KUTABIRIWA KWAKE NA MTUKUFU MTUME (S.A.W.W)

KUTABIRIWA KWAKE NA MTUKUFU MTUME (S.A.W.W)

(1) Kutabiriwa kwake na Mtukufu Mtume (s.a.w.):

Karibu katika vitabu vyote mashuhuri vya Hadithi za Mtukufu Mtume (s.a.w.) mna bishara zimhusuzo Imamu Mahdi na waandishi kadhaa; walikusanya hadithi zenye bishara hizo. Bwana Hafidh Muhammad-bin-Yusuf Shaffi katika kitabu chake kiitwacho "Al-Bayan-fi-Akhbar-i-Sahibiz-zaman". Bwana Hafidh Abu Na'im Isfahani amezikusanya hadithi hizi katika kitabu chake kiitwacho "dhikr Ni't Al-Mahdi", Bwana Abu Dawud Sajistani katika kitabu chake kiitwacho "Sunan" chini ya kichwa cha habari maalum cha "Al-Mahdi", Bwana Tirmidh katika kitabu chake kiitwacho "Sahih Tirmidhiy", Bwana Ibn Majah katika kitabu chake kiitwacho "Sunan Ibnu Maaja" na Bwana Hakim katika kitabu chake kiitwacho "Mustadrak" wameziandika hadithi kadha wa kadha kuhusu jambo hili, mojawapo ikiwa imesimuliwa na Bwana Ibn-i-Abbas, inasema kwamba, Mtukufu Mtume (s.a.w) alisema, "Mimi ni kiongozi wa Mitume na Ali ni kiongozi wa Mawalii. Wa kwanza katika Mawalii wangu kumi na mbili atakuwa Ali na wa mwisho ni Al-Mahdi (a.s.)".

(2) Kutabiriwa kwake na Bibi Fatimah (a.s.) bint wa Mtukufu Mtume (s.a.w.):
Kufuatana na hadithi katika kitabu kiitwacho "Usulil Kafi" cha Bwana Kulaini kimenukuu kua Jabir-bin-Abdullah Ansar alisema kwamba, Bibi Fatimah (a.s.) alikuwa na ubao ulioandikwa majina yote ya Mawalii na Maimamu na aliwataja Maimamu wote kumi na wawili kwa majina yao, watatu walikuwa wanaitwa Muhammad na wanne wanaitwa Ali na wa mwisho atakuwa wa kudumu.

3. Kutabiriwa kwake na Ali (a.s.):

Sheikh Saduq Muhammad-bin-Ali ameandika katika kitabu chake kiitwacho “Ikmaluddin” hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Ali Ridha (a.s.) kwamba, Ali bin Abi Talib (a.s.) alimwambia mwanawe Husain, "Imamu wa tisa katika kizazi chako atakuwa muenezaji wa dini ya kweli na haki".

4. Kutabiriwa kwake na Imamu Hasan (a.s.):

Imamu Hasan (a.s.) amesema katika Hadithi iliyoandikwa katika kitabu hicho "Ikmaluddin" kuwa, "Atakapozaliwa wa Imamu wa tisa katika ambaye atatokana na kizazi cha ndugu yangu Husain, Mwenyezi Mungu atampa maisha marefu katika muda ambo yeye hatadhihirika mbele za watu na utakapowadia wakati wa kudhihiri kwake Mwenye Enzi Mungu atamdhihirisha.

5. Kutabiriwa kwake na Imamu Husain (a.s.):

Imamu Husain alisema, "Imamu wa tisa watakaotokana na kizazi changu ni Imamu yule atakayeitetea Haki, na Mwenyezi Mungu ataihuisha hii Dunia iliyokufa na dini ya haki itazishinda dini zote. Muda wake wa kutoonekana utakuwa mrefu, na katika muda huo watu wengi watapotoka na wachache tu watabaki katika imani, nao watateswa. Kwani watu watawaambia, "Kama nyinyi ni wakweli, basi tuambieni lini ubashiri huo utatimia". Watavumilia (hao wenye kuamini) na watapata baraka sawa na zile za waliopigana pamoja na Mtume.”

6. Kutabiriwa kwake na Imamu Ali Ibnul- Husain (a.s.):

Imam Ali Zainul Abidin (a.s.) alisema “Wa mwisho wetu atakuwa yule ambaye kuzaliwa kwake kutakuwa kwa siri kiasi ambacho watu wa kawaida watasema kuwa bado hajazaliwa”.

7. Kutabiriwa kwake na Imamu Muhammad Al-Baaqir (a.s.):

Sheikh Kulini ameandika kuwa Imam Baqir (a.s.) alisema, "Wapo Maimamu tisa baada ya Husain, wa tisa wao atakuwa wa kudumu".

8. Kutabiriwa kwake na Imamu Jafar - Sadiq (a.s.):

Sheikh Saduq ameandika kuwa lmamu Jafar (a.s.) alisema,
"Wa tano katika kizazi cha mwanangu, Musa, atakuwa ni Imamu wa kudumu miongoni mwa Maimamu wanaotokanana ukoo wa Muhammad (s.a.w.)".

9. Kutabiriwa kwake na Imamu Musa Kadhim (a.s.)

Sheikh Saduq ameandika kuwa Imamu Musa (a.s.) alisema, "Mtu mmoja alimwuliza Imam Musa Kadhim, "Wewe ni Qaim bil Haqq” (msimamizi wa haki)? Alimjibu, “Ndiyo, mimi, lakini huyo al-Hasan atakayekuwa Qa’im (wa kudumu) ni yule atakayeisafisha ardhi ya Mwenyezi Mungu kutokana na maadui Wake Mwenyezi Mungu na ataijaza haki. ….

10. Kutabiriwa kwake na Imamu Ali Ridha (a.s.):

Mshairi mmoja Bwana Di'bal alipokuwa akisoma shairi lake maarufu Ienye sifa (za Maimamu) mbele ya Imamu Ridha (a.s.), alisoma kifungu kinachosema hivi:

"Na hakika Imamu wetu atakuja.
"Na ataliimarisha Jina Ia Mwenyezi Mungu na baraka Zake.
"Atatupambanulia baina ya jema na ovu.
"Na atawalipa watu wote thawabu na adhabu."

Imamu aliIia na alisema, "Unajua kwamba umeletewa vifungu hivi na Roho Mtakatifu? Unajua ni nani Imamu huyo na lini atadhihirika?" Yule mshairi alijibu kuwa hajui; alichokisikia ni kwamba atakuwepo Imamu katika ukoo wa Mtume (s.a.w.) atakayeitakasa dunia na kuijaza haki. Kisha Imamu alisema, "Ewe Di'bal, mwanangu Muhammad atakuwa Imamu baada yangu na baada yake mwanawe Ali, na baadaye mwanawe Hasan, na baadaye mwanawe Al-Qaim, ambaye atangojewa wakati wa kutoonekana kwake na atakapodhihirika, dunia nzima itamheshimu.”

11. Kutabiriwa kwake na Imamu Muhammad Taqi (a.s.):

Imamu Taqi (a.s.) amesema, “Wa kudumu katika sisi atakuwa yule Mahdi, atakayekuwa wa tatu katika mfululizo wa kizazi changu".

12. Kutabiriwa kwake na Imamu Ali Naqi (a.s.):

lmamu Naqi (a.s.) amesema, Mrithi wangu atakuwa mwanangu Hasan, lakini hali yenu itakuwaje wakati wa mrithi wake? Alipoulizwa aeleze zaidi alisema, "Hamtakuwa salama hata kulitaja jina lake, achilia mbali kutaka kumwona". Aliulizwa, "Basi vipi tukalitaja jina lake?" Alisema, "Itakuwa hivi: "kwa dalili kutoka miongoni mwa ukoo wa Mtume".

13. Kutabiriwa kwake na Imamu Hasan Askari (a.s.):

lmamu Hasan (a.s.) aliulizwa, "Masayyidi wako (amani ya Mwenyezi Mungu iwawie wote) walisema kwamba dunia haiwezi kumaliza bila ya dalili ya Mwenyezi Mungu kudhihiri (Imamu Mahdi (a.s) na yeyote yule atakayekufa bila kumjua lmamu wa wakati wake hufa kifo cha kikafiri". Alijibu, "Hakika,hii ni wazi kabisa kama mwanga wa mchana". Tena aliulizwa, "Basi nani atakayekuwa mrithi wako? Alijibu, "Mwanangu, Mwenye jina Ia Mtume atakuwa mrithi wangu na yeyote atakayekufa bila ya kumtambua atakufa kifo cha ujinga. Muda wa kutoonekana kwake utakuwa mrefu hata majahili (wale wasiomjua) watasumbuka hapa na pale na waovu watapata laana ya milele na wale watakaotabiri wakati wake maalum wa kuonekana (wa kudhihiri kwake) watakuwa wanasema uwongo".

Hadithi hizi na tabiri zote hizi zinaonyesha kwamba tokea wakati wa Mtume mwenyewe (s.a.w.) kumetajwa kuwapo kwa mtu "Aliyeongozwa" katika dini" (Imamu Mahdi a.s). Si hayo tu, lakini kisa cha shairi la Di'bal kinaonyesha kuwa suala hili ni muhimu sana hata washairi wakaanza kulitungia mashairi. Historia inaonyesha kwamba marafiki na maadui wote kwa pamoja walikuwa na taarifa kamili ya hadithi hizo na daima walijaribu kuzitumia hadithi hizi kwa kuendelezea hoja zao mbaya. Kwa mfano, Khalifa Muhammad wa ukoo wa Bani Abbasi, alijipa jina la Mahdi ili kuwadanganya watu. Katika dhuria wa Imamu Hasan (a.s.), Muhammad mwana wa Abdullah Mahaz vilevile aliaminiwa na baadhi ya watu kuwa yu Mahdi na madhehebu ya Kaisania yalitamja kuwa Muhammdd Hanafiyah yu Mahdi. Lakini dhana ya mtu Mtakatifu kutoka katika ukoo wa Mtume (s.a.w.) iliyashinda madai ya wale wote waliojifanya Mahdi. Kila mara dhuria wa Mtume (s.a.w.) wamekuwa wakitoa maelezo kamili kuhusu Mahdi wa kweli na kutoonekana kwake, maelezo ambayo yalionyesha wazi wazi kuwa Waislamu wamekuwa wakimngojea Mahdi wa kweli. Zaidi ya hapo hadithi za Mtume (s.a.w.) zinazowataja Maimamu hawa kumi na wawili zinaonyesha uwongo wa madai ya walaghai hawa. Lakini wakati wa Imamu Hasan Al-Askari, Maimamu kumi na moja wa Mtume (s.a.w.) walishatokea na ulimwengu wa Kiislamu ulikuwa na hamu ya Imamu aliyekuwa akingojewa kabla ya kuzaliwa kwake, na atakayengojewa katika muda wa kutoweka kwake baada ya kuzaliwa kwake.

MWISHO