MASHARTI YA KUFUTWA HUKUMU

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
NASKH NA MANSUKH NDANI YA QUR_ANI.3
MASHARTI YA KUFUTWA HUKUMU.
Katika makala iliyopita (makala no 2) tulizungumzia kuhusu ufutwaji wa hukumu za Aya ndani ya Qur-ani, katika makala hii basi tutazungumzia masharti ya kufutwa kwa hukumu hizo na kuletwa hukumu nyengine.

Ufutwaji wa hukumu una masharti yake nayo ni:-

1. Aya hizo ni lazima ziwepo katika masuala ya hukumu za kisheria, yaani aya zozote zile zitakazokuwa hazizungumzii masuala ya kisheria, haziwezi kuingia katika suala hili.

2. Maudhui ya mwanzo yaliyokuwepo katika aya na yanayotaka kufutwa ni lazima yawe maudhui hayo hayo yaliyokuja katika aya ya pili itakayofuta aya ya mwanzo, (yaani isije ikawa aya ya mwanzo inazungumzia hukumu fulani katika hali ya hiyari, au hali ya siha, na maudhui ya pili yaliyokuja katika aya ya pili yakawa yanazungumzia suala hilo katika hali ya ugonjwa), yaani (hukumu ya mwanzo ilikuwa ikimzungumzia mgonjwa, na hukumu iliyokuja kwa mara ya pili ikamzungumzia mtu mwenye afya kamili). Kwani kila maudhui yaliyokuja katika aya hizo mbili yatakua yana hukumu yake pekee wala hayaingiliani kimaudhui wala kihukumu.

3. Ni lazima aya hizo ziwe hazioani kwa njia yoyote ile, na moja iwe kinyume na nyengine,

Kiasi ya kwamba kuwe hakuna uwezekano wa kuzioanisha na kuzikusnya pamoja hukumu za aya hizo, kwa hiyo kama kutakuwa kuna uwezekano wa hukumu mbili hizo kupatikana katika zama moja bila ya mgongano, aya hizo zitakuwa hazihesabiwi kuwa aya ya pili imekuja kuifuta ile aya ya mwanzo,

4. Hukumu au aya ya mwanzo ni lazima iwe pale ilipoainishwa kwa mara ya mwanzo kabisa haikuwekewa muda maalumu hukumu hiyo, kwani iwapo aya hiyo itakapokuwa imewekewa muda maalumu pale ilipoainishwa, basi aya hiyo itakuwa haifanyi kazi tena baada ya kumalizika muda wake uliopangwa mwanzo, na hukumu hiyo yenyewe kwa wenyewe itakuwa imefutika bila ya kuhitajia aya nyengine kuja kuifuta hukumu ya aya hiyo.

Kwa hiyo kutokana na maelezo hayo tumefahamu kuwa:-

Ufutwaji wa Aya ndani ya Qur-ani unapatikana katika sura tofauti, baadhi yake ni zenye kukubalika, na nyengine sio zenye kukubalika, na sura hizo ni kama zifuatazo:-

1. Kufutwa Aya pamoja na maandishi yake, kiasi ya kwamba hukumu iliyobeba maneno hayo yote mawili yafutwe kabisa katika Qur-ani.

2. Kufutwa Aya peke yake, yaani maneno ya Aya yawe yamefutwa katika Qur-ani, lakini hukumu iwe bado inafanya kazi katika Qur-ani.

3. Hukumu ifutwe kutoka kwenye Qur-ani, lakini maneno yanayoizungumzia hukumu hiyo ya Qur-ani yabakie kama yalivyo. Na ufutwaji huo wa hukumu unaitwa ufutwaji wa yale yaliyomo ndani ya Aya.

4. Kufutwa hukumu ya Aya kutokana na sababu maalumu, na tofauti baina ya ufutwaji huu na ufutwaji wa namba ya tatu, ni kwamba ufutwaji tuliozungumzia katika kipengele cha tatu, ni kwamba hukumu huwa imefutwa na Aya hubakia katika sehemu yake na kusomwa kama kawaida, na hukumu hiyo huwa imefutwa moja kwa moja bila ya kurejeshwa tena, lakini ufutwaji tuliozungumzia katika namba ya nne, ni kwamba hukumu huwa imefutwa kwa sababu ya kupatikana masharti fulani, na wakati wowote masharti hayo yatakapoondoka hukumu hiyo itarudi kama kawaida, yaani (iwapo sababu zilizoifanya hukumu hiyo ipangwe zitapatikana tena katika zama zozote zile basi hukumu hiyo itarudia tena.

Kwa mtizamo wetu sisi, miongoni mwa vipengele vyote hivyo tulivyovitaja ni vipengele viwili vinavyokubalika na ndivyo vilivyokuja katika Qur-ani, navyo ni kipengele cha tatu na kipengele cha nne, lakini kipengele cha kwanza ambacho ni kufutwa kwa Aya pamoja na hukumu iliyokuja katika Aya hiyo, ingawaje ni kitu ambacho mtu anaweza kujaalia na kufikiria katika akili yake lakini hakikupatikana kipengele hicho katika Qur-ani, na kipengele cha pili ni hivyo hivyo, katika Qur-ani hatuna Aya ya aina kama hiyo ya ufutwaji katika Qur-ani, na wala kipengele hicho hakiingii, yaani Aya iwe imefutwa katika Qur-ani ,lakini hukumu iwe bado inafanya kazi.

 

MWISHO