Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

MAFANIKIO YA MITUME NO.3

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

MAFANIKIO YA MITUME

*Ni dalili gani zilizowasaidia Mitume kuweza kufikisha ujumbe wao kwa wanaadamu?

MAFANIKIO YA MITUME YA MWENYEEZI MUNGU NO.3

Katika makala iliyopita, (makala namba mbili) tulielezea sababu na dalili zilizopelekea Mitume kupata mafanikio katika kufikisha ujumbe wao kwa wanaadamu, katika maelezo ya makala hiyo tulielezea dalili mbili, katika makala hii tutaelezea sababu nyengine zilizosababisha kuwaletea Mitume mafanikio katika malinganio yao.
3. IKHLASI

Miongoni mwa mawaidha ya Mitume na chanzo cha mafanikio yao ni ikhlasi, kila walilofanya Mitume ni kwa ajili ya ridhaa ya Mola wao, kama inavyosema Qur-ani:-
قُلْ إِنَّمَا اَعِظُكُم بِوَاحِدَةٍ اَن تَقُومُوا لِلَّهِ مَثْنَي وَفُرَادَي ثُمَّ تَتَفَكَّرُوا مَا بِصَاحِبِكُم مِّن جِنَّةٍ إِنْ هُوَ إِلاَّ نَذِيرٌ لَّكُم بَيْنَ يَدَيْ عَذَابٍ شَدِيدٍ[1]

Sema: Mimi nakunasihini kwa jambo moja tu - ya kwamba msimame kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wawili-wawili na mmoja-mmoja; kisha mfikiri. Mwenzenu huyu hana wazimu. Yeye si chochote ila ni Mwonyaji kwenu kabla ya kufika adhabu kali.

Maelezo ya Aya.

*Uislamu hauogopi kupingwa kwa hoja, kwa hivyo unawataka watu wake, wafikiri juu ya mambo ya Uislamu, wayapime na yao, wataona kuwa Uislamu ndiyo haki.

Mitume, wao wenyewe waliendelea na harakati (juhudi) zao za kuwalingania watu, na walipokuwa wakipata tabu au kuhujumiwa na fikra za kishetani hawakutegemea kabila, kaumu, cheo au mali za watu, hata wale waliomkhalifu Mtume na wakajenga uadui nae kwa sababu ya kabila lake, pia hakurudi nyuma bali alitekeleza wajibu wake na kuwalingania watu hao kwa kuwaongoza katika njia ya Mwenyeezi Mungu. kama inavyosema Qur-ani kuhusiana na Nabii Shuayb (a.s):-

قَالَ يَا قَوْمِ اَرَهْطِى اَعَزُّ عَلَيْكُم مِّنَ اللهِ وَاتَّخَذْتُمُوهُ وَرَاءكُمْ ظِهْرِيّاً إِنَّ رَبِّى بِمَا تَعْمَلُونَ مُحِيطٌ[2]

Akasema: Enyi watu wangu! Kwani jamaa zangu ni watukufu zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu? Na Yeye mmemueka nyuma ya migongo yenu! Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kuyazunguka yote mnayo yatenda.

Lakini tusisahau kuwa Mwenyeezi Mungu ametuahidi kuwa kila mtu ambaye atamtegemea Yeye katika mambo yake, basi Mwenyeezi Mungu anatosha kuwa Mlinzi wake. Kama anavyosema Allah (s.w):-

وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لاَ يَحْتَسِبُ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلـٰي اللهِ فَهُوَ حَسْبُهُ إِنَّ اللهَ بَالِغُ اَمْرِهِ قَدْ جَعَلَ اللهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْراً[3]

Na humruzuku kwa jiha asiyo tazamia. Na anaye mtegemea Mwenyezi Mungu Yeye humtosha. Hakika Mwenyezi Mungu anatimiza amri yake. Mwenyezi Mungu kajaalia kila kitu na kipimo chake.

4.   KUWALINGANIA WATU BILA YA KUTAKA UJIRA.

Miongoni mwa dalili nyengine zilizopelekea mafanikio ya Mitume, ni kwamba walipokuwa wakiwalingania watu kwa ajili ya kufikisha ujumbe wa Mwenyeezi Mungu hawakutaka ujira au kitu chochote kutoka kwao , kama tunavyoshuhudia katika surat Shuaraa, ndani ya sura hiyo tunasoma kauli za Mitume ya Mwenyeezi Mungu pale waliposema:-


وَمَا اَسْاَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ اَجْرٍ إِنْ اَجْرِيَ إِلاَّ عَلـٰي رَبِّ الْعَالَمِينَ[4]

Na sikutakini juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

Basi hii ni njia moja wapo iliyowafanya wanaadamu wenye kufikiri kuweza kuwaamini Mitume, na kwa imani yao hiyo waliweza kuwatii na kuwaamini Mitume. Kama tunavyosoma katika Surat Yaasin kuhusiana na Nabii Mussa (a.s):-

وَجَاء مِنْ اَقْصَي الْمَدِينَةِ رَجُلٌ يَسْعَي قَالَ يَا قَوْمِ اتَّبِعُوا الْمُرْسَلِينَ. اتَّبِعُوا مَن لاَّ يَسْاَلُكُمْ اَجْراً وَهُم مُّهْتَدُونَ[5]

Na akaja mtu mbio kutokea upande wa mbali wa mjini, akasema: Enyi watu wangu! Wafuateni hawa walio tumwa. Wafuateni ambao hawakutakini ujira, hali ya kuwa wenyewe wameongoka.

[1] Surat Saba Aya ya 46

[2] Surat Hud Aya ya 92

[3] Surat Talaq Aya ya 3

[4] Surat Shuaraa Aya ya 109

[5] Surat Yaasin Aya ya 20-21

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini