NADHARIA KUHUSIANA NA DINI NO.3

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

NADHARIA KUHUSIANA NA DINI NO.3

Katika makala iliyopita, (makala namba mbili) tulielezea baadhi ya majibu yanayohusiana na nadharia iliyotolewa kuhusiana na ufafanuzi wa dini, katika makala hii tutaendelea kuijibu nadharia hiyo.

Tano: Kuna uhakika gani ndani ya hatima na malengo hayo ya mwisho, hatima ambayo inaweza kumfanya Mwenyeezi Mungu asiwe na nafasi yoyote katika hatima hiyo, na kinyume chake, hatima hiyo iwe inaendana sambamba na washirikina au wale wasio na itikadi ya kumuamini Mwenyeezi Mungu?

Sita: Kuna maana gani inaposemwa hatima ya malengo ya mwisho? Hivi hatima hiyo ni “daraja ya juu” au ni “daraja ya juu kabisa ya Mwenyeezi Mungu isiyodirikiwa na watu”? na hatimae ni uhakika wa mwisho. Ikiwa uhakika wa mwisho ni Mwenyeezi Mungu, (ambao kwa mtazamo wa watu waliotoa nadharia hiyo, hatima ya malengo ya mwisho sio Mwenyeezi Mungu) na ikiwa mazingatio ni uhakika wa daraja ya juu ya Mwenyeezi Mungi (ambao haudirikiwi na wanaadamu). yaani sifa tukufu za Mwenyeezi Mungu, kwa mfano:-

Mwenye nguvu na qudra, Mwenye rehema, mmiliki wa kila kitu, n.k. uhakika huo hauko katika nguvu au uwezo wa binaadamu, kwa sababu imani sio dini, imani ni kumuamini na kumkubali Mwenyeezi Mungu katika pande zote, hivyo mwenye kumkubali na kumtii Mwenyeezi Mungu ni lazima sifa zake, matendo yake, mwenendo wake, n.k. vyote viendane na maamrisho yake Allah (s.w). ikiwa kusudio la malengo ya hatima ya mwisho ni daraja ya juu, daraja hiyo haiwezi kufikiwa na mapagani, wala washirikina, wala watu wengine wowote wasio na imani na Mwenyeezi Mungu – kijumla watu wote- kwa sababu daraja hiyo ni mahasusi kwa Mola Mtakatifu tu.

kwa hiyo, natija tunayoipata kutokana na maelezo hayo ni kwamba; hatima ya malengo hayo ya mwisho ni madai ya baadhi tu yaliyobuniwa na watu wenyewe binafsi, inawezekana kutokana na mahitajio wanayoyahitajia, mahitajio ambayo hawawezi kuyapata kwa nguvu au uwezo wao wenyewe.

Hivi mbali na dhati na utukufu wake Mwenyeezi Mungu inawezekana kuwa na miungu mwengine?, basi uhakika wa hatima ya mwisho sio kitu chengine isipokuwa utukufu wake Allah (s.w), hivi kutokana na maelezo hayo hatuwezi kupata natija ya kuwa fikra hizo zinathibitisha ulazima wa kuwepo dini, dini ambayo inaweza kudhamini mahitajio ya wanaadamu, dini hiyo si nyengine isipokuwa ni dini ya Kiislamu.

Saba: Tukijaalia kwamba, kuwa na imani na hatima ya mwisho, kunaendana na kuwa na imani na Mwenyeezi Mungu, imani bila ya kuwa na imani na Mitume, siku ya Kiama, Malaika n.k. hiyo si imani wala sio dini. Na ikiwa imani hiyo itatumiwa katika kuifafanua dini, basi huo utakuwa ni ufafanuo wa dini usio sahihi, bali ni ubunifu wa watu, ambao wanaifafanua dini kutokana na fikra zao, na hiyo sio njia sahihi ya kuifafanua dini, bali ni kuifuta dini katika uhakika wake.

Natija ya hayo ni kuwa dini ya haki ni dini moja tu, nayo ni ile dini inayotoka kwake Mola mmoja, Mola ambaye ndiye anayestahiki kuabudiwa na kila mmoja wetu.

Nane: Kuna uthibitisho gani unaothibitisha kuwa kila hatima ya mwisho ina utakatifu?, utakatifu ambao una thamani na kumfanya mwanaadamu atafute muabudiwa?.

Tisa: kwa uthibitisho gani tunaweza kuthibitisha kuwa kutokana na malengo ya hatima ya mwisho mwanaadamu hulazimika kuwa na tabia njema? Basi kwa wale ambao hawana mazingatio hayo hawana ulazima wa kuwa na tabia hizo? Hivi kweli watu ambao hawanufaiki na mazingatio hayo hawajui mema na hawana mapenzi ya kitu chochote katika nafsi zao?.

Kumi: Hivi kweli kila kusalimu amri ni ibada? - kusalimu amri yaani kuporomoka kwa taadhima kwa ajili ya kutoa heshima – na hivi kweli kila aina ya kusalimu amri ni imani na maabudu ya dini? Kama sivyo hivyo basi ni kusalimu amri kwa aina gani kunadhihirisha imani na dini? Hivi kweli ibada ni miongoni mwa kusalimu amri? Basi kwa nini ni lazima tupambanue baina ya dini na kusalimu amri? Na ibada isiwe miongoni mwa uhakika wa dini?

Hayo yalikuwa ni baadhi ya majibu tu tuliyoyatoa kuhusiana na nadharia hiyo ya ufafanuzi wa dini.

MWISHO