KUTHIBITISHA KUWEPO KWA MUUMBA.

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

KUTHIBITISHA KUWEPO KWA MUUMBA.

SOMO LA PILI.

Mwanadamu pindi anapozitumia hisia zake halisi hupata dalili nyingi katika kila pembe ya dunia za kuthibitisha kuwepo kwa Muumba wa Ulimwengu huu.Kwa kutumia hisia hizo huweza kutambua vyema kuwa viumbe vyenye uhai ambavyo kwa hiari au bila hiari hufuata njia makhsusi na baada ya kipindi fulani huviachia viumbe vingine nafasi yavyo,kwani haviwezi kuwa vimejipa uhai venyewe.Njia hiyo yenye utaratibu huo maalum ambayo hufuatwa na viumbe hivyo haikuumbwa na viumbe hivyo.Viumbe hivyo havina hata uwezo mdogo wa kuchangia katika uumbaji wala kuratibu njia ya maisha yavyo.Na hii ni kwasababu mwanadamu hakujichagulia uwanadamu wake wala sifa zake bali ameummbwa tu na kupewe sifa hizo za uwanadamu.Kwa njia hiyo hiyo maumbile safi ya mwanadamu hayakubali kuwa kuna kitu kimejiumba au kimetokea hivi hivi chenyewe kighafla kighafla na hayakubali pia kuwa mfumo wa maisha yake hayana lengo lolote(maumbile ya mwanadamu hayakubali fikra ya namna hii).

Mwanadamu hawezi kulikubali jambo hilo hata katika matofali machache tu yaliyopangika katika mpangilio maalum.yaani kwa ibara nyingine ni kwamba hakuna mwanadamu anayeweza kusema kwamba matofali haya machache yenyewe ndio yaliyojipanga katika mpangilio huu maalum!. Kwa hiyo hisia safi za mwanadamu huthibitisha kwamba bila shaka ulimwengu huu una msingi ambao ni chanzo cha viumbe na pia kuwa kuna Muumba na Mlinzi wa msingi huo.Na chanzo hicho cha ulimwengu Elimu pia na Uwezo,kisichokuwa na mwisho wala mwanzo,cha tangu na tangu si kingine bali ni Mwenyeezi Mungu (s.w) Muumba wa kila kitu,na aliyekipa kila kitu umbo lake.Na Mwenyeezi Mungu (s.w) amelithibitisha hilo katika kitabu chake kitukufu pale aliposema:

*...الذي أعط? کل شي خلقه ثمَّ هد?*

"Aliyekipa kila kitu umbo lake kasha akakiongoza (kufuata kinachowafikiana na umbo lake". Tazama aya hii katika suurat twa'ha: Aya ya 50.

KUMJUA MWENYEEZI MUNGU NA MATAIFA.

Katika zama za hivi sasa, utakuta watu walio wengi duniani ni wafuasi wa dini na humwamini Mwenyeezi Mungu Muumba wa ulimwengu na humwabudu yeye tu.Mtu wa zama za kale pia alikuwa ni kama yule wa zama hizi za leo. Historia inaonyesha kwamba tangu zama za kale watu waliowengi wamekuwa wachaji Mungu na wakimwamini yeye Tu, hata kama kulikuwepo tofauti ya mtazamo au maoni kuhusiana na chanzo cha uumbaji katika jamii mbali mbali zilizokuwa zikimcha na kumwabudu Mwenyeezi Mungu lakini (jamii) zote hizo kwa pamoja zilikubaliana kimsingi kuhusiana na suala hilo.yaani tofauti hizo za maoni zilizokuwepo katika jamii hizo haikuwafanya watu hao wasikubaliane kwamba Mungu ni mmoja na ndiye anayestahiki kuabudiwa ,na kwamba yeye ndiye muumba wa mbingu na ardhi na vyote vilivyomo.

Hili ni jamba la msingi lililokuwa wazi ndani ya jamii hizo.Usije ukasema ni uislaam pekee uliyokuwa ukimiliki msingi! La hasha! Sio kweli ! kweli ni kwamba si uislaam pekee,bali hata dini nyinginezo kama vile ukiristo,uyahudia,umajusi na ubudha,na dini nyingine zote,zote zilikubaliana na zinakubaliana kuhusiana na jambo hili.Wale wachache wanaokana kuwepo kwa Mwenyeezi Mungu hawana dalili yoyote ya kuthibitisha madai yao kwamba Mungu hayupo.Wao husema kwamba: Hawamiliki dalili ya kukinaisha ili waweze kuthibitisha kuwepo kwa Mwenyeezi Mungu badala ya kusema kuwa :Wana dalili ya kukinaisha ya kuthibitisha kutokuwepo kwa Mwenyeezi Mungu! Na hii kauli yao ni yakushangaza sana! Yaani wao wanasema dalili ya kuthibisha yenye kukinaisha kuwa Mungu yupo hawana,lakini kwa upande wa pili tunawakuta pia hawana dalili ya kuthibitisha yenye kukinaisha kuwa Mungu hayupo,wakati kiakili ilitakiwa wakikataa kwamba hawana dalili ya kuthibitisha basi watuletee dalili ya kukanusha.!

Mtu wa kimaada mwenye kuitumia akili yake vizuri inavyotakiwa husema "Sijui" na hasemi "Hayupo".Kwa ibara nyingine mtu wa kimaada huwa ana "wasiwasi" na huwa "Hakatai"Mfano mzuri ni huu hapa kwamba:Mtu akimwambia kwamba baada ya maisha haya ya duniani ya muda mfupi kuna maisha mengine ya akhera ya muda mrefu ambayo mtu ataishi milele baada ya kufufuliwa na kakupatia dalili za kukinaisha zinazothibitisha hilo,ikiwa wewe hauna dalili zinazokinaisha zeznye kuthibitisha kuwepo kwa maisha ya milele baada ya maisha ya hapa dunia,inatakiwa useme "Sijui" sio unasema "Hakuna" ama ukisema hakuna hali ya kuwa dalili ya kukataa suala hilo hauna,(unadhani tu) basi wewe ujue kwamba unaenda kinyume na kanuni. Mwenyeezi Mungu (s.w) anasema:

*وقالوا ما هي إلاَّ ح?اتنا الدنيا نَمُوتُ ونحيا وما يهلکنا إلا الدهر،وما لهم بذالک من علمٍ،إن هُمٍ إلاَّ يظنُّونَ*

" Na walisema:Haukuwa (uhai) ila ni uhai wetu huu wa dunia,(Hakuna mwingine);tunakufa na tunaishi,wala hakuna kinachotuangamiza (ispokuwa huu huu) ulimwengu;(kwani ndio ada yake kufisha na kuhuisha).Lakini wao hawana Elimu ya hayo (wanayoyasema) wanadhani tu." Tazama aya hii katika Suurat Al-jathiyah:Aya ya 24. Watu hawa aliowazungumzia Mwenyeezi Mungu (s.w) katika aya hii,walikuwa wanakataa kuwa hakuna maisha baada ya maisha ya hapa duniani bali (wao walikiamini kwamba) mtu akifa basi ndio imetoka, hana tena athari yoyote na kwamba baada ya kifo hicho ndio mwisho wao wa kila kitu,hivyo watu hao walikikataa na kukanusha kwamba hakuna kufufuliwa na kurudia kuwa hai,lakini hawakuwa na dalili wala elimu ya hayo wayasemayo,bali walikidhani tu.

Hivyo alama za kumjua Mwenyeezi Mungu (s.w) zinaweza kuonekana hata katika athari za watu wa kale.Kuna dalili zisizopingika zinazothibitisha kuwa watu hao wa kale walikuwa wakiamini mambo ya kimaanawi,na yanayohusiana na Mwenyeezi Mungu (s.w). Hata watu waliokuwa wakiishi katika mabara ambayo ni mapya kwa kiwango- fulani kama vile America (Marekani) na Australia na visiwa vya mbali vya bara la kale ambavyo vimevumbuliwa katika karne za hivi karibuni -walikuwa ni watu wanaomuabudu Mwenyeezi Mungu (s.w).Watu hao waliweza kuthibitisha chanzo cha Ulimwengu kwa kuzikurubisha pamoja fikra zao hata kama historia haijathibitisha uhusiano wao na ulimwengu wa kale.

Suala la kwamba mwanadamu alikuwa akimwabudu Mwenyeezi Mungu kwa muda mrefu linaonyesha ukweli huu kwamba kumjua Mwenyeezi Munngu (s.w) ni jambo ambalo ni la kimaumbile kwa mwanadamu.Kwa maumbile hayo mwanadamu huweza kuthibitisha kuwepo kwa Mwenyeezi Mungu (s.w) ambaye ameumba ulimwengu huu na vyote vilivyomo. Qur'an Tukufu inaashiria katika sifa hii ya kimaumbile ya mwanadamu ikisema:

*ولئن سألتهم من خلقهم ل?قولون الله..*

Na ukiwauliza, ni nani aliyewaumba? Watasema: "Ni Mwenyeezi Mungu" Tazama aya hii katika suuratuz-zukhruf: Aya ya 87.

*ولئن سألتهم من خلق السماوات والأرض ل?قولون الله..*

Na kama ukiwauliza, ni nani aliyeumba Mbingu na Ardhi?Biala shaka watasema: "Mwenyeezi Mungu" Tazama aya hii katika Suurat Luqman: Aya ya 25.

MWISHO

USIKOSE KUFUATILIA SEHEMU YA TATU IJAYO KUHUSIANA NA SOMO HILI ILI UJUE ATHARI YA KUJIULIZA HUKU KATIKA MAISHA YA MWANADAMU.