USHAHIDI NA UTHIBITISHO

3 USHAHIDI NA UTHIBITISHO KWA KUPITIA  HADITH AL-MANZILAH

Wanazuoni wote wa Kishia na Kisunni wanakubali juu ya usahihi wa hadithi hii. Mtume Muhammad (S.A.W.W) alipokwenda katika vita vya Tabuk katika mwaka wa 9 Hijria, alimuacha Imam Ali kua Khalifa wake katika mji Madina, Tabuk (katika mpaka wa Syria) ilikuwa ni mbali sana na Mtume alipaswa kumuacha mtu madhubuti na mwenye imani kubwa ili kuulinda mji mkuu wa Dola ya Kiislamu Madina kutokana na uovu wa washirikina, na hususan wanafiki ambao walikuwa wanasubiri wapate nafasi japo ndogo ili walete mtafaruku Madina. Hivyo Mtume alimteua Imam Ali ili awe Khalifa wake katika kipindi hiki ambapo Mtume alikuwa safarini, Wanafiki walianza kumchokoza Imam Ali kuwa hakwenda Jihad ili kuokoa maisha yake na kwamba alikuwa anaogopa kifo. Imam Ali hakufurahia maneno haya, hivyo alikwenda kwa Mtume kumuomba aende naye vitani (Jihad), Mtume alijibu kwa haikuwa vizuri kwake yeye Mtume kuondoka bila kumteua Ali kama Khalifa wake, pale Madina. Kisha alisema: "AMAA TARDHAA AN TAKUUNA MINNI BI MANZILATI HAARUNA MIN MUSA, ILLAA ANNAHUU LAA NABIYYA BA'DII" - "Je hauridhiki kwamba wewe kwangu una nafasi kama ile aliyokuwa nayo Haruni kwa Musa, isipokuwa tu hakuna Mtume baada yangu?" Hadithi hii inathibitisha waziwazi kuwa nafasi ya Ali ni sawa na ile ya Haruni. Sasa tujiulize ni ipi ilikuwa nafasi ya Haruni ? Hebu tuiangalie nafasi ya Haruni katika Qur'an Tukufu. "Na nipatie Waziri kutoka katika familia yangu, Harun ndugu, na niongezee nguvu kupitia kwake na mfanye awe mshirika katika kazi yangu" (Taha 20:29-32).
"----- Na Musa alisema kumwambia ndugu yake Haruun; Kuwa Khalifa wangu miongoni mwa watu wangu ---- ". (A'araf 7:141). Aya hizo hapo juu zinathibitisha kuwa Harun alikuwa ni Ndugu, Waziri, Msaidizi, Khalifa na Mrithi wa Nabii Mussa. Halikadhalika kwa mujibu wa Hadithi Al-Manzilah, Imam Ali ni Ndugu, Wazir, Msaidizi, Khalifa, na Mrithi wa Mtume Muhammad baada yake. Je bado tu hamuielewi na kuitii amri ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) enyi Waislamu! Hadithi ya Manzilah imesimuliwa na mamia ya Wasimuliaji wa hadithi wa Kisunni, baadhi yao ni kama ifuatavyo : - Sahih Bukhari, Baab Ghazwat Tabuk, Juz. 3, uk. 54. - Sahih Bukhari, Baab Manaqib Ali Bin Abitalib, Juz. 2, uk. 185. - Sahih Muslim, Baab Fazail Ali, Juz. 2, uk. 236. - Musnad Ahmad bin Hambal, Juz. 1, uk. 98 na uk. 236. - Hakim katika Al -Mustadrak, Juz. 3, uk.109. - Suyuti katika Taariikhul Khulafaa, uk. 65. - Ibn-Kathiir katika Usudul Ghaabah, Juz. 4, uk. 26. - Ibn Hajr Al-Asqalaani katika Isaabah, Juz. 2, uk. 507. - An-Nasaai katika Khasais, Uk. 7 na Uk. 15. - Taariikh Ibn Asaakir, Juz. 4, Uk. 96 n.k.
Qur'an Tukufu inasema: "Na sema: Ukweli sasa umefika (umekuja), na uongo umeondoka, na daima uongo huwa ni wenye kuondoka". (Israa 17:81).