SIFA TUKUFU ZA MITUME NO.1

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

SIFA TUKUFU ZA MITUME (A.S) NO 1.

*Ni sifa gani muhimu wanazotakiwa Mitume kuwa nazo ili waweze kupewa Wahyi na ujumbe kutoka kwa Mwenyeezi Mungu kwa ajili ya kuwaongoza wanaadamu?

SIFA TUKUFU ZA MITUME

Mitume Mitukufu ya Mwenyeezi Mungu imetumwa ili kuwaongoza wanaadamu katika njia ya Mwenyeezi Mungu, Allah (s.w) amewachagua  viongozi hao kuwa ni watu bora katika jamii . Kwa hiyo watukufu hao ni lazima wawe na sifa njema tukufu zitakazowavutia watu na kuwatia matumaini ya kuwa mitume hiyo ina uwezo wa kuwaongoza waja hao katika njia njema,miongoni mwa sifa hizo ni kama hizi zifuatazo:-

Kuwa na elimu ya  juu kabisa, kuja na miujiza, na kuwa na isma au (maasumu) – isma yaani kutokuwa na madhambi na kujiepusha na kumuasi Mwenyeezi Mungu Mtukufu -

1. Elimu

Elimu ni sifa bora tukufu na ni chanzo cha ukamilifu wa mwanaadamu, na sifa hii bora na muhimu ndiyo iliyomfanya Nabii adam (a.s) awe kiumbe bora kuliko hata Malaika,na kunufaika na elimu ya Mwenyeezi Mungu, na kutokana na elimu hiyo basi aliweza kufahamu uhakika wa uumbaji wa Mwenyeezi Mungu, kama anavyosema Yeye Allah (s.w):-

وَعَلَّمَ آدَمَ الاَسْمَاء كُلَّهَا ثُمَّ عَرَضَهُمْ عَلـٰي الْمَلاَئِكَةِ فَقَالَ اَنبِئُونِى بِاَسْمَاء هَـؤُلاء إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ[1]

Na akamfundisha Adam majina ya vitu vyote, kisha akaviweka mbele ya Malaika, na akasema: Niambieni majina ya hivi ikiwa mnasema kweli.

*Majina ya vitu aliyofundishwa Nabii Adam (a.s), ni majina ya vitu vyenye roho, na visivyokuwa na roho, vilivyowekwa mbele ya Nabii Adam (a.s) akaambiwa avitaje,na ililopelekea vitu hivyo kutumiwa herufi - him – baada ya – ha -  ni kwa sababu vimechanganyika vilivyokuwa na akili na visivyokuwa na akili, na hii ndio desturi ya luhga ya kiarabu.

Mwenyeezi Mungu huwapa Mitume yake Mitukufu alimu yote ambayo wanahitajia katika kuufikisha ujumbe huo kwa wanaadamu, kama anavyosema kuhusiana na Mtume Muhammad (s.a.w.w)

وَلَوْلاَ فَضْلُ اللهِ عَلَيْكَ وَرَحْمَتُهُ لَهَمَّت طَّآئِفَةٌ مُّنْهُمْ اَن يُضِلُّوكَ وَمَا يُضِلُّونَ إِلاُّ اَنفُسَهُمْ وَمَا يَضُرُّونَكَ مِن شَيْءٍ وَاَنزَلَ اللّهُ عَلَيْكَ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَعَلَّمَكَ مَا لَمْ تَكُنْ تَعْلَمُ وَكَانَ فَضْلُ اللهِ عَلَيْكَ عَظِيماً[2]

Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako na rehema yake, kundi moja kati yao linge dhamiria kukupoteza. Wala hawapotezi ila nafsi zao, wala hawawezi kukudhuru kwa lolote. Na Mwenyezi Mungu amekuteremshia Kitabu na hikima na amekufundisha uliyo kuwa huyajui. Na fadhila za Mwenyezi Mungu zilizo juu yako ni kubwa.

*Hapa Mwenyeezi Mungu anataja kuwa hakuna fadhila mtu aliyopewa na Mwenyeezi Mungu iliyo kubwa zaidi – baada ya kuumbwa na kupewa Uislamu – kuliko fadhila ya kupewa elimu.

Kila mema ya duniani na akhera yanapatikana kwa elimu, qur-ani yote na hadithi za Mtume zinahimiza kweli kweli kutafuta elimu, ya kutengeneza Akhera na ya kutengeneza dunia pia,Mtume Muhammad (s.a.w.w) anasema hivi kuhusiana na umuhimu wa elimu:-

طلب العلم فریضة علی کل مسلم و مسلمة

Yaani: Kutafuta elimu ni jambo la lazima kwa kila Muislamu mwanamme na mwanamke.

 na hii Qur-ani na hadithi za Mtume zinahimiza hata kutoka nje kabisa kutafuta hiyo elimu, baadhi ya hizi aya za Qur-ani zilizohimiza haya ni aya ya 122 ya surat-Tawba:-

وَمَا كَانَ الْمُؤْمِنُونَ لِيَنفِرُواْ كَآفَّةً فَلَوْلاَ نَفَرَ مِن كُلِّ فِرْقَةٍ مِّنْهُمْ طَآئِفَةٌ لِّيَتَفَقَّهُواْ فِى الدِّينِ وَلِيُنذِرُواْ قَوْمَهُمْ إِذَا رَجَعُواْ إِلَيْهِمْ لَعَلَّهُمْ يَحْذَرُونَ[3]

Wala haiwafalii Waumini kutoka wote. Lakini kwa nini hawatoki baadhi katika kila kundi miongoni mwao, wakajifunze vyema Dini, na kisha waje kuwaonya wenzao watakapo warejea, ili wapate kujihadharisha?

Elimu waliyonayo Mitume inatoka kwake Allah (s.w), na inaitwa (ilmu laduniy), na wanapewa elimu hiyo kupitia kwa malaika wake (jibraiyl a.s), naye huipeleka ilmu hiyo kwa Mitume kwa uaminifu wa halii ya juu kabisa,bila ya kuzidisha wala kupunguza, na kwa sababu hiyo basi hawawezi kukosea katika kuipeleka elimu hiyo, kama tunavyoshuhudia ndani ya Qur-ani:-

وَإِنَّهُ لَتَنزِيلُ رَبِّ الْعَالَمِينَ  .  نَزَلَ بِهِ الرُّوحُ الاَمِينُ  . عَلـٰي قَلْبِكَ لِتَكُونَ مِنَ الْمُنذِرِينَ[4]

Na bila ya shaka hii ni Uteremsho wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.Ameuteremsha Roho muaminifu . Juu ya moyo wako, ili uwe katika Waonyaji.

Mbali na hukumu za dini, Mwenyeezi Mungu amewafundisha na kuwapa habari Mitume yake juu ya elimul-ghaibu, kama inavyosema Qur-ani:-

عَالِمُ الْغَيْبِ فَلاَ يُظْهِرُ عَلـٰي غَيْبِهِ اَحَداً .  ِلاَّ مَنِ ارْتَضَي مِن رَّسُولٍ فَإِنَّهُ يَسْلُكُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ رَصَداً[5]

Yeye ndiye Mwenye kujua ya siri, wala hamdhihirishii yeyote siri yake. Isipo kuwa Mtume wake aliye mridhia. Naye huyo humwekea walinzi mbele yake na nyuma yake.

*Hii ni moja katika zile aya nyingi kabisa zinazovunja habari za utazamiaji.

Wapiga bao waongo       Waongo sana kabisa

Yanapita kwao mambo    Hawayajui kabisa.

[1] suratulBaqarah Aya ya 31

[2] Suratun Nisaa aya ya 113

[3] Surat Tawba Aya ya 122

[4] Surat Shuaraa aya ya 192-194

[5] Suratul-Jinni Aya ya 26-27

MWISHO