaul-Bayan: “Yeye ni Nuh bin Mulk bin Matoshalkh bin Ukhnun, Mtume Idris. Na Nuh ni Mtume wa kwanza baada ya Idris.”

Inasemekana kuwa yeye alikuwa ni seremala na kwamba alizaliwa mwaka aliokufia Adam, Ama sisi, hatujui chimbuko la kusemekana huku.

Akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu, hamna Mungu mwingine zaidi yake. Hakika mimi ninawahofia na adhabu ya siku iliyo kuu.

Aliufupisha Nuh(a.s) ujumbe aliouchukua kwa watu wake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa jumla moja tu: Mwabuduni Mwenyezi Mungu peke yake kwa sababu hakuna Mola mwingine isipokuwa yeye. Na kwam- ba mwito wake huo kwao ni kuwahurumia na adhabu ya siku ya Kiyama.

Wakasema wakuu wa watu wake: Hakika sisi tunakuona umo katika upotofu ulio wazi.

Wakamshutumu kwa upotevu na usafihi si kwa jingine ila tu kwa vile amewakataza walioyazoea na kuyarithi ya kuabudu mawe.

Hivi ndiyo alivyo kila safihi na kila mpotevu, humzulia ule ugonjwa wake kila anayekwenda kwenye njia ya uongofu.

Akasema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika upotevu, lakini mimi ni Mtume nitokaye kwa Mola wa walimwengu wote. Nawafikishia ujumbe wa Mola wangu na ninawanasihi; na ninajua kwa Mwenyezi Mungu msiyoyajua.

Aliwajibu kwa kukanusha upotevu yeye mwenyewe na kujisifu kwa sifa tukufu kwamba yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, amempeleka ili awaokoe na upotevu na kuangamia, na kwamba yeye ni mtoaji nasaha mwaminifu, na anajua kutoka kwa Mwenyezi Mungu umoja na uadilifu wake. Na mwenye kuwa na sifa hizi hawezi kuwa mpotevu.

Je, mnastaajabu kuwafikia mawaidha kutoka kwa Mola wenu kupitia mtu anayetokana na nyinyi ili awaonye na ili muwe na takua na ili mpate kurehemiwa?

Watu wake walimwaambia wewe ni mtu tu kama sisi, Lau Mwenyezi Mungu angelitaka kutuma mjumbe angelimtuma Malaika. Akawajibu kwamba hakuna ajabu kutuma Mwenyezi Mungu mtu kwa watu wake akiwa hana masilahi yoyote au lengo lolote ila kuwaongoza kwenye lile lililo na kheri yao na utengenefu wao, isipokuwa ajabu ni kupuuzwa na kuachwa bila ya mwongozi.

Razi anasema huu ni utaratibu wa lengo zuri, kwani lengo la kutuma ujumbe ni kuonya, na lengo la kuonya ni takua, na lengo la takua ni kufuzu rehema ya Mwenyezi Mungu katika nyumba ya akhera.

Basi walimkadhibisha, Nasi tukamwokoa yeye na waliokuwa pamoja naye katika jahazi, na tukawazamisha waliozikadhibisha ishara zetu, Hakika wao walikuwa watu vipofu.

Milango ya mbinguni ilifunguka ikatoa maji na ardhi ikachimbuka chem-chemi. Hapo Mwenyezi Mungu akawaangamiza madhalimu wenye kukad- hibisha na akaokoka Nuh(a.s) na waumini aliokuwa pamoja nao. Yatakuja maelezo kwa ufafanuzi kuhusu Nuh(a.s) na watu wake katika Sura iliyoitwa kwa jina lake (71) inshaallah.

وَإِلَىٰ عَادٍ أَخَاهُمْ هُودًا قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ أَفَلَا تَتَّقُونَ ﴿٦٥﴾

65. Na kwa Adi (tulimpeleka) ndugu yao Hud. Akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu, nyinyi hamna Mungu mwingine zaidi yake, Basi hamwogopi?

قَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن قَوْمِهِ إِنَّا لَنَرَاكَ فِي سَفَاهَةٍ وَإِنَّا لَنَظُنُّكَ مِنَ الْكَاذِبِينَ ﴿٦٦﴾

66. Wakasema wakuu waliokufuru katika watu wake: Hakika sisi tunakuona umo katika upumbavu na tunakudhania ni katika waongo.

قَالَ يَا قَوْمِ لَيْسَ بِي سَفَاهَةٌ وَلَـٰكِنِّي رَسُولٌ مِّن رَّبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٦٧﴾

67. Akasema: Enyi watu wangu! Mimi sina upumbavu, lakini mimi ni Mtume nitokaye kwa Mola wa walimwengu.

أُبَلِّغُكُمْ رِسَالَاتِ رَبِّي وَأَنَا لَكُمْ نَاصِحٌ أَمِينٌ ﴿٦٨﴾

68. Nawafikishia ujumbe wa Mola wangu na mimi kwenu nimtoa nasaha, mwaminifu.

أَوَعَجِبْتُمْ أَن جَاءَكُمْ ذِكْرٌ مِّن رَّبِّكُمْ عَلَىٰ رَجُلٍ مِّنكُمْ لِيُنذِرَكُمْ وَاذْكُرُوا إِذْ جَعَلَكُمْ خُلَفَاءَ مِن بَعْدِ قَوْمِ نُوحٍ وَزَادَكُمْ فِي الْخَلْقِ بَسْطَةً فَاذْكُرُوا آلَاءَ اللَّـهِ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٦٩﴾

69. Je, mnastaajabu kuwafikia ukumbusho kutoka kwa Mola wenu kupitia mtu anayetokana na nyinyi ili awaonye. Na kumbukeni alivyowafanya makhalifa baada ya watu wa Nuh, Na akawazidisha nguvu katika umbo. Basi kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu ili mpate kufaulu.

قَالُوا أَجِئْتَنَا لِنَعْبُدَ اللَّـهَ وَحْدَهُ وَنَذَرَ مَا كَانَ يَعْبُدُ آبَاؤُنَا فَأْتِنَا بِمَا تَعِدُنَا إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ﴿٧٠﴾

70. Wakasema: Je, umetujia ili tumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake na tuyaache waliyokuwa wakiyaabudu baba zetu? Basi tuletee unayotuahidi ukiwa ni miongoni mwa wasemao kweli.

قَالَ قَدْ وَقَعَ عَلَيْكُم مِّن رَّبِّكُمْ رِجْسٌ وَغَضَبٌ أَتُجَادِلُونَنِي فِي أَسْمَاءٍ سَمَّيْتُمُوهَا أَنتُمْ وَآبَاؤُكُم مَّا نَزَّلَ اللَّـهُ بِهَا مِن سُلْطَانٍ فَانتَظِرُوا إِنِّي مَعَكُم مِّنَ الْمُنتَظِرِينَ ﴿٧١﴾

71. Akasema: Hakika adhabu na ghadhabu zimekwishawaangukia kutoka kwa Mola wenu. Je, mnanijadili katika majina mliyoyaita nyinyi na baba zenu ambayo Mwenyezi Mungu hakuyateremshia dalili yoyote? Basi ngojeni; mimi pia ni pamoja nanyi katika wangojao.

فَأَنجَيْنَاهُ وَالَّذِينَ مَعَهُ بِرَحْمَةٍ مِّنَّا وَقَطَعْنَا دَابِرَ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَمَا كَانُوا مُؤْمِنِينَ ﴿٧٢﴾

72. Basi tukamwokoa yeye na waliokuwa pamoja naye kwa rehema zetu na tukakata mizizi ya wale waliokadhibisha ishara zetu, na hawakuwa wenye kuamini.

HUD

Aya 65 – 72

MAANA

Imesemwa katika Tafsir Al-Manar kwa kunukuliwa kutoka kwa Is-haq bin Bashar na Ibn Asakir: “Nabii Hud(a.s) ndiye wa kwanza kuzungumza Kiarabu, alikuwa na watoto wane: Qahtan, Muq-hit, Qahit na Faligh ambaye ni baba wa Mudhar. (Abu Mudhar) Na Qahtan ni baba wa Yemen (Abul-Yaman), Ama Qahit na Muqhit hawana kizazi.”

Wafasiri wamesema: Watu wa Hud(a.s) walikuwa ni katika kizazi cha Nuh(a.s) na walikuwa kwenye dini yake. Baada ya muda kuwa mrefu, shetani aliwachezea, wakaabudu masanamu na wakafanya ufisadi katika ardhi.

Katika Tafsir Tabari imeelezwa kuwa Imam Ali alimwambia mtu mmoja kutoka Yemen: “Je, umeona katika ardhi ya Hadharamauti chungu ya tifu-tifu jekundu iliyochanganyika na madongo mekundu, ina mipilipili na mikunazi mingi sehemu kadha wa kadha?” Akasema: “Ndio Ewe Amirul Muminin, wallah unapasifu sifa ya mtu aliyepaona.” Akasema Amirul-Muminina: “Hapana, nimehadithiwa”. Yule mtu akasema: “Kwani pana nini Ewe Amirul-Muminin?” Akasema: “Pana kaburi ya Nabii Hud(a.s)

Ikiwa ni sahih Riwaya hii, basi itabidi iondolewe sehemu iliyoandikwa kwenye kaburi ya Imam Ali, isemayo: Amani ishuke juu yako na juu ya jirani zako Hud na Swaleh, ila ikiwa ujirani wenyewe ni katika akhera sio hapa duniani, au iwe mwili wa Hud ulihamishwa baada ya kufa Imam.

Aya hizi zilizoshuka kuhusu kisa cha Hud(a.s) zinaafikiana na Aya zilizotangulia, ambazo zimeshuka kuhusu kisa cha Nuh(a.s) kimaneno na kimaana isipokuwa katika mambo yafuatavyo:-

Nuh(a.s) aliwaambia watu wake: “Hakika mimi nawahofia na adhabu ya siku iliyo kuu”. Na Hud(a.s) akawaambia watu wake:Basi hamwogopi ? Hiyo ni kwa sababu kabla ya Nuh(a.s) hakukuwahi kutokea mfano wa adhabu hiyo, ambayo ni tufani. Na watu wa Hud(a.s) walikuwa wakijua, ndipo akawahadharisha na akawaamrisha kumwogopa Mwenyezi Mungu, kwa kuacha kumshirikisha na kumthibitishia umoja.

Nuh(a.s) aliambiwa na watu wake: ‘Hakika sisi tunakuona umo katika upotofu ulio dhahiri.’ Na watu wa Hud(a.s) walimwambia:

Hakika sisi tunakuona umo katika upumbavu, na hakika sisi tunakudhania ni katika waongo.

Kwa sababu Nuh(a.s) alikuwa akitengeneza safina mahali pasipo na bahari wala mito. Na kazi hii ukitazama kwa dhahiri ni ujinga na upotevu.

Ama Hud(a.s) hakufanya namna hii, isipokuwa aliwafanya wapumbavu watu wake kwa kuabudu masanamu. Kwa hiyo nao wakamrudishia na kumnasibishia upumbavu.

Nuh(a.s) aliwaambia watu wake: ‘Ili mpate kurehemiwa.’ Na Hud(a.s) aliwaambia watu wake:

Ili mpate kufaulu.

Nuh(a.s) alikusudia rehema, na kuondolewa adhabu na Hud(a.s) naye akakusudia kufaulu na kuongoka kwenye njia iliyo sawa, Maana zote mbili zinaungana, haziachani.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja katika Aya hizi mambo ambayo watu wa Hud(a.s) walimwambia mtume wao, lakini hakutaja kama watu wa Nuh(a.s) walimwambia Mtume wao nayo ni:

Wakasema: Je, Umetujia ili tumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake na tuyaache waliyokuwa wakiyaabudu baba zetu?

Ibara inayotumiwa na kila jahili na mwenye kufuata. Basi tuletee unayotuahidi ukiwa ni miongoni mwa wasemao kweli”

Likaja jawabu la mkato na la haraka kutoka kwa Mtume akasema: Hakika adhabu na ghadhabu zimekwishwaangukia kutoka kwa Mola Wenu. Maana ya kuwaangukia hapa ni kuwawajibikia, na makusudio ya adhabu ni sababu yenye kuwajibisha adhabu.

Je, Mnanijadili katika majina mliyoyaita nyinyi na baba zenu ambayo Mwenyezi Mungu hakuyateremshia dalili yoyote?

Waungu mnaowaabudu hawako, na kila kisichokuweko hakina athari wala dalili. Kwa hali hii majina waliyopewa yanakuwa ni maneno matupu yasiyokuwa na maana.

Basi ngojeni, mimi pia ni pamoja nanyi katika wangojao.

Hili ni jibu la kauli yao: “Basi tuletee unayotuahidi ukiwa miongoni mwa wasemao kweli.”

Basi tukamwokoa na waliokuwa pamoja naye kwa rehema zetu na tukakata mizizi ya wale waliokadhibisha ishara zetu, na hawakuwa wenye kuamini.

Kukatwa mizizi, ni kuangamizwa mpaka wa mwisho wao. Amebainisha Mwenyezi Mungu mahali pengine aina ya adhabu aliyowaangamizia watu wa Hud(a.s) , aliposema:

وَأَمَّا عَادٌ فَأُهْلِكُوا بِرِيحٍ صَرْصَرٍ عَاتِيَةٍ ﴿٦﴾ سَخَّرَهَا عَلَيْهِمْ سَبْعَ لَيَالٍ وَثَمَانِيَةَ أَيَّامٍ حُسُومًا فَتَرَى الْقَوْمَ فِيهَا صَرْعَىٰ كَأَنَّهُمْ أَعْجَازُ نَخْلٍ خَاوِيَةٍ ﴿٧﴾ فَهَلْ تَرَىٰ لَهُم مِّن بَاقِيَةٍ ﴿٨﴾

“Na ama Adi waliangamizwa kwa upepo mkali usiozuilika, Aliwapelekea masiku saba na siku nane mfululizo. Utawaona watu wameanguka kama kwamba ni magogo ya mitende yaliyo wazi, Basi je, unamwona mmoja wao aliyebaki?” (69: 6 – 8).

Inshallah yatakuja maelezo zaidi kuhusu Hud(a.s) na watu wake katika Sura (11) iliyoitwa kwa jina lake.

وَإِلَىٰ ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ قَدْ جَاءَتْكُم بَيِّنَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ هَـٰذِهِ نَاقَةُ اللَّـهِ لَكُمْ آيَةً فَذَرُوهَا تَأْكُلْ فِي أَرْضِ اللَّـهِ وَلَا تَمَسُّوهَا بِسُوءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٧٣﴾

73. Na kwa Thamud (tulimpeleka) ndugu yao Swaleh. Akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu, nyinyi hamna Mungu mwingine zaidi yake. Hakika umekwishawafikia ubainifu kutoka kwa Mola wenu. Huyu ni ngamia wa Mwenyezi Mungu aliye ishara kwenu, Basi mwacheni ale katika ardhi ya Mwenyezi Mungu, wala msimtie dhara, isije ikawashika adhabu ya Mwenyezi Mungu iumizayo.

وَاذْكُرُوا إِذْ جَعَلَكُمْ خُلَفَاءَ مِن بَعْدِ عَادٍ وَبَوَّأَكُمْ فِي الْأَرْضِ تَتَّخِذُونَ مِن سُهُولِهَا قُصُورًا وَتَنْحِتُونَ الْجِبَالَ بُيُوتًا فَاذْكُرُوا آلَاءَ اللَّـهِ وَلَا تَعْثَوْا فِي الْأَرْضِ مُفْسِدِينَ ﴿٧٤﴾

74. Na kumbukeni alipowafanya makhalifa baada ya Ad na kuwakalisha katika ardhi mkajenga makasri katika nyanda zake na mkachonga majumba katika majabali, Basi zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu, wala msifanye ufisadi katika ardhi.

قَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا مِن قَوْمِهِ لِلَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا لِمَنْ آمَنَ مِنْهُمْ أَتَعْلَمُونَ أَنَّ صَالِحًا مُّرْسَلٌ مِّن رَّبِّهِ قَالُوا إِنَّا بِمَا أُرْسِلَ بِهِ مُؤْمِنُونَ ﴿٧٥﴾

75. Wakasema wakuu wa watu wake waliotakabari kuwaambia walio wanyonge walioamini miongoni mwao: Je, mwajua kuwa Swaleh ametumwa na Mola wake? Wakasema: Hakika tunayaamini yale aliyotumwa.

قَالَ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا إِنَّا بِالَّذِي آمَنتُم بِهِ كَافِرُونَ ﴿٧٦﴾

76. Wakasema wale waliotakabari: Hakika Sisi tunayakataa yale mnayoyaamini.

فَعَقَرُوا النَّاقَةَ وَعَتَوْا عَنْ أَمْرِ رَبِّهِمْ وَقَالُوا يَا صَالِحُ ائْتِنَا بِمَا تَعِدُنَا إِن كُنتَ مِنَ الْمُرْسَلِينَ ﴿٧٧﴾

77. Wakamchinja ngamia na wakaasi amri ya Mola wao na Wakasema: Ee Swaleh! Tuletee unayotuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa Mitume.

فَأَخَذَتْهُمُ الرَّجْفَةُ فَأَصْبَحُوا فِي دَارِهِمْ جَاثِمِينَ ﴿٧٨﴾

Ukawanyakua mtetemeko wakawa wameanguka hawajimudu majumbani mwao.

فَتَوَلَّىٰ عَنْهُمْ وَقَالَ يَا قَوْمِ لَقَدْ أَبْلَغْتُكُمْ رِسَالَةَ رَبِّي وَنَصَحْتُ لَكُمْ وَلَـٰكِن لَّا تُحِبُّونَ النَّاصِحِينَ ﴿٧٩﴾

79. Basi Swaleh akawaacha na kusema: Enyi watu wangu! Kwa hakika nimewafikishia ujumbe wa Mola wangu na nikawanasihi, lakini hampendi wenye nasaha.

SWALEH

Aya Ya 73 – 79

MAANA

Na kwa Thamud (tulimpeleka) ndugu yao Swaleh. Akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu, nyinyi hamna Mungu mwingine zaidi yake.

Thamud ni kabila katika Waarabu. Waliitwa kwa jina la babu yao Thamud bin Amir. Makazi yao yalikuwa Hijr, baina ya Hijaz na Sham mpaka Wadil-qura. Mwenyezi Mungu anasema:

وَلَقَدْ كَذَّبَ أَصْحَابُ الْحِجْرِ الْمُرْسَلِينَ ﴿٨٠﴾

“Na hakika watu wa Hijr walikadhibisha Mitume (15:80).

Huyu ni ngamia wa Mwenyezi Mungu aliye ishara kwenu.

Kikundi cha Wafasiri wamesema kuwa watu wa Nabii Swaleh(a.s) walimwomba awatolee ngamia kutoka kwenye jiwe; na yeye alimwomba Mola wake hilo. Basi jiwe likashikwa na uchungu wa kuzaa kama mwanamke, likazaa ngamia wa kike mchangamfu mwenye manyoya.

Sisi tunaamini kiujumla kwamba ngamia alikuwa ni ubainifu na ishara kutoka kwa Mwenyezi Mungu; na kwamba hakuja kwa njia ya kawaida; na Mwenyezi Mungu alimtegemeza kwake kwa kumwadhimisha. Tunaamini hivi, bila ya kuongeza chochote ambacho hakikuelezwa na Wahyi au Hadith Mutawatir iliyotoka kwa Maasum.

Basi mwacheni ale katika ardhi ya Mwenyezi Mungu, wala msimtie dhara, isije ikawashika adhabu ya Mwenyezi Mungu iumizayo.

Swaleh(a.s) aliwaamrisha watu wake wamuache ngamia akae katika ardhi ya Mwenyezi Mungu, na akawahadharisha na mwisho mbaya ikiwa watamtaaradhi kwa udhia. Kisha akawaambia:

Na kumbukeni alipowafanya makhalifa baada ya Ad.

Mwenyezi Mungu aliangamiza kabila la Ad kwa dhambi zao, akawakumbusha neema hii ya kuwa makhalifa. Vilevile aliendelea kuwakumbusha kwa kuwaambia:

Na kuwakalisha katika ardhi mkajenga makasri kati- ka nyanda zake na mkachonga majumba katika majabali.

Kauli hii inafahamisha kuwa Thamud waliishi katika majengo yaliyoendelea na kwamba walikuwa katika neema na starehe.

Basi zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu, wala msifanye ufisadi katika ardhi.

Baada ya kuwakumbusha neema alizowamiminia Mwenyezi Mungu aliwaamrisha wakumbuke na washukuru neema hizo na kuwakataza wasifanye ufisadi. Hilo ni kuwahadharisha na uovu wa Mwenyezi Mungu na adhabu yake.

Wakasema wakuu wa watu wake waliotakabari kuwaambia wale walio wanyonge walioamini miongoni mwao.

Wale wapenda anasa katika watu wa Swaleh(a.s) waliendelea na utaghuti na kung’ang’ania kuabudu masanamu. Ama wale wanyonge kuna walioamini katika wao na waliobakia kwenye shirki kwa kuwafuata wapenda anasa. Basi hawa wakawaambia wale walioamini katika mafukara na wanyonge:

Je, mnajua kuwa Swaleh ametumwa na Mola wake?

Waliwauliza wanyonge swali hili kwa kupinga na kutishia au kwa dharau na stihzai.

Wakasema – wale wanyonge –Hakika tunayaamini yale aliyotumwa.

Waliyasema haya bila ya kujali vitisho na stizai. Kwa sababu wao wana yakini na dini yao.

Wakasema wale waliotakabari kuwaambia wale wanyonge: Sisi tunayakataa yale mliyoyaamini.

Pamoja na dalili na ubainifu mkataa juu ya utume wa Swaleh. Kwa sababu masilahi yao ni zaidi kuliko dini za Mwenyezi Mungu na dalili ya kiakili. Razi anasema Aya hii ni miongoni mwa hoja kubwa kuwa kiburi kinatokana na wingi wa mali na jaha. Kwa sababu wingi huo ndio uliowafanya waendele kuasi na kukufuru.

Wakamchinja ngamia na wakaasi amri ya Mola wao.

Hakika yao inadhihirisha uasi huu, na kwamba wao hawajali isipokuwa masilahi yao tu. Wakamchochea Nabii Swaleh(a.s) kuleta adhabu haraka na wakasema:

Ee Swaleh!: Tuletee unayotuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa Mitume.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakuwachelewesha kuwalipa inadi hiiUkawanyakua mtetemeko wakawa wameanguka hawajimudu majumbani mwao [3] .

Mwenyezi Mungu anasema katika Aya nyingine:

وَفِي ثَمُودَ إِذْ قِيلَ لَهُمْ تَمَتَّعُوا حَتَّىٰ حِينٍ ﴿٤٣﴾ فَعَتَوْا عَنْ أَمْرِ رَبِّهِمْ فَأَخَذَتْهُمُ الصَّاعِقَةُ وَهُمْ يَنظُرُونَ ﴿٤٤﴾

Na katika Thamud walipoambiwa jifurahisheni kwa muda mdogo tu. Wakaasi amri ya Mola wao ikawanyakua rindimo na huku wanaona.” (51:43-44)

Basi Swaleh akawaacha na akasema: Enyi watu! Kwa hakika nimewafikishia ujumbe wa Mola wangu na nikawanasihi, lakini hampendi wenye nasaha.

Nabii Swaleh(a.s) alipoona adhabu iliyowapata watu wake aliachana nao na akijiepusha na mwisho wao huu walioutaka wenyewe kwa uasi na jeuri.

Razi anasema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) : “Ewe Ali! Mwovu zaidi wa kwanza ni mchinja ngamia wa Swaleh, na mwovu zaidi wa mwisho ni muuaji wako”.

Tutarudia habari ya Nabii Swaleh(a.s) mara nyingine inshallah.

15

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NANE

وَلُوطًا إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ أَتَأْتُونَ الْفَاحِشَةَ مَا سَبَقَكُم بِهَا مِنْ أَحَدٍ مِّنَ الْعَالَمِينَ ﴿٨٠﴾

80. Na Lut alipowaambia watu wake: Je, mnafanya uchafu ambao hajawatangulia yeyote kwa hilo katika walimwengu.

إِنَّكُمْ لَتَأْتُونَ الرِّجَالَ شَهْوَةً مِّن دُونِ النِّسَاءِ بَلْ أَنتُمْ قَوْمٌ مُّسْرِفُونَ ﴿٨١﴾

81. Hakika nyinyi mnawaendea wanaume kwa matamanio badala ya wanawake! Bali nyinyi ni watu warukao mipaka.

وَمَا كَانَ جَوَابَ قَوْمِهِ إِلَّا أَن قَالُوا أَخْرِجُوهُم مِّن قَرْيَتِكُمْ إِنَّهُمْ أُنَاسٌ يَتَطَهَّرُونَ ﴿٨٢﴾

82. Na halikuwa jibu la watu wake isipokuwa kusema: Watoeni mjini mwenu, maana hao ni watu wanaojitakasa.

فَأَنجَيْنَاهُ وَأَهْلَهُ إِلَّا امْرَأَتَهُ كَانَتْ مِنَ الْغَابِرِينَ ﴿٨٣﴾

83. Tukamwokoa yeye na jamaa zake isipokuwa mkewe alikuwa miongoni mwa waliobakia.

وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهِم مَّطَرًا فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُجْرِمِينَ ﴿٨٤﴾

84. Na tukawamiminia mvua, basi tazama jinsi ulivyokuwa mwisho wa waovu.

LUT

Aya 80 – 84

MAANA

Na Lut alipowaambia watu wake: Je, mnafanya uchafu.

Amenukuu Mwenye Tafsir Al-Manar kutoka Kitabu Ansabul Arabiya ya kwamba Nabii Lut ni mwana wa ndugu wa Nabii Ibrahim Khalili(a.s) . Na kwamba yeye alizaliwa kaldayo (Chaldeans)

Hiyo ni sehemu iliyo upande wa Mashariki ya kati kusini mwa Iraq upande wa Magharibi katika jimbo la Basra, Sehemu hiyo wakati huo ikiitwa nchi ya Babel. Kisha Nabii Lut akasafiri na Nabii Ibrahim(a.s) ami yake hadi sehemu iliyo baina ya mito miwili, sehemu inayozungukwa na Dijla, mamlaka ya Ashwar, Kisha Nabii Ibrahim(a.s) akamweka mashariki mwa Jordan.

Ambao hajawatangulia yeyote kwa hilo katika walimwengu.

Inafahamisha kuwa watu wa Nabii Lut(a.s) ndio wa kwanza kuzusha aina hii ya ufisadi.

Hakika nyinyi mnawaendea wanaume kwa matamanio badala ya wanawake.

Hii ni tafsir ya uchafu; na makusudio yake ni ulawiti ambao kisasa unaitwa kinyume na maumbile au kitendo kibaya.

Bali nyinyi ni watu warukao mipaka.

Mmepetuka mpaka katika kila kitu, mpaka mmefikilia kiasi hiki cha upotofu ambao unakataliwa na maumbile na kuhalifu desturi ya maisha.

Na halikuwa jibu la kaumu yake isipokuwa kusema: Watoeni mjini mwenu,maana hao ni watu wanaojitakasa.

Ndio! Utakatifu na kujistahi ni dhambi kwa mzinzi mchafu; na uaminifu ni kosa kwa mhaini kibaraka. Watoeni, maana hao ni watakatifu. Hivi ndivyo jamii chafu hukataaa wasafi na wema, si kwa lolote ila kwamba wao ni wasafi. Usawa ni kinyume cha hivyo.

Tukamwokoa yeye na jamaa yake isipokuwa mkewe alikuwa miongoni mwa waliobaki.

Makusudio ya jamaa yake ni kila aliyeamini, ni sawa awe ni katika familia yake au la. Kubaki ni kwamba mke wa Nabii Lut alibakia pamoja na walioangamia, na hakufuatana naye wakati alipoondoka usiku kukimbia adhabu, kwa sababu alikuwa mnafiki akila njama pamoja na washirikina dhidi ya mumewe. Inasemekana kuwa jina lake ni Wahila.

Mwenyezi Mungu ametumia dhamir ya wanaume “waliokuwa nyuma” kwa vile waume walikuwa wengi zaidi.

Yalimpata mke wa Nabii Lut yale yaliyowapata washirikina kwa sababu yeye ni katika wao, wala haukumfaa uhusiano wake na Mtume wa Mwenyezi Mungu na kuwa naye. Kuna Hadith isemayo: “Mtu yu pamoja na kipenzi chake.”

Na tukawamiminia mvua.

Amebainisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) adhabu aliyowateremshia kuwa ni aina ya mvua, lakini ni ya mawe sio ya maji, kama ilivyoelezwa katika Aya isemayo:

وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهَا حِجَارَةً مِّن سِجِّيلٍ ٍ ﴿٨٢﴾

Tukawateremshia mvua ya changarawe za udongo mkavu. (11:82)

Utakuja ufafanuzi huko mbele inshallah.

Basi tazama jinsi ulivyokuwa mwisho wa waovu.

Ni adhabu iumizayo, na mwenye akili ni yule anayepata funzo kwa wengine.

Utauliza : manabii Nuh, Hud na Swaleh(a.s) kila mmoja aliwalingania watu wake kwenye ibada ya Mwenyezi Mungu peke yake; kama ilivyoelezwa katika Aya zilizotangulia.

Lakini Nabii Lut aliwalingania watu wake kujizuia na uchafu; kama inavyoelezwa katika Aya hizi. Je, hii inamaanisha kuwa watu wa Nabii Lut walikuwa ni watu wa Tawhid, lakini walikuwa waovu kwa kitendo chao hiki kibaya?

Jibu : watu wa Nabii Lut walikuwa makafiri, na aliwalingania kwa Mwenyezi Mungu mmoja, na kuwakataza na shirk na ukafiri, kama alivyowakataza ulawiti; kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ ﴿١٦٢﴾ فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُونِ ﴿١٦٣﴾

“Hakika mimi kwenu ni Mtume Mwaminifu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na nitiini”

(26: 162-163).

Isipokuwa alijishughulisha sana na uchafu huu, kwa vile ulikuwa umeenea sana kwao, na kuwafanya kuwa waasi wenye kuipinga haki na kuthubutu kuwakadhibisha Mitume wa Mwenyezi Mungu.

Yamekongamana madhehebu ya Kiislamu kwa kauli moja kuharamisha ulawiti, na kwamba ni katika madhambi makubwa, Wametofautiana katika adhabu yake.

Hanafi anasema ni kuaziriwa kwa aonavyo hakimu. Na madhehebu mengine yaliyobaki wamesema ni kuuliwa; kwa Hadith isemayo: “Mtakayempata anafanya vitendo vya watu wa Lut, basi muueni mfanyaji na mfanywa.”

Serikali ya Uingereza imehalalisha ulawiti na kupitishwa na bunge la Britania mnamo mwaka 1967. Gazeti la Al-Ahram la 6.9.1974 likinakili gazeti la Times la London linasema kwamba watu wakubwa wa Uingereza walifanya hafla kusherehekea kuhalalishwa huku kwa ulawiti.

Na wakajionyesha mbele ya mamia ya watazamaji, Hakuna mwenye shaka kwamba kuweko mabibi na wapenzi katika starehe hii kuliongeza shangwe na furaha!

وَإِلَىٰ مَدْيَنَ أَخَاهُمْ شُعَيْبًا قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ قَدْ جَاءَتْكُم بَيِّنَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ فَأَوْفُوا الْكَيْلَ وَالْمِيزَانَ وَلَا تَبْخَسُوا النَّاسَ أَشْيَاءَهُمْ وَلَا تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ بَعْدَ إِصْلَاحِهَا ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿٨٥﴾

Na kwa wa Madian (tulimpeleka) ndugu yao Shuaib akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu nyinyi hamna Mungu mwingine zaidi yake, Hakika umewajia ubainifu kutoka kwa Mola wenu. Basi kamilisheni kipimo na mizani wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye uharibifu katika ardhi baada ya kutengenea kwake, Hayo ndiyo bora kwenu ikiwa nyinyi mmeamini.

وَلَا تَقْعُدُوا بِكُلِّ صِرَاطٍ تُوعِدُونَ وَتَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ مَنْ آمَنَ بِهِ وَتَبْغُونَهَا عِوَجًا وَاذْكُرُوا إِذْ كُنتُمْ قَلِيلًا فَكَثَّرَكُمْ وَانظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُفْسِدِينَ ﴿٨٦﴾

Wala msikalie kila njia kumwogopesha na kumzuilia njia ya Mwenyezi Mungu mwenye kumuamini na kutaka kuipotosha. Na kumbukeni mlipokuwa wachache Akawafanya kuwa wengi, na tazameni jinsi ulivyokuwa mwisho wa wafisadi.

وَإِن كَانَ طَائِفَةٌ مِّنكُمْ آمَنُوا بِالَّذِي أُرْسِلْتُ بِهِ وَطَائِفَةٌ لَّمْ يُؤْمِنُوا فَاصْبِرُوا حَتَّىٰ يَحْكُمَ اللَّـهُ بَيْنَنَا وَهُوَ خَيْرُ الْحَاكِمِينَ ﴿٨٧﴾

Na kama liko kundi miongoni mwenu lililoamini yale niliyotumwa kwayo, na kundi (jingine) halikuamini, basi subirini mpaka Mwenyezi Mungu ahukumu baina yetu; naye ndiye mbora wa wenye kuhukumu.

SHUAIB

Aya 85 – 87

MAANA

Na kwa Wamadian (tulimpeleka) ndugu yao Shuaib. Akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu, hamna Mungu mwingine zaidi yake.

Umepita mfano wake katika Aya 59 ya Sura hii.

Nabii Shuaib ni miongoni mwa Mitume waarabu; kama vile nabii Hud(a.s) na Nabii Swaleh. Watu wa Madian ni waarabu walikuwa wakikaa katika ardhi ya Maa’n viungani mwa mji wa Sham.

Hakika umewafikia ubainifu kutoka kwa Mola wenu.

Ubainifu ni kila linalobainishiwa haki, ni sawa liwe ni dalili ya akili, au muujiza. Hakuna mwenye shaka kwamba Nabii Suhaib aliwaletea muujiza watu wake unaofahamisha utume wake; vinginevyo angelikuwa ni mtabiri sio Mtume, Hakuna nukuu ya Qur’an inayofahamisha aina ya muujiza huu. Kuuelezea ulivyokuwa, kama ilivyo katika baadhi ya Tafsir, ni kusema juu ya Mwenyezi Mungu bila ya ujuzi.

Basi kamilisheni kipimo na mizani wala msiwapunje watu vitu vyao.

hii inashiria kwamba wao walikuwa wanafanyiana vibaya katika biashara, na kwamba hilo lilikuwa limeenea kwao. Kwa hivyo aliwaamrisha kukamilisha kipimo cha ujazo na mizani baada ya kuwaamrisha kumpwekesha Mwenyezi Mungu (Tawhid). Kisha akawaamrisha uadilifu na kuacha kupunja katika haki zote za kimaada, kama vile elimu na maadili; wasimsifu mjinga kwa elimu wala kwa mhaini kwa uaminifu.

Wala msifanye ufisadi katika ardhi baada ya kutengenea kwake.

Imepita tafsir yake katika Aya 56 ya Sura hii kifungu ‘Mwenyezi Mungu aliitengeneza ardhi na mtu akaiharibu’

Hayo ndiyo bora kwenu ikiwa nyinyi mmeamini.

Hayo, ni ishara ya hayo matano yaliyotangulia: Kumwabudu Mwenyezi Mungu, kukamilisha vipimo na mizani, na kuacha kupunja na ufisadi.

Wala msikalie kila njia kumuogopesha na kumzuilia njia ya Mwenyezi Mungu mwenye kumwamini na kutaka kuipotosha.

Huu ni ubainifu na tafsir ya kauli yake Mwenyezi Mungu: Wala msifanye uharibufu katika ardhi. Kwa sababu maana yake ni: Msiwatie shaka na kuwatisha ikiwa wanataka kumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msimzuie Muumin kusimamisha nembo za dini, msije mkamzuia na njia ya Mwenyezi Mungu iliyo sawa na kujaribu kuwapeleka watu kufuata njia ya kombo mnayoifuata nyinyi.

Ufafanuzi zaidi na ufupi wa tafsir ya Aya hii ni yale yaliyopokewa kutoka kwa Ibn Abbas kwamba wao walikuwa wakikaa njiani kuwahofisha watu wasimwendee Nabii Shuaib(a.s) na kuwaambia kuwa yeye ni mwongo atawafitini na dini yenu.

Na kumbukeni mlipokuwa wachache akawafanya kuwa wengi.

Mwenyezi Mungu amewajalia kuwa matajiri baada ya kuwa mafukara, wenye nguvu baada ya kuwa wanyonge, na wengi baada ya kuwa wachache. Na tazameni jinsi ulivyokuwa mwisho wa waharibifu.

Yaani yasije yakawapata yaliyowapata waliofanya uharibifu katika nchi; mfano watu wa Nu, Hud, Swaleh na Lut(a.s) .

Na kama liko kundi miongoni mwenu lililoamini yale niliyotumwa kwayo na kundi (jingine) haliamini, basi subirini mpaka Mwenyezi Mungu ahukumu baina yetu.

Kundi moja lilimwamini Nabii Shuaib(a.s) na jingine likamkanusha. Akayataka makundi yote yaishi kwa amani na kila kundi liachane na jingine bila ya kumtaaradhi yeyote kwa kukumuudhi; ni sawa awe amechagua ukafiri au imani, kisha yote mawili yataongoja mpaka Mwenyezi Mungu awahukumu.

Naye ndiye mbora wa wenye kuhukumu.

Wala hakuna wa kupinga mantiki hii. Utampinga na nini anayekuambia: ‘Ngoja Mungu atakuhukumu?.

15

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein (a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA JUZUU YA NANE