Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

AINA ZA DHULMA NDANI YA QURANI.

2 Voti 02.0 / 5

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

AINA ZA DHULMA NDANI YA QURANI.
Maana ya dhulma ni kuweka kitu si katika pahala pake. Na dhulma ziko aina mbalimbali. Kwa mfano Shirki yaani kumshirikisha Mwenyezi Mungu Mtukufu na kitu kingine ni dhulma kwa sababu mambo yanayohusu Uungu yote ni haki ya Mwenyezi Mungu S.W.T. peke Yake. Atakayejaalia kitu kingine sawasawa na Mwenyezi Mungu Mtukufu atakuwa ameweka jambo si katika mahali pake. Na atakuwa amefanya mshirika katika sifa za Uungu Ambaye hashirikiyani na yeyote yule. Na kwa kuwa jambo linalohusu haki ya Mola Muumbaji wa kila kitu huwa dhulma yake ni zaidi kuliko dhulma za aina nyingine.

AINA TOFAUTI ZA DHULMA
Qur-ani tukufu imehadithia kuhusu dhulma na madhalimu na adhabu alizowaandalia Mwenyezi Mungu S.W.T. katika aya chungu nzima. Nazo ni hizi zifuatazo:

1. SHIRKI
Dhulma ya aina ya kwanza ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu S.W.T.. Nayo ni dhulma kubwa zaidi kuliko zote. Na kwa ajili hiyo ndio maana ilikuwa ni usia wa kwanza wa Luqmaan kumuusia mwanawe. Kama alivyosema Luqmaan kwa kauli ya Mwenyezi Mungu S.W.T., kasema katika Surat Luqmaan aya ya 13, "
وَإِذْ قَالَ لُقْمَانُ لِابْنِهِ وَهُوَ يَعِظُهُ يَابُنَيَّ لا تُشْرِكْ بِاللَّهِ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ
Maana yake, "Na (wakumbushe), Luqmaan alipomwambiya mwanawe; na hali ya kuwa anamnasihi. "Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu, kwa hakika kushirikisha ni dhulma kubwa."

Na shirki imekuwa ni dhulma kubwa kwa sababu ni haki ya Mwenyezi Mungu kwa waja Wake wamuamini na kumuabudu Yeye peke Yake wala wasimshirikishe na yeyote yule katika ibada Yake. Na wamtii Mola wao kwa anayowaamuru na kuacha anayowakataza. Na atakayeabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu S.W.T. kama vile kumuabudu mmoja wa waja Wake atakuwa ameweka kitu si mahali pake. Au kumtukuza kiumbe katika viumbe Vyake akamfanya sawasawa na Yeye hata katika jambo au sifa katika sifa Zake na yote hayo ni dhulma kubwa.

Katika Hadithi iliyopokelewa na Ibn Masoud R.A.A. na kutolewa na L-Bukhari na Muslim kasema,
لَمَّا نَزَلَتْ قوله تعالي: "الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُمْ بِظُلْمٍ''  شَقَّ ذَلِكَ عَلَى الْمُسْلِمِينَ، فَقَالُوا: يَا رَسُولَ اللَّهِ وَأَيُّنَا لا يَظْلِمُ نَفْسَهُ؟ قَالَ: لَيْسَ ذَلِكَ إِنَّمَا هُوَالشِّرْكُ: أَلَمْ تَسْمَعُوا مَا قَالَ لُقْمَانُ لِابْنِهِ؟ '' يَا بُنَيَّ لا تُشْرِكْ بِاللَّهِ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم

Maana yake, "Ilipoteremka (aya ya Qur-ani) ((Wale walioamini na hawakuchanganya imani yao na ushirikina basi hao ndio walioongoka.)) Ikawapa taabu Waislamu. Wakasema, "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu nani asiyedhulumu nafsi yake? Akajibu "Sivyo hivyo! Kwa hakika hiyo ni shirki, "Jee, hamkusikia aliyosema Luqmaan kumwambia mwanawe?" ((Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu, kwa hakika kushirikisha ni dhulma kubwa))."

2. KUVUKA MIPAKA YA MWENYEZI MUNGU S.W.T..
Miongoni mwa dhulma ni kuvuka mipaka aliyoiweka Mwenyezi Mungu S.W.T. kwa ajili ya waja Wake ili waepukane na haramu na wafuate faraidhi (vitendo vya lazima) au wajibu. Na yeyote yule mwenye kuivuka ile mipaka basi atakuwa amemuasi Mola wake. Na kama inavyojulikana kumuasi Mola ni dhulma ya haki Yake kwa ajili ya waja Wake. Na kwa ajili hiyo ndio maana Qur-ani tukufu imeelezea kuhusu wale wenye kudhulumu kuwa wanavuka mipaka aliyowawekea Mwenyezi Mungu Mtukufu na amewaita kuwa ni waasi na mafasiki hata kama wao ni Waislamu.

Na aya hiyo iliyotolewa hapo chini inawaonya Waislamu kuhusu kunywa ulevi, kucheza kamari, kuwadhulumu mayatima, kuhusu ndoa, imani, yanayohusu talaka ikiwa pamoja na kuishi na mke na mengi mengineo bila kuyataja moja moja. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Baqarah aya ya 229, "
تِلْكَ حُدُودُ اللَّهِ فَلا تَعْتَدُوهَا وَمَنْ يَتَعَدَّ حُدُودَ اللَّهِ فَأُوْلَئِكَ هُمْ الظَّالِمُونَ…
Maana yake, "Hii ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu; basi msiivuke. Na watakaoivuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, hao ndio madhalimu."

3. MTU KUJIDHULUMU NAFSI YAKE
Mfano wa mtu kujidhulumu nafsi tumechukuwa katika Qur-ani mfano wa Nabii Yuunus A.S. alipoamrishwa na Mola wake aende kwa watu wake watu wa mji ulioyoitwa Ninawah katika nchi ya Iraq. Lakini watu wake hawakumwamini, kwa hali hiyo akaondoka bila idhini ya Mola wake na kuwaachilia mbali watu wake akikhofia kuwateremkia adhabu ya Mola wao na huku Nabii Yuunus amewakasirikia. Kwa ajili hiyo akamezwa na samaki alipokuwa kajitumbukiza yeye mwenyewe baharini baada ya ile jahazi aliyoipanda kuzidi uzito na kumwangukia yeye kura ya kutumbukizwa baharini.

Alipokuwa ndani ya tumbo la samaki alimuomba Mola wake amsamehe kwa sababu ya yeye kudhulumu nafsi yake. Kama alivyoeleza Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Anbiyaa aya ya 87 na ya 88, "
وَذَا النُّونِ إِذْ ذَهَبَ مُغَاضِبًا فَظَنَّ أَنْ لَنْ نَقْدِرَ عَلَيْهِ فَنَادَى فِي الظُّلُمَاتِ أَنْ لا إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنْ الظَّالِمِينَ * فَاسْتَجَبْنَا لَهُ وَنَجَّيْنَاهُ  مِنْ الْغَمِّ وَكَذَلِكَ نُنْجِي الْمُؤْمِنِينَ
Maana yake, "Na Dhun-Nuun (yaani Nabii Yuunus) alipoondoka hali ameghadhibika, na akadhani ya kwamba hatutakuwa na uwezo juu yake. Basi (alipozongwa) aliita katika giza (akasema): "Hapana mungu isipokuwa Wewe Uliye takasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa wenye kudhulumu (nafsi zao). Basi tukamwitikia na tukamuokoa kutokana na dhiki. Na hivyo ndivyo tunavyowaokoa Waumini."

4. KUDHULUMU HAKI ZA WATU
Dhulma nyingine ni kudhulumu haki za watu. Na jinsi ilivyokuwa kudhulmu watu ni kitu kibaya kabisa basi hata Mwenyezi Mungu S.W.T. amejiharamishia Yeye Mwenyewe na akaifanya baina ya waja Wake kuwa ni haramu. Kama ilivyokuja katika Hadithi Qudsy iliyopokelewa na Abu Dharr R.A.A. na kutolewa na Muslim, kutokana na Mtume S.A.W., Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema, "
''إِنِّي حَرَّمْتُ عَلَى نَفْسِي الظُّلْمَ وَعَلَى عِبَادِي أَلا فَلا تَظَالَمُوا…''
 Maana yake, "Hakika Mimi nimeharamisha dhulma juu ya nafsi Yangu, na juu ya waja Wangu, basi msidhulumiane..."

Kutokana na Hadithi hii Mwenyezi Mungu S.W.T. amejifananisha sawasawa na viumbe Wake kuhusu dhulma. Kwa sababu kajiharamishia nafsi Yake kama alivyoiharamisha kwa waja Wake. Na kwa kuwa kajiharamishia nafsi Yake kwa hali hiyo hamdhulumu mtu yeyote yule hata kama punje ya uwele. Kama alivyosema katika Suratin Nisaa aya ya 40,
إِنَّ اللَّهَ لا يَظْلِمُ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ وَإِنْ تَكُنْ حَسَنَةً يُضَاعِفْهَا وَيُؤْتِ مِنْ لَدُنْهُ أَجْرًا عَظِيمًا
Maana yake, "Hakika Mwenyezi Mungu hawadhulumu (viumbe Vyake hata kitu kilicho sawa na) uzito wa mdudu chungu; na kama likiwa ni jambo jema atalizidisha na kutoa ujira mkubwa unaotoka Kwake."

Pia kasema katika Surat Yuunus aya ya 44, "
إِنّ الله لا يَظْلِمُ النَّاسَ شَيْئًا وَلَكِنَّ النَّاسَ أَنْفُسَهُمْ يَظْلِمُون
Maana yake, "Hakika Mwenyezi Mungu hawadhulumu watu chochote; lakini watu wanajidhulumu (wenyewe) nafsi zao." Na dhulma itakuwa giza kwa mwenye kudhulumu siku ya Kiyama. Kama ilivyokuja katika Hadithi iliyopokelewa na Ibn Umar R.A.A. na kutolewa na Muslim, "
''إِنَّ الظُّلْمَ ظُلُمَاتٌ يَوْمَ الْقِيَامَة''
Maana yake, "Hakika dhuluma ni giza siku ya Kiyama."

Na kama wanavyosema Waswahili kwamba: Siku za mwizi ni arubaini, basi na ndivyo hivyo hivyo kwa mwenye kudhulumu anapewa muda kidogo na Mwenyezi Mungu Mtukufu ili labda huenda akatubia, lakini akiendelea na dhulma yake basi Mwenyezi Mungu S.W.T. humkamata bila kumwachia. Kama alivyotuelezea Mtume S.A.W. katika Hadithi iliyopokelewa na Abu Musa L-Ash`ary R.A.A. na iliyotolewa na Muslim, "

 إِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ يُمْلِي لِلظَّالِمِ ، فَإِذَا وَكَذَلِكَ أَخْذُ رَبِّكَ أَخَذَهُ لَمْ يُفْلِتْهُ'' ثُمَّ قَرَأَ '' إِذَا أَخَذَ الْقُرَى وَهِيَ ظَالِمَةٌ إِنَّ أَخْذَهُ أَلِيمٌ شَدِيدٌ
Maana yake, "Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu anampa muda mwenye kudhulumu. Lakini akimkamata hamuachii." Kisha akasoma Surat Huud aya ya 102, ((Na namna hivi ndivyo inavyokuwa kukamata kwa Mola wako anapowakamata (watu wa) miji wanapokuwa wameacha mwendo walioambiwa. Hakika mkamato Wake (Mwenyezi Mungu) ni mchungu na mkali.))"
MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini