SIFA TUKUFU ZA MITUME NO.2

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

SIFA TUKUFU ZA MITUME (A.S) NO 2.

Katika makala iliyopita tulielezea kuhusu sifa tukufu za Mitume (s.a), na tukaelezea miongoni mwa sifa hizo kuwa ni elimu, katika makala hii tutaendelea kuelezea sifa nyengine ambazo wanatakiwa Mitume (a.s) kuwa nazo. Sifa ya pili ni kuwa Maasumu.

2. Ismat (maasumu).

Ismat au (maasumu) ni kujiepusha na kufanya madhambi au kumuasi Mwenyeezi Mungu, kifikra kimoyo, au kimatendo, sifa hii ni miongoni mwa sifa muhimu wanazotakiwa Mitume kuwa nazo,ili wafikie kupewa cheo cha Utume, kwa sababu kuwa maasumu ni dalili muhimu inayowapelekea watu kuwaamini na kuwa na matumaini na Mitume hiyo.

Kila mwanaadamu anayemcha Mola wake akamtii na kufuata maamrisho yake anaweza akajaaliwa kupata sifa hiyo tukufu ya kuwa maasumu, na Mwenyeezi Mungu Mtukufu huwajaalia Mawalii wake kuwa na sifa hiyo, kwa sababu Yeye ni Latifu, basi huwaongoza waja wake na kuwaepusha na hatari ya kumuasi Mola wao au kufanya madhambi. Kama anavyosema Allah (s.w):-

يَا اَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللهَ وَآمِنُوا بِرَسُولِهِ يُؤْتِكُمْ كِفْلَيْنِ مِن رَّحْمَتِهِ وَيَجْعَل لَّكُمْ نُوراً تَمْشُونَ بِهِ وَيَغْفِرْ لَكُمْ وَاللهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ[1]

Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na muaminini Mtume wake, atakupeni sehemu mbili katika rehema yake, na atakujaalieni muwe na nuru ya kwenda nayo. Na atakusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.

Ismat ya Mawalii wa Mwenyeezi Mungu, na ismat ya wacha Mungu ni kutokana na kutofanya maasi, ama Mitume ya Mwenyeezi Mungu wao kuwa maasumu ni kutokana na kuwa wao wana wadhifa wa kufikisha ujumbe wa Mwenyeezi Mungu kwa wanaadamu, kwa hiyo Mwenyeezi Mungu Latifu amewajaalia Mitume yake hiyo kutofanya makosa hata kwa kukosea, kuwa na nia ya kufanya maasi, au hata kufikiria na kuwa na mawazo ya kufanya maasi, Mwenyeezi Mungu amewaepusha nayo, yote hayo ni kwa sababu wanaadamu wawaamini na wawe na uhakika ya kile wanachobainishiwa na Mitume hiyo, kuwa ni kutoka kwa Mwenyeezi Mungu, hakijapunguzwa wala kuzidishwa, Mwenyeezi Mungu huwajaalia Mitume yake sifa hiyo tukufu, pale wakati wanapozaliwa, yaani tokea utotoni hadi mwisho wa umri wao, na hii ni kutokana na kuwa mitume hiyo ilikuwa na dhati hiyo nyoyoni mwao, yaani Mitume hawafanyi madhambi wala kumuasi Mola wao kwa kutokutii amri zake. Kama tunavyosoma:-

قَالَ رَبِّ السِّجْنُ اَحَبُّ إِلَيَّ مِمَّا يَدْعُونَنِى إِلَيْهِ وَإِلاَّ تَصْرِفْ عَنِّى كَيْدَهُنَّ اَصْبُ إِلَيْهِنَّ وَاَكُن مِّنَ الْجَاهِلِينَ

فاسْتَجَابَ لَهُ رَبُّهُ فَصَرَفَ عَنْهُ كَيْدَهُنَّ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ[2]

Yusuf akasema: Ee Mola Mlezi wangu! Nastahabu kifungo kuliko haya anayo niitia. Na usipo niondoshea vitimbi vya wanawake mimi nitamili kwao, na nitakuwa katika wajinga.

*Wale wanawake baada ya kumuona Nabii Yussuf siku ile, walipandwa na mapenzi makubwa nao, ikawa wanampelekea wajumbe kwa mfululizo, basi Nabii Yussuf akaona ni bora awe jela asalimike na wajumbe hao, kheri nusu shari kuliko shari kamili.

Basi Mola wake Mlezi akamwitikia, na akamwondoshea vitimbi vyao. Hakika Yeye ni Msikizi Mjuzi.

Vile vile Mitume ya Mwenyeezi Mungu haifanyi hiyana katika Utume wao, au katika maisha yao. Kama inavyosema Qur-ani:-

وَمَا كَانَ لِنَبِيٍّ اَن يَغُلَّ وَمَن يَغْلُلْ يَاْتِ بِمَا غَلَّ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ثُمَّ تُوَفَّي كُلُّ نَفْسٍ مَّا كَسَبَتْ وَهُمْ لاَ يُظْلَمُونَ[3]

Na haiwezekani kwa Nabii yeyote kufanya khiyana. Na atakaye fanya khiyana, atayaleta Siku ya Kiyama aliyo yafanyia khiyana, kisha kila mtu atalipwa kwa aliyo yachuma, kwa ukamilifu; wala hawatadhulumiwa.

*Hapa inakatazwa mtu kukhini hata kidogo, Hata akiwa ndiye mkubwa wao hana ruhusa kuchukua kitu japo kidogo pasi na kuwapa habari na kuwapa ridhaa zao kwanza, hata mwenyewe Mtume,seuze mtu mwengine, na kuonyesha kuwa siku ya Kiama kila mwenye kuhini atakuja na kile alichokichukua kwa khiyana, atakhayarishwe mbele ya Umma zote, kisha atiwe motoni. Kwa hiyo kama Mitume isingelikuwa waaminifu basi Mwenyeezi Mungu asingeliwapa cheo hicho cha Utume, na kama ingelikuwa inafanya khiyana basi pia Mwenyeezi Mungu asingeliwapa cheo hicho cha Utume, na angeliwalipa malipo ya adhabu yaliyo shadidi kabisa. Kama anavyosema kuhusiana na Mtume Muhammad (s.a.w.w):-

وَلَوْ تَقَوَّلَ عَلَيْنَا بَعْضَ الاَقَاوِيلِ . لاَخَذْنَا مِنْهُ بِالْيَمِينِ.  ثُمَّ لَقَطَعْنَا مِنْهُ الْوَتِينَ[4]

Na lau kama angeli tuzulia baadhi ya maneno tu, Bila ya shaka tungeli mshika kwa mkono wa kulia, Kisha kwa hakika tungeli mkata mshipa mkubwa wa moyo!

Maelezo kuhusiana na Aya ya 44 ya Surat Haaqqah.

Iliposemwa "na kama angelizua juu yetu baadhi ya maneno" inamaanisha kuzidisha au kupunguza maneno, kwa lugha ya wanazuoni yaani ni "BID-A". lakini katika kipengele hiki hatutaelezea kuhusiana na Bid-a, basi katika makala inayofuata, (makala namba 3), tutaelezea kwa kina kuhusu Bid-a na hatari zake. Tunafunga makala hii, kwa kubainisha kile tulichozungumza kuhusiana na sifa wanazotakiwa Mitume kuwa nazo. na hiyo ilikuwa ni sifa ya pili, sifa ya kwanza ilikuwa ni elimu, na sifa ya pili ni kuwa maasumu, sifa ya tatu tutaelezea katika makala zinazofuata, tunategemea mtakuwa mmefaidika na maudhui hayo, na tunamuomba Mola atuongoze katika njia anayoiridhia yeye Allah (s.w).

[1] Surat Alhadiyd Aya ya 28

[2] Surat Yussuf Aya ya 33-34

[3] Surat Al-Imrani Aya ya 161

[4] Suratul Haqah Aya ya 44-46

MWISHO