TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA Juzuu 11

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 9730
Pakua: 1402

Maelezo zaidi:

Juzuu 11
Juzuu 1
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 15 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 9730 / Pakua: 1402
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA Juzuu 11

Mwandishi:
Swahili

4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA

مَا كَانَ لِأَهْلِ الْمَدِينَةِ وَمَنْ حَوْلَهُم مِّنَ الْأَعْرَابِ أَن يَتَخَلَّفُوا عَن رَّسُولِ اللَّـهِ وَلَا يَرْغَبُوا بِأَنفُسِهِمْ عَن نَّفْسِهِ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ لَا يُصِيبُهُمْ ظَمَأٌ وَلَا نَصَبٌ وَلَا مَخْمَصَةٌ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَلَا يَطَئُونَ مَوْطِئًا يَغِيظُ الْكُفَّارَ وَلَا يَنَالُونَ مِنْ عَدُوٍّ نَّيْلًا إِلَّا كُتِبَ لَهُم بِهِ عَمَلٌ صَالِحٌ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُضِيعُ أَجْرَ الْمُحْسِنِينَ ﴿١٢٠﴾

120. Haiwafalii watu wa Madina na Mabedui walio kandoni mwao kubaki nyuma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu; wala kujipendelea nafsi zao kuliko nafsi yake. Hayo ni kwa sababu ya kuwa hakiwapati kiu wala taabu wala njaa katika njia ya Mwenyezi Mungu; wala hawakanyagi ardhi ichukizayo makafiri, wala hakiwapati chochote kutokana na adui, ila huandikiwa kuwa ni amali njema. Hakika Mwenyezi Mungu haupotezi ujira wa watendao mazuri.

وَلَا يُنفِقُونَ نَفَقَةً صَغِيرَةً وَلَا كَبِيرَةً وَلَا يَقْطَعُونَ وَادِيًا إِلَّا كُتِبَ لَهُمْ لِيَجْزِيَهُمُ اللَّـهُ أَحْسَنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٢١﴾

121. Wala hawatoi chochote cha kutumiwa kidogo wala kikubwa wala hawalikati bonde ila wanaandikiwa kuwa Mwenyezi Mungu awalipe mema ya yale waliyokuwa wakiyatenda.

HAIFAI WATU WA MADINA KUBAKI NYUMA

Aya 120 – 121

MAANA

Haiwafalii watu wa Madina na Mabedui walio kandoni mwao kubaki nyuma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu; wala kujipendelea nafsi zao kuliko nafsi yake.

Mtume wa Mwenyezi Mungu ni Muhammad(s.a.w.w) . Makusudio yake hapa ni dini ya Mwenyezi Mungu na haki, Kwa sababu dini ya haki inaun- dika katika utu wake mtukufu.

Kuinusuru haki ni wajibu kwa kila Mwislamu, wala hakuhusiki na watu wa Madina na walio kandoni mwao; isipokuwa wametajwa hao kwa kuwa karibu kwao na kuwa jirani, na pia kwa kulingana na mazungumzo ya vita vya Tabuk. Maana ni kuwa ni juu ya kila Mwislamuu kuinusuru haki na kuizuia batili wala asiathirike na manufaa na masilahi kuliko dini ya Muhammad, kwa kutoa visababu vya uwongo, kama walivyofanya wanafiki.

Hayo ni kwa sababu ya kuwa hakiwapati kiu wala taabu wala njaa katika njia ya Mwenyezi Mungu; wala hawakanyagi ardhi ichukizayo makafiri, wala hakiwapati chochote kutokana na adui, ila huandikiwa kuwa ni amali njema.

Hayo ni ishara ya kukataza kubaki nyuma na kuacha kuwapiga jihadi wabatilifu.

Ni jambo la kutia uchungu kwa mtu yeyote, awe Mwislamuu au la, kumwacha akanyage mchanga wa mji wake na nchi yake; pengine awe kibaraka asiye na dini wala dhamiri. Uislamu haumruhusu yeyote, vyovyote alivyo, kukanyaga ardhi ya mwingine ila kwa sababu mbili; Kuzuia madhara ya watu; kama vile kuzima moto kukinga mali na mali ya jirani.

Kuingiza nguvu iliyoadilifu itakayowazuia watu wa hapo na dhuluma na uadui kwa mji mwingine; kama alivyofanya Mtume(s.a.w.w) katika vita vya Tabuk, baada ya Waroma kuazimia kuipiga madina na kuumaliza Uislamu na Mtume wake.

Hakika Mwenyezi Mungu haupotezi ujira wa watendao mazuri.

Hakuna kitu rahisi kwa mtu kuliko kufanya wema, maadamu Mwenyezi Mungu anakuandikia wema kukaa kwake, kusimama kwake, na hata unyao mmoja tu anaoukanyaga kwa ajili ya kumtii Mwenyezi Mungu.

Wala hawatoi chochote cha kutumiwa kidogo wala kikubwa wala hawalikati bonde ila wanaandikiwa kuwa Mwenyezi Mungu awalipe mema ya yale waliyokuwa wakiyatenda.

Haya na yaliyo kabla yake yanafupilizwa na kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu:

فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ ﴿٧﴾

“Na atakayefanya heri uzani wa sisimizi ataiona” (99:7).

Lengo la ufafanuzi huu ni kuhimiza mali ya heri na kuhimiza kumpiga jihadi anayeeneza ufisadi katika ardhi.

وَمَا كَانَ الْمُؤْمِنُونَ لِيَنفِرُوا كَافَّةً فَلَوْلَا نَفَرَ مِن كُلِّ فِرْقَةٍ مِّنْهُمْ طَائِفَةٌ لِّيَتَفَقَّهُوا فِي الدِّينِ وَلِيُنذِرُوا قَوْمَهُمْ إِذَا رَجَعُوا إِلَيْهِمْ لَعَلَّهُمْ يَحْذَرُونَ ﴿١٢٢﴾

122. Wala haiwafalii waumini kutoka wote, Kwa nini kisitoke kikundi katika kila kundi miongoni mwao kuji funza dini na kuwaonya watu wao watakapowarudia, Ili wapate kujihadhari.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قَاتِلُوا الَّذِينَ يَلُونَكُم مِّنَ الْكُفَّارِ وَلْيَجِدُوا فِيكُمْ غِلْظَةً وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ مَعَ الْمُتَّقِينَ ﴿١٢٣﴾

123. Enyi mlioamini! Piganeni na wale walio karibu yenu katika makafiri na wakute kwenu ugumu; na jueni kuwa Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye takua.

KWA NINI KISITOKE KIKUNDI

Aya 122 – 123

MAANA

Wala haiwafalii waumini kutoka wote.

Aya hii inaungana na Aya iliyotangulia kuwa haifai watu wa Madina kubaki nyuma. Njia ya kuungana ni kwamba iliposhuka Aya iliyotangulia Makabila ya Kiislam yalisema: Wallahi kuanzia leo hatutabaki nyuma ya Mtume katika vita. Wakamiminika kutoka madina kwa lengo hili.

Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akateremsha Aya hii, tuliyonayo, kuwa hawatakiwi kutoka wote kwa jihadi, bali hali hiyo inatofautiana kwa kutofautiana vita. Mara nyingine jihadi inakuwa ni wajibu kwa kila mtu, mara nyingine inakuwa ni wajibu kifaya, wakitekeleza baadhi basi wajibu umewaondokea wote.

Ama atakayetofautisha kati ya wajib hizo mbili ni Mtume(s.a.w.w) . Watatoka Waislamu wote kama akitaka watoke, na watatoka baadhi akitaka hivyo.

Kwa nini kisitoke kikundi katika kila kundi miongoni mwao kujifunza dini na kuwaonya watu wao watakapowarudia.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kubainisha kuwa si wajibu kwa kundi lote kutoka katika kila vita, sasa ana bainisha kuwa kuna wajibu mwingine usiokuwa jihadi ambao ni wajibu kuutekeleza, sawa na jihadi; kama vile kutoka kikundi katika kila mji au kabila kwenda Madina au mahali penginepo, kujifunza dini ya Mwenyezi Mungu – wajue halali na haramu; kisha warudi kwa watu wao wawongoze na kuwatahadharisha na adhabu ya Mwenyezi Mungu inayotokana na kumwasi na kuhalifu amri zake.

Ili wapate kujihadhari.

Yaani wawasikilize wanowaongoza na wawatii.

Hivi ndivyo tulivyoona katika kufasiri Aya hii, tukiwa tumetofautiana na wafasiri wengi ambao wamefanya ‘kujifundisha’ ni sifa ya watakaobaki, sio watakaotoka; wakasema katika ufanuzi wao kuwa ni wajibu kwa Waislamu kugawanyika makundi mawili: Kundi liende kwenye Jihad na kundi jingine libaki Madina kujifunza sunna na faradhi.

Tafsiri tuliyokwenda nayo sisi ndiyo yenye asili katika riwaya za Ahlu Bait wa Mtume(s.a.w.w) ambao ndio wajuzi zaidi wa Qur’ani na siri zake.

Miongoni mwa riwya hizo ni ile isemayo kuwa Mtu mmoja alimwuliza Imam Ja’far Asswadiq(a.s) kuhusu maana ya kauli ya Mtume(s.a.w.w) : “Kutofautiana umati wangu ni rehema”. Akasema: Makusudio ya kutofautiana sio kuzozana, vinginevyo kuafikiana kwao ingelikuwa ni adhabu; isipokuwa makusudio ni kuhangaika duniani kutafuta elimu. Kisha Imam akaitolea dalili Aya hii kwa makusudio ya maana hayo.

Hakuna mwenye shaka kwamba dalili hiyo haikamliki ila ikiwa kujielimisha ni sifa ya kikundi kinachotoka sio kinachobaki.

Wanachuoni wa usul wameitolea dalili Aya hii kuwa ‘Habari Moja’ inayo nukuliwa kutoka kwa Masumu ni hoja inayopasa kutumiwa katika hukumu za kisharia Njia ya kutoa dalili ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ame- wajibisha kwa ulama kufundisha na kuonya. Na, ukishakuwa wajibu huu kwa ulama, basi imekuwa wajibu kwa asiyejua kukubali kauli ya ulama na kuitumia; vinginevyo itakuwa wajibu wa kujifundisha na kuonya; ni mchezo tu.

Vile vile ikiwa ni wajibu kwa asiyejua kujifundisha, basi imekuwa ni wajibu kwa ulama kufundisha; vinginevyo itakuwa wajibu wa asiyejua kujifundisha ni mchezo tu. Imam Ali(a.s.) anasema:“Mwenyezi Mungu hatawaadhibu wajinga kwa kutojifundisha mpaka awaadhibu wenye elimu kwa kutofundisha”.

Enyi mlioamini! Piganeni na wale walio karibu yenu katika makafiri.

Aya hii inawahimiza Waislamu kulinda mipaka na maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui zao. Katika Majmaul-bayan kuna maelezo kuhusu tafsiri ya walio karibu yenu katika makafiri kuwa ni walio karibu zaidi, isipokuwa kama kuna mapatano. Hii ni dalili kuwa ni wajibu kwa watu walio katika hali ya hatari kujilinda wakihofia kuchafuliwa Uislamu au mji wa Waislamu, hata kama hayuko Imam mwadilifu”.

Tumezungumizia kwa ufafanuzi kuhusu kupigana na makafiri katika Juz: (2:193) Kwa anuani ya ‘Uislamu unapiga vita dhulma na ufisadi’.

IMAM ZAINULABIDIN NA MSINGI WA VITA

Na wakute kwenu ugumu.

Ugumu hapa ni fumbo la nguvu na kuilinda vizuri mipaka.

Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye takua.

Ambao wameamini imani ya kweli; wakafanya ikhlasi katika kupigana na adui yao na adui wa Mwenyezi Mungu; wakajiandaa kwa nguvu zao zote, kama alivyo waamrisha Mwenyezi Mungu.

Maelezo ya kupendeza kuhusu maudhui haya ni dua ya Imam Zainul Abidin, Ali Bin Hussein(a.s.) , akimlingania Mola wake na kuwaombea watu walio katika hatari ya kushambuliwa na walinzi wa miji ya Kiislamu. Alisema katika aliyoyasema:

“Ewe Mola Wangu! Mrehemu Muhammad na Ali wa Muhammad. Na uifanye nyingi idadi yao, uzinoe silaha zao, uzilinde nchi zao, uzuie kushambuliwa kwao, ushikamanishe mjumuiko wao, uyaaangalie vizuri mambo yao, uwatoshelezee mahitaji yao, uwasaidie kwa kuwapa subra (uvumilivu), uwahurumie kwa kuwakinga na hadaa, uwafahamishe wasiyoyajua, uwaelimishe wasiyokuwa na ujuzi nayo.

Wanapokutana na adui wasahaulishe kukumbuka dunia yao iliyo na hadaa na ghururi, ufute katika nyoyo zao mawazo ya mali yenye fitna na uijalie pepo machoni mwao.”

Hiyo ndiyo misingi ya ushindi wa kuweza kulizuwiya jeshi lolote kadiri litakavyokuwa na silaha za kisasa; hata tonoradi, mizinga, mapesa ya kuwalipa wapiganaji, elimu ya vita na kutumia silaha pamoja na mbinu zote za kupigana.

Silaha kubwa zaidi ni kuunganisha majeshi na kuzifanya nyoyo ziwe na ikhlasi ya kupigana na kuwa na uvumilivu hadi kufa, kuisahau dunia na kuamini kuwa mtu kufa shahidi, katika kupigania dini yake na nchi yake ndio faida na kufuzu kukubwa.

Je, si Waarabu na Waislamu, wa zamani na wasasa, wamekuwa ni chakula kwa sababu tu ya mali yenye fitina? Dalili ya hayo ni janga la tarehe 5 June,1967.

Maneno haya ya Imam Zainul Abidin yamepitiwa na zaidi ya karne 13, lakini pamoja na hayo lau, hivi sasa, kamanda mkuu angetaka kusoma sababu za ushindi, basi hatahitajia ila kufafanua matamko haya mafupi aliyoyatamka Imam.

وَإِذَا مَا أُنزِلَتْ سُورَةٌ فَمِنْهُم مَّن يَقُولُ أَيُّكُمْ زَادَتْهُ هَـٰذِهِ إِيمَانًا فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا فَزَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَهُمْ يَسْتَبْشِرُونَ ﴿١٢٤﴾

124. Na inapoteremshwa Sura yoyote, basi miongoni mwao kuna wanaosema: Ni nani miongoni mwenu Sura hii imemzidishia imani? Basi wale walioamini inawazidishia imani, nao wanafurahi.

وَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ فَزَادَتْهُمْ رِجْسًا إِلَىٰ رِجْسِهِمْ وَمَاتُوا وَهُمْ كَافِرُونَ ﴿١٢٥﴾

125. Ama wale wenye maradhi katika nyoyo zao, basi inawazidshia uovu juu ya uovu wao, Na wanakufa hali ni makafiri.

أَوَلَا يَرَوْنَ أَنَّهُمْ يُفْتَنُونَ فِي كُلِّ عَامٍ مَّرَّةً أَوْ مَرَّتَيْنِ ثُمَّ لَا يَتُوبُونَ وَلَا هُمْ يَذَّكَّرُونَ ﴿١٢٦﴾

126. Je, hawaoni kwamba wao wanajaribiwa kila mwaka mara moja au mara mbili? Kisha hawatubu wala hawakumbuki.

وَإِذَا مَا أُنزِلَتْ سُورَةٌ نَّظَرَ بَعْضُهُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ هَلْ يَرَاكُم مِّنْ أَحَدٍ ثُمَّ انصَرَفُوا صَرَفَ اللَّـهُ قُلُوبَهُم بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَّا يَفْقَهُونَ ﴿١٢٧﴾

127. Na inapoteremshwa Sura wanatazamana: Je, kuna yeyote anyewaona? Kisha hugeuka, Mwenyezi Mungu amezigeuza nyoyo zao kwa kuwa wao ni watu wasiofahamu.

INAPOTEREMSHWA SURA

Aya 124 – 127

MAANA

Na inapoteremshwa Sura yoyote, basi miongoni mwao kuna wanaosema: Ninani miongoni mwenu Sura hii imemzidishia imani?

Yaani baadhi ya wanafiki walikuwa wakidharau Qur’ani na kuulizana kuwa kuna ajabu gani ya hii?

Kwa hiyo wanazifanya nafsi zao, zilizochafuliwa na tamaa na dhambi, kuwa ni kipimo cha haki na ukweli.

La kushangaza ni kuwa washirikina walikuwa wakiukubali ukuu wa Qur’ani na athari zake zinazoingia nyoyoni, wakuwa wanausiana kuwa wasisikilize, kwa kuhofia kuvutwa kwenye Uislamu bila ya kujitambua. Mwenyezi Mungu anasema:

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَا تَسْمَعُوا لِهَـٰذَا الْقُرْآنِ وَالْغَوْا فِيهِ لَعَلَّكُمْ تَغْلِبُونَ ﴿٢٦﴾

“Na Walisema waliokufuru: Msisikilize Qur’ani hii na fanyeni zogo, huenda mkashinda” (41:26)

Hii inafahamisha, moja kwa moja, kuwa wanafiki wana athari mbaya zaidi kuliko washirikina.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewajibu wanafiki kwa kuwaaambia:

Basi wale walioamini inawazidishia imani.

Yaani, ikiwa katika nafsi zenu enyi wanafiki, haina athari yoyote nzuri, baada ya kupigwa chapa ya matamanio, basi waumini inawazidishia uongofu na yakini. Kwa sababu nafsi zao ni safi hazina taka ya uchafu kama nafsi zenu.

Nao wanafurahi kila inapoteremshwa Sura au Aya katika Qur’ani, kwa sababu inawapa bishara ya Pepo na kuwaongoza kwenye njia iliyo sawa.

Ama wale wenye maradhi katika nyoyo zao, basi inawazidshia uovu juu ya uovu wao.

Kila mwenye kuwa mbali na haki na hali halisi, na imani yake na rai yake ikavutwa kwenye dhati yake na mawazo yake, basi yeye ni mgonjwa wa moyo na akili. Na anapotakiwa kuwa kwenye hukumu halisi na akakataa huzidi maradhi yake.

Unafiki ni maradhi kwa sababu ni upotevu. Wanafiki wa sasa jinsi wanavyopupia dunia ni kama mfano wa funza; kila anavyozidi kujikunja ndio anakuwa mbali zaidi na kutoka mpaka anakufa.

Na wanakufa hali ni makafiri kwa uchaguzi wao mbaya; kama anavyok- ufa funza kwa sababu yake mwenyewe.

Je, hawaoni kwamba wao wanajaribiwa kila mwaka mara moja au mara mbili?

Makusudio ya kujaribiwa hapa ni kufedheheshwa na kufichuka njama zao kwa wote. Aya hii inaambatana na Aya iliyo tangulia: “Na inapoteremshwa Sura …”

Njia ya kuungana ni kuwa wanafiki walikuwa wakimlia njama Mtume(s.a.w.w) na wakimshutumu; kama vile kusema kuwa ni sikio, lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t) alikuwa akimfahamisha Mtume wake njama zao, na Mtume akiwafedhei. Mara nyingine hilo hukaririka zaidi ya mara moja katika mwaka.

Katika hilo kuna dalili mkataa juu ya ukweli wa Mtume na kwamba Qur’ani inatoka mbele ya Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo ilikuwa ni wajibu kwao wapate mawaidha na wamwamini badala ya kudharau na kucheza chere kwa kusema: Ni nani miongoni mwenu amezidishiwa imani hii na hii?

Kisha hawatubu wala hawakumbuki.

Na hawakumbuki ila wenye akili; na hawa wamepofushwa akili zao na nyoyo zao kwa matamanio.

Na inapoteremshwa Sura hutazamana.

Ndivyo walivyo wanafiki kila wakati na kila mahali – wanaposhindwa kuikabili haki kwa hoja basi wanakonyezana, kuonyesha kuzama kwao kwenye ukafiri na upotevu.

Je kuna yeyote anayewaona.

Yaani wanayasema haya kwa mdomo au kwa vitendo:

يَسْتَخْفُونَ مِنَ النَّاسِ وَلَا يَسْتَخْفُونَ مِنَ اللَّـهِ وَهُوَ مَعَهُمْ إِذْ يُبَيِّتُونَ مَا لَا يَرْضَىٰ مِنَ الْقَوْلِ ﴿١٠٨﴾

“Wanajificha kwa watu wala hawajifichi kwa Mwenyezi Mungu, na yeye yu pamoja nao walipokula njama usiku kwa maneno asiyoyapenda” Juz.5 (4:108)

Kisha hugeuka.

Yaani wanafanya wanayoyafanya kisha hugeukia kwenye shughuli zao; kama vile hawakufanya kitu.

Mwenyezi Mungu amezigeuza nyoyo zao kwa kuwa wao ni watu wasiofahamu.

Mwenyezi Mungu amezigeuza nyoyo zao na haki baada ya kuwasimamishia hoja na ubainifu, na baada ya kuwafanyia inadi na kukataa kusalimu amri. Kwa hiyo wao ndio sababu ya moja kwa moja ya kugeuka na ikategemzwa kwa Mwenyezi Mungu kupita kwao.

Ni desturi ya Qur’ani Tukufu kutegemeza mambo mengi ya waja kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuangalia kuwa yeye ni muumbaji wao na mwenye kuutengeneze ulimwengu na vitu vyake.

لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُم بِالْمُؤْمِنِينَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿١٢٨﴾

128. Hakika amewajia Mtume kutokanana nyinyi wenyewe, Yanamhuzunisha yanayo-wataabisha, anawahangaikieni sana, kwa waumini nimpole, mwenye huruma.

فَإِن تَوَلَّوْا فَقُلْ حَسْبِيَ اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَهُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ ﴿١٢٩﴾

129. Basi wakikengeuka, sema: Anitoshelezeaye ni Mwenyezi Mungu, hakuna Mola (apasaye kuabudiwa) ila yeye tu; kwake ninategemea; naye ndio bwana wa Arshi.

KWA WAUMINI NI MPOLE

Aya 128 – 129

MAANA

Hakika amewajia Mtume kutokana na nyinyi wenyewe.

Msemo huu anaambiwa kila mwanadamu anayetafuta uhakika na kutaka kuongozwa kwake. Mtume ni Muhammad bin Abudullah(s.a.w.w) , aliyetumwa na Mwenyezi Mungu kwa watu wote kuwaokoa na ujinga na upotevu na kuwaongoza kwenye njia ya haki na heri.

Analotakiwa kufanya mwenye kutaka njia ya heri na haki ni kuangalia kwa ufahamu tu sera ya Muhammad(s.a.w.w) na desturi yake na Kitabu alichokuja nacho kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Walimwamini mamilioni tangu zamani na sasa, wakiwemo maulama na wanafalsafa walioacha dini ya mababa na mababu, wakakubali Uislamu baada ya kutulia akili zao na nyoyo zao na kumuona Mtume wake mtukufu, kama alivyomsifu Mwenyezi Mungu kwa kauli yake:

Yanamhuzunisha yanayowataabisha, anawahangaikieni sana, kwa Waumini ni mpole, mwenye huruma.

Anahuzunika kwa kila baya linalomfika yeyote aliye ardhini; hata kama ni mnyama; mwenye kuhangaikia uwongofu na wema wa watu wote. Ama upole wake na rehema yake imewaenea watu wote:

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِّلْعَالَمِينَ ﴿١٠٧﴾

“Nasi hatukukutuma ila uwe rehema kwa walimwengu wote” (21:107)

Na miongoni mwa Hadith zake ni: “Mimi ni rehema niliyetolewa zawadi”

“Wenye huruma huwarehemu Mwenyezi Mungu.” “Wahurumieni walio katika ardhi watawahurumia walio katika mbingu”.

Utauliza : Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema kwa Waumini ni Mpole mwenye huruma. Na katika Aya nyingine anasema: Nasi hatukukutuma ila uwe rehema kwa walimwengu wote; yaani waumini na wasiokuwa waumini, Sasa zinaungana vipi Aya mbili?

Jibu : Makusudio ya kauli yake “Nasi hatukutuma ila uwe rehema kwa walimwengu wote,” ni kuwa dini ya Muhammad ni dini ya ubinadamu na sharia yake ni rehema kwa watu wote. Lau kama watu wangelifuata na wakaitumia ardhi ingelijaa heri na uadilifu.

Ama kauli yake Mwenyezi Mungu: “Kwa waumini ni Mpole,” maana yake ni kwamba yeye ni Mpole sana na mwenye huruma kwa anayeamini haki na akajizuia kuwaudhi watu.

Ama anayewafanyia uadui na kuichezea haki yeye anamchukulia ugumu wala hamfanyii upole.

Hii nidyo dini ya utu na rehema. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekataza upole katika kutekeleza hadi (adhabu) kwa wakosaji. Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema:

الزَّانِيَةُ وَالزَّانِي فَاجْلِدُوا كُلَّ وَاحِدٍ مِّنْهُمَا مِائَةَ جَلْدَةٍ وَلَا تَأْخُذْكُم بِهِمَا رَأْفَةٌ فِي دِينِ اللَّـهِ ﴿٢﴾

“Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mpigeni, kila mmoja katika wao, mijeledi mia wala isiwashike huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Mwenyezi Mungu” (24:2)

Anasema Ibin Al-Arabi katika Kitabu Futahahtuli-Makkiyya J2 “Makusudio ya waumini ni wenye kuamini haki na batili, sio wenye kuamini haki tu.” Lakini haya ni katika mambo ya kisufi.

Basi wakikengeuka, sema: Anitoshelezeaye ni Mwenyezi Mungu, hakuna Mola (apasaye kuabudiwa) ila yeye tu; kwake ninategemea; naye ndio bwana wa Arshi tukufu.

Hio ndiyo kazi ya Mtume – kufikisha tu. Mwenye kuongoka ni faida yake na mwenye kupotea ni hasara yake mwenyewe.

Mtume(s.a.w.w) alikuwa na yakini kabisa kwamba Mwenyezi Mungu anamtosha, na ndiye anayempa nguvu za ushindi wake, kwa sababu anamtegemea yeye peke yake.

Tutamalizia Sura hii kwa alivyomalizia Mwenye Tafsir Al-Manar, aliposema:

“Ama uteuzi wake Mwenyezi Mungu mtukufu kwa Bani Hashim, ni kwa kuwa walikuwa wanatofautiana na Maquraishi wote kwa fadhila na ukarimu. Hashim ndiye aliyekuwa mwenye msafara wa Maquraish ambao aliuchukulia ahadi kuuwahami kutoka kwa Kizair wa Roma katika msafara wa kaskazi; na kutoka serikali ya Yemen katika msafara wa kusi.

Yeye ndiye wa mwanzo kuwalisha mafukara na mahujaji wote mkate na mchuzi, Na alimpa malezi ya ukarimu mtoto wake, Abdul-Muttwalib. Kwa ujumla ni kuwa Bani Hashim walikuwa ni wenye tabia njema kuliko Maquraish wote, walikuwa hawana kiburi wala ubinafsi.

Baadhi ya mapokezi yanasema kuwa Aya ya mwisho kushuka ni hii: “Anitoshelezeaye ni Mwenyezi Mungu, hakuna Mola (apasaye kuabudiwa) ila yeye tu; kwake ninategemea; naye ndio bwana wa Arshi tukufu”

MWISHO WA SURA YA TISA: SUART AT – TAWBA

5

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA

Sura Ya Kumi: Suart Yunus

Imeshuka Makka, Inasemekana kuwa Aya tatu au nne zilishuka Madina; maudhui yake ni kama maudhui ya Sura za Makka, ya kuthibitisha misingi ya kiitikadi. Ina Aya 109.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.

الر تِلْكَ آيَاتُ الْكِتَابِ الْحَكِيمِ ﴿١﴾

1. Alif Lam Ra. Hizo ni Aya za Kitab chenye hekima.

أَكَانَ لِلنَّاسِ عَجَبًا أَنْ أَوْحَيْنَا إِلَىٰ رَجُلٍ مِّنْهُمْ أَنْ أَنذِرِ النَّاسَ وَبَشِّرِ الَّذِينَ آمَنُوا أَنَّ لَهُمْ قَدَمَ صِدْقٍ عِندَ رَبِّهِمْ قَالَ الْكَافِرُونَ إِنَّ هَـٰذَا لَسَاحِرٌ مُّبِينٌ ﴿٢﴾

2. Je, imekuwa ni ajabu kwa watu, kwamba tumempa wahyi mmoja wao, kuwa uwaonye watu na uwape bishara wale walioamini kwamba wana cheo kikubwa mbele ya Mola wao? Wakasema Makafiri: “Hakika huyu ni mchawi aliye wazi.”

HIZO NI AYA ZA KITAB CHENYE HEKIMA

Aya 1 – 2

MAANA

Alif Lam Ra.

Yametangulia maelezo kuhusu herufi hisi katika mwanzo wa Sura Baqara Juz.1

Hizo ni Aya za Kitab chenye hekima.

Hizo ni ishara kwamba kila Aya katika Aya za Qur’ani inakusanya hekima.

Je, imekuwa ni ajabu kwa watu, kwamba tumempa wahyi mmoja wao

Wapinzani waliona ajabu Mwenyezi Mungu kuwasiliana na mja miongoni mwa waja wake. Mshangao huu ulikuwa na sababu zifuatazo:-

1. Walimpima Muhammad(s.a.w.w) na wao wenyewe, kwamba ikiwa Mwenyezi Mungu hawasiliani na wao, basi inatakikana asiwasiliane na mwingine.

Jibu la hilo tunalipata katika Aya isemayo:

اللَّـهُ أَعْلَمُ حَيْثُ يَجْعَلُ رِسَالَتَهُ ﴿١٢٤﴾

“Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi, zaidi wa kujua mahali anapoweka ujumbe wake”Juz.8 (6:124)

Yaani Muhammad(s.a.w.w) ana sifa za kumwezesha kuchukua utume kuliko wengine.

2. Wao hawakujua aina ya mawasiliano na Mwenyezi Mungu, wakadhani kwamba kuwasiliana kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu na Muhammad ni sawa na wanavyowasiliana wao kwa wao. Jibu la mawazo haya tunalipata katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَمَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُكَلِّمَهُ اللَّـهُ إِلَّا وَحْيًا أَوْ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ أَوْ يُرْسِلَ رَسُولًا ﴿٥١﴾

“Na haiwi kwa mtu kusema na Mwenyezi Mungu ila kwa wahyi au nyuma ya pazia au humtuma mjumbe…” (42:51)

3. Kwamba Muhammad aliwaletea lile wasiloliitakidi wala kuzoweya. Na hili ndilo muhimu zaidi.

Jibu lake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

قَالَ لَقَدْ كُنتُمْ أَنتُمْ وَآبَاؤُكُمْ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٥٤﴾

“Akasema: Hakika nyinyi na baba zenu mlikuwa katika upotevu uliowazi” (21:54)

Kuwa uwaonye watu na uwape bishara wale walioamini kwamba wana cheo kikubwa mbele ya Mola wao.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kubainisha kustajabu kwa makafiri wahyi kwa Muhammad(s.a.w.w) , anabainisha hakika ya aliyoyatumia wahyi kuwa ni maonyo na bishara – kumuonya na adhabu kali yule anayehalifu na kuasi amri ya Mwenyezi Mungu na kumpa bishara ya thawabu yule anayefuata amri. Thawabu zimetajwa kwa ibara ya cheo kikubwa.

Ikiwa wahyi wenyewe ndio huu na Muhammad(s.a.w.w) akawa na sifa za kuuchukua na kuufikisha, sasa yako wapi maajabu?

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hawezi kuwaacha watu bila ya kuwatumia mjumbe mwaminifu awafikishie wanayoyataka katika heri na wanayoyachukia katika shari, wajiepushe na hili na wafanye lile. Na pia ili wasiwe na hoja, kama wakihalifu. Na Muhammad(s.a.w.w) ndiye mwaminifu wa ujumbe huu kuliko watu wengine. Kwa hiyo imepasa yeye awe ndiye mjumbe wa Mwenyezi Mungu.

Wakasema Makafiri: Hakika huyu ni mchawi aliye wazi.

Walimsifu Muhammad(s.a.w.w) kwa uchawi, kwa vile wao waliikana Qur’ani kuwa ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Vile vile walishindwa kuleta Sura iliyo mfano wake, Kwa hiyo hawakubakiwa na jingine ila kudai uchawi tu. Walishindwa na wakajitia kushindwa kujua kuwa kila lililo katika Qur’ani ni hakika isiyo na shaka, na kwamba uchawi ni uwongo usio na msingi.

إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ يُدَبِّرُ الْأَمْرَ مَا مِن شَفِيعٍ إِلَّا مِن بَعْدِ إِذْنِهِ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ فَاعْبُدُوهُ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ ﴿٣﴾

3. Hakika Mola wenu ni Mwenyezi Mungu ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita, kasha akastawi juu ya Arshi, Yeye hutengeneza mambo. Hakuwa mwombezi ila baada ya idhini yake, Huyo ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wenu, basi mwabuduni, Je hamkubuki?.

إِلَيْهِ مَرْجِعُكُمْ جَمِيعًا وَعْدَ اللَّـهِ حَقًّا إِنَّهُ يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ لِيَجْزِيَ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ بِالْقِسْطِ وَالَّذِينَ كَفَرُوا لَهُمْ شَرَابٌ مِّنْ حَمِيمٍ وَعَذَابٌ أَلِيمٌ بِمَا كَانُوا يَكْفُرُونَ ﴿٤﴾

Kwake ndiye marejeo yenu nyote, Hii ni ahadi ya Mwenyezi Mungu iliyo ya kweli. Hakika yeye ndiye anayeanzisha kiumbe kasha hukirejesha ili awalipe wale walioamini na wakafanya amali njema kwa uadilifu. Na waliokufuru, watapata kinywaji cha maji yachemkayo na adhabu chungu kwa kuwa walikuwa wakikufuru.

KUUMBA KATIKA SIKU SITA

Aya 3 – 4

MAANA

Hakika Mola wenu ni Mwenyezi Mungu ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha akatawala juu ya Arshi, Yeye hutengeneza mambo yote.

Siku za Mwenyezi Mungu si kama siku zetu hizi, Zingelitokea wapi siku kabla ya kuumbwa ulimwengu? Kwa hiyo makusudio ya siku hapa ni awamu au vipindi. Ama Arshi ni kutawala. Aya hii imetangulia pamoja na tafsir yake katika Juz. 8 (7:54)

Hakuna mwombezi ila baada ya idhini yake.

Vile vile hii imetangulia katika Juz.3 (2:255)

Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu, basi mwabuduni.

Kwa sababu yeye ndiye anayestahiki kuabudiwa, Ama mali, nasabu na ufalme sio Mungu wa kuabudiwa wala nguvu ya kunyeyekewa.

Je, Hamkumbuki?

Kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja peke yake anayestahiki kuabudiwa.

HISABU NA MALIPO NI LAZIMA

Kwake yeye ndiyo merejeo yenu nyote.

Hii ni ahadi ya Mwenyezi Mungu iliyo ya kweli.

Hakika yeye ndiye anayeanzisha uumbaji kisha ataurejesha.

Suala la kuanzishwa na kurudishwa kiumbe ni moja ya mushkeli mkubwa wa kifalsafa, Watu wengine wanasema ulimwengu ulipatikana wenyewe tu bila ya kuweko mpatishaji.

Fikra hii ni sawa na mtu aliyeona mandishi, kisha aseme yamepatikana kibahati; kwa vile tu hakumwona mwandishi kwa macho yake. Yule aliyechora ulimwengu ni mkuu zaidi kuliko aliyechora msitari kwa wino juu ya karatasi.

Jicho ni duni sana kuweza kumwona; na akili zimemwona katikati njia zinazosababishia kumwamini.

Tumetunga vitabu viwili kuhusu njia hizo: Allahu Wal-aq’ na Falsafa Tul- Maad. Baadhi yake tumezielezea kwa ufupi katika Juz. 1 (2:21) na Juz. 4 (3: 190)

Ama kufufuliwa wafu, kurudishwa mara ya pili kwa hisabu na malipo kumeelezwa na wahyi na wala akili haikatai, kwa hiyo ni wajibu kuku- sadiki na kukuamini.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amebainisha hekima ya kurudishwa wafu kwa kusema:

Ili awalipe kwa uadilifu wale walioamini na wakatenda mema. Na waliokufuru, watapata kinywaji kinachochemka na adhabu chungu kwa vile walivyokuwa wakikufuru.

Mwenyezi Mungu amemwezesha mtu kutenda na akampa akili inayopambanua kheri na shari akamwamrisha hili na akamkataza lile. Basi akamtii mwenye kumtii na akamwasi mwenye kumwasi.

Kila mmoja akaingia shimo lake, bila ya kupewa thawabu mtiifu wala kuadhibiwa mwasi, Tena waasi wengi wanapetuka mipaka na kufanya dhulma na kuijaza dunia dhulma na jeuri bila ya kuulizwa na yeyote.

Tukichukulia kuwa hakuna ufufuo wala hisabu basi maana yake ni kuwa dhalimu na mdhulumiwa na mumin na kafir ni sawa, bali kafiri atakuwa ni bora kuliko mumin; na taghut mharibifu atakuwa mtukufu kuliko yule aliyekufa shahidi katika njia ya radhi yake.

Hakuna shaka kuwa haya yanapingana na uadilifu wa Mwenyezi Mungu, na hekima yake na uwezo wake; bali hata na kuweko kwake Mwenyezi Mungu. Ametakata Mwenyezi Mungu na hayo kutakata kukubwa.

Tumeona wadhulimiwa wengi wakipiga kelele wakisema: Lau Mwenyezi Mungu angelikuwako kusingelibakii dhalimu yeyote katika ardhi.

Kauli hii haifahamishi chochote isipokuwa kuakisi matakwa ya kuweko mwadilifu mwenye uwezo atakayemchukulia kisasi mdhulumiwa, Lakini wamefanya haraka kwa uchungu, wakasahau maumbile aliyowaumbia Mwenyezi Mungu[3] , ndio wakasema waliyoyasema.

Nimeandika vitabu na makala kuhusu ufufuo, hisabu na malipo. Vilevile wakati wa kufasiri Aya inayoambatana na hayo, Na sasa Aya hii tena inanirudisha. Nimepata kufahamu kuwa dalili yenye nguvu ya kuthibitisha ufufuo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

الْيَوْمَ تُجْزَىٰ كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ لَا ظُلْمَ الْيَوْمَ إِنَّ اللَّـهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ ﴿١٧﴾

“Leo italipwa kila nafsi kwa iliyoyachuma, hapana dhulma leo, Hakika Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuhisabu.” (40:17)

Ayah hii ni kama Aya tuliyonayo, lakini hii iko wazi zaidi, inajichukulia dalili yenyewe na kujijibu. Inasema: Leo italipwa kila nafsi kwa iliyoyachuma, kwa nini? Kwa sababu hakuna dhulma kwa Mwenyezi Mungu bali yeye ni mwepesi wa kuhisabu.

Utatuzi wa kiakili wa suala hili ni kwamba lau sio siku hii ambayo kila mtu atalipwa, basi Mwenyezi Mungu angelikuwa dhalimu, kuweko kwake ni mateso na sharia zake ni mchezo: Ametakata Mwenyezi Mungu (s.w.t) na wanayombandika.

Kwa hiyo natija ya mwisho ya mantiki haya ni kwamba kila mwenye kukana ufufuo, hisabu na malipo atakuwa amekana kuweko Mwenyezi Mungu, atake asitake.

هُوَ الَّذِي جَعَلَ الشَّمْسَ ضِيَاءً وَالْقَمَرَ نُورًا وَقَدَّرَهُ مَنَازِلَ لِتَعْلَمُوا عَدَدَ السِّنِينَ وَالْحِسَابَ مَا خَلَقَ اللَّـهُ ذَٰلِكَ إِلَّا بِالْحَقِّ يُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ ﴿٥﴾

5. Yeye ndiye aliyefanya jua kuwa mwanga na mwezi kuwa nuru, na akaupimia vituo ili mjue idadi ya miaka na hisabu. Mwenyezi Mungu hakuviumba hivyo ila kwa haki. Anazipambanua Aya kwa watu wanaojua.

إِنَّ فِي اخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَمَا خَلَقَ اللَّـهُ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَّقُونَ ﴿٦﴾

6. Hakika katika kuhitalifiana usiku na mchana na alivyoviumba Mwenyezi Mungu katika mbingu na ardhi kuna ishara kwa watu wamchao.

إِنَّ الَّذِينَ لَا يَرْجُونَ لِقَاءَنَا وَرَضُوا بِالْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَاطْمَأَنُّوا بِهَا وَالَّذِينَ هُمْ عَنْ آيَاتِنَا غَافِلُونَ ﴿٧﴾

7. Hakika wale wasiotaraji kuku- tana nasi na wakawa radhi na maisha ya dunia na wakatua nayo, na wale walioghafilika na ishara zetu.

أُولَـٰئِكَ مَأْوَاهُمُ النَّارُ بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٨﴾

8. Hao makazi yao ni motoni kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ يَهْدِيهِمْ رَبُّهُم بِإِيمَانِهِمْ تَجْرِي مِن تَحْتِهِمُ الْأَنْهَارُ فِي جَنَّاتِ النَّعِيمِ ﴿٩﴾

9. Hakika wale walioamini na wakatenda mema, Mola wao atawaongoza kwa sababu ya imani yao. Itapita mito chini yao katika Mabustani yenye neema.

دَعْوَاهُمْ فِيهَا سُبْحَانَكَ اللَّـهُمَّ وَتَحِيَّتُهُمْ فِيهَا سَلَامٌ وَآخِرُ دَعْوَاهُمْ أَنِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٠﴾

10. Wito wao humo ni: Umetakasika eweMwenyezi Mungu! Na maamkuzi yao ni ‘Salaam’ na mwisho wa wito wao ni: ‘Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu wote.

IDADI YA MIAKA NA HISABU

Aya 5 – 10

MAANA

Yeye ndiye aliyefanya jua kuwa mwanga na mwezi kuwa nuru.

Imesemekana kuwa mwanga na nuru yana maana moja, Na ikasemekana kuwa maana yanatofautiana. Neno mwanga linafahamisha kuwa nuru yake haitegemei kitu kingine; na neno nuru lina maana ya kuwa nuru yake imetokana na kitu kingine; kama vile nuru ya mwezi iliyotokana na jua.

Lakini ilivyo ni kuwa Aya haikuja kubainisha chochote katika hayo, isipokuwa makusudio ni kutanabahisha umoja wake Mwenyezi Mugu na uwezo wake; sawa na Aya iliyotangulia; na kwamba hekima ya jua na mwezi ni ile aliyoashiria Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kauli yake:

Na akaupimia vituo ili mjue idadi ya miaka na hisabu.

Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameufanyia mwezi vitu visivyobadilika wala kugeuka; sawa na desturi nyngine za maumbile. Makusudio ya kutogeuka huko ni kudhibiti nyakati ambazo uhai hauwezi kutimia ila kwazo.

Hayo tumeyazungumzia kwa ufafanuzi katika Juz.7 (6:96) na Juz.10 (9:36).

Mwenyezi Mungu hakuviumba hivyo ila kwa haki. Anazipambanua ishara kwa watu wanaojua.

Mwenyezi Mungu amepambanua ishara za ulimwengu kimaumbile na kupatikana, na kwa kufafanua na kubainisha ili azingatie vizuri kila ambaye Mwenyezi Mungu amempa maandalizi ya kuchunguza na kutia akilini jambo ambalo linapelekea kumwamini Mwenyezi Mungu, uwezo wake na hekima yake.

Yametangulia maelezo, mara kadhaa, kuwa Mwenyezi Mungu mtukufu hutegemeza dhahiri za kiulimwengu na mabadiliko kwenye desturi yake ya kimaumbile ili mtu, daima, abakie kukumbuka muumbaji wa yaliyo katika ulimwengu.

Hakika katika kuhitalifiana usiku na mchana na alivyoviumba Mwenyezi Mungu katika mbingu na ardhi kuna ishara kwa watu wamchao.

Umetangulia mfano wa Aya hii na tafsiri yake katika Juz.2 (2:164).

Hakika wale wasiotaraji kukutana nasi na wakawa radhi na maisha ya dunia na wakatua nayo, na wale walioghafilika na ishara zetu.

Aya hii ni kemeo na kiaga kwa yule asiyeamini akhera na hisabu yake, kwa kusema kuwa aliyekufa yake yamekwisha. Akiyasema haya kwa kusukumwa na hawa zake na matamanio yake akiwa ameghafilika na ulimwengu na yaliyomo ndani yake yakiwa ni pamoja na mazingatio mawaidha na mito ya Mitume na watu wema.

Hao makazi yao ni motoni kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.

Haya ndiyo malipo ya kila mwenye kukadhibisha siku ya malipo na akayafanya matamanio yake ndiyo Mola wake, bila ya kujali haki wala uadilifu.

Ilivyo ni kuwa makemeo haya hayahusiki na mwenye kukana kukutana na Mwenyezi Mungu kwa kauli na vitendo tu, bali yanamhusu pia yule mwenye kuamini kinadharia tu, lakini akakana kimatendo. Kwa hiyo wanaoswali na kufunga wakiwa wanaamini hisabu na adhabu, kisha wasichunge haramu ya Mwenyezi Mungu watakuwa katika Jahanam pamoja na wanaopinga hisabu.

WAKO WAPI WACHA MUNGU?

Hakika wale walioamini na wakatenda mema, Mola wao atawaongoza kwa sababub ya imani yao. Itapita mito chini yao katika Mabustani yenye neema.

Makusudio ya kuongozwa hapa ni thawabu; yaani Mwenyezi Mungu atawalipa thawabu kwa sababu ya imani yao.

Mwenyezi Mungu (s.w.t), katika Aya zilizotangulia, amewataja wapinzani na sifa zao na mwisho wao. Katika Aya hii anawataja waumini, sifa zao na mwisho wao; kama desturi yake Mwenyezi Mungu Mtukufu yakutaja vitu na vinyume vyake.

Kwa hiyo waumini wako kinyume na wapinzani, wanatarajii kukutana na Mwenyezi Mungu, wanachunga miko yake kwa mujibu wa dini yao na imani yao. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawapa thawabu ya Pepo ipitayo mito chini yake.

Yamekuja maelezo katika Hadith kuwa Muumba, Mwenyezi Mungu Mtukufu, atasema siku ya Kiyama: “Leo nitaondoa nasabu yenu na niweke nasabu yangu, Wako wapi wacha mungu? Huo ndio mwito wa Mwenyezi Mungu siku hiyo ya haki ‘wako wapi wacha Mungu, walio wakweli katika kauli zao wenye ikhlasi katika vitendo vyao’. Ama mwito wa shetani hapa duniani, nyumba ya dhulma na ufisadi, ni: Wako wapi mataghuti wanaovunja miko walio wafisadi?

Kila mwenye kumtukuza mumin kwa sababu ya imani yake na takua yake, basi atakuwa ametoa mwito wa Mwenyezi Mungu ‘wako wapi wacha Mungu’ Na kila mwenye kumheshimu taghuti kwa makosa yake, basi atakuwa ametoa mwito wa Sheitan ‘wako wapi wakosaji’

Imam Ja’far As-Swadiq(a.s) anasema: “Ni makruh kumsimamia mtu kwa kumheshimu ila mtu wa dini” Na akasema tena: “Usibusu mkono wa yoyote ila mkono wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) au wa anayekusudiwa kwaye Mtume(s.a.w.w) .

Hukumu ya kumheshimu mtu inatofautiana kulingana na hali ilivyo. Ikiwa ni kwa kutia mori wa dhambi na maasi ya Mwneyezi Mung basi ni haramu. Ikiwa ni kwa mapenzi na mshikamano au kutekeleza haja ya mhitaji basi ni kuzuri.

Ama kumheshimu na kumtukuza mpigania jihadi kwa juhudi yake, mwenye ikhlasi kwa ikhlasi yake, msuluhishaji kwa suluhu yake na ulama kwa elimu yake, basi hiyo ni katika kuadhimisha nembo za Mwenyezi Mungu na miko yake, ambako amekuashiria kwa kusema:

وَمَن يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّـهِ فَإِنَّهَا مِن تَقْوَى الْقُلُوبِ ﴿٣٢﴾

“Na anayezitukuza alama za Mwenyezi Mungu, basi hilo ni katika uchaji wa Moyo” (22:32).

ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ حُرُمَاتِ اللَّـهِ فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ عِندَ رَبِّهِ ﴿٣٠﴾

“Na anayevitukuza vitu vitakatifu vya Mwenyezi Mungu, basi hiyo ni heri kwake mbele ya Mola wake…” (22:30).

Wito wao humo ni ‘Umetakasika ewe Mwenyezi Mungu! Na maamkuzi yao ni ‘Salaam’ na mwisho wa wito wao ni: ‘Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu Wote.’

Aya hii kwa ujumla inaelezea habari za watu wa Peponi wakiwa katika raha hawashughlishwi na lolote katika yale yaliyokuwa yakiwashughulisha duniani ya kutaka masilahi au kukinga madhara; hawataki uadilifu wala amani, au kuzidishiwa malipo na cheo.

Hawataki chochote kwa sababu kila kinachotamaniwa na nafsi na kuburudisha macho kiko tayari; wakitaka kitu kazi yao ni kukifikiria tu katika nyoyo zao.

Kwa ajili hiyo wanajishughulisha na Tasbih na Tahmid tu:

لَا يَسْمَعُونَ فِيهَا لَغْوًا وَلَا تَأْثِيمًا ﴿٢٥﴾ إِلَّا قِيلًا سَلَامًا سَلَامًا ﴿٢٦﴾

“Hawatasikia humo porojo wala maneno ya dhambi, isipokuwa maneno: Salaam, Salaam”.(56:25–26).

Salam hii waliisikia kutoka kwa Mwenyezi Mungu walipokutana naye:

تَحِيَّتُهُمْ يَوْمَ يَلْقَوْنَهُ سَلَامٌ وَأَعَدَّ لَهُمْ أَجْرًا كَرِيمًا ﴿٤٤﴾

“Maamkuzi yao siku ya kukutana naye yatakuwa ni Salaam” (33:44)

Salaam hiyo wataisikia kutoka kwa Malaika:

وَقَالَ لَهُمْ خَزَنَتُهَا سَلَامٌ عَلَيْكُمْ طِبْتُمْ فَادْخُلُوهَا خَالِدِينَ ﴿٧٣﴾

“Na walinzi wake watawaambia: Salaamun Alaykum, furahini, iingieni make milele (39:73).

Na, pia wataamkiana wenyewe kwa wenyewe.

Tumezungumzia kuhusu Maamkuzi ya Kiislam katika Juz.7 (6:54).