VIPENGELE VYA MUUJIZA WA QUR_ANI

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
VIPENGELE VYA MUUJIZA WA QUR-ANI (2). A

Katika somo lililopita tulielezea na kukumbushana kuwa muujiza wa Qur-ani umegawika katika vipengele vitatu, vipengele hivyo ni muujiza wa mabainisho, muujiza wa kisheria, na muujiza wa kielimu, kipengele cha mwanzo ambacho ni muujiza wa mabainisho tulikielezea katika makala iliyopita, na vipengele viwili vilivyobakia tutavielezea katika makala hii.

2. MIUJIZA YA KIELIMU ILIYOMO NDANI YA QUR-ANI:

Makusudio yaliyokusudiwa katika muujiza wa kielimu ni ishara za kielimu zilizoashiriwa katika baadhi ya aya za Qur-ani, mabainisho hayo ya kielimu hayakuwa hadafu (madhumuni) asili katika ubainishwaji wake, kwa sababu Qur-ani ni kitabu cha uongofu, na hadafu au dhumuni asili ya kuteremshwa kitabu hicho ni kumfunza mwanaadamu njia za kuishi ili afikie katika saada ya Mwenyeezi Mungu na sio kubainisha masuala ya kielimu, kwa hiyo kama katika Aya za Qur-ani tutakabiliana na ishara za kielimu ni kwa sababu maelezo hayo yaliyomo ndani ya Qur-ani yametokana na elimu pamoja na hikima za Mwenyeezi Mungu. Kwa mfano katika Suratul-Furqan Aya ya 6 tunasoma:-

قُلْ اَنزَلَهُ الَّذِى يَعْلَمُ السِّرَّ فِى السَّمَاوَاتِ وَالاَرْضِ إِنَّهُ كَانَ غَفُوراً رَّحِيماً[1]

Sema: “Ameyateremsha haya yule ajuaye siri za mbinguni na ardhini; bila shaka Yeye ni mwingi wa msamaha(na) Mwingi wa rehema. (Lau kama si hivyo mngeona).”

Katika Qur-ani kumeashiriwa ishara nyingi za kielimu, baadhi ya ishara hizo zimeonekana kwa kupita muda, na pengine baadhi ya ishara nyengine nyingi za kielimu zinaweza kudhihirika kwa kupita muda mrefu, - wanaelimu – katika zama hizi – wamefanya jitihada sana katika masuala hayo, ijapokuwa kuna baadhi yao walikosea, ama vile vile wengi wao wamefanikiwa katika kuyathibitisha masuala kama hayo, mifano mengine ya ishara hizo za kielimu imeashiriwa katika  kitabu cha Tamhiydiy, juzuu ya 6, na katika Kitabu cha Elimu ya Qur-ani, katika sehemu ya miujiza ya Qur-ani. Katika sehemu hii ili kufupisha maelezo tutaiainisha mifano miwili tu.
A. KUPATA TABU KUVUTA PUMZI KUTOKANA NA UZITO  WANAOUHISI VIFUANI MWAO   

Allah (s.w) katika suratul-Al-An-aam Aya ya 125 anasema:-

فَمَن يُرِدِ اللّهُ اَن يَهْدِيَهُ يَشْرَحْ صَدْرَهُ لِلإِسْلاَمِ وَمَن يُرِدْ اَن يُضِلَّهُ يَجْعَلْ صَدْرَهُ ضَيِّقاً حَرَجاً كَاَنَّمَا يَصَّعَّدُ فِى السَّمَاء كَذٰلِكَ يَجْعَلُ اللّهُ الرِّجْسَ عَلـٰي الَّذِينَ لاَ يُؤْمِنُونَ[2]

Basi yule ambaye Mwenyeezi Mungu anataka kumwongoza, hufungulia kifua chake Uislamu; na yule ambaye Mwenyeezi Mungu anataka kumhukumu kupotea, hufanya kifua chake kizito kinaona tabu kubwa (kufuata huo uislamu); kama kwamba anapanda mbinguni (kusikokuwa na pumzi). Namna hivi Mwenyeezi Mungu anajaalia uchafu juu ya wale wasioamini.   

Aya hiyo inaelezea kuhusu tabu ya maisha watakayoipata wale watu waliopotea, watu hao wametolewa mfano na kufananizwa kuwa wanafanya jitihada kupanda juu (mbinguni), na kwa sababu ya tabu wanayoipata hushindwa kuvuta pumzi, na kujihisi kuwa vifua vyao ni vizito.
Wafasiri wa zama zilizopita wamehitilafiana nadhari kuhusiana na Aya hiyo, baadhi ya watu hao wamesema kuwa;

Makusudio ya Aya hiyo inamzungumzia mtu ambaye anafanya jitihada katika jambo ambalo haliwezekani katu kufanyika, mtu huyo anataka kuruka mbinguni kwa kutumia mbawa mfano wa ndege anavyoruka angani, ama kutokana na kwamba ni jambo lisilowezekana, hughadhibika na kukasirika, na kutokana na ghadhabu alizonazo hufikia hali ya kupata tabu na kushindwa kuvuta pumzi, na watu wengine wamesema:-

Mfananizo uliotolewa katika Aya hiyo, ni mfano wa miti michanga inayotaka kukuwa katika msitu ulio na miti mikubwa mikubwa, ama kutokana na kuwa katika msitu huo kuna miti ya iliyosongamana na kushikamana pamoja, miti hiyo michanga haipati nafasi ya kukuwa vizuri.

Maudhui hayo yaliyotolewa kutokana na Aya hiyo hayaleti ufahamu wowote utakaofafanua kwa uwazi kusudio la Aya hiyo,

Ama kuna mtizamo mwengine wa elimu ya kileo unafahamisha zaidi maana ya Aya hii na kutowa ufafanuzi wenye muelekeo zaidi, kwa kutumia mtizamo wa kielimu unaohusiana na elimu ya kigeographia na elimu ya science kwa ujumla, kwani katika mtizamo wa kisayansi imeelezewa wazi kabisa kwamba mwanaadamu hawezi kunasibiana na hali ya hewa iliyoko angani, kwani kila anapoiwacha ardhi kwa masafa marefu zaidi ndipo hewa ya oxygen inazidi kutengana naye, na ni hali hiyo hiyo ukielekea chini ya ardhi (baharini).

Makosa waliyoyafanya wafasiri wa zama zilizopita ni kuyafafanua maelezo ya Aya hii يَصَّعَّدُ فِى السَّمَاء – kutokana na shida iliyopo katika (صاد) na (عين), na wameifahamu herufi (فِى) kuwa inaleta maana ya - kwa ajili ya kupanda mbinguni - katika hali ambayo kama ikichukuliwa maana hiyo ni lazima ingelitumika herufi (الي), badala ya herufi (فِى), na neno (يَصَّعَّدُ), kilugha lisingelikuwa na maana ya (صعود), yaani (kupanda juu).

Bali kutumika neno (يَصَّعَّد) – katika mlango wa (ثفعل), : (tafaulu) (تصعد) ) ( tasaudu) lina maana ya (kuwa katika tabu), na kutokana na kupata tabu huko humsababishia mtu kupata tabu katika kuvuta pumzi, na, katika istilaha za kilugha neno (تصعد نفسه), ).

 (tasaada nafsuhu) lina maana ya kuvuta pumzi kwa tabu, na kifua huhisi maumivu makali, na neno (صعود) na (صعد), lina maana ya kupata tabu, au lina maana ya jambo ambalo ni gumu sana.

Katika Suratul-Jinni Aya ya 17 Allah (s.w) anasema:-

لِنَفْتِنَهُمْ فِيهِ وَمَن يُعْرِضْ عَن ذِكْرِ رَبِّهِ يَسْلُكْهُ عَذَاباً صَعَدا[3]

Ili tuwajaribu; (tuwafanyie mtihani) kwa hayo, na anayepuuza kumkumbuka Mola wake atamsukuma katika adhabu ngumu.

Na katika Suratul-Mudathir Aya ya 17 anasema:-

سَاُرْهِقُهُ صَعُوداً[4]

Basi nitamtesa kwa mateso makuu.

Kutokana na maana hiyo basi يَصَّعَّدُ فِى السَّمَاء كَاَنَّمَا, litakuwa na maana hii ifuatayo: yaani mfano wa mtu aliyepanda juu sana, na kutokana na tabu hiyo ngumu atakayoipata atapata tabu katika kuvuta pumzi.

Kwa hakika yule mtu ambaye atapotea (atapotoka) katika njia ya Mwenyeezi Mungu atakuwa ni mfano wa mtu atakayepata tabu sana kwa kutaka kupanda juu (mbinguni), na katika hali hiyo basi atapata tabu katika kuvuta pumzi.

Kwa kuzingatia ufafanuzi wa Aya hiyo itafahamika kuwa maana hiyo tuliyoifafanuwa ni sahihi zaidi kulinganisha na zile nadharia zilizotolewa na baadhi ya watu. Kwa hiyo pindi itakapokuwa mtu atakosa njia ya kujihifadhia wakati anapopanda juu atakutwa na matatizo hayo ya kuvuta pumzi, na kwa ishara ya masuala hayo katika zama zilizopita ilijulikana ni moja wapo katika miujiza ya elimu ya Qur-ani.

[1] Suratul-Furqan Aya ya 6

[2] suratul-Al-An-aam Aya ya 125

[3] Suratul-Jinni Aya ya 17

[4] Suratul-Mudathir Aya ya 17

MWISHO