DINI YA KIISLAMU NI DINI YA HAKI No.4

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

DINI YA KIISLAMU NI DINI YA HAKI NO.4

Ni sahihi kuwa neno “Dini” kwa mtazamo wa wanalugha ni neno lililozoeleka, na kila mmoja analifahamu neno hilo, lakini maana hasa ya dini si ile maana ambayo kila mmoja wetu amezoea kuisikia. Dini katika mtazamo wa kitaalamu (kiistilaha) lina maana pana zaidi.

Dini sio neno kuu lililokusanya ndani yake aina au maana zote za dini kiasi ya kwamba wakati lisilikapo liwe linamaanisha aina yoyote ile ya dini, ufafanuzi wa dini unaokubalika unatakiwa uwe umepatikana katika dini yenyewe, yaani katika vitabu vya dini. Kwa hiyo maana asili ya neno hilo inayokusudiwa hapa, ni dini ya Kiisalamu. Ndio, neno hilo lina maana maalumu, na linatumika katika dini ya Kiislamu tu .kama anavyosema Allah (s.w):-

إِنَّ الدِّينَ عِندَ اللهِ الإِسْلاَمُ وَمَا اخْتَلَفَ الَّذِينَ اُوْتُواْ الْكِتَابَ إِلاَّ مِن بَعْدِ مَا جَاءهُمُ الْعِلْمُ بَغْياً بَيْنَهُمْ وَمَن يَكْفُرْ بِآيَاتِ اللهِ فَإِنَّ اللهِ سَرِيعُ الْحِسَابِ[1]

Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu. Na walio pewa Kitabu hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa sababu ya uhasidi ulio kuwa baina yao. Na anaye zikataa Ishara za Mwenyezi Mungu basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.

Kwa hiyo Aya hiyo inathibitisha kuwa :“dini”ni neno maalumu linalotumika kwa ajili ya dini ya kiislamu tu. Na dini ya Kiislamu ndio dini ya haki aliyoiteremsha Mwenyeezi Mungu kwa ajili ya waja wake.

Kumerushwa tata na kasumba nyingi kuhusiana na kuwepo dini nyingi tofauti, baadhi ya watu wamedai kuwa dini zote ni sahihi, na watu wa dini yoyote watapata saada na ujira kutoka kwake Mola Mtakatifu, kwa hiyo saada haipatikani katika dini ya Kiislamu au madhehebu fulani tu, bali saada itapatikana katika dini zote.

Tata nyengine inayodaiwa ni kuwa dini ya Mayahudi na dini ya Manasara pia ni dini za Mwenyeezi Mungu na zimeteremshwa kupitia Mitume yake Allah (s.w). Hivyo kwa nini dini ya haki iwe ni dini ya Kiislamu tu? watu hao wanathibitisha kauli na madai yao kupitia Qur-ani takatifu, pale Allah (s.w) aliposema:-


إِنَّ الَّذِينَ آمَنُواْ وَالَّذِينَ هَادُواْ وَالنَّصَارَي وَالصَّابِئِينَ مَنْ آمَنَ بِاللهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ وَعَمِلَ صَالِحاً فَلَهُمْ اَجْرُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ وَلاَ خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلاَ هُمْ يَحْزَنُونَ[2]

Hakika Walio amini, na Mayahudi na Wakristo, na Wasabai; yeyote atakaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na akatenda mema basi watapata malipwa yao kwa Mola wao Mlezi,wala haitakuwa khofu juu yao, wala hawatahuzunika.

Maelezo kuhusiana na Aya

Muradi wa Aya hii ni kwamba jambo kubwa la kupatia mema, na kuepuka khofu na huzuni za siku ya Kiyama ni kumuamini Mwenyeezi Mungu na siku ya Mwisho, na kufanya amali njema, na hili halikuhusiana na Waislamu peke yao, bali linakusanya watu wa dini zote zilizotajwa hapo. Makubwa katika mambo mema ni kufuatwa amri za Mwenyeezi Mungu zilizobainishwa katika vitabu vyake vitakatifu, na miongoni mwa amri zilizomo katika vitabu vya Mayahudi na Manasara, ni kumuamini Mtume Mtukufu Muhammad (s.a.w.w).


[1] Surat Al-Imrani Aya ya 19

[2] Suratul-Baqarah Aya ya 62

MWISHO