UTUKUFU WA MWANAMKE

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI 

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

UTUKUFU WA MWANAMKE

MWANAMKE NDANI YA QUR_ANI

Mwenyeezi Mungu Mtukufu anasema:-

وَيَسْتَفْتُونَكَ فِى النِّسَاء قُلِ اللّهُ يُفْتِيكُمْ فِيهِنَّ وَمَا يُتْلَي عَلَيْكُمْ فِى الْكِتَابِ فِى يَتَامَي النِّسَاء الَّلاتِى لاَ تُؤْتُونَهُنَّ مَا كُتِبَ لَهُنَّ وَتَرْغَبُونَ اَن تَنكِحُوهُنَّ وَالْمُسْتَضْعَفِينَ مِنَ الْوِلْدَانِ وَاَن تَقُومُواْ لِلْيَتَامَي بِالْقِسْطِ وَمَا تَفْعَلُواْ مِنْ خَيْرٍ فَإِنَّ اللّهَ كَانَ بِهِ عَلِيماً[1]

Wanakuuliza nini sharia ya wanawake. Sema: Mwenyezi Mungu ana kutoleeni fatwa juu yao, na mnayo somewa humu Kitabuni kukhusu mayatima wanawake ambao hamwapi walicho andikiwa, na mnapenda kuwaoa, na kukhusu wanyonge katika watoto, na kwamba mwasimamie mayatima kwa uadilifu. Na kheri yoyote mnayo fanya Mwenyezi Mungu anaijua.

Ufafanuzi

Aya hii inahadidisha adhabu ya wenye kuwadhulumu wanawake, kama ilivyoshadidishwa adhabu ya wenye kuwadhulumu mayatima. hao wote takriba ni wanyonge basi isiwe “Mnyonge Msonge.”

Kwa ufupi maana ya Aya ni kuwa waislamu walimtaka Mtume kuwabainishia hukumu ya wanawake. Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamwambia Mtume wake:

waambie Mwenyezi Mungu amewabainishia sehemu ya hukumu hii na sasa anawabainishia sehemu nyingine, la muhimu kwenu ni kufanya uadilifu na kuitumia hukumu hiyo. Kisha akawabainishia Mwenyezi Mungu (s.w.t.), katika Aya inayofuatia hukumu ya mwanamke, anayehofia unashiza wa mumewe na kuachana na mumewe.

 وَإِنِ امْرَأَةٌ خَافَتْ مِن بَعْلِهَا نُشُوزًا أَوْ إِعْرَاضًا فَلاَ جُنَاْحَ عَلَيْهِمَا أَن يُصْلِحَا بَيْنَهُمَا صُلْحًا وَالصُّلْحُ خَيْرٌ وَأُحْضِرَتِ الأَنفُسُ الشُّحَّ وَإِن تُحْسِنُواْ وَتَتَّقُواْ فَإِنَّ اللّهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا[2]

 Ikiwa mke atahofia mumewe kuwa nashiza au kumtelekeza, basi hapana vibaya juu yao kusikilizana kwa suluhu; Na suluhu ni bora. Na nafsi zimewekewa mbele uchoyo. Na mkifanya wema na mkajihifadhi, basi Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa myatendayo.

Maelezo kuhusiana na Aya

Mambo ya kuachana yanavunjwa nguvu sana katika sheria ya kiislamu, na watu wengine mara huchokana wakaona tabu kutekelezeana haki zao za ndoa, Ima mke hamkamilishii mume haki zake, au mume hamkamilishii mke haki zake.

Basi inataka yule asiyekamilishiwa asipande mori akaacha (akiwa mwanamume) au akataka kuachwa akiwa mwanamke, kwani subira yavuta kheri.

Lakini nyoyo zina ubahili kila mmoja hakubali kusamehe haki yake, Basi kila mtu apigane na moyo wake akubali kusamehe baadhi ya haki zake- bali hata zote pia-  Na Mwenyeezi Mungu atampa haki kubwa, na wanawake ndio sana wasiokubali kuona wanaonewa,basi ndiyo maana hapa akatajwa mke kuambiwa astahamili, basi na mume ndiyo vivyo hivyo.

 وَلَن تَسْتَطِيعُواْ أَن تَعْدِلُواْ بَيْنَ النِّسَاء وَلَوْ حَرَصْتُمْ فَلاَ تَمِيلُواْ كُلَّ الْمَيْلِ فَتَذَرُوهَا كَالْمُعَلَّقَةِ وَإِن تُصْلِحُواْ وَتَتَّقُواْ فَإِنَّ اللّهَ كَانَ غَفُورًا رَّحِيمًا[3]

 Nanyi hamwezi kufanya uadilifu (kweli kweli) baina ya wake, ijapokuwa mtataka kufanya hivyo kwa hiyo msielekee (upande mmoja) kabisa kabisa msije, mkamwacha (huyo mwingine msiyempenda) kama aliyetundikwa. Anasukumika huku na huku , hajijuwi kuwa ana mume au mjane, Na mkisuluhiana , mkisikilizana na mkamcha Mungu, basi Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

Maelezo kuhusiana na Aya

Tumebainisha katika Aya ya tatu ya Surat nisaa kuwa ukewenza umevunjwa nguvu sana na uislamu, ila ikiwa hapana budi ndiyo ufanywe. Kwani moyo ni moyo. Takriba muhali moyo kupenda vitu viwili sawa sawa na kuvifanya insafu sawa sawa, lazima utamili kumoja,Basi hapa wanaambiwa hao waume wenye kuweka uke wenza kuwa wakimili upande mmoja wajitahidi mwisho wa jitihada yao wasimili kabisa kabisa, hata kama akawa huyo mwengine hajijuwi kuwa mke au si mke, anajiona katundikika kwa uzi, anasukumika huku na huku,hajijui kasimama wapi.

 وَإِن يَتَفَرَّقَا يُغْنِ اللّهُ كُلاًّ مِّن سَعَتِهِ وَكَانَ اللّهُ وَاسِعًا حَكِيمًا[4]

 Na watakapotengana, Mwenyezi Mungu atamtosheleza kila mmoja kwa wasaa wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa Mwenye hekima.

Maelezo kuhusiana na Aya

Na ikiwa hapana budi kabisa nawaachane kama Aya ya 130 inavyosema. Ukimwacha wewe hatakuwa kaachwa na Mungu,atampata aliye bora kuliko wewe.

[1] Suratun Nisaa aya ya 127

[2] Surat Nisaa Aya ya 128

[3] Surat Nisaa Aya ya 129

[4] Surat Nisaa Aya ya 130

 

MWISHO