TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA Juzuu 9

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 10616
Pakua: 1286

Maelezo zaidi:

Juzuu 9
Juzuu 1
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 15 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 10616 / Pakua: 1286
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA Juzuu 9

Mwandishi:
Swahili

2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

تِلْكَ الْقُرَىٰ نَقُصُّ عَلَيْكَ مِنْ أَنبَائِهَا وَلَقَدْ جَاءَتْهُمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَمَا كَانُوا لِيُؤْمِنُوا بِمَا كَذَّبُوا مِن قَبْلُ كَذَٰلِكَ يَطْبَعُ اللَّـهُ عَلَىٰ قُلُوبِ الْكَافِرِينَ ﴿١٠١﴾

101. Miji Hiyo tunakusimulia baadhi ya habari zake, Hakika waliwajia Mitume wao kwa ishara zilizo wazi-wazi, lakini hawakuwa wenye kuamini waliyoyakadhibisha zamani, Namna hii Mwenyezi Mungu anazipiga muhuri nyoyo za makafiri.

وَمَا وَجَدْنَا لِأَكْثَرِهِم مِّنْ عَهْدٍ وَإِن وَجَدْنَا أَكْثَرَهُمْ لَفَاسِقِينَ ﴿١٠٢﴾

102. Na hatukuona kwa wengi wao ahadi yoyote. Na hakika tuliwakuta wengi wao ni mafasiki.

MIJI HIYO TUNAKUSIMULIA

Aya 101 – 102

MAANA

Miji hiyo tunakusimulia baadhi ya habari zake.

Miji hiyo ni ishara ya watu wa miji hiyo ambao ni aina tano: Watu wa Nuh, wa Hud, wa Swaleh, wa Lut na wa Shuaib.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, Nabii Muhammad(s.a.w.w) wakikusudiwa waislamu kupewa habari ya hali za waliopita, ili wazingatie na watahadhari.

Hakika waliwajia Mitume wao kwa ishara zilizo waziwazi, lakini hawakuwa wenye kuamini waliyoyakadhibisha zamani.

Ametaja Razi njia tatu za kutafsiri kipande hiki cha Aya, na Tabrasi naye akazidisha ya nne. Hakuna hata moja waliyoitilia nguvu, na wakamwacha msomaji wa kawaida kwenye mataa; ambapo maana yako wazi yasiyokuwa na undani wowote.

Kwa ufupi ni kuwa watu wa miji hiyo kabla ya kupelekewa Mitume wa Mwenyezi Mungu, walikuwa kwenye shirki na upotevu; na kwamba wao waliendelea katika shirki yao na upotevu baada ya kuwafikia Mitume kwa dalili na miujiza. Na hawakuathirika na chochote, wakawa kama ambao hawakupelekewa mjumbe anayetoa bishara na maonyo. Haya yanafahamishwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

Namna hii Mwenyezi Mungu anazipiga muhuri nyoyo za makafiri.

Muhuri hapa ni fumbo la kususuwaa kwa nyoyo zao na kwamba hazijali kupotea kwake wala haitarajiwi kheri yake.

Na hatukuona kwa wengi wao ahadi yoyote.

Hawaamini dini ya Mwenyezi Mungu wala hawalazimiani na chochote kinachohusiana na ubinadamu. Hata hivyo wanayo ahadi moja tu wanayolazimiana nayo wala hawapingani nayo, nayo ni kufuata masilahi na hawaa.

Na hakika tuliwakuta wengi wao ni mafasiki.

Yaani wamepotea kufuata njia.

ثُمَّ بَعَثْنَا مِن بَعْدِهِم مُّوسَىٰ بِآيَاتِنَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِ فَظَلَمُوا بِهَا فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُفْسِدِينَ ﴿١٠٣﴾

103. Kisha baada yao tukamtuma Musa na ishara zetu kwa Firauni na wakuu wake lakini wakazikanusha. Basi tazama jinsi ulivyokuwa mwisho wa wafisadi.

وَقَالَ مُوسَىٰ يَا فِرْعَوْنُ إِنِّي رَسُولٌ مِّن رَّبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٠٤﴾

104. Akasema Musa: Ewe Firauni! Hakika mimi ni Mtume nitokaye kwa Mola wa walimwengu.

حَقِيقٌ عَلَىٰ أَن لَّا أَقُولَ عَلَى اللَّـهِ إِلَّا الْحَقَّ قَدْ جِئْتُكُم بِبَيِّنَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ فَأَرْسِلْ مَعِيَ بَنِي إِسْرَائِيلَ ﴿١٠٥﴾

105. Yanipasa nisiseme juu ya Mwenyezi Mungu isipokuwa haki. Nimewajia na dalili wazi itokayo kwa Mola wenu. Basi waache wana wa Israel waende nami.

قَالَ إِن كُنتَ جِئْتَ بِآيَةٍ فَأْتِ بِهَا إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ ﴿١٠٦﴾

106. Akasema: Ikiwa umekuja na ishara, basi ilete ukiwa ni miongoni mwa wasemao kweli.

فَأَلْقَىٰ عَصَاهُ فَإِذَا هِيَ ثُعْبَانٌ مُّبِينٌ ﴿١٠٧﴾

107. Akaitupa fimbo mara ikawa nyoka dhahiri.

وَنَزَعَ يَدَهُ فَإِذَا هِيَ بَيْضَاءُ لِلنَّاظِرِينَ ﴿١٠٨﴾

108. Na akautoa mkono wake. Mara ukawa mweupe kwa watazamao.

قَالَ الْمَلَأُ مِن قَوْمِ فِرْعَوْنَ إِنَّ هَـٰذَا لَسَاحِرٌ عَلِيمٌ ﴿١٠٩﴾

109. Wakasema wakuu wa watu wa Firauni: Hakika huyu ni mchawi mjuzi.

يُرِيدُ أَن يُخْرِجَكُم مِّنْ أَرْضِكُمْ فَمَاذَا تَأْمُرُونَ ﴿١١٠﴾

110. Anataka kuwatoa katika ardhi yenu. Basi mnatoa shauri gani?

قَالُوا أَرْجِهْ وَأَخَاهُ وَأَرْسِلْ فِي الْمَدَائِنِ حَاشِرِينَ ﴿١١١﴾

111. Wakasema: Mwache kidogo yeye na ndugu yake, na uwatume wakusanyao watu mijini.

يَأْتُوكَ بِكُلِّ سَاحِرٍ عَلِيمٍ ﴿١١٢﴾

112. Wakuletee kila mchawi, mjuzi.

MUSA NA FIRAUNI

Aya 103 – 112

MUHTASARI WA KISA

Tumepitia Aya kadhaa zinazoeleza kisa cha Nabii Musa(a.s) na wa Israel. Sasa tunaeleza kisa cha Nabii Musa(a.s) na Firauni katika Aya hizi tunazofasiri.

Neno ‘Firauni’ ni msimbo wa wafalme wa Misri wa zamani; kama vile msimbo wa Kaizari kwa wafalme wa Roma, Kisra kwa wafalme wa Fursi (Iran ya sasa) na Najashi kwa wafalme wa Uhabeshi (Ethiopia ya sasa).

Imenukuliwa kutoka kwa wale wanaojishughulisha sana na Historia ya Misri ya zamani, kwamba jina la Firauni aliyekuwa wakati wa Nabii Musa ni Munfitah.

JINA LA MAMAKE MUSA NA VIGANO

Ama Nabii Musa(a.s) ni mtoto wa Imran ambaye watu wa Kitab wanamwita Imram. Katika Juz.1 (2:51), tumeeleza kwamba jina la Nabii Musa ni maneno mawili yaliyochanganywa: neno ‘Mu’ lenye maana ya maji na ‘Sa ‘ lenye maana ya mti. Kwa sababu mama yake alimweka katika sanduku, akalifunga kufuli na akalitupa katika mto Nile kwa kumhofia Fir’aun.

La kushangaza ni uzushi wa mgunduzi wa kufuli hii, aliyotumia mama yake Nabii Musa kumfungia mwanawe, kuzusha kigano kilichoenea na kutangaa karne kwa karne na ambacho wamekiamini wapuzi wengi.

Nacho ni kuwa hakuna kufuli yoyote ila hufunguka ikisomewa jina la mama yake Nabii Musa. Kwa ajili hii hawalijui jina hilo isipokuwa watu maalum wenye siri.

Siku moja nilikwenda kwa mtu mmoja katika watu wa dini mwenye jina kubwa kati ya watu wake. Nikamkuta anapekua kwa hima sana mijalada ya kitabu Biharul-Anwar cha Allama Majlisi. Nikamwuliza: “Kwani una nini?” Akajibu: “Ninataka kujua jina la mama yake Nabii Musa.”

Miaka miwili iliyopita, bwana mmoja alinifuata akidhani mimi ni katika watu wa siri na kuniuliza jina la mama yake Nabii Musa. Nikamwambia: “Wewe wajua zaidi kuliko mimi,” lakini hakukubali. Nikamwambia: “Lakini huu ni upuuzi.” Akaona kuwa mimi namuhepa tu, sitaki kumfichulia siri hii. Nilipokata tamaa kabisa ya kumtuliza nikamwambia: “Haifai nikufichulie, kwa sababu sikuamini, utaiba mali za watu.” Basi akaapa kwa kiapo kizito kwamba yeye hataiba lakini mimi nikajifanya simwamini.

Siku zikapita nikaingilia kufasiri Qur’an Tukufu, nilipofika Aya hii nikawa narudia rejea mbalimbali, miongoni mwazo ni kitabu Qasasul–Quran kili- choandikwa na waandishi wane wa Kimisri: Muhammad Ahmad Jadul-Maula, Ali Muhammad Al-Bajawi, Muhamad Abul-Fadhl na Sayyid Shahatih, mara nikaona jina la mama yake Nabii Musa Yukabid (Jochebed) lakini watungaji hawakulinasibisha kwenye chimbuko lake.

Baada ya kutoka nje kidogo, turudie kisa cha Musa na Firauni; kama kilivyokuja katika Aya tulizo nazo. Kwa ufupi maana yake ni kwamba Firauni alikuwa akidai uungu badala ya Mwenyezi Mungu na alikuwa akiwakandamiza WaIsrael.

Mwenyezi Mungu akamtuma Nabii Musa na Harun kwa Firauni. Wakaenda na kujitosa kwenye kikao chake bila ya kuhofia usultani na utaghuti wake. Nabii Musa akamkabili na kumwambia: “Ewe Firauni! Mimi ni Mtume kutoka kwa Mola wa viumbe vyote nimetumwa kwako na kwa kila mpizani; na ninayo yanayothibitisha ujumbe wangu, Sasa waache waisrael na uwape uhuru waende watakapo”

Firauni akadharau akasema: “Lete hayo yanayothibitisha utume wako.” Nabii Musa akaitupa fimbo yake mara ikawa nyoka. Akaweka mkono wake kwenye mfuko wa kanzu yake alipoutoa ukawa unameremeta kwa weupe, na Nabii Musa hakuwa mweupe bali maji ya kunde.

Watu wa Firauni na halmashauri yake wakasema huyu ni mchawi bingwa, Basi Firauni akawakusanya wachawi. Kabla ya kuanza mazingaombwe yao walimwambia Firauni, “Je, tutapata malipo tukimshinda Musa?” Akasema: “Mtakuwa na malipo na kuwa karibu yangu.”

Wachawi wakaanza kutupa kamba na fimbo zao; mara watazamaji wakaona ni kama nyoka wanaotembea, Nabii Musa akatupa fimbo yake, ikameza yote waliyoyabuni. Wale wachawi wakasilimu na kuamini utume wa Nabii Musa. Firauni akawatishia kuwaadhibu na kuwatesa, lakini hawakurudi nyuma na wakathibiti kwenye imani yao, Riwaya nyingi zimeeleza kuwa Firauni alitekeleza vitisho vyake. Na hali ilivyo inalitilia nguvu hilo.

Firauni akawa anampa Nabii Musa na waliokuwa pamoja naye aina kwa aina za adhabu, lakini Nabii Musa aliendelea na mwito wake kwa Mwenyezi Mungu. waisrael wakampigia kelele Nabii Musa: “Tumeudhiwa kabla ya wewe kutujia na baada ya kutujia pia.” Nabii Musa akawaamuru kuvumilia na kuwapa tamaa ya kufaulu.

Mwenyezi Mungu akawaadhibu watu wa Firauni kwa kahati na dhiki. Akawapelekea mvua ya kuharibu mimea na mazao yao, nzinge waliokula vilivyobakishwa na athari ya mafuriko, chawa waliouma miili yao na vyura walioharibu maisha yao. Zaidi ya haya yote, maji yao yaligeuka na kuwa damu.

Hapo walifazaika kwa Nabii Musa. Wakamwambia: “Mola wako akituondolea adhabu tutakuwa miongoni mwa walioamini.” Mwenyezi Mungu akawaondoloea adhabu ili nao warejee, lakini wakavunja ahadi na wakaendelea na ukafiri. Mwenyezi Mungu akawaangamiza kwenye bahari na ikakatwa mizizi ya makafiri. Huu ndio muhtasari wa haraka haraka unaoelezwa na Aya tulizo nazo kuanzia Aya (103) mpaka mwisho wa Aya (137).

Sasa tufafanue yanayofahamishwa na Aya hizo.

MAANA

Kisha baada yao tukamtuma Musa na ishara zetu kwa Fir’aun na wakuu wake lakini wakazikanusha.

Dhamir ya baada yao inawarudia Mitume watano. Nuh, Hud, Swaleh, Lut na Shuaib. Ishara alizotumwa nazo Nabii Musa ni miujiza inayofahamisha utume wake. Wakuu wa Fir’aun, ni wale watukufu wa watu wake ambao mambo yote yako mikononi mwao, wengine ni kufuata na kunyenyekea tu.

Basi tazama jinsi ulivyokuwa mwisho wa wafisadi.

Ambao ni Fir’aun na wasaidizi wake waliozikalia shingo za watu. Mwisho huu utaelezwa katika mfumo mzima wa maelezo.

Akasema Musa: Ewe Firauni! Hakika mimi ni Mtume nitokaye kwa

Mola wa walimwengu.

Hivi ndivyo alivyomwita, “Ewe Firauni” bila ya kumtukuza na kumwadhimisha. Kwa sababu Nabii Musa alikuwa akizungumza lugha ya Mwenyezi Mungu na akafiksha ujumbe wa Mwenyezi Mungu ambao unamfanya mdogo mkubwa yeyote.

Kutokana na hivi ndio tunajua siri ya sera ya watu wema, wakijitukuza kwa mafasiki na kuwanyenyekea kwa udhalili na huruma waumin.

Yanipasa nisiseme juu ya Mwenyezi Mungu isipokuwa haki.

Hivi ndivyo ilivyo kwa kila Mtume aliyeaminiwa na Mwenyezi Mungu juu ya wahyi na kumchaguwa kuwa ni mjumbe wake.

Nimewajia na dalili wazi itokayo kwa Mola wenu.

Inayofahamisha kuwa mimi ni Mtume kutoka kwa Mola wa walimwengu.

Basi waache wana wa Israel waende nami.

Firauni alikuwa amewafanya waisraili watumwa na kuwatumia katika kazi ngumu, Ndipo Nabii Musa akataka waachiwe huru waende popote watakapo.

Akasema: Ikiwa umekuja na ishara, basi ilete ukiwa ni miongoni mwa wasemao kweli.

Inaonyesha kuwa Firauni alikuwa akidhani kuwa Nabii Musa ni mwongo katika madai yake, akataka kumfedhesha mbele ya wakuu, akamwambia: “Ilete hiyo hoja kama ni mkweli.” Nabii Musa akamziba mdomo wake kwa hoja mkataa.

Akatupa fimbo yake, mara ikawa nyoka dhahir . yaani nyoka halisi. Hapo Firauni akafazaika, lakini akajikaza kwa vile alikuwa akidai kuwa yeye ni Mungu Mkuu.

Nabii Musa tena akamshutukizia na muujiza wa pili.Na akautoa mkono wake. Mara ukawa mweupe kwa watazamao na mkono wa Nabii Musa ulikuwa rangi ya kahawia, sasa umekuwaje mweupe bila ya ugonjwa wowote?

Fir’aun akahisi unyonge na udhalili, akajiona yuko chini kabisa. Wale waliokaa naye wakatambua hilo kwamba Nabii Musa amewangusha kutoka juu.

Wakasema wakuu wa watu wa Firauni: Hakika huyu ni mchawi mjuzi.

Hiyo ndiyo hoja ya mwenye kushindwa nayo ni kutuhumu watu wema. Kisha wakuu wakaendelea kusema:

Anataka kuwatoa katika ardhi yenu .

Yaani Nabii Musa anataka kuwaondoa kwenye ufalme. Fir’aun aliposikia hivi akasema:

Basi mnatoa shauri gani? Wakasema: Mwache kidogo yeye na ndugu yake kwa sababu ukiwaua, watu watakasirika na utawala wako utakuwa hatarini.

Na uwatume mijini wakusanyao Yaani askariWakuletee kila mchawi mjuzi.

Watu wa Historia wanasema kuwa nchi ya Misri wakati wa Mafir’aun ilikuwa ikichemka na uchawi. Makuhani na waangalizi wa miungu ndio waliokuwa wakiendeleza kazi ya Uchawi. Anasema Aqqad katika Kitabu Iblisi kwenye kifungu cha Maendeleo ya Kimisr:

“Mafirauni wenyewe walikuwa wakikimbilia wachawi kwa kushindana na roho zilizojifiicha. Na tunayo mabaki ya visa vya uchawi ambayo hawakuyachagua wanaokusanya athari, lakini waliafikiana kuwa ni kazi za kichawi.

Walikuwa wakiugawanya uchawi kwenye mafungu: Kuna ule unaosaidiwa na uwezo wa mungu wa kheri dhidi ya mungu wa shari na ule unaosaidiwa na uwezo wa shetani mkubwa dhidi ya shetani mdogo.”

Kuenea uchawi wakati wa Firauni kunatufasiria sisi fimbo ya Nabii Musa na unatilia nguvu msingi unasema kuwa kila mwujiza wa Mtume ulikuja kulingana na aina iliiyoenea wakati wake, ili ushindi uwe mkubwa katika hoja na kukata kila udhuru – hoja mkataa.

Kwa hiyo Nabii Musa alivunja uchawi kwa vile ulienea zama zake.

Nabii Isa akafufua wafu, na Nabii Muhammad akawanyamazisha wanafasihi, kwa lengo hilo hilo.

وَجَاءَ السَّحَرَةُ فِرْعَوْنَ قَالُوا إِنَّ لَنَا لَأَجْرًا إِن كُنَّا نَحْنُ الْغَالِبِينَ ﴿١١٣﴾

113. Wakaja wachawi wa Firauni, wakasema: Tutapata ujira ikiwa tutashinda?

قَالَ نَعَمْ وَإِنَّكُمْ لَمِنَ الْمُقَرَّبِينَ ﴿١١٤﴾

114. Akasema: Ndio, nanyi hakika mtakuwa miongoni mwa wanaokurubishwa.

قَالُوا يَا مُوسَىٰ إِمَّا أَن تُلْقِيَ وَإِمَّا أَن نَّكُونَ نَحْنُ الْمُلْقِينَ ﴿١١٥﴾

115. Wakasema: Ewe Musa utatupa wewe au tutupe sisi?

قَالَ أَلْقُوا فَلَمَّا أَلْقَوْا سَحَرُوا أَعْيُنَ النَّاسِ وَاسْتَرْهَبُوهُمْ وَجَاءُوا بِسِحْرٍ عَظِيمٍ ﴿١١٦﴾

116. Akasema: Tupeni. Walipotupa waliyazuga macho ya watu na wakawaogopesha, wakaleta uchawi mkubwa.

وَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ مُوسَىٰ أَنْ أَلْقِ عَصَاكَ فَإِذَا هِيَ تَلْقَفُ مَا يَأْفِكُونَ ﴿١١٧﴾

117. Tukampelekea wahyi Musa kwamba tupa fimbo yako, mara ikavimeza walivyovibuni.

فَوَقَعَ الْحَقُّ وَبَطَلَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١١٨﴾

118. Ukweli ukasimama na yakabatilika waliyokuwa wakiyatenda.

فَغُلِبُوا هُنَالِكَ وَانقَلَبُوا صَاغِرِينَ ﴿١١٩﴾

119. Kwa hiyo hapo walishindwa wakageuka wakawa wadogo.

وَأُلْقِيَ السَّحَرَةُ سَاجِدِينَ ﴿١٢٠﴾

120. Wachawi wakapomoka kusujudu.

قَالُوا آمَنَّا بِرَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٢١﴾

121. Wakasema: Tumemwamini Mola wa Walimwengu.

رَبِّ مُوسَىٰ وَهَارُونَ ﴿١٢٢﴾

122. Mola wa Musa na Harun.

قَالَ فِرْعَوْنُ آمَنتُم بِهِ قَبْلَ أَنْ آذَنَ لَكُمْ إِنَّ هَـٰذَا لَمَكْرٌ مَّكَرْتُمُوهُ فِي الْمَدِينَةِ لِتُخْرِجُوا مِنْهَا أَهْلَهَا فَسَوْفَ تَعْلَمُونَ ﴿١٢٣﴾

123. Akasema Firauni: Je, mmemwamini kabla sijawaruhusu. Hakika hizi ni njama mlizozipanga mjini ili muwatoe wenyewe lakini punde mtajua.

لَأُقَطِّعَنَّ أَيْدِيَكُمْ وَأَرْجُلَكُم مِّنْ خِلَافٍ ثُمَّ لَأُصَلِّبَنَّكُمْ أَجْمَعِينَ ﴿١٢٤﴾

124. Nitawakata mikono yenu na miguu yenu kwa kubadilisha, kisha nitawasulubu nyote.

قَالُوا إِنَّا إِلَىٰ رَبِّنَا مُنقَلِبُونَ ﴿١٢٥﴾

125. Wakasema: Hakika sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu.

وَمَا تَنقِمُ مِنَّا إِلَّا أَنْ آمَنَّا بِآيَاتِ رَبِّنَا لَمَّا جَاءَتْنَا رَبَّنَا أَفْرِغْ عَلَيْنَا صَبْرًا وَتَوَفَّنَا مُسْلِمِينَ ﴿١٢٦﴾

126. Na wewe hutufanyii kisasi ila kwa sababu tumeziamini ishara za Mola wetu zilipotujia. Ewe Mola, tumiminie subira na utufishe hali ya kuwa waislamu.

WAKAJA WACHAWI

Aya 113 – 126

MAANA

Wakaja wachawi kwa Firauni, wakasema: Tutapata ujira ikiwa tutashinda? Akasema, ndiyo, nanyi hakika mtakuwa miongoni mwa wanaokurubishwa.

Wachawi hawa waliojiuza kwa Firauni dhidi ya Nabii Musa walikuwa wanawakilisha dini katika zama zao, Nao wana mifano kila wakati. Wanauza dini yao na dhamiri kwa kila mwenye kutoa pesa. Siku hizi Wazayuni na Wakoloni wamewanunua wengi wenye kofia na vilemba wakawalipa na kuwashika sawasawa wasaidie ukoloni na unyonyaji kwa kuwavunga watu na kuwapoteza. Wakaanzisha jumuia mbalimbali na vitengo kwa jina la dini kwa lengo hilo. Lakini ni haraka mno kufedheka na kuwa kwenye midomo ya dharau ya kila mwenye mwamko mwenye ikhlasi.

Wakasema: Ewe Musa! Utatupa wewe au tutatupa sisi?

Walimuhiyarisha kuanza au waanze wao kwa kutegemea uchawi wao kuwa watashinda na kutomjali Nabii Musa(a.s) . La kushangaza ni kauli ya Razi, kwamba wachawi walimuhiyarisha Nabii Musa kwa kumheshimu.

Akasema: Tupeni ! Akiwadharau wao na uchawi wao.

Walipotupa waliyazuga macho ya watu na wakawaogopesha, na wakaleta uchawi mkubwa.

Kunasibisha kuzuga kwenye macho ya watu ni dalili kwamba uchawi wao si tukio la kweli, isipokuwa ni kuwavunga watu tu.

Kuwaogopesha, ni kwamba wachawi waliwatisha watazamaji na wakaleta uchawi mkubwa katika kuzuga na kupoteza si katika uhakika au hali halisi.

Tukampelekea wahyi Musa kwamba tupa fimbo yako, Mara ikavimeza walivyovibuni, Ukweli ukasimama na yakabatilika waliyokuwa wakiyabuni.

Nabii Musa alihofia wajinga wasihadaike na mizungu ya wachawi na upotevu wao. Mwenyezi Mungu akamfunga mkanda na kumpa wahyi kwamba yuko pamoja naye; na kwamba waliyoyaleta si chochote ni mizungu tu.

Akamwamrisha atupe fimbo, Alipoitupa ikameza yale waliyoyabuni kukabatilika kujifanya kwao ikadhihiri haki machoni kwa wote.

Firauni akaduwaa kwa mshtuko uliompata mbele ya umma wa watu. Amewaleta wachawi kutoka kila pembe ili wakilinde kiti chake na awathibitishie watu uwongo wa Nabii Musa na uzushi wake, Leo mambo yamebadilika kichwa chini miguu juu. Wote wakiwemo wachawi wameamini ukweli wa Nabii Musa na uaminifu wake na kukadhibisha uwongo wa Firauni na hiyana yake.

Kwa hiyo hapo walishindwa wakageuka wakawa wadogo baada ya kiburi kile.

Lau mambo yangeishia hivyo hivyo, kidogo Firauni angelipumua, lakini alishtukiziwa kwa jambo zito na chungu.

Na wachawi wakapomoka wakasujudu, Wakasema: Tumemwamini Mola wa waliimwengu (wote), Mola wa Musa na Harun si Firauni aliyewaleta kubatilisha mwito wa Mwenyezi Mungu na wa haki.

Utauliza : kuna makusudio gani ya kauli ya Wachawi ‘Mola wa Musa na Harun’ ambapo ingelitosha tu kusema ‘Mola wa walimwengu’?

Jibu : Firauni alikuwa akiwaambia watu:

فَقَالَ أَنَا رَبُّكُمُ الْأَعْلَىٰ ﴿٢٤﴾

“Mimi ndiye Mola wenu mkubwa (79: 24)

مَا عَلِمْتُ لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرِي ﴿٣٨﴾

“Simjui kwa ajili yenu Mungu asiyekuwa mimi” (28: 38).

Lau wachawi wangelitosheka na kusema Mola wa walimwengu, basi Firauni angeligeuza na kujisifu yeye na kusema wananikusudia mimi Mola wa walimwengu. Ndipo wakaikata njia ya majisifu yake na kubadilisha kwake mambo.

UCHAWI

Katika Juz.1 (2:103) Tulizungumzia kuhusu uchawi kwa anuani ya ‘Uchawi na hukumu yake’, Tukasema katika tuliyoyasema, kwamba sisi tuko pamoja na wale waonao kuwa uchawi hauna chochote na tukatoa dalili ya hilo. Kuunganisha yaliyopita hapa tunaongezea haya yafuatayo:

Kauli yake Mwenyezi Mungu Wakayazuga macho ya watu ni dalili wazi kwamba uchawi hauna kitu chochote, na kwamba ni ujanja na kiini macho.

Ama kauli yake Mwenyezi Mungu: wakaleta uchawi mkubwa maana yake ni kwamba walifika kikomo cha ujanja na kubadilisha mambo. Maana haya yafafanuliwa na kusisitizwa na kauli yake Mwenyezi Mungu.

فَإِذَا حِبَالُهُمْ وَعِصِيُّهُمْ يُخَيَّلُ إِلَيْهِ مِن سِحْرِهِمْ أَنَّهَا تَسْعَىٰ ﴿٦٦﴾

“Mara kamba zao na fimbo zao zikadhaniwa mbele yake, kwa uchawi wao, kuwa zinapiga mbio”(20:66).

Hazikuwa zikienda hasa, bali ni dhana na mawazo tu. Mtume mtukufu(s.a.w.w) amesema: “Mwenye kumwendea mchawi au kuhani na mwongo akamsadiki, basi amekufuru aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu.”

Wafasiri wengi wamesema kuwa wachawi wa Firauni walifanya hila ya kutingisha kamba na fimbo kwa kuziwekea Zebaki ili zitingishike na joto la jua.

Vyovyote iwavyo tunaamini kwa imani isiyo na shaka kwamba mchawi ni mwongo hakuna anayemsadiki ila mpuzi; na kwamba waliyoyafanya wachawi wa Firauni na wanayofanya wahindi na wengineo ambayo yanashangaza, yana sababu bila ya shaka yoyote.

Na sisi ijapokuwa hatujui sababu yenyewe, tunaamini kwa yakini kabisa kwamba uchawi hauwezi kubadilisha kitu, vinginevyo basi mchawi angeliweza kujizuia yeye na madhara na kujinufaisha na kutawala ulimwengu wote kwa kutaka kwake na matabano yake; na angelikuwa mshirika wa Mwenyezi Mungu katika milki yake Mwenyezi Mungu. Ametukuka kabisa na hayo Mwenyezi Mungu.

Akasema Firauni: Je, mmemwamini kabla sijawaruhusu?

Unaona mantiki hii? Anawataka wamwombe ruhusa katika mambo ya nyonyo zao imani, mapenzi na chuki. Hata mtu ulimwenguni asiutawale moyo wake mwenyewe! Lakini hiyo ni mantiki ya kitaghuti.

Hakika hizi ni njama mlizozipanga mjini ili muwatoe wenyewe, lakini punde mtajua.

Firauni anawaelekezea wachawi tuhuma hizi kuwa kumwamini kwao Nabii Musa hakukuwa kwa hoja na kukinaika, isipokuwa ni hila na hadaa tu walizozipanga pamoja kabla na kwamba lengo la njama hizi ni kuwatoa watawala na kuwavua utawala wao katika Misri.

Firauni alisema maneno haya akiwa anajua kwamba yeye ni mwongo katika kauli yake, lakini alitaka kuwababaisha watu akihofia wasimwache yeye wakamwamini Nabii Musa, lakini watu wanajua kwamba wachawi hawakuamini isipokuwa kwa kuona na kukinai. Vilevile watu wanajua kwamba Nabii Musa hakuwa pamoja na wachawi. Kwa sababu Firauni aliwakusanya huku na huko.

Nitawakata mikono yenu na miguu yenu kwa kubadilisha, kisha nitawasulubu nyote.

Kukata kwa kubadilisha ni kukata mkono wa kuume na mguu wa kushoto, na kinyume.

Hiyo ndiyo silaha ya mataghuti katika kuikabili haki, Anasema Masud katika kitabu Muruju-dhahab: “Katika mwaka 59 (A.H.) Muawiya ali- wakusanya watu ili wambai mwanawe Yazid. Akasimama kuhutubu mtu mmoja kutoka Azdi akasema:

“Akifa huyu akimwonyesha Muawiya basi ni huyu,akimwonyesha Yazid. Na atakayekataa basi ni huu, akautingisha upanga. Muawiya akamwambia: “Kaa, wewe ni hatibu bora kuliko watu wote.”

Wakasema: Hakika sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu.

Fanya utakavyo hatukujali wewe wala kuua kwako, Sisi tuna yakini ya kukutana na Mola wetu na uadilifu wake.

Kila mwenye kuamini kukutana na Mwenyezi Mungu anakuwa na msimamo huu bali anaona kufa shahidi ni kheri na nyenzo ya kupata radhi ya Mwenyezi Mungu na thawabu zake, Ama wale ambao wanaoogopa mauti katika njia ya Mwenyezi Mungu, wanaamini kinadharia tu; ama kimatendo wao wanakanusha.

Na wewe hutufanyii kisasi ila kwa sababu tumeziamini ishara za Mola wetu zilipotujia.

Kauli yao hii ina madhumuni ya kumtisha Firauni. Kwa sababu maana yake ni kwamba wewe hutuchukulii kisasi isipokuwa unamchukulia kisasi Mwenyezi Mungu na Mtume Muhammad(s.a.w.w) wake hasa. Kwa sababu hatuna kosa sisi ila kumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake Nabii Musa:

أَلَمْ يَعْلَمُوا أَنَّهُ مَن يُحَادِدِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَأَنَّ لَهُ نَارَ جَهَنَّمَ ﴿٦٣﴾

“Je hawajui kwamba anayeshindana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi yeye atapata moto wa Jahanam.” (9:63).

Ewe Mola wetu tumiminie subira . Katika msimamo huu.

Unasifiwa uvumilivu (subira) kwa kuuliwa na kuadhibiwa katika njia ya Mwenyezi Mungu (s.w.t). Walimuomba Mungu awaruzuku fadhila hii kwa kuhofia wasilegeze mkanda na kurudi nyuma watakapohisi upanga ukipenya milini mwao.

Na utufishe hali ya kuwa ni waislamu, wanyenyekevu kwako na kwa Mtume wako tukiwa radhi na adhabu na mateso katika njia yako.

3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

وَقَالَ الْمَلَأُ مِن قَوْمِ فِرْعَوْنَ أَتَذَرُ مُوسَىٰ وَقَوْمَهُ لِيُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ وَيَذَرَكَ وَآلِهَتَكَ قَالَ سَنُقَتِّلُ أَبْنَاءَهُمْ وَنَسْتَحْيِي نِسَاءَهُمْ وَإِنَّا فَوْقَهُمْ قَاهِرُونَ ﴿١٢٧﴾

127. Na wakasema wakuu wa kaumu ya Firauni: Je, utamwacha Musa na watu wake walete uharibifu katika nchi na kukuacha wewe na waungu wako. Akasema: Tutawauwa watoto wao wa kiume na tutawaacha hai wanawake wao. Na hakika sisi ni wenye nguvu juu yao.

قَالَ مُوسَىٰ لِقَوْمِهِ اسْتَعِينُوا بِاللَّـهِ وَاصْبِرُوا إِنَّ الْأَرْضَ لِلَّـهِ يُورِثُهَا مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ وَالْعَاقِبَةُ لِلْمُتَّقِينَ ﴿١٢٨﴾

128. Musa akawaambia watu wake: Ombeni msaada kwa Mwenyezi Mungu na subirini. Ardhi ni ya Mwenyezi Mungu atamrithisha amtakaye katika waja wake na mwisho ni wa wenye takuwa.

قَالُوا أُوذِينَا مِن قَبْلِ أَن تَأْتِيَنَا وَمِن بَعْدِ مَا جِئْتَنَا قَالَ عَسَىٰ رَبُّكُمْ أَن يُهْلِكَ عَدُوَّكُمْ وَيَسْتَخْلِفَكُمْ فِي الْأَرْضِ فَيَنظُرَ كَيْفَ تَعْمَلُونَ ﴿١٢٩﴾

129. Wakasema: Tumeudhiwa kabla hujatufikia na baada ya kutujia. Akasema: Huenda Mola wenu atamwangamiza adui yenu na kuwafanya makhalifa katika ardhi aone jinsi mtakavyokuja fanya.

UTAMWACHA MUSA?

Aya 127 – 129

MAANA

Na wakasema wakuu wa kaumu ya Fir’aun: Je, utamwacha Musa na watu wake walete uharibifu katika nchi.”

Baada ya kwisha tukio hilo la kutisha ambalo Nabii Musa alipata ushindi na kufedheheka Firauni. Nabii Musa aliendelea kuwalingania kwenye ibada ya Mwenyezi Mungu peke yake, na dalili yake ni yaliyotukia jana tu kati yake na wachawi, Watu wengi wakamkusanyikia.

Wakuu wa Firauni wakahofia hali isibadilike na mambo yakawageukia wao na bwana wao, hapo wakamchochea Firauni na kumwambia: “Mpaka lini utamnyamazia Musa na kumwacha akiharibu nchi?” Kuharibu nchi, wanamaanisha watu kumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake.

Na wakuache wewe na waungu wako.

Kauli hii ya wakuu wa Firauni inafahamisha kuwa alikuwa nao waungu anaowaabudu; nayo inapingana, kwa dhahiri yake, na kauli ya Firauni kuwa Mimi ndiye mola wenu mkubwa na simjui kwa ajili yenu Mungu asiyekuwa mimi.

Wafasiri wamelijibu hilo kwa majibu kadhaa. Lenye nguvu zaidi ni kuwa Firauni alikuwa na miungu akidai kuwa yeye ni mwana kipenzi wa hiyo miungu na kwamba yeye anaitegemeza hukumu yake na utawala wake kwenye hiyo miungu. Kwa hiyo kauli yake simjui kwa ajili yenu Mungu na Mola isipokuwa yeye peke yake inamaanisha kuwa hakuna yeyote mwenye kuhukumu kwa jina la mungu isipokuwa yeye. Maana haya yanatiliwa nguvu na kauli yake:

أَلَيْسَ لِي مُلْكُ مِصْرَ وَهَـٰذِهِ الْأَنْهَارُ تَجْرِي مِن تَحْتِي ﴿٥١﴾

“Kwani ufalme wa Misri si wangu na hii mito inapita chini yangu?” (43:51).

Akasema: Tutawaua watoto wao wakiume na tutawaacha hai wanawake wao.

Kabla ya kuzaliwa Nabii Musa, Fir’aun alikua akwaiua watoto wa kiume wa Bani Israel waliposisitizia wakuu katika watu wake apambane na Nabii Musa, aliwajibu atarudisha mpango huo wa mwanzo.

Na hakika sisi ni wenye nguvu juu yao.

Yaani tuna nguvu juu yao kama ilivyokuwa kabla ya Musa.

Musa akawaambia watu wake: Ombeni msaada kwa Mwenyezi Mungu na subirini. Ardhi ni ya Mwenyezi Mungu atamrithisha amtakaye katika waja wake na mwisho ni wa wenye takuwa.”

Waisrael waliposikia vitisho vya Firauni na kiaga chake waliogopa. Nabii Musa(a.s) akawatuliza na kuwaamrisha kuwa na subira (uvumilivu) na kumtegemea Mwenyezi Mungu; na akawapa tumaini la ushindi ikiwa wao watasubiri na kumwogopa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu ardhi ni ya Mwenyezi Mungu si ya Firauni, na Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye kumcha.

Wakasema: Tumeudhiwa kabla hujatufikia na baada ya kutujia!

Firauni alikuwa akiwakandamiza waisrael kabla ya kuja Nabii Musa na akawashtua kuwakandamiza zaidi baada ya kuja kwake. Walipomwambia Nabii Musa hivyo akasema:

Huenda Mola wenu akamwangamiza adui yenu na kuwafanya makhalifa katika nchi aone jinsi mtakavyokujafanya.

Nabii Musa(a.s) alikuwa anajua wazi kuwa Firauni ataangamia na kwamba Mungu atawaokoa wana wa Israil na kuwamakinisha katika ardhi, lakini alitoa ibara ya huenda ili wasibweteke na ahadi yake.

Kisha akaishiria Nabii Musa kwamba, si muhimu kuwa adui ataangamia na wao kuwa makhalifa katika ardhi, lakini muhimu zaidi ni kumcha Mungu na kuutumia vizuri huo ukhalifa katika ardhi yake; na kwamba Mungu atawaangalia je, watatengeza au wataharibu?

Na wamefanya mengi sana katika ardhi; hapo mwanzo waliwaua mitume na viongozi wema, baadae wakaunda dola isiyokuwa na sharia isipokuwa matamanio ya kuua na kufukuza watu makwao.

Mwaka huu wa 1968, kimetoka kitabu huko Israil kinaitwa Siyakh lokhamim yaani simulizi za wanajeshi. Gazeti la Al-ahram la Misr toleo la tarehe 23-8-1968, limefasiri baadhi ya yaliyomo katika kitabu hicho:

“Ambaye hawezi kuvunja nyumba na kuwafurusha waliomo katika nyumba hiyo, basi bora akae nyumbani kwake tu. Sisi tulipokuja kwenye nchi ya Palestina kulikuwa na watu wengine wanaoishi humo; hatukuwa na matumaini kuwa wataweza kukubali kutuachia mashamba yao na majumba yao. Kwa hiyo ikawa hakuna budi tuwaue au kuwatishia kuwaua ili wakimbie watuachie majumba na mashamba”

Hii ndiyo sharia na lengo la Israil: kuua na kufukuza. Hii sio dola kama dola nyinginezo; isipokuwa ni kikosi cha kizayuni cha mauaji chenye lengo la kuwafukuza wenyeji na kukalia nchi zao kuanzia mto Nail hadi Furat.

Je Waarabu wamejiandaa na nini? Hakuna njia wala mbinu yoyote isipokuwa misimamo ya kivietnam inayosema: ‘Kufa na kupona’ ama kusiweko na Israil au kusiweko na Mwarabu.

وَلَقَدْ أَخَذْنَا آلَ فِرْعَوْنَ بِالسِّنِينَ وَنَقْصٍ مِّنَ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَذَّكَّرُونَ ﴿١٣٠﴾

130. Na hakika tuliwaadhibu watu wa Firauni kwa ukame na kwa kupungukiwa na mazao, ili wapate kukumbuka.

فَإِذَا جَاءَتْهُمُ الْحَسَنَةُ قَالُوا لَنَا هَـٰذِهِ وَإِن تُصِبْهُمْ سَيِّئَةٌ يَطَّيَّرُوا بِمُوسَىٰ وَمَن مَّعَهُ أَلَا إِنَّمَا طَائِرُهُمْ عِندَ اللَّـهِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿١٣١﴾

131. Ulipowafikia wema, walisema: Huu ni kwa ajili yetu na ulipowafikia ubaya walimnasibishia mkosi Musa na walio pamoja naye. Sikilizeni! Hakika mkosi wao unatoka kwa Mwenyezi Mungu lakini wengi wao hawajui.

وَقَالُوا مَهْمَا تَأْتِنَا بِهِ مِنْ آيَةٍ لِّتَسْحَرَنَا بِهَا فَمَا نَحْنُ لَكَ بِمُؤْمِنِينَ ﴿١٣٢﴾

132. Na wakasema: Hata ukituletea ishara yoyote kutur- oga hatutakuamini.

فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمُ الطُّوفَانَ وَالْجَرَادَ وَالْقُمَّلَ وَالضَّفَادِعَ وَالدَّمَ آيَاتٍ مُّفَصَّلَاتٍ فَاسْتَكْبَرُوا وَكَانُوا قَوْمًا مُّجْرِمِينَ ﴿١٣٣﴾

133. Basi tukawapelekea tufani na nzige na chawa na vyura na damu kuwa ishara mbalimbali, lakini wakatakabari na wakawa watu wakosefu.

TULIWAADHIBU WATU WA FIRAUNI

Aya 130-133

MAANA

Na hakika tuliwaadhibu watu wa Firauni kwa ukame na kwa kupungukiwa na mazao, ili wapate kukumbuka.

Misri ilikuwa ikibubujika rutuba na mazao. Firauni akajifaharusha kwa rutuba hii na kusema:

وَهَـٰذِهِ الْأَنْهَارُ تَجْرِي مِن تَحْتِي ﴿٥١﴾

"Na pia mito hii ipitayo chini yangu" (43:51)

Mwenyezi Mungu alitia balaa ya kahati na dhiki ya maisha wakati wa Firauni wa Musa ili ajutie upotevu wake na aitikie mwito wa haki. Kuna Hadith isemayo: "Wakiwa waovu watawala hufungwa mvua."

Ni sawa iwe kulikuwako na uhusiano baina ya dhuluma ya mtawala na kahati kwa njia ya ujumla au isiweko, lakini Mwenyezi Mungu aliwaadhibu watu wa Firauni kwa dhulma yao ili wao wakumbuke kabla ya kuwaingiza ndani kwenye uchungu.

Ulipowafikia wema, walisema: Huu ni kwa ajili yetu na ulipowafikia ubaya walimnasibishia mkosi Musa na walio pamoja naye.

Wanafasiri matukio kwa mantiki haya, Kila heri inayowapata basi wanaistahiki wao. Kwa sababu wao wanatawala watu, na kila ubaya unaowapa- ta, basi sababu yake ni yule anayewalingania kwenye haki. Ama rutuba na ukame wanautenga na Mwenyezi Mungu na maumbile aliyo yaumba.

Ndipo Mwenyezi Mungu akawajibu kwa kusema: Sikilizeni! Hakika mkosi wao unatoka kwa Mwenyezi Mungu lakini wengi wao hawajui. Mkosi wao ni fumbo la ukame uliowapata na huo ni kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu ambayo sababu zote huishia kwake, na kumnasibishia Musa na ujinga na upumbavu tu.

Utauliza : Kwa nini Mwenyezi Mungu ametumia neno wema kwa ibara yenye al (Al-Hasana) ambayo katika sarufi ya Kiarabu inaitwa ma'rifa, na neno ubaya aktumia bila ya al ambyo ni nakira?

Jibu : Sio mbali kuwa ni ishara ya kwamba maumbile ya heri, kama vile rutuba n.k, ni mengi, na kwamba ubaya, kama vile matetemeko na tufani na ukame ni machache.

Na wakasema: Hata ukituletea ishara yoyote kuturoga hatutakuamini

Huku ni kukiri wazi, kwamba wao wanaikataa haki, wakati huo huo wanakiri kushindwa kwao kwa hoja na dalili. Yakawa malipo ya inadi yao hii ni kuwapata balaa ya aina tano za adhabu:

1.Tukawapelekea tufani ya mvua ikaharibu mimea na mifugo.

2.Na nzige waliokuja baada ya tufani,kama kawaida, wakala mimea yao iliyobakia.

3.Na chawa.

4.Na vyura waliowaghasi maisha yao.

5.Na damu. Inasemekana maji yao yaligeuka kuwa damu na wasi weze kupata maji matamu. Na inasemekana walipatwa na maradhi ya kutokwa na damu za pua.

وَلَمَّا وَقَعَ عَلَيْهِمُ الرِّجْزُ قَالُوا يَا مُوسَى ادْعُ لَنَا رَبَّكَ بِمَا عَهِدَ عِندَكَ لَئِن كَشَفْتَ عَنَّا الرِّجْزَ لَنُؤْمِنَنَّ لَكَ وَلَنُرْسِلَنَّ مَعَكَ بَنِي إِسْرَائِيلَ ﴿١٣٤﴾

134. Na ilipowaangukia adhabu wakasema: Ewe Musa Tuombee kwa Mola wako kwa yale aliyokuahidi. Kama ukituondolea adhabu bilashaka tutakuamini na hakika tutawaacha wana wa Israil waende nawe.

فَلَمَّا كَشَفْنَا عَنْهُمُ الرِّجْزَ إِلَىٰ أَجَلٍ هُم بَالِغُوهُ إِذَا هُمْ يَنكُثُونَ ﴿١٣٥﴾

135. Lakini tulipowaondolea adhabu kwa muda watakaoufikia, mara wakavunja ahadi.

فَانتَقَمْنَا مِنْهُمْ فَأَغْرَقْنَاهُمْ فِي الْيَمِّ بِأَنَّهُمْ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَكَانُوا عَنْهَا غَافِلِينَ ﴿١٣٦﴾

136. Basi tuliwapatiliza na tukawazamisha baharini kwa sababu walizikadhibisha ishara zetu na wakaghafilika nazo

وَأَوْرَثْنَا الْقَوْمَ الَّذِينَ كَانُوا يُسْتَضْعَفُونَ مَشَارِقَ الْأَرْضِ وَمَغَارِبَهَا الَّتِي بَارَكْنَا فِيهَا وَتَمَّتْ كَلِمَتُ رَبِّكَ الْحُسْنَىٰ عَلَىٰ بَنِي إِسْرَائِيلَ بِمَا صَبَرُوا وَدَمَّرْنَا مَا كَانَ يَصْنَعُ فِرْعَوْنُ وَقَوْمُهُ وَمَا كَانُوا يَعْرِشُونَ ﴿١٣٧﴾

137. Tukawarithisha watu walionekana wadhaifu mashariki na magharibi ya ardhi tuliyoibariki. Na likatimia neno jema la Mola wako kwa wana wa Israil, kwa sababu walikuwa na subira; na tukayaangamiza yale aliyokuwa akiyafanya Firauni na kaumu yake na yale waliyokuwa wakiyajenga.

ILIPOWAANGUKIA ADHABU

Aya 134-137

MAANA

Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja aina tano za adhabu alizowaadhibu watu wa Firauni. Na walikuwa kila inapowapata adhabu hutawasali kwa Musa kutaka kuondolewa adhabu hiyo kwa karamu yake mbele ya Mwenyezi Mungu.

Walikuwa wakijiwekea ahadi wao wenyewe kwa Musa kuwa akifanya, basi wataitikia mwito wa haki. Mwenyezi Mungu naye alikuwa akiwaondolea adhabu kwa muda fulani ili wajiandae na toba na kuwasimamishia hoja, Lakini walikuwa wakivunja ahadi, hawakutekeleza wanayoyasema.

Hapo Mwenyezi Mungu huwateremshia mara ya pili, Tena wanarudia kunyenyekea na kutawasali, na Mwenyezi Mungu huwaondolea. Ikawa namna hii mpaka adhabu ya tano, au jaribio la tano, ndipo akawatesa na kuwatupa ndani ya bahari.

Baada ya muda mrefu kupita tangu kufamaji Firauni na kufariki Musa na Harun, alitokea katika waisrail, Daudi na Suleiman wakafanya dola yenye mipaka mashariki na magharibi.

Lakini haraka sana dola iliyeyuka na Waisrail wakatawaliwa na Ebuchadnezer, wafursi na makhalifa wa Alexandria kisha wa Roma.

وَجَاوَزْنَا بِبَنِي إِسْرَائِيلَ الْبَحْرَ فَأَتَوْا عَلَىٰ قَوْمٍ يَعْكُفُونَ عَلَىٰ أَصْنَامٍ لَّهُمْ قَالُوا يَا مُوسَى اجْعَل لَّنَا إِلَـٰهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ قَالَ إِنَّكُمْ قَوْمٌ تَجْهَلُونَ ﴿١٣٨﴾

138. Na tukawavusha bahari wana wa Israil na wakawafikia waliokuwa wakiyaabudu masanamu yao; wakaema: Ewe Musa! Hebu nasi tufanyie waungu kama hawa walivyo na waungu. Akasema Hakika nyinyi ni watu wafanyao ujinga.

إِنَّ هَـٰؤُلَاءِ مُتَبَّرٌ مَّا هُمْ فِيهِ وَبَاطِلٌ مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٣٩﴾

139. Hakika waliyona hawa yatawangamiza na ni bure waliyokuwa wakiyafanya.

قَالَ أَغَيْرَ اللَّـهِ أَبْغِيكُمْ إِلَـٰهًا وَهُوَ فَضَّلَكُمْ عَلَى الْعَالَمِينَ ﴿١٤٠﴾

140. Akasema je, niwatafutie mungu badala ya Mwenyezi Mungu, hali yeye ameweafadhilisha juu ya walimwengu?

وَإِذْ أَنجَيْنَاكُم مِّنْ آلِ فِرْعَوْنَ يَسُومُونَكُمْ سُوءَ الْعَذَابِ يُقَتِّلُونَ أَبْنَاءَكُمْ وَيَسْتَحْيُونَ نِسَاءَكُمْ وَفِي ذَٰلِكُم بَلَاءٌ مِّن رَّبِّكُمْ عَظِيمٌ ﴿١٤١﴾

141. Na Tulipowaokoa kwa kaumu ya Firaun waliowapa adhabu mbaya wakiwaua watoto wenu wa kiume na kuwaacha hai wanawake wenu. Na katika hayo ulikuwa mtihani mkubwa uliotokea kwa Mola wenu.

TULIWAVUSHA WANA WA ISRAIL

Aya 138-141

MAANA

Na tukawavusha bahari wana wa Israil na wakawafikia waliokuwa wakiyaabudu masanamu yao; wakaema: Ewe Musa! Hebu nasi tufanyie waungu kama hawa walivyo na waungu. Akasema: Hakika nyinyi ni watu wafanyao ujinga.

Baadhi ya riwaya zinaeleza kuwa Musa aliendelea miaka ishirini na tatu akipigana jihadi na Firauni kwa ajili ya Tawhid na kuwakomboa wana wa Israil kutokana ukandamizaji, Wakashuhudia miujiza ya kushangaza iliyodhihiri mikononi mwa Musa.

Mwisho wakaona kupasuka bahari kwa fimbo ya Musa, na jinsi zilivyotokea njia kavu kumi na mbili. Kila ukoo ukawa na njia yake. Vile vile waliona jinsi bahari ilivyofungika kwa Firauni na askari wake.

Yote hayo waliyashuhudia, lakini kabla ya kupita muda walisahau miujiza waliyoiona na macho yao yakawa kwa watu wanaoabudu masanamu, wakamtaka Musa awafanyie sanamu la kuabudu. Walitaka haya wakiwa wanajua kwamba Musa ni mtu wa Mwenyezi Mungu na kwamba umuhimu wake wa kwanza ni mwito wa Tawhid na kupiga vita ushirikina. Vile vile walikuwa wakijua kuwa Mwenyezi Mungu alimwangamiza Firauni na jeshi lake, kwa sababu ya ushirikina wake. Baadhi ya wafisri wanasema; "Lau wao wenyewe wangejifanyia mungu, mshangao ungelikuwa mdogo kuliko kumtaka Mtume wa Mola wa walimwengu wote kuwafanyia mungu. Lakini hao ndio Waisrail!

Hakika yaliyo na hawa yatawangamiza na ni bure waliyokuwa wakiyafanya.

Musa(a.s) alianza kuwajibu watu wake kuwa wao ni wajinga na wapumbavu; kisha akawapa habari kwamba mwisho wa washirikina na waabudu masanamu ni hasara na maangamizi.

Akasema je, niwatafutie mungu badala ya Mwenyezi Mungu, hali yeye ameweafadhilisha juu ya walimwengu?

Imepita tafsiri yake katika Juz.1 (2:47)

Kwa vyovyote kufadhilishwa kwao juu ya Firauni na watu wake hakuhisabiwi kuwa ni fadhila kubwa.

Na Tulipowaokoa kwa kaumu ya Firaun waliowapa adhabu mbaya wakiwaua watoto wenu wa kiume na kuwaacha hai wanawake wenu. Na kati- ka hayo ulikuwa mtihani mkubwa uliotokea kwa Mola wenu.

Umepita mfano wake katika Juz.1(2:49)