ALIYOBAINISHA MOLA KATIKA KUIFAHAMU QUR_ANI

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

MSINGI WA KUIFAHAMU QUR_ANI.3

ALIYOBAINISHA MOLA KATIKA KUIFAHAMU QUR_ANI

Katika makala iliyopita (makala no. 2) ambayo inahusiana na msingi wa kuifahamu Qur-ani, tulielezea misingi aliyobainisha Mwenyeezi mungu na Mtume wake katika kuifahamu Qur-ani, katika makala hiyo tumetaja msingi wa mwanzo, na katika makala hii ya sasa tutaendelea kuelezea msingi mwengine aliyoubainisha Mwenyeezi mungu katika kuifahamu Qur-ani.

2- Na akamtia il-hamu ya nguvu kabisa katika moyo wake kuwa Mungu anamwambia Mimi (Mungu) ndiye Mola wako, na Mola wa ulimwengu wote, na Mimi ndiye Mola wako, na Mungu wa ulimwengu wote. Na Mimi ndiye Mfalme wako, na Mfalme wa ulimwengu wote. Usiwe katika ulimwengu wangu huu huru kabisa kabisa, umetakabari unafanya unavyotaka wala hujali. Wala usiwe mtumwa wa asiyekuwa miye, hakuna asiyekuwa miye anayestahiki kumuabudu, kumtii na kumnyenyekea, na huu uhai uliopewa ndani yake Huriya kidogo, ndiyo wakati wa mtihani, utarejea kwangu badala yake, nitazame uliyoyafanya, niwapambanue wepi waliofuzu, na wepi walioanguka, na njia nzuri ya kufuata ni hii.

Nifanye mimi ndiye Mola wako peke yangu na ndiye wa kukuhukumu peke yangu, ufanye amali zako kama nilivyokuongoza, na uishi hapa duniani, na hali ya kua unajua kuwa umo ndani ya mtihani, na jitihadi yako yote upaasi, na ukienda kinyume na haya basi kila mwendo unaouenda ni wa makosa tu,, na ukifuata ule mwendo wa kwanza, - na wewe ni huru katika kuufuata mwendo huo, hakuna cha kukuzuilia, - si ustarehe hapa tu duniani na kutua moyo wako, bali nitakupa neema kubwa kabisa utakaporejea kwangu katika hapo mahala panapoitwa pepo, upate neema ya daima na raha ya milele bila ya kuchoka wala kutaabika, na ukifuata huo mwendo mwengine – na wewe ni huru katika kufuata mwendo huo pia- basi utapata balaa na shari na kuangamia hapa hapa duniani tu, bali akhera utakwenda motoni uipate adhabu ya milele na mchungu ya daima, na ghamu isiyokwisha.

3) Mwenyeezi Mungu amewaweka binaadamu hapa katika ardhi badala ya kuwatengezea yale tuliyoyataja, akawaleta wale watu wawili wa mwanzo – Adam na Hawa – na akawaongoa kwa uwongozi wake ili waufuate wao na kizazi chao mpaka mwisho wa ulimwengu, hakumwumba mtu katika kiza na ujahili, bali kamleta ulimwenguni kwa nuru na elimu, akawa huyo mtu wa mwanzo anajua nini haki, na akafundishwa yanayohitajiwa katika uhai huu. Nayo ni taa (kutii) ya Mwenyeezi mungu (Uislamu).

Na yeye akawausia wanawe na kizazi chake chote kuwa wasimwabudu ila Mwenyeezi Mungu, na wasife ila katika Uislamu, lakini baada ya miaka mingi aliingia kuiacha njia hii ya haki na kufuata njia zilizo potoka na kwenda upogo. Na wakapotea na kumjua Mwenyeezi Mungu vilivyo, ima kwa kutomjali au kwa kumkanusha, wakamfanyia Mwenyeezi Mungu chungu ya washirika katika viumbe vya ardhi na mbinguni, wengine wa kuonekana na wengine wako katika fikra zao tu, na wengine wa kibinaadamu na wengine, na wengine viumbe wengine.

Na ile elimu ya haki waliichanganishia namna namna na elimu nyengine zisizokuwa za kutegemewa

4) Na ile huria ya kiasi maalumu aliyopewa mwanaadamu haimpelekei Mwenyeezi Mungu kumrejeza – kwa nguvu – aliyepotea ili aende njia sahihi, akitaka asitake, na ule muda aliompa wa kuishi haumpelekei Mwenyeezi Mungu kwenda kumuangamiza mara moja kwa kuwa anakhalifu amri zake, Kisha Mwenyeezi Mungu akajiwajibishia – tangu mwanzo wa kuja ubinaadamu – kuwatengenezea wanaadamu njia ya kuwaongoza katika huu uhao wao, na akawachagua Mwenyeezi Mungu kwa Irada yake watu katika wanaadamu wamemuamini vilivyo wakafuata wanayoyapenda, akawafanya wajumbe wake, akawapelekea ujumbe wake, na akawaletea elimu ya haki, akawafundisha njia njema ya kuwaongoza, tena akawaamrisha wawalinganie wanaadamu wenzao kufuata njia iliyonyooka waliyoitupa na kuiwacha.

5)Mitume hawa wakapelekwa kwa watu mbali mbali, Mwenyeezi Mungu akadumu kuwaleta tu tangu alfu ya miaka baada ya miaka, hata idadin yao ikawa alfu nyingi, na  wote waliokuwa juu ya dini moja- mwendo ule ule aliokuja nao yule binaadamu wa mwanzo alipoteremka kwenye ardhi, wakawa wanaufuata uongozi ule ule katika sharia na Akhlaqi na ustaarabu, na makusudio yao yalikuwa mamoja, nayo ni kuwaongoza wanaadamu katika dini ya Mwenyeezi mungu na uwongozi wake, basi wale waliokubali mwendo wao walichanganyika wakawa umma mmoja unaofuata hukumu za Mola wake na kutii njia yake, na wakajipania kuwazuilia wengine kukhalifu mwendo huo mzuri, basi hao Mitume walifanya jitihada kuufikisha ujumbe waliopewa, lakini wengi wa watu hawakufuata, na waliofuata waliingia kidogo kidogo katika kufisidi na kupotea. Kuna wengine waliopotea kabisa kabisa, na kuna wengine walioyageuza maneno ya Mwenyeezi Mungu waakayaandika kwa namna waipendayo wao.

6)Na mwisho kabisa (katika uma wa mwisho) akaletwa Nabii Muhammad(s.a.w.w) katika ardhi ya Waarabu kwa ile ile kazi waliyoletwa Mitume wengine waliotangulia. Kukawa kulingania kwake ni kulingania wanaadamu wote pia hata wale waliokuwa wafuasi wa Mitume waliotangulia wakapotea njia, ikawa kazi yake ni kuwalingania wanaadamu wote wende njia iliyonyooka na uongozi wa Mwenyeezi Mungu, wakawa wale walioamini ulingano huu ni Uma mmoja unaofuata ulingano wake, na wakawalingania wengine kufuata ulingano huo wa kuwatengenezea dunia yao, ili itengenee na Akhera yao pia.

Na hii Qur-ani ndicho kitabu cha kulingania hayo na uteremsho wake Mwenyeezi Mungu juu ya Nabii Muhammad, uwe uongofu na nuru ya kuongozwa anaowataka katika waja wake.

Basi baada ya kwisha kujua msingi wa Qur-ani, kutakuwa kwepesi kwake kufahamu hakika ya kitabu hiki, na lipi la kulitafuta ndani yake.

MWISHO