MIUJIZA INAYOELEZEA MAMBO YA KISHERIA

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
 VIPENGELE VYA MUUJIZA WA QUR-ANI (2). C
3. MIUJIZA INAYOELEZEA MAMBO YA KISHERIA
Mwanaadamu siku zote yuko katika hali ya kujiuliza masuala kuhusiana na uumbaji na vile vilivyomo ulimwenguni, na anafanya jitihada sana ili kupata jawabu ya kumkinaisha ya masuala yake hayo, miongoni mwa masuala anayojiuliza ni kama haya yafuatayo:-

Amekuja kutoka wapi? Sababu gani iliyomfanya aje? Na baadaye atakwenda wapi? Na masuala mengi mengineyo …, ama jitihada zote anazozifanya hajaweza kupata jawabu itakayomuonyesha kwa uwazi siri ya uumbwaji wa dunia hii na vilivyomo.

Alla (s.w) katika Suratul- al-Israa Aya ya 85 anasema:-

وَيَسْاَلُونَكَ عَنِ الرُّوحِ قُلِ الرُّوحُ مِنْ اَمْرِ رَبِّى وَمَا اُوتِيتُم مِّن الْعِلْمِ إِلاَّ قَلِيلاً[1]

Na wanakuuliza habari ya roho. Sema: “Roho ni jambo lililokhusika na Mola wangu (Mwenyeezi Mungu). Nanyi hamkupewa katika elimu (ujuzi) ila kidogo kabisa. (Nayo ni ilimu ya vitu visivyokhusika na roho)”.

Dini – vile ambavyo imeelezewa katika Qur-ani – imeelezea na kuyajibu masuala yote hayo kwa kiasi cha kutosheleza kabisa, kama tutazingatia kwa makini kile ambacho kimeelezewa ndani ya Qur-ani akili za wanaadamu zitakuwa ni zenye kufikiri kwa kiadilifu, na watagunduwa njia ya kuwaongoza katika ukamilifu.

Na katika Suratul-Yunus Aya ya 57 anasema:-

اَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاء لِّمَا فِى الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ[2]

Enyi watu! Yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu na poza la (dawa ya) yale yaliyomo vifuani, na uongofu (mkubwa) na rehema kwa wanaoamini. (Nayo ni Qur-ani ambayo ikifuatwa humtengenezea mtu dunia yake na Akhera yake).

Maelezo kuhusiana na Aya ya 57 ya Suratu-Yunus

Hapa wanatajiwa wanaadamu fadhila kubwa kabisa iliyowajia kwa kuteremshiwa Qur-ani, aliyokuja nayo Nabii Muhammad; tena wanatakiwa waishukuru neema hiyo – si Waislamu tu. Kwani ustaarabu tunauona umetapakaa ulimwengu mzima kwa wasita wa Wazungu, hawa wazungu wameupata kwa Waislamu walipotawaliwa na hao Waislamu huko kwao Ulaya. Wakakaa chini ya utawala wa Kiislamu kwa upande wa Magharibi kiasi cha miaka mia sita, na kwa upande wa Mashariki kiasi cha miaka mia nne. Wakati huo ndipo walipouona ustaarabu wa Kiislamu, na wakasoma elimu za kiislamu katika vyuo vikubwa (university) vya kiislamu.

Mpaka baadhi ya Ma-Pope walisoma katika maskuli ya hao waislamu yaliyokuwako huko Ulaya, na yaliyokuwako Asia nzima na yaliyokuwako kaskazini ya Africa.

Kama sasa watu wanavyokwenda kusoma katika maskuli ya wazungu, basi ndivyo ilivyokuwa hapo zamani – hata wasiokuwa Waislamu – wanakwenda kusoma katika skuli za Kiislamu. Basi hii wanayoitapakaza sasa ulimwenguni ni bidhaa waliyoipata kwa waislamu, wakakisia kwa hiyo, na wakaongeza.

Kama si wenyewe        Tungeyasemaje?

Basi – kama wanajua fadhila – nawashukuru uislamu na Mtume wake – Nabii Muhammad – badala ya kumtaja kwa uovu wa kumsingizia tu.

Hayo yalikuwa ni maelezo kuhusiana na Aya ya 57 ya Surat Yunus.

Kusudio lililokusudiwa katika Aya hiyo pale Mwenyeezi Mungu aliposema atawapa watu waumini poza la dawa ya yale yaliyomo vifuani ni kumuondolea mwanaadamu huyo matatizo na mashaka aliyonayo katika maisha yake, kwani ni fitra (yaani hisia za kimaumbile) iliyomo katika kila nafsi ya mwanaadamu kujihisi ana udhaifu fulani na anahitajia mtu ambaye atamsaidia katika kumuondolea udhaifu wake huo – huyo siyo mwengine isipokuwa Mwenyeezi Mungu Mtukufu – kwa hiyo Mwenyeezi Mungu anapom-bainishia kwa uwazi mtu huyo kwamba atampa poza la maisha yake, na kumuondolea matatizo na mashaka ambayo yanamkabili katika maisha yake basi mwanaadamu huyo hatojisikia upweke kwani ana uhakika kuwa yuko mtu ambaye anamuongoza, kwa hiyo Qur-ani imemuelezea mwanaadamu kuwa ana fitra (hisia za kimaumbile) katika nafsi yake, ya kutaka msaada na muongozi katika maisha yake, lakini mwanaadamu huyo kutokana na kughafilika na dunia hawezi kujitanabahi kutokana na hali yake hiyo, basi hii ni dalili nyengine ya kuthibitisha muujiza wa Qur-ani. Kwa sababu kama Mwenyeezi Mungu hakumtanabahisha mja wake huyo kama mimi ndiye ninayekuongoza basi mwanaadamu huyo asingeliyafikia yale anayoyahitajia.

Katika makabila na tamaduni za watu wa zama za kale hadi watu wa zama za sasa wana shaka na kujiuliza masuala mbali mbali yanayohusiana na uhakika wa uumbaji wa dunia na vilivyomo, ijapokuwa Mwenyeezi Mungu aliwateremsha Mitume ili kuwaongoza wanaadamu, lakini baada ya kupita muda maelezo na miongozo iliyotowa Mitume hiyo ilibadilishwa na watu ambao walisimama kidete kupinga dini za Mwenyeezi Mungu, kwa hiyo wanaadamu hawakuweza kufahamu, wamekuja kutoka wapi, na kwanini wamekuja, na baadae watakwenda wapi? hadi pale Mwenyeezi Mungu alipoiteremsha Qur-ani ambayo aliyajibu masuala yote hayo kwa uzuri na ufafanuzi wa hali ya juu kabisa, kwa hiyo dini imejengwa kwa nyanja mbili, nazo ni maarifa ya kiislamu, na hukumu zake za kisheria, maarifa ya Kiislamu yaliyoelezewa ndani ya Qur-ani yamehifadhika na hakuna mtu yoyote atakayeyabadilisha na kuyasongomanisha, na hukumu za kiislamu vile vile ziko kamili na zimehifadhika.

 Sheria na hukumu za kiislamu zimekamilika na zina umuhimu mkubwa kwa wanaadamu, kiasi ya kwamba hakuna sheria za dini nyengine zilizokamilika zaidi ya hizo:

Moja: Sheria hizo zilizomo ndani ya Qur-ani zimeepukana na dosari yoyote yenye kuwapelekea watu kupotea kifikra,  na vile vile zimeepukana na uharibifu wowote ambao unaweza kuleta athari mbaya katika kanuni hizo za kiislamu.

Mbili: Kuzingatia mambo matatu ambayo ni muhimu katika maisha ya mwanaadamu, na jamii kwa ujumla katika dunia hii, kwa mfano uhusiano alionao mwanaadamu mwenyewe binafsi na watu wengine, uhusiano alionao mwanaadamu katika jamii, na uhusiano alionao mwanaadamu na Mola wake.

Kanuni ambazo zimewekwa na wanaadamu ni mambo mawili ya mwanzo, yaani uhusiano wa mawanadamu mwenyewe binafsi na wayu wengine, na uhusiano wa mwanaadamu na jamii, katika mambo matatu hayo watu huzingatia kwa kiasi kidogo sana katika kipengele hicho cha mwanzo, na hukipa umuhimu mkubwa kipengele cha pili, na kwa hakika wameghafilika na kipengele cha tatu yaani uhusiano uliopo baina ya mwanaadamu na Mola wake. Katika hali ambayo kipengele hichi cha tatu ndiyo kipengele bora kinachomuongoza mwanaadamu na kumpa maisha mema, na kumuondolea mahitajio yake mbali mbali yakiwemo mahitajio ya kimwili na kumfikisha mwanaadamu huyo karibu na Mola wake.

Katika sehemu hii tutaelezea kwa ufupi na kuashiria baadhi ya miujiza ya uongofu wa Qur-ani katika mambo mawili, maarifa ya kiislamu na hukumu za kiislamu.

[1] Suratul- al-Israa Aya ya 85

[2] Suratul-Yunus Aya ya 57

MWISHO