TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI Juzuu 10

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 9975
Pakua: 1265

Maelezo zaidi:

Juzuu 10
Juzuu 1
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 13 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 9975 / Pakua: 1265
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI Juzuu 10

Mwandishi:
Swahili

4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI

Surah Ya Tisa: Suart At – Tawba.

Vile vile inaitwa Surat baraa na fadhiha, kwa vile inawafedhehi wanafiki. Aya zake ni 129. Imeshuka Madina.

Wameafikiana Masahaba na watalaamu wa kisomo cha Qur’an (qurrau) kutokuwa na Bismillahi mwanzo wake, kwa sababu ni Sura iliyoshuka kuondosha aibu na Bismillahi ni amani kutokana na Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu. Imesemekana kuwa hiyo na Sura Anfal (iliyotangulia) ni Sura moja.

بَرَاءَةٌ مِّنَ اللَّـهِ وَرَسُولِهِ إِلَى الَّذِينَ عَاهَدتُّم مِّنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿١﴾

1. (Tangazo la) Kujitoa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa wale mlioahidiana nao miongoni mwa washirikina.

فَسِيحُوا فِي الْأَرْضِ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَاعْلَمُوا أَنَّكُمْ غَيْرُ مُعْجِزِي اللَّـهِ وَأَنَّ اللَّـهَ مُخْزِي الْكَافِرِينَ ﴿٢﴾

2. Basi tembeeni katika nchi miezi minne; na jueni kwamba nyinyi hamuwezi kumshinda Mwenyezi Mungu, na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuwadhalilisha makafiri.

وَأَذَانٌ مِّنَ اللَّـهِ وَرَسُولِهِ إِلَى النَّاسِ يَوْمَ الْحَجِّ الْأَكْبَرِ أَنَّ اللَّـهَ بَرِيءٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ وَرَسُولُهُ فَإِن تُبْتُمْ فَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ وَإِن تَوَلَّيْتُمْ فَاعْلَمُوا أَنَّكُمْ غَيْرُ مُعْجِزِي اللَّـهِ وَبَشِّرِ الَّذِينَ كَفَرُوا بِعَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٣﴾

3. Na ni tangazo litakalo kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa watu siku ya Hijja kubwa ya kwamba Mwenyezi Mungu amejitoa na washirikina na pia Mtume wake. Basi kama mkitubu ndiyo heri kwenu, na kama mkikengeuka, basi jueni kwamba nyinyi hamuwezi kumshinda Mwenyezi Mungu na wabashirie waliokufuru adhabu iumizayo.

إِلَّا الَّذِينَ عَاهَدتُّم مِّنَ الْمُشْرِكِينَ ثُمَّ لَمْ يَنقُصُوكُمْ شَيْئًا وَلَمْ يُظَاهِرُوا عَلَيْكُمْ أَحَدًا فَأَتِمُّوا إِلَيْهِمْ عَهْدَهُمْ إِلَىٰ مُدَّتِهِمْ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُتَّقِينَ ﴿٤﴾

4. Ispokuwa wale mlioahidiana nao miongoni mwa washirikina kisha hawakuwapunguzia chochote wala hawakumsaidia yeyote juu yenu, basi watimizieni ahadi yao mpaka muda wao Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wenye takua.

KUJITOA

Aya 1-4

MAANA

Mwaka wa nane wa Hijra Mtume(s.a.w.w) aliiteka Makka, mwaka wa tisa ilishuka Sura hii, katika mwaka wa kumi Mtume alihiji hija ya mwisho, na katika mwaka wa kumi na moja akafariki. Kwa hiyo Sura hii siyo ya mwisho kushuka, lakini ni katika Sura za mwisho mwisho. Hivoyo imekusanya hukumu za mwisho za uhusiano wa waislamu na washirikina, Twaha Hussein anasema katika kitab Mir-atul-Islam.

“Waarabu walizidi kuukubali Uislamu baada ya Hijja aliyohiji Abu Bakr mwaka wa tisa. Katika Hijja hii alimtuma Ali amuwahi Abu Bakr na awasomee watu Qur’an. Ikawa ni upambanuzi wa zama mbili: Zama ambazo Uislamu ulikuwa unapata nguvu kidogo kidogo, huku ushirikina ukiwa umebaki katika baadhi ya makabila ya Kiarabu. Na zama ambazo bara ya Arabu yote ilikuwa na Uislamu.

Qur’an yenyewe - ambayo Ali aliwasomea watu na kutenganisha baina ya zama hizo mbili - ni Aya hizi tukufu za Sura ya baraa, akatangaza kujitoa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na washirikina, akawaharamisha, katika tangazo hilo, washirikina wasikurubie Ka’aba au kuipitia au kutufu uchi’.

(Tangazo la) Kujitoa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa wale mlioahidiana nao miongoni mwa washirikina.

Tumetangulia kueleza kuwa Sura hii ilishuka mwaka uliofuatia kutekwa Makka ambapo Uislamu ulikuwa na kuenea bara Arabu yote, lakini pamoja na hayo ushirikina ulikuwa umebakia vifuani mwa baadhi ya makabila ya Kiarabu ili vifua hivyo visiwe kikosi cha tano[3] katika jamii ya Kiislamu, Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake katika Sura hii kutangaza kujitoa katika dhima na washirikina.

Kwa ufasaha zaidi kumpa onyo la vita kila mshirikina anayekaa bara Arabu mpaka aseme: Lailaha Illa Llah na aingie waliyoingia wenzake.

Onyo hilo liliwahusu washirikina wote, hata wale waliowekeana mkataba wa amani na Mtume; isipokuwa katika hali moja tu ambayo Mwenyezi Mungu ameiashiria kwa kusema:

Ispokuwa wale mlioahidiana nao miongoni mwa washirikina kisha wasiwapunguzie chochote.

Tafsir yake inafuatia.

Basi tembeeni katika nchi miezi minne; na jueni kwamba nyinyi hamwezi kumshinda Mwenyezi Mungu, na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuwadhalilisha makafiri.

Yaani semeni: Enyi waislamu kuwaambia washirikina: Tembeeni katika nchi kwa usalama katika muda huu. Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwatangazia vita washirikina, aliwapa muda wa miezi minne wahame kwa amani waende watakako bila ya kuguswa na yeyote.

Wakisilimu baada ya hapo basi wamesalimika na kufuzu duniani na akhera. Wakiendelea na ushirikina basi malipo yao ni kuuawa katika dunia na adhabu kali katika Akhera na hawataweza kuheba hayo.

Utauliza : kupigana na washirikina mpaka watamke shahada, hakuafikiani na kauli ya Mwenyezi Mungu:

لَا إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ ﴿٢٥٦﴾

“Hakuna kulazimishwa katika dini” Juz.3 (2:256)

Pia hakuafikiana na kauli ya Mwenyezi Mungu:

أَفَأَنتَ تُكْرِهُ النَّاسَ حَتَّىٰ يَكُونُوا مُؤْمِنِينَ ﴿٩٩﴾

“Je, wewe utawalazimisha watu wawe waumini?”. (10:99)

Na Uislamu ni dini ya usalama si dini ya vita?

Jibu : ni kweli kuwa Uislamu hamlazimishi yeyote kutamka: Lailaha Illa Llah; isipokuwa unalingania kwa hekima, na dalili. Mwenyezi Mungu anasema:

وَقُلِ الْحَقُّ مِن رَّبِّكُمْ فَمَن شَاءَ فَلْيُؤْمِن وَمَن شَاءَ فَلْيَكْفُرْ ﴿٢٩﴾

“Na sema haki inatoka kwa Mola wenu basi atakaye aamini na atakaye akufuru” (18:29)

Lakini hutokea, katika hali maalum, haja ya kutokuwepo washirikina kwa sababu wao wanaeneza ufisadi katika ardhi. Katika hali hii inajuzu kwa kuwalazimisha washirikina watamke kalima ya shahada. Na, washirikina wa bara Arabu wakati huo walikuwa ni kikosi cha tano katika jamii ya kiislamu mpya.

Kwa ajili hiyo ndipo ikawa hukumu kwao ni kuuawa au kudhihirisha Uislamu na wawe na walionayo Waislamu. Kwa maneno mengine ni kwamba hukumu hiyo ilikuwa ni maalum kwa washirikina wa bara Arabu wakati huo tu, yametangulia maelezo kuhusu hayo katika Juz.3 (2:256)

Na ni tangazo litokalo kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa watu siku ya Hijja kubwa ya kwamba Mwenyezi Mungu amejitoa na washirikina na pia Mtume wake. Basi kama mkitubu ndiyo heri kwenu, na kama mkikengeuka, basi jueni kwamba nyinyi hamuwezi kumshinda Mwenyezi Mungu na wabashirie waliokufuru adhabu iumizayo.

Siku ya Hijja kubwa ni ile siku ya kuchinja (siku ya kumi ya Dhul-Hijja). Miezi minne ilianzia hapo, mnamo mwaka wa tisa wa Hijra na kumalizikia siku ya kumi, Rabiul-Akhar, mwaka wa kumi Hijra. Baada ya muda huo ndipo ikawa sasa washirikina wa bara Arabu wachague mawili. Kusilimu au kupigwa, kwa sababu ilikuwako haja ya kufanya hivyo kama tulivyoashiria.

Wafasiri, akiwemo Tabari, Razi na Abu Hayan Al-Andalusi, wamesema kwamba: iliposhuka Sura Tawba Mtume(s.a.w.w) alimwamrisha Ali awaendee watu kwenye msimu wa Hijja awasomee. Akaambiwa: kwa nini usimpe Abu Bakr, akasema: Hanitekelezei ila mtu anayetokana na mimi. Ali akasimama kwenye Jamratul-Aqaba siku ya kuchinja na kusema: “Enyi watu! Mimi ni mjumbe wa mjumbe wa Mwenyezi Mungu” Akawasomea Aya hizo.

Ispokuwa wale mlioahidiana nao miongoni mwa washirikina kisha hawakuwapunguzia chochote wala hawakumsaidia yeyote juu yenu, basi watimizieni ahadi yao mpaka muda wao.

Baada ya Mwenyezi Mungu kumwamrisha Mtume wake(s.a.w.w) kuwapa muda wa miezi minne washirikina; hata wale ambao walivunja ahadi na waislamu, aliwatoa katika washirikina wale waliokuwa na mkataba wa amani na waislamu na hawakuvunja mkataba huo.

Aliwatoa hawa na kuwapa muda wa miezi minne tu, bali aliwapa muda wao kadiri watakavyokuwa wanatekeleza mkataba wao. Wafasiri wengi wanasema kuwa washirikina hao waliotekeleza mkataba ni watu wa Kinana, na muda wao ulikuwa umebakia miezi tisa, Ndipo mtume akawatimizia muda wao.

Aya hii inafahamisha kwamba si wajibu kutekeleza mkataba ila ikiwa upande wa pili nao unatekeleza. Ukiharibu kipengele chochote, basi huhis- abiwa uhaini na uvunjaji ahadi. Wala hapana ahadi kwa anayevunja ahadi.

Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wenye takua ambao wanaogopa kuvunja ahadi na ufisadi mwengineo.

فَإِذَا انسَلَخَ الْأَشْهُرُ الْحُرُمُ فَاقْتُلُوا الْمُشْرِكِينَ حَيْثُ وَجَدتُّمُوهُمْ وَخُذُوهُمْ وَاحْصُرُوهُمْ وَاقْعُدُوا لَهُمْ كُلَّ مَرْصَدٍ فَإِن تَابُوا وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ فَخَلُّوا سَبِيلَهُمْ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٥﴾

5. Ikisha miezi mitukufu, basi waueni washirikina popote mtakapowakuta, na wakamateni na muwazingire na wakalieni katika kila njia. Lakini wakitubu na wakasimamisha swala na wakatoa zaka, basi iacheni njia yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

وَإِنْ أَحَدٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّىٰ يَسْمَعَ كَلَامَ اللَّـهِ ثُمَّ أَبْلِغْهُ مَأْمَنَهُ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَّا يَعْلَمُونَ ﴿٦﴾

6. Na kama yeyote katika washirikina akikutaka hifadhi, basi mhifadhi apate kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu, kisha mfikishe mahali pake pa amani. Hayo ni kwa kuwa wao ni watu wasiojua.

كَيْفَ يَكُونُ لِلْمُشْرِكِينَ عَهْدٌ عِندَ اللَّـهِ وَعِندَ رَسُولِهِ إِلَّا الَّذِينَ عَاهَدتُّمْ عِندَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ فَمَا اسْتَقَامُوا لَكُمْ فَاسْتَقِيمُوا لَهُمْ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُتَّقِينَ ﴿٧﴾

7. Itakuwaje ahadi kwa washirikina mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya Mtume wake. Isipokuwa wale mlioahidiana kwenye msikiti mtakatifu. Basi maadamu wanakwenda na nyinyi sawa nanyi nendeni nao sawa, Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wenye takua.

كَيْفَ وَإِن يَظْهَرُوا عَلَيْكُمْ لَا يَرْقُبُوا فِيكُمْ إِلًّا وَلَا ذِمَّةً يُرْضُونَكُم بِأَفْوَاهِهِمْ وَتَأْبَىٰ قُلُوبُهُمْ وَأَكْثَرُهُمْ فَاسِقُونَ ﴿٨﴾

8. Itakuwaje! nao wakiwashinda hawaangalii kwenu ujirani wala ahadi. Wanawafurahisha kwa midomo yao tu, hali nyoyo zao zinakataa. Na wengi wao ni mafasiki.

MIEZI MITUKUFU IKIISHA

Aya 5-8

MAANA

Ikisha miezi mitukufu, basi waueni washirikina popote mtakapowakuta, na wakamateni na muwazingire na wakalieni katika kila njia.

Kuwakamata ni kuwachukua mateka. Kuwazingira, kuwafunga na kuwakalia kila njia ni kuwachunga katika kila njia wanayopita na kutowaacha wasichomeke.

Ama miezi mitukufu tumetaja katika Juz.2 (2:194) kwamba Mwenyezi Mungu ameharamisha kupigana katika miezi minne: Dhul-Qaada, Dhul- Hijja, Muharram na Rajab[4] .

Miezi hii siyo iliyo kusudiwa hapa; isipokuwa makusudio ya miezi mitukufu hapa ni miezi minne ambayo Mwenyezi Mungu aliharamisha ndani yake kupigana na washirikina wa Bara Arabu. Akawahalalishia ndani ya muda huu watembee kwa amani katika nchi, kuanzia tarehe 10, Dhul-Hijja 9 A.H mpaka tarehe 9 Rabiul- Akhar 10A.H.

Baada ya hapo aliamrisha kuwapiga washirikina na kuwateka na kuwafunga na kuwaandama popote watakapoelekea, ikiwa hawakusilimu au wahame kabla ya kwisha muda. Hiyo ni kwa ajili ya kuchelea shari yao na ufisadi wao.

Lakini wakitubu na wakasimamisha swala na wakatoa zaka, basi iacheni njia yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

Yaani wakisilimu kabla ya kwisha muda na wakaendeleza nembo za dini ambazo miongoni mwa zilizo muhimu ni kuswali na kutoa zaka, basi wao wako katika amani. Watakuwa kama waislamu wengine bila ya tofauti yeyote.

Na kama yeyote katika washirikina akikutaka hifadhi, basi mhifadhi apate kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu, kisha mfikishe mahali pake pa amani.

Yaani mshirikina yeyote ambaye inajuzu kumwua, akijitolea au kutaka hifadhi ya amani kwa waislamu basi wamhifadhi na kumpa amani ya nafsi yake na mali yake, na kumlingania kwenye Uislam kwa hikima na mawaidha mazuri.

Akikubali basi atachukuliwa kama waislamu wengine, na kama akikataa basi si halali kumuua na ni wajibu kwa waislamu kumfikisha mahali atakapo kuwa salama.

Hayo ni kwa kuwa wao ni watu wasiojua.

Hayo ni ishara ya kutoa hifadhi kwa mshirikina, kumwambia maneno ya Mwenyezi Mungu na kumfikisha mahali pa salama yake. Kusema kwake Mwenyezi Mungu: ‘Hayo ni kwa kuwa wao ni watu wasiojua’ ni kubainisha sababu ambayo ni kutojua wale washirikina wanaotaka hifadhi Uislamu na hakika yake.

Wametoa fat-wa mafaqih kwamba waislamu wawape amani washirikina kwa sharti ya kutokuweko uchafuzi wa amani, kwa yule mtaka hifadhi asiwe ni jasusi na wala jihadi isiyumbe kwa kumpa amani.

Itakuwaje ahadi kwa washirikina mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya Mtume wake.

Aya hii inakamilisha Aya ya kwanza na ya nne ya Sura hii. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewajibisha, katika Aya ya kwanza, kuvunja mkataba na washirikina waliofanya hiyana, Hawa ndio wanaokusudiwa hapa. Na amewajibisha, katika Aya ya nne, kutekeleza mkataba na washirikina wanaoheshimu mkataba bila ya kupunguza kitu, hao ndio wanaokusudiwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

Isipokuwa wale mlioahidiana kwenye msikiti mtakatifu. Basi maadamu wanakwenda na nyinyi sawa nanyi nendeni nao sawa, Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wenye takua.

Yaani bakieni nao na mkataba wa amani maadamu wao wamebaki hivyo. Kwa sababu Mwenyezi Mungu anawachukia watu wa hiyana na anawapenda wanaotekeleza wenye kumcha Mwenyezi Mungun (takua).

Kusema kwake kwenye msikiti mtakatifu, ni kuashiria mahali palipofanyi- ka mkataba wa amani na Bani Kinana. Kwani Mtume(s.a.w.w) aliwekeana nao mkataba aliopatana nao Hudaibiya karibu na Makka.

Itakuwaje! nao wakiwashinda hawaangalii kwenu ujirani wala ahadi. Wanawafurahisha kwa midomo yao tu, hali nyoyo zao zinakataa. Na wengi wao ni mafasiki.

Dhamir inawarudia wavunjaji mkataba, Amewataja, Mwenyezi Mungu, kwa mambo matatu mabaya:

1. Uovu, kwa sababu wao lau wangeliwashinda waislam wangewalifanya vya kuwafanya bila ya kuchunga ahadi wala ubinadamu.

2. Unafiki kwamba wao wanasema mdomoni yale yasiyokuwa nyoyoni mwao.

3. Ufasiki.

Sifa moja tu miongoni mwa sifa hizi tatu inawahukumu kuadhibiwa na kuwatoa katika haki zote za ubinadamu, sikwambii kuwatekelezea ahadi tena. Sasa itakuwaje wakisifika na zote tatu kwa pamoja!

Utauliza : makafiri wote ni mafasiki kwa sababu, ukafiri ni ufasiki na zaidi. Sasa vipi Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewatoa wengine kwa kauli yake. ‘Na wengi wao ni mafasiki?.

Jibu : maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu na wengi wao ni mafasiki ni kwamba makafiri wengi huendelea na ukafiri na ufasiki wao, wala hawatarajiwi kuongoka kwa hali yeyote.

Na wako wachache miongoni mwao wanaoacha upotevu wao, Kwa hiyo makusudio ya ufasiki hapo ni kuendelea na kutouacha. Aina ya ibara kama hii ni nyingi katika Qur’an.

اشْتَرَوْا بِآيَاتِ اللَّـهِ ثَمَنًا قَلِيلًا فَصَدُّوا عَن سَبِيلِهِ إِنَّهُمْ سَاءَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٩﴾

9. Wamenunua thamani ndogo kwa ishara za Mwenyezi Mungu, kwa hiyo wakazuilia na njia yake. Hakika ni mabaya waliyokuwa wakiyafanya.

لَا يَرْقُبُونَ فِي مُؤْمِنٍ إِلًّا وَلَا ذِمَّةً وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُعْتَدُونَ ﴿١٠﴾

10. Hawaangalii kwa Mumin ujirani wala ahadi; na hao ndio warukao mipaka.

فَإِن تَابُوا وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ فَإِخْوَانُكُمْ فِي الدِّينِ وَنُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ ﴿١١﴾

11. Kama wakitubu na wakasi- mamisha Swala na wakatoa Zaka, basi ni ndugu zenu katika dini na tunazifafanua Aya kwa watu wanaojua

وَإِن نَّكَثُوا أَيْمَانَهُم مِّن بَعْدِ عَهْدِهِمْ وَطَعَنُوا فِي دِينِكُمْ فَقَاتِلُوا أَئِمَّةَ الْكُفْرِ إِنَّهُمْ لَا أَيْمَانَ لَهُمْ لَعَلَّهُمْ يَنتَهُونَ ﴿١٢﴾

12. Na kama wakivunja viapo vyao baada ya kuahidi kwao na wakatukana dini yenu, basi piganeni na viongozi wa ukafiri, Hakika hao hawana viapo (vya maana), Ili wapate kukoma.

أَلَا تُقَاتِلُونَ قَوْمًا نَّكَثُوا أَيْمَانَهُمْ وَهَمُّوا بِإِخْرَاجِ الرَّسُولِ وَهُم بَدَءُوكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ أَتَخْشَوْنَهُمْ فَاللَّـهُ أَحَقُّ أَن تَخْشَوْهُ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٣﴾

13. Je, hamtapigana na watu waliovunja viapo vyao na wakawa na hamu ya kumtoa Mtume nao ndio waliowaanza mara ya kwanza? Je, mnawaogopa? Basi Mwenyezi Mungu anastahiki zaidi mumuogope ikiwa nyinyi ni waumin.

قَاتِلُوهُمْ يُعَذِّبْهُمُ اللَّـهُ بِأَيْدِيكُمْ وَيُخْزِهِمْ وَيَنصُرْكُمْ عَلَيْهِمْ وَيَشْفِ صُدُورَ قَوْمٍ مُّؤْمِنِينَ ﴿١٤﴾

14. Piganeni nao, Mwenyezi Mungu awaadhibu kwa mikono yenu, na awafedheheshe, na awanusuru muwashinde na avipoze vifua vya kaumu ya waumin.

وَيُذْهِبْ غَيْظَ قُلُوبِهِمْ وَيَتُوبُ اللَّـهُ عَلَىٰ مَن يَشَاءُ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿١٥﴾

15. Na aondoe hasira ya nyoyo zao Na Mwenyezi Mungu humkubalia toba amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni mjuzi, mwenye hekima.

WANAZIUZA AYA ZA MWENYEZI MUNGU

Aya 9-15

MAANA

Wamenunua thamani ndogo kwa ishara za Mwenyezi Mungu, kwa hiyo wakazuilia na njia yake. Hakika ni mabaya waliyokuwa wakiyafanya.

Dhamir inawarudia washirikina ambao Mwenyezi Mungu ameamrisha wauawe, Maana ni kuwa hawa wameupinga Uislam wakaupiga vita na kuzuilia watu nao, kwa kuhofia masilahi yao waliyoathirika nayo kuliko ishara za Mwenyezi Mungu na ubainifu wake uliowajia.

Aya hii sio kama inahusika na washirikina na watu wa Kitab tu, bali inawakusanya ambao wanaiharibu dini kwa ajili ya kuafiki matakwa ya wakoloni na wanyonyaji.

Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz. 4 (3:187).

Hawaangalii kwa Mumini ujirani wala ahadi; na hao ndio warukao mipaka.

Utauliza kuwa : Aya hii ni mfano wa Aya iliyotangulia (ya nane) kwa nini imerudiwa?

Jibu : Mwenyezi Mungu (s.w.t), katika Aya iliyotangulia, alikuwa akiwambia maswahaba wa Mtume(s.a.w.w) na kuwa lau washirikina watawashinda basi watafanya maajabu. Huenda hapo mtu akadhania kwamba washirikina wanadhamiria chuki na uadui kwa Mtume(s.a.w.w) na maswahaba tu.

Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akaondoa dhana hii kwamba uadui wa washirikina, kwa waislamu wakati huo ni uadui wa msingi wenyewe, sio uadui wa watu; ni uadui wa kufuru kwa imani na batili kwa haki:

وَمَا نَقَمُوا مِنْهُمْ إِلَّا أَن يُؤْمِنُوا بِاللَّـهِ الْعَزِيزِ الْحَمِيدِ ﴿٨﴾

“Nao hawakuwachukia ila ni kwa vile wamemwamini Mwenyezi Mungu mwenye nguvu mwenye kusifiwa”. (85:8)

Kama wakitubu na wakasimamisha Swala na wakatoa Zaka, basi ni ndugu zenu katika dini na tunazifafanua Aya kwa watu wanaojua.

Aya hii inaafikiana na Aya ya tano katika sharti (wakitubu na wakasimamisha Swala na wakatoa Zaka), lakini inatofautiana katika jawabu la sharti. Jawabu katika Aya iliyotangulia ni kuwachia njia na mambo yao na kutowataaradhi na chochote. Jawabu katika Aya hii ni kuwa ni ndugu zenu, yaani nyinyi na wao mkeo sawa katika haki, hakuna bwana wala mtumwa; mwenye kula au kuliwa; kama ilivyokuwa hali ya washirikina.

Kwa kutofautiana huko katika jawabu la sharti,kunafutika kukaririka, ingawaje kukaririka katika Qur’an sio jambo la nadra.

Na kama wakivunja viapo vyao baada ya kuahidi kwao na wakatukana dini yenu, basi piganeni na viongozi wa ukafiri, Hakika hao hawana viapo (vya maana), Ili wapate kukoma.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameleta ibara ya kupigana na makafiri kwa kusema ‘piganeni na viongozi wa makafiri,’ kwa vile wao ndio wanaowaon- goza kwenye vita na kuvunja ahadi, na wanatukana na kuwahimiza wafuasi wao wamtukane Mtume(s.a.w.w) na Qur’an.

Kauli yake Mwenyezi Mungu ‘ili wapate kukoma’ inaashiria makusudio ya kupigana, - Kuwazuia washirikina wasiendelee kupigana na waislam.

Je, hamtapigana na watu waliovunja viapo vyao na wakawa na hamu ya kumtoa Mtume nao ndio waliowaanza mara ya kwanza?

Maneno yanaelekezwa kwa waislamu na dhamir inawarudia makafiri wa Kiquraish, kwa sababu wao ndio waliomwahidi Mtume wa Mwenyezi Mungu kuacha kupigana miaka kumi, kuishi kwa amani makundi yote mawili na walioungana nao.

Hapo ilikuwa ni mwaka wa sita wa Hijra. Lakini hawakudumu na mkataba huo. Vile vile wao ndio waliodhamiria kumuua Mtume(s.a.w.w) mpaka akalazimika kuhama na ndio wao walioanza kupigana siku ya Badr.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwakumbusha waislam walivyofanya washirikina kuvunja ahadi na kumtoa Mtume na kuanza vita, aliwahimiza jihadi na kupigana, ambapo hakuna njia nyingine isiyokuwa hiyo.

Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawaondolea hofu waumini kwa kusema:

Je, mnawaogopa? Basi Mwenyezi Mungu anastahiki zaidi mumuogope ikiwa nyinyi ni waumin.

Kauli yake Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni waumini, inaashiria kwamba kumwogopa Mwenyezi Mungu kiuhakika hasa, hakuwi wala haku-takuwa ila kwa anayemwamini Mwenyezi Mungu kiuhakika hasa.

Ama mwenginewe, hamwogopi Mwenyezi Mungu hasa, ispkokuwa kumwogopa kwake ni kama njozi tu zinazopita.

Imam Ali anasema: “Kila hofu ina uthibitisho, isipokuwa kumhofia Mwenyezi Mungu, huko kuna ila”. Yaani Mtu kumwogopa asiyekuwa Mwenyezi Mungu ni jambo la uhakika, lakini kumhofia Mwenyezi Mungu hakuwi na uhakika halisi, isipokuwa ni njozi tu zinazoondoka kwa kitu kidogo.

Piganeni nao, Mwenyezi Mungu awaadhibu kwa mikono yenu, na awafedheheshe, na awanusuru muwashinde na avipoze vifua vya kaumu ya waumin na aondoe hasira ya nyoyo zao.

Sifa hizi zinanasibiana na ushindi wa kuiteka Makka. Kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwadhalilisha na kuwafedhehesha vigogo vya Maqureish na kuwapa ushindi waislamu na kuvipoza vifua vya waumini ambao walikandamizwa na waonevu wa Kiqureish kabla ya Hijra, na kuwepo aina kwa aina ya mateso.

Na Mwenyezi Mungu humkubalia toba amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni mjuzi, mwenye hekima.

Makka ulikuwa ndio makao makuu ya nchi ya Hijaz na kituo cha harakati zote katika Bara Arabu. Wakuu wake walikuwa wakimchomolea upanga wa dhulma na utisho kila mwenye kutaka kujiunga na Mtume Muhamad(s.a.w.w) .

Baada ya kutekwa, Makka ilikuwa chini ya kivuli cha Uislamu na wakasilimu wale mataghuti. Hata hivyo baadhi yao walisilimu kwa kupenda sio kwa kuhofia. Wakasilimu kidhati na kindani. Hawa ndio wale ambao Mwenyezi Mungu amewakubalia toba na atawalipa kwa ikhlasi yao na ukweli wa nia yao.

Baada ya hayo, hakika kila hukumu iliyofungamana na Aya hizi inahusika na washirikina wa Kiarabu wakati huo. Kwa sababu wao ndio waliomtoa Mtume(s.a.w.w) , wakampiga vita na wakaacha kuheshimu mkataba.

Lakini kwa kukadiria kwamba Aya hizo zinawajibisha jihadi dhidi ya washirikina kila mahali na kila wakati, basi jihadi hiyo haijuzu ila kwa uongozi wa dola ya Kiislamu kwa kuongozwa na Maasum au naibu wake.

Yuko wapi huyo hivi sasa? Amedai hayo mwenye kudai, akaanzisha chama kwa ajili kwa uongozi wake, kisha akabainika kuwa ni kibaraka, wakamuepuka wale aliowahadaa waliokuwa wameghafilika na wala hajulikani alipo mpaka sasa.

Hata hivyo, jihadi ya mtu kulinda uhuru wake, mali yake na nchi yake haingoji kupatikana dola ya Kiislam wala haihitaji idhini ya maasum au asiyekuwa maasum.

Kwa sababu kulinda nafsi na nchi na kuwapiga wakoloni wanyonaji ni haki inayotukuzwa na sharia zote na kanuni zote. Tumeyaeleza katika kufasiri Juz.1 (2:19-193) Juz.4 (3:95) na katika Juzuu hii tuliyonayo sura (8:47).