TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI Juzuu 10

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 9961
Pakua: 1258

Maelezo zaidi:

Juzuu 10
Juzuu 1
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 13 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 9961 / Pakua: 1258
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI Juzuu 10

Mwandishi:
Swahili

8

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI

وَمِنْهُم مَّن يَقُولُ ائْذَن لِّي وَلَا تَفْتِنِّي أَلَا فِي الْفِتْنَةِ سَقَطُوا وَإِنَّ جَهَنَّمَ لَمُحِيطَةٌ بِالْكَافِرِينَ ﴿٤٩﴾

49. Na miongoni mwao kuna anayesema: Niruhusu wala usinitie katika fitina, Hakika wamekwishatumbukia katika fitina, Na hakika Jahannam imewazunguka makafiri.

إِن تُصِبْكَ حَسَنَةٌ تَسُؤْهُمْ وَإِن تُصِبْكَ مُصِيبَةٌ يَقُولُوا قَدْ أَخَذْنَا أَمْرَنَا مِن قَبْلُ وَيَتَوَلَّوا وَّهُمْ فَرِحُونَ ﴿٥٠﴾

50. Ukikupata wema unawachukiza, Na ukikusibu msiba husema: Tuliangalia vizuri mambo yetu tangu mwanzo na hugeuka kwenda zo wakiwa wamefurahi.

قُل لَّن يُصِيبَنَا إِلَّا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَنَا هُوَ مَوْلَانَا وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ ﴿٥١﴾

51. Sema halitatusibu ila alilotuandikia Mwenyezi Mungu. Yeye ni Mola wetu, basi waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu.

قُلْ هَلْ تَرَبَّصُونَ بِنَا إِلَّا إِحْدَى الْحُسْنَيَيْنِ وَنَحْنُ نَتَرَبَّصُ بِكُمْ أَن يُصِيبَكُمُ اللَّـهُ بِعَذَابٍ مِّنْ عِندِهِ أَوْ بِأَيْدِينَا فَتَرَبَّصُوا إِنَّا مَعَكُم مُّتَرَبِّصُونَ ﴿٥٢﴾

52. Sema: Nyinyi hamtutazami ila moja ya mema mawili Na sisi tunawatizamia kuwa Mwenyezi Mungu awafikishie adhabu itokayo kwake au kwa mikono yetu, Basi ngojeni nasi tunangoja pamoja nanyi.

NA MIONGONI MWAO KUNA ANAYESEMA: NIRUHUSU

Aya 49 – 52

MAANA

Na miongoni mwao kuna anayesema: Niruhusu wala usinitie katika fitina.

Wamekubaliana wafasiri kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alipotoa mwito wa kwenda kwenye vita vya Tabuk, Jad bin Qays, aliyekuwa ni katika wakuu wa kinafiki, alisema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ni ruhusu, kwa vile mimi ni mtu ninayependa wanawake, ninaogopa nikawaona wanawake wa Kirumi nitafitinika nao”, ndipo akashuka Aya hiyo. Mnaafiki huyu alidai kuwa anahofia dhambi kwa wanawake kama atapigana pamoja na Mtume(s.a.w.w) , lakini asiogope kuingia katika ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Hakika wamekwishatumbukia katika fitina.

Yaani walidai kukimbia dhambi na wakaingia katika dhambi waliyoikimbia au zaidi yake.

Na hakika Jahannam imewazunguka makafiri katika pande zote wala hawatapa kimbilio.

Mtume aliwapa mwito wa kujitakasha kwa kutubia dhambi zao ambazo zimewazunguka kila upande, lakini wakakataa mwito wake, ndipo ikawazunguka adhabu kila upande.

Ukikupata wema unawachukiza.

Kama ilivyo kawaida ya mtu mbaya, huchukia sana watu wema wanapopata yanayowapendeza; na hufurahi sana wanapopatwa na yanayowachukiza.

Na ukikusibu msiba husema: Tuliangalia vizuri mambo yetu tangu mwanzo, na hugeuka kwenda zao wakiwa wamefurahi.

Mfumo unafahamisha kwamba makusudio ya msiba ni kuvunjika jeshi la waislamu. Kwa sababu kusema kwao: ‘Tuliangalia vizuri mambo yetu,’ maana yake ni kuwa waislamu walipokuwa wakipata machukivu, basi wanafiki walikuwa wakizungumziana kwa furaha na kuambiana kuwa sisi tulichukua tahadhari, umetangulia mfano wa hayo katika Juz. 4 (3: 120) na Juzuu hii (8:49).

Sema: halitatusibu ila alilotuandikia Mwenyezi Mungu.

Yaani sema ewe Mtume kuwaambia wanafiki, Sisi ndio ambao tumezinduka na kuchukua tahadhari, sio nyinyi kwa sababu nyinyi mmekaa tu, na sisi tumepigana jihad baada ya kujiandaa; na tumepitia desturi ya Mwenyezi Mungu katika vita, kuna siku yetu na siku yao, mapambano bado yanaendelea, mambo huangaliwa mwisho wake, ushindi ni wetu mwishoni na kila lijalo likaribu.

Yeye ni Mola wetu, basi waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu.

Ambao wanajiandaa kisha wakaendelea kwa jina la Mwenyezi Mungu. Wakipatwa na vizuri husema: Hii ni katika fadhila za Mwenyezi Mungu na rehema yake, na wakipatwa na msiba husema hiyo ni kudura ya Mwenyezi Mungu; wakiwa katika hali ya ikhlas na yakini ya dini yao; na kwamba Mwenyezi Mungu ataidhihirisha kuliko dini zote wajapochukia makafiri.

Sema: Nyinyi hamtutazami ila moja ya mema mawili, ambayo ni ushindi au kufa shahidi.

Katika ushindi kuna kuwadhalilisha makafiri na wanafiki; na katika shahada kuna thawabu kubwa. Yote mawili ni utukufu na heshima.

Na sisi tunawatizamia kuwa Mwenyezi Mungu awafikishie adhabu itokayo kwake au kwa mikono yetu, Basi ngojeni nasi tunangoja pamoja nanyi.

Kwa vyovyote mwisho wa wanaopigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu ni moja ya mambo mawili mazuri: ushindi au kufa shahidi.

Na, mwisho wa wanafiki na makafiri ni moja ya maovu mawili: Ama adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu au kupigwa na waumini wanapopata idhini ya Mwenyezi Mungu.

قُلْ أَنفِقُوا طَوْعًا أَوْ كَرْهًا لَّن يُتَقَبَّلَ مِنكُمْ إِنَّكُمْ كُنتُمْ قَوْمًا فَاسِقِينَ ﴿٥٣﴾

53. Sema: toeni kwa kupenda au kuchukia haitakubaliwa kwenu, Hakika nyinyi mmekua watu mafasiki.

وَمَا مَنَعَهُمْ أَن تُقْبَلَ مِنْهُمْ نَفَقَاتُهُمْ إِلَّا أَنَّهُمْ كَفَرُوا بِاللَّـهِ وَبِرَسُولِهِ وَلَا يَأْتُونَ الصَّلَاةَ إِلَّا وَهُمْ كُسَالَىٰ وَلَا يُنفِقُونَ إِلَّا وَهُمْ كَارِهُونَ ﴿٥٤﴾

54. Na hawakuzuiliwa kukubaliwa michango yao, ila ni kwamba wao wamemkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Wala hawaiendei swala ila katika hali ya uvivu, wala hawatoi ila kwa kuchukia.

فَلَا تُعْجِبْكَ أَمْوَالُهُمْ وَلَا أَوْلَادُهُمْ إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُعَذِّبَهُم بِهَا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَتَزْهَقَ أَنفُسُهُمْ وَهُمْ كَافِرُونَ ﴿٥٥﴾

55. Basi zisikushangaze mali zao wala watoto wao, Hakika Mwenyezi Mungu anataka tu kuwaadhibu kwayo katika maisha ya dunia. Na roho zao zitoke na hali wao ni makafiri.

وَيَحْلِفُونَ بِاللَّـهِ إِنَّهُمْ لَمِنكُمْ وَمَا هُم مِّنكُمْ وَلَـٰكِنَّهُمْ قَوْمٌ يَفْرَقُونَ ﴿٥٦﴾

56. Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba wao ni katika nyinyi, na wala wao si katika nyinyi. Lakini wao ni watu wanaogopa.

لَوْ يَجِدُونَ مَلْجَأً أَوْ مَغَارَاتٍ أَوْ مُدَّخَلًا لَّوَلَّوْا إِلَيْهِ وَهُمْ يَجْمَحُونَ ﴿٥٧﴾

57. Lau wangelipata pa kukimbilia au mapango au mahali pa kuingia wangeligeukia huko kwa kasi sana.

SADAKA ZA WANAFIKI

Aya 53 – 57

MAANA

Sema: toeni kwa kupenda au kuchukia haitakubaliwa kwenu.

Baada ya Mtume(s.a.w.w) kujiandaa kwa vita vya Tabuk, mnafiki mmoja alimtaka amruhusu asiende kwenye jihadi, akatoa kitu kidogo katika mali yake.

Mwenyezi Mungu akamwamuru Mtume wake amwambie mnafiki huyu na mfano wake kuwa Mwenyezi Mungu haana haja na mali zenu na zichukueni wenyewe, hata kama mmetoa kwa kupenda au kutopenda.

Utauliza : Tunajua njia ya kukataa ikiwa kutoa ni kwa kutopenda; sasa kuna wajihi gani wa kukataa ikiwa kutoa ni kwa kupenda?

Jibu : Wao hawakutaka kutoa kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, isipokuwa walitaka umashuhuri na jaha. Hakuna tofauti kati ya kutoa kwa lengo hili na kutoa kwa kutopenda kwa kuhofia kutojulikana hakika yao – yote mawili ni kwa ajili ya asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Kwa ajili hii ndipo Mwenyezi Mungu akawaambia:

Hakika nyinyi mmekua watu mafasiki.

Na,kuwaita mafasiki kunaashiria kuwa ufasiki ndio sababu ya kutokubaliwa.

Na hawakuzuiliwa kukubaliwa michango yao, ila ni kwamba wao wamemkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake,

Wanafiki walitoa mali zao ili tu waambiwe kuwa nao wametoa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na huku wanamkanusha. Na, unafiki huu na ria hii ndio sababu ya kutokubaliwa wanachokitoa.

Lau wangelitoa kwa ubinadamu tu, kama vile mlahidi anapomlisha mwenye njaa, ingeliweza kusemwa: ‘Hakuna malipo ya hisani ila hisani.’ Lakini unafiki ni uovu; na mwenye kufanya uovu atalipwa Kwa maelezo zaidi angalia Juz.4 (3:177) Kifungu cha ‘Kafiri na amali ya Kheri’

Wala hawaiendei swala ila katika hali ya uvivu, wala hawatoi ila kwa kuchukia.

Hali hiyo ndiyo natija ya ukafiri kwa sababu kuswali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kutoa kwa ajili yake ni matawi ya imani.

Basi zisikushangaze mali zao wala watoto wao, Hakika Mwenyezi Mungu anataka tu kuwaadhibu kwayo katika maisha ya dunia.

Unaweza kuuliza kuwa: mali na watoto inaweza kuwa ni sababu ya adhabu ya Akhera, ambapo watu wengi, siku za shida wamewahi kuahidi wema, lakini wanapojiwa na fadhila za Mwenyezi Mungu hupetuka mpaka na kufanya uovu; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

كَلَّا إِنَّ الْإِنسَانَ لَيَطْغَىٰ ﴿٦﴾ أَن رَّآهُ اسْتَغْنَىٰ ﴿٧﴾

“Hakika binadamu hupetuka mpaka kwakujiona ametajirika” (96:6-7)

Na akasema:

وَاعْلَمُوا أَنَّمَا أَمْوَالُكُمْ وَأَوْلَادُكُمْ فِتْنَةٌ ﴿٢٨﴾

“Na jueni kwamba mali zenu na watoto wenu ni fitna” Juz.9 (8:28)

Lakini kuwa mali na watoto ni sababu ya adhabu katika dunia, hilo ni kinyume; hasa mali iliyotafutwa chini ya ardhi na ndani ya bahari na wa kati ambapo teknolojia imeendelea kufikia kuitafuta mwezini na kwengineko. Zaidi ya hayo, kauli hii haiafikiani na kauli isemayo:

الْمَالُ وَالْبَنُونَ زِينَةُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ﴿٤٦﴾

“Mali na watoto ni pambo la maisha ya dunia” (18:46)

Na kama itakuwa mali ni sababu ya adhabu katika maisha haya, basi adhabu haitahusika na wanafiki tu, bali itawaenea watu wote” Sasa itakuwaje?

Jibu : Ni kweli huu ni mushkel, lakini ikiwa Aya inawahusu wote. Ama ikiwa inakusudia tukio maalum, basi hakutakuwa na mushkeli wowote.

Mfumo wa maneno ulio kabla ya Aya hii na iliyo baada yake, unafahamisha waziwazi kwamba dhamiri katika ‘Anataka kuwadhibu”, inarudia kuhusisha wanafiki waliokuwa wakati wa Mtume na kuwahusu hasa wale waliojitoa katika vita vya Tabuk ambao walikuwa kiasi watu themanini na kitu, kama ilivyosemekana, na walikuwemo wenye mali nyingi na watoto wengi.

Ili isisemwe kuwa vipi watu hawa ni wafasiki na Mwenyezi Mungu amewaneemesha kwa mali na watoto. Ndipo Mwenyezi Mungu akasema: “Hakika tu Mwenyezi Mungu anataka kuwaadhibu kwayo katika maisha ya dunia”.

Na, kweli Mwenyezi Mungu aliwaadhibu kwa watoto wao. Kwani watoto wao walikubali Uislam na wakawa na ikhlasi, kinyume na mababa zao. Hakuna hasara mbaya kwa mzazi kuliko kuwa mwanawe ana dini nyingine na itikadi nyingine. Mwana wa Abdallah bin Ubayya, alisilimu na kupendekeza kwa Mtume(s.a.w.w) amuue baba yake, mkuu wa wanafiki, lakini Mtume akakataa.

Vile vile aliwaadhibu kwa mali zao, kwa vile wao walikuwa na yakini kuwa itawageukia wale ambao hawako katika dini yao na njia yao.

Kwa hiyo Aya inahusika na wanafiki waliokuwa katika zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) . Na kwa hali hiyo basi hakuna wajihi wowote kwa waliyoyataja wafasiri, kwamba kuadhibiwa na Mwenyezi Mungu kwa mali zao ni kutabika kuitafuta, na kwamba kuadhibiwa kwa wototo wao ni kuona uchungu wakiugua na wakiwakosa. Kwani tabu hiyo na machungu hayo hayahusiki na wanafiki peke yao, bali ni kila mwenye mali na familia.

Na roho zao zitoke na hali wao ni makafiri.

Yaani watakufa wakiwa makafiri na Mwenyezi Mungu atawaadhibu kwa kufuru yao huko Akhera, kama alivyowaadhibu kwa mali zao katika dunia.

Tabrasi katika Majmaul-bayan anasema: “Matakwa ya Mwenyezi Mungu yamefungamana na kutoka roho zao sio ukafiri wao; kama kusema: Nataka kumpiga akiwa asi, Hapa kutaka kumefungamana na kupiga sio kuasi.”

Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba wao ni katika nyinyi, na wala wao si katika nyinyi.

Kuna faida gani ya kiapo hiki na Mwenyezi Mungu ameshuhudia kwamba wao wamesilimu kwa kuhofia, sio kwa kukinai.

Lakini wao ni watu wanaogopa.

Nyoyo za wanafiki zilijazwa na hofu kwa nguvu ya waislamu

Lau wangelipata pa kukimbilia au mapango au mahali pa kuingia wangeligeukia huko kwa kasi sana.

Yaani wangelikimbilia huko kwa kasi sana. Wanafiki hawakuweza kutoka Madina, pia hawakuthubutu kudhihirisha ukafiri kwa vile Uislamu ulikuwa umeingia katika kila nyumba ya Aus na Khazraj. Kwa hiyo wakalazimika kusilimu kwa ncha za ndimi zao wakiwa ni makafiri nyoyoni wakingoja fursa ya kuufanyia vitimbi Uislamu.

وَمِنْهُم مَّن يَلْمِزُكَ فِي الصَّدَقَاتِ فَإِنْ أُعْطُوا مِنْهَا رَضُوا وَإِن لَّمْ يُعْطَوْا مِنْهَا إِذَا هُمْ يَسْخَطُونَ ﴿٥٨﴾

58. Na miongoni mwao wako wanao kulaumu katika sadaka, Na wanapopewa katika hizo huridhika, na wasipopewa katika hizo huchukia.

وَلَوْ أَنَّهُمْ رَضُوا مَا آتَاهُمُ اللَّـهُ وَرَسُولُهُ وَقَالُوا حَسْبُنَا اللَّـهُ سَيُؤْتِينَا اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ وَرَسُولُهُ إِنَّا إِلَى اللَّـهِ رَاغِبُونَ ﴿٥٩﴾

59. Na lau wangeliridhia kile alichowapa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosheleza, Mwenyezi Mungu atatupa katika fadhila zake, na Mtume wake; hakika sisi ni wenye kumtaka Mwenyezi Mungu.

WANAPOPEWA HURIDHIA

Aya 58 – 59

MAANA

Na miongoni mwao wako wanao kulaumu katika sadaka.

Dhamir ya miongoni mwao inawarudia wanafiki, Maana ni kuwa baadhi ya wanafiki walikuwa wakimsema Mtume(s.a.w.w) na kumtia ila katika kugawa kwa kudai kuwa anapendelea.

Katika Tafsir Tabari imepokewa kutoka, kwa Said Al-Khudri, amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alipokuwa akigawa mafungu, alijiwa na Ibn Dhulkhuwayswara Tamimi, akasema: Fanya uadilifu ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mtume akasema: Ole wako! Ninani atafanya uadilifu ikiwa mimi sikufanya? Umar akasema: Niruhusu ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu nikate shingo yake. Mtume(s.a.w.w) akasema: Mwache yeye ana wenzake ambao mmoja wenu atadharau kuswali nao na kufunga nao, watachomoka katika dini kama unavyochomoka mshale kwenye upinde; alama yao ni mtu mweusi[10] , moja ya mikono yake ni kama titi la mwanamke” Ndipo ikashuka: ‘Na miongoni mwao wako wanao kulaumu katika sadaka’.

Anaendelea kusema Abu Said: Ninashuhudia kuwa mtume alisema haya na nashuhudia kuwa alipouawa Ali (rehema za Mwenyezi Mungu ziwe kwake) aliletwa mtu aliyekuwa na sifa hizo”

Na wanapopewa katika hizo huridhika, na wasipopewa katika hizo huchukia.

Mtume alikuwa akigawanya sadaka, kama alivyobainisha Mwenyezi Mungu. Waumin walikuwa wakiridhia na wanafiki wakichukia na kumlaumu katika kugawanya kwake.

Aya inamchanganya kila asiyeridhia fungu lake. Lau watu wote wangeliridhia wanayostahiki, watu wote wangeliishi katika amani na raha.

Na lau wangeliridhia kile alichowapa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosheleza, Mwenyezi Mungu atatupa katika fadhila zake, na Mtume wake; hakika sisi ni wenye kumtaka Mwenyezi Mungu kututoshea na sadaka na mengineyo ya kuwahitajia watu.

Aya hii inahimiza mtu kujizuilia na vilivyo mikononi mwa watu, kumtege- mea Mwenyezi Mungu na kula jasho lake.

Imam AIi(a.s) anasema:“Utajiri mkubwa ni kutokuwa na tamaa na vilvyo mikononi mwa watu” .

Sijui kama kuna anayestahiki kudharauliwa kuliko yule anayetarajia watu na huku anaweza kujitosha nao japo kwa subira.

إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَابْنِ السَّبِيلِ فَرِيضَةً مِّنَ اللَّـهِ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿٦٠﴾

60. Hakika sadaka ni ya (hawa) tu: Mafukara na masikini na wanaozitumikia na wanaotiwa nguvu nyoyo zao Na kuwakomboa watumwa na wenye madeni na katika njia ya Mwenyezi Mungu na mwana njia. Ni faradhi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kujua mwenye hekima.

WANASTAHIKI ZAKA

Aya 60

MAANA

Makusudio ya sadaka hapa ni zaka ya wajibu. Mafakihi wameizungumzia zaka, hukumu zake, sharti zake, vitu ambavyo ni wajibu vitolewe zaka na wenye kustahiki kupewa. Sisi tumezungumzia kwa ufafanuzi katika Kitab Fiqhul-Imam Jaffer Assadiq Juz: 2. Katika Juz: 3 (2:272) tumeizungumzia zaka kama msimamo uliothibitishwa na Uislamu.

Hapa tutazungumzia aina nane za wanaostahiki kupewa zaka kulingana na Aya tukufu:

1.Hakika Sadaka Ni Ya(Hawa) Tu. Mafukara.

Shia Imamia wanasema: Fukara wa kisharia ni yule asiyemiliki gharama yake ya mwaka na ya watoto wake. Hanafi wanasema ni yule anayemiliki chini ya kiwango cha zaka. Shafii na Hambal wanasema mwenye kupata nusu ya mahitaji yake hahisabiwi kuwa fukara. Shia Imamia, Shafii na Hambal wanasema: Mwenye kuweza kuchuma si halali kwake zaka, lakini Hanafi na Malik wamesema ni halali.

2.Na Masikini.

Wamesema jamaa, kuwa neno fukara na maskini yakiwa pamoja kila moja linakuwa na maana nyingine; na yakiwa mbali mbali basi yanakuwa na maana moja. Wakasema tofauti ni kuwa fukara haombi na maskini huomba. Vyovyote iwavyo la kuzingatia ni haja, na wote ni wahitaji.

3.Na Wanaozitumikia.

Ni wale wanaokusanya zaka, waliowekwa na Imam au naibu wake, kusimamia kukusanya zaka na kuihifadhi; kisha kuitoa kwa atakayeigawanya kwa anayestahiki. Kile wakichukuacho wakusanyaji kinazingatiwa kuwa ni malipo ya kazi yao, sio sadaka. Kwa hiyo wanapewa hata kama ni matajiri.

4.Na Wanaotowa Nguvuu Nyoyo Zao.

Ni wale wanaovutiwa kwenye Uislamu au wanatakiwa msaada na Waislamu kwa manufaa ya Uislamu.

5.Na Kuwakomboa Watumwa.

Yaani inatolewa zaka kwa ajili ya kuwakomboa watumwa wawe huru. Mambo haya hayako siku hizi.

6.Na Wenye Madeni.

Ni wale walio na madeni yanayowashinda kuyalipa watapewa zaka, kwa sharti yakuwa wawe hawakutumia madeni hayo katika dhambi.

7.Na Katika Njia Ya Mwenyezi Mungu.

Njia ya Mwenyezi Mungu ni kila analoliridhia ambalo hutakiwa kujikurubisha kwake, kwa namna yoyote itakavyo kuwa, kama vile kutegeneza njia, kujenga zahanati au vyuo. Bora zaidi ni kutoa katika kupigania dini na nchi.

8.Na Mwana Njia.

Huyo ni msafiri aliyeishiwa njiani, atapewa kiasi kitakachomfikisha kwao; hata kama ni tajiri, kwa sharti ya kuwa safari yake isiwe ya maasi.