SIFA TUKUFU ZA QUR_ANI NO.2

                                                                                                                                       KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

MSINGI WA QUR_ANI TAKATIFU NO.2.

Katika makala zilizopita tulielezea misingi ya kuifahamu Quran takatifu, na tukaelezea baadhi ya sifa za Suratul-Faatiha, katika makala hii tunaendelea kuzielezea sifa nyengine za sura hiyo hiyo.

Suratul-Fatiha.

Imeitwa kwa jina tukufu hili kwa ajili ya mnasaba na muwafka wake, kwani tamko la Fatiha katika lugha ya kiarabu maana yake ni chanzo (mwanzo_cha kila kitu kile- kikiwa maneno au kitendo, basi hii Suratul-Fatiha ndiyo dibaji na ndio utangulizi wa Qurani.

Wakati wa kuteremka kwake.

Imeteremka sura hii mwanzo wa kuja Utume. Na hii ndio sura ya awali kuteremka kamili. Kabla yake ziliteremka Aya tu zilizomo katika sura ya Iqraa na Suratul-Muddathiri na Suratul-Muzzammil.

Miongoni mwa sifa za suratul-fatiha ni hizi zifuatazo:-

FATIHATUL_KITAAB.

KWA NINI JINA LA SURA HII NI FATIHATUL-KITAB?

Fatihatul-Kitabu inayo maana ya “mwanzo” (au utangulizi, dibaji, na kadhalika), na kutoka kwenye simulizi tofauti ambazo zimesimuliwa kutoka kwa Mtume (s.a.w.), inaweza kueleweka vema sana, kwamba Sura hii ilijulikana kwa jina hili wakati wa kipindi cha Mtukufu Mtume (s.a.w.).

Ijapokuwa Sura Al-Hamd haikuwa Sura ya kwanza kuteremshwa kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.), Qur’ani Tukufu ilipangwa wakati wa kipindi chake Mtukufu Mtume (s.a.w.) kama hivi ilivyo sasa, na mwanzo wake ulikuwa ni Sura hii hii ya Al-Hamd.

Nyaraka nyingine nyingi zipo ambazo zina thibitisha ukweli huu, kwamba Qur’ani Tukufu katika umbo ilivyo leo, ilipangwa kwa amri ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w)

Uthibitisho mwingine ni kwamba Khwarizmi, mwanachuoni maarufu wa Madhehebu ya Ahlu Sunna, kwenye kitabu kiitwacho “Manaqib” anasimulia kutoka kwa Ali ibn Riyah ambaye anasimulia kwamba Ali Bin Abi Talib na Abi ibn Ka’b walikusanya na kuipanga Qur’ani Tukufu wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.)

Ushahidi wa tatu ni usemi kwamba Hakim, mwandishi mashuhuri ameleta kutoka kwa Zayd Bin Thabit, kwenye kitabu chake “Mustadrak” kwamba Zayd anasema.

 Sisi, tuliokuwa kwenye huduma ya Mtukufu Mtume (s.a.w.), tulikuwa tunaikusanya Qur’ani Tukufu kutoka kwenye sehemu zilizo sambaa, na kila mtu, chini ya uongozi wa Mtukufu Mtume (s.a.w.), aliiweka mahali pake mwenyewe panapo stahiki.  Lakini kwa njia hii maandishi bado yalikuwa yamesambaa, hivyo Mtukufu Mtume (s.a.w.) alimuelekeza Ali (a.s.) kuikusanya (na kuipanga) Qur’ani Tukufu, na alituonya isije ikapotea.”  “Qur’ani Tukufu wakati wa Mtukufu Mtume (s.a.w.) ilipangwa na kuwa katika umbo hili ilivyo sasa.”

Kwa hali yoyote, kwa dhati, hadithi mashuhuri ya “Thaqalayn” kwamba umma wote wa Waislamu wanakubaliana pale Mtukufu Mtume (s) aliposema, “mimi ninaondoka miongoni mwenu na ninawaachieni vitu viwili …….” Kimojawapo ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) inaonesha kwamba Qur’ani Tukufu tayari ilikwisha kusanywa kuwa kitabu kimoja kilicho kamili.

Na kama tumeona simulizi ambazo zinatoa uthibitisho wa kukusanywa kwa Qur’ani Tukufu na kundi la masahaba chini ya usimamizi wa Mtukufu Mtume (s.a.w.), zinasimulia idadi tofauti za watu na haileti tatizo lolote; inawezekana kwamba kila simulizi inataja baadhi yao tu.

Majina yake

Wametaja majina mengi; yaliyo maarufu ni haya yafautayo:-

1 – Faatiha (ufunguzi): Kwa sababu ndiyo sura ya kwanza katika msahafu, na ni wajibu kuisoma mwanzo wa swala.

2 – Al-Hamdu: kwa sababu ndilo tamko la mwanzo katika sura hiyo.

3 – Ummul-Kitab na Ummul-Qur’an (mama wa Qur’an): kwa sababu imetangulia sura nyingine, ijapokuwa ni kwa kimandishi tu.  Kwani mama huwatangulia wanawe.  Na kwa vile imekusanya misingi miwili; kutaja utawala wa Mungu na utumwa wa mja, na mambo mawili hayo ndiyo nguzo ya mafundisho ya Qur’an.

4 – Sab’ul Mathani (Saba mbili) kwa sababu ina aya saba, au ina Aya saba zinazorudiwa mara mbili katika swala, au ni kwa sababu inataja mambo mawili:  Mola na mja wake.

MWISHO