TUSIKUBALI KULAZIMISHWA

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

TUSIKUBALI KULAZIMISHWA

Magharibi wasitulazimishie 'demokrasia' yao yenye utata.
Nchi zote za Magharibi, kwa kutaja chache tu; Marekani, Uingereza, Ufaransa, Japan na nyingine zina demokrasia. Lakini je, zote zina aina moja ya mfumo wa demokrasia? Mfumo upi kati ya hiyo ni wa kidemokrasia zaidi? 'Demokrasia' za Magharibi zenyewe zina tofauti kubwa katika aina ya tawala za kisiasa zinazolenga kupata matokeo yale yale katika jamii yenye demokrasia.

Ikiwa matokeo ya kujenga taifa la kidemokrasia ni kanuni ya thamani au faida inayotumiwa, basi swali linaloletwa hapa kwa hakika ni la balagha, yaani lisilohitaji jibu, kwa sababu patakuwapo mifumo mingi yenye ufanisi ya demokrasia kwa kadiri ya idadi za mataifa na nchi zilizopo duniani.

Ikiwa tunu za demokrasia ni aina moja kwa wanadamu wote, na zinapendwa na wote, nini hiki kinachodaiwa kuwa ni 'Magharibi' kumiliki demokrasia kwa sababu tu, katika historia, wao (mataifa ya Magharibi) yalianza zamani safari yao kuuendea uhuru wakati wengine waliachwa nyuma kwa sababu mbalimbali, ukiwamo ukoloni (sema 'unyimi wa haki za kidemokrasia') na nchi hizo hizo za Magharibi?

Ikiwa, kwa ajili ya hoja au ubishani, jibu la swali lililoulizwa hapo ni 'NDIO', na marejeo kwa aina ya demokrasia ya Magharibi yanamaanisha kiukweli kupendekeza kwamba aina pekee za demokrasia za Magharibi ndizo zinatakiwa kunakiliwa au kufuatwa na mataifa mengine, bila kujali historia za jadi ya sehemu husika na taasisi zake, basi ni muhimu kabisa kutabiri kwamba patakuwapo na asilimia 100 ya pingamizi au upinzani wa kutoa na kulazimishia matumizi ya 'mfumo wa demokrasia ya Magharibi', tena kutoka maeneo mawili tofauti katika nchi zinazoitaka demokrasia.

Kwanza, ni upinzani ambao ungeweza kutoka kwa wengi wa wale wanaounga mkono demokrasia, lakini ambao wanaona upigiaji debe wa demokrasia ya Magharibi kuwa kimsingi ni majaribio mapya na dhaifu ya kurejesha ukoloni mamboleo, unaoendeshwa an uchumi au maslahi mengine binafsi, badala ya kuwa aina ya uungaji mkono unaotolewa katika ari ya umoja na uhamasishaji wa uhuru na haki duniani, na hivyo amani kwa wanadamu.

Ni hivyo kwa sababu moja rahisi, kwamba katika macho ya wale waliopata uzoefu wa ukoloni na aina nyingine za tawala zisizokuwa za kidemokrasia za Magharibi katika maisha yao na wangali na kumbukumbu hizo, hao wa Magharibi hawana utashi wala usomi wowote wa hali ya juu kiasi cha kuwa viongozi katika wa demokrasia duniani. Watu wote na mataifa yote lazima sasa wakae chini na kufanya kazi pamoja kwa ajili ya demokrasia ya dunia kama watu walio sawa, na kwa wakati mwafaka, wazike yote yenye kuchukiza yaliyopita.

Eneo la pili la upinzani (kwa demokrasia ya Magharibi) ni kutoka kwa makundi ambayo kwa idadi ni machache, lakini yanajumuisha watu wenye misimamo madhubuti, mikali, wanaopenda wakati mwingine kutumia nguvu na wanaoweza kusababisha uharibifu katika jamii. Ni hao ndio wanaoweza kukabiliana na tabia ya Magharibi ya kumiliki au kutangaza aina ya demokrasia, kuwa ni uthibitisho au ushahidi wa majaribio ya kuleta tunu za Kiyahudi - Kikristu kuhusu ustaarabu na watu wenye historia tajiri na tunu zao wenyewe, tena zenye nguvu. Utajwaji huu wa demokrasia kuwa ni mfumo wa tunu ya kijamii ya 'Magharibi' ungeweza tu kusaidia magaidi na wahalifu wa dunia kujipandisha chati wenyewe hadi kwenye ngazi ya "Wapiganaji Shujaa wa Uhuru, wakipinga uhuishaji wa mashambulizi ya waungaji mkono wa Vita Takatifu."
Gerrand Alexander ananukuliwa tena katika hitimisho la makala hii; "Ikiwa Marekani na washirika wake wa karibu zaidi wana nia ya kushawishi ukuaji wa demokrasia endelevu, basi wakati umewadia wao kuingia katika ile ile hali ya tafakuri jadidi juu ya matakwa ya demokrasia kama yale yaliyoletwa kwa kuchelewa kwenye uundaji sera kulenga uhamasishaji wa ukuzaji maendeleo endelevu ya uchumi."

Ingeweza kuongeza hapa kwamba, inaweza kuwa na thamani na tija zaidi, kwa wasomi wa Magharibi wanaojihusisha na suala hili na kutoa ushauri wa kisera kwa serikali zao, kuchangamana na, na kujifunza kutoka, kwa wasomi wanaoishi katika nchi zilizo katika mchakato wa kuanzisha demokrasia. Wasomi wa Magharibi lazima wakiri kwamba wenyewe hawana uzoefu wa moja kwa moja au wa binafsi juu ya mchakato wa ukuzai demokrasia kama sehemu ya maisha yao, kwa sababu mchakato huo katika nchi zao ni jambo lililokwishapita!

Misaada ya Magharibi imekuwa ikitumiwa kabla kama chombo cha sera za nje na haijasaidia sana kupunguza umasikini. Sababu moja ni kwamba, wasomi na viongozi wa 'sekta ya misaada' (kutoka Magharibi) walidharau na kushindwa kupata ushauri kutoka kwa wataalamu katika umasikini - MASIKINI wenyewe bila shaka.

Ni majaliwa hayo hayo ya kushindwa, yanayozisubiri jitihada za Magharibi katika kushadidia demokrasia kama sehemu ya mkakati wote wa sera za nje kwa nchi ambamo hakuna demokrasia, ikiwa utungaji wa sera kwa ajili ya kukuza demokrasia utaendelea kutawaliwa na maslahi binafsi na hivyo nyakati zote kubaki kuwa matokeo ya mijadala ya wasomi kati ya washauri mabingwa wa Magharibi, wakiwa tu na marejeo ya haraka na juu juu tu, ikiwa hata hayo yapo, kuhusu fikra za wasomi na washauri mabingwa wa asili katika karne ya 20 kutoka Asia, Afrika na Amerika Kusini.

Dunia hii inamilikiwa kwa usawa na watu wote, na tunaweza kufanikiwa kuifanya iwe sehemu nzuri zaidi ya kuishi na kukaa humo pamoja, kama kuna heshima kutoka pande zote mbili na kuhakikisha utu wa wtau wote unalindwa. Inawasilishwa hapa kwamba, aina pekee ya mfumo wa demokrasia unaopokewa na watu wote, ni ule utakaokuza uhuru, haki ya kijamii, udugu wa watu wote kwa ushirikishi sawa. Aina hiyo ya demokrasia haiwezi kudaiwa kuwa ni ya 'Kimagharibi' wala yenye kumilikiwa na wanasiasa wanaofuata mrengo watu fulani. Inamilikiwa kwa usawa na watu wote katika roho huru ya kiuanadamu.
Yapo matakwa ya aina moja kwa ukuzaji wa demokrasia kuwezekana, kama ambavyo kuna hali kinzani ambazo ni za kawaida na lazima kwa ajili ya kuanzisha na kufanya endelevu mfumo wa siasa wa kidemokrasia katika jamii.

Kazi kubwa mbele katika kukuza demokrasia na amani duniani kote ni kufanya kazi pamoja kuweka matakwa na hali kinzani kwa ajili ukuzaji wa demokrasia endelevu. Mkutano ule wa The Community of Democracies Ministerial Meeting - Mkutano wa Mawaziri wa Jamii ya Demokrasia) wa Juni, 2000 ulitoa fursa kamili kwa mataifa ya dunia kuanza kufanya kazi pamoja kukuza demokrasia kote duniani, na katika muktadha huo, Azimio la Mwisho la Warsaw lilisisitiza kwa mara nyingine azma hiyo ya pamoja: "Jamii ya Demokrasia inasisitiza azma yetu ya kufanya kazi pamoja kwa ajili ya kukuza na kuimarisha demokrasia, kutambua kwamba tupo katika hatua tofauti za maendeleo ya demokrasia."

Kwa kuhitimisha, makala hii imejaribu kuwasilisha hoja yenye mantiki yenye kuambatana na haya yanayoorodheshwa hapa chini. Kwamba tunu za demokrasia ni sawa kwa watu wote kama ilivyoelezwa kwenye Azimio la Mwisho la Warsaw la Juni, 2000 lililotolewa na mkusanyiko wa mataifa (Jumuiya ya Demokrasia) ambayo ni kweli wakilishi katika utofauti uliopo wa wandamu kijamii, kitamaduni, kisiasa, kiitikadi na kidini.

Kwamba kuna matakwa fulani ambayo lazima yawepo ili demokrasia ikuzwe na kufanywa endelevu katika jamii. Utamaduni wa eneo husika, mila na tunu za kijamii ndivyo vitakavyoamua jinsi ya uanzishwaji wa demokrasia na kasi yake katika ukuaji, pamoja na njia ya maendeleo kuendea ujenzi wa jamii yenye demokrasia na yenye uwazi.

Utawala wa nchi pamoja na viwango vya uongozi kwenye ngazi zote, uhuru wa ushirika wa kisiasa, uwapo wa uchumi huria na taasisi zenye ufanisi katika udhibiti na urekebishaji wake, kwa pamoja mihimili ya muundo na matofali ya ujenzi wa jumla la demokrasia.

Marekani na washirika wake wa Magharibi lazima waheshimu na kufanya kazi na majeshi yanayosonga mbele ndani ya mataifa ya dnia kwa lengo la ujenzi wa demokrasia na kukuza uhuru, haki ya kijamii na udugu miongoni mwa wanadamu, alazima uwe shirikishi. Hata hivyo, demokrasia lazima ikuzwe kwa kuzingatia historia ya jamii husika, na nguvu za kijamii, kisiasa, kitamaduni na kiuchumi. Kwa hiyo basi, demokrasia haiwezi kutolewa wala kuingizwa kwenye nchi moja kwa mafanikio.

Huu ni mwito wa kuwaamsha Waafrika ili wachague na kuwaunga mkono viongozi wa kweli watakaotoa miongozo kwa mataifa yao katika njia ya maendeleo kwa kujenga demokrasia na jamii huru., kutokana na hali halisi ya uchumi usioendelea na kwa kiasi fulani mifumo dhaifu ya kijamii na kisiasa, kuna kila dalili kwamba Afrika itajikuta upande wa pili ikipokea 'demokrasia' ya Magharibi katika mfumo wa mkakati wa sera ya nje.

Wasomi wa Afrika wasiwaangushe watu wao, na katika muktadha huu, lazima wazame katika tafakuri ya kina na kwa vitendo wachukue hatamu za uongozi kuzisaidia nchi zao ziendelee na kubadilika, hatua kwa hatua kufikia demokrasia za kweli na jamii zenye uwazi. Ikiwa wasomi wa Afrika watashindwa kuitikia mwito huu adili, wengine watalazimishia matakwa yao kwa Bara la Afrika, wakiwa na matakwa yao binafsi.

Kwa kumalizia makala hii juu ya demokrasia katika muktadha wa dunia, Marekani na washirika wake wa karibu zaidi wa Magharibi, walitumia vibaya fursa ya kwanza ya kuongoza ukuzaji wa demokrasia kote duniani kwa msaada wa Jamii ya Demokrasia, iliyokutana Juni, 2000.

MWISHO