TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI Juzuu 10

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 9966
Pakua: 1263

Maelezo zaidi:

Juzuu 10
Juzuu 1
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 13 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 9966 / Pakua: 1263
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI Juzuu 10

Mwandishi:
Swahili

9

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI

وَمِنْهُمُ الَّذِينَ يُؤْذُونَ النَّبِيَّ وَيَقُولُونَ هُوَ أُذُنٌ قُلْ أُذُنُ خَيْرٍ لَّكُمْ يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ وَيُؤْمِنُ لِلْمُؤْمِنِينَ وَرَحْمَةٌ لِّلَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَالَّذِينَ يُؤْذُونَ رَسُولَ اللَّـهِ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٦١﴾

61. Na miongoni mwao wako wanaomuudhi Mtume na kusema: Yeye ni sikio tu. Sema: ni sikio la heri kwenu. Anamwamini Mwenyezi Mungu na ana imani na waumini. Na ni rehema kwa wale wanaoamini miongoni mwenu. Na wale wanaomuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu wana adhabu iumizayo.

يَحْلِفُونَ بِاللَّـهِ لَكُمْ لِيُرْضُوكُمْ وَاللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَحَقُّ أَن يُرْضُوهُ إِن كَانُوا مُؤْمِنِينَ ﴿٦٢﴾

62. Wanawaapia Mwenyezi Mungu ili wawaridhishe na hali Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ndiye mwenye haki zaidi ya kumridhisha, ikiwa wao ni waumini.

أَلَمْ يَعْلَمُوا أَنَّهُ مَن يُحَادِدِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَأَنَّ لَهُ نَارَ جَهَنَّمَ خَالِدًا فِيهَا ذَٰلِكَ الْخِزْيُ الْعَظِيمُ ﴿٦٣﴾

63. Je, Hawajui kuwa anayeshindana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi huyo atapata moto wa Jahanamu adumu humo? Hiyo ni hizaya kubwa.

WANASEMA YEYE NI SIKIO TU

Aya 61-63

MAANA

Na miongoni mwao wako wanaomuudhi Mtume na kusema: Yeye ni sikio tu.

Mtume(s.a.w.w) alikuwa akiwachukuliwa wote kwa dhahiri yao, bila ya kumtafuta mtu undani wake, kwa kuchukulia msingi wa kuwa dhahiri ni ya watu na undani ni wa Mwenyezi Mungu.

Hiyo ni miongoni mwa misingi ya Kiislamu ya sharia inayochukuliwa hukumu nyingi. Waliitumia wanafiki; wakawa wanaepuka kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakitoa udhuru na Mtume akiwakubalia.

Ajabu ni kwamba wao walitumia fadhila hii kuwa ni njia ya kumtukana na kumnasibisha kuwa anakubali haraka kila analolisikia bila ya kufikiria na kupambanua lipi la kukubalia na lipi la kukataa.

Lau kama Mtume angeliwakubalia kwa uwongo wao na unafiki wao, na kuwapa adhabu inyostahili, basi ingelikuwa shari kwao na wangelisema ni mwenye moyo mgumu na mwenye hasira.

Hiyo ndiyo ajabu kumwaibisha na lile lenye manufaa yanayowarudia wao! Lakini mwenye kulaumu hilo si ajabu kwake. Kwa vile anaangalia kila kitu kwa kioo cha nafsi yake kilicho cheusi; hata yule anayemfanyia wema pia.Amesema kweli yule aliyesema: “Asiyejua kizuri si mzuri yeye”.

Sema: ni sikio la heri kwenu.

Hili ni jibu la Mwenyezi Mungu kwa hao wanafiki. Kwa ufupi ni kwamba mtume ni sikio la heri sio la shari. Anawakubalia yale yasiyo na mad- hara kwa mtu na anakataa yaliyo na madhara; kama vile kusengenya na kufitini.

Anamwamini Mwenyezi Mungu na ana imani na waumini.

Yaani anawasadiki wakweli, kusadiki kwa kukinai, Ama wanafiki anawasadiki katika ambayo hapana madhara kuyasadiki.

Na ni rehema kwa wale wanaoamini miongoni mwenu.

Haya yanaungana na sikio la heri. Hiyo ni katika kuunganisha jumla kwenye mahsusi. Kwa sababu sikio la heri ni rehema vile vile.

Na wale wanaomuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu wana adhabu iumizayo.

Kwa sababu mwenye kumuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu ndio amemuudhi Mwenyezi Mungu.

Wanawaapia Mwenyezi Mungu ili wawaridhishe na hali Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ndiye mwenye haki zaidi ya kumridhisha, ikiwa wao ni waumini, kama wanavyodai.

Maneno ya wanawaapia na kuwaridhisha yanaelekezwa kwa Mtume na waumini. Mwenyezi Mungu amewapa habari katika Aya hii kwamba wanafiki walipojua kuwa mmewagundua waliwahofia; wakakimbilia viapo vya uwongo, Afadhali wao wangemridhisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa toba na ikhlasi.

Kuna hadith isemayo: “Mwenye kuapa kiapo cha uwongo, akiwa anajua kuwa yeye ni mwongo, basi amejitokeza kupambana na Mwenyezi Mungu”.

Ibara ya kusema ‘ndiye mwenye haki zaidi ya kumridhisha’, badala ya ndio wenye haki zaidi ya kuwaridhisha,’ ni kufahamisha kua kumridhisha Mtume ndio kumridhisha Mwenyezi Mungu; kama ambavyo kumuudhi ndiko kumuudhi yeye pia.

Je, Hawajui kuwa anayeshindana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi huyo atapata moto wa Jahanamu adumu humo? Hiyo ni hizaya kubwa.

Aya hii ni msisitizo wa Aya iliyotangulia. Sheikh Ismail Haqi anasema, katika tafsiri yake Rawhul Bayan: “Kila Mtume aliudhiwa kiasi kisichosemeka, na Muhammad(s.a.w.w) alikuwa ni zaidi; kama alivyosema mwenyewe: Hakuudhiwa Mtume kama nilivyoudhiwa mimi.”

Kwa kuwa kuudhiwa ni sababu ya kuimarika, basi maana ni kuwa hakuna Mtume aliyeimarika kuliko yeye. Hasan alipewa sumu na Husein akachinjwa kwa sababu ukamilifu ulikuwa ukiwakabili kwa kufa shahidi.

Mtume(s.a.w.w) alikuwa anaweza kuwaokoa kwa kuwaombea, lakini aliona ukamilifu wa daraja yao ulikuwa na nguvu kuliko kuokolewa; kiasi ambacho Mtume alimpa mmoja wa wakeze chupa mbili na kumwambia, kama moja ikiwa rangi ya njano, basi Hasan atakuwa amekufa shahidi kwa kupewa sumu; na kama nyingine ikiwa nyekundu basi Husein atakuwa shahidi kwa kuchinjwa, Na kweli hayo yakawa”.

يَحْذَرُ الْمُنَافِقُونَ أَن تُنَزَّلَ عَلَيْهِمْ سُورَةٌ تُنَبِّئُهُم بِمَا فِي قُلُوبِهِمْ قُلِ اسْتَهْزِئُوا إِنَّ اللَّـهَ مُخْرِجٌ مَّا تَحْذَرُونَ ﴿٦٤﴾

64. Wanaogopa wanafiki kuteremshiwa sura itakayowatajia yaliyomo nyoyoni mwao, Sema: Fanyeni mzaha tu, hakika Mwenyezi Mungu atayatoa mnayoyaogopa.

وَلَئِن سَأَلْتَهُمْ لَيَقُولُنَّ إِنَّمَا كُنَّا نَخُوضُ وَنَلْعَبُ قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ ﴿٦٥﴾

65. Na ukiwauliza, kwa hakika watasema: Sisi tulikuwa tukipiga porojo na kuchezea tu. Sema: Je, mlikuwa mkimfanyia mzaha Mwenyezi Mungu na Aya zake na Mtume wake?

لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ إِن نَّعْفُ عَن طَائِفَةٍ مِّنكُمْ نُعَذِّبْ طَائِفَةً بِأَنَّهُمْ كَانُوا مُجْرِمِينَ ﴿٦٦﴾

66. Msitoe udhuru, mmekwisha kufuru baada ya kuamini kwenu, Tukisamehe kundi moja miongoni mwenu tutaliadibu kundi jingine kwa vile wao walikuwa wakosefu.

WANAOGOPA WANAFIKI

Aya 64 – 66

MAANA

Wanaogopa wanafiki kuteremshiwa sura itakayowatajia yaliyomo nyoyoni mwao, Sema: Fanyeni mzaha tu, hakika Mwenyezi Mungu atayatoa mnayoyaogopa.

Wanafiki hawakuogopa hasa kushukiwa na wahyi kuwahusu wao, isipokuwa walidhihirisha hadhari kwa njia ya dharau na stihzai – walikuwa wakimbeza Mtume(s.a.w.w) huku wakiambizana kwa dharau: Angalieni, msije mkateremshiwa Sura!

Kwa upande mwingine wanafiki hawaamini wahyi, vipi watauogopa kiuhakika? Wafasiri wengi wamesma kuwa dhamiri katika ‘kuteremshiwa’, inawarudia waumini, na ile ya nyoyoni mwao inawarudia wanafiki. Lakini hayo yako mbali kwa sababu zifuatazo:

Kwanza : waumini hawakutajwa katika Aya na kwamba waliotajwa wazi- wazi ni wanafiki; kama ambavyo Aya iliyotangulia imewataja wao tu.

Pili : katika kufasiiri hivi, itabidi kuweko kutopatana dhamiri jambo amba- lo halina dalili.

Kwa ajili hii tunatilia nguvu kauli ya anayesema kuwa dhamiri zote zinawarudia wanafiki, Kwa hiyo maana yanakuwa wanaogopa kwa dharau, wanafiki kuteremshiwa Sura itakayofichua uadui wao kwa Uislamu na waislamu.

Mwenyezi Mungu naye akawapa kiaga cha kuwa Sura itakyowafichua itashuka tu, na itawakabili wao ana kwa ana; waombe msamaha usifae msamaha wao.

Na ukiwauliza, kwa hakika watasema: Sisi tulikuwa tukipiga porojo na kuchezea tu.

Jamaa katika wanafiki walisema yale yasiyostahiki kuhusu Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) . Alipowauliza walisema tulikuwa tunafanya mchezo tu.

Wafasiri wametofautiana kuhusu majina ya walio sema hayo na aina ya maneno waliyoyasema. Aya haidokezi chochote katika hayo; nasi tunanya- maza kama alivyowanyamazia Mwenyezi Mungu.

Sema: Je, mlikuwa mkimfanyia mzaha Mwenyezi Mungu na Aya zake na Mtume wake?

Kusema kwao kuwa tulikuwa tukichezea ni kubaya zaidi kuliko dhambi waliyoitakia msamaha. Je, Mwenyezi Mungu ambaye umetukuka ukuu wake ni wakufanyiwa mchezo? Je, amewatuma Mitume wake waje wachezewe? Aya inafahamisha kwamba kila mwenye kuifanyia mchezo dini na huku- mu yake yenye kuthibiti kwa uwazi basi huyo ni kafiri.

Msitoe udhuru, mmekwisha kufuru baada ya kuamini kwenu.

Utauliza : Je, si hii inafahamisha kuwa wao walikuwa waumin kabla ya kufanya mzaha; na kwamba sababu ya kuyawajibisha ukafiri wao ni istihzai; na inajulikana kwamba wao walikuwa makafiri kabla; na huo ukafiri wao ndio sababu ya mchezo wao?

Jibu : Kabla ya kukiri kwao kuifanyia mchezo dini walikuwa ni makafiri kwa hali halisi, lakini walikuwa ni waislamu kihukumu, Kwa sababu wao walidhihirisha Uislamu,Kwa hiyo zikawapitia hukumu za waislam ambazo zinaangalia dhahiri sio hali halisi.

Mara tu baada ya kukiri kwao kuifanyia mchezo dini wamekuwa ni makafiri kwa hali halisi na kwa kihukumu, wakiwa sasa kwenye hukumu ya waliortadi.

Tukisamehe kundi moja miongoni mwenu tutaliadhibu kundi jingine kwa vile wao walikua wakosefu.

Wanafiki walikuwa aina mbili: Viongozi wanaofuatwa ambao wana utakia mabaya Uislamu, kumfanyia vitimbi Mtume wake na kumchezea. Kundi jingine ni wale madhaifu wanaofuata.

Ndipo akamwamrisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) Mtume wake mtukufu kuwasamehe hao wanyonge kwa unyonge wao na kuwaadhibu wale wengine.

Kwa sababu wao ndio sababu, Inasemekana kuwa Mwenyezi Mungu aliwasamehe waliotubia na kuwaadhibu waliog’ang’ania ukafiri na unafiki.

الْمُنَافِقُونَ وَالْمُنَافِقَاتُ بَعْضُهُم مِّن بَعْضٍ يَأْمُرُونَ بِالْمُنكَرِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمَعْرُوفِ وَيَقْبِضُونَ أَيْدِيَهُمْ نَسُوا اللَّـهَ فَنَسِيَهُمْ إِنَّ الْمُنَافِقِينَ هُمُ الْفَاسِقُونَ ﴿٦٧﴾

67. Wanafiki wanaume na wanafiki wanawake ni hali moja. Wanaamrisha maovu na kukataza mema na wanafumba mikono yao. Wamemsahau Mwenyezi Mungu na yeye amewasahau, Hakika wanafiki ndio mafasiki.

وَعَدَ اللَّـهُ الْمُنَافِقِينَ وَالْمُنَافِقَاتِ وَالْكُفَّارَ نَارَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا هِيَ حَسْبُهُمْ وَلَعَنَهُمُ اللَّـهُ وَلَهُمْ عَذَابٌ مُّقِيمٌ ﴿٦٨﴾

68. Amewaahidi Mwenyezi Mungu wanafiki wanaume na wanafiki wanawake na makafiri moto wa Jahanam hali ya kudumu humo.Ni tosha yao, Na Mwenyezi Mungu amewalaani, Na wana wao adhabu ya kudumu.

كَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ كَانُوا أَشَدَّ مِنكُمْ قُوَّةً وَأَكْثَرَ أَمْوَالًا وَأَوْلَادًا فَاسْتَمْتَعُوا بِخَلَاقِهِمْ فَاسْتَمْتَعْتُم بِخَلَاقِكُمْ كَمَا اسْتَمْتَعَ الَّذِينَ مِن قَبْلِكُم بِخَلَاقِهِمْ وَخُضْتُمْ كَالَّذِي خَاضُوا أُولَـٰئِكَ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ ﴿٦٩﴾

69. Ni kama wale waliokuwa kabla yenu. Walikuwa na nguvu zaidi kuliko nyinyi na mali nyingi na watoto. Basi walistarehea sehemu yao, na nyinyi mwastarehea sehemu yenu kama walivyostarehe kwa sehemu yao wale waliokuwa kabla yenu na mkazama (katika batili) kama walivyozama. Hao zimeporomoka amali zao katika dunia na akhera, Na hao ndio waliopata hasara.

أَلَمْ يَأْتِهِمْ نَبَأُ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ قَوْمِ نُوحٍ وَعَادٍ وَثَمُودَ وَقَوْمِ إِبْرَاهِيمَ وَأَصْحَابِ مَدْيَنَ وَالْمُؤْتَفِكَاتِ أَتَتْهُمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيَظْلِمَهُمْ وَلَـٰكِن كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴿٧٠﴾

70. Je, hazikuwafikia habari za wale walio kuwa kabla yao, kaumu ya Nuh na Ad na Thamud na kaumu ya Ibrahim na watu wa Madyan na miiji iliyopinduliwa. Basi Mwenyezi Mungu hakuwa ni mwenye kuwadhulumu, lakini wao walikuwa wakijidhulumu wenyewe.

WANAFIKI WANAUME NA WANAWAKE

Aya 67 – 70

MAANA

Wanafiki wanaume na wanafiki wanawake ni hali moja.

Hilo ni fumbo la kufanana kwao kisifa na kimatendo. Kisha akabainisha jinsi walivyofanana, kwa kauli yake:

Wanaamrisha maovu na kukataza mema na wanafumba mikono yao. Wamemsahau Mwenyezi Mungu na yeye amewasahau.

Maovu waliyoyamrisha ni ukafiri na unafiki; na wema walioukataza ni imani na kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Ama mikono yao wameifunga kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu. Kumsahau Mwenyezi Mungu ni kuacha kwao kumtii; na yeye kuwasahau ni kuwanyima rehema yake.

Hakika wanafiki ndio mafasiki wenye kuacha njia ya Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema na kufuata njia ya shetani.

Amewaahidi Mwenyezi Mungu wanafiki wanaume na wanafiki wanawake na makafiri moto wa Jahanam hali ya kudumu humo.

Baada ya kubainisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) maovu ya wanafiki, aliwa- pa kiaga na kumpa kiaga kila kafiri moto wa Jahanam.

Ni tosha yao.

Yaani malipo yanatoshana na matendo yao

Na Mwenyezi Mungu amewalaani Amewaweka mbali na rehema yake.Na wana wao adhabu ya kudumu Haipungui wala kukatika

Ni kama wale waliokuwa kabla yenu. Walikuwa na nguvu zaidi kuliko nyinyi na mali nyingi na watoto. Basi walistarehea sehemu yao, na nyinyi mwastarehea sehemu yenu kama walivyostarehea sehemu yao wale waliokuwa kabla yenu na mkazama (katika batili) kama walivyozama.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawambia: Enyi wanafiki mlio wakati wa Muhammad! Ni sawa na wanafiki waliopita. Walistarehe na maraha ya dunia, tena walikuwa na nguvu, mali na watoto kuliko nyinyi; basi na nyinyi stareheni na mmezama katika batili kama walivyozama.

Hao zimeporomoka amali zao katika dunia na akhera.

Yaani mema yao yamebatilika, ikiwa wanayo, kama vile kuishi kwa jasho lao. Kubatilika katika akhera ni kutolipwa hayo. Ama kubatilika kwake duniani ni kwamba hilo si chochote kwa makafiri na manafiki mbele za watu wenye mwamko na imani.

Na hao ndio waliopata hasara.

Kwa vile wao wamejichokesha kupanga njama kwa waumini wema, kisha ubaya wa dunia na akhera ukawarudia wao. Kwa ufupi ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaaambia wanafiki waliokuwa wakati wa Mtume(s.a.w.w) . Acheni ukafiri na unafiki na chukueni funzo kwa wale waliokuwa kabla yenu kabla ya kuchukua funzo watakao kuja baada yenu.

Je, hazikuwafikia habari za wale walio kuwa kabla yao, kaumu ya Nuh na Ad na Thamud na kaumu ya Ibrahim na watu wa Madyan na miiji iliyopinduliwa.

Watu wa Madyan ni kaumu ya Shuaib, na wa miji iliyopinduliwa ni kaumu ya Lut.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawakumbusha wanafiki kuhusu watu hawa, kwa sababu miji yao ilikuwa karibu na miji ya waarabu; nao walikuwa na mali nyingi na watoto:

Watu wa Ibrahim waliangamizwa kwa kunyang’a nyangwa neema, wa Adi kwa upepo, wa Nuh kwa gharika, wa Thamud kwa ukelele, na wa Madyan kwa adhabu ya wingu, na wale wa miji iliyopinduliwa ni kwa kupinduliwa juu chini, Yametangulia maelezo ya hayo katika sura ya 7.

Basi Mwenyezi Mungu hakuwa ni mwenye kuwadhulumu, lakini wao walikuwa wakijidhulumu wenyewe kwa kung’anga’ania kwao makosa na dhambi.

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ أُولَـٰئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللَّـهُ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴿٧١﴾

71. Na waumini wanaume na waumin wanawake ni mawalii wao kwa wao. Huamrishana mema na kukatazana maovu, Na husimamisha swala, Na hutoa zaka. Na humtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Hao Mwenyezi Mungu atawarehemu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hekima.

وَعَدَ اللَّـهُ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا وَمَسَاكِنَ طَيِّبَةً فِي جَنَّاتِ عَدْنٍ وَرِضْوَانٌ مِّنَ اللَّـهِ أَكْبَرُ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ ﴿٧٢﴾

72. Amewaahidi Mwenyezi Mungu waumini wanaume na waumin wanawake bustani (Pepo) zipitazo mito chini yake; hali ya kudumu humo na maskani mema katika mabustani ya milele, Na radhi za Mwenyezi Mungu ndizo kubwa zaidi, Huko ndiko kufuzu kukubwa.

NA WAUMIN WANAUME NA WAUMINI WANAWAKE

Aya 71 – 72

MAANA

Na waumini wanaume na waumin wanawake ni mawalii wao kwa wao.

Makusudio ya walii hapa ni kusaidiana. Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja wanafiki na uchafu wao, anawataja waumin kwa fadhila zao; na kwamba wanasaidiana. Yeyote anayedai kumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake wala asimsaidie ndugu yake katika imani hii basi yeye ni mnafiki aliyetajwa na Aya iliyotangulia, iliyowashukiwa wanafiki.

Huamrishana mema na kukatazana maovu Kinyume na wanafiki ambao wanaamrisha maovu na hukataza mema.Na husimamisha swala kiuhakika, sio ria kama wanafiki.

Na hutoa zaka Wala hawafanyi ubakhili kama wanafiki. Na humtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake

Na wanaendelea na utiifu huo vyovyote iwavyo.

Hao Mwenyezi Mungu atawarehemu.

Ama wanafiki amewalaani na kuwaandalia moto wa Jahannam hali ya kudumu humo.

Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hekima.

Mwenye uwezo wa kuwapa nguvu waumini na kuwadhalilisha wanafiki na makafiri.

Amewaahidi Mwenyezi Mungu waumini wanaume na waumin wanawake bustani (Pepo) zipitazo mito chini yake; hali ya kudumu humo na maskani mema katika mabustani ya milele. Na radhi za Mwenyezi Mungu ndizo kubwa zaidi

Kila anayemridhisha Mwenyezi Mungu katika amali zake na makusudio yake, basi Mwenyezi Mungu atamridhia.

Huko ndiko kufuzu kukubwa

Huko ni ishara ya huko kupata bustani na makazi mema. Umetangulia mfano wake katika Juz.(3:15).

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ جَاهِدِ الْكُفَّارَ وَالْمُنَافِقِينَ وَاغْلُظْ عَلَيْهِمْ وَمَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ ﴿٧٣﴾

73. Ewe Mtume! Pambana na makafiri na wanafiki na uwawekee ngumu. Na makazi yao ni Jahanamu, nayo ni marejeo mabaya.

يَحْلِفُونَ بِاللَّـهِ مَا قَالُوا وَلَقَدْ قَالُوا كَلِمَةَ الْكُفْرِ وَكَفَرُوا بَعْدَ إِسْلَامِهِمْ وَهَمُّوا بِمَا لَمْ يَنَالُوا وَمَا نَقَمُوا إِلَّا أَنْ أَغْنَاهُمُ اللَّـهُ وَرَسُولُهُ مِن فَضْلِهِ فَإِن يَتُوبُوا يَكُ خَيْرًا لَّهُمْ وَإِن يَتَوَلَّوْا يُعَذِّبْهُمُ اللَّـهُ عَذَابًا أَلِيمًا فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَمَا لَهُمْ فِي الْأَرْضِ مِن وَلِيٍّ وَلَا نَصِيرٍ ﴿٧٤﴾

74. Wanaapa kwa Mwenyezi Mungu, hawakusema na hakika wamekwisha sema neno la kufuru, Na wakakufuru baada ya kusilimu kwao, Wakajihimu kufanya wasioyoweza kuyafikia. Na hawakuchukia ila ni kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake amewatajirisha kwa fadhila zake. Wakitubia, itakuwa heri kwao; na kama wakikengeuka, Mwenyezi Mungu atawaadhibu adhabu iumizayo duniani na Akhera, Hawana mlinzi katika ardhi wala msaidizi.

SHINDANA NA MAKAFIRI NA WANAFIKI

Aya 73 – 74

MAANA

Ewe Mtume! Pambana na makafiri na wanafiki na uwawekee ngumu. Na makazi yao ni Jahanamu, nayo ni marejeo mabaya.

Mtume(s.a.w.w) aliwachukulia upole wanafiki, lakini haikufaa, bali ndio walimtusi na kumwambia kuwa ni sikio; ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamwamrisha kuwawekea ngumu na kupambana nao, Lakini hakubain- isha aina ya kupambana nao. Je, ni kwa upanga ulimi au kwa njia nyingine. Maana yake ni kuwa Mwenyezi Mungu amemwachia Mtume(s.a.w.w) kukadiria vile hekima na masilahi yanavyotaka.

Wanaapa kwa Mwenyezi Mungu, hawakusema na hakika wamekwisha sema neno la kufuru.

Waliosema ni jamaa katika wanafiki. Kwani wao walitamka neno la kufuru kuhusu Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) , Alipowauliza waliogopa, wakaapa. Ndipo Mwenyezi Mungu akawakadhibisha na yakathibiti yale yaliyonasibishwa kwao.

Mwenyezi Mungu, mtukufu hakutaja majina ya walioapa kiapo cha uwon- go wala hilo neno la kufuru walilolitamka ili waislam wasiliabudu kwa kulisoma.

Sheikh Maraghi anasema: “Yamesahihika, yaliyopokewa, kwamba Mtume(s.a.w.w) alipokuwa amelala chini ya kivuli cha mti, alisema: Atawajia mtu atawangalia kwa macho ya shetani, Akija msizungumze naye. Mara akatokea mtu mwenye mandhari ya kiuadui.Mtume akamwita na kumwambia: Kwa nini unanishutumu wewe na sahaba zako? Yule mtu akaondoka na kuleta wenzake; wakaapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa hawakusema. Akateremsha Mwenyezi Mungu Aya hii

Na wakakufuru baada ya kusilimu kwao.

Mfano huu ni kama wa Aya 66 ya Sura hii.

Wakajihimu kufanya wasioyoweza kuyafikia.

katika Tafsir Razi, Bahrul-muhit Al-Manar, Maraghi na nyinginezo imeelezwa kuwa kikundi cha wanafiki kiliafikiana kummaliza Mtume. Mwenyezi Mungu akamfahamisha hilo akajiepusha nalo bila ya kutimia makusudio.

Katika Kitabu Ala’yan, cha Sheikh Muhammad Al-amin, kuna maelezo haya: “Mtume(s.a.w.w) alipokuwa akirudi kutoka Tabuk akielekea Madina, ali- fanyiwa njama na watu katika maswahaba zake, Wakala njama ya kumtupa kutoka katika njia inayopitia juu mlimani, Basi Mtume akapewa habari yao”.

Na hawakuchukia ila ni kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake amewatajirisha kwa fadhila zake.

Dhamiri inawarudia wanafiki, Wengi wao walikuwa katika dhiki ya maisha wakiwa na hali ngumu sana ya ufukara kabla ya kusilimu. Baada ya kutamka tamko la kusilimu kwa midomo yao tu, ziliwamiminikia riziki. Kwa vile Mtume alikuwa akiwagawanyia ngawira sawa na waislam wengine. Vile vile baadhi yao aliwalipia madeni yao.

Malipo yao yakawa ni hayo waliyoyasema na kuazimia kumua. Ndipo Mwenyezi Mungu akawatahayariza, na kukufuru kwao neema, kwa mfumo huu; sawa na kumwambia mtu uliye mfanyia wema kisha akakuudhi “Ubaya wangu ni kukufanyia wema?!”.

Wakitubia, itakuwa heri kwao

Mlango wa toba uko wazi kwa kila mwenye kuubisha. Njia ya kuuendea ni nyepesi sana, kiasi ambacho makafiri na wanafiki hawatakiwi lolote zaidi ya kuomba msamaha kwa yaliyopita na kusadikisha yajayo.

Na kama wakikengeuka, Mwenyezi Mungu atawaadhibu adhabu iumizayo katika duniani na Akhera.

Adhabu yao huko Akhera inajulikana ama adhabu katika dunia ni kwamba wanafiki daima watakuwa katika hofu ya kuwafedheheka na kufichuka.

Kwa ajili hiyo wanaogopa kila kitu na wanadhani kuwa kila neno wanaambiana wao tu; kama alivyowatajia Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kauli yake:

وَإِذَا رَأَيْتَهُمْ تُعْجِبُكَ أَجْسَامُهُمْ وَإِن يَقُولُوا تَسْمَعْ لِقَوْلِهِمْ كَأَنَّهُمْ خُشُبٌ مُّسَنَّدَةٌ يَحْسَبُونَ كُلَّ صَيْحَةٍ عَلَيْهِمْ ﴿٤﴾

“Na ukiwaona miili yao inakupendeza, na wakisema, unasikiliza usemi wao; wao ni kama boriti zilizotegemezwa, wanadhani kila kishindo ni juu yao” (63:4).

Hawana mlinzi katika ardhi wala msaidizi.

Ninani anayeweza kumsaidia au kujaribu kumsaidia ambaye aibu yake na maovu yake yamefichuka kwa watu wote.

وَمِنْهُم مَّنْ عَاهَدَ اللَّـهَ لَئِنْ آتَانَا مِن فَضْلِهِ لَنَصَّدَّقَنَّ وَلَنَكُونَنَّ مِنَ الصَّالِحِينَ ﴿٧٥﴾

75. Na miongoni mwao wako waliomwahidi Mwenyezi Mungu: Akitupa fadhila zake hakika tutatoa sadaka na hakika tutakuwa miongoni mwa watendao wema.

فَلَمَّا آتَاهُم مِّن فَضْلِهِ بَخِلُوا بِهِ وَتَوَلَّوا وَّهُم مُّعْرِضُونَ ﴿٧٦﴾

76. Lakini alipowapa katika fadhila zake, walizifanyia ubakhili wakageuka na huku wakipuuza.

فَأَعْقَبَهُمْ نِفَاقًا فِي قُلُوبِهِمْ إِلَىٰ يَوْمِ يَلْقَوْنَهُ بِمَا أَخْلَفُوا اللَّـهَ مَا وَعَدُوهُ وَبِمَا كَانُوا يَكْذِبُونَ ﴿٧٧﴾

77. Kwa hiyo ukawalipa unafiki katika nyoyo zao mpaka siku ya kukutana nao. Kwa sababu ya kumhalifu Mwenyezi Mungu yale waliyomwahidi na kwa sababu ya kusema kwao uwongo.

أَلَمْ يَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ سِرَّهُمْ وَنَجْوَاهُمْ وَأَنَّ اللَّـهَ عَلَّامُ الْغُيُوبِ ﴿٧٨﴾

78. Je,hawajui kwamba Mwenyezi Mungu anajua siri zao na minong’ono yao, na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye sana mambo ya ghaibu.

MIONGONI MWAO WAKO WALIO MWAHIDI MWENYEZI MUNGU

Aya 75 – 78

MAANA

Na miongoni mwao wako waliomwahidi Mwenyezi Mungu: Akitupa fadhila zake hakika tutatoa sadaka na hakika tutakuwa miongoni mwa watendao wema. Lakini alipowapa katika fadhila zake, walizifanyia ubakhili wakageuka na huku wakipuuza

Watu wa Tafsir wamesema kuwa Aya hii ilimshukia mtu mmoja katika Ansar anayeitwa Tha’lab bin Hatib. Alimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) : Niombee kwa Mwenyezi Mungu aniruzuku mali.

Mtume akamwambia: Ee Tha’laba! Kichache unachoweza kishukuria ni bora kuliko kingi usichokiweza. Kwani hupati kiigizo chema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu! Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi kwake! Lau ningelitaka jabali linigeukie dhabu na fedha, lingegeuka.

Lakini Tha’laba, hakukinai, akamnaga’ang’ania Mtume na kusema: Naapa kwa ambaye amekupa utume kwa haki! Kama Mungu akiniruzuku mali nitampa kila mwenye haki haki yake. Mtume akasema: Ewe Mola wangu! Mruzuku Tha’alaba mali.

Basi Tha’laba akawa na mbuzi wakazaana kama wadudu, Pakawa pale mjini, hapamtoshi, akahamia nje, Ikawa tena hawezi kuhudhuria Swala ya Jamaa wala ya Ijumaa.

Mtume akamtumia mtu akachuke zaka kwake, akakataa na kufanya ubakhili, akasema. Hii tena ni kama kodi. Mtume akasema: Ole wake Tha’laba, Ndipo zikashuka Aya hizo.

Iwe ni kweli Aya hizi zimeshuka kwa Tha’laba au kwa mwengine, lakini tukio hilo linabainisha kwa ufasaha sana makusudio ya Aya hizi. Tumezungumzia kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 4 (3:143) kifungu cha: ‘Mabadiliko ya hulka na fikra’

Kwa hiyo ukawalipa unafiki katika nyoyo zao mpaka siku ya kukutana nao.

Katika Tafsir Albahrul Muhit kuna maelezo kuwa Hasan, Qatada na Abu Muslim, walisema kuwa dhamir ya ukawalipa inarudia kwenye ubakhili.

Pia kauli hiyo ameichagua Tabrasi na Maraghi. Yaani ubakhili umewalipia unafiki hautaachana nao mpaka siku ya kukutana na malipo ya ubakhili.

Mwenyezi Mungu ametaja sababu mbili za hayo:

1.Kwa sababu ya kumhalifu Mwenyezi Mungu yale waliyomwahidi.

2.Kwa sababu ya kusema kwao uwongo.

Sifa hizi mbili za kuhalifu ahadi na uwongo ni sifa mahsusi za wanafiki zilizoelezwa katika Hadith. Anasema Mtume Mtukufu(s.a.w.w) : “Alama za mnafiki ni tatu: Akizungumza husema uwongo na akiahidi huhalifu na akiaminiwa hufanya hiyana.”

Je, hawajui kwamba Mwenyezi Mungu anajua siri zao na minong’ono yao, na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye sana mambo ya ghaibu.

Siri ni ile iliyo moyoni, na mnong’ono ni maneno ya siri wanayoizungumza wawili au zaidi na ghaibu ni ile wasiyoijua viumbe wote. Maana ni kuwa vipi hawa wanafiki wanathubutu kuficha ukafiri na kuunong’ona? Hawajui kuwa Mwenyezi Mungu anajua yaliyo katika nyoyo zao na yanayozunguka katika ndimi zao, na kwamba halifichiki kwake lolote la kufichika katika ardhi na mbingu?