NJIA ZA UFUMBUZI WA DINI NO.1

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

NJIA ZA UFUMBUZI WA DINI NO. 1

Tunaweza kuufafanua ufumbuzi wa dini katika njia mbili zifuatazo:-

1. kwa kuifanyia uhakiki nafsi ya mwanaadamu mwenyewe.

2. Katika ulimwengu wa MIYTHAAQ (میثاق).

Ulimwengu wa Miythaaq unarejea katika kile kipindi ambacho Mwenyeezi Mungu alimuumba mwanaadamu. Pale Allah (s.w) alipowauliza waja wake,

 وَإِذْ اَخَذَ رَبُّكَ مِن بَنِى آدَمَ مِن ظُهُورِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَاَشْهَدَهُمْ عَلـٰي اَنفُسِهِمْ اَلَسْتَ بِرَبِّكُمْ قَالُواْ بَلَي شَهِدْنَا اَن تَقُولُواْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّا كُنَّا عَنْ هَذَا غَافِلِينَ[1]

Na pale Mola wako Mlezi alipo waleta katika wanaadamu kutoka migongoni mwao kizazi chao, na akawashuhudisha juu ya nafsi zao, akawaambia: Je, Mimi si Mola Mlezi wenu? Wakasema: Kwani! Tumeshuhudia. Msije mkasema Siku ya Kiyama sisi tulikuwa tumeghafilika na hayo.

Maelezo kuhusiana na Aya:-

Muradi wa Ayah ii ni kuwa; Mwenyeezi Mungu amemtia kila Binaadamu ujuzi wa kujitambua kuwa yeye ameumbwa, na yuko aliyemuumba, na huyo ndiye Mwenyeezi Mungu. Basi hana hoja ya kusema kuwa alipotezwa na wazee wake wala nani. Sio hoja hiyo kwani kila mmoja amepewa akili na utambuzi, kwa nini anajifuatia tu.

2. Dini ni jambo la haki na lenye uhakika kifitra linalothibitishwa katika nafsi za wanaadamu wote, na katika vipindi vyote vya historia ya mwanaadamu, kwa hiyo dini imeteremshwa wakati mmoja pale tu alipoumbwa mwanaadamu. (yaani, dini na wanaadamu vimetumwa na Mwenyeezi Mungu wakati mmoja), dini ni mfumo maalumu wenye fungamano na unaoendana na matakwa ya wanaadamu. Kwa hiyo kuna fungamano baina ya nafsi ya mwanaadamu na dini. kwa hakika matakwa ya dini ndio matakwa ya mwanaadamu. Kwa ufupi tunaweza kusema hivi:

Dini imetengenezwa kwa mujibu wa matakwa ya ndani ya nafsi yanavyotakiwa kuwa. Ili kuifafanua dini kwa uwazi zaidi inatupasa turejee katika historia ya uumbwaji wa mwanaadamu. Nyanja zinazoweza kutoa natija bora katika uhakiki wa suala la dini ni nafsi na nyoyo za wanaadamu, yaani pale mmoja wetu anapotaka kuihakiki dini ni lazima uhakiki wake auanze katika hatua ya mwanzo ya hali halisi ya nyoyo na roho za wanaadamu zilivyo kimaumbile. Kwani yeye atakapoanza uhakiki wake katika suala la maumbile ya roho za wanaadamu, atagundua kuwa nyoyo zote za wanaadamu ni zenye fungamano moja la hisia, nayo ni ile hali ya kila mmoja wetu kuhisi kuwa anahitajia dini ili kuweza kumtatulia maisha yake kijumla, na hilo ndilo lililopelekea aina mbali mbali za dini kuzaliwa ulimwenguni, pale wanaadamu wanaposhindwa kuitambua dini halisi ya Allah (s.w) ima kiujinga au kiubabe. Kumerushwa tata au kwa lugha nyengine tunaweza kusema kasumba inayosema kuwa dini imeteremshwa kwa mujibu wa utamaduni wa watu, Au kwa maana nyengine dini haiteremshwi bila ya kuwepo utamaduni.

Hivi kweli kauli hiyo ni sahihi? Ili kuipatia jawabu tata hiyo naturejee katika historia ya dini na chanzo chake. Kwa ufupi tunaweza kuijibu tata hiyo kwa kusema:-

Dini ndio iliyovumbua tamaduni, na sio tamaduni zimevumbua dini, kwa hiyo utamaduni umo ndani ya dini, na sio dini imo ndani ya utamaduni, dini kwa mwanaadamu ni fitra yaani (nature)- religion is nature from the God -. Dini ndio iliyokuja kuwafundisha wanaadamu maadili mema, na kupinga maadili mabaya yaliyokuwa yakifanywa na makafiri na washirikina, na sio utamaduni wa baadhi ya watu ndio uliokuja kuwafunza watu umuhimu wa dini au maadili mema.

[1] Surat Al-Aaraf Aya ya 172

MWISHO