ATHARI NJEMA BAADA YA UTUME NO.4

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

ATHARI NJEMA BAADA YA UTUME NO.4

* Mapinduzi ya Mitume yalileta athari gani katika jamii?.

BAADA YA KUBASHIRIWA UTUME

Mapinduzi ya Mitume hayakuwa na harakati zisizokuwa na malengo, bali yalikuwa ni hadafu na madhumuni ya juhudi zilizofanywa kwa ajili ya kufikia katika malengo maalumu, nayo ni kusuluhisha jamii, na kuwatakasa watu wa jamii nzima duniani.

Hapana shaka kuwa Mitume imeteuliwa miongoni mwa watu.

Katika makala no.3 tulielezea baadhi ya athari njema zilizopatikana baada ya Mitume kubashiriwa utume, katika makala hii tunaendelea na mada yetu hiyo hiyo, athari nyengine zilizopatikana ni:-

3. VITA NA SULUHU.

Mitume Mitukufu baada ya kupewa Utume waliwalingania watu na kuwataka kuja katika dini ya Mwenyeezi Mungu kwa dalili zilizowazi kabisa, na hawakumlazimisha mtu kuikubali dini ya Mwenyeezi Mungu bila ya hiyari yake kama anavyosema Allah (s.w):-

لاَ إِكْرَاهَ فِى الدِّينِ قَد تَّبَيَّنَ الرُّشْدُ مِنَ الْغَيِّ فَمَنْ يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَيَ لاَ انفِصَامَ لَهَا وَاللّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ[1]

Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu umekwisha pambanuka na upotofu. Basi anaye mkataa Shet'ani na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti,kisicho vunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.

* Baadhi ya Waarabu wa Madina kabla ya kwenda Nabii Muhammad (s.a.w.w.) huko walikuwa wanafuata dini ya Kiyahudi, lakini wengi wao wakiabudu masanamu, ulipokuja Uislamu, takriban wote hao waliokuwa wakiabudu masanamu walisilimu, ama katika wale waliokuwa na dini ya Kiyahudi walisilimu kidogo tu, na wengine wakasalia na Mayahudi japokuwa ni Waarabu, basi baba zao waliosilimu, na ndugu zao na wakubwa wao, na waume zao, walitaka wawatie katika Uislamu kwa nguvu, basi wakakatazwa hapa na Mwenyeezi Mungu kuwa:

Hakuna ruhusa kumkalifisha mtu asiyetaka, kila mtu kapewa akili ya kutambua jema na baya, basi akifuata upotofu hiari yake mwenyewe, na Mungu atampa adhabu huko Akhera na sio hapa.

Basi umefedheheka hapa uwongo wa wale wanaozua kuwa Uislamu unalazimisha watu kwa nguvu kuingia katika dini hiyo japo wenyewe hawataki, basi uislamu gani huo wanaousingizia hivyo? Na Uislamu ni huu uliomo katika Qur-ani.

Baada ya Mitume kuwalingania watu kafuata dini ya Mwenyeezi Mungu, kuna walioamini na kuna baadhi yao walikufuru:-

تِلْكَ الرُّسُلُ فَضَّلْنَا بَعْضَهُمْ عَلـٰي بَعْضٍ مِّنْهُم مَّن كَلَّمَ اللّهُ وَرَفَعَ بَعْضَهُمْ دَرَجَاتٍ وَآتَيْنَا عِيسَي ابْنَ مَرْيَمَ الْبَيِّنَاتِ وَاَيَّدْنَاهُ بِرُوحِ الْقُدُسِ وَلَوْ شَاء اللّهُ مَا اقْتَتَلَ الَّذِينَ مِن بَعْدِهِم مِّن بَعْدِ مَا جَاءتْهُمُ الْبَيِّنَاتُ وَلَـكِنِ اخْتَلَفُواْ فَمِنْهُم مَّنْ آمَنَ وَمِنْهُم مَّن كَفَرَ وَلَوْ شَاء اللّهُ مَا اقْتَتَلُواْ وَلَـكِنَّ اللّهَ يَفْعَلُ مَا يُرِيدُ[2]

MITUME hao tumewatukuza baadhi yao juu ya wengineo. Katika wao wapo ambao Mwenyezi Mungu alisema nao, na wengine akawapandisha vyeo. Na tukampa Isa mwana wa Mariyam hoja zilizo wazi, na tukamtia nguvu kwa Roho Takatifu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli pigana walio kuwa baada yao baada ya kuwajia hoja zilizo wazi. Lakini walikhitalifiana. Basi wapo kati yao walio amini, na wengine kati yao walio kufuru. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli pigana. Lakini Mwenyezi Mungu hutenda atakavyo.

Makafiri hawakuweza kuwacha itikadi zao za kikafiri na kijahilia tu, bali walimpinga Mtume kutokana na amri za Mwenyeezi Mungu walizokuja nazo, walijenga khitilafu na kufanya uadui nao, na Mitume iliwaongoza lakini makafiri hao hawakukubali miongozo hiyo, baada ya hapo basi Mitume ilikabiliaana na makafiri hao kutokana na kiwango cha uadui walioufanya makafiri hao.

Mwenyeezi Mungu anasema:-

وَإِنْ عَاقَبْتُمْ فَعَاقِبُواْ بِمِثْلِ مَا عُوقِبْتُم بِهِ وَلَئِن صَبَرْتُمْ لَهُوَ خَيْرٌ لِّلصَّابِرينَ[3]

Na mkilipiza basi lipizeni sawa na vile mlivyo adhibiwa. Na ikiwa mtasubiri, basi hakika hivyo ni bora zaidi kwa wanao subiri.

[1] Suratul-Baqarah Aya ya 256

[2] Suratul-Baqarah Aya ya 253

[3] Suratun-Nahli Aya ya 126

MWISHO