SUALA LA KUPOTOSHWA QURANI

BSMILAHI AR-RAHMANI AR-RAHIIMI.

SUALA LA KUPOTOSHWA QURANI

Swali:
Ni vipi kuhusu zile Hadith zisemazo kwamba baadhi ya Aya si sehemu ya Qur'an? Shia hawaamini kwamba mwandishi au mpokezi ana kinga ya kutofanya makosa, na kwa hivyo hawachukulii kwamba Hadith zote ni sahihi. Kitabu pekee chenye kinga ya kutokuwa na kosa lolote ni Qur'an. Mara nyingi Hadith hizi huchukuliwa kuwa ni dhaifu au maneno uliyo teremshwa nje ya Qur'an.

" Ni vizuri itajwe kwamba kuna baadhi ya Hadith kwenye Sahih al-Bukhari na Sahih Muslim zisemazo kwamba Aya nyingi za Qur'an haziko. [Al-Bukhari, Al-Sahih, Juz. 8 Uk. 208; Muslim, Al-Sahih, Juz. 3 Uk. 1317]. " Si hivyo tu, Hadith hizi za Sunni zadai kwamba Sura mbili za Qur'an hazipo, ambapo mojawapo ni kama ya Sura ya al-Bara'ah (Sura ya 9) kwa kirefu!!! [Muslim, Al-Sahih, Kitab al-Zakat, Juz. 2 Uk. 726]. " Hata kuna baadhi ya mapokezi ya Hadith ya Sunni yanayodai kuwa Sura ya al-Ahzab (33) ilikuwa ni ndefu kama ilivyo Sura ya al-Baqarah (2)!!! Ambapo hakika Sura ya al-Baqarah ndio Sura iliyo kubwa zaidi katika Qur'an. Kuna hata Hadith ndani ya Sahih al-Bukhari na Muslim ambazo zimetaja kwa urefu baadhi ya Aya ambazo hazipo. [Al-Bukhari, Al-Sahih, Juz. 8 Uk. 208].

Kwa bahati nzuri, Shia katu hawajawatuhumu ndugu zao Sunni kwa kuamini kwamba Qur'an haikukamilika. Sisi tunasema kwamba Hadith hizi za Sunni, ama ni dhaifu, au zimezushwa.

Hitimisho:
"Sisi twaamini kwamba Qur'an ambayo Mwenyezi Mungu alimteremshia Mtume wake Muhammad (s.a.w.w.) ni kama ile iliyoko baina ya jalada mbili. Na ndiyo hiyo hiyo iliyoko mikononi kwa watu, na haina tofauti zaidi ya ile… Na anayedai kuwa sisi tunasema kwamba (Qur'an) ni tofauti kuliko hii (ya sasa), huyo ni muongo." [As-Saduq, Kitabu'l-I`tiqadat (Tehran: 1370 AH) Uk. 63; Tafsir ya kiingereza, The Shi'ite Creed, tr. A.A.A. Fyzee (Calcutta: 1942) Uk. 85]. Kwa hakika sisi tumeuteremsha ukumbusho huu (Qur'an) na hakika sisi ndio tuulindao. (Qur'an: Sura 15, Aya 9)
Je Mashia wanaamini Qur'an nyingine?
Mashia mara kwa mara wanatuhumiwa kwa imani ya Tahrif ndani ya Qur'an, ambayo maana yake ni kuamini kwamba Qur'an imepotoshwa na haiko sawa na ile aliyoteremshiwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.).

HII SI KWELI!!!
Wanavyuoni wakubwa wote wa Shi'ah Imaamiya tangu siku za mwanzo hadi karne za sasa wanaamini kuwa Qur'an imehifadhiwa kikamilifu. Wanavyuoni mashuhuri wa Shia wa mwanzoni wamesema hivi wazi katika vitabu vyao, miongoni mwao ni: " Shaykh al-Saduq (aliyefariki 381 AH), Kitabu'l-Itiqadat, (Teheran.1370) Uk. 63;

" Shaykh al-Mufid (aliyefariki 413 AH), Awa'ilu l-Maqalat, Uk. 55-6;
" Sharif al-Murtadha (aliyefariki 436 AH), Bahru 'l-Fawa'id (Teh, 1314) Uk. 69;
" Shaykh at-Tusi (aliyefariki 460 AH), Tafsir at-Tibyan, (Najaf, 1376), Juz. 1 Uk. 3;
" Shaykh at-Tabrasi (548AH), Majma'u 'l-Bayan, (Lebanon), Juz. 1 Uk. 15.

Baadhi ya Wanavyuoni waliokuja baadaye waliotoa maoni kama hayo ni:
" Muhammad Muhsin al-Fayd al-Kashani (aliyefariki 1019 AH), Al-Wafi, Juz. 1 Uk. 273-4, na al-'Asfa fi Tafsir al-Qur'an, Uk. 348;
" Muhammad Baqir al-Majlisi (aliyefariki 1111 AH), Bihar al-'Anwar, Juz 89 Uk. 75.

Imani hii iliendelea bila ya kukatizwa mpaka leo hii. Wanavyuoni wa Shia wa karne hii waliokariri imani hii, kwamba Qur'an imehifadhiwa kikamilifu na haikubadilishwa, ni wale miongoni mwa wenye majina mashuhuri kama vile Sayyid Muhsin al-Amin al-'Amili (aliyefariki 1371 AH); Sayyid Sharaf al-Din al-Musawi (aliyefariki 1377 AH.); Shaykh Muhammad Husein Kashif al-Ghita' (aliyefariki 1373 AH); Sayyid Muhsin al-Hakim (aliyefariki 1390 AH); 'Allamah at-Tabataba'i (aliyefariki 1402 AH); Sayyid Ruhullah al-Khumayni (aliyefariki 1409 AH); Sayyid Abu al-Qasim al-Khu'i (aliyefariki 1413 AH) na Sayyid Muhammad Ridha al-Gulpaygani (aliyefariki 1414 AH).Hii, kwa kweli, si orodha nzima.
Swali:
Lakini ni vipi kuhusu Mashia waliokuwapo kabla ya Wanavyuoni hawa, je wao waliamini tahrif? Hapana! Hebu chukulia mfanio wa 'Ubaydullah b. Musa al-'Absi (120-213 AH), Mwanachuoni wa Shia mwaminifu ambaye masimulizi yake kutoka kwa Maimamu yanapatikana katika mkusanyo wa Hadith wa Shia kama vile al-Tahdhib na al-Istibsar. Hebu na tuangalie baadhi ya Wanavyuoni wa Sunni wanasema nini kumhusu: " "... ni mcha Mungu, miongoni mwa Wanavyuoni muhimu wa Shia ...alikubaliwa kuwa mwaminifu na Yahya b. Ma'in. Abu Hatim amesema: 'Alikuwa mwaminifu, mkweli...' al-'Ijli amesema kwamba yeye alikuwa ni mtu mwenye cheo kikuu katika elimu ya Qur'an..."

[Al-Dhahabi, Tadhkirat al-Huffaz (Haydarabad, 1333 AH), Juz. 1 Uk. 322] " "...Yeye alikuwa ni Imam katika Fiqh, Hadith na Qur'an, alisifika kwa uchaji Mungu na wema, lakini alikuwa mmoja kati ya wakuu wa Shia." [Ibn al-'Imad al-Hanbali, Shadharat al-Dhahab (Cairo, 1350 AH), Juz. 2 Uk. 29] Kama wanavyuoni hawa wa Sunni wangeona kuwa yeye aliamini kuwapo kwa Qur'an nyingine, basi hata mmoja wao asingelimsifu kwa ujuzi wake! Na Ubaydullah alikuwa akichukuliwa kuwa ni mwaminifu sana, licha ya kuwa alikuwa ni Shia, kiasi kwamba Wanavyuoni maarufu wa kisunni wa Hadith, al-Bukhari, Muslim na wengineo wengi, katika mikusanyiko ya Hadith, wamechukuwa Hadith kutoka kwake! [The Creed of the Imaam of Hadeeth al-Bukhari (Salafi Pub., UK, 1997), Uk. 87-89]

Swali:
Je Shia hawaamini Msahafu wa Fatimah ambao mkubwa mara tatu ya ukubwa wa Qur'an? Qur'an ni Mushaf (Kitabu), lakini, si kwamba kila kitabu lazima kiwe Qur'an! Hakuna kamwe "Qur'an ya Fatimah"! Mushaf Fatimah kilikuwa ni kitabu kilichoandikwa au kuelezwa na Fatimah (a.s.) baada ya kufariki Mtume (s.a.w.w). Hicho si sehemu ya Qur'an na hakina uhusiano wowote na amri za Mwenyezi Mungu au hukmu za kisharia.

Swali:
Lakini je, hakuna Hadith katika vitabu vya Shia zinazotaja Aya za Qur'an zenye maneno mengine zaidi ya hii tuliyo nayo leo? Kuna baadhi ya mifano ambapo maneno zaidi yametajwa lakini kwa minajili ya kufafanua tu, haimaanishi kwamba Aya asili za Qur'an zimegeuzwa. Hii hutokea pande zote, kwa upande wa Shia na wa Sunni. Hebu zingatia mifano ifuatayo, yote ni kutoka upande wa sherhe maarufu za Qur'an za Sunni: " "Ubayy b. Ka'b alikuwa akisoma '…basi wale mnao faidi nao kwa kipindi maalum, wapeni mahari yao kama ilivyoamriwa…' (Qur'an, Sura 4, Aya 24), na Ibn Abbas pia alikuwa akisoma hivyo hivyo." [Fakhr al-Din al-Razi, Mafatih al-Ghayb (Beirut, 1981), Juz. 9 Uk. 53] [Ibn Kathir, Tafsir al-Qur'an al-'Adhim (Beirut, 1987), Juz. 2 Uk. 244]

Maelezo yaliyomo katika hashia ya Tasfir ya Ibn Kathir yanafafanua kwamba maneno yaliyoongezwa hapo juu, ambayo si sehemu ya Qur'an, yalisomwa na maswahaba wa Mtume (s.a.w.w.) kwa ajili ya tafsir na ufafanuzi tu. " "Ibn Mas'ud amesema: "Wakati wa Mtume (s.a.w.w.) tulikuwa tukisoma, 'Ewe Mtume wetu (Muhammad) fikisha lile ulilotumwa kutoka kwa Mola wako nalo ni 'Ali ni Bwana wa Waumini na kama hukufanya, basi hujafikisha ujumbe Wake.'" (Qur'an Sura 5, Aya 67). [Jalal al-Din al-Suyuti, Durr al-Manthur, Juz. 2 Uk. 298] Katika hali hii pia inavyoonyesha, kipande kilichoandikwa kwa mshazari (italics) kwa hakika si sehemu ya Qur'an, hata hivyo, swahaba Ibn Mas'ud alikuwa akisoma hivyo alipokuwa akifafanua ufunuo wa Qur'an.

MWISHO