MAFUNZO YA QURANI

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

MAFUNZO YA QURANI

 Njia , haja na sababu za mabadiliko katika jamii
KWA mujibu wa Qur-an zipo sababu kadhaa ambazo huchochea mabadiliko makubwa katika jamii. Miongoni mwa hizo kuu zimetajwa kuwa ni:
(1). Kushitadi kwa maovu, dhulma na ukandamizaji
(2) Watu wanaoamrisha mema na kukataza mabaya
(3) Kutetea na kulinda maadili mema
(4) Migongano na migogoro(conflicts) kati ya makundi yenye nguvu katika jamii; moja likitaka kuondoa lingine ili kuondoa au kupunguza dhulma na ukandamizaji.
1. Kushitadi kwa maovu, dhulma na ukandamizaji Kushitadi kwa maovu, ufisadi, ukandamizaji na dhulma ni sababu ya kwanza inayoweza kuchochea mabadiliko. "Hakika Firauni alitakabari katika ardhi, akawafanya watu wa huko makundi mbali mbali. Akalidhoofisha kundi moja miongoni mwao, akiwachinja watoto wao wanaume na kuwaacha hai watoto wao wanawake. Hakika yeye alikuwa miongoni mwa waharibifu(kabisa).Na tukawafanyia ihsani wale waliodhoofishwa katika ardhi hiyo na kuwafanya viongozi, na kuwafanya warithi(wa neema hizo).

Na kuwapa nguvu ardhini; na kumwonyesha Firauni na Hamana na majeshi yao, yale waliyokuwa wakiyaogopa". (28:3-6). Aya hizi zinatufahamisha mabadiliko yaliyotokea baada ya kudumu muda mrefu utawala wa kabaguzi wa Mafarao (Firaun) nchini Misri ambao ulichinja bila huruma kila mtoto wa kiume aliyezaliwa na jamii ya kiyahudi. Baada ya muda mrefu wa mauaji hayo hatimaye msaada wa Allah ukawa juu ya wale waliodhulumiwa huku dhalimu na majeshi yake wakiangamia. Haya yalikuwa mabadiliko makubwa ya kihistoria.

Tawala mbali mbali hivi leo zimekuwa zikichinja watu kwa makundi kwa njia zinazokubaliana na mazingira ya sasa. Kwa mfano hapa kwetu kundi kubwa la vizazi vya hali za chini kwa makusudi limekuwa 'likichinjwa' kielimu na kupotezewa roho ya namna ya kuyaendea mazingira yao. Ni unyama ulio mbaya zaidi kuliko wa zama za Firauni ambao ulikomea kumuua mtu kimwili. Kutokana na dhulma hizi si muda mrefu jamii itegemee mabadiliko ya kihistoria.

Qur-an huitazama jamii kwa mitazamo miwili; mtazamo wa kwanza ni ule unaotua katika kuangalia mgawanyiko wa watu katika hali za maisha (material conditions) ambapo tabaka la wachache hujipa haki ya umiliki wa mali na rasilimali za jamii likilenga kunufaisha familia, kabila au koo zao chini ya 'cover' la utawala ambalo huwatengenezea mazingira mazuri ya kuweza kuwafanya waishi raha mustarehe huku tabaka la wengi likitaabika kwa kukosa hata mahitaji muhimu ya maisha; mtazamo wa pili unaangalia suala la maadili linavyoweza kugawa kambi mbili hasimu huku moja ikishajiisha maovu:
"Na kadhalika tulijaalia kila mji wakuu(watawala) wao ndio waovu (mujirimuun). Ikawa humo wanafanya hila. Wala hawafanyii hila isipokuwa nafsi zao, lakini hawatambui. (6:123). Vitendo vya dhulma, ukandamizaji na ufisadi hukithiri sambamba na kutakabari kwa watawala ambao hutumia hila mbali mbali kuwanyamazisha watu wema wenye kuwakilisha malalamiko ya wengi kama Qur'an inavyotufahamisha: "Wakasema wale watawala waliokufuru katika watu wake: "Hakuwa huyu (Nuhu) ila ni mtu kama nyinyi. Anataka kujipatia umaarufu juu yenu. Na kama Mwenyezi Mungu angependa (kukufundisheni), kwa yakini angeliteremsha Malaika. Hatukusikia haya kwa wazee wetu wa mwanzo".(7:65)

Tabia ya dharau, propaganda, kejeli na vitisho vya watawala inapokithiri watu hushindwa kuvumilia, huanzisha harakati kupinga mfumo dhalimu na hatimaye mapambano ambayo baadaye husababisha mabadiliko makubwa ya kijamii. Qur'an imetumia staili na istilahi maalum kuelezea migawanyiko hasimu ya kitabaka yenye kuweza kuzaa mabadiliko makubwa ya kihistoria katika jamii:
Kwanza kuna kule kujitokeza uhasama wa kitabaka katika haki ya kila mtu kupata mahitaji ya msingi(basic human needs) bila kukwazwa. Mahitaji hayo ni pamoja na chakula, makazi, mavazi, elimu na matibabu ambapo kwa upande mmoja historia imeshuhudia kuwepo kwa tabaka tawala fisadi (corrupt dominant class) linalomiliki na kujilimbikizia haki hizi kisha kuzuia zisifike kwa wengine, ambalo hukataa kata kata kurejea kwenye haki.

Tabaka hili limetajwa kwa istilahi tafauti katika Qur'an baadhi ya hizo ni; mal'au (system makhsusi) au tabaka tawala la wachache (ruling clique) lenye kupanga na kuendesha mambo; mustakbiruun yaani tabaka lililotakabari la wanyonyaji, wakandamizaji na watumia mabavu (The arrogant, oppressors,tyrants); Dhaalimuun yaani madhalimu wanaodhulumu au kuzuia aina zote za haki katika jamii; mujrimuun yaani maharamia, majambazi, waporaji, waharibifu na wachafuzi wa mazingira ya kiuchumi, kisiasa; mufsiduun yaani mafisadi wenye kufisidi maadili ya jamii na kuponda mali au rasilimali zilizozunguka jiografia ya mahali husika; na mutrafuun yaani wenye tamaa na wapupiaji wa sifa, hadhi na utajiri wa mali na anasa.

Faarihiin wenye kujiona, kujigamba na kujifakharisha kwa utajiri au elimu waliyonayo kama inavyojitokeza kwa Qaaruun:
"Hakika Qaaruun alikuwa katika watu wa Musa, lakini aliwafanyia dhulma. Na tulimpa hazina ambazo funguo zake zinawatopeza watu wenye nguvu. Walimwambia watu wake: "Usijione; hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wanaojiona. Na utafute - kwa yale aliyokupa Mwenyezi Mungu- makazi mazuri ya akhera, wala usisahau sehemu yako ya dunia, na ufanye wema kama Mwenyezi Mungu alivyokufanyia, wala usitafute kufanya ufisadi katika nchi; bila shaka Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi. Akasema: Hakika nimepewa haya kwa sababu ya ilimu niliyonayo." Je, hakujua ya kwamba Mwenyezi Mungu amewaangamiza kabla yake watu waliokuwa wenye nguvu zaidi kuliko yeye na wenye mkusanyiko mwingi zaidi(kuliko wake yeye)? Na wabaya hawataulizwa makosa yao.

Basi akawatokea watu wake na pambo lake. Wakasema wale wanaotaka maisha ya dunia: "Laiti tungalipata kama aliyopewa Karuni; hakika yeye ni mwenye bahati. Na wakasema wale waliopewa ilimu: "Ole wenu! Malipo ya Mwenyezi Mungu ni mazuri kwa yule anayeamini na kufanya vitendo vizuri wala hawatapewa hayo isipokuwa wafanyao subira. Basi tukamdidimiza yeye(Karuni) na nyumba yake ardhini; wala hapakuwa na kundi lolote la kumsaidia kinyume na Mwenyezi Mungu, wala hakuwa miongoni mwa walioweza kujisaidia.(28:76-81)

Kwa upande wa pili lipo tabaka au jamii ya wanaokandamizwa, makabwela wanaoangalia wenzao "wakitesa" kielimu na kimali, wanaotumikishwa kwa ujira mdogo, walionyongeshwa kwa kunyimwa fursa na haki za msingi kijamii (underpriviledged); ambalo hupigania haki,uadilifu na usawa. Tabaka hili limetajwa kwa istilahi za mustadh'afuun yaani wanyonge wanaoonewa na kunyanyaswa; dhurriyyah yaani wapinzani wa tabaka tawala; ardhaluun yaani tabaka la chini(the lowest class); na fuqara na masaakin yaani mafukara na masikini.

Qur'an imeziita Tabaka hizo kuwa ni kambi mbili hasimu (pinzani).
Pili Qur'an imeitazama jamii inavyoweza kujigawa kiroho na kimaadili ambapo kwa upande mmoja kuna tabaka lililopewa istilahi za: Kaafiruun (makafiri) yaani wenye kuficha, kuzuia au kupindua haki; Twaaghuut wanaokiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu; mushrikuun yaani washirikina wale wenye kutii, kuogopa, kunyenyekea na kuongozwa kinyume au pamoja na Mwenyezi Mungu wakiwa sambamba na wale wenye kukubali kutiiwa, kuogopwa, kunyenyekewa na kuongoza kinyume au pamoja na Mwenyezi Mungu; munafiquun au wanafiki yaani wenye kuyumba baina ya haki na baatil; faasiquun au mafasiki yaani waasi; na mufsiduun yaani wavurugaji na waharibifu wa mazingira ya kimaada na kimaadili.

Kwa upande wa pili ipo jamii adilifu(ideal society) ambayo imeitwa kwa majina ya: muwahiduun wanye kumpwekesha Mwenyezi Mungu; Muttaquun yaani wachaMungu; abidiin-wenye kumuabudu Mwenyezi Mungu ipasavyo; abdiin- waja au watumishi watii wa Mwenyezi Mungu; muhsiniin - watenda mema; saalihuun - watu wanaojiepusha na maovu; muslihuun yaani walinganiaji na wanaharakati; mujahiduun(the warriors) yaani mashujaa wapigania haki na mabadiliko, wanamapinduzi na wakombozi wa jamii; na shuhadaa(the martyrs) yaani waliozitoa muhanga nafsi zao kwa ajili ya kusimamisha haki na Uadilifu katika jamii; waliokuwa tayari kupoteza au kukosa fursa mbali mbali, kutaabika, kudhalilika, kukimbia makwao, kupigana, kufungwa na hata kufa kwa ajili ya kutaka mabadiliko sahihi ya kijamii. Historia inaonyesha harakati zote za ukombozi za kale na hivi karibuni zimepita mkondo huu wa Historia.

Kama ilivyoelezwa awali matabaka haya yanapojitokeza, jamii hutoka katika kipindi fulani cha historia na kuingia kipindi kingine.
(2) Watu wanaoamrisha mema na kukataza mabaya Si katika kawaida na utaratibu wa Allah kuifanya jamii ibadilike toka hali moja hadi nyingine kwa kuiteza nguvu. Bali watu wenyewe waamue kuibadili. Kwa hiyo jamii iliyojaa dhulma na uonevu, yaweza kubadilika na kuwa jamii ya amani, furaha na uadilifu endapo watatokea waumini wa kweli wakafanya harakati za kuondoa tawala zinazo kaidi maamrisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu. Hili linapotokea jamii hutoka katika kipindi fulani cha historia na kuingia kipindi kingine.

(3) Kutetea na kulinda maadili Nadharia za masuala ya jamii zinaeleza kwamba katika historia ya ulimwengu, desturi na ustaarabu wa baadhi ya mataifa, makabila au koo umekuwa chimbuko la maendeleo aliyofikia mwanaadamu hivi leo. Baadhi ya jamii zimejitokeza kuwa na uwezo wa kutengeneza mila, ustaarabu na uungwana huku nyingine zikikosa vipaji hivyo. Hali ni hiyo hiyo katika sayansi, falsafa, sanaa na ufundi kwa baadhi ya jamii kutoa mchango mkubwa, nyingine zikiwa watumiaji(consumers) tu wa mila, desturi, ustaarabu na fani hizo.

Hili linajitokeza pia katika kubuni taaluma, mafunzo,ufundi stadi na teknolojia. Jamii nyingine zimeongoza katika kazi za harubu zisizohitaji matumizi makubwa ya akili kuweza kuzitekeleza. Kwa kuliona hili baadhi ya watu huamini kwamba zipo jamii maalum zenye wajibu wa kuuelekeza mkondo wa historia ya mwanaadamu katika ustaarabu(japo kila jamii ina wake), mila na ubunifu katika elimu au maarifa mbali mbali kama ilivyojitokeza kwa nchi za Uajemi ya kale, Misri ya kale , Shamu ya kale, Uyunani ya kale, Urumi ya kale na hivi leo nchi za ulaya magharibi na Marekani.

Kwa sababu hii na ile ya mvuto wa kijamii mara nyingi jamii ambazo haziongozwi na sheria ya Allah, zimekuwa zikiibuka na nadharia, sera, staarabu,desturi na taratibu ambazo huangusha maadili ya jamii (moral corruption and degenaration). Katika hali hii jamii hunusurika tu endapo watakuwepo waumini watakaosimama kutetea maadili na kupinga sera mbaya. Historia yatuonyesha kuwa awali Ulaya na Marekani hazikuwa zimeanguka kimaadili kama ilivyo leo. Baadae katika kipindi fulani cha historia wakabuni nadharia na sera ambazo zilichochea uzinzi na ulevi katika jamii. Kwa vile walikosekana waumini madhubuti wa kutetea maadili mema; leo nchi hizo zimezama katika ufuska, ulevi wa kupindukia, mauaji n.k., licha ya kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya vitu. Endapo wangekuwapo waumini wa kutetea maadili mema isingefikwa na kipindi hicho cha historia.

Nchi zinazoitwa za ulimwengu wa tatu hivi sasa zinapiga mbio kutekeleza sera za kudhibiti uzazi na zimeanza kufundisha elimu ya ngono mashuleni. Haya pamoja na mambo mengine huandamana na kampeni za ugawaji wa mipira ya zinaa(kondomu). Kwa bahati mbaya wengi wa wanaojiita waumini hawaioni hatari hii. Sera na mipango hiyo ya kuiangamiza jamii inapitishwa na kutekelezwa bila upinzani wowote. Pasipokuwepo harakati za kupinga mfumo wa utawala unaoshajiisha hayo, jamii iwe tayari kushuhudia kipindi cha historia kitakachojaa ufuska na yanayoandamana nayo muda si mrefu.
(4) Migongano na migogoro(conflicts) kati ya makundi yenye nguvu katika jamii; moja likitaka kuondoa lingine ili kuondoa au kupunguza dhulma na ukandamizaji.

Basi (hao watu wa Taluti) wakawaendesha mbio (hao maadui zao) kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na Daudi akamwua Jaluti, na Mwenyezi Mungu akampa (huyu Daud) ufalme na hikma. (Utume) na akamfundisha aliyoyapenda. Na kama Mwenyezi Mungu asingalizuia watu, baadhi yao kwa wengine, kwa yakini ardhi ingaliharibika. Lakini Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhili (kubwa) juu ya walimwengu wote. (2:251).

Kupitia Mitume na watu wema katika jamii, Allah (S.W.) huwaokoa watu kutokana na mateso wanayoyapata chini ya tawala za kidhalimu. Lakuzingatia hapa ni kuwa nusura ya Allah haiji kama mvua inavyonyesha bila ya juhudi ya mwanadamu. Bali watu wenyewe wanaodhulumiwa wanapaswa kutoka jasho ili kujikomboa. Ndio maana ruhusa ya kupigana ikawepo kwa wale waliodhulumiwa: Wameruhusiwa (kupigana) wale wanaopigwa, kwa sababu wamedhulumiwa. Na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni muweza wa kuwasaidia:Ambao wametolewa majumbani (mjini) mwao pasipo haki ila kwa sababu wanasema; Mola wetu ni Mwenyezi Mungu."


Na kama Mwenyezi Mungu asingeliwakinga watu, baadhi yao kwa wengine, bila shaka yangalivunjwa mahekalu na makanisa na nyumba nyingine za Ibada na misikiti ambamo jina la Mwenyezi Mungu hutajwa kwa wingi: Na bila shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anayeisaidia dini yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye kushinda. (22:39-40). Na nusura ya Allah itawajia wakiwa katika harakati za kujikomboa: "Na tutakukalisheni(nyinyi) katika nchi hizi(hizi) baada yao." Watapata haya wale walioogopa kusimamishwa mbele yangu na wakaogopa maonyo yangu." Na walitafutatafuta, na akashindwa kila jabari mkaidi(14:14-15).

MWISHO