TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA Juzuu 9

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 893
Pakua: 163

Maelezo zaidi:

Juzuu 9
Juzuu 1
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 15 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 893 / Pakua: 163
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA Juzuu 9

Mwandishi:
Swahili

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA

IMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA

IMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED

IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu

UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI

Kitabu hiki kilichoko mikononi mwako hivi sasa ni juhudi ya miaka mingi sana ya watu waliojitolea kuona kazi hii imefanikiwa bila ya kumsahau Marhum Abu Muhammad wa London.

Kama lilivyo jina la Tafsiri yenyewe ndivyo ilivyo Tafsiri yenyewe ambayo mwanachuoni huyu mahiri kabisa aliyeifafanua ni mtu aliyebobea katika fani zote ambazo mfasiri (Mfafanuzi) anatakiwa awe nazo. Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya ameonesha cheche zake katika vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbali mbalimbali na hivyo kujipatia wasomaji wengi sana.

Msomi huyu, mwenye fikra huru na anayetetea kile anachokiamini, ni mtu mwenye mawazo mapana na kuyaangalia mambo kwa undani sana, kipaumbele chake ni katika maslahi ya umma huu na amejaribu sana kwenda na wakati.

Sifa kubwa pekee ya mwanachuoni huyu ni kuwa yeye hakujihusisha sana na kung'ang'ania madhehebu fulani tu, labda hii yatokana na wadhifa wake wa ukadhi aliokuwa nao katika nchi ya Lebanon ambayo ina madhehebu mengi, ambapo sula la madhehebu ni nyeti nchini humo, hata hivyo yeye aliweza kuamua matatizo ya watu kwenye ofisi yake kulingana na madhehebu yao pale walipomwendea, hiyo ilimsaidia sana hata kuweza kutoa kitabu kitwacho 'Al-Fiqh a'laa madhaahabil-khamsah' (Fikhi ya madhehebu matano) yaani ya Hanafi, Maaliki, Shafi, Hambali na Shia (ambacho twataraji kitatoka hivi karibuni Inshaallah).

Jambo lililotupa msukumo wa kukifasiri kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ni zile faida nyingi atakazozipata msomaji na kujua mambo mengi na ya ajabu yaliyo mapya kwake ambayo si rahisi kuyapata kwa wafasiri wengine.

Msomaji atapata faida katika fani za Sayansi, Siasa, Historia, Mashairi, visa vizuri, na Saikolojia miongoni mwa mengine; ndiyo maana msomaji atashangaa kidogo anapoisoma Tafsiri hii atakapoona mwandishi amewataja na kuwanukuu watu kama kina Mfalme Edward, wanasyansi kama kina Enstein, Charlie Champlin (Mchekeshaji maarufu), na wengineo, hali inayoifanya tafsiri hii kuwa ni ya kipekee kabisa.

Mtindo alioutumia mwandishi ni sahali uliokusudiwa watu wa tabaka mbalimbali, wanavyuoni na watu wa kawaida.

Nia yetu ni kukigawanya kitabu hiki bure lakini tumelazimika kukiuza kwa bei nafuu ili kurudisha gharama za uchapishaji.

Mwisho: Shukrani kubwa iwaendee bila ya kuwataja watu waliojitolea usiku na mchana, jopo la wafasiri, wahariri, wachapaji, waliotupa moyo na kutoa maoni yao na walioisimamia ili kuhakikisha kwamba kitabu kimemfikia msomaji.

MAKOSA YA CHAPA

Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa, Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo. Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa.

Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswutu kwa swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146). Imeandikwa La Ya'alamuun, (hawajui) badala ya Ya'alamuun (wanajua), Mfano wa makosa haya hausameheki.

Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya Pili, sura (5:212), imeandikwa "Fawqahum ila yawmil qiyama” badala ya “Fawqahum yawamal qiyama",Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile.

Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu jabal amail 'Makosa ya chapa.'

Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: " Hatta idha balagha arbai' na sanah badala ya: Hattaidha balagha ashuddahu arbai ' na sanah"

Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko na kuufungia macho uzuri wa maana.

Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: "Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa, kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.

Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin(a.s) :"Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu."

Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mwenye jukumu la kunikubali- ayale niliyoyapatia na kunisamehe niliyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani (Amin).

MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH

1

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

Mwendelezo Wa Sura Ya Saba: Surat Al-A’raf

قَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا مِن قَوْمِهِ لَنُخْرِجَنَّكَ يَا شُعَيْبُ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَكَ مِن قَرْيَتِنَا أَوْ لَتَعُودُنَّ فِي مِلَّتِنَا قَالَ أَوَلَوْ كُنَّا كَارِهِينَ ﴿٨٨﴾

88. Wakuu waliotakabari katika kaumu yake wakasema: Ewe Shuaib! Tutakutoa wewe na wale walioamini pamoja nawe katika mji wetu au mrejee katika mila yetu. Akasema: Je, ingawa tunaichukia?

قَدِ افْتَرَيْنَا عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا إِنْ عُدْنَا فِي مِلَّتِكُم بَعْدَ إِذْ نَجَّانَا اللَّـهُ مِنْهَا وَمَا يَكُونُ لَنَا أَن نَّعُودَ فِيهَا إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ رَبُّنَا وَسِعَ رَبُّنَا كُلَّ شَيْءٍ عِلْمًا عَلَى اللَّـهِ تَوَكَّلْنَا رَبَّنَا افْتَحْ بَيْنَنَا وَبَيْنَ قَوْمِنَا بِالْحَقِّ وَأَنتَ خَيْرُ الْفَاتِحِينَ ﴿٨٩﴾

89. Hakika tutakuwa tumemzulia Mwenyezi Mungu uwongo ikiwa tutarudi katika mila yenu baada ya kwisha kutuokoa nayo Mwenyezi Mungu, Wala haiwi kwetu kuirudia mpaka akipenda Mwenyezi Mola wetu. Ujuzi wa Mola wetu umeenea katika kila kitu, Kwa Mwenyezi Mungu tunategemea. Mola wetu! Hukumu baina yetu na baina ya kaumu yetu kwa haki, nawe ndiwe bora wa wenye kuhukumu.

TUTAKUTOA EWE SHUAIB

Aya 88 – 89

MAANA

Wakuu waliotakabari katika kaumu yake wakasema: Ewe Shuaib! Tutakutoa wewe na wale walioamini pamoja nawe katika mji wetu au mrejee katika mila yetu.

Tumetangulia kueleza katika Juz.8, kwamba Shuaib aliwataka makafiri kuishi kwa amani na wale walioamini na kumwachia hiyari anayetaka kuingia dini anayotaka. Lakini makafiri wakakataa mwito wake na wakamuhiyarisha mambo mawili tu: Ama atoke yeye na wale walioamini mjini mwao, au wale walioamini warudie ukafiri, na yeye arudie msimamo wake wa kwanza, kabla ya utume, asiwe wa kuunga mkono dini yao wala kuipinga. Kwa maneno mengine ni kuwa hali irudie kama ilivyokuwa kabla ya Utume.

Akasema: Je, ingawa tunaichukia?

Hiyo ndiyo mantiki ya mwenye kuchunga haki mwenye ikhlasi, hamchukii yeyote kwa analolichukia, wala hataki yeyote amchukue kwenye lile asilolitaka. Kisha je, inawezekana imani kwa kulazimishwa? Je, Mu’min wa kweli dini yake na itikadi yake inaathirika kwa kukaa katika mji?

Hakika tutakuwa tumemzulia Mwenyezi Mungu uwongo ikiwa tutarudi katika mila yenu baada ya kwisha kutuokoa nayo Mwenyezi Mungu.

Washirikina walimtaka Shuaib(a.s) artadi awe kwenye shirk. Akawaambia, kurtadi ni kumzulia Mwenyezi Mungu uwongo; na mwisho wa kumzulia Mwenyezi Mungu ni balaa na adhabu; na Mwenyezi Mungu amekwisha tuokoa nayo, sasa vipi tumzulie? Ama kuwa murtadi ni kumzulia Mwenyezi Mungu uwongo ni wazi, kwa sababu maana yake ni kuwa kumshirikisha Mwenyezi Mungu ni bora kwake kuliko kumwamini.

Wala haiwi kwetu kuirudia mpaka akipenda Mwenyezi Mola wetu.

Dhamir ya ‘kuirudia’ ni ya mila ya ukafiri na shirk. Sharti la kupenda kwa Mwenyezi Mungu hapa ni sharti la muhali (lisilowezekana). Kwa sababu Mwenyezi Mungu hapendi shirki na ukafiri, ni sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu katika Aya ya 40 ya Sura hii:“Wala hawataingia peponi mpaka ngamia apite kwenye tundu ya sindano.”

Ujuzi wa Mola wetu umeenea katika kila kitu.

Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz 7 (6:80).

Kwa Mwenyezi Mungu tunategemea.

Na mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu haogopi vitisho wala makamiano; Kwa sababu anajua kwa yakini kwamba kiumbe hadhuru wala kunufaisha.

Mola wetu! Hukumu baina yetu na baina ya kaumu yetu kwa haki, nawe ndiye bora wa wenye kuhukumu.

Baada ya Shuaib kukata tamaa nao na kuona kung’ang’ania kwao ukafiri, alikimbia kwa Mwenyezi Mungu na akanyenyekea kwake ahukumu baina yake na waliokufuru katika watu wake. Kwa sababu Yeye Mwenyezi Mungu ndio rejea ya nguvu na uadilifu.

وَقَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن قَوْمِهِ لَئِنِ اتَّبَعْتُمْ شُعَيْبًا إِنَّكُمْ إِذًا لَّخَاسِرُونَ ﴿٩٠﴾

90. Na wakuu waliokufuru katika kaumu yake wakasema: Kama nyinyi mkimfuata Shuaib, hapo hakika mtakuwa wenye hasara.

فَأَخَذَتْهُمُ الرَّجْفَةُ فَأَصْبَحُوا فِي دَارِهِمْ جَاثِمِينَ ﴿٩١﴾

91. Ukawanyakua mtetemeko wakaamkia majumbani mwao wamejifudikiza.

الَّذِينَ كَذَّبُوا شُعَيْبًا كَأَن لَّمْ يَغْنَوْا فِيهَا الَّذِينَ كَذَّبُوا شُعَيْبًا كَانُوا هُمُ الْخَاسِرِينَ ﴿٩٢﴾

92. Wale waliomkadhibisha Shuaib wakawa kama kwamba hawakuwako. Wale waliomkadhibisha Shuaib ndiyo wenye hasara.

فَتَوَلَّىٰ عَنْهُمْ وَقَالَ يَا قَوْمِ لَقَدْ أَبْلَغْتُكُمْ رِسَالَاتِ رَبِّي وَنَصَحْتُ لَكُمْ فَكَيْفَ آسَىٰ عَلَىٰ قَوْمٍ كَافِرِينَ ﴿٩٣﴾

93. Basi (Shuaib) akaachana nao na akasema: Enyi watu wangu! Kwa hakika nimewafikishia ujumbe wa Mola wangu na nikawanasihi, basi vipi nihuzunike juu ya watu makafiri.

MKIMFUATA SHUAIB

Aya 90 – 93

MAANA

Na wakuu waliokufuru katika kaumu yake wakasema: Kama nyinyi mkimfuata Shuaib, hapo hakika mtakuwa wenye hasara.

Washirikina kwanza walimkabili Shuaib, mwenye mwito, walimtisha na kumkamia. Walipokata tamaa naye waliwageukia wale waliomuamini wakijaribu kuwafitini na dini yao, wakasema miongoni mwa waliyoyasema: “Nyinyi mtakuwa wenye hasara mkifuata Shuaib.” Hii ndiyo desturi ya asiye na hoja ila kupoteza tu.

Ukawanyakua mtetemeko wakaamkia majumbani mwao wamejifudikiza.

Hili ndilo jibu sahihi kwa mpinzani na akakataa ila upotevu. Imetangulia Aya hii kwa herufi. Aya ya 78, ya Sura hii.

Wale waliomkadhibisha Shuaib wakawa kama kwamba hawakuwako.

Iliwajia adhabu kwao na kwenye majumba yao na athari zao zote, kama kwamba maisha haya hawakuyajua nayo yamewajua, Kila mtu atalipwa alilofanya sasa au baadaye.

Wale waliomkadhibisha Shuaib ndiyo wenye hasara.

Washirikina waliwaambia wale walioamini: nyinyi mtakuwa kwenye hasara, lakini wao mwisho ndio waliokuwa wenye hasara na maangamizi na waumini wakafaidika na kuokoka.

Mwenye akili hawezi kumwambia mwenye kiburi ‘Pongezi’ na kumwambia mnyonge ‘Ole wako’ kwa sababu zama zinaficha na kuleta mambo ghafla. Na mambo huzingatiwa kwa mwisho wake.

Imekaririka jumla “wale waliomkadhibisha Shuaib” kwa kutilia mkazo hasara yao na maangamizi yao.

Basi (Shuaib) akaachana nao na akasema: Enyi watu wangu! Kwa hakika nimewafikishia ujumbe wa Mola wangu na nikawanasihi, basi vipi nihuzunike juu ya watu makafiri.

Vipi nihuzunike na yule aliyejiangamiza mwenyewe kwa kung’ang’ania kumkufuru Mwenyezi Mungu, vitabu vyake na Mitume yake; na kumfanyia stizai aliyemwamini na kufuata njia yake ya sawa. Umetangulia mfano wake katika Aya 79 katika Sura hii.

وَمَا أَرْسَلْنَا فِي قَرْيَةٍ مِّن نَّبِيٍّ إِلَّا أَخَذْنَا أَهْلَهَا بِالْبَأْسَاءِ وَالضَّرَّاءِ لَعَلَّهُمْ يَضَّرَّعُونَ ﴿٩٤﴾

94. Na hatukumtuma Nabii yeyote katika mji wowote isipokuwa huwapatiliza watu wake kwa tabu na mashaka ili wapate kunyenyekea.

ثُمَّ بَدَّلْنَا مَكَانَ السَّيِّئَةِ الْحَسَنَةَ حَتَّىٰ عَفَوا وَّقَالُوا قَدْ مَسَّ آبَاءَنَا الضَّرَّاءُ وَالسَّرَّاءُ فَأَخَذْنَاهُم بَغْتَةً وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٩٥﴾

95. Kisha tukabadilisha mahali pa ubaya kwa wema, hata wakazidi na wakasema: Tabu na raha ziliwafikia baba zetu. Basi tuliwaadhibu kwa ghafla hali hawatambui.

HATUKUMLETA NABII YOYOTE KATIKA MJI

Aya 94 – 95

MAANA

Na hatukumtuma Nabii yeyote katika mji wowote isipokuwa huwap- atiliza watu wake kwa tabu na mashaka ili wapate kunyenyekea.

Makusudio ya mji ni ule ambao aghlabu hukaliwa na viongozi.

Katika Aya zilizotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) maangamivu yaliyowafikia wakadhibishaji katika watu wa Nuh, Hud, Swaleh, Lut, na Shuaib na mwisho wao ulio na mazingatio na mawaidha; na kwamba kheri ndio mwisho wa wenye kumcha Mwenyezi Mungu, na uovu uliwarudia wabatilifu.

Katika Aya hii anabainisha kuwa yaliyowapitia watu wa Mitume hiyo hayahusiki na wao tu peke yao, lakini ni desturi ya Mwenyezi Mungu, inawapitia kila watu wanaomkadhibisha Mtume wao. Anawaadhibu Mwenyezi Mungu kwa shida na mashaka katika nafsi zao, miili yao na mali zao. Si kwa lolote ila ni kwa ajili wawaidhike na wazingatie wao na watakaokuja baada yao.

Kisha tukabadilisha mahali pa ubaya kwa wema, hata wakazidi na wakasema: Tabu na raha ziliwafikia baba zetu.

Makusudio ya ubaya hapa ni dhiki na uzito na wema ni wasaa na wepesi. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwajaribu kwa dhiki na shida ili wawaidhike na kwa wasaa na afya ili washukuru lakini ni wachache wanao waidhika na ni wachache zaidi wanaoshukuru.

Neema ilipowazidi na kizazi kuwa kingi, waliidharau haki na kuwafanyia stihizai watu wake; wakawa wanafasiri desturi ya Mwenyezi Mungu kwa ujinga wao na hawaa zao, wakisema: taabu waliyoipata baba zetu haikuwa ni mateso kutokana upotevu na uharibifu wao; wala raha waliyoipata haikuwa na malipo ya wema wao na uongofu wao, isipokuwa ni sadfa tu iliyokuja shaghala-baghala.

Ikiwa hawa wanaghafilika na kuhukumiwa na Mwenyezi Mungu na hekima yake, basi Mwenyezi Mungu mtukufu hakughalifika nao na vitendo vyao.

Basi tuliwaadhibu kwa ghafla hali hawatambui.

Yakiwa ni malipo ya kughurika kwao na kuwa huru na hawa na malengo yao. Namna hii Qur’an inawahadharisha wale ambao hawachungi haki na kutojali chochote wasiadhibiwe ghafla hali hawatambui.

وَلَوْ أَنَّ أَهْلَ الْقُرَىٰ آمَنُوا وَاتَّقَوْا لَفَتَحْنَا عَلَيْهِم بَرَكَاتٍ مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ وَلَـٰكِن كَذَّبُوا فَأَخَذْنَاهُم بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٩٦﴾

96. Na lau kama watu wa mji wangeliamini na kuogopa, kwa hakika tungewafungulia baraka za mbingu na ardhi. Lakini walikadhibisha, kwa hiyo tukawapatiliza kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.

أَفَأَمِنَ أَهْلُ الْقُرَىٰ أَن يَأْتِيَهُم بَأْسُنَا بَيَاتًا وَهُمْ نَائِمُونَ ﴿٩٧﴾

97. Je, watu wa miji wameaminisha ya kuwa adhabu yetu haitawafikia usiku, hali wamelala?

أَوَأَمِنَ أَهْلُ الْقُرَىٰ أَن يَأْتِيَهُم بَأْسُنَا ضُحًى وَهُمْ يَلْعَبُونَ ﴿٩٨﴾

98. Au watu wa miji wameaminisha kuwa adhabu yetu haitawafikia mchana, hali wanacheza?

أَفَأَمِنُوا مَكْرَ اللَّـهِ فَلَا يَأْمَنُ مَكْرَ اللَّـهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْخَاسِرُونَ ﴿٩٩﴾

99. Je, wamejiaminisha na hila ya Mwenyezi Mungu? Hawaaminishi hila ya Mwenyezi Mungu ila watu wenye hasara.

أَوَلَمْ يَهْدِ لِلَّذِينَ يَرِثُونَ الْأَرْضَ مِن بَعْدِ أَهْلِهَا أَن لَّوْ نَشَاءُ أَصَبْنَاهُم بِذُنُوبِهِمْ وَنَطْبَعُ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ فَهُمْ لَا يَسْمَعُونَ ﴿١٠٠﴾

100. Je, hawaongoki ambao wamerithi ardhi baada ya wenyeji wake kwamba tukitaka tutawasibu kwa dhambi zao?

NA LAU KAMA WATU WA MJI

Aya 96 – 100

MAANA

Na lau kama watu wa mji wangeliamini na kuogopa, kwa hakika tungewafungulia baraka za mbingu na ardhi.

Baraka ya mbingu iliyodhahiri zaidi ni mvua na baraka ya ardhi, iliyo dhahiri zaidi, ni mimea mifugo na aina kadhaa za madini.

Tumebainisha katika kufasiri Juz, 7, (5:100) kifungu: ‘Je riziki ni sadfa au majaaliwa, kwamba kumwamini Mwenyezi Mungu peke yake hakuwezi kuotesha ngano.

Vilevile tumebainisha katika kufasiri Juz.6 (5:66) kifungu ‘Riziki na ufisadi’ kwamba makusudio ya imani yenye kuwajibisha riziki ni kumwamini Mwenyezi Mungu pamoja na kufanya amali kwa hukumu zote za Mwenyezi Mungu na misingi yake. Vilevile kufanya uadilifu katika kila kitu, na kwamba utakapoenea uadilifu na kutawala, basi hali itakuwa nzuri, na kutoweka ubaya na uovu.

Lakini walikadhibisha, kwa hiyo tukawapatiliza kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.

Yaani hawakujua hukumu za Mwenyezi Mungu, bali walihangaika katika ardhi kueneza ufisadi, dhulma, unyang’anyi na kulimbikizaa mali ya jasho la wanyonge. Mwenyezi Mungu amewapatiliza kwa maangamizi. Kwa sababu wao wamekufuru na kujilimbikiza vyote.

Je, watu wa miji wameaminisha ya kuwa adhabu yetu haitawafikia usiku, hali wamelala?

Huu ni uhofisho na tahadhari kutoka kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa waasi na wenye kujilimbikizia mali kuwa Mwenyezi Mungu atawashtukizia na adhabu yake wakiwa wameghafilika; kama alivyofanya kwa waliokuwa kabla yao.

Je, mtu ataweza kuizuia hukumu ya Mwenyezi Mungu? Vipi ataweza naye atakuwa kama aliyekufa?

Au watu wa miji wameaminisha kuwa adhabu yetu haitawafikia mchana, hali wanacheza?

Wanacheza, hapa ni fumbo la kughafilika kwao na mshtukizo na kujisahau.

Utauliza : hakuna tofauti kabisa baina ya kuwa macho mtu na kughafilika kwake mbele ya adhabu ya Mwenyezi Mungu. Sasa je, kuna makusudio gani ya kutaja usingizi na mchezo?

Jibu : Ni kuwa binadamu atambue udhaifu wake, ili awaidhike au aogope.

Je, wamejiaminisha na hila ya Mwenyezi Mungu? Hawaaminishi hila ya Mwenyezi Mungu ila watu wenye hasara.

Makusudio ya hila ya Mwenyezi Mungu hapa ni adhabu ambayo inawajia ghafla bila ya kutangulia hadhari yoyote.

Yametangulia maelezo kuhusu hila ya Mwenyezi Mungu katika kufasiri Juz.3 (3:54); kwamba yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t) anajisifu kuwa ni mwenye hila, kwa vile yeye anapangua hila za wenye hila; na anajisifu kuwa ni mwingi wa shukrani kwa vile anawapa thawabu wenye kushukuru.

Ama kuwa wao ni wenye hasara ni kwamba wao wamejingiza katika hasara kwa sababu ya inadi yao na kutojali kwao.

Je, hawaongoki ambao wamerithi ardhi baada ya wenyeji wake kwamba tukitaka tutawasibu kwa dhambi zao?

Yaani hawa washirikina waliorithi ardhi ya wale tuliyowaangamiza kwa dhambi zao, nao walikuwa na nguvu kuliko wao hawabainishi kwamba hali yetu kwao ni sawa na hali yetu kwa waliokuwa kabla yao? Lau tunataka itawapata adhabu yetu, kama ilivyowapata wengineo kabla yao? Hakika desturi ya Mwenyezi Mungu ni moja kwa viumbe vyake vyote.

Lengo la kuendelea sana huku katika nasaha na tahadhari ni kuwa mtu ajichunge wala asighafilike, na awaidhike na mwengine wala asidan- ganyike na mambo ya dhahiri yasiyo na chochote, “Watu wasioamini, haziwafai kitu ishara na maonyo” (10:101).

Na tutapiga muhuri juu ya nyoyo zao, kwa hiyo hawasikii.

Yametangulia maelezo yake katika Juz.1 (2:53).