MAISHA YA IMAMU BAAQIR (A.S)

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

MAISHA YA IMAMU BAAQIR (A.S)

Tarehe saba mwezi wa Dhihijja inasadifiana na siku ya kukumbuka siku aliyoaga dunia mmoja wa wajukuu watoharifu wa Mtume Muhammad (saw). Tonakupeni mkono wa pole enyi wapenzi Waislamu kwa mnasaba huu mchungu na tunakukaribisheni kusikilza machache kuhusu maisha ya mtukufu huyo.

Siku ambayo habari za kuaga dunia Imam Muhammad Baqir (as) zilienea katika mji mtakatiu wa Madina, mji huo ulighubikwa na huzuni kubwa ya wapenzi wa Watu wa Nyumba ya Mtume (saw). Hii ni kwa sababu hawakuwa wakiuona tena uso wenye nuru wa mjukuu huyo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu wala kusikia sauti yake changamfu na yenye kutuliza nyoyo katika Msikiti wa Mtume (saw). Hali hiyo ya huzuni iliwaathiri zaidi wafuasi wa karibu wa Imam Baqir na hasa Jabir bin Yazid Ju'fi.

Siku na wakati ulikuwa ukimpitia kwa tabu kubwa Jabir. Alikuwa na kumbukumbu nzuri na ya kuvutia kutoka kwa Imam Baqir (as). Alipomwona Imam kwa mara ya kwanza, alikuwa kwenye Msikiti wa Mtume (saw) ambapo alikuwa amezungukwa na watu walioonekana kuwa na hamu kubwa na kusikiliza kwa makini maneno ya hekima aliyokuwa akiyasema. Imam alikuwa akizungumzia utafutaji elimu na umuhimu wake. Alipomkaribia, alimsikia Imam akisema: "Tafuteni elimu, kwa sababu utafutaji elimu ni jambo zuri. Elumu ni mwongozi wako kwenye giza, msaidizi wako katika mazingira magumu na rafiki mwema wa mwanadamu."

Nasaha hiyo ya Imam Baqir ilimvutia sana Jabir na kumfanya ashiriki katika vikao vya kielimu na midahalo ya Imam Baqir (as) na hivyo kunufaika kwa kiwango kikubwa na bahari ya elimu ya mtukufu huyo. Kumbukumbu ya mambo hayo yote ilimfanya Jabir alie kwa majonzi makubwa alipokuwa akikumbuka kifo cha Imam Baqir (as). Alikuwa akijikumbusha maneno haya ya Imam huyo mwenye huruma alipomwambia: "Ewe Jabir! Mtu aliye na mapenzi ya Mwenyezi Mungu moyoni, moyo wake haushughulishwi na mapenzi ya mtu au jambo jingine. Watu wampendao Mwenyezi Mungu huwa haegemei wala kuitegemea dunia hii. Kwa hivyo fanya juhudi za kulinda kile Mwenyezi Mungu amekiweka kwako amana katika dini na hekima Yake." Jabir aliungana na umati mkubwa wa waombolezaji wenzake katika mazishi ya Imam Baqir katika makaburi ya Baqee katika mji mtakatifu wa Madina. Hiyo ilikuwa ni tarehe 7 Dhil Hijja mwaka 114 Hijiria.

Kila sehemu inapoonekana alama na ishara ya uadilifu, ukweli na hakika, basi jina la Ahlul Beit wa Mtume (saw) hun'gara na kumetameta. Walikuwa waenezaji na washajiishaji wakubwa wa thamani za hali ya juu zaidi za kiutu na kimaadili. Mtukufu Imam Muhammad Baqir (as) alichanganyika na watu na kuwaongoza kwenye njia ya ukamilifu na kuwepo kwake kwenye jamii kulikuwa mfano wa jua linavyowaangazia wanadamu njia njoofu ya wongofu.

Kipindi cha uimamu wa miaka 19 cha Imam Baqir kilianza mwaka wa 95 Hijiria. Katika kipindi hicho jamii ya Kiislamu ilishuhudia kumalizika kwa kipindi cha utawala wa makhalifa wa Bani Umaiyya na kuingia madarakani makhalifa wa Bani Abbas. Wakati huohuo, kipindi hicho pia kilishuhudia harakati kubwa ya kutarjumiwa vitabu vya kifalsafa na midahalo ya kielimu na kiitikadi. Katika upande wa pili, baadhi ya makundi potovu pia yalikichukulia kipindi hicho kuwa fursa nzuri ya kueneza fikra zao potovu katika jamii ya Kiislamu. Katika kipindi hicho cha historia ambapo jamii ilikuwa ikikabiliwa na wimbi kubwa la hujuma ya fikra potofu na hatari, Imam Baqir na mwanawe Imam Ja'far (as) walitekeleza vyema jukumu lao zito la kuwaongoza Waislamu kwenye njia nyoofu na kuwakinga na madhara ya fikra hizo zilizokuwa zikienezwa kwenye jamii na watu waliokuwa na nia mbaya dhidi ya jamii ya Kiislamu. Katika kipindi hicho, ni watukufu wawili hao tu ndio waliokuwa warithi halisi wa mafundisho ya Mtume Muhammad (saw) na ndio waliostahiki kukusanya na kubuni misingi ya mafundisho hayo ya Uislamu halisi.

Kwa msingi huo, Imam Baqir (as) alianzisha harakati kubwa ya kusambaza mafundisho ya Mtume na kuwafahamisha malengo halisi ya dini tukufu ya Kiislamu. Kwa msingi huo Imam Baqir alianzisha kituo muhimu cha mafundisho ya Ahlul Beit (as) mjini Madina ambapo watu wengi waliokuwa na hamu ya kupata maarifa kutoka pembe mbalimbali za dunia walienda huko ili kunufaika na elimu ya mtukufu huyo. Chimbuko kubwa la elimu ya Imam pamoja na kipawa chake cha kufafanua elimu kwa kina, ni mambo yaliyompelekea Imam Baqir kupewa lakabu ya 'Baqir al-Elm' yaani mchimbuaji, mfunguaji au mchanuaji elimu. Katika zama zake Imam Baqir (as) alikuwa mlindaji mkubwa wa thamani na utamaduni wa Kiislamu na alikuwa na nafasi muhimu katika kueneza maadili na mafundisho ya Kiislamu duniani. Kuimarisha misingi na imani ya kidini, kukosoa na kuchambua fikra na itikadi potovu ni miongoni mwa huduma muhimu aliyotoa Imam Baqir kwa umma wa Kiislamu.

Viongozi na watawala wana nafasi muhimu katika mustakbali wa jamii. Bila shaka watawala dhalimu ambao hufikiria tu namna ya kudhamini maslahi yao binafsi na kutofahamu lolote katika maadili ya kiutu ni watu wanaoielekeza jamii kwenye mporomoko wa ufisadi na uovu. Zama za Imam Baqir ziliambatana na utawala wa watu waliokuwa wakipora mali za watu na kukiuka wazi haki zao kutokana na tamaa na mielekeo yao ya kuhodhi kila jambo. Katika kukabiliana na upotovu huo, Imam Baqir (as) alikuwa akiwabainishia watu mafundisho ya dini ya Kiislamu na kuwafahamisha sifa za mtawala bora. Alikuwa akikosoa vikali watawala dhalimu waliokuwa wakiwadhulumu watu na kukanyaga haki zao. Kutokana na jambo hilo, Imam alikuwa akiwekwa chini ya mashinikizo makubwa ya watawala wa Bani Abbas na hasa kutoka kwa khalifa Hisham bin Abdul Malik. Katika kubainisha sifa za kiongozi bora, Imam Baqir alikuwa akisema: "Bila shaka mtu hafai kuwa kiongozi wa watu isipokuwa anapokuwa na sifa tatu. Ya kwanza ni awe mwenye kumuogopa Mwenyezi Mungu na ajiepushe kutumbukia kwenye maasi. Ya pili, awe ni mwenye subira na mwenye kudhibiti hasira yake, na tatu aamiliane na kuwatendea wema walio chini yake, kama anavyofanya baba mwenye huruma."

Kuwasaidia wanyonge na wahitaji ni jambo linalofahamika vyema katika maisha ya Imam Baqir (as). Imam alikuwa akichukulia kukidhi, kimaada na kimaanawi, mahitaji ya wanyonge kuwa shughuli yake muhimu ya kijamii. Alikuwa akiwasiliana na matabaka mbalimbali ya wanyonge na watu masikini, kusikiliza mahitaji na matatizo yao na kisha kuwaliwaza. Huku akifanya juhudi za kuwasaida na kulinda heshima yao, Imam alikuwa akiwasihi watu wengine wawaite na kuwahutubu kwa majina mazuri na kutowadhalilisha kwa njia yoyote ile. Imam alikuwa akiingiliana na kuzungumza na matabaka mbalimbali ya watu wa kawaida katika jamii kwa kiasi ambacho watu hawakuwa wakiona tofauti yoyote ya kitabaka kati yao na Imam. Licha ya kuwa Imam alikuwa kwenye kilele cha elimu na maarifa, lakini mwenendo wake ulikuwa ni wa upole, unyenyekevu na wala hakuwahi kuonyesha tabia zozote za majivuno na majigambo. Ni sifa hizi ndizo zilizowafanya watu wavutiwe na mtukufu huyo wa Ahlul Beit (as). Imam Baqir (as) amesema: "Mja huwa ni mwenye elimu anapojiepusha kuwafanyia husuda walio bora kumliko yeye, na kutowadharau walio chini yake."

Katika kipindi cha uimamu wake, Imam Baqir (as) aliipa jamii ya mwanadamu huduma kubwa zaidi ya kielimu na kiutamaduni. Alitumia juhudi zake zote kuimarisha mafundisho ya Uislamu halisi na kuwalea wanafunzi wengi mashuhuri katika uwanja huo. Kuna hadithi nyingi ambazo zimepokelewa kutoka kwa mtukufu huyo ambazo zinatatua matatizo mengi ya jamii ya mwanadamu katika zama tofauti. Ni wazi kuwa juhudi za kielimu na za kuwaongoza watu kifikra za Imam Baqir zilikuwa zikimkera na kumtia wasiwasi mkubwa Hisham bin Abdul Malik. Hisham, alikuwa mtawala mporaji na mrundikaji mali, bakhili na katili.

Alikuwa akiwaamuru watumishi wake kumuudhi na kumbughudhi Imam Baqir (as) kwa njia mbalimbali. Licha ya hayo, lakini maudhi hayo yote hayakumfanya Imam asite hata kidogo katika utekelezaji wa majukumu yake. Hatimaye chuki na uadui wa Hisham kwa Imam uliongezeka kiasi cha kumfanya aanze kufikiria njia za kumua mtukufu huyo wa Nyumba ya Mtume (saw). Alitekeleza njama hiyo mbovu na ya kinyama katika siku kama hii. Kwa msingi huo, Imam Baqir (as) aliuawa katika siku kama ya leo kwa kupewa sumu na Hisham. Huku tukitoa mkono wa pole kwa Waislamu wote wapendao haki duniani kwa mnasaba huu mchungu wa kuuawa shaihidi Imam Baqir (as), tunatumai kwamba mafundisho tuliyopata kutokana na maisha ya Imam huyu mtukufu, yatakuwa ni taa ya kutuangazia njia ya wema kwetu sote. Tunaihitimisha makala hii kwa kusikiliza tena maneno yenye nuru ya mtukufu huyo. Anasema: "Jiepushe na uzembe na ulegevu kwa sababu mawili haya ni ufunguo wa maovu yote. Kila mtu anayefanya uzembe, hafanyi haki (hatekelezi haki) na kila mtu anayelegea na kuwa na hofu, hasubiri kuhusu haki

MWISHO