TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA Juzuu 9

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 10664
Pakua: 1310

Maelezo zaidi:

Juzuu 9
Juzuu 1
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 15 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 10664 / Pakua: 1310
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA Juzuu 9

Mwandishi:
Swahili

10

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

Sura Ya Nane: Surat Al-Anfal

Ina Aya 75. Imeshuka Madina, isipokuwa Aya 30 hadi 36, hizo zimeshuka Makka.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْأَنفَالِ قُلِ الْأَنفَالُ لِلَّـهِ وَالرَّسُولِ فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَصْلِحُوا ذَاتَ بَيْنِكُمْ وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١﴾

1. Wanakuuliza juu ya Anfal. Sema Anfal ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na msuluhishe mambo baina yenu, na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake ikiwa nyinyi ni waumini.

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ ﴿٢﴾

2. Hakika waumini ni wale ambao anapotajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa hofu, Na wanaposomewa Aya zake huwazidisha imani, Na wanamtegemea Mola wao.

الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿٣﴾

3. Ambao wanasimamisha Swala. Na wanatoa katika yale tuliyowaruzuku.

أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا لَّهُمْ دَرَجَاتٌ عِندَ رَبِّهِمْ وَمَغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ ﴿٤﴾

4. Hao kweli ndio waumini. Wao wana vyeo kwa Mola wao, na maghufira na riziki bora.

ANFAL NI YA MWENYEZI MUNGU NA MTUME

Aya 1 – 4

MAANA

Wanakuuliza juu ya Anfal

Katika Aya hii Mwenye Mungu (s.w.t) ametaja kwamba: watu walimuuliza Mtume(s.a.w.w) kuhusu Anfal, wala hakubainisha makusudio yake.

Wameifikiana watu wa elimu ya dini kwamba neno lolote litakalokuja katika kitabu cha Mwenyezi Mungu na Hadith za Mtume bila ya kuelezwa maana yake, basi litachukuliwa kwenye maana wanayoifahamu watu, Ikiwa watu hawalijui maana yake, zitarudiwa kamusi za lugha.

Kamusi zinasema: Anfal ni ngawira na ziada kwa ujumla bila ya kuyafunga maana yake na ngawira au ziada maalum.

Kwa ajili hiyo ndipo wafasiri wakatofautiana katika makusudio ya Anfal, Je, ni ngawira zote au ni ngawira za Badr tu au ni ngawira nyingine.

Shia Imamia wamesema: “Hakuna sababu ya kutofautiana huku. Kwa sababu imethibiti katika Hadith za Mtume kwa riwaya za Ahlul-bait wa Mtume Muhammad(s.a.w.w) kwamba makusudio ya Anfal ni ardhi iliyochukuliwa kwa wasiokuwa waislamu bila vita na ardhi iliyokufa, ni sawa iwe ilikuwa ikimilikiwa kisha akatoweka mmiliki au la. Pia vilele vya milima, mabonde, misitu minene na kila kinachohusika na vita, kwa sharti ya kuwa kisiwe kimechukuliwa kwa mwislamu au mwenye mkataba. Vilevile na mirathi ya asiyekuwa na mrithi.

Haya yanaafikiana na madhehebu ya Malik, kwa sababu wao wamefasiri Anfal kuwa ni kilichochukulia bila ya vita. Hayo yanapatikana katika Kitab Ahkamul Qur’an cha Abu Bakar, maaruf kwa jina la Ibn Arabi Al-Muafiri. Abu Is-haq Al-fairuzbadi, wa madhehebu ya Shafi, anasema:

Anfal ni kutoa ziada Amiri jeshi kwa aliyefanya tendo lililopelekea kushindwa adui; kama vile uchunguzi, kuonyesha njia au ngome n.k.

Naye Al-Jisas wa madhehebu ya Hanafi anasema: “Ni kusema Amiri jeshi: Atakayemuuwa mtu basi vitu vyake ni vyake na atakayepata kitu ni chake.”

Sema Anfal ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume.

Huu ni ubainifu wa mahali pa Anfal, na kwamba ni ya Mwenyezi Mungu, na cha Mwenyezi Mungu ni cha Mtume wake, na cha Mtume wake hutolewa kwa kuinua tamko la Uislam na maslahi ya waislamu, Atachukua kila mwenye haja kiasi cha haja yake, Ufafanuzi umo katika vitabu vya Fiqh, kikiwemo kitabu chetu Fiqhul-Imam Jafar As-Sadiq Juz. 2.

Basi mcheni Mwenyezi Mungu na msuluhishe mambo baina yenu, na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake ikiwa nyinyi ni waumini.

Hii inatambulisha kuwa swahaba walizozana juu ya Anfal, na walipomuuliza Mtume(s.a.w.w) aliwaambia, kwa amri itokayo kwa Mwenyezi Mungu, kuwa hiyo ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume, na kwamba ni juu yao kuitoa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake wala wasigombane juu ya Anfal na mengineyo, waungane wapendane kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kama ilivyo kwa waumini wa kweli.

Kisha Mwenyezi Mungu mtukufu akawafafanulia kwamba waumini wa kweli ni wale wanaosifika na sifa zifuatazo:

1.Hakika waumini ni wale ambao anapotajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa hofu.

Hofu inakuwa kwa waumini, kwa sababu ya kukutana kwao na Mwenyezi Mungu, hisabu yake na malipo yake, Lakini wao wakati huo huo wanataraji rehema ya Mwenyezi Mungu. Kwa sababu wao vilevile wanaamini kauli yake Mwenyezi Mungu:

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ ﴿٥٣﴾

“Enyi waja wangu mliojidhulumu nafsi zenu msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika yeye ni Mwingi wa kusamehe mwingi wa kurehemu” (39:53).

Na pia kauli ya Mwenyezi Mungu:

كَتَبَ رَبُّكُمْ عَلَىٰ نَفْسِهِ الرَّحْمَةَ ﴿٥٤﴾

Mola wenu amejilazimisha rehema. (6:54)

Miongoni mwa aliyoyasema Imam Ali(a.s) katika kuwasifu waumini:“Wao na pepo ni kama waliyoiona wakiwa ndani wananeemeshwa. Na wao na moto ni kama waliouona, wakiwa ndani wanaadhibiwa”

Anasema mshairi katika kuwasifu: Yalingana hofu na matarajio si kwa kuogopa wala tamanio

2.Na wanaposemewa Aya zake huwazidisha Imani.

Kwa sababu wao na dini yao ni kama vile wameiona ghaibu kwa macho. Bali wanaweza kutilia shaka wanaloliona kwa jicho. Kwa sababu macho mara nyingine hudanganya mtu akadhani mangati ni maji na uvimbe ni shahamu, Lakini kauli yake Mwenyezi Mungu haina shaka hata chembe.

DINI HAIOTESHI NGANO

3.Na wanamtegemea Mola wao.

Maana ya kutegemea sio tu kusema kwa midomo yetu: Tumemtegemea Mungu, pia sio kuacha visababishi na kuacha kufanya kazi kwa kutegemea mambo yaje yenyewe tu, na sisi tumekaa. Isipokuwa kutegemea ni kuhangaika, kama alivyotuamrisha Mwenyezi Mungu, tukitaraji tawfik kutoka kwake katika kuhangaika kwetu tukiamini kuwa kazi ni sharti la msingi la kutegemea. Na kwamba hiyo ni ibada, na kutii kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu:

فَامْشُوا فِي مَنَاكِبِهَا وَكُلُوا مِن رِّزْقِهِ ُ ﴿١٥﴾

Basi tembeeni katika pande zake zote na kuleni katika riziki zake. (67:15).

Hakika kuamini na kumtegemea Mwenyezi Mungu bila ya kazi hakuwezi kuotesha ngano wala kuponesha mgonjwa; vinginevyo Mwenyezi Mungu asingetuumbia mikono na miguu kwa ajili ya kufanya kazi.

Ndio! Dini ya kweli inaotesha upendo, ikhlas na msimamo, lakini sio mkate na dawa, hata elimu haitupatii chakula wala haitupozi magonjwa; isipokuwa inatufundisha jinsi ya kulima chakula na kutengeneza dawa; kisha haitushughulikii kuwa tutakufa na njaa na magonjwa au hatutakufa.

Dini inatuhimiza kushghulikia maisha yetu, Ndiyo maana inatuhimiza elimu na kufuata njia zake, na inazingatia kuwa kuipuuza ni kosa, kwani kutasababisha madhara na ufisadi.

Elimu nayo inapanga mkakati wa maisha mazuri. Na hayo ndiyo yanayolengwa na Uislamu. Kwa ajili hiyo Uislamu umeamrisha na kuhimiza elimu; sawa na Swaumu na Swala, na ataadhbiwa atakayeitumia elimu kwa unyang’anyi na uchokozi; kama ambavyo ataadhibiwa atakayeiharibu dini kwa manufaa yake ya kiutu.

Kwa ufupi ni kwamba, ikiwa ni sawa kuwa mtu hawezi kuishi kwa mkate peke yake, Vilevile hawezi kuishi kwa Swala peke yake.

4.Ambao wanasimamisha Swala. Na wanatoa katika yale tuliy- owaruzuku.

Sifa zilizotangulia ni za hali ya moyo, na Swala na Zaka ni katika vitendo vya mwili, vyote viwili ni natija ya kumwamini Mwenyezi Mungu na kumhofia na kumtegemea. Mwenye kuacha Swala hahisabiwi kuwa ni katika waumini wa kweli, na dalili ni kauli yake Mwenyezi Mungu:

Hao kweli ndio waumini, Wao wana vyeo kwa Mola wao, na maghufira na riziki bora.

Hao, ni ishara ya wale waliokusanya sifa tano; waumini wa kweli, ni wale ambao imani yao inaonekana katika vitendo vyao, si katika kauli zao tu. Vyeo mbele ya Mwenyezi Mungu vinatofautiana kufuatana na juhudi na kujitolea mhanga, mwenye cheo cha juu zaidi ni yule ambaye watu wamenufaika naye na akavumilia mengi ili waja wa Mwenyezi Mungu wote waishi katika kivuli cha amani na uadilifu. Maghufira ni kukiuka utelezi; na riziki bora ni pepo.

كَمَا أَخْرَجَكَ رَبُّكَ مِن بَيْتِكَ بِالْحَقِّ وَإِنَّ فَرِيقًا مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ لَكَارِهُونَ ﴿٥﴾

5. Kama alivyokutoa Mola wako nyumbani kwako kwa haki, na hakika kundi moja la waumini linachukia.

يُجَادِلُونَكَ فِي الْحَقِّ بَعْدَ مَا تَبَيَّنَ كَأَنَّمَا يُسَاقُونَ إِلَى الْمَوْتِ وَهُمْ يَنظُرُونَ ﴿٦﴾

6. Wanajadiliana nawe katika haki baada ya kubainika. Kama kwamba wanasukumwa katika mauti na huku wanaona.

وَإِذْ يَعِدُكُمُ اللَّـهُ إِحْدَى الطَّائِفَتَيْنِ أَنَّهَا لَكُمْ وَتَوَدُّونَ أَنَّ غَيْرَ ذَاتِ الشَّوْكَةِ تَكُونُ لَكُمْ وَيُرِيدُ اللَّـهُ أَن يُحِقَّ الْحَقَّ بِكَلِمَاتِهِ وَيَقْطَعَ دَابِرَ الْكَافِرِينَ ﴿٧﴾

7. Na alipowaahidi moja ya makundi mawili kuwa ni lenu. Nanyi mkapenda lile lisilo na nguvu ndio liwe lenu. Na Mwenyezi Mungu anataka kuihakikisha haki kwa maneno yake na kuikata mizizi ya makafiri.

لِيُحِقَّ الْحَقَّ وَيُبْطِلَ الْبَاطِلَ وَلَوْ كَرِهَ الْمُجْرِمُونَ ﴿٨﴾

8. Ili kuihakikisha haki na kuivunja batili; ijapokuwa watachukia wafanyao makosa.

KAMA ALIVYOKUTOA MOLA WAKO

Aya 5 – 8

KWENDA BADR

Mtume(s.a.w.w) alitumwa kufikisha ujumbe akiwa na umri wa miaka arubaini na akakaa Makka, miaka kumi na tatu, Kisha akahamia Madina ambako aliingia siku ya Jumatatu tarehe 12 Rabiul-Awwal (Mfungo sita).

Akaishi hapo kwa muda wa mika kumi, na kufariki Jumatatu, tarehe 12 Rabiul-Awwal akiwa na umri wa miaka Sitini na tatu[1] .

Alipotulia Madina akawa anatuma vikosi kwenye misafara ya washirikina kuchunguza habari zao na kuwashtua. Al-Mas’udi anasema: Vita alivyoviongoza Mtume mwenyewe ni 26, katika hivyo alipigana tisa.

Hapa tunaeleza kutoka kwake kwenda Baadr kwa sababu ni maudhiu ya Aya tulizo nazo sasa, vita hii ilidhihirisha mwanzo wa nguvu za waislamu dhidi ya washirikina ambao walikuwa wakiwanyanyasa na kuwaudhi waislamu zaidi ya miaka kumi na tatu, huku waislamu wakipata mateso hayo na maudhi kwa kuvumilia kwa kustahmili. Kwa sababu kushindana nao na udhaifu waliokuwa nao ni sawa na kujichinja.

Kwa ufupi kisa cha Badr ni kwamba Mtume(s.a.w.w) alisikia kuwa Abu Sufyan anarudi kutoka Sham na msafara ulio na mali nyingi. Katika jumla ya mali hizo ni zile walizozitaifisha kutoka kwa Muhajirin (Wahamiaji) walizoziacha Makka.

Basi Mtume akawakusanya maswahaba akawahimiza kutoka kuchukua mali za msafara. Baadhi wakaingia uvivu na kuchukia kutoka kwa kuhofia Maquraish. Kisha wakaenda pamoja na Mtume.

Hapo ilikuwa ni tarehe 17 Ramadhan mwaka wa pili wa Hijra. maswahaba walikuwa hawajui kuwa sasa wanakwenda kwenye mojawapo ya vita kuu ya waislamu na yenye athari kubwa katika maisha ya Kiislamu na waislamu.

Mayahudi wakamtuma mtu wa kumwonya Abu Sufyan akiwa njiani. Naye akatuma ujumbe kwa maquraish akiwataka waende wakawaokoe. Kukatokwa huko Makka, hakubaki hata mtu mmoja awezaye kushika silaha,Waislamu wakati huo bado wako njiani kuelekea Badr. Lakini Abu Sufyan akabadisha njia akapitia mwambao wa Bahari nyekundu.

Mtume alipopata habari hiyo akawashauri Maswahaba kuwa je, waaendelee na vita au watarudi Madina? Wakati huo huo akawaambia kuwa Mungu amewaahidi mojawapo ya makundi mawili kama wakienda kupigana.

Makundi mawili hayo, ni masfara uliobeba mali, na jeshi la maquraish waliotoka kuja kuhami mali. Wengi wakashauri kuendelea na vita, na baadhi wakachukia, kama walivyochukia tangu mwanzo.

Hatimaye wakaungana kuwakabili maquraish, Hapo Mtume(s.a.w.w) akawaambia: “Nendeni kwa baraka ya Mwenyezi Mungu. Wallah kana kwamba mimi ninaona vifo vya watu, basi jiandaeni na vita.”

Idadi ya maquraish walikuwa wapiganaji elfu moja wakiwemo wapanda farasi mia moja, Waislamu walikuwa mia tatu wakiwa na mpanda farasi mmoja tu, wengine wanasema walikuwa wawili. Wakawaua washirikina sabini na kuteka sabini waliobaki wakakimbia. Kwa upande wa Waislamu walikufa mashahidi watu 14 na hakuna aliyetekwa.

Vita hii ilikuwa ushindi wa kwanza wa waislamu uliobadilisha hali zao, na kupata watu wengi, wakawa wanakabili nguvu kwa nguvu na ukali kwa ukali sio tena kunyamaza au kukimbia nchi.

Baada ya utangullizi huuu, sasa tunaingilia kufasiri Aya:

MAANA

Kama alivyokutoa Mola wako nyumbani kwako kwa haki, na hakika kundi moja la Waumini linachukia.

Makusudio ya nyumba ni Madina. Wakati Mtume alipotaka kutoka Madina kwenda kuukamata msafara, baadhi ya jamaa walikuwa wazito na wakasema: “Hatuwawezi Maquraish.” Wakatoka kwa kuchukia pamoja na waliotoka kwa kupenda.

Huko njiani Mtume akawapa habari ya maquraish kuwa wanakuja kutoka Makka, Akawataka ushauri kuwa wataendelea na vita au watarudi Madina? Baadhi wakachukia na kusema kuwa sisi tumetoka kwa ajili ya msafara tu. Lakini wengi wakasema: “Tutakwenda nawe kupigana.” Kisha wakaenda wote kwa baraka ya Mwenyezi Mungu.

Aya hii inaashiria misismamo miwili ya baadhi ya Swahaba: Kuchukia kutoka Madina kwenda kwenye msafara na wapili ni kuchukia kuendelea na vita, baada ya kutoka kwa ajili ya msafara tu.

Hayo ndiyo maana ya Aya hiyo, yako wazi na hayana ugumu wowote. Lakini baadhi ya wafasiri wamedangana katika kuifasiri kwake, Mwenye Al-bahrul Muhit ametaja kauli kumi na tano.

Ajabu ni yale aliyoyasema mfasiri huyu katika Kitab kingine kwamba yeye ametaja kauli 15 katika Bahrul-muhit. Lakini hakukinaika na kitu chochote katika kauli hizo, mpaka akaota usingizini kwamba yeye anatembea kwenye njia iliyotandikwa mawe mapana akiwa na mtu mwingine akifanya naye utafiti kuhusu kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu: “Kama alivyokutoa Mola wako nyumbani kwako.”

Akamwambia: “Haujanipitia mushkeli katika Qur’an mfano wa huu.” Pengine kuna maneno yaliyokadiriwa yanayotengeneza maana ambayo hakuyaeleza mfasiri yeyote, Kisha nikamwambia yule mtu: “Nimejua sasa, kuwa yale maneno yaliyokadiriwa ni ‘Nusura yako.’

Ninachotaka kusema, sio kumdharau mfasiri huyu mkubwa; isipokuwa ninataka kutoa dalili kuwa hata ulamaa, mwenye akili, mara nyingine akili yake inafungika; mpaka akawa anafasiri Qur’an kwa ndoto, na yeye katika hali halisi yuko kwenye makosa naye hajijui, Ni ajabu, lakini ndivyo ilivyo. Dalili ya kuwa yeye yuko kwenye makosa ni kwamba lau ataona jengine, basi lile angelilipinga.

Wanajadiliana nawe katika haki baada ya kubainika.

Kundi moja la waumini walibishana katika kupigana na kikosi cha waliotoka Makka ingawaje kupigana huku ni haki na kheri. Wakaathirika na msafara wa ngamia, kwa vile ulikuwa na mali nyingi na watu wachache.

Kauli yake Mwenyezi Mungu: “Baada ya kubainika” inaashiria kwamba wao walibishana baada ya Mtume(s.a.w.w) kuwapa habari ya ushindi.

Kama kwamba wanasukumwa katika mauti na huku wanaona wazi sababu za mauti.

Hii ni Sura inayochorwa na Qur’an ya kuwogopa kwao Maquraish sana. Kwa sababu wamejiandaa kwa nguvu na wako wengi.

Utauliza : Waislamu wanawatukuza sana watu wa Badr na kuwaweka kwenye cheo cha juu; na hapa Qur’an inawadunisha waziwazi. Na kwamba wao walibishana na Mtume pamoja na kubainishiwa haki na kuwekewa wazi, kwa sababu wahyi umemshukia.

Jibu : Hili haliwagusi na wala haligusi imani yao kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Wao ni wanadamu, nafsi zao hutetema zionapo mauti japo wana imani na utulivu. Zaidi ya hivyo, hayo yalikuwa ni mawingu ya Kaskazi tu, yalifunga kisha yakaondoka. Wakaenda pamoja na Mtume wakayakabili mauti kwa azma na uthabiti.

Na alipowaahidi moja ya makundi mawili kuwa ni lenu.

Ama ushindi katika vita bila ya mali ya msafara; au mali ya msafara bila ushindi.

Nanyi mkapenda lile lisilo na nguvu ndio liwe lenu.

Lisilo na nguvu ni msafara wa mali zao, ambalo ndilo waliloathirika nalo kuliko jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Lakini Mwenyezi Mungu aliwatakia kheri wao na Uislamu kwa kuvunja ushirikina na utaghuti.

Na Mwenyezi Mungu anataka kuihakikisha haki kwa maneno yake na kuikata mizizi ya makafiri.

Makusudio ya haki hapa ni ushindi wa waislamu dhidi ya washirikina. Na makusudio ya maneno yake, kuwa ni ahadi yake kuwa mojawapo ya makundi mawili ni ya waislamu.

Maana ni kuwa: “Enyi waislamu! Nyinyi mmetaka mali inayokwisha, na Mwenyezi Mungu ametaka kuwanusuru juu ya mamwinyi wa Kiquraish, maadui wa Mweneyzi Mungu na maadui zenu; awaangamize kwa mikono yenu, aing’oe mizizi ya makafiri na ahakikishe ahadi yake kwa kuwanusuru. Basi ni nini bora katika haya? Utukufu huu, au ngamia na shehena zao?

Ili kuihakikisha haki na kuivunja batili; ijapokuwa watachukia wafanyao makosa.

Makusudio ya haki katika Aya iliyotangulia, ni ushindi wa waislamu dhidi ya washirikina. Na makusudio ya haki hapa ni Uislamu, na wenye makosa ni maadui wa Uislamu. Makusudio ya batili ni shirki.

Kuihakikisha haki na kuitangaza na kuidhihirisha kwa watu au kwa kuwanusuru watu wake, au yote mawili. Na kuivunja batili ni kwa kui- tangaza au kuwadhalilisha wabatilifu, au yote pamoja. Ufafanuzi zaidi wa tafsir ya Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu:

هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ ﴿٣٣﴾

“Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki ili ipate kushinda dini zote, ijapokuwa watachukia washirikina.” (9:33).

إِذْ تَسْتَغِيثُونَ رَبَّكُمْ فَاسْتَجَابَ لَكُمْ أَنِّي مُمِدُّكُم بِأَلْفٍ مِّنَ الْمَلَائِكَةِ مُرْدِفِينَ ﴿٩﴾

9. Mlipokuwa mkimwomba msaada Mola wenu. Naye akawajibu kuwa: Hakika mimi nitawasaidia kwa Malaika elfu moja wanaofuatana mfululizo.

وَمَا جَعَلَهُ اللَّـهُ إِلَّا بُشْرَىٰ وَلِتَطْمَئِنَّ بِهِ قُلُوبُكُمْ وَمَا النَّصْرُ إِلَّا مِنْ عِندِ اللَّـهِ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴿١٠﴾

10. Na Mwenyezi Mungu hakuyafanya haya ila ni bishara na ili nyoyo zenu zitue kwayo. Na hakuna msaada ila utokao kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu, mwenye hekima.

إِذْ يُغَشِّيكُمُ النُّعَاسَ أَمَنَةً مِّنْهُ وَيُنَزِّلُ عَلَيْكُم مِّنَ السَّمَاءِ مَاءً لِّيُطَهِّرَكُم بِهِ وَيُذْهِبَ عَنكُمْ رِجْزَ الشَّيْطَانِ وَلِيَرْبِطَ عَلَىٰ قُلُوبِكُمْ وَيُثَبِّتَ بِهِ الْأَقْدَامَ ﴿١١﴾

11. Alipowafunika kwa usingizi uliokuwa amani itokayo kwake, na akawateremshia maji kutoka mawinguni ili awatwaharishe kwayo, na kuwaondolea uchafu wa shetani na kuzikazanisha nyoyo zenu na kuimarisha nyayo zenu kwayo.

إِذْ يُوحِي رَبُّكَ إِلَى الْمَلَائِكَةِ أَنِّي مَعَكُمْ فَثَبِّتُوا الَّذِينَ آمَنُوا سَأُلْقِي فِي قُلُوبِ الَّذِينَ كَفَرُوا الرُّعْبَ فَاضْرِبُوا فَوْقَ الْأَعْنَاقِ وَاضْرِبُوا مِنْهُمْ كُلَّ بَنَانٍ ﴿١٢﴾

12. Mola wako alipowapa wahyi Malaika: Hakika mimi niko pamoja nanyi, basi watieni nguvu wale walioamini; nitatia woga katika nyoyo za makafiri, basi wapigeni juu ya shingo na wapigeni kwenye kila ncha za vidole.

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ شَاقُّوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَمَن يُشَاقِقِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَإِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ ﴿١٣﴾

13. Hayo ni kwa kuwa wamemwasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hakika Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.

ذَٰلِكُمْ فَذُوقُوهُ وَأَنَّ لِلْكَافِرِينَ عَذَابَ النَّارِ ﴿١٤﴾

14. Ndiyo hivyo! Basi onjeni! Na hakika makafiri wana adhabu ya moto.

MLIPOKUWA MKIMWOMBA MSAADA MOLA WENU

Aya 9 – 14

MAANA

Mlipokuwa mkimwomba msaada Mola wenu, Naye akawajibu kuwa: Hakika mimi nitawasaidia kwa Malaika elfu moja wanaofuatana mfululizo.

Waislamu walipohakikisha kwamba kupigana na adui mwenye nguvu na idadi kubwa ya wapiganaji, kutakuwa tu, basi walikimbilia kwa Mwenyezi Mungu wakitaka kuokoka na ugumu huu. Naye Mwenyezi Mungu alipoona ukweli wa nia na azma yao, aliwapa habari kupitia kwa Mtume wake(s.a.w.w) , kwamba yeye amewatikia dua yao kwa Malaika elfu moja wanaofuatana.

Utauliza : hapa Mwenyezi Mungu amesema: Nitawasaidia kwa Malaika elfu moja wanaofuatana, mahali pengine akasema: “Je, haiwatoshi kuwasaidia Mola wenu kwa Malaika elfu tatu wenye kuteremshwa?”

Tena akasema: “Atawasaidia Mola wenu kwa Malaika elfu tano wenye alama” Juz.4 (3:124-125).

Jibu la swali hili tumelijibu huko Juz,4 (3:124-125).

Na Mwenyezi Mungu hakuyafanya haya ila ni bishara na ili nyoyo zenu zitue kwayo. Na hakuna msaada ila utokao kwa Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hakima.

Mwenyezi Mungu anasema lengo la msaada huu ni kutua nyoyo zenu na mvumilie katika kupigana na adui sio, kutegemea Malaika. Bali ni juu yenu kumaliza juhudi zenu zote. Ama ushindi hauwi wala hautakuwa ila kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, si kwa juhudi zenu na wala kwa msaada wa Malaika. Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz.4. (3:126).

Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akataja njia sita za neema yake kwa Waislamu:

1.Alipowafunika usingizi uliokuwa amani itokayo kwake.

Waislamu waliwahofia Washirikina kwa wingi wao, Mwenyezi Mungu akaipoza hofu yao kwa usingizi; Hawakuamka ila nafsi zao zimejawa na uutulivu.

Sote tunajua, kwa majaribio, kwamba usingizi unapunguza sehemu ya huzuni na hofu. Imam Ali(a.s) anasema:“Ni kuvunja kulikoje kwa usingizi, kwa tatizo la siku.” Yaani mtu anaweza kufikiria tatizo fulani akilala, mpaka atakapoamka hulikuta limetatuka.

2.Na akawateremshia maji kutoka mawinguni ili awatwaharishe kwayo.

Baada ya waislamu kupumzika kwa usingizi walijikuta wana haja ya maji; Kwa sababu walikuwa hawajafika Badr wakati huo. Ndipo Mwenyezi Mungu akawateremshia mvua, wakanywa na wakajisafisha. Hii ni neema ya pili baada ya usingizi.

3.Na kuwaondolea uchafu wa shetani.

Shetani alikuwa akiwatia wasiwasi waislamu na kuwahofisha na washirikina. Mwenyezi Mungu akawaondolea hofu hii, ambayo ameiita uchafu wa shetani, kwa usingizi na kusaidiwa na Malaika.

4.Na kuzikazanisha nyoyo zenu kwa kuondoa hofu na fazaa.

5.Na kuimarisha nyayo zenu kwayo.

Wafasiri wengi wanasema kuwa dhamir ya kwayo inarudi kwenye maji, na nyayo ni miguu. Kwamba waislamu walikuwa katika tifu tifu, miguu yao haina uimara, mvua iliponyesha mchanga ukashikana na miguu ya waislamu ikawa imara.

Hayo ndiyo yalioelezwa katika tafsir nyingi, Ama sisi tunaona kuwa dhamir ya kwayo inarudia kwenye kukazana nyoyo, Kwamba makusudio ya kuimarika nyayo ni uimara katika uwanja wa vita, na kuacha kukimbia. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amewapa uimara katika uwanja wa vita kama alivyowapa utulivu na uimara wa moyo.

6.Mola wako alipowapa wahyi Malaika: Hakika mimi niko pamoja nanyi, basi watieni nguvu wale walioamini; nitatia woga katika nyoyo za makafiri.

Msemo katika ‘Mola wako’ unaelekezwa kwa Mtume Muhammad(s.a.w.w) na katika ‘pamoja nanyi’ na ‘watieni nguvu’ ni kwa Malaika. Hiyo ni kwa kuangalia dhahir ya mfumo wa maneno.

Utauliza : Malaika walishiriki kinamna gani katika kuwasaidia waislamu siku ya Badr? Je, ilikuwa ni kwa kupiga na kuua au ni kwa kushajiisha; kwamba wao walikuwa wanakwenda mbele ya safu kwa sura za watu wanaopigana na wala hawapigani, isipokuwa kuwaambia waislamu: Furahini, hakika Mwenyezi Mungu atawanusuru; kama walivyosema baadhi ya wafasiri?

Jibu : Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaamrisha Malaika kuwapa uimara waumini. Hakuna mwenye shaka kwamba wao walifanya, kwa sababu wao wanafanya yale wanayoamrishwa, Vilevile hakuna mwenye shaka kwamba washirikina waliwaogopa waislamu.

Kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwaahidi na ahadi yake ni kweli na kwamba waumini wali- washinda washirikina.

Haya ndiyo yanayofahamishwa na dhahiri ya Aya. Ama ufafanuzi na vipi walivyofanya, hayo ni katika mambo ya ghaibu yaliyonyamaziwa na wahyi. Na sisi ni bora kuyanyamazia.

Kunyamaza kwa wahyi ni dalili mkataa kwamba kuamini ufafanuzi si chochote katika itikadi, vinginevyo ingelikuwa wajibu kubainisha.

Basi wapigeni juu ya shingo na wapigeni kwenye kila ncha za vidole.

Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa msemo ‘Pigeni’ unaelekezwa kwa Malaika, Wengine wakasema wanaambiwa waislamu, Kisha wakatofautiana katika makusudio ya juu ya shingo.

Kuna waliosema makusudio ni shingo zenyewe na kwamba maana ya juu ni kwenye; na wengine wakasema ni vichwa. La kushangaza ni kauli ya baadhi ya masufi kwamba makusudio ni nafsi chafu.

Tuonavyoona sisi ni kwamba maneno hayo wanaambiwa waislamu, kwa sababu ndio waliokusudiwa kupigana. Na kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Juu ya shingo na kila ncha ya vidole’ ni fumbo la kuwahimiza waislamu kukazana kuwaua; wasiwape nafasi ila wawapige kiungo chochote katika viungo vyao.

Aya hii inafanana na Aya isemayo:

وَلَا تَأْخُذْكُم بِهِمَا رَأْفَةٌ فِي دِينِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ﴿٢﴾

“Wala isiwashike huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Mwenyezi Mungu ikiwa mnamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho” (24:2).

Hayo ni kwa kuwa wamemwasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hakika Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.

Hayo ni ishara ya ulazima wa kuwatumilia ukali washirikina, kwa vile wao wamekuwa katika msimamo wa upinzani na uhalifu.

Ndiyo hivyo! Basi onjeni! Na hakika makafiri wana adhabu ya moto mbali na yale yaliyowapata duniani, miongoni mwa kuuawa, kutekwa na kushindwa, na hayo si chochote kulinganisha na moto mkubwa.