QUDSI

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

QUDSI

Viongozi wa makundi ya mapambano ya Palestina wameonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Ayatullah Ali Khamenei katika uzinduzi wa kongamano la Mshikamano wa Kitaifa na Kiislamu kwa Ajili ya Mustakbali wa Palestina.

Ayatullah Ali Khamenei amesema katika mkutano huo kwamba Palestina na Quds Tukufu utarejea katika mikono ya umma wa Kiislamu chini ya kivuli cha mapambano, kusimama kidete na jihadi, na hatima ya utawala ghasibu wa Israel itakuwa ni kushindwa na kutoweka.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amepongeza mapambano ya kishujaa ya taifa la Palestina na wananchi wa Ukanda wa Gaza na akasema: "Hapana shaka kwamba Palestina itakombolewa chini ya kivuli cha kudumishwa mapambano ya taifa la Palestina, umoja wa makundi ya mapambano ya jihadi, imani na kumtegemea Mwenyezi Mungu; na waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni hawatapata lolote ghairi ya fedheha na jina baya katika historia.

Amesema kuwa kusimama kidete kwa wananchi wa Palestina hususan huko Gaza ni jambo la kustaajabisha na linalotia nguvu na kuimarisha misimamo ya Wapalestina. Amelishukuru mno taifa la Palestina na akasema: "Kustahamili masaibu na mashinikizo yasiyokuwa na kikomo huko Gaza na katika ardhi yote ya Palestina ni jambo lisolowezekana bila ya hidaya na msaada wa Mwenyezi Mungu, na taifa la Palestina linastahili kupewa lakabu ya 'taifa shujaa kuliko yote katika historia'.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kulinda na kuimarisha moyo wa mapambano na kusimama kidete katika taifa la Palestina ndio wajibu muhimu zaidi wa harakati za jihadi na mapambano na sharti la kudumishwa ushindi wa Palestina. Amesema kuwa maadui Wazayuni na pande nyingine zinawawekea mashinikizo makubwa na ya aina mbalimbali wananchi wa Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi mwa mto Jordan na zinafanya jitihada za kusimamisha mapambano yao na kuwalazimisha wasalimu amri; hata hivyo taifa la Palestina, kwa kuwa na ari na matumaini makubwa zaidi, linapaswa kuwa na imani kwamba harakati yake kubwa itazaa matunda.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa nguvu inayozidi kila uchao ya kambi ya mapambano dhidi ya kambi ya ubeberu na ukafiri ni ukweli wa wazi usioweza kukanushwa. Amewaambia viongozi wa harakati za kupigania uhuru za Palestina kwamba nguvu na maendeleo yanayoonekana wazi ya kambi ya mapambano ni matokeo ya kuingizwa masuala ya kiroho katika mapambano, imani na kumtegemea Mwenyezi Mungu; kwa msingi huo kuna udharura wa kuimarishwa zaidi hisi za kidini na imani ya kweli katika taifa la Palestina na kuzidisha kutawakali, matarajio, na kuwa na matumaini na ahadi zake Mola Mlezi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa ushindi wa taifa la Iran dhidi ya utawala wa kidhalimu wa kifalme ni mfano nzuri wa kutimia ahadi za kwezi za Mola Mlezi. Amesema, kuundwa Jamhuri ya Kiislamu katika nchi ambayo ilikuwa ikipata misaada ya pande zote ya Marekani na nchi nyingine za Magharibi lilionekana kuwa ni jambo muhali, lakini kumtegemea Mwenyezi Mungu, mapambano yaliyoegamia kwenye umoja, imani na kusimama kidete na vilevile msimamo imara wa Imam Khomeini viliwezesha kufanyika jambo hilo muhali, na hapana shaka kwamba ukombozi wa Palestina si mgumu zaidi kuliko ushindi wa taifa la Iran dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Shah.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya udharura na umuhimu wa kuwazindua watu na kukabiliana na propaganda chafu za nchi za Magharibi dhidi ya kadhia ya Palestina. Ameashiria kashfa ya kufedhehesha ya Marekani na nchi nyingine zinazodai kutete haki za binadamu katika vita vya siku 22 huko Gaza na akasema: "Marekani na pande nyingine zinazouhami na kuusaidia utawala wa Kizayuni wa Israel zilifumbia macho kabisa maafa makubwa zaidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika Ukanda wa Gaza na mataifa mbalimbali duniani yalipojitokeza kupinga jinai hizo baadhi ya watu wa Ulaya na jumuiya zinazodai kutetea uhuru na haki za binadamu ziliamua kulaani jinai hiyo kwa maneno matupu ili kuzuia kashfa na fedheha kubwa zaidi.

Vilevile ameitaja misimamo ya Umoja wa Mataifa kuhusu jinai na uhalifu wa Wazayuni katika vita vya siku 22 vya Israel dhidi ya Gaza kuwa ni aina fulani ya kashfa na fedheha na akaongeza kuwa: "Kwa mujibu wa ripoti ya tume ya Jaji Goldstone, viongozi wahalifu wa utawala wa Kizayuni wa Israel walipaswa kufikishwa mahakamani na kuadhibiwa, lakini kwa nini hadi sasa hilo halijatendeka na kinyume chake, himaya kwa dola ghasibu na bandia la Israel imeongezeka zaidi?

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha mtihani mbaya uliozikumba nchi nyingi za Kiarabu wakati wa mashambulizi ya siku 22 ya Israel dhidi ya raia wa Gaza na akasema: "Nchi hizo zinaitaja kadhia ya Palestina kuwa ni suala la Kiarabu, lakini lilipojitokeza suala la kutuma misaada kwa wananchi wa Palestina nchi hizo za Kiarabu hazikutenda kwa mujibu wa madai hayo na ziliwaacha Wapalestina peke yao mbele ya adui wao na waitifaki wake." Amesisitiza kuwa msimamo huo utasajiliwa katika historia. Ayatullah Khamenei amesema kaulimbiu ya mabadiliko iliyotolewa na Rais mpya wa Marekani ilikuwa harakati ya kukarabati sifa mbaya na heshima iliyotoweka ya Washington. Ameongeza kuwa juhudi hizo za urongo pia hazitakuwa na tija kwani Wamarekani wanasema uongo katika suala la Palestina na masuala mengine mengi. Amesisitiza kuwa taifa la Iran limezoea kusikia urongo kama huo katika kipindi chote cha miaka 30 iliyopita.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kadhia ya Palestina ni changamoto kubwa kwa ustaarabu wa Magharibi na wanaodai kufuata mfumo wa kiliberali. Amesisitiza kuwa mapambano ya taifa la Palestina yameweka wazi na kufedhehesha madai ya miaka mia kadhaa ya nchi za Magharibi kuhusiana na uhuru na haki za binadamu. Amesema leo hii kadhia ya Palestina imekuwa kigezo cha kuainisha watetezi halisi na wa urongo wa uhuru na haki za binadamu. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa mustakbali wa Marekani ni kushindwa kikamilifu mbele ya mapambano ya taifa la Palestina. Ameongeza kuwa: "Hapana shaka kwamba hatua za miaka 60 hadi 70 ya uungaji mkono wa serikali zilizoshika madaraka huko Marekani kwa Wazayuni ni fedheha kubwa kwa nchi hiyo itakayobakia katika historia.

Ayatullah Ali Khamenei amesisitiza juu ya kuundwa Mashariki ya Kati mpya yaani Mashariki ya Kati ya Kiislamu na akasema, kulitetea taifa la Palestina ni wajibu wa kibinadamu na Kiislamu. Ameongeza kuwa nchi za Kiislamu zinawajibu mzito zaidi katika uwanja huo na mataifa yamezinduka na yanataka kutolewe misaada na himaya zaidi kwa Palestina.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema suala la kuisaidia Palestina ni suala la kiitikadi kwa Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran na kuongeza kuwa: "Kwetu sisi suala la Palestina si taktiki na mbinu au stratijia ya kisiasa bali ni suala la kiroho na imani yetu; kwa sababu hiyo wananchi wa Iran wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kote nchini katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds na kudhihirisha hisia zao za kweli za kuwatetea wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina kama wanavyojitokeza kwa wingi katika maandamano ya tarehe 11 Februari ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambayo ni siku muhimu kwa nchi yao.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, nafasi na hatima iliyozikumba pande zinazofanya mazungumzo ya mapatano na Wazayuni inaonyesha kutokuwa na itibari wala faida mazungumzo hayo na amekumbusha kuwa, watu ambao wanaidharau njia sahihi na ya kweli ya ukombozi wa Quds na Palestina yaani mapambano na kusimama kidete hawana njia nyingine isipokuwa kusalimu amri mbele ya masuala wanayotwishwa na adui kwani kila wanapojaribu kujipapatua katika hali hiyo hudhalilishwa au kufutiliwa mbali.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, kupinga na kuikataa mapambano kwa kujua au kutojua husababisha madhara kwa taifa la Palestina. Amesema uhakika huo inabidi ubainishwe na kuwekwa wazi wakati wote mbele ya fikra za walio wengi.

Ayatullah Ali Khamenei amesema, Mwenyezi Mungu ameahidi kuwanusuru waumini wa kweli duniani na Akhera na kwamba uwezo wa kiuchumi, kisiasa, kijeshi na kipropaganda wa taifa la Iran ni mdogo ukilinganishwa na wa Marekani lakini kutokana na nusra ya Mwenyezi Mungu taifa la Iran linaonekana makini na madhubuti zaidi na linaendelea kupiga hatua kubwa za kimaendeleo kwa msaada wa Mwenyezi Mungu huku Marekani ikizidi kurudi nyuma na kufeli katika siasa zake.

Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, Inshaallah Quds Tukufu itakombolewa na itarejea mikononi mwa Waislamu na walimwengu na taifa sujaa la Palestina litashuhudia siku hiyo. Mwanzoni mwa mkutano huo, Bw. Manouchehr Mottaki, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa ripoti kuhusu malengo ya kongamano la "Mshikamano wa Kitaifa na Kiislamu kwa ajili ya Mustakbali wa Palestina" na kuashiria mwenendo unaopamba moto wa mapambano ya wananchi wa Palestina dhidi ya Wazayuni. Amesema, hivi sasa hali imekuwa kwa mamna ambayo, hata waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni wamekumbwa na shaka kubwa kuhusu suala la kuendeleza uungaji mkono wao kwa utawala huo na mashirika ya kimataifa yanalazimika kuchunguza sehemu ndogo ya faili la jinai za miongo kadhaa za Wazayuni.

Baada ya hapo Bw. Khalid Mash-al Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ameshukuru sana kuitishwa kongamano la "Mshikamano wa Kitaifa na Kiislamu kwa ajili ya Mustakbali wa Palestina" katika wakati huu wa kuanza Wiki ya Umoja ndani ya siku za kuadhimisha Maulidi yenye baraka ya Bwana Mtume Muhammad SAW na kuongeza kuwa mazingira yanayotawala hivi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati yanatofautiana sana na ya huko nyuma. Amesema leo hii kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na kwa misimamo ya kishujaa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kambi ya mapambano imezidi kuimarika na kupata ushindi mkubwa mbele ya utawala wa Kizayuni jambo ambalo amesema lilikuwa ni ndoto na ni vigumu hata kulifikiria katika siku za huko nyuma.

Amesisitiza kwamba hivi sasa utawala wa Kizayuni wa Israel umo kwenye mkondo wa kuangamia na kukumbusha kuwa, mapambano ndiyo njia pekee ya kupata ushindi na kwamba Wapalestina wote wameungana katika kambi moja. Amesema kuwa, watu wanaotaka kuzusha mifarakano katika kambi ya mapambano ya ukombozi kamwe hawatafanikiwa katika njama hizo na kama ambavyo Marais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Syria walivyosema siku chache zilizopita, mantiki na lengo la kambi ya mapambano ni moja.

Vile vile amemshukuru Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa uungaji mkono wake kwa kadhia ya Palestina pamoja na uungaji mkono wa wananchi na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kadhia hiyo, na ameuonya utawala wa Kizayuni kwa vitendo vyake vya kuuharibu Msikiti wa al Aqsa na maeneo mengine matakatifu ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Naye Dkt. Ramadhan Abdullah, Katibu Mkuu wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina amesema katika mkutano huo kwamba kuitishwa kongamano hilo kwenye wakati nyeti kama huu katika ni jambo muhimu sana. Amekumbusha kuwa, suala la Palestina linaweza kutatuliwa tu kupitia umoja na kushirikiana umma mzima wa Kiislamu na kwa umoja wa makundi yote ya Palestina. Amesema ana matumaini kwamba kongamano la "Mshikamano wa Kitaifa na Kiislamu kwa ajili ya Mustakbali wa Palestina" la mjini Tehran, litaandaa uwanja wa kupatikana umoja madhubuti wa kitaifa kuhusu suala la Palestina.

Amesema njia pekee ya kutatua kadhia ya Palestina ni mapambano na kusimama kidete mbele ya adui Mzayuni na kwamba uzoefu wa miaka ya huko nyuma umethibitisha kuwa njia za kisiasa hazina matunda yoyote isipokuwa kuzidi kukanyagwa haki za wananchi wa Palestina.

Kwa upande wake, Bw. Ahmad Jibril, Katibu Mkuu wa Harakati ya Wananchi kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina ametumia hotuba yake fupi kuashiria mashaka na matatizo aliyopata Bwana Mtume Muhammad SAW katika kukabiliana na washirikina na maadui na kuongeza kuwa: "Sisi ni waendelezaji wa njia ya Mtume huyo huyo na tumechagua mapambano kama njia pekee ya kuweza kupata ushindi mbele ya adui Mzayuni na tunajivunia chaguo letu."

Amegusia pia ushindi mkubwa wa wanamapambano wa Lebanon na Ghaza na kusisitiza kuwa, hali inayotawala hivi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati inatofautiana sana na hali iliyokuwepo katika siku za huko nyuma na kwamba adui Mzayuni ambaye alikuwa hafikirii kwamba kuna siku atashindwa, hivi sasa ameonja uchungu wa kushindwa mara kadhaa.

Kwa upande wake, Bw. Abu Musa, Katibu Mkuu wa Harakati ya Fat'h (Intifadha) amesema katika mkutano huo kwamba hivi sasa Quds na maeneo matakatifu ya Palestina yanatishiwa na hatari mbali mbali kutoka kwa Wazayuni na kwamba kitendo cha utawala wa Kizayuni cha kuteka na kukalia kwa mabavu maeneo na ardhi zilizoko pembeni mwa Msikiti wa al Aqsa pamoja na kujenga nyumba za walowezi wa Kizayuni katika maeneo hayo kimeufanya utawala huo kuizingira kikamilifu Quds na hivi sasa utawala huo unaendeleza njama zake za kuufanya mji wa Baitul Muqaddas kuwa wa Kiyahudi kikamilifu.

Amesema ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran umesaidia na kuwa na taathira kubwa katika suala zima la mapambano na kupatikana ushindi dhidi ya adui katika miaka ya hivi karibuni. Ameongeza kuwa, misimamo ya Rais Ahmadinejad wa Iran na Rais Bashar al Asad wa Syria katika mkutano wao mjini Damascus Syria, ni majibu ya kishujaa kwa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel naimewafurahisha Waislamu wote duniani na hasa wananchi wa Palestina.

Naye Bwana Mahir Tahir, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Wananchi wa Palestina amepata fursa ya kuzungumza katika mkutano huo na ameitumia fursa hiyo kuashiria nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo na athari za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran katika kuundika kambi ya mapambano na kuongeza kuwa: "Sisi sote tunajua kwamba mashinikizo ambayo Iran inakabiliana nayo hayatokana na suala la nyuklia bali yanatokana tu na uungaji mkono wake kwa kadhia ya Palestina na kusimama kidete.

Huku akishukuru misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hususan Bw. Ahmadinejad amesema: "Ahmad Saadat, Katibu Mkuu wa Harakati ya Wananchi wa Palestina ambaye hivi sasa yuko katika jela za Wazayuni, ametuma ujumbe maalumu akishukuru misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu kadhia ya Palestina."

Naye Bw. Haytham Satai, mjumbe maalumu wa Rais Bashar al Asad mjini Tehran sambamba na kuwasilisha salamu za Rais huyo wa Syria kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa nchi yake inashiriki katika kongamano la Tehran pembeni mwa makundi ya mapambano ya Palestina na lengo lake ni kutoa ujumbe kwamba kambi ya istikama ina kauli moja, imeshikamana na iko bega kwa bega katika kukabiliana na Uzayuni na waungaji mkono wake.

Amesema, Syria inaliona suala la kuunga mkono mapambano ya Wapalestina kuwa ni jukumu lake na kwamba ushindi mbalimbali wa miaka ya hivi karibuni uliopata kambi ya mapambano umeleta mazingira mapya katika eneo la Mashariki ya Kati na inapasa mazingira hayo yalindwe na vile vile inabidi kuwa imara zaidi katika njia ya mapambano.